‘‘Haya chukua zawadi
yako hii, kachezee eeh, hizi ndio zawadi za kuchezea watoto, usichezee uchafu,
unanisikia eeh, mtoto mnzuri, mimi ni nani….’
Sauti hii ikawa
inanijia kila mara kichwani, hadi nikajisikia kichwa kikiuma, nikawa najiuliza ni
kwanini sauti hiyo imekuwa ikinijia mara kwa mara kichwani kwangu, je kuna kitu
nahitajika kukitenda, ina maana nihitajika nikamuokoe shemeji yangu, kama baba
mkubwa wa mtoto wangu au….
Na hapo ukumbuke kuwa,
kwa wakati huo shemeji yangu alikuwa akinisubiria niondoke naye, ili kaka yake
aweze kupewa dhamana, ….na wakati huo baba wa kufikia keshasema nisiondoke. Je nitafanyeje
Tuendelee ni
sehemu hii iliyokuwa imebakia kutoka sehemu iliyopita.
************
‘Baba tafadhali nakuomba tuongee pembeni kwanza’nikamsihi
baba yangu huyo wa kufikia, na yeye kusikia hivyo, akawa kama kashituka, na
kuniangalia kwa jicho la kushangaa na kusema;
‘Ina maana unataka kunisaliti?’ akaniuliza na kabla
sijamjibu huyo shemeji yangu akasema;
‘Mzee nakuomba tafadhali,….sio kwamba anakusaliti, …. naomba
niende na shemeji ili akanisaidie kwa hili, na mimi ninaahidi kuwa nitayasawazisha
haya yote na tutaishi kwa amani ..lengo langu mimi nataka familia hii iwe na
amani,na mimi kama mzazi, nataka nisaidie kote, bila kubagua..’akasema.
‘Mimi msimamo wangu ni huo huo,…kwanza niwaulize nyote
wawili, hebu niambieni mke wangu yupo wapi, kama haya mengine mnayapuuzia, na
mpo tayari kuyasawazisha, ..lakini je mnasema nini kuhusu mke wangu, je hicho
alichofanyiwa ni sahihi, je haki yake ipo wapi, au nyote mumekubaliana na hayo
yaliyotokea kuwa yalistahili kuwa hivyo, kama mzee, kama mnavyoona ni mchawi,
basi hiyo ndio ilikuwa haki yake kutendewa hivyo…?’ akauliza.
‘Baba mimi sijasema kuwa nimekusaliti, mimi nipo na wewe na
nitapigania haki ya mama mpaka mwisho, hatua yangu ya kwanza ilikuwa
kuhakikisha kuwa mali zangu zimerudi mikononi mwetu, na hilo la mama ilikuwa
hatua ya pili…lakini tunahitajika kuwapenda adui zetu, ili tuweze kusimama
kwenye usahihi..na sio kulipiza kisasi’akasema huyo mwanamama.
‘Sasa sikiliza binti, naona umeshawishika, sijui kwa vile
umempenda huyu jamaa, au kwa vile ni baba damu ya baba wa mtoto wako,…mimi
nayafanya haya kwa ajili yako, kwahiyo nakuomba unisikilize mimi …..nina maana yangu kubwa
sana,kama umeamua kuwasikiliza hawa jamaa, mimi naondoka, lakini uakuja kunikumbuka,mimi
msimamo wangu ni huo huo, sasa uamuzi ni wako…’akasema huyo baba na kuanza
kuondoka.
‘Mzee sio hivyo…..’akasema mwanasheria akijaribu kumzuia
huyo mzee asiondoke kwanza, na wakati huo mwanamama naye alikuwa naye
keshachanganyikiwa hakujua afanye nini. Akasimama huku kashika mdomo kwa
mshangao, alikuwa keshatahayari, na hakupenda baba yake wa kufikia aondoke
akiwa na kinyongo naye,
‘Baba tafadhali usiniache kihivyo , mimi ni binti yako, na
sijasema kuwa nitakuwa upande wao, kamwe siwezi kukusaliti….’akasema mwanamama.
‘Mimi nafanya hivyo kwavile nimeshagundua mengi….na
ninawafahamu hawa watu, nimeshayafahamu malengo yao, ndio maana nikakuelezea
vikao vyao walivyofanya,jiulize nimegunduaje hayo yote ….hii ni kukutambulisha
kuwa ninajua mambo yao mengi waliyoyapanga, na hili la kuja kukurubuni wewe ni
moja ya mipango yao….nisingelipenda kuongea kila kitu hapa, maana mengine ni
ushahidi ….’akasema akiwa kasimama.
‘Mzee mimi sikukatalii kwa hayo unayotaka kufanya, hiyo ni
haki ya kila mtu, kudai, na kulalamika pale anapoona kuwa umeonewa, lakini kwa
hili la sasa ninaloomba ni ili tuweze kumwekea kaka yangu dhamana, …na hataweza
kufanikiwa kwa hilo, kama shemeji hatakwenda kumtetea kuwa hilo lililotokea dhidi
yake...ilikuwa ni bahati mbaya tu, ni hasira tu, ulikuwa ni mzozo kidogo wa
kifamilia, na hilo tungeliweza kulisawazisha wenyewe, najua kweli kaka
alikosea, kwa hasira zake, lakini ina maana kwa hilo akafungwe, hatuwezi
kulisawazisha nyumbani…?’ akawa kama anauliza na kabla hajajibiwa akasema.
‘Kaka ana tatizo hilo…na kutokana na mzozo huo, akatumia
mbinu ile kama kutishia, lakini hakuwa na nia mbaya, ninachotaka shemeji
akasema huko , ni hizi, ya kuwa ule ulikuwa ni mzozana kidogo wa kifamilia, na
kaka alikasirika, na pale alipoonekana kashikwa shingoni ilikuwa ni kutishana
tu , hakukuwa na maana ya kuumizana…basi kwa hilo kaka atakubaliwa dhamana,
maana wamemshikilia na kusema wanaogopa akiachiwa atakuwa ni tishio kwa
shemeji…..’akasema huyo mwanasheria.
‘Kwa mtizamo wangu, ni bora ndugu yako akashikiliwa hivyo
hivyo kwa muda,….ili asishirikiane na hawo watu…maana kesi iliyopo mbele yao ni
kubwa sana, wewe hujui ni nini kilichopo nyuma ya pazia, …..yaliyoyotokea ni
makubwa sana, na yote yameshawekwa mezani yanamsubiria hakimu…..’akasema.
‘Mzee hio silipingi,…maana kila mmoja anastahili kufanya
hivyo, akiona kadhulumiwa, lakini tunachohitajika kwa sasa ni kumsaidia huyu
ndugu yetu, kupata hiyo dhamana, mimi namfahamu sana kaka yangu, hataweza
kuvumilia kukaa rumande siku mbili, kama atandelea kubakia huko
rumande,….hatutakuja kuelewana naye tena…..tutakuwa tumejenga uhasama wa kudumu’akasema.
‘Ndio hivyo…..mimi ninayajua ambayo wewe huyajui…siwezi
kukuambia kwa sasa ni kwanini nataka iwe hivyo, na sitaweza kukuelezea kwa sasa
kwanini sitaki shemeji yako muondoke naye kwenda huko, cha muhimu, ili kumsaidia ndugu yako, …..wewe
nenda kamshawishi akubali kusema ukweli…kwani anafahamu mambo mengi ambayo
ndiyo yatamponza, kwa ufahamu wake huo, wenzake ….oh, haya ni ya siri….. na
yeye bila kujijua anajiingiza kichwa kichwa tu…muokoe ndugu yako, na njia pekee
ya kumuokoaa ni kumuacha huko huko rumande’akasema huyo mzee.
‘Unajua mzee hapo hatujaelewana, hilo silipingi,….lakini
kila raia ana haki ya kupata dhamana, na dhamana nyingine hazitolewi , kama mtu
anaonekana ni tishio, kwa amani za wengine…sio kweli kuwa kaka yangu ni tishia,
kwa amani ya shemeji ….basi ili isionekene hivyo, ni kitu kidogo tu, kwa
shemeji kwenda kusema kuwa hakuna tishia kwake kutoka kwake apewe dhamana…..’akasema
huyo mwanasheria.
‘Kijana, mimi sijazaliwa leo, nafahamu sana ni nini
mnakitafuta kwa huyu binti,na mimi kama mzazi wake sitakubali aingie kwenye huo
mtego ilihali nimeshagundua lengo lenu ni nini…’ akasema huku akiinua inua
fimbo yake kama anatishia.
‘Ninachokuambia tena na tena, hili ni kwa kuwasaidia tu, wewe nenda huko rumande, kaongee na huyo
ndugu yako, kwanza mkanye na muweke sawa maana hilo kundi alilojiunga nalo
halina malengo mema kwake,….pili kama kweli anajali haki, basi ajitakase yeye
mwenye kwanza, maana huwezi kuweka kitu kisafi kwenye chombo kichafu,…na tatu
awe tayari kusema ukweli,…na hapo atakuwa keshajiokoa yeye mwenyewe,
vinginevyo, yeye, na hata ikibidi wewe, mtakuwa hatiani, kwa kushirikiaan na
wauaji…’akasema huyo mzee.
‘Mzee tafadhali….kwanza una ushahidi gani na hayo, ya kuwa
hilo kundi la hawo wazee ni wauwaji….hawa wazee nawafahamu sana, wanaheshimika
hapa kijijini, leo hii unawashutumu kwa hayo mauaji yaliyofanywa na hawo
wahuni, kwanza vijana wenyewe wameshakufa….una ushadi wowote wa hiyo shutuma
yako?’akawa anajitetea huyo mwanasheria na akauliza hilo swali.
‘Kijana, usituone ni wazee ukatuzarau, nay a kuwa hatujaenda
shule kwahiyo hatujui kutafuta ushahidi,
hatujui sheria….kumbuka mambo kama haya yalikuwepo zamani, na kipindi hicho
hapakuwa na shule, …..kukitokea jambo, uchunguzi unafanyika na ushahidi unapatikana,….mimi
hayo nayajua sana, msione nilikuwa kimiya, mkazania huyo mzee keshaisha …hivi
kweli watu wamfanyie vile mke wangu, mimi nikae kimiya tu….sasa sikiliza
nakuambia kwa mara ya mwisho,…na hili linatoka moyoni….’akatulia na kumkazia
macho huyo mwanasheria.
‘Mimi mzee, ninakuapia, …labda hawo watu wanitangulize mimi kaburini,
kabla kesi hiyo haijasikilizwa. Lakini kama nitaendelea kuwepo hai, hawo wote waliohusika na hili,….wataishia jela…ushahidi
ninao, sina shaka…hata kama wataupindisha vipi, hawo watu hawaokoki kipindi
hiki…’akasema huyo mzee.
‘Mzee, hilo ni haki yako, ila mimi ninakuomba sana mzee,
usimtishe huyu shemeji yangu, muachie uhuru, ili tuweze kuyamaliza haya
kinyumbani…haya ya kwake, na huyo shemeji
yake, yaliyotokea hapa ni madogo kama tutayachukulia kibinadamu, lakini
ni makubwa kama tutayachukulia kiuhasama…na tukichukulia kiuhasama, mimi sizani
kama yatatusaidia lolote huko mbeleni, tukianza kulipizana kisasi, hatutaweza
kufika mwisho wa haya , nakuomba sana mzee utumie hekima zako….tulimalize hili
kwa amani’akasema huyo mwanasheria.
‘Hekima yangu, tena ya hali ya juu, ni hawo wote
walioshiriki kwenye haya maasi, wafikishwe mbele ya sheria, wakajibu na
wahukumiwe kutokana na makosa yao, na haki hiyo haitapatikana bila kufikishana mahakama,
wewe mwenyewe unafahamu hilo, sasa ngoja sheria ifanye kazi yake….bila hivyo,
bado tutakuwa tunamficha nyoka mwenye sumu kali ndani ya chumba tunapolala…na
hili kama hatutajitolea watu wengine kupambana nalo, kizazi hadi kizazi
kitakuwa kwenye matatizo….sheria imewekwa na itekelezwe kwa haki..na kiukweli haya
yatabainishwa vyema mahakamani, na sio huku majumbani….huku majumbani
tutadanganyana…’akasema huyo mzee.
‘Sawa mzee, kama umeamau hivyo, basi, na mimi itabidi nikajiandae
kwa hilo maana nakuona lengo lako ni shari, nilijua wewe ni mzee wa hekima, na
upo tayari kutumia hekima yako ili na sisi vijana tuige kwako, lakini ….nakuona
una chuki, na nia na lengo lako ni kulipiza kisasa….na mimi sitakubali ndugu
yangu ashitakiwe kwa kosa ambalo hajalifanya,….kama ndugu, kama mwanasheria,
nitamtetea kwa nguvu zangu zote…’akasema huyo mwanasheria huku akikunja uso wa
chuki.
‘Sawa kabisa kijana, basi tutakutana huko huko
mahakamani,..mimi ni mwanasheria wa kizamani,sijafika darasani, lakini nimeenda
darasa la nje, la kihalisia, jinsi tunavyoishi ndivyo tunavyojifunza, kuishi
kwangu nimekuwa nikitafiti mambo mengi, mojawapo ni haya, ya kisheria…kama
umeamua hivyo, basi tutaona mbele ya sheria wewe na kisomo chako, mimi na
uzoefu wangu, je ni elimu ipi yenye nguvu, ukumbuke mimi nasimamia kwenye haki na
ukweli, ….kutetea wanyonge, …wewe unasimama kwenye udugu na kulindana, kutetea
wenye nacho, kutetea masilahi….’akasema na kugeuka kumwangali binti
yake.akamuuliza
‘Je bnti yangu upo pamoja na mimi….?’ Akauliza na kabla
hajasikia jibu la huyo binti simu ya huyo binti aikaita, yule binti akawa kama
kashituka kutokana na huo mlio, na kwa haraka akaitoa simu yake kwenye mkoba,
uliokuwa mezani, na kuangalia ni nani aliyempigia, …alikuwa wakili mwanadada,
na akageuka kumwangalia mwanasheria ambaye alikuwa kasimama mlangoni, akiwa
bado anasita kuondoka,na aliposikia hiyo simu ikiita akageuka kumwangalai
shemeji yake na macho yao yakakutana, na mwanamama, akageuka pembeni, na kusema.
‘Samahani kidogo…nataka nikaipokee hii simu pembeni.’akasema
mwanamama na kutoka nje ya hiyo na mwanasheria akatoka vile vile na kwenda
kusimama barabarani, alikuwa hajakata tamaa.
‘Unasubiri nini kijana, nenda ….kama nilivyokuambia, hapa
unapoteza muda, usipowahi wewe wenzako atamuwahi , na hujui lengo la hawo
wazee, na nikuambie ukweli usipozina ufa kwa sasa, utakuja kujuta….nakuasa
kwasababu wewe ni kijana mzuri, na haya yote umejikuta unaingizwa bila yaw ewe kujua
undani wake, na kama ungelijua undani wake, kwa jinsi ninavyokuwazia ulivyo,
nina uhakika usingelipoteza muda wako kuwatetea watu kama hao…’akasema huyo
mzee.
‘Kwanini usiniambi ukweli, nikajua , yakaisha, maana kama
kuna ukweli ambao utanisaidia mimi, ni bora uuseme, vinginevyo ninachukulia
hayo kama kujitetea tu, kwa kuogopa kuwa nitasimama kama wakili kumtetea ndugu
yangu,…’akasema.
‘Mimi sijitetei, na wala siongei hili kwa kukuogopa
wewe..hata siku moja siwezi kukuogopa wewe, maana huna lolote lakuweza
kunitisha,elimu yako ni ndogo sana ukilinganisha na elimu yangu ya uzoefu….na
sitetei kwa ajili ya maslahi, sitetei kwa vile ninataka kumlinda mtu,
ninachotetea ni haki…nalalamika kutokana na dhuluma aliyotendewa mke wangu,
wanayotendewa wajena…je hilo peke yake halitoshi kuwa silaha….’akasema huku
akiangalia kule alipokuwa binti yake akiendelea kuongea na simu.
‘Huwezi ukasema unatetea haki bila vigezo vya ushahidi…inawezekana
ukaiita ni haki kumbe ni kwa utashi wako tu, …hiyo unayoiita haki kwa utashi
wako, ukiipeleka kwenye mizani ya sheria, inaweza ikawa ni mbinu za kupotosha
haki…kumbe sio haki ni batili…sasa mimi nimesomea sheria, na pia nimeishi na
kaka yangu,….sijaona kosa la ndugu yangu kwa hilo, unalotaka kumshitaki nalo….’akasema.
‘Kijana mimi sijamshitakia ndugu yako, ndugu yako
kashitakiwa na jamuhuri…ukumbuke wao kama serikali,walikuwa wakifanya uchunguzi wao, na
baadaye wakagundua kuwa ndugu yako ni muhusika mkuu….sijajua wao waligundua
nini…mimi nikapeleka malalamiko yako kwa dhuluma aliyofanyiwa mke wangu,
nikaambiwa hilo wanalifanyia kazi, na pindi tu, watawasimamisha wahusika wote
mahakamani, na wameshaanza kuwakamata mmoja baada ya mwingine, kwahiyo
kukamatwa kwa ndugu yako, ni sehemu tu ya mikakati yao, watakamatwa wengi, na ……mengi
yatagundulika..sisi wananchi tunaokitakai vyema kijiji hichi tunahitajika kutoa
ushirikiano wetu, ili kufichua huu udhalimu….’akasema mzee.
‘Mimi tangu mwanzo nimejiweka wazi, kuwa hilo la kesi, sina
utata nalo, ngoja kesi ifikishwe mahakamani, na haki itatambulikana,…..nilichokuwa
nataka ni kutimiza wajibu wangu, kama mwanasheria, lakini pia kama ndugu,…huyo
mtu apewe dhamana, maana ninamfahamu …lolote linaweza kutokea, …na sitakubali
nije kulaumiwa kwa hilo….’akasema huku akiangalia saa yake na akamwangalia
mwanamama ambaye alikuwa kamaliza kuongea na simu,...
‘Unasemaje shemeji, utanisaidia kwa hili, au umeamua
kuitelekeza familia yetu, ukumbuke sisi ni wanafamilia, baba za mtoto….uliolewa
na ndugu yetu, na ukitutupa sisi , hutakuwa umetutendea haki, timiza wajibu
wako, ili ukidai haki yako isionekane unalipiza kisasi….’akasema huku kashika
kidevu, akijua huenda sasa shemeji yake atakubaliana naye, na akikataa , basi,….,
na mwanamama akamsogelea baba yake huku akiwa kamwangalia shemeji yake, na kumshika
baba yake wa kufikia mkono, akasema;
‘Baba nakuomba,…..hili sio kwamba nalisema mimi tu, bali
hata mwanadada, yaanii wakili wetu, katuomba tukamtoe huyo shemeji huko
rumande, maana tukifanya hivyo, tutakuwa tumejionyesha jinsi tulivyo, kuwa
kweli tunatetea haki, na sio vinginevyo, na wakili wetu huyo kasema atafika
hapa karibuni, kwa ajili ya kutetea haki ya mama na haya yote…anasema tusifanye
mambo kama tunalipiza kisasi, tudai haki kwa
haki bila kuweka chuki na visasi mbele….’akasema mwanadada.
‘Kwa hilo sitakubali, awe mwanadada, au mwanasheria,
sitakubali wewe kwenda huko, kama utaamua kwenda, ujue ,umenisalit I na hatupo
pamoja na wewe..mimi kama mzazi nimekuambia ninafahamu lengo la hawa watu,
siongei kwa kuwa nataka kulipiza kisasi naongea kwa kile
ninachokifahamu..nisikilze mimi..usiende huko…..’akasema huyo mzee.
‘Lakini mzee….kasema wakili mwanadada…’akaanza kujitetea na
mwanasheria akasema kwa sauti,
‘Mzee muache twende, mimi nipo pamoja na haki, nitamlinda
kwa lolote lile….’akasema kwa sauti na mzee akageuka kumwangalia huyo mwanamama,
na kusema;
‘Usiende….’
NB: Nenda, usiende, wewe unamshauri nini huyo mwanamama, na
je huyo mzee ana nini kikubwa, ni kisasi na chuki au….tuendelee kuwepo.
WAZO LA LEO: Kila
mtu ana mtizamo wake wa kudai haki, na ni haki ya kila mtu kufanya hivyo, hata
kama haki hiyo isiwe ni haki, lakini kwa
mtizamo wako unaiona ni haki yako,je ikifikia hali kama hii, wewe unadai haki,uionayo
ni haki yako na wenzako wanaiona hiyo sio haki na batili, utafanayeje. Cha
msingi kuliko kujenga uhasama, chuki, na visasi, ni bora tukaenda kwenye vyomvo vya sheria, kwenye mabaraza ya
usuluhishi, au hata kwa wakuu wa dini, ili tukasikilizwe madai yetu. Tukiamua
kuchukua sheria mikononi mwetu, tutakuwa hatudai haki tena na mwisho wake, ni
kujuenga chuki, uadui, na visasi visivyokwisha.
Ni mimi:
emu-three
3 comments :
Jamani asiende alivyokuwa anamnyonga angekufa nani angeenda kuwatetea au ndio ingekuwa marehemu hana haki❓asiendeee
Jamani asiende alivyokuwa anamnyonga angekufa nani angeenda kuwatetea au ndio ingekuwa marehemu hana haki❓asiendeee
Asieendeee, nya n kini ichi❓
Post a Comment