Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, September 4, 2013

WEMA HAUOZI-59


Mwanadada alifike nyumbani kwa mwanamama, akiwa hana gari lake, na alipofike eneo la nyumba hiyo, alimuona mwanamama, kakaa uwani, akiwa kajiinamia chini, akionekana mwingi wa mawazo.Mwanadada akamsogelea taratibu na kumshika bega ,mwanamama , na mwanamama, akainua kichwa kuangalia ni nani aliyemshika bega, na alipomuona kuwa ni mwanadada akasimama haraka na kuuliza;

‘Vipi anaendeleaje?’ akauliza akiwa anfahamu kuwa mwanadada katokea wapi, na mwanadada akageuka kuangali kule alipotokea na kusema;

‘Hajambo kidogo, bado hajazindukana, lakini wanasema uwezekano wa uhai upo, dalili zimeanza kuonekana, japokuwa sio uhakika wa moja kwa moja wa kuishi.....hawajatoa vile vifaa vya kumsaidia kupumua, angalau hiyo imenipa tumaini....’akasema na kugeuka kumwangalia mwanamama ambaye alionekana kuwa na mawazo mengi, hata zaidi ya mwanadada.

‘Mungu atamsaidia, maana kila siku namuota anacheza na mtoto, sijui kwanini namuota hivyo...’akasema mwanamama

‘Kwasababu unamuwaza sana, unamuwaza yupo na wewe karibu kama familia moja, ...au sio?’ akauliza mwanadada huku akitabasamu.

‘Kama familia moja ya baba mdogo, ukumbuke hilo, ...sio zaidi ya hapo, ni mtu ambaye alizoea kucheza na mtoto wangu, nahisi ndio sababu namuwaza hivyo , sina zaidi ya hayo,hata mtoto alishamzoea sana, na kila mara anamuulizia...’akasema na kumfanya mwanadada ageuke pembeni na kusema.

‘Kwa hali kama hiyo, ..huoni ni muhimu ukubali kurithiwa na yeye, awe baba watoto wako, maana akiondoka na kumuoa mkwe mwingine,anaweza asiwe karibu tena na wewe ,karibu na mtoto wako....’akasema

‘Nina uhakika akikuoa wewe tutakuwa karibu tu, ...sina shaka na hilo, hata hivyo, yote hayo ni maswala ya muda, watu tunasahau na maisha yanaendelea kinachoumiza ni kuwa yeye, yaani mwanasheria anaumwa, na yupo kwenye hali kama hiyo isiyotabirika...ndio maana tunamuwaza, tunamuonea huruma’akasema mwanamama.

‘Hebu niambie ukweli toka moyoni mwako, unampenda mwanasheria?’ akauliza mwanadada, na kumfanya mwanamama agune, na kugeuka kumwangalia mwanadada huku kakunja uso, japokuwa sio kwa kukasirika, akasema;

‘Swali gani tena hilo mwanadada, ilitakiwa mimi ndio nikuulize swali kama hilo, mimi sio binti kama wewe , mimi ni mama watoto, sihitajiki kuulizwa swali kama hilo, kupenda ilishapitwa na wakati..’akawa anaongea huku akimwangalia mwanadada kwa tabasamu, na mwanadada akawa kama anamkwepa wasiangaliane.

‘Unajua mwanadada, na ukiniuliza je upo tayari kupendana na mwanaume nitakuambia, sipo tayari...nimeshajiuzulu..mimi swala la kupendana, halinipi shida,hata kama ningelihitajia kuwa na mume, swala hilo lingelikuwa baki, ningeliangalia swala la kukubaliana, na kuridhiana.....’akasema mwanamama na mwanadada akamtupia jicho, huku akijaribu kutabasamu na mwanamama akawa kaangalia chini akitabasamu.

‘Siwezi kuamini hilo....upendo upo wakato wowote, hata muewe na umri gani, hicho ndicho kipimo cha kuishi pamoja na kuridhiana, kama hakuna upendo ni kudanganyana tu,...wewe unasema hivyo kwa vile imetokea hivyo, lakini nina uhakika, kama mwanasheria asingelikuwa kwenye hali kama hiyo, ya njia panda, kuwa amchague nani,  ungelikuwa tayari kuolewa na yeye maana nahisi unampenda, sisemi hivyo kwa wivu, bali nasema ukweli ulivyo,usinielewe vibaya...’akasema mwanadada.

‘Hivi huniamini mwanadada, wewe sasa ni ndugu yangu, wewe ni mdogo wangu, hivi kweli mnaweza kuchangia mume, mtu na mdogo wake,...?’ akawa kama anauliza halafu akatabasamu huku akiwa kainamisha kichwa, na huku akimwangalia mwanadada, na mwanadada alipobakia kimiya bila kusema neno, yeye akaendelea kuongea kwa kusema;

‘Kama kweli ningelikuwa na haja ya mwanaume, kwani yeye ndiye mwanaume peke yake hapa duniani, mimi sasa hivi nina akili ya kiutu uzima, siwezi kubabaishwa na mwanaume, mmoja, wakati wapo wengi, na kila siku wanazaliwa warembo, ..mbona wapo wengi na wazuri zaidi yake, na wameshanifuata kuniomba uchumba, lakini nimewakatalia...’akatulia kidogo.

‘Amini hivyo ninavyokuambia, mimi kinachonifanay nimuwaze sana huyo mwanasheria, ni kwa vile ni mtu tumemzoea na yupo kwenye hiyo hali, kila mtu anayemfahamu vyema, kwa tabia yake,na ukarimu wake, atamuonea huruma...’akasema mwanamama

‘Ni kweli tuyaache hayo...’akasema mwanadada huku akifungua mkoba wake na kutoa barua ya kutoka mahakamani,akaifungua na akawa kama anaisoma, halafu akasema

‘Na jingine ni kuwa kesho ni siku ya hukumu..’akasema mwanadada na kumfanya mwanamama amtizame kwa muda bila kusema neno, akitarajia mwanadada ataongeza neno zaidi kwani alikuwa kaishikilia ile barua kama vile anaendelea kuisoma, lakini mwanadada akawa katulia huku akiwa anaitizama ile barua.

‘Kwahiyo....?’ akauliza mwanamama.

‘Kwahiyo nini tena....ni kwenda mahakamani kusikiliza hukumu, na nina imani mtaalamu anaweza kufungwa miaka mingi, kama sio kifungo cha maisha...’akasema mwanadada.

‘Lakini namuonea huruma, kwa yale maneno yake, kuwa alikuwa akihangaika kuilinda ardhi kwa ajili ya vizazi vijavyo, ina maana huenda kweli eneo hili lina madini, sisi tumelikalia bila kujua manufaa yake..’akasema mwanamama.

‘Kila mahali kuna madini, kuna mali yenye thamani, lakini ni kwa umbali gani, au ni kwa utaratibu gani wa kuyapata... kuna utaratibu uliokubalika kisheria, maana nch haiendeshwi kwa hisia, za kila mtu anavyojisikia, hatuwezi kuvunja makazi kwa hisia kama hizo, kama kweli yapo, muda muafaka utafika, na makazi ya watu yanaweza kusogezwa sehemu nyingine, huo ndio utaratibu mwema...’akasema mwanadada.

‘Na wakati kama huo ukifika, kweli unafikiria kuna kulipwa fidia tena hapo, na je huenda sis tumeshajifia, au huenda kama alivyosema, tukafukuzwa neo hilo waje kuchukua wawekezaji...’akasema mwanamama huku akionyesha mashaka, na akawa anageuka kuangalia eneo hilo, akilikagua kwa macho.

‘Cha muhimu ni kuwa una hati miliki, hiyo diyo itakulinda, kuwa unamiliki hi ardhi kwa miaka kadhaa, kwahiyo akija mumwekezaji wewe utamkodi, na kuwa na mamlaka na eneo lako,serkali haiwezi kuwatupa wananchi wake, ikifanya hivyo, basi hiyo sio serkali, ni sirikali, ....Cha muhimu kwasasa na ambalo ndilo nalihangaikia, ngoja kesi iishe, tukamilikishe maswala ya hati miliki kwa jina lako...na ukitaka na la mtoto wako’akasema mwanadada.

‘Ina maana ni mpaka kesi iishe, hukusikia alivyosema mwanasheria?’ akauliza mwanamama.

‘Ndio ukumbuke eneo hili lipo kwenye kesi mahakamani huhitajiki kufanya lolote mpaka hukumu ipite, Na nina uhakika kuwa kesho siku ya hukumu tutauwa ndege wawili kwa jiwe moja....’akasema mwanadada

‘Una maana gani kusema hivyo?’ akauliza mwanamama.

‘Ni kuwa hukumu ya kes I hiyo, itatoa mamlaka ya wewe kurejeshewa mali zako zote, ikiwemo shamba na kumilikishwa kisheria, na wakati huo huo huyo anayejiita mtaalamu atawajibika, mali yake yote itapigwa mnada, na kutoa fidia kwa waathirika wote waliotokana na mipango yake ya kitapeli, ikiwemo kumtibia mama mkunga,....’akatulia.

‘Tuna mpango apelekwe nje, akatengenezwe ngozi yake vyema,.....na inawezekana maana pesa ipo,...’akasema mwanadada kwa kujiamini.

‘Pesa ipo kutoka kwa huyo huyo mtaalamu, hilo nimeshalijengea hoja,....halina utata, lakini pia kutokana na kesi hii, mengi yamejulikana kichwani mwa watu, watu sasa hivi wataamuka kudai haki zao, awe mwanaume, au mwanamke,  hakutakuwa na usumbufu tena na watu kama hawa...’akasema mwanadada akionyesha furaha.

‘Kweli hatimaye naanza kuamini..’akasema mwanamama

‘Kuamini nini?’ akauliza mwanadada

‘Kuwa wema, wakati wote ni kinga ya matatizo, wema, huwa ni kama taa inayokumilikia njia, hasa wakati kukiwa na giza na hakuna namna nyingine ya kupata mwanga. Wema, kamwe hauozi, tenda leo, au kesho au miaka mingi iliyopita, wema utakusubiria, wakati ukiwa na shida. Hii yote tumefanikiwa kwasababu ya matendo yetu mema, kwa jamii, nakushukuru sana mwanadada, ....sijui nitakulipa nini...’akasema mwanamama

‘Mimi ninatalipwa tu, kutoka kwa huyo huyo Mtaaalmu, unafahamu mali yake ina thamani gani, ina thamani ya mabilioni ya pesa, na kumegundulika vito vingi vya thamani ndani ya handaki lake vikiwemo madini, na pesa za kigeni.....’akasema mwanadada na wote wakakaa kimiya kwa muda, halafu mwanamama akauliza swali

‘Lakini nikulize swali uligunduaje kuwa  mtaalamu ndiye yupo nyuma ya haya yote?’ akaulizwa

‘Unapofanya kazi hii, unakuwa na hisia ya ziada, ....na mara nyingi, sisi kama mawakili, tunajeng hoja zetu pale tunapokuhoji, maelezo yako ndiyo yatatupa dira, na muelekeo wa jambo jingine, na ndivyo ilivyofanyika kwenye kesi hii...’akasema mwaandada.

‘Mtaalamu alijifanya ana akili sana, akayapanga mambo yake kiakili na kuwafanya wengine wajinga, hakujua kuwa ipo siku atajikanyaga, ...japokuwa kwakweli aliifanya kazi hiyo kwa namna ya kipekee, kwani amekuwa akiwahadaa watu kwa miaka mingi bila kulitambua hilo, na amekuwa akiwa na sura mbili bila watu kumtambua,lakini nilihisi kuwa kutoweka kwake, sio kama anavyodia eti ni mizimu, nilihisi alikuwa akiogoap jambo ....’akatulia mwanadada.

‘Alikaa huko alipokuwa kajificha akijenga hoja na jisni gania anaweza kurejea kwa jamii,na alipoweka mambo yake sawa, ndio akajitokeza...’akasema mwanadada.

‘Alifika akiwa kajiamini akijua wananchi ni mbumbumbu, atawahadaa kwa mmbo yake,hakujua na sisi tulihamshuku, kutokana na matendo yaliyotokea nyuma, kwanini alitoweka ghafla, alipojitokeza tukawa tunaanza kujuenga hoja...’akatulia mwanadada.

‘Ukiangalia siku ile ya uchomaji wa nyumba ya mama mkunga, alijua kabisa kuwa ndugu yake huyo atakuwa hayupo, akachukua mwanya huo na kujifanya yeye ndiye kiongozi wa kijiji, hatukuwa tunafahamu kuwa ni yeye, utambue hilo, lakini tulijiuliza ni nani huyu aliyemuita mume wa mama mkunga...kuna mtu hapa kajificha ni nani, ni jemedari, ni kiongozi mwenyewe wa kijiji.

‘Ukumbuke kuwa wakati mzee huyo anafika nyumbani kwa mjumbe, alisema kuwa alishangaa kuona kiongozi huyo wa kijiji hayupo na alipomuuliza mke wakiongozi wa kijiji , mke huyo akawa anashangaa, na kuwambia kuwa mbona mume wake hayupo, kaondoka toka mchana....na mzee huyo akabakia akiwaza kuna nini, na yeye hakuwa na mashaka kuwa kuna lolote litatokea huko kwake..akawa anaongea na mke wa kiongozi huyo wa kijiji kwa muda kidogo , na baadaye akarejea kwake, na kukuta moto ukiwaka,....

‘Lakini pia, mzee huyu alisema kuwa wakati anafika, alimuona mtu akitokea mlango wa nyuma, ambapo ni sehemu mara nyingi, anaishi mtalaamu, kama akiwa na shida zake, ukumbuke kuwa mtaalamu japokuwa ana nyumba, lakini kwa vile hana mke, yeye alikuwa akija kukaa kwa kaka yake huyo, na nyumba yake alipangaisha,...na mzee alisema aliyemuona akitoka kwa mlango wa nyuma  ana uhakika ni kiongozi wa kijiji... huenda hilo alilipana hivyo mtaalamu, lakini pia ni kosa moja wapo alilolifanya...’akasema mwanadada.

‘Hapo kuna kosa gani?’ akauliza mwanamama.

‘Kama kiongozi wa kijiji alikuwa hayupo, mzee aliitwa na nani, na huyo aliyetokea mlango wa nyuma ni nani, ina maana mke wake ni muongo, yule mama sio muongo, tulimpima na tukagundu akuwa alichokuwa akiongea ni sahihi...na ukumbuke kuwa mama mkunga aliona mtu akielekeza jinsi ya kuchoma nyumba yake, na alisema alimuona kiongozi wa kijiji, huyo kiongozi wa kijiji ni yupi, maana kweli kiongozi wa kijiji alikuwa hayupo ,...’akasema mwanadada.

‘Lakini kama alipanga hivyo kiongozi wa kijiji, si ndio angedanganya hivyo kuwa akondoka kumbe kajificha mahali’akasema mwanamama.

‘Hiyo ingeliwezekana, na kwa mpango wa mtaalamu ilitakiwa ionekane hivyo, lakini tulipofika huko ambapo kiongozi wa kijiji alikwenda tuliambiwa kweli alikwua huko, na kikao kilikuwepo, na hakikuisha hadi usiku wa manane, ambapo nyumba ya mama mkunga ilikuwa imeshachomwa moto....ushahidi huo tuliupata, hakuna mashaka....’akasema mwanadada.

‘Angalia sumu iliyotumika kumuua Jemedari, yule mtu aliyetumwa,alisema aliondoka na chupa, lakini uchunguzi, uligundua chupa iliyokuwa na sumu ilipatikana pale mezani, karibu na kitanda cha marehemu, ni nani aliileta hiyo chupa, na ninani angeligundua kuwa sumu ile ya mwanzo isingelifanya kazi, na alihitajika kuleta sumu nyingine ili kutimiza lengo lililokusudiwa. Ni huyo huyo aliyepanga haya, na ni lazima huyo awe mtaalamu wa kutengeneza hizo sumu....hapo nilihiisi kuna jambo, kuna mtu mwingine nyuma ya pazia...’akasema mwanadada.

‘Ukirudi nyuma, siku alipopotea yule binti wa mkuu wa kitengo cha upelelezi, ni nani aliyemrejesha nyumbani, ...ni huyo mtaalamu, japokuwa huyo binti hakuwa muwazi, lakini aliweza kuongea kidogo kwa rafiki wake wa kiume,...na alisema alikuwa kwenye nyumba iliyojengwa ndani ya pango...na ndiyo siku niliyokuwa na hamu sana ya kuongea na huyu mtalaamu, lakini hakuwepo...nikajiuliza huyu mtu atakuwa kaenda wapi, ni kweli katoweka kimzimu kama anavyodai, ...na aliporejea tena, nikataka kumdadidi hayo, akatunga uwongo wake.......’akasema mwanadada.

‘Siku hiyo nilipokuatana na huyu mtaalamu, akiwa katokea huko msituni, akaniambia kuwa yupo tayari kuelezea yale anayoyajua, kwani kaagizwa na mizimu, nikamtilia mashaka, japokuwa alipanga mambo yake kwa utaalamu...lakini kwenye maongezi yake,nikagundua udhaifu fulani, ...alijuaje yote hayo...na kumbe yey ndiye mtaalamu wa kutengeneza hizo sumu....na nilipoanza kumfuatilia nikaanza kugundua kimoja baada ya kingine, na kumbe, wanafanana na kiongozi wa kijiji..hilo lilijificha sana..’akasema mwanadada.

‘Hilo la sura yake lilijificha kwasababu alikuwa hapendi kubadili mavazi yake, ambayo yalikuwa yakifunika pia sehemu kubwa ya uso wake, na kubakia sehemu hii ya mbele tu....na ndevu zake za kiaina, ambazo alikuwa akizivaa...’akasema mwanadada

‘Ina maana hata zile ndevu sio zake, za asili?’ akauliza mwanamama.

‘Anazo ndevu zake za asili, lakini mara nyingi huzinyoa kama anavyofanya kiongozi wa kijiji, huzinyoa na kubadika hizo za bandia, ili akizitoa afanane na kiongozi wa kijiji’akasema mwanadada.

‘Lakini ukiangalia alivyopanga, mbona inaonekana kama kweli alifanya hivyo kwa ajili ya kulinda ardhi na maliasili ya kijiji, kutokana na hoja yake?’ akauliza tena mwanamama

‘Sio kweli....hawa watu ni wajanja sana, wanafahamu jinsi gani ya kuwavuruga watu wakili zao....’akasema mwanadada huku akitikisa kichwa na kuwa kama anawaza jambo, na mwanamama akamwangalia kwa makini halafu akasema;

‘Basi kama ni hivyo, huyo kweli ni mtaalamu...’akasema mwanamama

‘Huo sio utaalamu... utaalamu gani wa hadaa, wa kutumia mbinu kuwatapeli wenzako, kuhadaa jamii, unyang’anyi na ubakaji, ushirikina,huo sio utaalamu, ni ujinga,..utaalmu wa kupata kwa kutumia migongo ya wenzako, ..hapana huo sio utaalamu, utaalamu ni ule unaotokana na jasho lako, mikono yako na akili yako  kwa manufaa ya watu, ya jamii...’akasema mwanadada.

‘Lakini hukusikia hoja yake kuwa alifanya hayo kwa minajili ya kulinda maliasili ya kijiji, kwa ajili ya vizazi vijavyo?’ akaulizwa mwanamama.

‘Hiyo ndio hoja yake, lakini hoja hiyo aliitunga kichwani, na watu kama hawa hujaribu kutafuta hoja ya kusimamia, ...na kujipa moyo kuwa anachofanya ni sahihi kutokana na hoja hiyo, ..hata viongozi wa siasa, wa dini, wa makabila, wote hutafuta hoja ya kusimamia, ikilenga matakwa na msilahi yake binafsi, ilimradi ajifanye, asionekane ni mkosaji na huijengea hoja yake hiyo ushahidi na mashahidi..’akasema mwanadada.

‘Lakini tukumbuke kuwa hoja, isiyo ya kisheria, hoja isiyokubalika na jamii, hoja yenye maangamizi, haina tija, na mwisho wa siku hoja hiyo hiyo itakuumbua tu maana sio wote wajinga, sio wote watakaa kimiya, ssheria ipo, utaratatibu uliokubalika na jamii, upo, maandiko matakatifu yapo, katiba ipo, ina maana wote watakuwa hawachunguzi hayo, hata kama umjanja kisia gani, lakini dhuluma haidumu, na uovu hauna mshiko, una mwisho mbaya...’akasema mwanadada.

‘Ni kweli mpendwa nakuaminia, ngoja tusubiri hukumu, maana huwezi kujiaminisha, moja kwa moja, tulijiaminisha kwenye kesi yetu ya kwanza, kumbe kuna mambo yalifanyika, na tukaonekana tumeshindwa, 
...siwezi kuamini mpaka hakimu atamke mwenyewe...’akasema mwanamama.

‘Ni kweli uhalali wa kushinda ni pale hakimu atakapoginga rungu lake chini, baada ya kusoma hukumu, lakini huo ndio ukweli, na ukweli haujifichi,...twende tukamuona mgonjwa, maana nahisi moyo ukienienda mbio, ....’akasema mwanadada.

‘Hata mimi....nahisi hivyo hivyo, lakini ..mungu yupo nasi, na kwa wema wake, mungu atamsaidia atapona, tutakuwa naye, kama shemeji yangu, baba mdogo wa mtoto wangu..’akasema mwanamama

‘Mhh, sio mbaya akiwa baba halisi,mimi niko radhi, ...au unelipenda tuishi kama wake wenza...eti unaonaje haitapendeza hiyo...?’akasema mwanadada huku akicheka , na mwanamama akawa anamwangalia kwa 
mashaka,na mshangao na kuuliza

‘Eti nini...umechanganyikiwa nini,...hahaha...haipo hiyo, ?’

‘Je kama mwanasheria aking’ang’ania, na unavyoona, afya yake itakuwa njema zaidi akipata kile akipendacho, na moja ya wazo lake ni kuwa sisi tuishi kama wake wenza, utamkatalia,...?’akauliza mwanadada.

‘Mimi sipendi hayo mawazo yao....ooh, mbona unaleta mambo nisiyoyafikiria kwanini umesema hivyo?’ akauliza mwanamama na mwanadada akatabsamu na kuangalia chini, huku akimuwaza mwanasheria, akitamani amkute keshainuka kitandani, na moyo akahidi kutimiza kila atakalolitaka, hata kama hatalifurahia.

NB: Haya tuendelee kuwepo pamoja.


WAZO LA LEO: Tunapokuwa viongozi, wa aina yoyote ile, na tukawa na mamlaka, na maamuzi ya kufanya jambo, tusitumie mwanya huo vibaya, tukahalalisha yale yasiyo sahihi kwa masilahi yetu,tukumbuke uongozi dhamana, na dhamana ni deni, sio mali yako. Timiza wajibu wako kwa uadilifu,hiyo iwe ndio dira yako.
Ni mimi: emu-three

1 comment :

Yasinta Ngonyani said...

Bonge la simumulizi inasisimua ila du kupenda kuwa na mke mwenza? ..Kazi kwelikweli