Nikamjenga rafiki
yangu, ili aweze kusimama kwa miguu yake mwenyewe, lakini pia ili aweze
kunisaidia kibiashara. Tukaingia naye mkataba....
Nikawa kila mara nampa
kazi, au au wakati mwingine anapata kazi zake binafsi, na haikutokea siku
nikampa kazi, akaikataa,...na hata nilipoona umri unazidi kwenda, haolewi,
ndipo nikaja na wazo hilo la kumshauri kuwa atafute mwanaume wa kuzaa naye, na
hilo wazo akalifanyia kazi, na sasa ana mtoto, lakini ni nani mwanaume aliyezaa
naye, ikawa ni kitendawili. Hata hivyo, kwa vile mimi ni yule asiyekubali
kushindwa, niliamua ni lazima nimfahamu huyo mwanaume.
Lakini wakati nina
mikakati hiyo ya kumfahamu huyo mwanaume, likazuka tatizo la mume, mume wangu
akapatwa na ajali,..ajali ambayo ilianza kuleta sintofahamu nyingi, na hadi
ikafikia hatuoa nione kuwa kuna umuhimu wa kufanya uchunguzi, na ni nani ambaye
angenisaidia, hiyo kazi, hakuna mwingine ni huyu rafiki yangu, ambaye miongoni
mwa kazi yake ni ya kunifanyia upelelezi maswala yangu binafasi nay a kikazi,
...ndio nikamuita nikiwa hospitalini, ili tuongeee, na kumpa hiyo kazi, ikiwa
na masharti kuwa isijulikane, ....na hata rafiki ya mume wangu asijue kuwa
nimempa hiyo kazi, lakini...
Lakini nilihisi rafiki
wa mume wangu ameshafahamu huo mpango, lakini pia, nilijikuta katika wakati
mgumu, kwani yule niliyetegemea kuwa atanisaidia hiyo kazi, ...ambayo kwangu
niliiona ni kazi ndogo kwake, maana nilishampa kazi ngumu zaidi ya hiyo na
akafanya bila pingamizi, bila kulalamika, lakini kazi hii ikaiona ni mzigo
mzito..akaonekana kama , anaikataa kinamna
nikajikuta nikishikwa na mshangao..kwanini anaikataa hiyo kazi, japokuwa
hakukataa moja kwa moja, lakini kulalamika kwake, kuliashiria hivyo, hii sio kawaida yake...
‘Kuna nini
hapa....’nikajiuliza
endelea
*********
Nilikuwa bado
nimeshikilia ile simu mkononi, huku nikiongea na huyo rafiki yangu, na wakati
huo rafiki wa mume wangu alikuwa akinisubiria pembeni, na alipoona naongea na
simu, akaondoka, nafikiri kulekea huko alipolazwa mume wangu, ...nilitamani
nimsimamishe ili nimwambie twende wote huko alipolazwa mume wangu, lakini
niliona kuwa ni lazima nimalizane na huyo mtu ninayeongea naye kwenye
simu....nikasema kuongea na huyo rafiki yangu;
‘Sijakuelewa ina maana hutaweza kuifanya kazi hii kwa vile
...ok, nimekuelewa, na ni kweli ulihitajia miezi kama mwili kwa ajili ya kulea,...ni nitakuwa
nakufanyia vibaya kukushinikiza kwenye kazi, wakati unatakiwa uwe kwenye
mapumzika ya uzazi,-mateniti...., lakini bado unaweza kuifanya kwa muda wako, unaweza
ukatumia mbinu mbali mbali kujua hata bila ya wewe kwenda kufuatilia moja kwa
moja...wewe hilo halikushindii , naona kwako ni dogo sana, labda uniambie sababu
nyingine...’nikasema.
Nikasikia kama anavuta pumzi, ya mafua au kama mtu an
analia, ikabidi nimuulize;
‘Lakini mbona nakuona kama haupo sawa, nahisi kama unalia,
kuna tatizo jingine, au....?’ nikauliza.
‘Hapana nina mafua....na nimechoka, unafahamu kulea sio
mchezo, sikufahamu kazi hii ni ngumu kiasi hiki, na sitaki kutafuta mfanyakazi
kwa sasa, huyo niliyenaye anaweza kuifanya hii kazi, lakini nataka nihakikishe
nakaa na mtoto wangu kwa karibu sana, ..’akasema.
‘Huyo uliye nani ni nani, sikumbuki kumuona mfanyakazi hapo
nyumbani kwako?’ nikamuuliza.
‘Nilipojifungua tu, mama alinitumia huyo mfanyakazi,
sikutaka kuwakatalia, ....’akasema
‘Ok, hamna shida, kwahiyo kumbe utaweza kuwa na muda wa
kuifanya hiyo kazi, sio kwa kutoka, hapana, ina maana kazi ndogo ndogo, kama za
kufua,...kupika, kuna mtu wa kukusaidia, na kwa hiyo utaitumia simu yako na
mtandao kuifanya hii kazi niliyokupa, ...hilo nalo haliwezekani, suitake
nikufundishe kazi zako...’nikasema
‘Mara nyingi inapokuwa ni kazi yako sitaki niifanye ovyo....sitaki
nikuangushe, na ikizingatiwa kuwa akzi hii inagusa ndani ya familia yako, ina
maana nawachunguza nyie...kwahiyo ni kazi inayohitajia hekima,..ndio maana nahitaji
muda wa kulitafakari hili kwa makini, vinginevyo, tunaweza kuja kukosana kabisa.....’akasema
na mimi nikamdakia na kusema;
‘Sawa nimekuelewa, ...samahani sana, maana nimechukulia
mambo yangu ni muhimu hata bila kukujali wewe, ila nimefanya hivyo kwasababu
sikutaka kumuhusisha mtu mwingine, ..kwasababu sitaki kashifa...ndio maana
nikakuambia wewe, mimi na wewe tumetoka mbali, langu ni lako, nikiwa na shida
nakutegemea wewe..’nikasema na nikasikia kama anavuta pumzi na kitu kama
kwikwi...ilionekana dhahiri alikuwa analia. Sikutaka kumuuliza tena, nikasema;
‘Rafiki yangu, nakuomba, ingawaje sikuhitajia kufanya hivyo,
kwani ni moja ya majukumu yako,...lifanyie kazi hili, kama rafiki yako, sizani
kama utaona mume wangu anapotea ukae kimiya ni lazima tumtafute huyo mbaya
wetu, nafahamu hutashindwa kutumia njia nyingine yoyote, ilimradi tatizo hili
lisije likawekwa magazetini....’nikasema. Kikapita kitambo, halafu mapaka
nikahisi huenda keshakata simu, lakini muhemo wake wa kuvuta pumzi, na kuvuta
pua kama mtu mwenye mafua iliashiria kuwa bado yupo hewani, ..akasema;
‘Ngoja nikuulize kitu...huyo docta anasemaje, maana ninavyomfahamu
mimi mume wako na huyo docta ni kama mapacha walivyoivana na mara nyingi
wanakuwa pamoja kwenye majumba ya starehe, kwanini tusimtumie yeye, anaweza
kujua hilo...hajakudokezea lolote....?’akaniulizia
‘Hata mimi nilikuwa nawazia hilo hilo, nikajaribu kumdadisi..nmeongea
naye kwa mapana, tukiwa hapo hospitalini, lakini yeye alianza kwa kudai kuwa tatizo lipo,
au limeanzia ndani ya familia, yaani mimi na mume wangu tunaoenekana hatupo
pamoja, na hilo linaweza likawa ndio chanzo kikubwa. Eti ndio sababu za mume
wangu kuwa hivyo, eti huenda hana raha na mimi,..kwa vile huenda siwajibiki
kwake, kama mke wake,... kwahiyo anakunywa pombe kupita kiasi kuondoa hayo mawazo...’nikatulia
kidogo
‘Mimi sikubaliani na madai yake, na wazo lake hilo
haliniingii akilini..hivi kweli mtu anaweza kuwa na akili ndogo ya kuwazia hayo
...akakimbilia kujiathiri afya yake, kwasababu kama hiyo, wakati yeye ni
mwanaume,...kiongozi wa familia, si ndivyo ilivyo, kuwa mwanaume ndiye kiongozi
wa familia, sasa kwanini hilo limshinde....hainiingii akilini, kabisa.....’nikasema.
‘Lakini rafiki yangu, tuseme ukweli, wewe na shemeji mpo
shwari kweli, hakuna tatizo lolote kati yenu wawili ambalo haujawahi kuniambia?’
akaniuliza huyo rafiki yangu, nikageuka kumwangalia rafiki wa mue wangu ambaye
alikuwa karejea huko alipokuwa kaenda na safari hii alikuwa nay eye akiongea na
simu na alikuwa kanipa mgongo.
‘Kwanini unaniuliza hivyo?’ nikamuuliza
‘Rafiki yangu , nakubali hilo kuwa mimi na wewe tupo karibu
sana, lakini sio yote tunaweza kuambizana, kwa mfano mambo yako na mume wako ya
chumbani, hujawahi kuniambai kiundani, huwa tunaongea kwa juu juu tu, na sio
kwa kuelezea matatizo, mara nyingi unaongelea kwa kujisifia...nafahamu hilo kuwa
hayo ni mambo ya mke na mume....’akasema na mimi nikawa kimiya kusikiliza hoja
yake.
‘Na kwahiyo basi,
kama kweli unataka mimi niifanye hii kazi, ina maana mimi nahitajika kujua kila
kitu, na kazi hii huenda ikanibidi nianzie kwako, ili nijue undani wenu, kwa
mambo ambayo sio rahisi kwako kuniambia,....,mambo ya matumizi yako , mambo ya
ndani kabisa, yanakuhusu wewe na mume wako, je utakuwa tayari kuniambia
hayo,ndio maana naingiwa na shaka na hili unalotaka mimi nilifanye....’akasema.
‘Sijui kama hukunielewa vyema...mimi sijakuambia unichunguze
mimi na mume wangu tunavyoishi, mimi nataak umchunguze mume wangu, kama ana
tatizo nje ya familia, nje ya ndoa yangu....umesikia sana,.....’nikasema.
‘Huenda tatizo linatoka ndani kwenu, ...huenda tukajikuta
tunapoteza muda, kumbe chanzo cha haya yote ni wewe mwenyewe..ndio maana kwanza
nataka kukuuliza je hakuna tatizo ambalo wewe na mume wako hamjawahi
kutokusikilizana?’ akaniuliza na mimi nikakaa kimiya kidogo kutafakari, niliona
kama hajanielewa, au hataki kunielewa, lakini nikaona isiwe taabu kwa vile
nataka kazi hiyo ifanyike, basi nikamwambia;.
‘Unakumbuka siku moja niliwahi kukuambia kuwa nahisi kama
nina tatizo fulani japokuwa sio muhimu sana,...na sizani kama ni tatizo
linaloweza kumkwaza mtu mzima kama mume wangu, ...’nikatulia kidogo.
‘Hili tatizo lilianza nilipojifungua huyu mtoto wa mwisho,
sijui kimetokea nini, na sikuwa na haja sana ya kulifuatilia, maana niliona ni
jambo la kawaida tu, ....unasikia, eeh, tangu ujauzito, nilikuwa namchukia sana
mume wangu , hii haikuwepo kabla, ilianza pale nilipoanza hali ya mimba,..basi
ikawa ajabu mume wangu, akija tu naanza kujisikia vibaya, na akiongea jambo
nakasirika namkaripia kama mtoto mdogo, mapaka akawa ananiogopa, na ili kuondoa
shari, akawa ananikwepa, ...anaweza
akafika mara moja akanisalimia, huyoo, akaondoka zake, akirudi tena kalewa, na
mwanzoni kwa aibu ya kulewa hivyo, alikuwa akikimbilia kulala..labda ilianzia
hapo....’nikasema.
‘Lakini hayo si mambo ya ujauzito tu, ambayo nafahamu baada
ya kujifungua ulirudi kwenye hali yako ya kawaida, kwani hali hiyo ilikuja
kuendelea...au hakuna tatizo jingine ambalo linamsumbua mume wako,..au wewe mwenyewe
kiasi kwamba mnakuwa sio karibu sana, kama mume na mke..?’ akaniuliza.
‘Ni kweli hata nilipojifungua, nimekuwa sina hamu na mume
wangu, yaani sijisikiii kabisa....unajua ile kabisa...na kwa vile tupo bize na
kazi, mimi nimelichukulia powa tu, nikihisi na mwenzangu atakuwa hivyo
hivyo.....’nikasema na yeye akawa kimiya akisikiliza.
‘Na kwa hali kama hiyo, kwa vile sijisikii, na akili
imetekwa na kazi mara nyingi najaribu kumkwepa kwa kisingizio hiki na kile, na baya
zaidi linalonifanya nisiwe karibu sana nay eye ni hasa akiwa amekuja akiwa
amelewa, kwakweli hapo siwezi kumvumilia, namfukuza kabisa, hata kama ni kulala,
namwambia akalale chumba cha akiba..na kwa hali hiyo tumekuwa tunaishi tu..
hata hivyo , sioni kwamba hilo ni muhimu saana, kiasi cha mtu kukimbilia kulewa
zaidi na zaidi, ...mimi kwangu haina shida, na yeye keshalijua hilo ndio maana
hatugombani kabisa.. tumeshaliongelea na kukubaliana.’nikamwambia.
‘Mimi sijaolewa, na
hayo ni mambo ya kindoa zaidi , ila kwangu mimi naona hilo ni kosa, ....japokuwa
sijawahi kuolewa, lakini nafahamu sana mambo ya ndoa kinadharia, kama vile
nimeolewa, hasa mambo ya unyumba, waansema, usimpe mume wako kisingizio,...kwa
kuona hili au lile sio muhimu , au kwanini mimi nifanye hivyo tu.....’akasema.
‘Kuna sehemu nilisoma, na huyo mtaalamu alitoa onyo kwa
kusema, ukijifanya wewe hujali, ukampa mume wako mgongo, utakuja kujuta
mwenyewe, na mwisho wake utakuja kujilaumu, ukiwa umeshachelewa, ..na hatima ya
yote ni nani anayeumia, ni nani anayeathirika, utakuwa ni wewe mwanamke...na
chanzo ni nani, ukichunguza sana chanzo
ni wewe mwenyewe mwanamke kwa uzarau mambo kama hayo.....’akasema na mimi
nikawa kimiya
‘Hata hivyo rafiki yangu mimi hapo sioni tatizo kubwa sana..hapo,
kama umekubaliana na hiyo hali ipotezee tu, cha masingi kwa sasa nikuangalia
hali ya mume wako, apone, halafu mje make muongee, muweke mambo yenu sawa, msahau
ya nyuma,....mimi ndio ushauri wangu, na ukumbuke kuwa sisi ni marafiki na mara
nyingi tunashauriana kwa nia njema, na sio kwa kuingizana kwenye matatizo, ndio
maana hata wewe uliponishauri nitembee na mwanaume , hata kama ni mume wa watu, ili
tu nipate mtoto, sikulipinga hilo wazo, nikifahamu kuwa limetoka kwa mtu wangu
wa karibu, na wazo hilo limetoka kwa mwanandoa, kuonyesha kuwa hujali sana
mambo hayo...hujali hata kama mume wako atatembea na mwanamke mwingine.’akaniambia.
‘Wewe...wewe...unasema nini, ...nimekuelewa, na hilo ni
kawaida kwa watu ambao hawajaingia kwenye ndoa, tatizo lako ni kuwa hujaolewa,
ndio maana huoni kuwa hilo ni tatizo kubwa sana, ...mimi nasema hivi, chunguza
hili, na kama mume wangu ana kimada nje, au kadiriki kutemba na mke wa mtu, au
kimwanamke chochote, na huenda ikafikia kufumaniwa au kuzaa nje,sitamsamehe kwa
hilo, maana mimi sijawahi kuwa na mwanaume nje, wewe ni rafiki yangu
unalifahamu hilo sina tabia ya kuendekeza mapenzi, umalaya, ...sina tabia hiyo,
kazi kwangu ndio muhumu kuliko upuuzi huo..’nikasema.
Ikapita muda kidogo, na nikahisi kama kakata simu, na
nilipotaka kuongea yeye akasema kwa haraka haraka;
‘Rafiki yangu, nilivyosoma mimi kwenye darasa la wanandoa,
nilisikia wakisema kuwa kwenye ndoa
mapenzi sio upuuzi, ...nashangaa wewe unasema hivyo, sikutarajia kusikia hilo
kwa mwanandoa an msomi kama wewe...kwanini ifikie hapo, mimi sielewi, mimi
nakushauri tena, jaribu kufikiria sana hilo la kujenga umbali kati yako na mume
wako,...’akasema.
‘Hakuna kitu kama hicho, sijajenga hicho unachokiita umbali,
mnalikuza hili swala, na kukwepa tatizo jingine.....chunguza kama lipo tatizo
jingine, na hayo ya mimi na mume wangu nitayafanyia kazi...’nikasema.
‘Wewe nahisi umeona kazi ndio kila kitu kwako, na nashangaa
kwanini watu kama nyie mkakimbilia kuolewa, vinginevyo ungelibakia uwe kama
sisi, ambapo unajiamulia mwenyewe ufanye utakavyo,.ingawaje kwa hivi sasa
nafikia hatua ya kujuta maana umri unakimbia na sina mume, nahitajia mume
simpati...
'Tatizo ni kuwa wanaopatikana hawana tija,wanachojali wao ni tamaa zao za kimwili, na kwa ujumla,...siwataki, na ikifikia nikampata yule ninayesema ananifaa, wengi wao wanakuwa ni waume za watu, wewe umejaliwa
kupata mume lakini naona kama humjali, hutimiza wajibu wako wa ndoa, kwa hali
kama hiyo sioni kwanini ulalamike..’akasema rafiki yangu huyo na moyoni nikahisi
hali ya kuzarauliwa, japokuwa kwa upande mwingine, nilikiri kuna tatizo
natakiwa nilifanyie kazi, lakini sikutaka kumpa nafasi huyo rafiki yangu ambaye
hajawahi kuolewa anione mjinga.
‘Sikiliza nikuambie,... hilo nimeshalifahamu nitalifanyia
kazi, lakini hili ambalo nimekuambia, nataka lifanyiwe kazi, kamwe sitaweza kumvumilia
mume wangu atumie kisngizio hicho kwa kutafuta kimada nje, .., hilo siwezi
kukubali, eti nisikie katembea na mtu, na huenda kamjaza mwanamke mwingine mimba nje..yaani huo ni ushahidi tosha wa kunifanya
mimi nifanye kitu kibaya ambacho hataamini...nitamfanyia kitu ambacho, hataweza
kunisahau maishani, na huyo mwanamke wake ataikimbia nchi..kama ataweza, ....labda
awahi kuondoka kabla hajaingia mikononi mwangu...atajuta.’nikasema kwa hasira.
‘Mungu wangu unasema maneno gani hayo tena rafiki yangu,
mbona unanitisha...’akasema rafiki yangu
‘Sasa nakuomba, na hili sio kukuomba maana wewe ni rafiki
yangu, tumesaidiana mengi, mtafaute huyo kinyamkera, tumuonyeshe kazi,
siunafahamu zile zetu, sasa nataka ziwe kweli, tukimgundua tu huyo
mwanamke....haina haja ya kumpeleka polisi, ...adhabu naifahamu mwenyewe....’nikasema.
‘Utampa adhabu gani...’akauliza.
‘Mtu kama huyo...eeh,anahitaji kuharibiwa kabisa, tunawatafuia
watoto wa kihuni waliokosa radhi za wazazi wao, wanamharibu kabisa, yaani
kabisa, ashindwe hata kutembea...ili akome kabisa kutembea na wake za watu,
asipewe nafasi hiyo tena,..na nitataka wafanye hilo nikiwa naonaa kwa macho
yangu....kabisa kabisa, wanamuharibu kote kote...na sizani kama ataishi,
atajiua mwenyewe...’nikasema kwa hasira.
‘Mungu wangu, ...Eti nini, muogope mungu wako, ...usifanye
hivyo’akasema huyo rafiki yangu akiashiria wasiwasi, kitu ambacho sio kawaida yake, maana rafiki
yangu huyu ni kama mwanajeshi, ni jasiri, na ukimtuma jambo anaweza kulifanya
kama mwanaume wa ukweli....namuaminia sana, nikimpa kazi ambazo zinahitajia
ujasiri,anazifanya bila kusita,...imekuwaje kwa kazi hii naona kama sio yule
rafiki niliyemfahamu...lakini sikujali nikasema;
‘Anza hiyo kazi mara moja, nataka majibu kesho,...fuatilia
huko alipokuwa akistarehe, ulizia marafiki zake, na unaweza kuanza na docta
maana yeye ananificha, lakini wewe kwa jinsi ninavyokuamini utaweza
kugundua,....mengine tutakuja kuiongea na kama kuna kitu kinahitajia gharama
wewe niambie, nitakurushia salio, pesa sio tatizo...’nikamwambia na yeye akawa kimiya...kama
vile hayupo hewani.
NB: Je ni nini kitaendelea
WAZO LA HEKIMA: Kuna
usemi usemao, furaha ya maisha huanzia nyumbani, ni kweli ili tuwe na maisha
bora, ya amani na utulivu, ili tuwe na utendaji bora makizini kwetu, ni bora
tukaanza kuangalia shina la maisha yetu,... je kuna utulivu kwa wananoda, je
kuna hali nzuri kwenye familia zetu, je wafanyakzi wetu wanapata huduma muhimu
za kimaisha,...kwani hili ndilo shina la maisha yetu, ambali huanzia kwa mume
na mke, huanzia nyumbani kwenye familia
zetu..
Ni mimi:
emu-three
3 comments :
Mmh kazi ndio unaanza ushauri umemponza huyu dada, mkuki kwa nguruwe sasa imekula kwake.
Mmh kazi ndio unaanza ushauri umemponza huyu dada, mkuki kwa nguruwe sasa imekula kwake.
Analo mdada ushauri umemponza, jmn pole yake
Post a Comment