Nilifika eneo la ilipokuepo nyumba ya wazee hawa, babu na
bibi yako wa kukulea, nilishangaa kuona kuwa kilichobakia ni matakataka na majivu
kila kitu kiliteketea, na watu walikuwa wakipita huku wakibeza, na kusema sasa
wamemkomoa mchawi wa kijiji;
‘Hili litakuwa fundisho kwa wale wote wanatuwangia na
kutuulia watoto wetu….’akasema mama mmoja na wenzake wakacheka kwa dharau,
kicheko kile cha akina mama.
Baadaye nilimpitia rafiki yangu, nkijaribu kukusanya habari,
huenda zikaweza kunisaidia kufungua kesi ya kuuliwa huyo mwanamama, na
kuharibiwa mali ya wazee hawa, na nilimkuta mwenzangu akihangaika na usafi wa
nyumba yake, na aliponiona,akaacha kila kitu na kunikaribisha. Tukaanza
mazungumzo, na bila kuficha nikamuuliza swali;
‘Hivi mna ushahidi gani kuwa huyo mwanamama wa watu
aliyeuwawa kinyama hivyo alikuwa ni mchawi?’ nikamuuliza rafiki yangu, na yeye
akaniangalia huku akionyesha mshangao, akasema.
‘Wewe unataka ushahidi gani mwingine, ….wakati mimi mwenyewe
nilikupeka kwa yule mtaalmu, mtaalamu anayeaminika na wanakijiji wote, hata nje
ya mkoa huu. Yule sio mchezo bwana, akikuambia kitu, amini…..anaiweza ile kazi
sio mchezo. Unakumbuka alivyokuamba kuwa mtoto wako anaumwa, na anayemfanya
hivyo ni mama mtu mzima aliyewahi kumlea, sasa ni nani mwingine aliyewahi
kumlea mwanao kama sio huyo mwanamama wako, ….unataka nini tena, ..’akaniambia
huyo rafiki yangu kwa kujiamini.
Nilishika kichwa , na kuangalia pembeni, huki
nikimuwazia huyo mwanamama wa watu ambaye nilikuwa na uhakika kabisa kuwa hayo
wanayomshutumu nayo, hakuwa nayo kamwe.
‘Mimi siamini kabisa hayo mambo…namshukuru mungu kwa hilo. Na
pili yule mama namfahamu sana, nimewahi kuishi naye, tena kwa karibu, kipindi
waliponipokea,…hana mambo hayo, zaidi ya utaalmu wake wa ukunga wa jadi….’nikasema.
‘Huo ukunga ndio anao, lakini pia anayo hayo mambo mengine,
unafikiri wanawake wangapi wamekufa akiwazalisha, angalia yaliyotokea nyuma,
hadi akafukuza hapa kijijini, lakini kwa ubishi wake akarejea,….’akasema huyo
rafiki yangu.
‘Mimi ninahisi kuna watu waliokuwa wakimchukia kwa ajili ya
wema wake, wakaona wamtafutie fitina na kumuangamiza….hili linaweza likawa moja
ya sababu, maana kama ni mwanga, ningemuona siku nilizowahi kuishi naye…..’nikamwambia
huyo rafiki yangu.
‘Shauri lako,….wanga wapo, na huwezi kuwajua hivi hivi,
mpaka upitie kwa wataalmu, watu hawo wengine wanajifanya wacha mungu
kwelikweli, au kujifanya wema kweli kweli, …lakini usiku sio wenzako…wanageuka
kuwa paka, …au mashetani….’akaniambia huku akiangalia huku na kule kama
anaogopa kitu..
‘Hizo ni imani haba, na mkiwa na imani kama hizo kamwe
hamtaendelea , mtaishia kushukiana uchawi, na kujengeana visasi…ndugu
watachukiana, majirani mtafarakana, sababu ni imani zisizo na ukweli. Hivi
mungu mnamuweka wapi katika imani zenu hizo,….hamuoni kuwa mnakufuru..?’
nikamuuliza.
‘Kwani mungu hajui kuwa kuna uchawi, anajua kabisa kuwa
kwenye viumbe wake kuna watakaokuwa wachawi, wezi, …ndio maana akatukanya
tujilinde kwa kuomba …’akasema.
‘Kumbe unajua hilo, kuwa tujilinde kwa kuomba, tumuombe
nani, ….?’ Nikamuuliza.
‘Tumuombe mungu…’akasema.
‘Je ndivyo mlivyofanya?’ nikamuuliza.
‘Tunaomba ndio, lakini wakati mwingine inabidi kuuondoa huo
uchawi kama tumeuona, maana ukiomba na huku uchawi upo unakuzunguka, utaingiwa
na uwoga, …ni bora kuuondoa huku ukiomba…’akasema.
‘Kwahiyo mungu hatoshi kutusaidia mpaka tumsaidie sisi?’
nikamuuliza.
‘Sio hivyo bwana, wewe sasa unaleta malumbano, …na hayo ndio
hayatakiwi,…kwani mtalumbana mwishowe mtagombana…wewe furahia kuwa kigagula
yule, keshaondolewa na sasa tuna aman, na kama yupo mwingine tutafanya hivyo
hivyo…’akasema huku akiinua mkono na kuonyesha kidole kuashiria manenoo yake.
‘Mimi nahisi kuna tatizo hapa kijijini, ….umasikini,ukosefu
wa elimu, magonjwa, vimekua ni tatizo hapa kijijini, na watu bila kujua kuwa
hayo ndiyo matatizo yetu, huo ndio uchawi unaotuangamiza, watu wanakimbilia
kunyosheana vidole…’nikasema huku nikimwangalia huyo rafiki yangu.
‘Wewe unafaa ukagombee ubunge, …..maana unayoongea hayafai
hapa kwetu, sisi hayo tumeyarithi toka kwa mababu, imani za asili, na kwa vile
wachawi wamegundua kuwa tumeyadharau hayo, wanaringa na kufanya uchawi wao kwa
kujiamini….’akasema huyo rafiki yangu.
‘Elimu ndio msingi mkubwa wa maisha, ni kama taa inayomulika
kwenye giza, mwanga ukitokea na giza hupotea, kama hakuna elimu, giza litatanda
kila mahali,…hatutaonana, tutaona vivuli na kuviita majinamizi…hili ndio tatizo
kubwa..’nikasema na yule mama akawa ananiangalia kwa mshangao.
‘Mimi sikuelewi unaonga nini..’akasema.
‘Hebu niambia, kijiji chetu kina shule ngapi, na kati ya
hizo wangapi wameenda sekondari,….shule ni chache, na hata zilizopo, hazina
vifaa, walimu wachache, na hawo walimu wenyewe, wanatumia muda mwingi
kuhangaika na kutafuta jinsi gani ya kujikimu, maana mshahara wanaopata
hauwatoshi na wanasema wanaupata ukiwa umechelewa, ….unafikiria elimu hiyo
itapatikana kweli..?’ nikamuuliza.
‘Kawaulize hawo wanahusika, mimi nimemaliza darasa la saba,
niakolewa, na watoto wangu, najua wakimaliza wanawake wataolewa, wanaume, ….watajiunga
na kilimo na ufugaji, …ilimradi wanajua kusoma na kuandika, inatosha…’akasema
huku akishika shavu.
‘Elimu ya msingi inatosha, kujua kusoma na kuandiak
kunatosha….hayo ndio mawazo yetu, …halafu unatarajia nini, kama sio wote kuwa
na mtizamo mmoja, …tutawapata wapi madakitari, kama sio kutayarisha waganga wa
kienyeji, ambao wengine ni matapeli wakuhadaa watu, inabidi kujifanya waganga
ili wapate kuiba mali zenu….angalia huyo mnayemuita mtalaamu, kwanini kila
akimaliza aandai kuku….mara mbuzi,….je hizo ndio dawa?’ nikamuuliza.
‘Hpo umefika mbali, …..funga mdomo wako, maana yule jamaa
anasikia kama kitufe cha kurekodia sauti, ukifika kwake atakuambia yote, kuwa
ulikuwa ukimteta, na umesema hivi na hivi….akikusarikia yule, utakikimbia
kijiji….’akasema.
‘Kama alivyomkasirikia huyo mwanamama wa watu, unafiki mimi
sijui hayo….yule mama alikuwa mstari wa mbele wa kumpinga, mambo yake, …watu
wakiumwa wanakimbilia kwake, na wakifika wanadanganywa, kuwa wasile baadhi ya
vyakula ambavyo ndio msingi wa afya ya mzazi na mtoto, wanatumwa kuleta kuku,
na hata kutoa mazao yao, na kumneemesha huyo mtaalamu….yule mwanamama alikuwa
akimpinga wazi wazi….’nikasema.
‘Ondoka hapa kwangu maana unataka kuniletea balaa, …..sitaki
maongezi yako, kama ndio yaliyokuleta hapa bora uondoke….’akasema na mimi
sikumsikiliza nikasema;
‘Hebu angalia sasa, unafikiri mume wa huyo marehemu atakuwa
na hisia gani moyoni, kama sio kulipiza kisasi kwa hawo waliomfanyia hivyo…visasi
juu ya visasi, watu hawakai wakaangalia maendeleo yao, wanakaa kuangaliana kwa
husuda, ….’nikamwambia.
‘Yule mwanaume alishawekwa mikononi mwa huyo mwanamke,
alikuwa hafurukuti, kawa zezeta kwa huyo mwanamke, alishalewesha madawa ya huyo
mchawi, ashukuru kuwa tumemuondolea nuksi, sasa akitaka anaweza kuoa mke
mwingine, na …akapata mtoto wa uzeeni, maana wanaume hawazeeki….’akasema,
sikutaka kuongea na watu wa namna hii tena, na kabla hatujaagana akaniuliza
‘Na mume wako anaonekena anaumwa, anaumwa nini, maana tangu
atoke jela, hali yake sio nzuri, anakohoa, anazidi kukonda, huoni kuwa ni
uchawi wa huyo mzee…mpeleke kwa mtaalamu wakamwangalia.’akasema.
‘Tutakwenda naye hospitalini, …inawezekana kapata mardhi
akiwa huko jela, siunafahamu jela zetu, …huko ukipelekwa ujua ukitoka mzima,
una ugonjwa….vinginevyo, utatolewa maiti. Jela zetu hazijaboreshwa kuwa chuo
cha mafunzo, ..ilitakiwa mtu akitoka hapo kabadilika, kaiva kitaalamu, na
kimaadili, ….Sasa mfungwa akitoka hapo, anakuwa wakala wa mgonjwa sugu, kama
sio kifua kikukuu ni ukimwi, au ukurutu, anatoka kuja kutuambukiza…huo ndio
utalaamu anaokuja nao, tutafika kweli …’nikasema na yeye akacheka na kusema.
‘Wewe lala tu, ..nakushauri umpeleke mumeo kwa huyo mtaalamu
kabla hujachelewa….’akasema na mimi nikaaga na kuondoka, sikutaka kuongea naye
tena.
Nilijaribu kufuatilia kwenye vyombo vya usalama, kama
wamechukua hatua gani, lakini ilikuwa kama naongea na viziwi, maana kila mmoja
alijifanya yupo na kazi nyingi, na hapo nikahisi kuwa hilo tukio lilikuwa kama
limebarikiwa.
‘Mimi sitaishia hapa, kama mumeshindwa kulifanyia kazi hili
tukio na waliofanya hivi wakafikishwa kwenye vyombo vya usalama, mimi
nitakwenda ngazi za juu…’nikawaambia.
‘Labda na wewe ni mshirika wake ndio maana mnamtetea sana
huyo mchawi….’akasema jamaa mmoja
‘Mshirika wa nini….hivi nyie watu mtaendelea na imani hizo
mapaka lini, maana wenzenu sasa hivi wanafikiria kuruka juu kwenda anga za
mbali, kuangalia kama kuna uwezekano wa kuishi huko ,nyie bado mpo kwenye
mawazo ya kizamani….’nikawaambia.
‘Nani kakudanganya kuwa uzunguni hakuna wanga, sema wao
hawajifichi kama huku kwetu, na uchawi wao ni wa kimaendeleo….’akasema askari
mmoja.
‘Kwahiyo kwa vile huku kwetu uchawi ni wa kificho ndio maana
mnawahukumu wale wote mnaowafikiria kuwa ni wachawi, hata bila ushahidi?
Eeh,.hebu niambieni nyie watu mliochaguliwa kuilinda sheria na kuhakikisha
sheria zinafuatwa hii kweli ndio sheria inavyosema kuwa watu wajichukulie
sheria mikononi mwao..?’ nikawauliza.
‘Wewe dada, nasikia mtoto wako ni mgonjwa, na wenzako
wamesema chanzo ni huyo mama, nilitarajia kuwa ungeliwashukuru hawo waliofanya
hivyo….na mume wako anaumwa pia, …sisi hatuhusiki na hilo, kama una ushahidi na
hawo watu, waliofanya hivyo walete….’akasema askari mmojawapo.
‘Mimi mtoto wangu anaumwa,…na sasa hivi natarajia kumpeleka
kwenye vipimo vikubwa, hajalogwa, ….ni tatizo la kawaida tu,..huo uzushi wa
watu, nyie hamtakiwi kuusikiliza….nyie ni watetezi wa haki, sio wasaidizi wa
kuvunja haki. Na kwanini amloge mtoto wangu wakati yeye mwenyewe ndiye
aliyemlea hadi akafikia hapo..’nikawaambia kwa hasira.
‘Sisi hatujui hayo, tunayasikia kutoka kwenu…..japokuwa
tunaishi pamoja…narudia tena kama unawafahamu waliofanya hivyo, walete hapa,…..kama
huwafahamu, sisi hatuwezi kufanya lolote,…’akasema.
‘Sawa,….naona hamtaweza kunisaidia kabisa kwa hili,
iliyobakia ni kwenda ngazi za juu….’nikasema an kuondoka.
Baadaye niliondoka hapo na kwenda kumuona babu yako, ambaye
alikuwa amegoma kabisa kula , na hataki kuongea na watu, ni mimi peke yake
ndiye niliyeweza kuongea naye, nikajaribu kumshawishi kuwa hiyo kesi inabidi
twende ngazi za juu.
‘Usisumbuke kabisa mwaanngu, kwasababu hatutaweza kumrejesha
mke wangu , hata kama kesi itasimama, na wakaonekana wana hatia hao waliofanya
hivyo, je wataweza kumrejesha mke wangu dunia…..kifupi ni kuwa hawataweza,
…kwahiyo sioni kwanini nipoteze muda wangu kwa kesi,…na unaowapelekea hizo kesi
ndio hao hao….imani zao, tabia zao, na mtizamo wao upo huko huko, kuwa mke
wangu alikuwa ni mchawi. Mimi mwenyewe nitajua jinsi gani ya kufanya….’akasema
na hakutaka kuongea tena.
‘Sasa baba, kesho mimi nampekeka mtoto hospitali za mjini,
tutaongozana na mume wangu, ili na yeye akatibiwe, wakafanyiwe vipimo vya
maana, ….’nikamwambia.
‘Mchawi wake si keshakufa, sasa una wasiwasi gani..’akasema
akiniangalia kwa macho ya huzuni.
‘Baba mimi siamini hayo ya uchawi hata kama upo…,lakini mimi
nina imani kabisa kuwa mama hajafanya hivyo wanavyosema wao, ….hayo waliyoyafanya
ni mauaji, na huenda yana sababu nyingine, lakini wakaona njia rahisi ni
kupitia ni kwenye dhana hiyo ya imani za kishirikina. Kwa ajili hiyo, hawo
waliofanya hivyo wanastahili kushitakiwa na kunyongwa…..’ nikamwambia babu
yako, lakini alionekana akiwaza mbali sana.
‘Baba mimi najua mtoto wangu anaumwa maradhi ya kawaida na
nina imani kuwa atatibiwa na atapona…kwahiyo kesho nitaondoka asubuhi sana,
wewe endelea kukaa hapa, nimeshafanya mpango wa kuanza ujenzi wa nyumba yako,
mungu akipenda itakamilika na itakuwa nyumba ya kisasa….’nikasema na kweli
kesho yake nikadamka kuondoka.
‘Baba , baba mimi naondoka…..’nikasema lakini kulikuwa
kimiya, nikaingia ndani alipokuwa kalala babu yako,…nilimkuta yupo sakafuni, …hajitambui.
‘Baba vipi tena….?’ Nikauliza lakini alikuwa kalala kimiya, …..mwili
ukaanza kuniishia nguvu, wasiwasi ukaniingia,…nikajua mzee huyo naye kamfuata
mkewe.
NB: Angalau kidogo, kuloko kutokuandika kabisa
WAZO LA LEO:
Kiini cha matatizo mengi ni kutokana na adui ujinga, na umasikini
uliokithiri. Watu wanakata tamaa, na kuwa na mafundo kwenye mioyo yao, hasira,
na chuki zinakuwa zimewatawala, na kukitokea upenyo, lolote linaweza kutokea.
Ni vyema, adui hawa wakaangaliwa kwa jicho pana, jinsi gani ya kupambana na
jinsi gani ya kuwasaidia wananchi kwa haki, kwani wengi wao ndio wanaoathiriwa
na adui hawa…tusikimbilie kuliangalia tatizo kwa juu juu, huku kiini cha tatizo
kikiendelea kuwepo. Kamwe hatufanikiwa.
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
Natumai umesalimika jirani yangu,ni muda mrefu sijapita mahali hapa,nimeona leo nipite niombe japo hata maji ya kunywa lol...salimia familia.
Karibu jirani yangu EDNA, maana kweli ni muda, hata nilifikiria umesafiri, lkn sio ajabu maana majirani wote siku hizi wamekuwa adimu, kila mtu ndani ya geti lake, akikuona anakupungia mkono kwa mbali, Tupo pamoja jirani mwema.
Post a Comment