Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, July 3, 2013

WEMA HAUOZI-29


‘Haya chukua zawadi yako hii, kachezee eeh, hizi ndio zawadi za kuchezea watoto, usichezee uchafu, unanisikia eeh, mtoto mnzuri, mimi ni nani….’

Sauti hii ikawa inanijia kila mara kichwani, hadi nikajisikia kichwa kikiuma, nikawa najiuliza ni kwanini sauti hiyo imekuwa ikinijia mara kwa mara kichwani kwangu, je kuna kitu nahitajika kukitenda, ina maana nihitajika nikamuokoe shemeji yangu, kama baba mkubwa wa mtoto wangu au….

Na hapo ukumbuke kuwa, kwa wakati huo shemeji yangu alikuwa akinisubiria niondoke naye, ili kaka yake aweze kupewa dhamana, ….na wakati huo baba wa kufikia keshasema nisiondoke. Je nitafanyeje

    Tuendelee ni sehemu hii iliyokuwa imebakia kutoka sehemu iliyopita.

                                                    ************
‘Baba tafadhali nakuomba tuongee pembeni kwanza’nikamsihi baba yangu huyo wa kufikia, na yeye kusikia hivyo, akawa kama kashituka, na kuniangalia kwa jicho la kushangaa na kusema;

‘Ina maana unataka kunisaliti?’ akaniuliza na kabla sijamjibu huyo shemeji yangu akasema;

‘Mzee nakuomba tafadhali,….sio kwamba anakusaliti, …. naomba niende na shemeji ili akanisaidie kwa hili, na mimi ninaahidi kuwa nitayasawazisha haya yote na tutaishi kwa amani ..lengo langu mimi nataka familia hii iwe na amani,na mimi kama mzazi, nataka nisaidie kote, bila kubagua..’akasema.

‘Mimi msimamo wangu ni huo huo,…kwanza niwaulize nyote wawili, hebu niambieni mke wangu yupo wapi, kama haya mengine mnayapuuzia, na mpo tayari kuyasawazisha, ..lakini je mnasema nini kuhusu mke wangu, je hicho alichofanyiwa ni sahihi, je haki yake ipo wapi, au nyote mumekubaliana na hayo yaliyotokea kuwa yalistahili kuwa hivyo, kama mzee, kama mnavyoona ni mchawi, basi hiyo ndio ilikuwa haki yake kutendewa hivyo…?’ akauliza.

‘Baba mimi sijasema kuwa nimekusaliti, mimi nipo na wewe na nitapigania haki ya mama mpaka mwisho, hatua yangu ya kwanza ilikuwa kuhakikisha kuwa mali zangu zimerudi mikononi mwetu, na hilo la mama ilikuwa hatua ya pili…lakini tunahitajika kuwapenda adui zetu, ili tuweze kusimama kwenye usahihi..na sio kulipiza kisasi’akasema huyo mwanamama.

‘Sasa sikiliza binti, naona umeshawishika, sijui kwa vile umempenda huyu jamaa, au kwa vile ni baba damu ya baba wa mtoto wako,…mimi nayafanya haya kwa ajili yako, kwahiyo nakuomba  unisikilize mimi …..nina maana yangu kubwa sana,kama umeamua kuwasikiliza hawa jamaa, mimi naondoka, lakini uakuja kunikumbuka,mimi msimamo wangu ni huo huo, sasa uamuzi ni wako…’akasema huyo baba na kuanza kuondoka.

‘Mzee sio hivyo…..’akasema mwanasheria akijaribu kumzuia huyo mzee asiondoke kwanza, na wakati huo mwanamama naye alikuwa naye keshachanganyikiwa hakujua afanye nini. Akasimama huku kashika mdomo kwa mshangao, alikuwa keshatahayari, na hakupenda baba yake wa kufikia aondoke akiwa na kinyongo naye,

‘Baba tafadhali usiniache kihivyo , mimi ni binti yako, na sijasema kuwa nitakuwa upande wao, kamwe siwezi kukusaliti….’akasema mwanamama.

‘Mimi nafanya hivyo kwavile nimeshagundua mengi….na ninawafahamu hawa watu, nimeshayafahamu malengo yao, ndio maana nikakuelezea vikao vyao walivyofanya,jiulize nimegunduaje hayo yote ….hii ni kukutambulisha kuwa ninajua mambo yao mengi waliyoyapanga, na hili la kuja kukurubuni wewe ni moja ya mipango yao….nisingelipenda kuongea kila kitu hapa, maana mengine ni ushahidi ….’akasema akiwa kasimama.

‘Mzee mimi sikukatalii kwa hayo unayotaka kufanya, hiyo ni haki ya kila mtu, kudai, na kulalamika pale anapoona kuwa umeonewa, lakini kwa hili la sasa ninaloomba ni ili tuweze kumwekea kaka yangu dhamana, …na hataweza kufanikiwa kwa hilo, kama shemeji hatakwenda kumtetea kuwa hilo lililotokea dhidi yake...ilikuwa ni bahati mbaya tu, ni hasira tu, ulikuwa ni mzozo kidogo wa kifamilia, na hilo tungeliweza kulisawazisha wenyewe, najua kweli kaka alikosea, kwa hasira zake, lakini ina maana kwa hilo akafungwe, hatuwezi kulisawazisha nyumbani…?’ akawa kama anauliza na kabla hajajibiwa akasema.

‘Kaka ana tatizo hilo…na kutokana na mzozo huo, akatumia mbinu ile kama kutishia, lakini hakuwa na nia mbaya, ninachotaka shemeji akasema huko , ni hizi, ya kuwa ule ulikuwa ni mzozana kidogo wa kifamilia, na kaka alikasirika, na pale alipoonekana kashikwa shingoni ilikuwa ni kutishana tu , hakukuwa na maana ya kuumizana…basi kwa hilo kaka atakubaliwa dhamana, maana wamemshikilia na kusema wanaogopa akiachiwa atakuwa ni tishio kwa shemeji…..’akasema huyo mwanasheria.

‘Kwa mtizamo wangu, ni bora ndugu yako akashikiliwa hivyo hivyo kwa muda,….ili asishirikiane na hawo watu…maana kesi iliyopo mbele yao ni kubwa sana, wewe hujui ni nini kilichopo nyuma ya pazia, …..yaliyoyotokea ni makubwa sana, na yote yameshawekwa mezani yanamsubiria hakimu…..’akasema.

‘Mzee hio silipingi,…maana kila mmoja anastahili kufanya hivyo, akiona kadhulumiwa, lakini tunachohitajika kwa sasa ni kumsaidia huyu ndugu yetu, kupata hiyo dhamana, mimi namfahamu sana kaka yangu, hataweza kuvumilia kukaa rumande siku mbili, kama atandelea kubakia huko rumande,….hatutakuja kuelewana naye tena…..tutakuwa tumejenga uhasama wa kudumu’akasema.

‘Ndio hivyo…..mimi ninayajua ambayo wewe huyajui…siwezi kukuambia kwa sasa ni kwanini nataka iwe hivyo, na sitaweza kukuelezea kwa sasa kwanini sitaki shemeji yako muondoke naye kwenda huko,  cha muhimu, ili kumsaidia ndugu yako, …..wewe nenda kamshawishi akubali kusema ukweli…kwani anafahamu mambo mengi ambayo ndiyo yatamponza, kwa ufahamu wake huo, wenzake ….oh, haya ni ya siri….. na yeye bila kujijua anajiingiza kichwa kichwa tu…muokoe ndugu yako, na njia pekee ya kumuokoaa ni kumuacha huko huko rumande’akasema huyo mzee.

‘Unajua mzee hapo hatujaelewana, hilo silipingi,….lakini kila raia ana haki ya kupata dhamana, na dhamana nyingine hazitolewi , kama mtu anaonekana ni tishio, kwa amani za wengine…sio kweli kuwa kaka yangu ni tishia, kwa amani ya shemeji ….basi ili isionekene hivyo, ni kitu kidogo tu, kwa shemeji kwenda kusema kuwa hakuna tishia kwake kutoka kwake apewe dhamana…..’akasema huyo mwanasheria.

‘Kijana, mimi sijazaliwa leo, nafahamu sana ni nini mnakitafuta kwa huyu binti,na mimi kama mzazi wake sitakubali aingie kwenye huo mtego ilihali nimeshagundua lengo lenu ni nini…’ akasema huku akiinua inua fimbo yake kama anatishia.

‘Ninachokuambia tena na tena, hili ni kwa kuwasaidia tu,  wewe nenda huko rumande, kaongee na huyo ndugu yako, kwanza mkanye na muweke sawa maana hilo kundi alilojiunga nalo halina malengo mema kwake,….pili kama kweli anajali haki, basi ajitakase yeye mwenye kwanza, maana huwezi kuweka kitu kisafi kwenye chombo kichafu,…na tatu awe tayari kusema ukweli,…na hapo atakuwa keshajiokoa yeye mwenyewe, vinginevyo, yeye, na hata ikibidi wewe, mtakuwa hatiani, kwa kushirikiaan na wauaji…’akasema huyo mzee.

‘Mzee tafadhali….kwanza una ushahidi gani na hayo, ya kuwa hilo kundi la hawo wazee ni wauwaji….hawa wazee nawafahamu sana, wanaheshimika hapa kijijini, leo hii unawashutumu kwa hayo mauaji yaliyofanywa na hawo wahuni, kwanza vijana wenyewe wameshakufa….una ushadi wowote wa hiyo shutuma yako?’akawa anajitetea huyo mwanasheria na akauliza hilo swali.

‘Kijana, usituone ni wazee ukatuzarau, nay a kuwa hatujaenda shule kwahiyo hatujui  kutafuta ushahidi, hatujui sheria….kumbuka mambo kama haya yalikuwepo zamani, na kipindi hicho hapakuwa na shule, …..kukitokea jambo, uchunguzi unafanyika na ushahidi unapatikana,….mimi hayo nayajua sana, msione nilikuwa kimiya, mkazania huyo mzee keshaisha …hivi kweli watu wamfanyie vile mke wangu, mimi nikae kimiya tu….sasa sikiliza nakuambia kwa mara ya mwisho,…na hili linatoka moyoni….’akatulia na kumkazia macho huyo mwanasheria.

‘Mimi mzee, ninakuapia, …labda hawo watu wanitangulize mimi kaburini, kabla kesi hiyo haijasikilizwa. Lakini kama nitaendelea kuwepo hai,  hawo wote waliohusika na hili,….wataishia jela…ushahidi ninao, sina shaka…hata kama wataupindisha vipi, hawo watu hawaokoki kipindi hiki…’akasema huyo mzee.

‘Mzee, hilo ni haki yako, ila mimi ninakuomba sana mzee, usimtishe huyu shemeji yangu, muachie uhuru, ili tuweze kuyamaliza haya kinyumbani…haya ya kwake, na huyo shemeji  yake, yaliyotokea hapa ni madogo kama tutayachukulia kibinadamu, lakini ni makubwa kama tutayachukulia kiuhasama…na tukichukulia kiuhasama, mimi sizani kama yatatusaidia lolote huko mbeleni, tukianza kulipizana kisasi, hatutaweza kufika mwisho wa haya , nakuomba sana mzee utumie hekima zako….tulimalize hili kwa amani’akasema huyo mwanasheria.

‘Hekima yangu, tena ya hali ya juu, ni hawo wote walioshiriki kwenye haya maasi, wafikishwe mbele ya sheria, wakajibu na wahukumiwe kutokana na makosa yao, na haki hiyo haitapatikana bila kufikishana mahakama, wewe mwenyewe unafahamu hilo, sasa ngoja sheria ifanye kazi yake….bila hivyo, bado tutakuwa tunamficha nyoka mwenye sumu kali ndani ya chumba tunapolala…na hili kama hatutajitolea watu wengine kupambana nalo, kizazi hadi kizazi kitakuwa kwenye matatizo….sheria imewekwa na itekelezwe kwa haki..na kiukweli haya yatabainishwa vyema mahakamani, na sio huku majumbani….huku majumbani tutadanganyana…’akasema huyo mzee.

‘Sawa mzee, kama umeamau hivyo, basi, na mimi itabidi nikajiandae kwa hilo maana nakuona lengo lako ni shari, nilijua wewe ni mzee wa hekima, na upo tayari kutumia hekima yako ili na sisi vijana tuige kwako, lakini ….nakuona una chuki, na nia na lengo lako ni kulipiza kisasa….na mimi sitakubali ndugu yangu ashitakiwe kwa kosa ambalo hajalifanya,….kama ndugu, kama mwanasheria, nitamtetea kwa nguvu zangu zote…’akasema huyo mwanasheria huku akikunja uso wa chuki.

‘Sawa kabisa kijana, basi tutakutana huko huko mahakamani,..mimi ni mwanasheria wa kizamani,sijafika darasani, lakini nimeenda darasa la nje, la kihalisia, jinsi tunavyoishi ndivyo tunavyojifunza, kuishi kwangu nimekuwa nikitafiti mambo mengi, mojawapo ni haya, ya kisheria…kama umeamua hivyo, basi tutaona mbele ya sheria wewe na kisomo chako, mimi na uzoefu wangu, je ni elimu ipi yenye nguvu, ukumbuke mimi nasimamia kwenye haki na ukweli, ….kutetea wanyonge, …wewe unasimama kwenye udugu na kulindana, kutetea wenye nacho, kutetea masilahi….’akasema na kugeuka kumwangali binti yake.akamuuliza

‘Je bnti yangu upo pamoja na mimi….?’ Akauliza na kabla hajasikia jibu la huyo binti simu ya huyo binti aikaita, yule binti akawa kama kashituka kutokana na huo mlio, na kwa haraka akaitoa simu yake kwenye mkoba, uliokuwa mezani, na kuangalia ni nani aliyempigia, …alikuwa wakili mwanadada, na akageuka kumwangalia mwanasheria ambaye alikuwa kasimama mlangoni, akiwa bado anasita kuondoka,na aliposikia hiyo simu ikiita akageuka kumwangalai shemeji yake na macho yao yakakutana, na mwanamama, akageuka pembeni, na kusema.

‘Samahani kidogo…nataka nikaipokee hii simu pembeni.’akasema mwanamama na kutoka nje ya hiyo na mwanasheria akatoka vile vile na kwenda kusimama barabarani, alikuwa hajakata tamaa.

‘Unasubiri nini kijana, nenda ….kama nilivyokuambia, hapa unapoteza muda, usipowahi wewe wenzako atamuwahi , na hujui lengo la hawo wazee, na nikuambie ukweli usipozina ufa kwa sasa, utakuja kujuta….nakuasa kwasababu wewe ni kijana mzuri, na haya yote umejikuta unaingizwa bila yaw ewe kujua undani wake, na kama ungelijua undani wake, kwa jinsi ninavyokuwazia ulivyo, nina uhakika usingelipoteza muda wako kuwatetea watu kama hao…’akasema huyo mzee.

‘Kwanini usiniambi ukweli, nikajua , yakaisha, maana kama kuna ukweli ambao utanisaidia mimi, ni bora uuseme, vinginevyo ninachukulia hayo kama kujitetea tu, kwa kuogopa kuwa nitasimama kama wakili kumtetea ndugu yangu,…’akasema.

‘Mimi sijitetei, na wala siongei hili kwa kukuogopa wewe..hata siku moja siwezi kukuogopa wewe, maana huna lolote lakuweza kunitisha,elimu yako ni ndogo sana ukilinganisha na elimu yangu ya uzoefu….na sitetei kwa ajili ya maslahi, sitetei kwa vile ninataka kumlinda mtu, ninachotetea ni haki…nalalamika kutokana na dhuluma aliyotendewa mke wangu, wanayotendewa wajena…je hilo peke yake halitoshi kuwa silaha….’akasema huku akiangalia kule alipokuwa binti yake akiendelea kuongea na simu.

‘Huwezi ukasema unatetea haki bila vigezo vya ushahidi…inawezekana ukaiita ni haki kumbe ni kwa utashi wako tu, …hiyo unayoiita haki kwa utashi wako, ukiipeleka kwenye mizani ya sheria, inaweza ikawa ni mbinu za kupotosha haki…kumbe sio haki ni batili…sasa mimi nimesomea sheria, na pia nimeishi na kaka yangu,….sijaona kosa la ndugu yangu kwa hilo, unalotaka kumshitaki nalo….’akasema.

‘Kijana mimi sijamshitakia ndugu yako, ndugu yako kashitakiwa na jamuhuri…ukumbuke wao kama serikali,walikuwa wakifanya uchunguzi wao, na baadaye wakagundua kuwa ndugu yako ni muhusika mkuu….sijajua wao waligundua nini…mimi nikapeleka malalamiko yako kwa dhuluma aliyofanyiwa mke wangu, nikaambiwa hilo wanalifanyia kazi, na pindi tu, watawasimamisha wahusika wote mahakamani, na wameshaanza kuwakamata mmoja baada ya mwingine, kwahiyo kukamatwa kwa ndugu yako, ni sehemu tu ya mikakati yao, watakamatwa wengi, na ……mengi yatagundulika..sisi wananchi tunaokitakai vyema kijiji hichi tunahitajika kutoa ushirikiano wetu, ili kufichua huu udhalimu….’akasema mzee.

‘Mimi tangu mwanzo nimejiweka wazi, kuwa hilo la kesi, sina utata nalo, ngoja kesi ifikishwe mahakamani, na haki itatambulikana,…..nilichokuwa nataka ni kutimiza wajibu wangu, kama mwanasheria, lakini pia kama ndugu,…huyo mtu apewe dhamana, maana ninamfahamu …lolote linaweza kutokea, …na sitakubali nije kulaumiwa kwa hilo….’akasema huku akiangalia saa yake na akamwangalia mwanamama ambaye alikuwa kamaliza kuongea na simu,...

‘Unasemaje shemeji, utanisaidia kwa hili, au umeamua kuitelekeza familia yetu, ukumbuke sisi ni wanafamilia, baba za mtoto….uliolewa na ndugu yetu, na ukitutupa sisi , hutakuwa umetutendea haki, timiza wajibu wako, ili ukidai haki yako isionekane unalipiza kisasi….’akasema huku kashika kidevu, akijua huenda sasa shemeji yake atakubaliana naye, na akikataa , basi,…., na mwanamama akamsogelea baba yake huku akiwa kamwangalia shemeji yake, na kumshika baba yake wa kufikia mkono, akasema;

‘Baba nakuomba,…..hili sio kwamba nalisema mimi tu, bali hata mwanadada, yaanii wakili wetu, katuomba tukamtoe huyo shemeji huko rumande, maana tukifanya hivyo, tutakuwa tumejionyesha jinsi tulivyo, kuwa kweli tunatetea haki, na sio vinginevyo, na wakili wetu huyo kasema atafika hapa karibuni, kwa ajili ya kutetea haki ya mama na haya yote…anasema tusifanye mambo kama tunalipiza kisasi, tudai haki kwa  haki bila kuweka chuki na visasi mbele….’akasema mwanadada.

‘Kwa hilo sitakubali, awe mwanadada, au mwanasheria, sitakubali wewe kwenda huko, kama utaamua kwenda, ujue ,umenisalit I na hatupo pamoja na wewe..mimi kama mzazi nimekuambia ninafahamu lengo la hawa watu, siongei kwa kuwa nataka kulipiza kisasi naongea kwa kile ninachokifahamu..nisikilze mimi..usiende huko…..’akasema huyo mzee.

‘Lakini mzee….kasema wakili mwanadada…’akaanza kujitetea na mwanasheria akasema kwa sauti,

‘Mzee muache twende, mimi nipo pamoja na haki, nitamlinda kwa lolote lile….’akasema kwa sauti na mzee akageuka kumwangalia huyo mwanamama, na kusema;

‘Usiende….’

NB: Nenda, usiende, wewe unamshauri nini huyo mwanamama, na je huyo mzee ana nini kikubwa, ni kisasi na chuki au….tuendelee kuwepo.


WAZO LA LEO: Kila mtu ana mtizamo wake wa kudai haki, na ni haki ya kila mtu kufanya hivyo, hata kama  haki hiyo isiwe ni haki, lakini kwa mtizamo wako unaiona ni haki yako,je ikifikia hali kama hii, wewe unadai haki,uionayo ni haki yako na wenzako wanaiona hiyo sio haki na batili, utafanayeje. Cha msingi kuliko kujenga uhasama, chuki, na visasi, ni bora tukaenda  kwenye vyomvo vya sheria, kwenye mabaraza ya usuluhishi, au hata kwa wakuu wa dini, ili tukasikilizwe madai yetu. Tukiamua kuchukua sheria mikononi mwetu, tutakuwa hatudai haki tena na mwisho wake, ni kujuenga chuki, uadui, na visasi visivyokwisha. 

Ni mimi: emu-three

3 comments :

Unknown said...

Jamani asiende alivyokuwa anamnyonga angekufa nani angeenda kuwatetea au ndio ingekuwa marehemu hana haki❓asiendeee

Unknown said...

Jamani asiende alivyokuwa anamnyonga angekufa nani angeenda kuwatetea au ndio ingekuwa marehemu hana haki❓asiendeee

Unknown said...

Asieendeee, nya n kini ichi❓