Mama mkunga aligeuka na kumwangalia mume wake, ambaye
alikuwa akitengeneza mtego wa kuwindia wanyama, huku akiwa kashikilia panga
lake, na mama huyu akiwa kashikilia safuria na mkono mmoja, akainama kuendelea
kufanya usafi wa vyombo vyake, mara wakasikia kelele za kuashiria kuwa kuna watu
wanakuja, kwa haraka akajifunika, maana hakutaka watu wawe wanamshangaa kwa
jinsi mwili wake ulivyoharibika na majeraha ya moto.
Mzee wa kijiji akashika panga lake mkononi, na kusogea
mbele, kama kuwakabili, na mkewe akashangaa kwanini mume wake, anaonekana na
wasiwasi na watu hawo wakati wanafahamika.
‘Mume wangu wageni hawo?’ akasema mkewe.
‘Una uhakika gani,...’akasema mumewe huku bado kashikilia
panga hadi wale wageni walipowakaribia, na hapo akaliweka panga lake karibu na
kuanza kuwakaribisha hawo wageni.
Walikuwa ni kiongozi wa kijiji na mkewe.
‘Tumeshukuru tumewakuta, maana mguu huu ulikuwa ni wenu...’
kiongozi wa kijiji ikasema huku akimtizama mama mkunga ambaye alikuwa akijaribu
kujifunika mwili wake, na kutikisa kichwa kwa kusikitika, na akasema;
‘Mtu huyu ni mnyama kweli, yaani amekuharibu, na kukufanya
uishe kwa mashaka, unaogopa hata watu wasione hata sehemu ndogo ya mwili
wako...’akasema kiongozi huyo.
‘Hata hivyo nashukuru kuwa nipo hai, maana ungelikuwepo siku
ile, moto jinsi ulivyokuwa makli, usingeliweza kuamini kuwa ningelitoka nikiwa
hai, nilizungukwa na moto.....nguo zinaungua..hapana kweli kama siku zako
hazijafika huwezi kufa....’akasema mama.
‘Pole sana lakini yote hayo yana mwisho, ...ubaya wake umejulikana
na tunasubiri haki itendeke, na sijali kama ni ndugu yangu,japokuwa juzi mke
wangu kanishurutisha twende kumuona, sikutaka kabisa kufanya hivyo...’akasema.
‘Kwahiyo mkaenda kumuona, ...usiniambie mlifanya hivyo...’akasema
mzee wa kijiji kwa hasira.
‘Mke wangu bwana, kasema yule ni ndugu, hata kama ana ubaya
gani, lakini ni haki yetu kutimiza wajibu wetu kama ndugu, tulibishana sana, na
baadaye nikaona isiwe taabu tuakenda kumuona...’akasema kiongozi huyo.
‘Vipi mlivyomkuta, mliweza kuongea naye, maana nasikia toka
alipotaka siku ile, kwenye kesi,alinga kauli kabisa, na haongei na mtu, je ni
kweli?’ akauliza mama mkunga.
‘Ni kweli, haongei ni mtu kabisa, kawa kama bubu, au zezeta
fulani, sisi tulipofika, tukaitiwa akafika mbele yetu, na alipotuona
akatuangalai tu, na akatikisa kichwa kama kusikitika, na niliona dalili za
machozi, akageuka kuondoka...tulimuita kujaribu kumpa chakula, akakataa kabisa
kula, walinzi wakamshika kwa nguvu kumlisha, ilikuwa kutumia nguvu, na baadaye
akawa anakula kama vile mtu aliyechanganyikiwa anavyofanya,anajaza
mdomoni..yaani kabadilika kabisa...pamoja na ubaya wake, ukimuona sasa hivi
utamsikitikia...’akasema kiongozi huyo.
‘Na tukiwa pale wakaja ndugu zake, upande wa mama yake, na
wakatuita pembeni tuongee, na ndio maana nimekuja hapa kwenu kuufikisha huo
ujumbe, japokuwa mimi sikuupendelea, ...lakini mjumbe hauwawi, au sio....?, na
kwa vile pia mimi bado ni mjumbe wenu, nina wajibu wakuhakikisha kuwa watu
wangu wanaishi kwa amani na masikilizano na cha muhimu ni kusuluhisha watu
wapatane...wasameheane, huo ndio uungwana’akasema huyo mjumba.
‘Unataka kusema nini?’ akauliza mzee wa kijiji akiwa
kashikilai panga lake mkononi na mkewe akamwangalia na kusema.
‘Hebu weka hilo panga pembeni mume wangu, kila mara panga
mkononi, huoni watu watakuwa wakikuogopa’akasema mama mkunga.
‘Hii imekuwa sehemu ya mwili wangu, siwezi kuiacha, ....huu
ndio urithi wa babu yangu, babu yangu alikuwa hivi hivi, yeye na panga mkononi,
na alisema hata akifa, azikwe na panga lake, na kweli walimzika na panga lake
mkononi....na mimi nataka mfanye hivyo hivyo. Na siwezi kufanya ubaya kama
hakuna ubaya...’akasema mzee huyo huku akiliangalia hilo panga lake likiwa
mkononi.
‘Hamna shida sisi tumeshamzoea mzee wetu huyu....’akasema
kiongozi wa kijiji.
‘Haya tuambie, mliongea nini na hawo ndugu wa upande wa mama
wa mtaalamu, maana hawo ni jamaa zenu, au sio?’ akauliza mama mkunga.
‘Ni kweli, siwezi kulikataa hilo, hawo ni jamaa zetu, na
hata walipotuita pembeni hatukupinga tulikaa pamoja na kuanza kuongea...kama
wanafamilia, na sio kama maadui, ...’akasema kiongozi huyo.
‘Ni lazima mfanye hivyo, kwa vile hamkuathirika sana,...’akasema
mzee wa kijiji na mkewe akamuangalia kwa jicho la kumkanya awe na subira. Na
kiongozi wa kijiji akaendelea kuongea kwa kusema;
‘Walituomba msamaha kwa niaba ya ndugu yetu huyo, na kusema
watu wanasema tabia hiyo imetoka kikeni, kwa mama yake , na kikeni ndio wao,
....na baya zaidi wanasema kuwa watu wengi wanawashuku wao kuwa walikuwa
wakifahamu tabia ya mtaalamu, na hayo aliyokuwa akiyafanya, na wao hawakutaka
kuifichua, kitu ambacho sio kweli kwa kauli yao wao...’akasema kiongozi huyo.
‘Ina maana kweli hawo watu walikuwa hawafahamu hayo yote?’
akauliza mzee wa kijiji akitikisha kichwa kukataa.
‘Kama wangelifahamu na kuficha, kwanini sisi ambao ni ndugu zake
wa karibu tusifahamu, mimi ninaweza kuwatetea kwa hilo, kuwa inawezekana
walikuwa hawafahamu kabisa na hayo aliyafanya hivyo kwa makusudi, akijua kuwa
hakuna siri ya watu wawili...na ndio maana hata wao wamejikuta wakingiwa na
mshangao kama ulivyotukuta sisi,....’akasema kiongozi huyo.
‘Tulipoongea nao pamoja , kwanza walianza kwa kuniomba
msamaha kwa niaba yao, na pili wakaniomba mimi kama mjumbe kufiksiha ombi lao
la kuomba msamaha kila aliyetendewa ubaya na ndugu yetu huyo, wameomba ikiwezekana
tukatanishwe sote, ili wasema kauli yao hiyo ambayo kubwa ni kuomba msahmaha
kwa niaba ya ndugu yao huyo na kuelezea jamii kuwa wao walikuwa hawafahamu chochote
na walikuwa hawajui hayo aliyokuwa akifanya ndugu yangu huyo...’akasema
kiongozi.
‘Na wakaongezea jambo ambalo hata mimi sikuliunga mkono, ila
kwa vile mimi ni mjumbe, nikaoana nilifikishe kwenu, ...’kiongozi huyo akatulia
kwa muda kidogo, na akunja uso, kuashiria kuwa neno analotaak kuliongea halipo
moyoni mwaka, analisma tu, kwa vile anawajibika kulisema;
‘Wanataka , hasa mama mkunga kwenda kwa hakimu, ...akiwa na
wengine waliopatwa na haya, kusema wamemsamehe, na hayo yaje yaongelewe
kinyumbani, maana hali ya ndugu yangu huyo ni mbaya, na sasa anaweza kwenda
kuchezea kitanzi,....atanyongwa au kufungwa kifungo cha maisha...’akasema
kiongozi huyo na hakuna aliyesema neno wote walikuwa wanamwangalia yeye
‘Kama nilivyosema mimi sikukubaliana na maneno yao hayo,
kwanza kisheria hilo halipo, maana kwa makosa hayo kashitakiwa na jamuhuri, sio
sisi, tulioathirika, sisi tumeitwa pale kama mashahidi, na kwahiyo hatuwezi
kubadili chochote, pili, yule kafanya ubaya, hata kama ni ndugu akifanya ubaya
ni lazima ashughulikiwe kisheria...’akasema mjumbe.
‘Lakini mimi kama mjumbe, mimi kama mwanafamilia, ilitakiwa
nitumie busara kuongea na wale ndugu zetu na kuwachukulia kibusara, kuwa hilo
ni swala la kujadiliana na wote wlioathirika, na kujaribu kusikia kuli ya kile
aliyeathirika...’akasema na kumwangalia mzee wa kijiji.
‘Lakini lililo bora ni hilo la kuomba msamaha, ili kuondoa
chuki na kuja kulipizana visasi...’akasema huyo kiongozi kwa kijiji akiwa
kaanngaliana na mzee wa kijiji.
‘Kwahiyo nimakuja kuleta huu ujumbe kwenu nisikie na nyie
mtasema nini....’akasema huku wakiwa wameangaliana na mzee wa kijiji. Mzee wa
kijiji, alikuwa kama kashikwa na butwaa, na mara ghafla akamsogelea mzee
mwenzake, akasogeza shati lake pembeni na kuangalia pale shingoni kwa mzee
huyo, halafu akatikisa kichwa huku akicheka.
‘Nimerizika, maana haya maneno yako yalinitia wasiwasi, isije
tukawa na mtaalamu hapa , akiendelea kujifanya yeye ndiye kiongozi wa kijiji na
kuendelea kutumia hadaa zake...’akasema mzee huyo na wote wakacheka.
‘Ina maana kweli kiongozi wetu huyu tumeishi naye miaka
mingi aje kutupotea sura yake, hapana, japokuwa wanafanana, lakini mkiwa karibu
hivi, unaweza kutambua kabisa kuwa huyu ni kiongozi wa kijiji...’akasema mama
mkunga.
‘Mbona walikuchanganya, wewe mwenyewe....?akauliza mume
wake.
‘Kwa hali ile ilivyotokea, ni usiku, na ikitokea kwa haraka,
na hukuwa na mawazo hayo, huwezi kweli kuwatofautisha, lakini kwa sasa tupo
makini, hawawezi kabisa kutuchanganya...mimi
hata akija yeye kwasasa siwezi kuchanganyikiwa tena, nitawatofautisha’akasema
mama mkunga.
‘Ni kweli, hata mimi sikujua kuwa tunafanana kihivyo, maana
aliondoka akiwa mkubwa, na aliporejea akawa anavaa hayo mavazi yake ya
kiuganga, siku zote....’akasema kiongozi huyo wa kijiji.
‘Hata mimi sikufahamu kuwa wanafanana hivyo...niliona ajabu
sana alipobadili hayo mavazi yake na kuletwa pale mahakamani, nilishikwa na
butwaa, nikasema hivi yupi ni mume wangu, maana kweli wanafanana na mume
wangu....’akasema mama mjumbe.
‘Kwa namna hiyo hakuweza kukuchezea kweli, maana jamaa huyo
haaminiki, na ukizingataia kuwa hana mke?’ akauliza mzee wa kijiji kwa utani na
wote wakacheka.
‘Sio rahisi kufanya hivyo, na kama angelifanya hivyo
ningelimgundua, ...ukiwa na mume wako mpo naye siku zote, utafahamu harufu
yake, matendo yake,...na hata kutembea kwake, kwahiyo hata wafanane vipi ,
utagundua kuwa huyu sio mume wako...’akasema mama mjumbe.
'Cheza na wanaume weye...shukuru mungu kama hakufanya hivyo...'akasema mzee wa kijiji akicheka kwa utani.
'Hawezi na hatawahi....muulize mume wangu ?' akasema huku akimwangalia mume wake.
‘Ni kweli, na ndugu yangu huyo pamoja na ubaya wake wote huo,
kwa hilo siwezi kumshuku, asingeliweza kufanya hilo..hilo namtetea kabisa’akasema
kiongozi wa kijiji , na wote wakabakia kimiya kwa sekunde chache, halafu
maongezi yakaendelea tena.
Na safari hii mama mkunga ndiye aliyekuwa wa kwanza kuongea akasema;
‘Pamoja na hayo poleni sana na mitihani iliyowakuta, maana
hata mimi nilishajenga chuki dhidi yenu, sikutegeema kuwa tunaweza kuja kuongea
hivi ana kwa ana, ...ama kwa hilo ombi lako, mimi sioni kama kuna ubaya, kutoka
moyoni kwangu mimi nimeshamsamahe...kabisa kabisa ...sina kinyongo naye, ...’akasema
mama mkunga na mzee wa kijiji akamwangalia kwa jicho baya na kusema;
‘Mimi sijamsamehe, na wala sitakaa kwenye hicho kikao..eti
cha kuombana msamaha, kama ungeliuwawa kwenye ule moto, wangekuja kumuomba nani
msamaha....kamwe, acheni na yeye akateseke, jela, na hata kama ni kunyongwa,
acheni anyongwe hastahili kuishi katika jamii ya wastaraabu..na kama ingelikuwa
mimi ningelimchoma moto, kama alivyomfanyia mke wngu...’akasema mzee wa kijiji,
na kiongozi wa kijiji akasema;
‘Ni kweli hata ingelikuwa ni mimi ningejisikia hivyo na kufanya
hivyo hivyo, na sikuwa na nafahamu kabisa kuwa kuna mtu alikuwa akichezea,mwili
wangu ...kwa hayo mabaya yote, na wakati mwingine nilikuwa nashikwa na
mshangao, ....na hata kumuuliza mke wangu hayo yametoka wapi...lakini sikuwa na
wasiwasi sana....’akasema na huku wenzake wakicheka
‘Ina maana ulikuwa ukichukuliwa msukule...?’ akatania mama
mkunga
‘Ndio hivyo, maana kama mtu anaigiza mwili wangu anafanya
maasi kwa niaba yangu, na jamii inafahamu kuwa ni mimi ndiye ninayefanya hayo, na
ubaya na chuki zote zinakuja kwangu basi huo ni msukule wa aina yake, mmh,
kweli ndugu yangu yule alivuka mpaka, sikutegemea kabisa kama angelifanya mambo
kama hayo...’akasema kiongozi wa kijiji.
‘Lakini baada ya haya tumejifunza nini, maana watu kama
mtaalamu bado wapo wengi, ...?’ akauliza mzee wa kijiji
‘Ikishapitishwa hukumu, na sisi kama wanakijiji inabidi
tukae tupitishe rasimu yetu, inayoainisha matakwa ya kijiji, ya kwamba hawo
watu wote wanaoitwa waganga wa kienyeji, au wataalamu wawe wana kibali,watambulikane
rasimi, na kazi zao, na wanakijiji wawe na kauli ya kusema huyu kweli ni mganga
au sio...na ili tiba zao zijulikane na kama kuna mmoja anatambulikana kama
tapeli, aweze kuwajibishwa...’akasema kiongozi wa kijij.
‘Lakini wapo watu wa namna hiyo hawataki kujulikana, na
wanafanya mambo yao kwa siri tutawafanya nini?’ akauliza mkewe
‘Hawo ndio wa kushughulikia, maana hawo ndio chanzo cha
matatizo mengi, ...wao ndio wachonganishi, kama kweli anajiamini kuwa ni
mtaalamu, ni mganga wa kienyeji kwanini ajifiche, utaratibu kama huo umepitwa
na wakati...hilo tutaliwekea mikakati, na kuhakikisha tatizo hilo linakwisha
kabisa hapa kijijini...’akasema huyo kiongozi.
‘Na tatizo la ardhi, umiliki na haki za kila mmoja ni lazima
zifahamike, hata kama kutatokea mmoja wa wanafamilia kuondoka, ni lazima kuwe
na iuataribu wa jinsi ya kulinda ile mali ili iende kwa mlengwa, na haya
tusiyaachie kwa familia peke yake, tuisaidia ile familia ili haki iweze
kutendeka....’akaongezea mama mkunga.
‘Na hilo nalo neno, maana ni kweli ukiiacha familia peke
yake, kunaweza kukatokea mmoja ana tabia kama ya mtaalamu, akawahadaa
wanafamilia na matokea yake, wastahili wanabakia wakitangatanga, na mtaokea
yake, watoto hawo wanakimbilia mjini na kuwa omba omba..laana itaturudia sisi
tulioshindwa kutimiza wajibu wetu...’akasema kiongozi wa kijiji.
‘Kweli kabisa, kama tiutashindwa kuwalea watoto wetu
wakakimbilia mjini bila ya malengo, na huko wakageuka omba omba majambazi,
wavuta unga, sisi wazazi ndio wakulaumiwa, na hili linasababishwa na kutokuwa
na utaratibu mzuri, na uongozi adilifu. Hilo tulianze kulifanyia kazi, mzee
mwanzangu, tuweze kujua familia zetu, kaya, watoto wetu, na jinsi gani
tutawalea kama wanajamii, kama wanafamilai...kila mtoto awe mtoto wa jamii, sio
mtoto wa familia peke yake, tukiliweza hili tutakuwa tumedhibiti hiyo
hali.....’akasema mke wa kiongozi wa kijiji ambaye ni kiongozi wa akina mama
hapo kijijini.
‘Haya jamani pamoja na kuja kusalimia, lakini pia tumekuja
kutoa taarifa kuwa kesho nis iku ya hukumu, na inatarajiwa kuwa hukumu ya
kihistoria, kwani kama mambo yatakwenda vyema hukumu hiyo itajenga taswira mpya
kwa wanajamii, tutaweza kujiunza mengi kuwa haki ya watu haitakiwi kuchezewa,
pia kuwa macho na watu kama akina mtaalamu ambao wanajaribu kucheza na udhaifu
wa wanadamu...’akasema mkuu.
‘Tukiwepo wengi pale mahakamani tukasikia hukumu hiyo,
tutaweza kujifunza,na hatutakuwa na uwoga tena wa kudai na kutetea haki zetu,
watu kama mtaaamu wanaotishia watu kwa mbinu za kshirikiana wataabika, na
kuonekana kuwa hawana lolote zaidi ya kucheza na hisia za watu...’akasema mama
mjumbe.
‘Na hizo tabia za kishirikina za kuwaandama akina mama,
ambao wanaaiwa kuwa ni wachawi, zitaisha, na hili liwe ni fundisho, na ni
lazima mama yetu ukatibiwe kwa pesa zake mwenyewe,...wahakikishe kuwa hali yako
inarejea kama awali, nasikia upo utaalamu wa ngozi....’
‘Je mna taarifa yoyote na hali ya mwanasheria?’ akauliza
mama mjumbe.
‘Hatuna, kwa mara ya mwisho kwenda kumuona tuliambiwa
haturuhusiwi kumuona zaidi ya watu waliokubalika, basi tukakata tamaa ya kwenda
kumuona, nasikia bado hajazindukana....’akasema mzee wa kijiji.
‘Hivi kweli anaweza kupona, au ameshakufa, lakini wanataka
kupoteza muda tu labda mpaka kesi hiyo iishe halafu wanatangaza kifo chake....’akasema
mama wa mjumbe.
‘Bado yupo hai, ....’akasema mzee wa kijiji.
Mara wakaona kwa mbali gari la polisi likija, na walipofika
pale waliposimama lile gari likasimama na kwa haraka askari wawili wakatoka, na
kumzonga kiongozi wa kijiji, na hata bila kusema kitu wakamfunga pingu, na
kumuingiza ndani ya gari
‘Vipi nyie mbona mnamshika mtu hata bila kuuliza, na hata
bila kusema ni kwasababu gani, na huyo ni kiongozi wa kijiji
anayeheshimika,....’akasema mzee wa kijiji akiwa kasimama mbele ya lile gari
lisondoke, huku kashika panga mkononi.
‘Mzee usitakae makubwa,...sisi tunatimiza wajibu wetu,
tumetumwa kumkamata huyu mzee...’akasema mmoja wa maasakri
‘Kwasaabbu gani mumumkamate, ipo wapi hati yenu ya kumkamata
mtu, ...?’ akasema mama wa huyo mjumbe.
`Mama, usiwe na shaka hati hii hapa, na hivi ni vitambulisho
vyetu, kama mnataka zaidi njooni kituo cha polisi, ....’akasema huyo askari.
‘Lakini kwasababu gani?’ akauliza mzee wa kijiji.
‘Mtaalamu katoroka rumande..’akasema mmoja wa maaskari.
‘Kwahiyo mnahisi huyu kiongozi wa kijiji ndiye mtaalamu?’
akauliza mzee wa kijiji.
‘Hilo halituhusu, ...sisi
tunatimiza wajibu wetu...’akasema huyo askari na mara wakageuza gari kwa
haraka, bila kujali kuwa kiongozi wa kijiji yupo mbele ya lile gari, na
lilimkosa kosa, na mzee wa kijiji akapepesuka kulikwepa lile gari, na vumbi
likawa limetimka, na kumfaya ashikwe na kikohozi cha mfululizo.
‘Hawa watu hawajui sheria, wanafanya kama vile sisi raia
hatuna uhuru, ni taartibu gani hizi za kuja kumkamta mtu kwa njia hii...’akalalamika
mzee wa kijiji.
‘Twendeni huko huko kituoni, na tumfahamishe mwanadada
akatusaidie, huenda anafahamu ni nini kinaendeleai...’akasema mke wa kiongozi
huyo wa kijiji na wote wakaelekea kituo kidogo cha polisi.
NB: Hii ilikuwa sehemu ya pili ya hitimisho la kisa hiki.
WAZO LA LEO: Wakati mwingine ni vigumu sana kusamehe makosa
tuliyotendewa, kutokana na uzito wake, lakini vyovyote iwavyo, kusamehe ni
wajibu wa kila mmoja wetu, japokuwa sheria inastahili kuchukua mkodno wake, ili
haki itendeke, ili kuwe fundisho kwa wengine. Tujenge mioyo ya kusameheana,
kwani kwa kufanya hivyo, tutaweza kupunguza chuki, na visasi, ambavyo ndivyo
vinavuruga amani katiak dunia yetu ya leo.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment