Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, October 18, 2013

Mkuki ni kwa nguruwe-12



Nikamjenga rafiki yangu, ili aweze kusimama kwa miguu yake mwenyewe, lakini pia ili aweze kunisaidia kibiashara. Tukaingia naye mkataba....



Nikawa kila mara nampa kazi, au au wakati mwingine anapata kazi zake binafsi, na haikutokea siku nikampa kazi, akaikataa,...na hata nilipoona umri unazidi kwenda, haolewi, ndipo nikaja na wazo hilo la kumshauri kuwa atafute mwanaume wa kuzaa naye, na hilo wazo akalifanyia kazi, na sasa ana mtoto, lakini ni nani mwanaume aliyezaa naye, ikawa ni kitendawili. Hata hivyo, kwa vile mimi ni yule asiyekubali kushindwa, niliamua ni lazima nimfahamu huyo mwanaume.

Lakini wakati nina mikakati hiyo ya kumfahamu huyo mwanaume, likazuka tatizo la mume, mume wangu akapatwa na ajali,..ajali ambayo ilianza kuleta sintofahamu nyingi, na hadi ikafikia hatuoa nione kuwa kuna umuhimu wa kufanya uchunguzi, na ni nani ambaye angenisaidia, hiyo kazi, hakuna mwingine ni huyu rafiki yangu, ambaye miongoni mwa kazi yake ni ya kunifanyia upelelezi maswala yangu binafasi nay a kikazi, ...ndio nikamuita nikiwa hospitalini, ili tuongeee, na kumpa hiyo kazi, ikiwa na masharti kuwa isijulikane, ....na hata rafiki ya mume wangu asijue kuwa nimempa hiyo kazi, lakini...

Lakini nilihisi rafiki wa mume wangu ameshafahamu huo mpango, lakini pia, nilijikuta katika wakati mgumu, kwani yule niliyetegemea kuwa atanisaidia hiyo kazi, ...ambayo kwangu niliiona ni kazi ndogo kwake, maana nilishampa kazi ngumu zaidi ya hiyo na akafanya bila pingamizi, bila kulalamika, lakini kazi hii ikaiona ni mzigo mzito..akaonekana kama , anaikataa kinamna  nikajikuta nikishikwa na mshangao..kwanini anaikataa hiyo kazi, japokuwa hakukataa moja kwa moja, lakini kulalamika kwake,  kuliashiria hivyo, hii sio kawaida yake...

‘Kuna nini hapa....’nikajiuliza

endelea
                                                     *********
 Nilikuwa bado nimeshikilia ile simu mkononi, huku nikiongea na huyo rafiki yangu, na wakati huo rafiki wa mume wangu alikuwa akinisubiria pembeni, na alipoona naongea na simu, akaondoka, nafikiri kulekea huko alipolazwa mume wangu, ...nilitamani nimsimamishe ili nimwambie twende wote huko alipolazwa mume wangu, lakini niliona kuwa ni lazima nimalizane na huyo mtu ninayeongea naye kwenye simu....nikasema kuongea na huyo rafiki yangu;

‘Sijakuelewa ina maana hutaweza kuifanya kazi hii kwa vile ...ok, nimekuelewa, na ni kweli ulihitajia miezi  kama mwili kwa ajili ya kulea,...ni nitakuwa nakufanyia vibaya kukushinikiza kwenye kazi, wakati unatakiwa uwe kwenye mapumzika ya uzazi,-mateniti...., lakini bado unaweza kuifanya kwa muda wako, unaweza ukatumia mbinu mbali mbali kujua hata bila ya wewe kwenda kufuatilia moja kwa moja...wewe hilo halikushindii , naona kwako ni dogo sana, labda uniambie sababu nyingine...’nikasema.

Nikasikia kama anavuta pumzi, ya mafua au kama mtu an analia, ikabidi nimuulize;

‘Lakini mbona nakuona kama haupo sawa, nahisi kama unalia, kuna tatizo jingine, au....?’ nikauliza.

‘Hapana nina mafua....na nimechoka, unafahamu kulea sio mchezo, sikufahamu kazi hii ni ngumu kiasi hiki, na sitaki kutafuta mfanyakazi kwa sasa, huyo niliyenaye anaweza kuifanya hii kazi, lakini nataka nihakikishe nakaa na mtoto wangu kwa karibu sana, ..’akasema.

‘Huyo uliye nani ni nani, sikumbuki kumuona mfanyakazi hapo nyumbani kwako?’ nikamuuliza.

‘Nilipojifungua tu, mama alinitumia huyo mfanyakazi, sikutaka kuwakatalia, ....’akasema

‘Ok, hamna shida, kwahiyo kumbe utaweza kuwa na muda wa kuifanya hiyo kazi, sio kwa kutoka, hapana, ina maana kazi ndogo ndogo, kama za kufua,...kupika, kuna mtu wa kukusaidia, na kwa hiyo utaitumia simu yako na mtandao kuifanya hii kazi niliyokupa, ...hilo nalo haliwezekani, suitake nikufundishe kazi zako...’nikasema

‘Mara nyingi inapokuwa ni kazi yako sitaki niifanye ovyo....sitaki nikuangushe, na ikizingatiwa kuwa akzi hii inagusa ndani ya familia yako, ina maana nawachunguza nyie...kwahiyo ni kazi inayohitajia hekima,..ndio maana nahitaji muda wa kulitafakari hili kwa makini, vinginevyo, tunaweza kuja kukosana kabisa.....’akasema na mimi nikamdakia na kusema;

‘Sawa nimekuelewa, ...samahani sana, maana nimechukulia mambo yangu ni muhimu hata bila kukujali wewe, ila nimefanya hivyo kwasababu sikutaka kumuhusisha mtu mwingine, ..kwasababu sitaki kashifa...ndio maana nikakuambia wewe, mimi na wewe tumetoka mbali, langu ni lako, nikiwa na shida nakutegemea wewe..’nikasema na nikasikia kama anavuta pumzi na kitu kama kwikwi...ilionekana dhahiri alikuwa analia. Sikutaka kumuuliza tena, nikasema;

‘Rafiki yangu, nakuomba, ingawaje sikuhitajia kufanya hivyo, kwani ni moja ya majukumu yako,...lifanyie kazi hili, kama rafiki yako, sizani kama utaona mume wangu anapotea ukae kimiya ni lazima tumtafute huyo mbaya wetu, nafahamu hutashindwa kutumia njia nyingine yoyote, ilimradi tatizo hili lisije likawekwa magazetini....’nikasema. Kikapita kitambo, halafu mapaka nikahisi huenda keshakata simu, lakini muhemo wake wa kuvuta pumzi, na kuvuta pua kama mtu mwenye mafua iliashiria kuwa bado yupo hewani, ..akasema;

‘Ngoja nikuulize kitu...huyo docta anasemaje, maana ninavyomfahamu mimi mume wako na huyo docta ni kama mapacha walivyoivana na mara nyingi wanakuwa pamoja kwenye majumba ya starehe, kwanini tusimtumie yeye, anaweza kujua  hilo...hajakudokezea lolote....?’akaniulizia

‘Hata mimi nilikuwa nawazia hilo hilo, nikajaribu kumdadisi..nmeongea naye kwa mapana, tukiwa hapo hospitalini,  lakini yeye alianza kwa kudai kuwa tatizo lipo, au limeanzia ndani ya familia, yaani mimi na mume wangu tunaoenekana hatupo pamoja, na hilo linaweza likawa ndio chanzo kikubwa. Eti ndio sababu za mume wangu kuwa hivyo, eti huenda hana raha na mimi,..kwa vile huenda siwajibiki kwake, kama mke wake,... kwahiyo anakunywa pombe kupita kiasi kuondoa hayo mawazo...’nikatulia kidogo

‘Mimi sikubaliani na madai yake, na wazo lake hilo haliniingii akilini..hivi kweli mtu anaweza kuwa na akili ndogo ya kuwazia hayo ...akakimbilia kujiathiri afya yake, kwasababu kama hiyo, wakati yeye ni mwanaume,...kiongozi wa familia, si ndivyo ilivyo, kuwa mwanaume ndiye kiongozi wa familia, sasa kwanini hilo limshinde....hainiingii akilini, kabisa.....’nikasema.

‘Lakini rafiki yangu, tuseme ukweli, wewe na shemeji mpo shwari kweli, hakuna tatizo lolote kati yenu wawili ambalo haujawahi kuniambia?’ akaniuliza huyo rafiki yangu, nikageuka kumwangalia rafiki wa mue wangu ambaye alikuwa karejea huko alipokuwa kaenda na safari hii alikuwa nay eye akiongea na simu na alikuwa kanipa mgongo.

‘Kwanini unaniuliza hivyo?’ nikamuuliza

‘Rafiki yangu , nakubali hilo kuwa mimi na wewe tupo karibu sana, lakini sio yote tunaweza kuambizana, kwa mfano mambo yako na mume wako ya chumbani, hujawahi kuniambai kiundani, huwa tunaongea kwa juu juu tu, na sio kwa kuelezea matatizo, mara nyingi unaongelea kwa kujisifia...nafahamu hilo kuwa hayo ni mambo ya mke na mume....’akasema na mimi nikawa kimiya kusikiliza hoja yake.

‘Na kwahiyo  basi, kama kweli unataka mimi niifanye hii kazi, ina maana mimi nahitajika kujua kila kitu, na kazi hii huenda ikanibidi nianzie kwako, ili nijue undani wenu, kwa mambo ambayo sio rahisi kwako kuniambia,....,mambo ya matumizi yako , mambo ya ndani kabisa, yanakuhusu wewe na mume wako, je utakuwa tayari kuniambia hayo,ndio maana naingiwa na shaka na hili unalotaka mimi nilifanye....’akasema.

‘Sijui kama hukunielewa vyema...mimi sijakuambia unichunguze mimi na mume wangu tunavyoishi, mimi nataak umchunguze mume wangu, kama ana tatizo nje ya familia, nje ya ndoa yangu....umesikia sana,.....’nikasema.

‘Huenda tatizo linatoka ndani kwenu, ...huenda tukajikuta tunapoteza muda, kumbe chanzo cha haya yote ni wewe mwenyewe..ndio maana kwanza nataka kukuuliza je hakuna tatizo ambalo wewe na mume wako hamjawahi kutokusikilizana?’ akaniuliza na mimi nikakaa kimiya kidogo kutafakari, niliona kama hajanielewa, au hataki kunielewa, lakini nikaona isiwe taabu kwa vile nataka kazi hiyo ifanyike, basi nikamwambia;.

‘Unakumbuka siku moja niliwahi kukuambia kuwa nahisi kama nina tatizo fulani japokuwa sio muhimu sana,...na sizani kama ni tatizo linaloweza kumkwaza mtu mzima kama mume wangu, ...’nikatulia kidogo.

‘Hili tatizo lilianza nilipojifungua huyu mtoto wa mwisho, sijui kimetokea nini, na sikuwa na haja sana ya kulifuatilia, maana niliona ni jambo la kawaida tu, ....unasikia, eeh, tangu ujauzito, nilikuwa namchukia sana mume wangu , hii haikuwepo kabla, ilianza pale nilipoanza hali ya mimba,..basi ikawa ajabu mume wangu, akija tu naanza kujisikia vibaya, na akiongea jambo nakasirika namkaripia kama mtoto mdogo, mapaka akawa ananiogopa, na ili kuondoa shari,  akawa ananikwepa, ...anaweza akafika mara moja akanisalimia, huyoo, akaondoka zake, akirudi tena kalewa, na mwanzoni kwa aibu ya kulewa hivyo, alikuwa akikimbilia kulala..labda ilianzia hapo....’nikasema.

‘Lakini hayo si mambo ya ujauzito tu, ambayo nafahamu baada ya kujifungua ulirudi kwenye hali yako ya kawaida, kwani hali hiyo ilikuja kuendelea...au hakuna tatizo jingine ambalo linamsumbua mume wako,..au wewe mwenyewe kiasi kwamba mnakuwa sio karibu sana, kama mume na mke..?’ akaniuliza.

‘Ni kweli hata nilipojifungua, nimekuwa sina hamu na mume wangu, yaani sijisikiii kabisa....unajua ile kabisa...na kwa vile tupo bize na kazi, mimi nimelichukulia powa tu, nikihisi na mwenzangu atakuwa hivyo hivyo.....’nikasema na yeye akawa kimiya akisikiliza.

‘Na kwa hali kama hiyo, kwa vile sijisikii, na akili imetekwa na kazi mara nyingi najaribu kumkwepa kwa kisingizio hiki na kile, na baya zaidi linalonifanya nisiwe karibu sana nay eye ni hasa akiwa amekuja akiwa amelewa, kwakweli hapo siwezi kumvumilia, namfukuza kabisa, hata kama ni kulala, namwambia akalale chumba cha akiba..na kwa hali hiyo tumekuwa tunaishi tu.. hata hivyo , sioni kwamba hilo ni muhimu saana, kiasi cha mtu kukimbilia kulewa zaidi na zaidi, ...mimi kwangu haina shida, na yeye keshalijua hilo ndio maana hatugombani kabisa.. tumeshaliongelea na kukubaliana.’nikamwambia.

‘Mimi  sijaolewa, na hayo ni mambo ya kindoa zaidi , ila kwangu mimi naona hilo ni kosa, ....japokuwa sijawahi kuolewa, lakini nafahamu sana mambo ya ndoa kinadharia, kama vile nimeolewa, hasa mambo ya unyumba, waansema, usimpe mume wako kisingizio,...kwa kuona hili au lile sio muhimu , au kwanini mimi nifanye hivyo tu.....’akasema.

‘Kuna sehemu nilisoma, na huyo mtaalamu alitoa onyo kwa kusema, ukijifanya wewe hujali, ukampa mume wako mgongo, utakuja kujuta mwenyewe, na mwisho wake utakuja kujilaumu, ukiwa umeshachelewa, ..na hatima ya yote ni nani anayeumia, ni nani anayeathirika, utakuwa ni wewe mwanamke...na chanzo ni nani, ukichunguza sana  chanzo ni wewe mwenyewe mwanamke kwa uzarau mambo kama hayo.....’akasema na mimi nikawa kimiya

‘Hata hivyo rafiki yangu mimi hapo sioni tatizo kubwa sana..hapo, kama umekubaliana na hiyo hali ipotezee tu, cha masingi kwa sasa nikuangalia hali ya mume wako, apone, halafu mje make muongee, muweke mambo yenu sawa, msahau ya nyuma,....mimi ndio ushauri wangu, na ukumbuke kuwa sisi ni marafiki na mara nyingi tunashauriana kwa nia njema, na sio kwa kuingizana kwenye matatizo, ndio maana hata wewe uliponishauri nitembee na mwanaume , hata kama ni mume wa watu, ili tu nipate mtoto, sikulipinga hilo wazo, nikifahamu kuwa limetoka kwa mtu wangu wa karibu, na wazo hilo limetoka kwa mwanandoa, kuonyesha kuwa hujali sana mambo hayo...hujali hata kama mume wako atatembea na mwanamke mwingine.’akaniambia.

‘Wewe...wewe...unasema nini, ...nimekuelewa, na hilo ni kawaida kwa watu ambao hawajaingia kwenye ndoa, tatizo lako ni kuwa hujaolewa, ndio maana huoni kuwa hilo ni tatizo kubwa sana, ...mimi nasema hivi, chunguza hili, na kama mume wangu ana kimada nje, au kadiriki kutemba na mke wa mtu, au kimwanamke chochote, na huenda ikafikia kufumaniwa au kuzaa nje,sitamsamehe kwa hilo, maana mimi sijawahi kuwa na mwanaume nje, wewe ni rafiki yangu unalifahamu hilo sina tabia ya kuendekeza mapenzi, umalaya, ...sina tabia hiyo, kazi kwangu ndio muhumu kuliko upuuzi huo..’nikasema.

Ikapita muda kidogo, na nikahisi kama kakata simu, na nilipotaka kuongea yeye akasema kwa haraka haraka;

‘Rafiki yangu, nilivyosoma mimi kwenye darasa la wanandoa, nilisikia wakisema kuwa  kwenye ndoa mapenzi sio upuuzi, ...nashangaa wewe unasema hivyo, sikutarajia kusikia hilo kwa mwanandoa an msomi kama wewe...kwanini ifikie hapo, mimi sielewi, mimi nakushauri tena, jaribu kufikiria sana hilo la kujenga umbali kati yako na mume wako,...’akasema.

‘Hakuna kitu kama hicho, sijajenga hicho unachokiita umbali, mnalikuza hili swala, na kukwepa tatizo jingine.....chunguza kama lipo tatizo jingine, na hayo ya mimi na mume wangu nitayafanyia kazi...’nikasema.

‘Wewe nahisi umeona kazi ndio kila kitu kwako, na nashangaa kwanini watu kama nyie mkakimbilia kuolewa, vinginevyo ungelibakia uwe kama sisi, ambapo unajiamulia mwenyewe ufanye utakavyo,.ingawaje kwa hivi sasa nafikia hatua ya kujuta maana umri unakimbia na sina mume, nahitajia mume simpati...

'Tatizo ni kuwa wanaopatikana hawana tija,wanachojali wao ni tamaa zao za kimwili, na kwa ujumla,...siwataki, na ikifikia nikampata yule ninayesema ananifaa, wengi wao wanakuwa ni waume za watu, wewe umejaliwa kupata mume lakini naona kama humjali, hutimiza wajibu wako wa ndoa, kwa hali kama hiyo sioni kwanini ulalamike..’akasema rafiki yangu huyo na moyoni nikahisi hali ya kuzarauliwa, japokuwa kwa upande mwingine, nilikiri kuna tatizo natakiwa nilifanyie kazi, lakini sikutaka kumpa nafasi huyo rafiki yangu ambaye hajawahi kuolewa anione mjinga.

‘Sikiliza nikuambie,... hilo nimeshalifahamu nitalifanyia kazi, lakini hili ambalo nimekuambia, nataka lifanyiwe kazi, kamwe sitaweza kumvumilia mume wangu atumie kisngizio hicho kwa kutafuta kimada nje, .., hilo siwezi kukubali, eti nisikie katembea na mtu, na huenda kamjaza  mwanamke mwingine mimba  nje..yaani huo ni ushahidi tosha wa kunifanya mimi nifanye kitu kibaya ambacho hataamini...nitamfanyia kitu ambacho, hataweza kunisahau maishani, na huyo mwanamke wake ataikimbia nchi..kama ataweza, ....labda awahi kuondoka kabla hajaingia mikononi mwangu...atajuta.’nikasema kwa hasira.

‘Mungu wangu unasema maneno gani hayo tena rafiki yangu, mbona unanitisha...’akasema rafiki yangu
‘Sasa nakuomba, na hili sio kukuomba maana wewe ni rafiki yangu, tumesaidiana mengi, mtafaute huyo kinyamkera, tumuonyeshe kazi, siunafahamu zile zetu, sasa nataka ziwe kweli, tukimgundua tu huyo mwanamke....haina haja ya kumpeleka polisi, ...adhabu naifahamu mwenyewe....’nikasema.

‘Utampa adhabu gani...’akauliza.

‘Mtu kama huyo...eeh,anahitaji kuharibiwa kabisa, tunawatafuia watoto wa kihuni waliokosa radhi za wazazi wao, wanamharibu kabisa, yaani kabisa, ashindwe hata kutembea...ili akome kabisa kutembea na wake za watu, asipewe nafasi hiyo tena,..na nitataka wafanye hilo nikiwa naonaa kwa macho yangu....kabisa kabisa, wanamuharibu kote kote...na sizani kama ataishi, atajiua mwenyewe...’nikasema kwa hasira.

‘Mungu wangu, ...Eti nini, muogope mungu wako, ...usifanye hivyo’akasema huyo rafiki yangu akiashiria wasiwasi,  kitu ambacho sio kawaida yake, maana rafiki yangu huyu ni kama mwanajeshi, ni jasiri, na ukimtuma jambo anaweza kulifanya kama mwanaume wa ukweli....namuaminia sana, nikimpa kazi ambazo zinahitajia ujasiri,anazifanya bila kusita,...imekuwaje kwa kazi hii naona kama sio yule rafiki niliyemfahamu...lakini sikujali nikasema;

‘Anza hiyo kazi mara moja, nataka majibu kesho,...fuatilia huko alipokuwa akistarehe, ulizia marafiki zake, na unaweza kuanza na docta maana yeye ananificha, lakini wewe kwa jinsi ninavyokuamini utaweza kugundua,....mengine tutakuja kuiongea na kama kuna kitu kinahitajia gharama wewe niambie, nitakurushia salio, pesa sio tatizo...’nikamwambia na yeye akawa kimiya...kama vile hayupo hewani.

NB: Je ni nini kitaendelea


WAZO LA HEKIMA: Kuna usemi usemao, furaha ya maisha huanzia nyumbani, ni kweli ili tuwe na maisha bora, ya amani na utulivu, ili tuwe na utendaji bora makizini kwetu, ni bora tukaanza kuangalia shina la maisha yetu,... je kuna utulivu kwa wananoda, je kuna hali nzuri kwenye familia zetu, je wafanyakzi wetu wanapata huduma muhimu za kimaisha,...kwani hili ndilo shina la maisha yetu, ambali huanzia kwa mume na mke,  huanzia nyumbani kwenye familia zetu.. 
Ni mimi: emu-three

3 comments :

Unknown said...

Mmh kazi ndio unaanza ushauri umemponza huyu dada, mkuki kwa nguruwe sasa imekula kwake.

Unknown said...

Mmh kazi ndio unaanza ushauri umemponza huyu dada, mkuki kwa nguruwe sasa imekula kwake.

Unknown said...

Analo mdada ushauri umemponza, jmn pole yake