Mwanadada alifike nyumbani kwa mwanamama, akiwa hana gari
lake, na alipofike eneo la nyumba hiyo, alimuona mwanamama, kakaa uwani, akiwa
kajiinamia chini, akionekana mwingi wa mawazo.Mwanadada akamsogelea taratibu na
kumshika bega ,mwanamama , na mwanamama, akainua kichwa kuangalia ni nani
aliyemshika bega, na alipomuona kuwa ni mwanadada akasimama haraka na kuuliza;
‘Vipi anaendeleaje?’ akauliza akiwa anfahamu kuwa mwanadada
katokea wapi, na mwanadada akageuka kuangali kule alipotokea na kusema;
‘Hajambo kidogo, bado hajazindukana, lakini wanasema
uwezekano wa uhai upo, dalili zimeanza kuonekana, japokuwa sio uhakika wa moja
kwa moja wa kuishi.....hawajatoa vile vifaa vya kumsaidia kupumua, angalau hiyo
imenipa tumaini....’akasema na kugeuka kumwangalia mwanamama ambaye alionekana
kuwa na mawazo mengi, hata zaidi ya mwanadada.
‘Mungu atamsaidia, maana kila siku namuota anacheza na
mtoto, sijui kwanini namuota hivyo...’akasema mwanamama
‘Kwasababu unamuwaza sana, unamuwaza yupo na wewe karibu
kama familia moja, ...au sio?’ akauliza mwanadada huku akitabasamu.
‘Kama familia moja ya baba mdogo, ukumbuke hilo, ...sio
zaidi ya hapo, ni mtu ambaye alizoea kucheza na mtoto wangu, nahisi ndio sababu
namuwaza hivyo , sina zaidi ya hayo,hata mtoto alishamzoea sana, na kila mara
anamuulizia...’akasema na kumfanya mwanadada ageuke pembeni na kusema.
‘Kwa hali kama hiyo, ..huoni ni muhimu ukubali kurithiwa na
yeye, awe baba watoto wako, maana akiondoka na kumuoa mkwe mwingine,anaweza
asiwe karibu tena na wewe ,karibu na mtoto wako....’akasema
‘Nina uhakika akikuoa wewe tutakuwa karibu tu, ...sina shaka
na hilo, hata hivyo, yote hayo ni maswala ya muda, watu tunasahau na maisha yanaendelea
kinachoumiza ni kuwa yeye, yaani mwanasheria anaumwa, na yupo kwenye hali kama
hiyo isiyotabirika...ndio maana tunamuwaza, tunamuonea huruma’akasema
mwanamama.
‘Hebu niambie ukweli toka moyoni mwako, unampenda mwanasheria?’
akauliza mwanadada, na kumfanya mwanamama agune, na kugeuka kumwangalia
mwanadada huku kakunja uso, japokuwa sio kwa kukasirika, akasema;
‘Swali gani tena hilo mwanadada, ilitakiwa mimi ndio
nikuulize swali kama hilo, mimi sio binti kama wewe , mimi ni mama watoto,
sihitajiki kuulizwa swali kama hilo, kupenda ilishapitwa na wakati..’akawa
anaongea huku akimwangalia mwanadada kwa tabasamu, na mwanadada akawa kama
anamkwepa wasiangaliane.
‘Unajua mwanadada, na ukiniuliza je upo tayari kupendana na
mwanaume nitakuambia, sipo tayari...nimeshajiuzulu..mimi swala la kupendana,
halinipi shida,hata kama ningelihitajia kuwa na mume, swala hilo lingelikuwa
baki, ningeliangalia swala la kukubaliana, na kuridhiana.....’akasema mwanamama
na mwanadada akamtupia jicho, huku akijaribu kutabasamu na mwanamama akawa
kaangalia chini akitabasamu.
‘Siwezi kuamini hilo....upendo upo wakato wowote, hata muewe
na umri gani, hicho ndicho kipimo cha kuishi pamoja na kuridhiana, kama hakuna
upendo ni kudanganyana tu,...wewe unasema hivyo kwa vile imetokea hivyo, lakini
nina uhakika, kama mwanasheria asingelikuwa kwenye hali kama hiyo, ya njia
panda, kuwa amchague nani, ungelikuwa
tayari kuolewa na yeye maana nahisi unampenda, sisemi hivyo kwa wivu, bali nasema
ukweli ulivyo,usinielewe vibaya...’akasema mwanadada.
‘Hivi huniamini mwanadada, wewe sasa ni ndugu yangu, wewe ni
mdogo wangu, hivi kweli mnaweza kuchangia mume, mtu na mdogo wake,...?’ akawa
kama anauliza halafu akatabasamu huku akiwa kainamisha kichwa, na huku
akimwangalia mwanadada, na mwanadada alipobakia kimiya bila kusema neno, yeye
akaendelea kuongea kwa kusema;
‘Kama kweli ningelikuwa na haja ya mwanaume, kwani yeye
ndiye mwanaume peke yake hapa duniani, mimi sasa hivi nina akili ya kiutu
uzima, siwezi kubabaishwa na mwanaume, mmoja, wakati wapo wengi, na kila siku
wanazaliwa warembo, ..mbona wapo wengi na wazuri zaidi yake, na wameshanifuata
kuniomba uchumba, lakini nimewakatalia...’akatulia kidogo.
‘Amini hivyo ninavyokuambia, mimi kinachonifanay nimuwaze
sana huyo mwanasheria, ni kwa vile ni mtu tumemzoea na yupo kwenye hiyo hali,
kila mtu anayemfahamu vyema, kwa tabia yake,na ukarimu wake, atamuonea
huruma...’akasema mwanamama
‘Ni kweli tuyaache hayo...’akasema mwanadada huku akifungua
mkoba wake na kutoa barua ya kutoka mahakamani,akaifungua na akawa kama
anaisoma, halafu akasema
‘Na jingine ni kuwa kesho ni siku ya hukumu..’akasema
mwanadada na kumfanya mwanamama amtizame kwa muda bila kusema neno, akitarajia mwanadada
ataongeza neno zaidi kwani alikuwa kaishikilia ile barua kama vile anaendelea
kuisoma, lakini mwanadada akawa katulia huku akiwa anaitizama ile barua.
‘Kwahiyo....?’ akauliza mwanamama.
‘Kwahiyo nini tena....ni kwenda mahakamani kusikiliza
hukumu, na nina imani mtaalamu anaweza kufungwa miaka mingi, kama sio kifungo
cha maisha...’akasema mwanadada.
‘Lakini namuonea huruma, kwa yale maneno yake, kuwa alikuwa
akihangaika kuilinda ardhi kwa ajili ya vizazi vijavyo, ina maana huenda kweli
eneo hili lina madini, sisi tumelikalia bila kujua manufaa yake..’akasema
mwanamama.
‘Kila mahali kuna madini, kuna mali yenye thamani, lakini ni
kwa umbali gani, au ni kwa utaratibu gani wa kuyapata... kuna utaratibu uliokubalika
kisheria, maana nch haiendeshwi kwa hisia, za kila mtu anavyojisikia, hatuwezi
kuvunja makazi kwa hisia kama hizo, kama kweli yapo, muda muafaka utafika, na
makazi ya watu yanaweza kusogezwa sehemu nyingine, huo ndio utaratibu
mwema...’akasema mwanadada.
‘Na wakati kama huo ukifika, kweli unafikiria kuna kulipwa
fidia tena hapo, na je huenda sis tumeshajifia, au huenda kama alivyosema, tukafukuzwa
neo hilo waje kuchukua wawekezaji...’akasema mwanamama huku akionyesha mashaka,
na akawa anageuka kuangalia eneo hilo, akilikagua kwa macho.
‘Cha muhimu ni kuwa una hati miliki, hiyo diyo itakulinda,
kuwa unamiliki hi ardhi kwa miaka kadhaa, kwahiyo akija mumwekezaji wewe
utamkodi, na kuwa na mamlaka na eneo lako,serkali haiwezi kuwatupa wananchi wake,
ikifanya hivyo, basi hiyo sio serkali, ni sirikali, ....Cha muhimu kwasasa na
ambalo ndilo nalihangaikia, ngoja kesi iishe, tukamilikishe maswala ya hati
miliki kwa jina lako...na ukitaka na la mtoto wako’akasema mwanadada.
‘Ina maana ni mpaka kesi iishe, hukusikia alivyosema
mwanasheria?’ akauliza mwanamama.
‘Ndio ukumbuke eneo hili lipo kwenye kesi mahakamani
huhitajiki kufanya lolote mpaka hukumu ipite, Na nina uhakika kuwa kesho siku
ya hukumu tutauwa ndege wawili kwa jiwe moja....’akasema mwanadada
‘Una maana gani kusema hivyo?’ akauliza mwanamama.
‘Ni kuwa hukumu ya kes I hiyo, itatoa mamlaka ya wewe
kurejeshewa mali zako zote, ikiwemo shamba na kumilikishwa kisheria, na wakati
huo huo huyo anayejiita mtaalamu atawajibika, mali yake yote itapigwa mnada, na
kutoa fidia kwa waathirika wote waliotokana na mipango yake ya kitapeli,
ikiwemo kumtibia mama mkunga,....’akatulia.
‘Tuna mpango apelekwe nje, akatengenezwe ngozi yake
vyema,.....na inawezekana maana pesa ipo,...’akasema mwanadada kwa kujiamini.
‘Pesa ipo kutoka kwa huyo huyo mtaalamu, hilo
nimeshalijengea hoja,....halina utata, lakini pia kutokana na kesi hii, mengi
yamejulikana kichwani mwa watu, watu sasa hivi wataamuka kudai haki zao, awe
mwanaume, au mwanamke, hakutakuwa na
usumbufu tena na watu kama hawa...’akasema mwanadada akionyesha furaha.
‘Kweli hatimaye naanza kuamini..’akasema mwanamama
‘Kuamini nini?’ akauliza mwanadada
‘Kuwa wema, wakati wote ni kinga ya matatizo, wema, huwa ni
kama taa inayokumilikia njia, hasa wakati kukiwa na giza na hakuna namna
nyingine ya kupata mwanga. Wema, kamwe hauozi, tenda leo, au kesho au miaka
mingi iliyopita, wema utakusubiria, wakati ukiwa na shida. Hii yote
tumefanikiwa kwasababu ya matendo yetu mema, kwa jamii, nakushukuru sana
mwanadada, ....sijui nitakulipa nini...’akasema mwanamama
‘Mimi ninatalipwa tu, kutoka kwa huyo huyo Mtaaalmu,
unafahamu mali yake ina thamani gani, ina thamani ya mabilioni ya pesa, na
kumegundulika vito vingi vya thamani ndani ya handaki lake vikiwemo madini, na
pesa za kigeni.....’akasema mwanadada na wote wakakaa kimiya kwa muda, halafu
mwanamama akauliza swali
‘Lakini nikulize swali uligunduaje kuwa mtaalamu ndiye yupo nyuma ya haya yote?’
akaulizwa
‘Unapofanya kazi hii, unakuwa na hisia ya ziada, ....na mara
nyingi, sisi kama mawakili, tunajeng hoja zetu pale tunapokuhoji, maelezo yako
ndiyo yatatupa dira, na muelekeo wa jambo jingine, na ndivyo ilivyofanyika
kwenye kesi hii...’akasema mwaandada.
‘Mtaalamu alijifanya ana akili sana, akayapanga mambo yake
kiakili na kuwafanya wengine wajinga, hakujua kuwa ipo siku atajikanyaga, ...japokuwa
kwakweli aliifanya kazi hiyo kwa namna ya kipekee, kwani amekuwa akiwahadaa
watu kwa miaka mingi bila kulitambua hilo, na amekuwa akiwa na sura mbili bila
watu kumtambua,lakini nilihisi kuwa kutoweka kwake, sio kama anavyodia eti ni
mizimu, nilihisi alikuwa akiogoap jambo ....’akatulia mwanadada.
‘Alikaa huko alipokuwa kajificha akijenga hoja na jisni
gania anaweza kurejea kwa jamii,na alipoweka mambo yake sawa, ndio
akajitokeza...’akasema mwanadada.
‘Alifika akiwa kajiamini akijua wananchi ni mbumbumbu,
atawahadaa kwa mmbo yake,hakujua na sisi tulihamshuku, kutokana na matendo
yaliyotokea nyuma, kwanini alitoweka ghafla, alipojitokeza tukawa tunaanza kujuenga
hoja...’akatulia mwanadada.
‘Ukiangalia siku ile ya uchomaji wa nyumba ya mama mkunga,
alijua kabisa kuwa ndugu yake huyo atakuwa hayupo, akachukua mwanya huo na
kujifanya yeye ndiye kiongozi wa kijiji, hatukuwa tunafahamu kuwa ni yeye,
utambue hilo, lakini tulijiuliza ni nani huyu aliyemuita mume wa mama mkunga...kuna
mtu hapa kajificha ni nani, ni jemedari, ni kiongozi mwenyewe wa kijiji.
‘Ukumbuke kuwa wakati mzee huyo anafika nyumbani kwa mjumbe,
alisema kuwa alishangaa kuona kiongozi huyo wa kijiji hayupo na alipomuuliza
mke wakiongozi wa kijiji , mke huyo akawa anashangaa, na kuwambia kuwa mbona
mume wake hayupo, kaondoka toka mchana....na mzee huyo akabakia akiwaza kuna
nini, na yeye hakuwa na mashaka kuwa kuna lolote litatokea huko kwake..akawa
anaongea na mke wa kiongozi huyo wa kijiji kwa muda kidogo , na baadaye
akarejea kwake, na kukuta moto ukiwaka,....
‘Lakini pia, mzee huyu alisema kuwa wakati anafika, alimuona
mtu akitokea mlango wa nyuma, ambapo ni sehemu mara nyingi, anaishi mtalaamu,
kama akiwa na shida zake, ukumbuke kuwa mtaalamu japokuwa ana nyumba, lakini
kwa vile hana mke, yeye alikuwa akija kukaa kwa kaka yake huyo, na nyumba yake
alipangaisha,...na mzee alisema aliyemuona akitoka kwa mlango wa nyuma ana uhakika ni kiongozi wa kijiji... huenda
hilo alilipana hivyo mtaalamu, lakini pia ni kosa moja wapo alilolifanya...’akasema
mwanadada.
‘Hapo kuna kosa gani?’ akauliza mwanamama.
‘Kama kiongozi wa kijiji alikuwa hayupo, mzee aliitwa na
nani, na huyo aliyetokea mlango wa nyuma ni nani, ina maana mke wake ni muongo,
yule mama sio muongo, tulimpima na tukagundu akuwa alichokuwa akiongea ni
sahihi...na ukumbuke kuwa mama mkunga aliona mtu akielekeza jinsi ya kuchoma
nyumba yake, na alisema alimuona kiongozi wa kijiji, huyo kiongozi wa kijiji ni
yupi, maana kweli kiongozi wa kijiji alikuwa hayupo ,...’akasema mwanadada.
‘Lakini kama alipanga hivyo kiongozi wa kijiji, si ndio
angedanganya hivyo kuwa akondoka kumbe kajificha mahali’akasema mwanamama.
‘Hiyo ingeliwezekana, na kwa mpango wa mtaalamu ilitakiwa
ionekane hivyo, lakini tulipofika huko ambapo kiongozi wa kijiji alikwenda
tuliambiwa kweli alikwua huko, na kikao kilikuwepo, na hakikuisha hadi usiku wa
manane, ambapo nyumba ya mama mkunga ilikuwa imeshachomwa moto....ushahidi huo
tuliupata, hakuna mashaka....’akasema mwanadada.
‘Angalia sumu iliyotumika kumuua Jemedari, yule mtu
aliyetumwa,alisema aliondoka na chupa, lakini uchunguzi, uligundua chupa
iliyokuwa na sumu ilipatikana pale mezani, karibu na kitanda cha marehemu, ni
nani aliileta hiyo chupa, na ninani angeligundua kuwa sumu ile ya mwanzo
isingelifanya kazi, na alihitajika kuleta sumu nyingine ili kutimiza lengo
lililokusudiwa. Ni huyo huyo aliyepanga haya, na ni lazima huyo awe mtaalamu wa
kutengeneza hizo sumu....hapo nilihiisi kuna jambo, kuna mtu mwingine nyuma ya
pazia...’akasema mwanadada.
‘Ukirudi nyuma, siku alipopotea yule binti wa mkuu wa
kitengo cha upelelezi, ni nani aliyemrejesha nyumbani, ...ni huyo mtaalamu,
japokuwa huyo binti hakuwa muwazi, lakini aliweza kuongea kidogo kwa rafiki
wake wa kiume,...na alisema alikuwa kwenye nyumba iliyojengwa ndani ya
pango...na ndiyo siku niliyokuwa na hamu sana ya kuongea na huyu mtalaamu,
lakini hakuwepo...nikajiuliza huyu mtu atakuwa kaenda wapi, ni kweli katoweka
kimzimu kama anavyodai, ...na aliporejea tena, nikataka kumdadidi hayo,
akatunga uwongo wake.......’akasema mwanadada.
‘Siku hiyo nilipokuatana na huyu mtaalamu, akiwa katokea
huko msituni, akaniambia kuwa yupo tayari kuelezea yale anayoyajua, kwani
kaagizwa na mizimu, nikamtilia mashaka, japokuwa alipanga mambo yake kwa
utaalamu...lakini kwenye maongezi yake,nikagundua udhaifu fulani, ...alijuaje
yote hayo...na kumbe yey ndiye mtaalamu wa kutengeneza hizo sumu....na
nilipoanza kumfuatilia nikaanza kugundua kimoja baada ya kingine, na kumbe,
wanafanana na kiongozi wa kijiji..hilo lilijificha sana..’akasema mwanadada.
‘Hilo la sura yake lilijificha kwasababu alikuwa hapendi
kubadili mavazi yake, ambayo yalikuwa yakifunika pia sehemu kubwa ya uso wake, na
kubakia sehemu hii ya mbele tu....na ndevu zake za kiaina, ambazo alikuwa
akizivaa...’akasema mwanadada
‘Ina maana hata zile ndevu sio zake, za asili?’ akauliza
mwanamama.
‘Anazo ndevu zake za asili, lakini mara nyingi huzinyoa kama
anavyofanya kiongozi wa kijiji, huzinyoa na kubadika hizo za bandia, ili
akizitoa afanane na kiongozi wa kijiji’akasema mwanadada.
‘Lakini ukiangalia alivyopanga, mbona inaonekana kama kweli
alifanya hivyo kwa ajili ya kulinda ardhi na maliasili ya kijiji, kutokana na
hoja yake?’ akauliza tena mwanamama
‘Sio kweli....hawa watu ni wajanja sana, wanafahamu jinsi
gani ya kuwavuruga watu wakili zao....’akasema mwanadada huku akitikisa kichwa
na kuwa kama anawaza jambo, na mwanamama akamwangalia kwa makini halafu
akasema;
‘Basi kama ni hivyo, huyo kweli ni mtaalamu...’akasema
mwanamama
‘Huo sio utaalamu... utaalamu gani wa hadaa, wa kutumia
mbinu kuwatapeli wenzako, kuhadaa jamii, unyang’anyi na ubakaji, ushirikina,huo
sio utaalamu, ni ujinga,..utaalmu wa kupata kwa kutumia migongo ya wenzako,
..hapana huo sio utaalamu, utaalamu ni ule unaotokana na jasho lako, mikono
yako na akili yako kwa manufaa ya watu,
ya jamii...’akasema mwanadada.
‘Lakini hukusikia hoja yake kuwa alifanya hayo kwa minajili
ya kulinda maliasili ya kijiji, kwa ajili ya vizazi vijavyo?’ akaulizwa
mwanamama.
‘Hiyo ndio hoja yake, lakini hoja hiyo aliitunga kichwani,
na watu kama hawa hujaribu kutafuta hoja ya kusimamia, ...na kujipa moyo kuwa
anachofanya ni sahihi kutokana na hoja hiyo, ..hata viongozi wa siasa, wa dini,
wa makabila, wote hutafuta hoja ya kusimamia, ikilenga matakwa na msilahi yake
binafsi, ilimradi ajifanye, asionekane ni mkosaji na huijengea hoja yake hiyo
ushahidi na mashahidi..’akasema mwanadada.
‘Lakini tukumbuke kuwa hoja, isiyo ya kisheria, hoja
isiyokubalika na jamii, hoja yenye maangamizi, haina tija, na mwisho wa siku
hoja hiyo hiyo itakuumbua tu maana sio wote wajinga, sio wote watakaa kimiya,
ssheria ipo, utaratatibu uliokubalika na jamii, upo, maandiko matakatifu yapo,
katiba ipo, ina maana wote watakuwa hawachunguzi hayo, hata kama umjanja kisia
gani, lakini dhuluma haidumu, na uovu hauna mshiko, una mwisho mbaya...’akasema
mwanadada.
‘Ni kweli mpendwa nakuaminia, ngoja tusubiri hukumu, maana
huwezi kujiaminisha, moja kwa moja, tulijiaminisha kwenye kesi yetu ya kwanza,
kumbe kuna mambo yalifanyika, na tukaonekana tumeshindwa,
...siwezi kuamini
mpaka hakimu atamke mwenyewe...’akasema mwanamama.
‘Ni kweli uhalali wa kushinda ni pale hakimu atakapoginga
rungu lake chini, baada ya kusoma hukumu, lakini huo ndio ukweli, na ukweli
haujifichi,...twende tukamuona mgonjwa, maana nahisi moyo ukienienda mbio, ....’akasema
mwanadada.
‘Hata mimi....nahisi hivyo hivyo, lakini ..mungu yupo nasi,
na kwa wema wake, mungu atamsaidia atapona, tutakuwa naye, kama shemeji yangu,
baba mdogo wa mtoto wangu..’akasema mwanamama
‘Mhh, sio mbaya akiwa baba halisi,mimi niko radhi, ...au unelipenda
tuishi kama wake wenza...eti unaonaje haitapendeza hiyo...?’akasema mwanadada
huku akicheka , na mwanamama akawa anamwangalia kwa
mashaka,na mshangao na kuuliza
‘Eti nini...umechanganyikiwa nini,...hahaha...haipo hiyo, ?’
‘Je kama mwanasheria aking’ang’ania, na unavyoona, afya yake
itakuwa njema zaidi akipata kile akipendacho, na moja ya wazo lake ni kuwa sisi
tuishi kama wake wenza, utamkatalia,...?’akauliza mwanadada.
‘Mimi sipendi hayo mawazo yao....ooh, mbona unaleta mambo
nisiyoyafikiria kwanini umesema hivyo?’ akauliza mwanamama na mwanadada
akatabsamu na kuangalia chini, huku akimuwaza mwanasheria, akitamani amkute
keshainuka kitandani, na moyo akahidi kutimiza kila atakalolitaka, hata kama
hatalifurahia.
NB: Haya tuendelee kuwepo pamoja.
WAZO LA LEO:
Tunapokuwa viongozi, wa aina yoyote ile, na tukawa na mamlaka, na maamuzi ya
kufanya jambo, tusitumie mwanya huo vibaya, tukahalalisha yale yasiyo sahihi
kwa masilahi yetu,tukumbuke uongozi dhamana, na dhamana ni deni, sio mali yako.
Timiza wajibu wako kwa uadilifu,hiyo iwe ndio dira yako.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Bonge la simumulizi inasisimua ila du kupenda kuwa na mke mwenza? ..Kazi kwelikweli
Post a Comment