Shahidi alipoona mwenyekiti anapiga simu, kwa minajili ya
kuwaambia kuwa yeye anafahamu yaliyotokea humo, na huenda anamfahamu muuaji wa
Makabrasha, shahidi akasema;
‘Mwenyekiti tafadhali nakuomba usiwaambie polisi kuwa mimi nafahamu
kilichotokea siku hiyo, nay a kuwa nimesema kuwa namfahamu huyo muuaji wa
Makabrasha. Elewa nafasi yangu kwa sasa,kwani nikiwaelezea hayo, kuna
watakaokimbilia kunikamata na kuniweka ndani, lakini utambue kuwa wanahusika
kwa namna moja au nyingine, na hawataki ukweli ugundulikane.
‘Nakuahidi mwenyekiti, wakati ukifika, mimi mwenyewe kwa
wakati wangu nitakwenda kuonana nao, bado kuna mambo nayafuatilia, na kama
wangelitaka kunikamata, wangeshamikamata , hujiulizi kwanini hawajanikamata,
ina maana wao ni wajinga muda wote huu wasifahamu kuwa nilikuwemo kwenye hilo
jengo wakati Makabrasha anauliwa, wanafahamu, lakini wana mbinu zao, kuna jambo
wanalifuatilia, a wanafahami ni kitu gani ninachokifanya....’akasema.
‘Kwahiyo unavyosema hivyo, wewe na polisi mnashirikiana?’
akauliza
‘Sijsema hivyo mwenyekiti, naomba usininakili vibaya, mimi
sina maingiliano na polisi, na kama ni uchunguzi wa kazi zangu, naufanya kwa
manufaa yangu,au kwa mtu aliyenituma, mimi ni mwekezaji tu...’akasema.
‘Kwa mimi nilivyoona, ninahisi umeifanya hiyo kazi hasa hasa kwa
manufaa ya mpenzi wako wa zamani, na ulikuwa tayari kufanya lolote kwa ajili
yake, nimeyafuatilia maelezo yako yote, na hasa pale ulipofikia kuacha kazi kwa
mtu wako wa kwanza kwa ajili ya kwenda kupambana na wale walioingilia maisha
yenu na mipango yenu,
‘Ni sawa kila mtu ana ndoto zake, lakini tuwe makini katika
kujitolea muhanga kwa nafsi nyingine, kwani hatuna uhakika kuwa kweli huyo
tunayejitolea muhanga kwake, yupo nawe moja kwa moja, huenda mwenzako anakutumia
tu, kwa masilahi yake, hali kama hiyo ni hatari. Kwa uhakika zaidi, hebu
mwangalie mwenzako, alivyokufanyia, wewe naona humfahamu vyema huyo mpenzi wako
wako, kama unavyodai unamfahamu kihivyo, yeye kwa tabia yake, imeonyesha
dhahiri kuwa ni mbinafsi, yupo tayari akutumie wewe kwa manufaa yake, na mwisho
wa siku anaweza asiwe nawe tena....’akasema mwenyekiti.
Mume wa familia, akainua kichwa na kumwangalia mwenyekiti, akiwa
kakunja uso,wa kutafari, nahisi kuna kitu alitaka kukizungumza, lakini akawa
anasita kukiongea, hakusema neno, alimwangalia mwenyekiti kwa muda, halafu akageuka
kumwangalia huyo shahidi, wakaangalia, na baadaye akatikisa kichwa kama
kusikitika, halafu akainamisha kichwa
chini na kutulia, hakusema neno, na mwenyekiti ambaye alikuwa akimwangalia,
akitaraji kauli kutoka kwa mume wangu, lakini alipomuona huyo mtu katulia tu,
akaendelea kusema kwa kumchokoza huyo mtu;
‘Kama ni uwongo kwa hitimisho langu, kama nimemzulia uwongo,
huyo hapo muulize, ...kama kweli yupo na wewe mia kwa mia, kama kweli, yupo na
wewe au kama kweli yupo na mke wake aliyemuo kwa ajali ya kujinufaisha, aseme
tusikie, uwanja ni wake, ...’akasema mwenyekiti.
Walipoona mume wa familia kakaa kimiya, shahidi aliyepita,
akasema;
‘Ndugu mwenyekiti, mimi nafahamu ni kitu gani
ninachokifanya, na sikufanya hayo kwa ajili yake tu, nilifanya hayo kwa vile
nawajibika kufanya hivyo, kama yeye ataona kuwa mimi ni mjinga, sikuwa na maana
njema kwake, hilo ni yeye na kichwa chake, na haliniumizi sana kichwa changu,ingeniumiza
sana, kama ningelikaa kimiya baada ya kuona hayo yalitokea, yanapita bila
kutafutiwa ufumbuzi, ndio maana nikaamua kuusema huo ukweli kwenu, kwani
nafahamu nyie ndio waathirika wakubwa wa kadhia hii yote...’akasema huyo
shahidi.
‘Sasa kama unakubali kusema ukweli na kufichua maovu kwanini
usishirikiane na wale walipewa dhamana hiyo na serikali, ambao ni polisi, kwanini
ufanye hayo kimiya kimiya, peke yako, huoni kuwa kwa kufanya hivyo ni makosa?’
akauliza mwenyekiti.
‘Muheshimiwa Mwenyekiti , nafahamu fika wewe unafahamu vyema
hilo ninalolifanya, na sio geni kwako, kuwa kuna mambo mengine hutakiwi
kukimbilia kuwaambia polisi, inabidi ujirizishe mwenyewe kwanza, kwani
ukikimbilia huko, wao watakachokifanya ni kukushika, wakisema unakamatwa kwa
ajili ya kuisaidia polisi, na hata kama hawatakukamata kwa bahati mbay, wao
watakuzuia usifanye uchunguzi wako,...’akatulia kidogo, halafu akasema.
‘Ndio ni utaratibu wao, kwa nia njema wakakushika au
kukuzuia, ila wao wafanye wajuavyo wao, kiutalaamu wako, huenda wakafanikiwa au
wasifanikiwe kwa kile ulichokianza au kukigundua. Lakini kwa vile wao wanaona
ni kazi yao, hata kama itwashinda hata kama watafanya yale unayoona wao, ni
uzuia haki, au yale uliyoyaona kuwa yapo, na yalitakiwa kufuatiliwa kivingine,
wao hawatakusikiliza watakuzuia, na watafuata wanavyotaka wao, na matokea yale
yale uliyotegemea kuyapata usiyapate tena, na wao pia wasiyapate, na unafikiri
kwako wewe uliyezuiliwa, itakuwaje, watakushika wee, huenda ukasota jela, mpaka
ukaathirika kiafya.
‘Mimi kutokana na utendaji wangu wa hii kazi,nimejifunza
mengi, kwahiyo sioni kama nafanya kosa, kutokuwaambia yale niliyoyaona,
nafahamu wengi mtaona hivyo,...ila mimi nafahamu nafasi yangu kama raia mwema,
ni wakati gani niwakilishe hayo niliyoyaona kwao, na muda huo ukifika, utaona
matunda yake, sio mara ya kwanza kufanya kazi kama hiyo, mwenyewe utakuja
kuoona, labda hawo wahusika waniwahi na kuniua...’akasema.
‘Na wakiniua ni ajali kazini, ni kama askari kufa vitani,
sioni ajabu...’akasema hivyo baada ya
kutulia kidogo, na mwenyekiti akatabsamu na kusema;
‘Ndio hapo unapokosea,...maana wao ni kazi yao kulinda raia,
na kuhakikisha haki inatendeka, na kwa jinsi unavyoongea ni kuwa una wasiwasi
kuwa hao jamaa wanaweza kukudhuru, ni vyema ukajisalimisha kwa usalama, na wao
watawajibika kwa hilo, kwani wao wana mamlaka na uwezo wa kukulinda...’akasema
mwenyekiti.
‘Una uhakika na hilo ndugu mwenyekiti, kuwa wanaweza
kunilinda, hahaha....wangapi wangapi waliambiwa hivyo, na sasa tumewasahau,
kukulinda kwako ni kukuweka jela, wanasema kwa manufaa yako, au manufaa ya
jamii, au sio..huko jela kweli ni kuzuri kukaa, ulishawahi kukaa jela ndugu
mwenyekiti, hebu muulize binti yako, akuambia, jela sio mahali pema kuishi,
kuna hatari zake hasa za kiafya, achilia mbali kuathirika kisaikolojia,....sawa
ikibidi nitaenda huko, lakini kuna jambo bado nalifuatiliaa, nisingependa
kuongea na kwa hivi sasa, tafadhali
mwenyekiti nakuomba unielewe hivyo...’akasema.
Mwenyekiti akamgeukia mume wa familia na kumwangalia,
akageuka kuniangalia mimi, halafu akasema,;
‘Kama alivyosema shahidi, hayo ya nani muuaji wa Makabrasha
ni mambo ya polisi, na hatutakiwi kuyaongea hapa, kilichotuweka hapa na mambo
yetu ya kifamilia, tufanye yale yaliyopo kwenye mipaka yetu, tusipende
kujifanya tunajua sana, na kuingilia kazi za watu, aheri mwenzetu anajua jua
mambo hayo, sasa sisi tukiulizwa kwanini, tutasema nini....’akasema mwenyekiti
na kuwaangalia mawakili.
‘Ninashukuru tuna watu wetu wa sheria, na wameona juhudi
zetu katika kuliweka hilo sawa, kama tunakosea wao watatusahihisha, ila cha
muhimu kutokana na ajenda yetu tumeshakipata, na kabla hatujaingia kwenye
kipengele cha mwisho, ambacho ni makubalian au hukumu, ningelipenda tumpe
nafasi mume wa familia aongee, ajitetee, kwa nafasi yake, na hili hatutaki
wakili wake aliingilie kati, kwani kwa hivi sasa kila kitu kipo wazi, ...ukweli
umedhihiri, na uwongo umejitenga...’akasema mwenyekiti, na kumwangalia mume wa
familia.
Mume wa familia, akainua kichwa na kumwangalia mwenyekiti,
akatikisa kichwa kama kukataa, haikueleweka, kwanini anatikisa kichwa vile, akabakia kimiya hakuongea, baadaye akainmisha
kichwa chake kama ilivyokuwa awali, akatulia kimiya.
‘Je mume wa familia hayo yaliyoongewa na mpenzi wako wa
zamani ni kweli au na yeye kajitungia uzushi wake?’ akaulizwa mwenyekiti, na kumwangalia
mume wa familia, ambaye alikuwa bado katulia kimiya, na mwenyekiti akaongeza
kuongea kwa kusema;
‘Huyo ni mtu wako, yupo kwenye moyo wako, kipenzi chako cha
asili, ...singeliweza kusema hayo aliyoyasema, kama anglijua kuwa anakuumiza,
kajitosa kwa ajili yako, sasa je hayo aliyoyaongea yana ukweli, unayakubali, au
ni kama yale yale ya rafiki wa mke wa familia, maana yanathibitisha yale
aliyoongea huyo rafiki wa mke wa familia, na uliyapinga kwa nguvu zote, sasa je
na haya unayapinga, ni uzushi, hayana ukweli, toa kauli yako kama
mwanaume...’akasema mwenyekiti, na mume wa familia akaendelea kukaa kimiya.
‘Kukaa kwako kimiya inaonyesha nini, ama ni kutuzarau, au ama
ni kiburi, au tusemeje?’ akauliza mwenyekiti, na mume wa familia akaendelea
kukaa kimiya, na mimi nilipoona hivyo, nikaona niingilie kati, nikasema;
‘Ndugu mwenyekiti, mimi naona tusipoteze muda, kuna mengi
yamesemwa na yote ni ukweli mtupu, kwa mwenye hekima, ataelewa, na kukiri kosa,
lakini kwa mtu mwenye tabia yake, ataona ni yale yale,tu,...lakini tuyaangalia
hayo kwa mapana yake, ni nani hasa alilengwa, utaona ni mimi, utaona ni mali za
familia ya mke, mali zilizotoka kwenu wazazi wangu,...ni kweli mimi, nilifanya
juhudi tukafika hapo tulipofika, na nilijaibu kumshirikisha mwenzangu, ili
ajifunze, na ilikuwa ni kazi kubwa, kumjenga mtu awa hulka yake...’nikasema.
‘Wakati mwingine, ilibid mimi nigeuka kuwa kama mume wa
familia, kufoka, na hakupendeza, alkini nilifanya hivyo, kwa vile mimi
nafahamu, kwa vile mimi nimekulia katika familia ya hali hiyo, kazi kwetu ni
kipimo cha utu, kazi kwetu ni jadi, hayo
mnayoyaona, hizo mali, na utaji, na ukiangalia, mwenye I wetu, haukuja hivi
hivi...nayasema haya ili watu waelewe....’nikamwangalia mume wa familia
aliyekuwa bado kainama.
‘Naafhamu kabisa kusudio lao hawa wenzetu, ni kuwa kila
tajiri, kila mwenye uwezo, kaupata kwa njia za kubumashi, kutepeli, kuiba,..sio
kweli, ...wapo wengine, kama sisi, ..najivunia hilo, kwani mimi nimeishi na
wazazi wangu, nimeona jinsi gani walivyokuwa wakijituma, wakajinyima,
...wakahangaia usiku na mchana, ..huku na kule, na matunda yake ndio
hayo...sasa mlitaka mimi nilale, nibweteke, na kusema mali zipo, mali za baba
na mama zipo, nitumie tu, hilo haliwezekani...’nikatulia kidogo.
‘Ndio maana ilifika mahali, nikasahau kila kitu, nikasema
sasa ni kazi, starehe baadaye, huenda kwa kufanya hivyo, nilimkwaza mwenzangu,
akaona nazarau majukumu muhimu ya ndoa,...lakini je huko mwanzo ilikuwa vipi,
kama ningelifanya hivyo, hawo watoto wangelipatikana,...ilifika mahali nikaona
kuna umuhimu wa kujitosa ili kukiokoa kile tulichokianza, hakuna kulala, hakuna
staeeh kwanza, mpaka uone kuna faida..ndilo lilikuwa lengo langu, sikueleweka
kivitendo, walitaka, au alitaka nitamke kwa ulimi.
‘Nimejifunza mengi kwa hili, na kwa akuli ya haraka haraka ,
ninaweza kusema, imekuwa kama mtoto akililia, wembe muache, ukimkata
atajifunda, lakini pia imekuwa changamoto kwangu, kwani yote haya yaliyotokea
muathirika mkubwa ni nani, ni mimi na watoto wangu..., ni kama vile wote walikuwa
na lengo moja la kuniadhibu mimi , kwa kosa nisilo lijua, ...naona wengine
wamefikia kusema ni kutokana na mimi kujisahau katika majukumu yangu ya ndoa,
nk...
‘Lakini hebu angalia huo mlolongo mzima, kumbe haya yalikuwa
yamepangwa kutoka huko kijijini hata kabla ya ndoa yangu, na ndoa yangu ikawa
kama kisingizio, na udhaifu wangu wa kibinadamu ukatumiwa kama ngazi ya
kutekeleza hayo yaliyokwisha pangwa, nashukuruni sana kwa hayo,nawashukuruni
sana, wote, mliokuja kwangu na kuwapa kial kitu changu, ikiwemo nafsi yangu
katika moyo, nikawaona kama ndugu, kama marafiki wema, kama mume
mpenzi,...lakini hii ndio faida yake, mtoto akililia wembe muache, ukimkata
atajifunza.
Kwa hivi sasa nina machungu moyoni, huenda nikitoa uamuzi
wangu, naweza kuharibu, nahitajai muda wa kulitafakari hili kwa undani,
...yaliyotokea yamenifungua macho, masikio, nimejua ni nini nahitajika
kukifanya, huenda kabla sijasema yale ya moyoni, ambayo nitakuja kuyasema kesho
au siku itakayopangwa na mwenyekiti, ningelipenda kumuuliza mume wa familia,
maswali machache, mbele yenu, na nataka ayajibu mwenyewe kwa kinywa chake,
...bila kuficha..'nikasema na kumgeukia mume wa familia,
'Mimi ninayekuuliza haya ni mke wa familia nakuuliza wewe kama mume wa familia, nategemea wewe kama mume wa familia, utayajibu hayo bila kuniogopa, kama utaniogopa
itakuwa ni ajabu, ...uume wako utatiliwa mashaka...’nikasema na watu wakacheka.
Na mume wangu akaniangalia kwa macho yaliyojaa hasira, ni
mimi sikujali macho yake, nikasema;
‘Swali langu la kwanza, ni lile lile swali la mwenyekiti, ni
swali la msingi na lenye hekima, je hayo
yaliyosemwa na wote hasa shahidi wa mwisho aliyekuja kuthibitisha, je hayo
aliyoyathibitisha ni ya kweli au kajitungia mwenyewe...nataka unijibu hilo
swali, kwani majibu yake, yataweza kunipa mimi mwanga,ili nisije nikahukumu kwa
dhuluma, na sio mimi nitakayehukumu, muelewe hivyo, ni sote mimi na yeye, kwani
tulipoandika huu mkataba, hatukusema mimi, tulisema sisi, yoyote atakyekiuka,
atawajibika, sasa isiwe mkuki ni kwa nini....’nikamwangalia mume wa familia na
yeye akaniangalia kwa macho yale yale yaliyojaa hasira, na akasema;
‘Nilijua kuwa itafika hapo, nilifahamu kuwa ni mtego wa panya, sawa, nimekubali, na sina
haja ya kung’ang’ania maliz zenu,...ninachoweza kusema kwa sasa na huenda ndiyo
kauli wengi wanaisubiria, ni kuwa nisamehe mke wangu,.....japokuwa yana ukweli,
ni kweli,....ila ukweli mwingine unafutika, chanzo , kwanini, hakitaanagliwa
tena,..sijali, nakubali kushindwa, nimekiri nimekosa,...lakini mke wangu,
katika maisha kuna kukosa, kuna kupanda an kushuka,..hayo ni majaiibu na kama
binadamu unaweza kuyapitia, na mimi sio wa kwanza....’akasema na sasa akabadili
uso wa hasira na kuwa uso wa huzuni.
‘Mke wangu, nakupenda sana...nilijitahidi kufanya hivyo,
kukupenda, na kumbuka watoto wetu wapo wananihitajia mimi, baba yao, wanakuhitajia
wewe mama yao, ndio maana nilifanya kila niliwezalo nionekane na mimi ni baba
wa familia, niwe mkali, niwe na mamlaka, lakini ikaja kuvurugwa na watu
wengine, ....sitaki kuwatupia wao lawama, nafahamu hakitaeleweka tena..hata
hivyo kauli yangu ni kuwa, mimi ndiye baba wa familia, na hayo niliyoyafanya,
nilitaka nieleweke hivyo, kama nimekosea nakubali na nakiri kosa...’akasema.
‘Hahaha hatimaye mume wa afmilia amekiri kosa, japokuwa kwa
shingo upande, lakini sio kutoka moyoni, akisema anakubali kwa vile ametegwa
kama panya, jamani, hebu angalieni huo mlolongo wote, kuna kutegwa hapa...au ni
huo mfumo dume, mnaotaka kutuonyesha jamani...wewe uwe kama jogoo, leo huyu
kesho yule..hivi kweli ni ubinadamu huo, ni utu huo...sikubali, na nilihitajia
kauli iliyonyooka, na kauli thabiti, kuwa hayo yaliyosema ni kweli au ni
uzushi..sijaiona hiyo kauli....’nikasema, na mwenyekiti aakingilia kati na
kusema;
‘Kwahiyo kwake yeye hayo aliyoyaongea ni kukubali kuwa yote
yaliyosemwa ni ya ukweli, ....labda tungelihitajia kauli ya kujiamini, ili
tupate jibu la uhakika, unafahamu mimi ni mwanaume, na inaniuam sana nikisikia,
hiyo kauli ya mfumo dume, kwanini mfumo dume, kwanini tusikubali ukweli, na
kuwa wawazi, kama tumekosea basi tukubali, kama wanaume, sasa mume wa familia, tunataka
jibu la kimwanaume kweli, usijifanye legelege, wewe ni mwanaume bwana...jitetee,
tetea uume wako’akasema mwenyekiti.
‘Nimeshajibu mwenyekiti, naona kama mnanizalilisha sasa,
hizo kauli zeni sizipendi, nafahamu kuwa nimekosea, na nimeshatoa kauli yangu,
lakina hizo kauli zenu ni za kunifanya mimi mtoto , si chochote, nafikiri ni
zarau, kutokana na asili yetu, kuwa labda sisi tumekulia, na kulelewa kitabia
mbaya, hatupendi kazi, tuna tamaa,na kitu kama hicho, lakini mkumbuke yoyote
anaweza kupitiwa, na shetani, akaghibilka na ni ibilisi, na .....ni nimeshawaambia
kuwa sikuwa na nia mbaya, kwa hayo niliyoyatenda, na hamtaki kukubali ukweli
kuwa nilifanya hayo yoate kwa ajili ya
kuilinda familia yangu, kwani kama nisingelifanya hivyo, hamjui ni kitu gani
Makabrasha alinitishia nacho...’akasema
‘Tunataka tusikie hicho kitisho alichokutishia Makabrasha,
maana kukutishia wewe ni kama alitishia familia yote hapa, je alikuambia nini,
sisi tunavyojua ni kuwa Makabrasha alikutishia kuwa usipofanya anavyotaka yeye,
atakuumbua kwa machafu yako uliyoyafanya, atakwenda kumwambia mke wako, na mkwe
wako, au sio?’ akauliza mwenyekiti.
‘Pamoja na hayo, ...’akatulia na kutikisa kichwa kama
kusikitika,
‘Hamkumjua Makabrasha nyie, hamkuwahi kuishi naye kwa
karibu, yeye alisema, anaweza kuiumiza familia yangu, hasa watoto, atawateka
nyara na kuwafanya wasionekane tena, ..hata wakionekana watakuwa mazezeta...hivi
wewe kama mzazi ukisikia hivyo, utachukua hatua gani...’akasema
‘Hivi wewe kwa akili zako uliamini kuwa Makabrasha
angeliweza kufanya hayo aliyokutishia, au alishakufahamu udhaifu wako kuwa wewe
ni mwoga, ...au hebu tupe mifano hai, ambayo yeye aliwahi kuwafanyia watu
wengine, ili tuamini kuwa vitisho vyake vilikuwa ni kweli...’akasema
mwenyekiti.
‘Mimi nawapenda watoto wangu, iwe ni kweli au si kweli, iwe
ni vitisho tu au ni kweli, mimi nilichotakiwa kufanya ni kile nilichoona ni
sahihi, kwa ajili ya kuilinda familia yangu...’akasema
‘Ina maana hata kutembea na wake za watu, mfanyakazi wako wa
ndani inatokana na vitisho vya Makabrasha?’ akaulizwa na hapo akakaa kimiya.
‘Au labda tukuulize hili swali huenda nalo linaweza kuwa ni
sababu ya Makabrasha, je ni kitu gani kilichokufanya uwe mnzizi na kuisaiti
ndoa yako?’ akaulizwa
‘Ni hali iliyokuwa imenizunguka, nilikuwa nimechanganyikiwa
na mambo mengi yalikuwa yakiniandama, ikiwemo hilo la mipango aliyoibuni
Makabrasha, na hata hivyo, mke wangu alikuwa na kazi nyingi sana, na yeye
alitakiwa awe karibu na mimi ili niweze kuyasahau yote hayo, lakini hata
nilipojaribu kumvuta ili aniliwaze, niliona kama yeye
ananisukuma...’akajitetea.
Mimi nikamwangalia kwa hasira na kusema; ‘Huo ndio utetezi
wako, kuwa mimi sikuwa karibu nawewe, je uliwahi kuniambia hilo, kwa kinywa
chako nikakukatalia au kukusukuma, ...?’ nikamuuliza
‘Kwa vitendo visivyo dhahiri, unaweza ukamkatalia mtu, kwa
vitendo visivyo vya moja kwa moja, na mimi
kama mtu mzima nililiona hilo, kuwa
hukuwa karibu na mimi na niliposema kusukuma sio kwa kusukuma kwa mikono, ni
kwa vitendo, visivyo moja kwa moja...’akasema
‘Kwa matendo hayo ina maana nilionyesha hivyo kwa vile sikupendi,au
ni kwa vile nilikuwa nawajibika kwa ajili ya kujiendeleza, kwa ajili ya maisha
yetu ya baadaye na familia?’ nikamuuliza
‘Hapana sijasema hivyo, kuwa hunipendi, na hujawahi
kunitamkia hivyo, kiukweli ulikuwa unanipenda na ulikuwa ukifanya hivyo kwa
ajili ya kuinua kipato chetu zaidi na zaidi, lakini hukufanya yale
yanayostahili kuonyesha upendo wa mke, ulijali sana kazi hata muda usio
wake...’akasema.
‘Ina maana wakati mke wako anahangaika na kazi hadi kusahau
majukumu yake ya ndoa wewe ulikuwa huna kazi , au sema ukweli huenda mke wako hakuwa na kazi kweli, alikuwa akijifanya
ana kazi kwa mbinu za kukwepa majukumu yake ya ndoa, sema ukweli, jitetee?’
akaulizwa.
‘Hayo yapo wazi, kazi ni kazi, na majukumu ya ndoa yapo pale
pale...siwezi kusema alifanya hivyo kwa ajili ya kukwepa majukumu yake ya ndoa,
hapana, ni kweli alikuwa akifanya kazi kiukweli, niliona kwa macho yangu, na
siwezi kumlaumu sana kwa hilo..’akasema
‘Kama huwezi kumlaumu kwanini ukamsaliti, kwani ukafikia hadi kutembea na mfanyakazi wako wa
ndani, kwanini ukafikia hadi kutembea na mke wa mtu,...tunataka kujua ukweli,
jitetee kwa hayo, huenda ulikuwa na sababu ya msingi, ambayo ukituambia
tutakuelewa, ?’ akaulizwa tena na mwenyekiti.
‘Nimeshasema ni .....ni ibilisi tu, tamaa zilinizidi,
nikashindwa kuvumilia, kama binadamu inaweza kufikia hatua hiyo,...,
nilipitiwa,......’akainama chini.
Mimi nikamwangalia na nikasema ;’ ‘Mwenyekiti, mimi
nimesharizika na jibu la swali hilo, ngoja nimuulize swali la pili...’nikasema
na mwenyekiti akatabasamu na akamwangalia mume wa familia, halafu akasema;
‘Haya muulize maana ni mume wako unamfahamu sana kuliko
sisi, ...’akasema mwenyekiti
Swali langu la pili, ni hili, ni muhimu sana , tena sana
unijibu kutoka moyoni mwako, ...maana ukinidanganya tutajua,...ni kwa ajili
yangu na wake wenzangu.’nikasema na kumwangalia na yeye akaniangalia kwa
mashaka, akisubiri hilo swali.
‘Je unampenda mpenzi wako wa asili?’ nikamuuliza na yeye
akawa kama anatabsamu, kama vile nimemzihaki, halafu kwa haraka akageuka
kumwangalia huyo mpenzi wake wa asili na baadaye akamwangalia rafiki yake,
yaani docta, halafu akasema;
‘Kwanini mnaniuliza swali kama hilo, ...sioni umuhimu wake
kwa sasa, hapa naona mnaendelea kunitega tu, hilo swali leni lina ajenda ya
siri, na mimi kama binadamu, siwezi kudanganyika, niliyoyafanya niliyafanya
nikijua mimi ni mume wa familia, nilikuwa na mimi nawajibika, kwa manufaa ya
familia yangu, mlitaka nikae tu,...’akawa katoa macho ya hasira akimwangalia mke
wake.
‘Mzee, samahani sana baba yangu kama nitakosea, ni hivi kweli kuna mtu anaweza kuja pale kwako baba akakupangia jinsi gani ya kuishi,wewe umeshaoa , una mke wako,halafu watu wengine waje na sera zao...au ni kwa vile mimi...hebu nikuulize baba ulipomuoa mama,
familia ya mama waliwahi kuja kwako na kuwapangia jinsi gani bora ya kuishi na familia
yako...mbona hayo hamyafikirii....’akasema huku akigeuka kumwangalia mama
yangu.Na mama akawa anamwangalia tu.
‘Kiukweli sio swali la kuniuliza hapa mbele ya kadamnasi, ni
kunizalilisha tu,ni kunitega tu ,sitaki maswali ya namna hiyo, nooh, now its too much...naona sasa
mnataka kunakila puani, mumeshanizalilisha vya kutosha, sasa ansema basi,
amueni mnalolitaka....’akasema kwa hasira huku akisimama na huku anamwangalia
mwenyekiti akiwa ametoa macho.
‘Huna haja ya kukasirika hivyo, na hoja uliyotoa, au kama ni swali uliloniuliza, halina msingi, ni kuonyesha jinsi gani usivyokuwa makini na ndoa yako,...kwanini tumefikia hapa, ni kwasababu umekiuka sheria za ndoa...hatukuja kuingilia ndoa yako, tumekuja kusikiliza mashitaka ....usitake kuturudisha nyuma....'akasema mwenyekiti.
'Na hilo swali kauliza mke wako,
anataka majibu, na ana maana yake kukuuliza hilo swali,kwa wenye hekima wanaelewa ni kwanini kakuuliza hivyo, hatumtetei, bali mimi kama mwenyekiti nimeona hekina ya hilo swali, kwahiyo, jibu swali baba,
usikwepe mada kwa jaziba, jaziba hapa hazitakusaidia kitu,hilo swali hata mimi naona lina umhimu wake, ili
kubainisha ukweli wako ndani ya moyo wako....jibu kama ulivyoulizwa.’akasema
mwenyekiti, na mume wa familia akainama kidogo, na watu walifikiria hatajibu,
lakini baadaye akainu akichwa na kusema;
‘Kwa hali iliyofikia naona
kama mnanilazimisha niseme hata yale yasiyostahili, sawa mimi nitasema ili
muweze kufanya mnayotaka, sitajali tena..nitajibu kama ifuatavyo...., hakuna asiye-elewa jibu la
swali hilo, japokuwa nafsi itatamani kusema vinginevyo, nakubali nimeshakubali kosa,
nakubali kuwa na sisi kutokana na umasikini wetu, tulikuwa katika harakati za
kutafuta maisha bora, na njia tuliyoona ni sahihi ni hiyo, kwa vile tulikuwa na
mwalimu wetu na yeye kwa kipindi hicho tulimuamini, ..hatukuwa na njia
nyingine...’akageuka kumwangalia docta.
‘Docta ataweza kunisaidia hilo, kuwa moyo wa binadamu
unakuwa na kitu kikishanasa kwenye moyo, inakuwa vigumu kukiondoa, kutegemeana
na mazingira,...tunaweza kujidanganya, tunaweza kujitahidi, lakini kama kitu
hicho kipo, kinaonekana kila siku, ..hutaweza kukisahau, huenda hilo ndilo kosa
lililotokea,...kama mwenzangu angeliolewa mbali kabisa, tukawa hatuonani,
huenda tungalisahauliana, lakini ukumbuke kuwa nyuma yetu alikuwepo Makabrasha,
anataka tutimize ahadi zake, mitihani ikawa mingi,..shauku na kutamani
kukanitawala....ni vitu ambavyo kama hujakutana navyo huwezi kuelewa...’akasema.
‘Swali bado lipo pale pale...hujalijibu kama linavyotakiwa
kujibiwa, je unampenda mpenzi wako wa asili, au tuulize hivi bado unampenda
mpenzi wako wa asili au ulikuwa ukimtumia tu, ili upate yale uliyokuwa
ukiyataka,....?’ akaulizwa na mwenyekiti.
‘Umeshasema mpenzi au
penzi la asili,...hilo kwa wengi, wanaolifahamu halifutikia,kuna watu walikuwa
na wapenzi wao wa asili, lakini hawakuoana, wakaenda kuoa wengine, lakini
moyoni bado ule upendo upo, ...siwezi kudanganya, nampenda, ...na ilikuwa ni
pendo la ujana, na la asili kama unavyosema, lakini sasa nimeoa, nina mke,
kwahiyo nafasi ya upendo wake kama mpenzi wa asili inafichika, unabakia upendo
kwa mume wangu..siwezi kusema haupo, upo,..na utaendelea kuwepo,kwa nafasi yake
na nafsi kubwa ni kwa mke wangu, nampenda sana mke wangu ...ndio maana
nikamuoa,...’akasema.
‘Hujaulizwa kuhusu mke wako, kuwa unampenda au la, vitendo
vyako vimeshajielezea,swali uliloulizwa ambalo ni muhimu kwako kulijibu ni je
bado unampenda mpenzi wako wa asili, ...au hayupo tena moyoni kwako, ikiwa na
maana ulikuwa unamyumia tu kukamilisha mambo yako....?’ akaulizwa swali hilo
tena.
‘Nampenda, sijasema kuwa simpendi, sio kweli kuwa nilikuwa
namtumia tu,upendo wetu haujafutika, ila ni kwa upendo huo wa kiasili, kwa hivi
sasa nina mke, kwahiyo mpenzi huyo wa zamani hana nafasi sawa kama ilivyokuwa
....ninaweza kusema hivyo, sina zaidi....’akasema na kuinama chini.
Mwenyekiti, mimi nimeshapata jibu la swali hilo, naomba
nieleweka hivyo,...’nikamwambia mwenyekiti na kumgeukia mume wa familia,
nikasema;
‘Nashukuru kwa jibu lako hilo, nimekuelewa, kama binadamu
hayo yapo...siwezi kuyapinga, lakini mlolongo mzima unajieleza, dhamira yenu,
ipo wazi, ....hayo maswali nimekuuliza kama nyongeza ili kusikia kauli yako kutoka
kwenye kinywa chako mwenyewe, kwani wenzako walishatamka yao kutoka moyoni,
wewe hukupenda kufanya hivyo kwa hiari yako mwenyewe, mpaka shinikizo la
ushahidi, sawa, hiyo ndio hulka yako hatuwezi kuigeuza..., sio shida,
nimeshakuelewa, ....’nikasema an kumgeukia mwenyekiti.
‘Ndugu mwenyekiti, mimi naona tufunge kikao, ili kila mtu
aweza kuyafikiria haya yote yaliyoongelewa hapa, na wanasheria, wayafanye kazi
kisheria, tufanye la msingi na kwa hekima, ile tuweze kujenga jamii yenye
kufuata haki na ukweli,...nafikiri tukiyafanya haya kwa familia moja moja,
jamii itabadilika,...na samahani sana kuwasumbua wazee wetu, nafahamu
mlihitajika kupumzika, lakini hili pia ni jukumu lenu, kama wazazi, naowaombeni
tena mkae mtumie hekima zenu, ili muone tutalitatuaje hili tatizo,na kwa upande
wangu na wa mwenzangu halikadhalika, tunahitajia muda wa kuliwazia hilo kwa
mapana zaidi.
‘Ila kiukweli, mimi napenda kusimamia kwenye haki, na haki
ya makubaliano ipo wazi,tulishakuabaliana na kurizia kuwa mkataba wetu uwe ndio
dira ya maisha yetu ya ndoa, na tulikuwa tunakwenda vyema tu, sasa limetokea
hili kubwa lao, kwanini tusahau yale tuliyokubaliana, kwa vile limemgusa
mtungaji, hapana, ni lazima tufike mahali tuseme sheria ni msumeno...kwahiyo
kitabu hiki,...mkataba huu, utasimamia kila kitu,...narudia tena, mkataba huu
ndio utasimamia kila kitu tulichokubaliana....’nikageuka kumwangalia mume wangu,
nilimuona akiniangalia kwa chuki, sikumjali tena.
Nikageuka kuwaangalia wanasheria wetu, huku nikiwa
nimekiinua kile kitabu cha mkataba wetu juu, na wao wakawa wanatikisa kichwa
kukubaliana name, halafu nikageuka kumwangalia mwenyekiti, na kuendelea kusema;
‘Lakini kwa sasa siwezi kusema zaidi naomba iwe hivyo kwa
sasa, labda ndugu mwenyekiti, kwa rizaa yako unaonaje tukikiahirisha hiki
kikao, akili yangu hapa haifanyi kazi tena,sijui tukuatane lini, kesho au kesho
kutwa, tatizo ni kuwa kuna wale wa kusafiri,..na kama ulivyosema kuna watu wa
usalama wapo nyuma yetu, sasa sijui.... tunaomba kama inawezekana wale wa
safari waahirishe safari zao, ni muhimu sana wakasikia kauli yangu ya mwisho
kuhusu jambo hili,na wakaona hukumu itakavyokuwa, kwani kila aliyeguswa na
hili, atahitaji, haki yake, au kuwajibika...
‘Sawa mke wa familia, lakini nakuonya, usiniingilie
uenyekiti wangu,...’akasema na kuangalia saa yake, halafu akageuka kuwangalia
watu, akasema;
‘Ni kweli, nikiaangalia saa muda umekwenda sana, na kuna
watu wapo hapa, japokuwa wanahusika kwa namna moja au nyingine, lakini wanakazi
zai, kuendelea kuwachosha hapa ni kuwatesa, yupo docta hapo, japokuwa kaniambia
yupo mapumziko, lakini anahitajia kupumzika, wapo mawakili wetu, na kulikuwa na
watu wa kusafiri kesho, tunaomba, ...kama ilivyoombwa, waahirishe safari
zao...’akasema na kumwangalia mke wa docta, na mke wa docta akasema;
‘Kwangu haina shida, nitaangalia, na muelekeo ulivyo, kama
nilivyokudokezea..’akasema na mwenyekiti
akamwangalia kwa mashaka, halafu
akageuka kuangalia wajumbe huku akisema;
‘Kwa upande wa binti yetu wa kufikia..oooh, hilo nitaongea
na mwenzangu, tutangalia kama inawezekana kuahirisha hiyo safari yake, maana
alishajiandaa kuondoka, hata hivyo kwa vile ni muhimu sana na inagusa hatima
yake na mtoto wake, tutaliangalia hilo, na nitawajulisha kesho asubuhi na
mapema kama kikao kipo au tupange siku nyingine
‘Hata hivyo wasi wasi wangu ni kwa watu wa usalama, nahitajia
kupata kibali chao, hili tatizo sio la ndani ya familia tu, tatizo letu
limegusa na maswala ya kijinai, ni muhimu sana mkalielewa hilo, kwahiyo kila
tunalolifanya kama familia, tunahitajika kuwajulisha wenzetu wa usalama, ili
tuweze kusaidiana nao, ndio jukumu letu kama raia wema,...
‘Kwa hivi sasa tunavyoongea hapa, wao , watu wa usalama wapo
kazini, wanahangaika kumtafuta muuaji wa Makabrasha, msifikiri kifo chake
kimefukiwa na mchanga, hapana, wanawajibika, usifikiri umesalamika kama
unahusika, kifo cha mtu kinamuandama mtendaji hadi siku anaingia kaburini, ...na
kwa taarifa tu, wapo katika kumnasa muuaji. Anaweza akawa miongoni mwetu,
hatujui, kwani kafanya hilo tendo kwa ujanja wa hali ya juu....’akakatiza
mazungumzo, kwani simu yake ilikuwa inalia, akaangalia mpigaji, akawaangalia
wajumbe, halafu akasema;
‘Samahani subirini kidogo niongee na watu wa usalama, naona
ndio hao wananipigia huenda kuna amri nyingine,...subirini kidogo msiondoke....’akasema huku akipokea hiyo simu...
NB: Haya tunasubiri hukumu..
WAZO LE LEO:Jehivi kweli kuna kisingizio cha kuisaliti ndoa yako? Je unaposalitiwa au kusaliti ndoa yako
kama mwanandoa unahitajika kufanya nini?. Ni maswali madogo lakini yenye mambo
makubwa, wewe kama mwanandoa kabla hujafanya kosa la kukiuka sheria za ndoa,fikiria
mara mbili, ni athari gani zitakazotokea baada ya tendo hilo,kwani matokea ya
dhambi hiyo ni kubwa sana, kitendo cha muda mfupi, lakini mazara yake yanaweza
kugharim maisha yako na athari kwenya familia yako. Tuweni makini.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
habari M3, plz post sehemu zinazoendelea hata weekend and public holidays niliomba wakati fulani ukaweka kama weekend moja halafu baaasi..
Post a Comment