Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, July 4, 2013

WEMA HAUOZI-30


  Kesi ya hukumu iliahirishwa eti kwa vile wahusika wengi wakuu walitakiwa kuwemo kwenye kesi hii nyingine ambayo ilitakiwa kusikilizwa kwenye mahakama hii ya juu,. Sisi hatukujali hilo kwani tulijua matokea yake yatakuwaje, na wenzetu waliposikia kuwa kesi hiyo imeahirishwa wakashangilia na kudai kuwa hakimu anaogopa kaona haki haijatenda itakiwavyo.

‘Nyie mlitaka haki gani, kwani ushahidi uliotolewa mahakamani hamjauafiki, je ina maana mwanamke akishaolewa hana haki, yaana hata haki yake aliyochuma mwenyewe haitambulikani?’ wakaulizwa.

‘Mwanamke akishaolewa bwanaaa, hana haki tena,haki zote zinakuwa mikononi mwa mume wake….’akasema mwanamume mmoja.

‘Nikuulize wapi inasema hivyo?’ akaulizwa.

‘Mila na desturi zetu zinasema hivyo, maana mke alikuwa mikononi mwa wazazi wake, sasa yupo mikononi mwa mwanaume, yule mwanamume anakuwa ni mzazi wake na ana mamlaka na huyo mke na kila kitu chake…’akasema huyo mwanaume.

‘Hebu tukuulize wewe , unafahamu ni nini maana ya ndoa, …?’ akaulizwa.

‘Ndoa ni muingiliano wa mke na mume kisheria,…kwa utaratibu maalumu baada ya kukubaliana, na kupendana?’ akasema.

‘Hutujasikia maneno yanayothibistisha kauli yako ya mwanzo,  kuwa ndoa ni kuchukuliwa mke na haki zake zote ziwe mikononi mwa mume…tulitaka kusikia hayo maneno kwenye tafsiri yako ya maana ya ndoa, mabona hakuna kitu kama hicho…..?’akasema mwanamke mmoja kama anauliza.

‘Huwezi ukafafanua kila kitu kwenye tafsiri ya ndoa, mengine nayakuta huko huko, yapo kwenyeyanakutakana na mila na desturi….mwanamke akishaolewa anaiingia kwenye mila za mume, kama kulikuwa na sheria kuwa mke akabidhi mali yake kwa mume, inabidi afanye hivyo, huoni mume anatoa mahari….’akasema huyo mwanamke.

‘Kwani mahari ina maana gani?’ akaulizwa.

‘Mahari mmmh, hapo hapo?’….akawa naye kama anauliza halafu akasema;

‘Mahari ndiyo kisithibitisho kuwa mume anamchukua mke, na kummiliki, …umeshamlipia mharai, wewe hujiulizi kwanini anayelipa mahari ni mwanaume na sio mwanamke..’akatulia kidogo, akawa kama anatafakari jambo.

‘Mimi nijuavyo, ….mahari ni zawadi ya mume kwa mke, mengine, ni hizo mila na desturi ambazo ukichunguza sana ndani yake ni taratibu za mfumo dume, ambao lengo lake lilikuwa kumfanya mwanamke kama kitu, kinachonunuliwa, thamani yake ni hayo mahari…lakini dini, zikaja na kuliondoa hilo,…hata hivyo bado wanajamii wengi, wanapofikia sehemu ya matakwa yao, wanashikilia upande wa mila zaidi kuliko dini inavyosema…’akasema mwanadini mmoja.

‘Hebu tusaidie wewe mtaalamu wa dini , ni kweli kuwa mke akiolewa, hana haki ya mali yake,…kama kachuma yeye mwenyewe, inakuwa ni mali ya mume wake, au ukoo wa mume wake?’ akaulizwa.

‘Mke na mume wanapoona wanakuwa kitu kimoja, na wanapochuma mali zao zinakuwa ni zao , yaani za familia yao, lakini hata hivyo, mume na mke wanaweza kila mmoja akawa na shughuli zake, kila mmoja anazalisha, na kukawa na makubaliano kuwa huyu anamiliki hiki na huyu kile, ndio maana akifa mmojawapo, kuna kurithi zile mali, mke akifa mume anarithii mali ya mkewe , …kuonyesha kuwa mke naye anaweza akawa anamiliki mali…’akasema huyo mtaalamu.

‘Ina maana mke ana haki ya kumiliki mali, kama kaichuma yeye, ndio swali letu hapo? Akaulizwa tena hilo swali kuonyesha kuwa jibu lake halikuwatosheleza watu, na yeye akachukua kitabu chake alichokuwa nacho na kuanza kusoma maneno haya;

’Ilivyo ni kuwa mwanamke ana haki ya kumiliki mali na kujipatia fedha, na mume hana haki ya kutenga mikono kwa kile alichojichumia mwanamke. Na wakati huo huo ni wajibu wa mume kubeba gharama zote za matunzo ya familia. Mume anapaswa kumtunza mkewe, watoto wake pamoja na wafanyakazi wa ndani na kununua vyombo vya ndani n.k..’’

‘Lakini wewe mtaalamu, sisi tujuavyo ni kuwa mke anapoolewa na mume, anakuwa kama kakabidhiwa kwa mzazi mwingine,..kwahiyo hana haki tena ya kudai, kumiliki..’akasema yule mwanamume kutetea maneno yake;

`Unajua watu wanasahau….’akasema huku akitulia kuonyesha anasoma kitu kwenye kitabu chake halafu akasema;

‘Hebu niwaelezee hapa, kwenye wajibu wa mzazi kwa mtoto, mzazi anatakiwa kumtunza mtoto wake na kumpa huduma zote,….hata kama yule mtoto anakazi, anazalisha, lakini kama bado yupo kwenye umri wa kuitwa mtoto, bado mzazi anawajibu naye, wa kumpa huduma  na haki za mtoto….kama huyo mtoto anahitajia,na hawezi kusema kuwa kwa vile mtoto ni wangu, basi hata kile anachokichuma ni mali ya mzazi…au sio’akasema huyo mtalaamu.

‘Kwahiyo jibu tulolihitajia hapa ni kuwa, mke ana haki ya kuchuma, kumiliki mali,…hata kama yupo kwenye miliki ya mume, na mali yake haiwezi kulazimishwa iwe sehemu ya mali ya mume…na mume bado anastahili kumtunza huyo mkewe, na kumgharimia…na hastahili kudai mchango kwa mke, labda mke mwenyewe apende….ndivyo hivyo ilivyo kidini’akasema huyo mtalaamu.

‘Huo ni uonevu..kwanini mke apendelewe kiasi hicho, ina  maana mimi nimuoe, nitoe mahari, nije nimgharamie, bado na mali anayochuma nisiwe na haki nayo….haiwezekani mtaalamu, wewe umepata wapi hayo maneno, isije ikawa ndio nyie mnazua?’ akauliza huyo mwanaume.

‘Nikuulize na wewe hayoo ya kwako unayodai kuwa mume ana haki ya kila kitu kwa mke umeyapata wapi…mimi nazungumza kama mtaalamu wa dini, na sijasimamia dini gani, lakini kwa ujumla wake ndio huo….dini zimekuja kumkomboa mwanamke, kuwakomboa watumwa, kuwakomboa wanadamu kwa ujumla, maana mwanadamu kwa ujumla ana ubinafsi,…’ akatulia akiangalia watu waliokuwa wakimsikiliza.

‘Ukimuachia afanye apendavyo mwenye nguvu atakuwa ndiye mwenye haki ya kila kitu na mnyonge atakuwa wa kudhulumiwa tu…na hili linakwenda hadi kwa wanawake…wanawake, wamekuwa wakidhulumia sana toka enzi za mambu zetu…, kuonewa na kuonekana kama kitu…wengine wakitoa sababu za mahari kama kisingizio...eti kwa vile mwanaume anatoa mahari, basi mke hana haki tena…sio kweli..’akasema huyo mtaalamu

Kuhusu mahari, ilivyo ni kuwa mahari hailipwi kwa mwanamke kama vile unavyonunua kitu, au ili mwanamke aje kwa mume kama vile kuuza mwili wake. Mahari ni haki ya mke kimaumbile, na sio haki ya wazazi kama wengine wafanyavyo, …hii ni hali ya mume kumuonyesha mke kuwa anampenda na wamekubaliana, …na mahari inaweza ikawa kwa kiasi chochote au kitu chochote,atakachotamke mke…’akasema huyo mtaalamu.

‘Sasa wewe mtaalamu, kwa kesi kama hii, inavyoonyesha ni kuwa mwanamke alipata pesa, akiwa ndani ya ndoa, na akajenga nyumba na duka,..wakati huo mumewe yupo jela, na mumewe alipotoka, akahisi kuwa nyumba ile na duka, ni kutokana na pesa zake alichokuwa akihisi kuwa huenda mkewe alikuja kumuiibia….uone utata wake, na marehemu hayupo, angejitetea mwenyewe, kwahiyo mke anaweza akabuni mbinu za hadaa….’akawa anauliza huyo mwanaume kwa maelezo.

‘Hilo kwanza tuwaachie mahakama wenyewe, sisi kama wataalamu wa dini tuna utaratibu wetu, kama kesi hiyo ingelifika kwetu, basi tungelihukumu kwa mujibu wa taratibu zetu za dini, ..na hizi zinajulikana, kama nilivyosema awali kuwa mke ana haki ya kumiliki, kuzalisha, na mali hiyo aliyoichuma, hailazimishwi kuwa mali ya mume wake,….labda wao wenyewe wakubaliane, sio kwa kulazimishana, na mke mwenyewe akubali, kwa utashi wake…kwahiyo kutokana na kesi hiyo, sitaki niingilie huko…tusubirini hukumu za sheria za nchi.’akasema huyo mtaalamu.

‘Ndio maana hakimu kasepa, kaogopa kuwa ataleta migongano, maana mila zinasema hivi, dini vile, sheria za nchi hivi, tutashika lipii..’akawa analalamika huyo mwanaume.

‘Mimi sizani kama mila na desturi zinasema mke asiwe na haki ya kuzalisha au kumiliki…chunguzeni kwa makini hilo, hizo taratibu zinawekwa na wanafamilia na jamii zao, ili kukidhi matakwa yao,…mila za mababu zetu zilikuwa na hekima zake, na wazee wetu hawakuwa na nia ya kumkandamiza mwanamke, kihivyo, bali ni baadhi ya watu waliokuja baadaye na kuchomeka mambo yao kwa manufaa yao…’akasema mzee mmoja.

‘Ina maana ni kweli kuwa mke anaruhusiwa kumiliki mali akiwa ndani ya ndoa, na mali hiyo isiwe kwenye mamlaka ya mume kwa taratibu za kimila?’ akaulizwa.

‘Unajua kuna kitu kidogo mnakisahau hapo, ndoa ni makubalianao ya mke na mume…hawa watu wakiishi kama ndoa inavyotakiwa, wakapendana, wakawa wanashauriana, wanakubaliana, mbona hilo jibu lake lipo wazi, tatizo mke na mume wanaishi kama wabia…yaani mke kaja kwa mume, lakini bado ana ubinfasi wake, na mume halikadhalika ana ubnafsi wake, ile hali ya ndoa kuwa ni kuwaunganisha mke na mume haipo..ndoa haijatendewa haki yake…’akasema huyo mzee.

‘Mzee unaongea sana..sisi swali letu ni hilo kuwa mke kimila akiwa ndani ya ndoa anastahili kumiliki mali aliyoichuma wakiwa pamoja na mkewe….?’ Akauliza huyo mwanaume tena.

‘Tatizo lenu vijana, mnataka sana kumeza,…lakini huwezi kumeza, bila kutafuna, na huwezei kutafuta bila kukipata hicho kitu na kukiweka mdomoni,…hapo ndipo kwenye tatizo, ili uelewe jambo, usikimbilie kumeza tu, ….nina maana kuwa msipende sana kukimbilia hitimisho la jambo, jaribuni sana kuangalia mzizi, chanzo, sababu…ili hata ukila kile kitu ujue kitakuwa na mafanikio gani kwenye mwili wako…isije ikawa ni sumu..’akasema huyo mzee.

‘Haya tunakusikiliza mzee, maana hawa wazee bwana, wana maneno ya ndani, hawajui kuwa sisi vijana akili zetu zina pupa, tunachotaka ni kujua,…sio kwanini, kwasababu gani, kiini chake ni nini, tunapoteza muda, tuna haraka na maisha…’akasema huyo kijana.

‘Kijana wewe umeoa?’ akaulizwa.

‘Nimeoa, juzi tu…’akasema.

‘Je kabla ya kuoa, ulijuaje taratibu za ndoa, jinsi gani mtaishi na mkeo, na kwanini unatakiwa kuoa?’ akauliza huyo mzee.

‘Kwani hiyo inahitajia shule, hilo lipo kiasili, ukifikia muda wa kuoa, unatakiwa uoe, mambo mengina yanakuja yenyewe…’akasema.

‘Hilo ndilo tatizo, …na chanzo cha yote haya ni hilo tatizo. Wewe kijana ni dereva, ulijuaje kuendesha gari lako, ulijuaje taratibu za barabarani,?’ akuliza mzee.

‘Nilijifunza, kwanza nilienda kusoma VETA, na..na..’akasita kidogo, halafu akasema;

‘Kwanini unauliza hivyo, kwani hilo unalouliza linahusianaje na maswala ya ndoa?’ akauliza huyo mwanaume.

‘Huo ni mfano, kuwa kila jambo lina elimu yake, huwezi kufanya jambo fulani bila kujua undani wake, ..usomee kwanza kitu fulani ili uwe mtaalamu wake. Huwezi kuwa mwanandoa mpaka uoe, na huwezi kuoa bila kujua kwanini unaoa, ..ndoa ni makubaliano ya hiari kati ya mke na mume,…hayo makubaliano lazima yajulikane, …’akasema huyo mzee, watu sasa wakawa wanakuja kusmsikiliza huyo mzee, na kuwa kundi kubwa.

‘Sio tu mumekutana , mkapendana basi hiyo iwe ndio elimu…kupendana ni muhimu, lakini sio kigezo cha kuingia kwenye ndoa moja kwa moja, …lazima kwanza kila mmoja kwa wakati wake ajitahidi kusomea undoa, muijue ndoa ni nini, ina nini ndani yake kutegemeana na imani zenu, je ikiwa hivi na vile tutafanyaje, mimi nina uhakika kuwa mkifanya hivyo, hamtakuwa na matatizi kwenye ndoa zenu….’akasema huyo mzee.
‘Sasa mzee mimi nina kosa gani, maana hakuna shule ya ndoa..ipo wapi hiyo shule?’ akauliza.

‘Shule sio lazima iwepo, kuwa kuna jengo,..sio lazima, walimu wenu hawo mnaowajua nyie walimu wa mambo hayo wanaweza kuwa ni mashangazi na wajomba, mabibi na mababu, hata wazazi wenu,…na zaidi ya hayo wapo wakufunzi wakubwa ambao nii viongozi wenu wa dini…’akasema

‘Labda tutawalaumu sana viongozi wa dini, ambao, mtu akija kwao kutaka kufunga ndoa, hawachukui muda kuwadadisi hawa watu uelewa wao wa ndoa…inahitajika wafanye hivyo, kuwe ni muda wa kuelimishana, kuhakikisha kuwa wamepima afya zao…huenda haya yanafanyika kwenye majumba ya ibada, lakini sio wote wanaoingia huko….’akasema huyo mzee.

‘Wazee kama nyie tunawahitajia sana…..sasa tutafanyaje mzee, maana kama unavyoona, watu wamegombana na sasa wamefikishana hadi mahakamani…na mengi yametokea kwa ajili ya hilo…?’ 
akaulizwa.

‘Jamii , inatakiwa ijue hilo, kuwa ndoa , maisha ya mume na mke, ndio…..chanzo za jamii, kama tutaiweka sawa hii jamii kuanzia hapo…hatutakuwa na tatizo, ..wengi wanafikiria kusoma ni kilele cha kila kitu , lakini tukumbuke katika kusoma kila mtu anasomea jambo lake, ambalo kabisa halihusiani na maisha yao ya ndoa…sasa hii ndoa itajulikanaje….ni lazima jamii yenyewe ielewe hili, hili sio jukumu la serikali…ni jukumu la mzazi, ni jukumu la jamii….’akasema mzee.

‘Mimi ninachowashangaa, inapofikia kipindi cha maandalizi ya harusi, kikubwa mnachoangalia ni shughuli itafanyikaje..magahrama kibao, kwanini hili la kumuelimisha huyu mwanandoa msiliweke kwenye ratiba zenu,….kuwa huyo, mke au mume, naye aambiwe kuwa anahitajika kuhudhuria kisomo, kipindi kile wapo kwenye michakato ya maandalizi ya hiyo ndoa…kuna hicho mnachokiita kitchen party, hivi huko mnajifunza nini….wengi mnaifanya hiyo kama sehemu ya miradi, kupeana zawadi,…’ akasema hivyo na akina mama wakacheka.

‘Ukweli ulivyo , huenda aliyekuwa kabuni hilo alikuwa na maana nzuri tu, lakini sasa wajanja wamechukulia hilo kama ni sehemu ya burudani, kuwezeshana, anayejua kupamba haya, apate chake, kupika haya apate chake,…hamna kusudio hasa la kuelewa nini maana ya ndoa...kwasabbu kitu hicho huwezi kukielimisha kwa siku moja…hebu anzisheni hili kwenye jamii…..na hili lingepewa wakina mama, ambao mnajua kuongea sana, japokuwa kwenye ndoa zenu hamfanyi hivyo…..’watu wakacheka.

‘Lakini pia ni muhimu sana, mambo haya wakahusishwa  wataalmu wa dini, ni muhimu sana, maana wanndoa wanjengwa kuishii kiimani zao, na wataogopa kuetendeana mabaya, kwani wakati wote mungu anawaona…mimi nina imani tukifanya hivyo jamii itaondoakana na maattizo mengi.

‘Kuna watu wanasema nyie kila saa mnazungumizia ndoa, ndoa,badala  ya maendelea, kiukweli maendelea bila amani ya moyoni, maendelea bila upendo, hayaji….maendeleo huanzia nyumbani, jamii iliyojipanga vyema kimaadili, ndiyo inayoweza kuleta maendeleo, maana kutakuwepo na amani, huruma, uaminifu…uhodari wa kuchapa kazi hakuna kutegeana, na vitu kama hivyo, na hivyo huanzia kwenye mke na mume, kwenye ndoa…..’akasema huyo mzee

`Keeesiiiii….’ Kelele za kuashiria kuwa muda wa kusikiliza kesi umefika, na hapo watu wakakimbilia ndani na huku wakimshukuru huyo mzee kwa hekima zake.

********

 ‘Msijali,..’akasema wakili mwanadada tukiwa kwenye mahakama ya juu, kusubria kusoma kwa kesi  ya mauaji yaliyokuwa yakitokea mara kwa mara hapo kijijini. Na mshitakiwa mkuu, akiwa ni shemeji yangu mkubwa, na wakaingizwa washitakiwa hawo, lakini shemeji mkubwa hakuonekana, tukafikiria huenda anaumwa….

‘Kesi ya hukumu  imeahirishwa , kwa vile hakimu kahamishiwa, na mwenzake aliyetakiwa kuja kushika nafasi yake ana dharura, na ukumbuke pia, anahitajika kuipitia kabla hajakubaliana na maamuzi ya mwenzake,….’akasema wakili mwanadada.

‘Hata hivyo ni heri kwetu, maana wahusika wakuu ni wale wale, …tunahitajika pia kwenye kesi hii hapa, hili litatusaidia sana, maana kufanikiwa kwa kesi hii kunasaidia sana,…kwanza kwa uelewi wa watu kuhusu kadhia nzima hii ya kudai haki za mke hazitambuliwi pale mke anapochuma akiwa ndani ya ndoa…lakini pili, ni hili la wanaume wengine kuchukua sheria mikononi mwao, na kuwafanya wanawake ni kama kitu tu…ukikasirika unapiga…’akatulia.

‘Na tatu ambalo ni baya sana, ni hizi imani za kishirikiana, ….hili sasa linakuwa ni tatizo,..kwanini watu wanafikia hatua hiyo,..kweli linaingia akilini, mzazi wako, eti amloge mwanao,amloge mjukuu wake, au shangazi yake….kwanini tunakosa huruma kwa wazee wetu hawa…..’akasema wakili mwanadada.

‘Hili ni tatizo, na tusipolifungia njuga,sheria ikasimama kidete, na kutoa hukumu kali kwa watu kama hawa, basi, laana zitatuandama, ….huwezi ukaishi bila wazee, na bila wao, sisi tusingelikuwepo, tunahitajika, kuwatunza, kuwahehimu, na kujaribu kuwahudumia, ,…maana hali zao zinazidi kuwa duni kila siku, na mabadiliko ya kimaumbile hayakwepeki, mengine yanatokana na hali duni….’akasema.

‘Mfano, wengine wanasema eti dalili za mchawi zipo kwenye macho yake, eti kwa vile wanatembea usiku…na vitu kama hivyo, unasahau kuwa huyo mama, anaishi kwenye nyumba duni, anapika kwa kuni, nyumba hiyo haipitishi hewa, ….macho yanaathirika na moshi…unafikiri macho, yake yatakuwaje, unafikiri ngozi yake ya mwili itakuwaje kwa hali kama hiyo, kaz I ngumu za suluba, hana muda wa kujipaka hata mafuta…’akajionyesha kama vila anajipka mafuta.

‘Huyu mtu kwa hali yake hiyo kutokana na suluba hiyo, unakuja kumuita mchawi,…hili kweli ni tatizo kubwa, na linasabishwa na adui ujinga…’akasema mwanadada.

‘Sasa ni kazi ya sheria, ni kazi ya jamii, ni kazi ya kila mmoja, viongozi wa dini nk, kulibadili hili, na kwenye katiba inatakiwa hili liwekwe wazi jinsi gani ya kuwalea wazee wetu….wazee watafutiwe njia ya kulelewa, na kuthaminiwa, wenzetu ulaya, wazee wana sehemu zao..lakini sisi bado tunahitajia kukaa na wazee wetu, …kinachohitajai ni jinsi gani ya kuwahudumia, hata ikibidi kukatwa kodi kwa ajili ya kuwahudumia wazee,

‘Kweli hili la kukatwa kodi kwa wazee hawa ni muhimu sana, na inastahili kabisa tufanye hivi maana leo yeye kesho na wewe utazeeka, wazee, wanaongezeka, na wanaachwa hivi hivi, baada ya kunyinywa kwenye kazi zisisoza na maslahi, na kuhudumia watoto, ambao baadaye wanakuja kuwaita wazee hawo wachawi….’akasema wakili mwanadada.

‘Sasa kwenye kesi yetu hii, tunahitajika kutoa ushahidi, mimi mwenyewe nitakuwa nawasaidia mashahidi, ….ili haki itendeke,….nawakata mseme ukweli ilivyokuwa, jinsi gani mnavyotendewa huko majumbani, hadi ikafikia hatua hiyo….’akasema wakili mwanadada.

‘Kama mlivyoona, bado mauji yanaendelea, hatukutarajia hilo tukio chanzo chake ni ndani ya jamii yetu kwasababu ya mambo ya kurithi, mambo ya mali ….za kifamilia, na wajanja wamelichukua na kuingiza mambo yao kiujanja  na hii nikuthibitisha kuwa kuna kundi, lenye mipango, na huenda linamizizi mahali, kuna wafadhili, na humu kwenye jamii kunatumika kama sehemu ya kueneza sumu zao.

‘Mimi matarajio yangu, jinsi kesi inavyokwenda, tutagundua mengi, ….sitaki kusema mengi, ila ninahisi kuna mhusika mkuu aliyejificha na hajakamatwa, huyo wanayesema ni muhusika mkuu, huenda ni chambo tu,na nahisi, huenda hakuwa yeye….ngoja tutaona ndani ya ulingo huu…..’ akasema akionyesha mbele ya mahakama,

‘Na mimi nitajitahidi kadri ya uweo wangu kumfichua kwa kutumia silaha ya maswali na majibu…’akasema wakili mwanadada.

Na wakati mwanadada huyu anaendelea kuongea mimi akili yangu ikawa inakumbuka tukio zima lilotokea, karibuni,…siku ile alipokuja shemeji, na kunishawishi twende kumuona kaka yake, ambaye kagoma kula, japokuwa nilijitahidi kukataa, lakini moyo wa huruma ukanijia, na kwa muda baba wa kufikia alikuwa hayupo, nikaona, sio ubinadamu, basi tukaondoka na shemeji yangu huyo hadi huko mahabusu alipokuwa kawekwa shemeji mkubwa, na tulipofika tulimkuta akiwa kwenye hali mbaya sana.

‘Tangu afike hapa  leo siku ya ngapi vile….., hajala kitu, kagoma kabisa kula….’akasema mlinzi wa hapo, na hapo mdogo mtu akamsogelea kaka yake pale alipokuwa kakaa, …akiwa hana nguvu kabisa, akamuinua huku akiwa na chakula mkononi, akitaka kumlisha, na yeye akawa anagoma, na baadaye mdogo mtu akakta tamaa, na kuniangali mimi kuwa ninaweza kusaidia akasema;

‘Kaka kula kidogo, huyu hapa shemeji yako, kasema yupo tayari kukusaidia….’akasema na ndugu yake huyo aliposikia akitajwa shemeji yake akainua uso, na kuniangalia, na mara nikaona machozi yakianza kumtoka,nikashangaa kulikoni, halafu kwa sauti ya shida akasema

 ‘Shemji hatimaye umefika, kuniona nikifa au ….hata hivyo nisamehe sana,….ila nasema, na ninakiri moyoni, sina kosa, nilifanya hayo niliyoyafanya kwa nia njema kabisa, nikiangalia pande zote,sijui nilikosea nini, lakini nina imani, ipo siku mtagundua hayo, na mtanikumbuka, …mimi tena basi….’akatoa hauli hiyo na hakuweza kusema neno jingine, akafumba macho….na kuelegea kabisa, wakajaribu kumfunua mdomo wamlishe kwa nguvu, lakini ikashindikana kabisa.

‘Oh, sasa hili tatizo,….’akasema mdogo mtu, huku mimi nikikumbuka kauli ya huyo shemeji mdogo, akisema kuhusu kaka yake kumwambia baba yangu wa kufikia;

 ‘Mzee hio silipingi,…maana kila mmoja anastahili kufanya hivyo, akiona kadhulumiwa, lakini tunachohitajika kwa sasa ni kumsaidia huyu ndugu yetu, kupata hiyo dhamana, mimi namfahamu sana kaka yangu, hataweza kuvumilia kukaa rumande siku mbili, kama atandelea kubakia huko rumande,….hatutakuja kuelewana naye tena…..tutakuwa tumejenga uhasama wa kudumu’akasema.

Hali ya kaka yake huyo siku hiyo ilizidi kuwa mbaya, ikabidi akimbizwe hospitalini, na alipofika huko akawekewa mipira ya kuongeza maji, na lishe….hali yake iliendelea vyema baadaye, na leo alitarajiwa kufika mahakamani, lakini cha ajabu hakuonekana kwenye kundi la washitakiwa.

Kabla hatupata muda wa kuulizana, na mara akaja shemeji mdogo, akiwa  kavalia tofauti na jinsi anavyovaa, kavalia kinyumbani zaidi, …huwa mara nyingi anakuwa kwenye suti na tai shingoni, lakini leo kavaa fulana na cha ajabu macho yalionekana kuvimba,  akionyesha kuwa alikuwa akilia. Mimi mwili ukaanza kunisisimuka, maana mwanaume akilia ujue kuna jambo….

‘Vipi kuna nini tena…?’ nikauliza huku nikisimama kumkabisli shemeji yangu huyo, yeye akasema kwa sauti ya uchungu;

 ‘Shemeji kwanini humkunisikiliza, kwanini hamkutaka kunielewa, niliwaambia kuwa ninamfahamu sana kaka yangu,hakuwa na kosa,nyie ndio mngeliweza kumuokoa, nikawasisitiza sana ….angalieni sasa ilivyotokea,…kaka yangu hayupo tena duniani….’akasema na kuangusha kilioa kama mtoto mdogo…na kesi ikaahirishwa.

NB: Ilikuwaje hapo…..


WAZO LA LEO: Huenda wakati sasa umefika kabla ya ndoa, wanandoa wahudhurie kisomo cha ndoa, ili kuziokoa ndoa nyingi zinazolega lega. Wapo wanandoa wanaishi kwa jina la mume na mke, lakini ukichunguza undani wake, uhalisia wake haupo, na huenda ndoa hiyo haipo tena. Je hatuoni kuwa chanzo cha kuvunjika kwa amani huanzia ndani ya jamii, jamii iliyotokana na mke na mume. Hawa wawili wakiishi kwa amani, upendo, na ushirikiano, ndio wanaoweza kuzaa matunda mema, ya watoto, ambao watakuja kulelewa kwa  maadili mema. Ni wazo muhimu la leo
Ni mimi: emu-three

5 comments :

Unknown said...

Acha aende na roho mbaya zake naona wanaangalia upande wao tu.

Unknown said...

Acha aende na roho mbaya zake naona wanaangalia upande wao tu.

Unknown said...

Wamemnyanyasa sn dada wawatu kipindi kafiwa namumewe sasa mungu ndo anawalipia yoote

emuthree said...

Ndugu yangu Nancy, hivi kule kwetu, akina mama(wajane) wanafanyiwa hivi?

Unknown said...

Hakuna kitu kama hicho wala hizo mila zao zisizo na haki hatufuatiliagi, sisi ni watu wastarabu sana ndio mn inaniuma km nafanyiwa Mimi yaani.