Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, May 10, 2013

WEMA HAUOZI-6



Nilifika eneo la ilipokuepo nyumba ya wazee hawa, babu na bibi yako wa kukulea, nilishangaa kuona kuwa kilichobakia ni matakataka na majivu kila kitu kiliteketea, na watu walikuwa wakipita huku wakibeza, na kusema sasa wamemkomoa mchawi wa kijiji;

‘Hili litakuwa fundisho kwa wale wote wanatuwangia na kutuulia watoto wetu….’akasema mama mmoja na wenzake wakacheka kwa dharau, kicheko kile cha akina mama.

Baadaye nilimpitia rafiki yangu, nkijaribu kukusanya habari, huenda zikaweza kunisaidia kufungua kesi ya kuuliwa huyo mwanamama, na kuharibiwa mali ya wazee hawa, na nilimkuta mwenzangu akihangaika na usafi wa nyumba yake, na aliponiona,akaacha kila kitu na kunikaribisha. Tukaanza mazungumzo, na bila kuficha nikamuuliza swali;

‘Hivi mna ushahidi gani kuwa huyo mwanamama wa watu aliyeuwawa kinyama hivyo alikuwa ni mchawi?’ nikamuuliza rafiki yangu, na yeye akaniangalia huku akionyesha mshangao, akasema.

‘Wewe unataka ushahidi gani mwingine, ….wakati mimi mwenyewe nilikupeka kwa yule mtaalmu, mtaalamu anayeaminika na wanakijiji wote, hata nje ya mkoa huu. Yule sio mchezo bwana, akikuambia kitu, amini…..anaiweza ile kazi sio mchezo. Unakumbuka alivyokuamba kuwa mtoto wako anaumwa, na anayemfanya hivyo ni mama mtu mzima aliyewahi kumlea, sasa ni nani mwingine aliyewahi kumlea mwanao kama sio huyo mwanamama wako, ….unataka nini tena, ..’akaniambia huyo rafiki yangu kwa kujiamini. 

Nilishika kichwa , na kuangalia pembeni, huki nikimuwazia huyo mwanamama wa watu ambaye nilikuwa na uhakika kabisa kuwa hayo wanayomshutumu nayo, hakuwa nayo kamwe.

‘Mimi siamini kabisa hayo mambo…namshukuru mungu kwa hilo. Na pili yule mama namfahamu sana, nimewahi kuishi naye, tena kwa karibu, kipindi waliponipokea,…hana mambo hayo, zaidi ya utaalmu wake wa ukunga wa jadi….’nikasema.

‘Huo ukunga ndio anao, lakini pia anayo hayo mambo mengine, unafikiri wanawake wangapi wamekufa akiwazalisha, angalia yaliyotokea nyuma, hadi akafukuza hapa kijijini, lakini kwa ubishi wake akarejea,….’akasema huyo rafiki yangu.

‘Mimi ninahisi kuna watu waliokuwa wakimchukia kwa ajili ya wema wake, wakaona wamtafutie fitina na kumuangamiza….hili linaweza likawa moja ya sababu, maana kama ni mwanga, ningemuona siku nilizowahi kuishi naye…..’nikamwambia huyo rafiki yangu.

‘Shauri lako,….wanga wapo, na huwezi kuwajua hivi hivi, mpaka upitie kwa wataalmu, watu hawo wengine wanajifanya wacha mungu kwelikweli, au kujifanya wema kweli kweli, …lakini usiku sio wenzako…wanageuka kuwa paka, …au mashetani….’akaniambia huku akiangalia huku na kule kama anaogopa kitu..

‘Hizo ni imani haba, na mkiwa na imani kama hizo kamwe hamtaendelea , mtaishia kushukiana uchawi, na kujengeana visasi…ndugu watachukiana, majirani mtafarakana, sababu ni imani zisizo na ukweli. Hivi mungu mnamuweka wapi katika imani zenu hizo,….hamuoni kuwa mnakufuru..?’ nikamuuliza.

‘Kwani mungu hajui kuwa kuna uchawi, anajua kabisa kuwa kwenye viumbe wake kuna watakaokuwa wachawi, wezi, …ndio maana akatukanya tujilinde kwa kuomba …’akasema.

‘Kumbe unajua hilo, kuwa tujilinde kwa kuomba, tumuombe nani, ….?’ Nikamuuliza.

‘Tumuombe mungu…’akasema.

‘Je ndivyo mlivyofanya?’ nikamuuliza.

‘Tunaomba ndio, lakini wakati mwingine inabidi kuuondoa huo uchawi kama tumeuona, maana ukiomba na huku uchawi upo unakuzunguka, utaingiwa na uwoga, …ni bora kuuondoa huku ukiomba…’akasema.

‘Kwahiyo mungu hatoshi kutusaidia mpaka tumsaidie sisi?’ nikamuuliza.

‘Sio hivyo bwana, wewe sasa unaleta malumbano, …na hayo ndio hayatakiwi,…kwani mtalumbana mwishowe mtagombana…wewe furahia kuwa kigagula yule, keshaondolewa na sasa tuna aman, na kama yupo mwingine tutafanya hivyo hivyo…’akasema huku akiinua mkono na kuonyesha kidole kuashiria manenoo yake.

‘Mimi nahisi kuna tatizo hapa kijijini, ….umasikini,ukosefu wa elimu, magonjwa, vimekua ni tatizo hapa kijijini, na watu bila kujua kuwa hayo ndiyo matatizo yetu, huo ndio uchawi unaotuangamiza, watu wanakimbilia kunyosheana vidole…’nikasema huku nikimwangalia huyo rafiki yangu.

‘Wewe unafaa ukagombee ubunge, …..maana unayoongea hayafai hapa kwetu, sisi hayo tumeyarithi toka kwa mababu, imani za asili, na kwa vile wachawi wamegundua kuwa tumeyadharau hayo, wanaringa na kufanya uchawi wao kwa kujiamini….’akasema huyo rafiki yangu.

‘Elimu ndio msingi mkubwa wa maisha, ni kama taa inayomulika kwenye giza, mwanga ukitokea na giza hupotea, kama hakuna elimu, giza litatanda kila mahali,…hatutaonana, tutaona vivuli na kuviita majinamizi…hili ndio tatizo kubwa..’nikasema na yule mama akawa ananiangalia kwa mshangao.

‘Mimi sikuelewi unaonga nini..’akasema.

‘Hebu niambia, kijiji chetu kina shule ngapi, na kati ya hizo wangapi wameenda sekondari,….shule ni chache, na hata zilizopo, hazina vifaa, walimu wachache, na hawo walimu wenyewe, wanatumia muda mwingi kuhangaika na kutafuta jinsi gani ya kujikimu, maana mshahara wanaopata hauwatoshi na wanasema wanaupata ukiwa umechelewa, ….unafikiria elimu hiyo itapatikana kweli..?’ nikamuuliza.

‘Kawaulize hawo wanahusika, mimi nimemaliza darasa la saba, niakolewa, na watoto wangu, najua wakimaliza wanawake wataolewa, wanaume, ….watajiunga na kilimo na ufugaji, …ilimradi wanajua kusoma na kuandika, inatosha…’akasema huku akishika shavu.

‘Elimu ya msingi inatosha, kujua kusoma na kuandiak kunatosha….hayo ndio mawazo yetu, …halafu unatarajia nini, kama sio wote kuwa na mtizamo mmoja, …tutawapata wapi madakitari, kama sio kutayarisha waganga wa kienyeji, ambao wengine ni matapeli wakuhadaa watu, inabidi kujifanya waganga ili wapate kuiba mali zenu….angalia huyo mnayemuita mtalaamu, kwanini kila akimaliza aandai kuku….mara mbuzi,….je hizo ndio dawa?’ nikamuuliza.

‘Hpo umefika mbali, …..funga mdomo wako, maana yule jamaa anasikia kama kitufe cha kurekodia sauti, ukifika kwake atakuambia yote, kuwa ulikuwa ukimteta, na umesema hivi na hivi….akikusarikia yule, utakikimbia kijiji….’akasema.

‘Kama alivyomkasirikia huyo mwanamama wa watu, unafiki mimi sijui hayo….yule mama alikuwa mstari wa mbele wa kumpinga, mambo yake, …watu wakiumwa wanakimbilia kwake, na wakifika wanadanganywa, kuwa wasile baadhi ya vyakula ambavyo ndio msingi wa afya ya mzazi na mtoto, wanatumwa kuleta kuku, na hata kutoa mazao yao, na kumneemesha huyo mtaalamu….yule mwanamama alikuwa akimpinga wazi wazi….’nikasema.

‘Ondoka hapa kwangu maana unataka kuniletea balaa, …..sitaki maongezi yako, kama ndio yaliyokuleta hapa bora uondoke….’akasema na mimi sikumsikiliza nikasema;

‘Hebu angalia sasa, unafikiri mume wa huyo marehemu atakuwa na hisia gani moyoni, kama sio kulipiza kisasi kwa hawo waliomfanyia hivyo…visasi juu ya visasi, watu hawakai wakaangalia maendeleo yao, wanakaa kuangaliana kwa husuda, ….’nikamwambia.

‘Yule mwanaume alishawekwa mikononi mwa huyo mwanamke, alikuwa hafurukuti, kawa zezeta kwa huyo mwanamke, alishalewesha madawa ya huyo mchawi, ashukuru kuwa tumemuondolea nuksi, sasa akitaka anaweza kuoa mke mwingine, na …akapata mtoto wa uzeeni, maana wanaume hawazeeki….’akasema, sikutaka kuongea na watu wa namna hii tena, na kabla hatujaagana akaniuliza

‘Na mume wako anaonekena anaumwa, anaumwa nini, maana tangu atoke jela, hali yake sio nzuri, anakohoa, anazidi kukonda, huoni kuwa ni uchawi wa huyo mzee…mpeleke kwa mtaalamu wakamwangalia.’akasema.

‘Tutakwenda naye hospitalini, …inawezekana kapata mardhi akiwa huko jela, siunafahamu jela zetu, …huko ukipelekwa ujua ukitoka mzima, una ugonjwa….vinginevyo, utatolewa maiti. Jela zetu hazijaboreshwa kuwa chuo cha mafunzo, ..ilitakiwa mtu akitoka hapo kabadilika, kaiva kitaalamu, na kimaadili, ….Sasa mfungwa akitoka hapo, anakuwa wakala wa mgonjwa sugu, kama sio kifua kikukuu ni ukimwi, au ukurutu, anatoka kuja kutuambukiza…huo ndio utalaamu anaokuja nao, tutafika kweli …’nikasema na yeye akacheka na kusema.

‘Wewe lala tu, ..nakushauri umpeleke mumeo kwa huyo mtaalamu kabla hujachelewa….’akasema na mimi nikaaga na kuondoka, sikutaka kuongea naye tena.

Nilijaribu kufuatilia kwenye vyombo vya usalama, kama wamechukua hatua gani, lakini ilikuwa kama naongea na viziwi, maana kila mmoja alijifanya yupo na kazi nyingi, na hapo nikahisi kuwa hilo tukio lilikuwa kama limebarikiwa.

‘Mimi sitaishia hapa, kama mumeshindwa kulifanyia kazi hili tukio na waliofanya hivi wakafikishwa kwenye vyombo vya usalama, mimi nitakwenda ngazi za juu…’nikawaambia.

‘Labda na wewe ni mshirika wake ndio maana mnamtetea sana huyo mchawi….’akasema jamaa mmoja

‘Mshirika wa nini….hivi nyie watu mtaendelea na imani hizo mapaka lini, maana wenzenu sasa hivi wanafikiria kuruka juu kwenda anga za mbali, kuangalia kama kuna uwezekano wa kuishi huko ,nyie bado mpo kwenye mawazo ya kizamani….’nikawaambia.

‘Nani kakudanganya kuwa uzunguni hakuna wanga, sema wao hawajifichi kama huku kwetu, na uchawi wao ni wa kimaendeleo….’akasema askari mmoja.

‘Kwahiyo kwa vile huku kwetu uchawi ni wa kificho ndio maana mnawahukumu wale wote mnaowafikiria kuwa ni wachawi, hata bila ushahidi? Eeh,.hebu niambieni nyie watu mliochaguliwa kuilinda sheria na kuhakikisha sheria zinafuatwa hii kweli ndio sheria inavyosema kuwa watu wajichukulie sheria mikononi mwao..?’ nikawauliza.

‘Wewe dada, nasikia mtoto wako ni mgonjwa, na wenzako wamesema chanzo ni huyo mama, nilitarajia kuwa ungeliwashukuru hawo waliofanya hivyo….na mume wako anaumwa pia, …sisi hatuhusiki na hilo, kama una ushahidi na hawo watu, waliofanya hivyo walete….’akasema askari mmojawapo.

‘Mimi mtoto wangu anaumwa,…na sasa hivi natarajia kumpeleka kwenye vipimo vikubwa, hajalogwa, ….ni tatizo la kawaida tu,..huo uzushi wa watu, nyie hamtakiwi kuusikiliza….nyie ni watetezi wa haki, sio wasaidizi wa kuvunja haki. Na kwanini amloge mtoto wangu wakati yeye mwenyewe ndiye aliyemlea hadi akafikia hapo..’nikawaambia kwa hasira.

‘Sisi hatujui hayo, tunayasikia kutoka kwenu…..japokuwa tunaishi pamoja…narudia tena kama unawafahamu waliofanya hivyo, walete hapa,…..kama huwafahamu, sisi hatuwezi kufanya lolote,…’akasema.

‘Sawa,….naona hamtaweza kunisaidia kabisa kwa hili, iliyobakia ni kwenda ngazi za juu….’nikasema an kuondoka.

Baadaye niliondoka hapo na kwenda kumuona babu yako, ambaye alikuwa amegoma kabisa kula , na hataki kuongea na watu, ni mimi peke yake ndiye niliyeweza kuongea naye, nikajaribu kumshawishi kuwa hiyo kesi inabidi twende ngazi za juu.

‘Usisumbuke kabisa mwaanngu, kwasababu hatutaweza kumrejesha mke wangu , hata kama kesi itasimama, na wakaonekana wana hatia hao waliofanya hivyo, je wataweza kumrejesha mke wangu dunia…..kifupi ni kuwa hawataweza, …kwahiyo sioni kwanini nipoteze muda wangu kwa kesi,…na unaowapelekea hizo kesi ndio hao hao….imani zao, tabia zao, na mtizamo wao upo huko huko, kuwa mke wangu alikuwa ni mchawi. Mimi mwenyewe nitajua jinsi gani ya kufanya….’akasema na hakutaka kuongea tena.

‘Sasa baba, kesho mimi nampekeka mtoto hospitali za mjini, tutaongozana na mume wangu, ili na yeye akatibiwe, wakafanyiwe vipimo vya maana, ….’nikamwambia.

‘Mchawi wake si keshakufa, sasa una wasiwasi gani..’akasema akiniangalia kwa macho ya huzuni.

‘Baba mimi siamini hayo ya uchawi hata kama upo…,lakini mimi nina imani kabisa kuwa mama hajafanya hivyo wanavyosema wao, ….hayo waliyoyafanya ni mauaji, na huenda yana sababu nyingine, lakini wakaona njia rahisi ni kupitia ni kwenye dhana hiyo ya imani za kishirikina. Kwa ajili hiyo, hawo waliofanya hivyo wanastahili kushitakiwa na kunyongwa…..’ nikamwambia babu yako, lakini alionekana akiwaza mbali sana.

‘Baba mimi najua mtoto wangu anaumwa maradhi ya kawaida na nina imani kuwa atatibiwa na atapona…kwahiyo kesho nitaondoka asubuhi sana, wewe endelea kukaa hapa, nimeshafanya mpango wa kuanza ujenzi wa nyumba yako, mungu akipenda itakamilika na itakuwa nyumba ya kisasa….’nikasema na kweli kesho yake nikadamka kuondoka.

‘Baba , baba mimi naondoka…..’nikasema lakini kulikuwa kimiya, nikaingia ndani alipokuwa kalala babu yako,…nilimkuta yupo sakafuni, …hajitambui.

‘Baba vipi tena….?’ Nikauliza lakini alikuwa kalala kimiya, …..mwili ukaanza kuniishia nguvu, wasiwasi ukaniingia,…nikajua mzee huyo naye kamfuata mkewe.
NB: Angalau kidogo, kuloko kutokuandika kabisa

WAZO LA LEO: Kiini cha matatizo mengi ni kutokana na adui ujinga, na umasikini uliokithiri. Watu wanakata tamaa, na kuwa na mafundo kwenye mioyo yao, hasira, na chuki zinakuwa zimewatawala, na kukitokea upenyo, lolote linaweza kutokea. Ni vyema, adui hawa wakaangaliwa kwa jicho pana, jinsi gani ya kupambana na jinsi gani ya kuwasaidia wananchi kwa haki, kwani wengi wao ndio wanaoathiriwa na adui hawa…tusikimbilie kuliangalia tatizo kwa juu juu, huku kiini cha tatizo kikiendelea kuwepo. Kamwe hatufanikiwa.


Ni mimi: emu-three

2 comments :

EDNA said...

Natumai umesalimika jirani yangu,ni muda mrefu sijapita mahali hapa,nimeona leo nipite niombe japo hata maji ya kunywa lol...salimia familia.

emuthree said...

Karibu jirani yangu EDNA, maana kweli ni muda, hata nilifikiria umesafiri, lkn sio ajabu maana majirani wote siku hizi wamekuwa adimu, kila mtu ndani ya geti lake, akikuona anakupungia mkono kwa mbali, Tupo pamoja jirani mwema.