Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, October 21, 2013

MKUKI NI KWA NGURUWE-13



‘,.... ndio maana hata wewe uliponishauri nitembee na mwaume , hata kama mume wa watu, ili tu nipate mtoto, sikulipinga hilo wazo, nikifahamu kuwa limetoka kwa mtu wangu wa karibu, na wazo hilo limetoka kwa mwanandoa, kuonyesha kuwa hujali sana mambo hayo...hujali hata kama mume wako atatembea na mwanamke mwingine.’akaniambia.

‘Mtu kama huyo...eeh,anahitaji kuharibiwa kabisa, tunawatafuia watoto wa kihuni waliokosa radhi za wazazi wao, wanamharibu kabisa, yaani kabisa, ashindwe hata kutembea...ili akome kabisa kutembea na wake za watu...’nikamwambia nikiwa nimejaa hasira moyoni, na nahisi mtu kama huyo angelipatikana na tukaonana naye uso kwa uso, ningefanya jambo baya ambalo ningelikuja kujuta baadaye.

‘‘Anza hiyo kazi mara moja, nataka majibu kesho,...fuatilia huko alipokuwa akistarehe, ulizia marafiki zake, na unaweza kuanza na docta maana yeye ananificha, lakini wewe kwa jinsi ninavyokuamini utaweza kugundua,....mengine tutakuja kuongea na kama kuna kitu kinahitajia gharama wewe niambie, nitakurushia salio, pesa sio tatizo...’nikamwambia na yeye akawa kimiya...kama vile hayupo hewani.

Endelea na kisa chetu.

`Umanisika nilivyokueleza....?’ nikauliza pale nilipoona yupo kimiya lakini nilifahamu simu bado ipo hewani.

‘Nimekusikia lakini....’akataka kujitetea na mimi sikuwa na muda huo tena, nikamwambia;

‘Sitaki maelezo zaidi, au kuna nini kinachokufanya usite kuifanya hiyo kazi, ..kama unaona hutaweza basi niambie moja kwa moja, sio kujikanyaga kkanyaga, mbona sio kawaida yako ....kuna nini kinaendelea ambacho mimi sikijui...ukumbuke huo ni wajibu wako, au umesahau ?’ nikamuuliza

‘Mimi sijasahau hilo,...ila hata mimi ninakushangaa kukuona umenigeuka, unakumbuka ni wewe uliyenishauri kuwa nikatembee nje ili nipate mimba, na ukanishauri nitafute hata mume wa mtu, sasa naona ajabu wewe ukipaniki kiasi hicho, kwani huyo mume wa mtu uliyenishauri nikatembee nay eye ana tofauti gani na mume wako...au mkuki ni kwa nguruwe tu..’akaniuliza na mimi nikacheka kidogo na kusema kwa hasira;

‘Mume wangu huwezi kumlinganisha na waume wengine bwana, ...wewe acha hiyo kauli yako, mume wangu atembee nje..wewewee.....,kamwe usitoe kauli kama hiyo,  hilo sikubali, hilo sikubali,..piga ua, sikubali,....nisikiliza sana, acha maneno hayo, hapa tunachozungumizia ni mume wangu, sio waume wa wengine,....unafahamu, na kwanini usilione hilo lina uzito, huyo ni shemeji yako, ni mume wangu, mimi ni rafiki yako mpendwa, nilitarajia kuwa wewe ungeniunga mkono, kwa silimia nyingi,....’nikasema.

‘Rafiki yangu, ...huenda ni muda muafaka wa kuelezana ukweli, ...na mimi sikutarajia kuwa ingelifikia hatua hii, inaniuma sana, na kama ningelijua,....kama ....’akatulia, na mimi sikumuelewa ana maana gani, nikamuuliza.

‘Kwani kuna tatizo ganio rafiki yangu....?’ nikamuuliza na yeye akakaa kimiya, na hapo nikasema kwa sauto ya bosi kwa mfanyakazi wake.

‘Sasa kalifanyie kazi hili swala, maana kama unavyoona mimi nipo hospitalini, na siwezi kuondoka hapa kwa sasa, na huu ni wakati muafaka, wa kuweza kulifanya hili, ili mume wangu akipona, akute kila kitu kipo wazi,...ninachotaka mimi ni tumpate huyo mtu, na hiyo kazi kwako sio ngumu sana, wewe kama rafiki yangu mpenzi, nafahamu huwezi kuniangusha kwa hilo...’nikasema kwa ukali.

‘Siwezi kukuangusha ndio maana nataka tuliongelee ....nikueleze ukweli ulivyo...’akasema.

‘Huo ukweli tutaupata baada ya kufanya uchunguzi, wewe anza hiyo kazi mara moja.. tafuta mawasiliano tumia ujuzi wako ....kama tulivyozoea, wewe nakuaminia bwana, hiyo kwako ni kazi ndogo sana, hiyo ya kutafuta watoto wa kihuni niachie mwenyewe, kuna mabaunza fulani, nawafahamu, walishaifanya hiyo kazi kwa rafiki yangu mmoja,....’nikasema.

‘Mungu wangu....’akasema.

‘Yaani hawo jamaa ni pesa yako tu, huyo kinyamkera, alikuja kujiua baadaye..maana aliharibiwa, hata kutembea akawa hawezi, aibu, fedheha,....na akaona ni bora ajiue...’nikasema.

‘Lakini kwanini kufanya unyama wa aina hiyo wakati wewe mwenyewe ndio uliyetaka iwe hivyo, kuna haja gani ya kushauri jambo huku mwenyewe hutaki, au ...’akasema na mimi nikamwambia.

‘Naona hatuelewani, ..kafanye hiyo kazi , halfu nitakuja tuongee vyema, kwani rafiki wa mume wangu ananisubiri, ..anataka kuongea na mimi...’nikasema na kukata simu.

                                         **********

‘Haya niambie kuna habari gani huko, maana mambo yamekuwa mengi, nina mambo mengu yakufuatilia..?’ nikamuuliza, na yeye kwanza akanitupia jicho, halafu akageuka kuangalia pembeni. Nikamsogelea na tukaangaliana, na hapo nikagundua kama kuna kitu kinamsumbua, alikuwa kakunja uso wa hasira, na tulipoangalia,akaukunjua na kujifanya anatabasamu, na sikuwa na uhakika na hali hiyo kama ni kuhusiana na mume wangu, au ni kutokana na mazungumzo yetu ya awali.

‘Hakuna tatizo, mume wako yupo salama,...mambo mengine bado yapo kwenye uchunguzi,  na docta wamesema unaweza kwenda kuongea na yeye, lakini sio watu wengu, katoa tahadahari kuwa tusimzonge kwa maswali mengi, bado anahitajia muda wa kupumzika....kwahiyo hilo ni angalizo....’akaanza kusema.

‘Sijakuelewa shemeji, ongea ueleweke, sipendi mambo ya kufumba fumba, rafiki yako ana tatizo gani, je walipomchunguza wamegundua tatizo lolote, na je huo uchunguzi mwingine ni wa nini ...nataka unieleze kwa uwazi, sio kwa kunifumba fumba, mimi sio mtoto mdogo...’nikasema kwa hasira.

‘Sikiliza shemeji, ni kuwa  mume wako, bado yupo kwenye uchunguzi, lakini kwa silimia nyingi, hana tatizo, kwa hivi sasa kuna kitu ambacho wanakitilia mashaka, lakini sio rahisi kukigundua kwa haraka, kwani hayo maumivu ya mgongo na kiuno yanatokana na hitilafu kwenye uti wa mgongo, na hii itamfanya ashindwe kutembea kwa muda,...lakini ni kwa muda tu,na hatutakiwi kumshitua mgonjwa kwa hali hiyo....kingine ni kuwa kama kuna athari kwenye uti wa mgongo, kuna mengine yanaweza kuja kujitokeza, lakini sio rahisi kulitambua hilo kwa sasa ..’akasema na hakumalizia hizo athari nyingine ndipo nikamuuliza.

‘Kitu gani kinaweza kuja kujitokeza baadaye au kuna athari gani nyingine zinzweza kutokea?’ nikamuuliza

‘Hilo ndilo wanalifanyia kazi, kwasasa, bado lipo kwenye uchunguzi...lakini sio tatizo kubwa sana la kuwatia wasiwasi, cha muhimu, mnisikilize mimi, ndio maana nataka niwe naongea na docta, kwani mimi ni docta wa mambp hayo ya saikolojia, na wenzangu wanaweza kuongea kiutalamu, bila kujua kuwa anayemueleza, hana ufahamu mwingi wa mambo hayo, na kusababisha tafsiri nyingine ambazo sio kweli...’akasema.

‘Sawa nimekuelewa, ..lakini huenda kukatokea athari gani nyingine, hata kama ni huenda, nataka kujua tu..’nikasema.

‘Inawezekana ikamuathiri, asiwezi kuzaa...hiyo huwa inatokea, na atahri nyingine ndio kama hiyo kushindwa kutembea kwa muda, ....lakini hii ya kushindwa kutembea kwa muda, wameshaona, sio tatizo kubwa, kwani viungo vimeshaanza kufanya kazi,...’akasema.

‘Unaposema kuwa anaweza kushindwa kuzaa, una maana gani, maana mzaaji ni mwanamke, au sio, fafanua hapo, ...docta nieleze wazi, mimi sio mtoto mdogo....’nikasema kwa ukali na kabla huyo docta hajafafanua, .....

Mara akaja, docta aliyekuwa akimshughulikia mume wangu, na huyo rafiki wa mume wangu akamuwahi kabla hajafika pale tuliposimama, na kitendo hiki sikukipenda, niliona kama anazuia nisisikie jambo fulani, nikawasogelea na yule docta akasema kwa haraka;.

‘Mnaweza kwenda kumuona mgonjwa, yupo katika hali nzuri tu, ila kwa tahadhari, msimuongeleshe sana, na mengine bado tunayafanyia kazi, bado kuna vipimo havijakamilika, na bado yupo kwenye uchunguzi, ....kwa ujumla hali yake inaendelea vyema...’akasema na nilipotaka kuuliza swali, rafiki wa mume wangu akadakia na kusema,..

‘Hakuna shida docta, mimi nitahakikisha mgonjwa hapati shida, ...na tunashukuru sana, nitakuja tuongee vizuri....’akasema na yule docta akaondoka, na mimi nikageuka kumwangalia huyo rafiki wa mume wangu na kumuuliza.

‘Hivi kwanini unakuwa hivyo, inakuwa kama kuna jambo hutaki mimi nilisikie kutoka kwa huyo docta, mimi ni mke wa mgonjwa, nina haki ya kufahamu kila kitu...kwanini mnataka kuniweka roho juu...?’ nikauliza.

‘Sikiliza mimi ni docta, na pili mimi niliwahi kuwa mpenzi wako, nakufahamu ulivyo, ndio maana nataka habari zote kwako ziwe kwa maslahi yako, zisije zikakufanya ukawa na mshituko,..au ukawa na mawazo mengi, niamini mimi, nayafanya haya kwa nia jema kabisa..nilikupenda na nitaendelea kukupenda.’akasema na mimi nikamtupia jicho na kuangalia pembeni.

‘Wasiwasi wangu ni kuwa inavyoonekana kuna tatizo la kiafya kwa mume wangu, na hamtaki kuniambia, ndio wasiwasi wangu huo...’nikasema.

‘Ninachotaka hapa ni hekima, mara nyingi docta akisema mgonjwa wako anahisiwa kuwa tatizo, watu hulichukulia kama ndio tatizo, uvumi husambaa, na hata kumfikia mgonjwa, kwa hivi sasa hatutaki mgonjwa apate kitu cha kumuumiza kichwa, ....inaonekena ana mfadhaiko fulani unaomkera....’akasema.

‘Mfadhaiko....?’ nikauiliza kwa mshangao.

‘Ndio kuna jambo lina mkera, linampa shida,na kwa minajili hiyo, anajikuta hana amani...au nafsi inaogopa kuwa kutatokea jambo fulani baya..naweza kusema hivyo...’akasema.

‘Mhh, hapo sijui kama nitaelewa labda mpaka aniweke wazi....’nikasema.

‘Ndio maana nataka utumie hekima kubwa katika kuliongelea hili , tumia hekima sana kuongea na mum e wako, na kwepa sana kumshinikiza kwa maswali magumu na shutuma, ndio maana nilitaka wakati unaongea na yeye na mimi niwepo, kipindi kama hiki kwake ni kigumu sana, ... na hebu nikuulize, je mwenzako hajawahi kukuambia lolote kuwa ana hamu sana ya kupata mtoto wa kiume.....’akaniuliza.

‘Mtoto wa kiume...mmh, kwani linahusianaje nah ii ajali yake?’ nikauliza kwa mshangao.

‘Nauliza tu,...ni kutaka kudodosa huenda tukapata ukweli fulani.....’akasema.

‘Mhh, kwangu mimi mtoto ni mtoto bwana, kwanini watu msimwamini mungu, kama kweli wewe ni muumini wa mungu, unatakiwa umshukuru mungu kwa kukujalia mtoto au watoto,na sio utie dosari ya imani yako kwa kuangalia ni mtoto gani...kuna watu hawana watoto kabisa, hawo utasemaje..’nikasema.

‘Mimi sijasema lolote kuhusiana na utashi wangu, nimekuuliza tu je mume wako hajawahi kuliongelea hilo, kuwa anapendelea sana hivi sasa kupata mtoto wa kiume?’ akaniulizia.

‘Ameshasema mara nyingi,...na sio yeye tu, hata mimi naweza kusema hivyo,.... na hata mtoto wetu wa pili, tulitarajia kuwa huenda anelikuwa ni  kiume,....unakumbuka hata vipimo vya mwanza vya kuangalia tumboni, sijui ilikuwaje, walisema nina mtoto wa kiume....na tuliamini hivyo, lakini tukajifungua mtoto wa kike....lakini mimi nilifurahi sana, na hata sasa hivi kama nitazaa tena, hata akiwa wa kike, nitafurahia sana..sioni utofauti wake,...sina kasumba hiyo..’nikasema.

‘Lakini moyoni ungelipendelea upate mwanaume au sio?’ akaniuliza.

‘Kibinadamu ndio hivyo, maana sasa nina watoto wa kike, mtu unapenda kuwe na mchanganyiko, lakini hatujui mapenzi ya mungu, kwanini anapenda upate watoto wa kike tu au wa kiume tu...’nikasema.

‘Kwahiyo huamini sayansi, ...kuwa kuna jinsi unaweza ukafanya kukapatikana mtoto wa kiume au wa kike?’ akaniuliza.

‘Vyovyote ufanyavyo, mwisho wa siku muamuzi ni mungu, sipingi sayansi, maana nayo ina mchango wake mkubwa, ila nasemea ile hali ya kuchukia watoto, eti kwa vile umepata mtoto wa kike, ndio unakuwa huna raha, ...mwisho wa siku unakwenda kutembea nje, au kuachana na mkeo kwa kisingizio cha kutokukuzaliwa mtoto kiume...ni ujinga’nikasema.

‘Huo ni utashi wa kibiandamu, ndio maana nikakuuliza kuwa na wewe moyoni, hapo ulipo, ungelipendelea upate mtoto gani kwa hivi sasa, na umesema ungelipendelea upate mtoto wa kiume, huo ni utashi wa kibinadamu,..., ni hisia zetu ndivyo zilivyo...na kunakutofautiana katika kuzihimili hizi hisia zetu, ...na nahisi kwa mume wako ndio hivyo hivyo, ila yeye inaonyeha imemkaa sana moyoni, kushinda kujihimili....’akasema

‘Mimi sikatai kuwa kibinadamu, tunapenda tupate watoto mchanganyiko, sio mbaya, na ilivyo bora ni kukubali hali yoyote  kwa wema, kuwa yote ni mapenzi ya mungu, na usihalifu hayo mapenzi ya mungu ukakufuru kwa tamaa zako, unaweza ukatenda jambo likja kukuletea madhara,  ....lakini kinachotokea kwa nyie wanaume, ni kuhamaki na kutenda yale yasiyotakiwa..kwa pupa bila sitahimilivu...hamjui jinsi gani mnavyotuumiza sisi.’nikasema.

‘Huenda hayo yanayomtokea mume wako yanahusiana na hilo, ....’akasema.

‘Eti nini....na lipi?’ nikauliza kwa mshangao na nikajikuta nikihamaki na mara simu ya huyo rafiki wa docta  ikawa inaita na yeye akaangalia mpigaji na kusema;

‘Tutaongea baadaye hii simu ni muhimu sana...na naona ni vyema ukatangulia  tu kumuona mgonjwa, nakuja, ila kumbuka,....usimuulize maswali mengi ya kumuumiza kichwa’akasema docta huyo rafiki wa mume wangu, akisogea pembeni , huku akianza kuongea na hiyo simu yake, , na mimi kwanza nilikuwa ha hamasa ya kusikia kauli yake ya `huenda....’ lakini nikaona hilo halina haja kwa sasa.
Nilisimama kwa muda, huku nikishika kichwa na kwanza nikuna kichwa change kwa hasira na nywele zikavurugika,....yaani sijui nilikuwa najisikiaje....

Moyoni nikawa kama nawashwa washwa, nataka kujikuna .....nilikuwa naanza kujaa pumzi ya hasira, na sikuweza kuvumilia, nikasema kimoyomoyo,nikienda kuonana na mume wangu swali la kwanza ni kumuuliza kuhusu dhana hiyo, kuwa huenda alikwenda kutembea na wanawake nje, ili apate mtoto wa kiume, na huenda katika kufanya hivyo, ndio akaingia kwenye matatizo... je inawezekana kweli mume wangu kabadilika kiasi hicho, mbona siamini,....

Nikashika kichwa nikiwaza,;

‘Lakini kwanini niteseke kwa mawazo wakati muhusika yupo...kwanini nisiende kumuona na kumuuliza mwenyewe....’nikajisemea mwenyewe kwa sauti ya chini chini.

‘Hilo siwezi kuvumilia ni lazima nimuulize..’nikajikuta nasema kwa sauti kubwa, na kumbe huyo rafiki wa mume wangu alinisikia akageuka kuniangalia, na mimi sikumjali nikaharakisha kwenda huko kwa mgonjwa, na nilipofika mlango wa kuingia kwa mgonjwa, niligeuka nyuma, na huyo rafiki wa mume wangu akawa ananonyoshea mkono kuwa nisubiri kwanza...sikumsubiri nikaingia ndani kukabiliana na mume wangu...

                                                             **********
NB: Nimeona siku ya leo isipotee bure, soma sehemu hiyo ndogo,...kwa leo, na ujumbe huo hapo chini ni muhimu sana, na ukitaka kujua zaidi nenda hospitalini, uone watu wanavyoteseka na matatizo ya shinikizo la damu, kisukari, na kansa.....tuweni na huruma. Kama ni deni, kama ni kukosana kwa hili na lile tujaribu kujenga hekima  ya mongezi...tupendane, tuhurumiane...maana dunia ni mapito tu!

WAZO LA LEO: Mwili wa binadamu ni mdhaifu sana, na kosa dogo linaweza likaharibu utaratibu mzima wa mwili wa binadamu, mfano angalia wengi waliofikiwa na matatizo ya kupatwa na kiharusi, kupooza kwa viungo, ...ukichunguza sana utaona kuwa tatizo hilo lilitokea baada ya jambo dogo tu, kwako wewe mzima, uliona ni jambo dogo tu, lakini kwa mwenzako mwenye tatizo, anashindwa kuhimili, hasira kidogo, au  mshituko tu, na vitu kama hivyo, vimeharibu utaratibu mzima wa mwili wake, na kupelekea kupooza sehemu za viungo vyake.


Ni muhimu, tunapokabiliana na watu wenye matatizo kama hayo iwe ni matatizo ya moyo, shinikizo la damu, sukari, au vidonda vya tumbo, tuwe na hekima ya kuongea na hawo watu tujaribu kufuata masharti ya dakitari, na tusipuuze, maana tunaweza kuja kujuta wakati tumeshaharibu.

Ni mimi: emu-three

No comments :