Ukumbuke kuwa hapa
nilikuwa na mama akinithibitishia yale aliyokwisha kunisimulia babu, na sasa
tulikuwa tukiangalia maisha ya mama, ambayo mama alikuwa akinielezea vizuri kwa
vile yeye ndiye aliyekuwa mhusika mkuu wa maisha hayo….haya tuendelee na kisa chetu, tupate mafunzo yaliyopo ndani yake.
^^^************^^^
Baada ya kufuatilia polisi na wao kunieleza kuwa mume wangu
keshapelekwa huko nyumbani kujibu mashitaki, sikuwa na la kufanya,….sikuwa na mtu
wa kuwasiliana naye ili anipe uhakika wa hilo, nilichowaza akilini mwangu ni
kutafuta nauli na pesa za kwenda huko kijijini na kufuatilia kesi yake. Kwahiyo
nikajibidisha na biashara za karanga, na ubuyu…hata hivyo haikuwa kazi rahisi
kihivyo, mitihani bado iliniandama.
Nilikuwa nikiweka kila senti niliyopata, na kudunduliza,
hadi nikawa na kiasi kizuri cha nauli, kwahiyo nikawa sasa natafuta pesa ya
kuniwezesha kufanya lolote nikifika huko nyumbani. Siku nilipoona sasa
nimefikisha kiasi cha kuniwezesha, nikawa nimekaa kwenye chumba change cha
kimasikini, na kuzihesabu hizo pesa.
‘Oh, hizi zinatosha, kwa nauli na akiba kidogo,…kesho ngoja
nikakate tiketi nrudi nyumbani…’nikasema huku nikijilaza kwenye kigodoro change,
na kwa jaili ya kuchoka, usingizi ukanishika. Mara mlango ukagongwa, na kabla
sijainuka, mshindo mkubwa ukasikika….Mlango wote ukavunjika, na jiwe kubwa
likatua mbele yangu, ….wanaliita Fatuma.
‘Pesa zipo wapi….’mtu mmoja aliyejifunika uso akasema.
‘Pesa gani, nyie wezi…wazi jamani…’nikasema na kabla sijatoa
kauli nyingine, nilisikia kitu kigumu kikigonga kichwani nikapoteza fahamu.
Wahuni hawo wakanipora pesa zote.
Siku hiyo nililiia kama mtoto mdogo, kwani pesa za mtaji
wote, nauli yangu ya kunifikisha kijijini walizichukua, na kunibakizia bidhaa
chache za karanga na ubuyu,…
‘Mungu nimekosa nini jamani,…yaani hawa watu wamechukua pesa
zangu zote, je nitawezaje kwenda nyumbani kumuona mtoto wangu, na kusimamia
kesi ya mume wangu…oh mtaji wote umeguduka, sina kitu tena…’nikajikuta nikilia,
lakini haikusaidia kitu.
‘Pole sana jirani yangu, ..haina haja ya kulia sana,
kilichobakia ni kumshukuru mungu na kuanza moja, hawo wezi hawatafanikiwa, ni
wahuni tu hawo, wala sio majambazi, ….kwani nijuavyo hawo watu wakipata pesa
kama hizo za dhuluma hukimbilia kulewa tu, hawana maendeleo yoyote, na siku ya
kiyama makazi yao ni motoni…’akawa akiniliwaza jirani yangu.
Kweli kesho yake nikadamka na kuanza biashara kidogo ya
karanga na ubuyu uliobakia,….maisha ya upweke, maisha ya taabu dhiki, na
umasikini uliokithiri, nikiwa peke yangu, nilijikuta nikilia sana, kwakweli ilikuwa
kazi nzito, maana kama nilivyowaambia, mitaani mauzi ni mengi , kejeli zilikuwa
ndio wimbo wa kila siku , lakini sikujali, nikaendelea na biashara zangu.
Siku zilikwenda kama mchezo, nikajikuta mwezi unaisha hivi
hivi, na pesa ilikuwa bado haitoshi, kwani mwenye nyumba alitaka pesa ya pango,…hata
hivyo sikukata tamaa, nikawa kila siku najipa matumaini kuwa ipo siku nitafanikiwa.
Usiku nilikuwa nikiamuka kufunga karanga na nikimaliza namlilia mungu wangu, na
kweli muomba mungu hachoki, siku moja nikafanikiwa.
Ilikuwa jioni baada ya kazi kubwa,ya kuhangaika huku na kule
,,,,nikiwa nimechoka sana, nikaona nijipumzishe kwenye duka moja, nikanunua
soda, na nikawa nimekaa huku nikiwazia mambo yangu ya kimaisha, mara simu yangu
yakimasikini ikaita, ….mwanzoni sikutaka kuipokea, lakini baadaye nikaishika na
kuangalia;
Lilionekana jina la moja ya kampuni za simu za mkononi,
moyoni nikajua ni matangazo yao ya biashara, nikataka kuikata, lakini baadaye nikaingiwa
na shauku ya kujua ni kitu gani kitasikika, huenda ni muongozo mzuri wa
kujikwamua na umasikini, nikaiweka ile namba hewani na mara nikasikia sauti ya
mwanadada ikiuliza;
‘Hallohoooo, wewe ndiye mwenye simu hii?’ akauliza huyo
mwanadada, na kwa hasira nilitaka kumjibu maneno mabaya, kwasababu simu ni ya
kwangu bado ananiuliza wewe ndio mwenye simu, lakini nikaona niwe na hekima
nikasema kwa sauti ya kukasirika.
‘Ndio mimi, ….kwani vipi?’ nikauliza.
‘Hebu nitajie namba yako kwa usahihi…’akasema na hapo
nikatulia kidogo, nikaona iswe shida nikamtajia kwa usahihi, na baadaye akasema;
‘Je ulishawahi kujiunga na promosheni yetu ya ushinde?’
akauliza na hapo nikaanza kujiamini kidogo, roho ikatulia, …nislishangaa hasira
nilizokuwa nazo zikawa zimeyeyuka, kwani huenda nikapata mkopo,….nikamwambia
ndio, halafu akasema;
‘Nikikuambia kuwa wewe umekuwa mshinda wetu wa kwenye
promosheni hii ya ushinde utasemaje?’ akauliza, nikaguna, nikijisemea moyoni,
toka lini masikini kama mimi nikaweza kushinda …..sisi tumezaliwa kuwa waombaji
tu, wanyanyaswaji tu….nikasema kwa suti ndogo ya kinyonge, sio ile ya hasira
tena;
‘Nitashukuru tu, japokuwa sitaamini ..hata hivyo, ningesema
nini, mimi mlala hoi….’nikasema nikiwa na machungu ya adha, madhila ninayopata
katka kuhangaika kutafuta angalau nauli ya kufika kwetu. Na hapo, niliona kama
ananipotezea muda wangu, nilikuwa nataka nitoke nikazunguke tena.
‘Sasa hivi wewe sio mlalahoi tena…., sasa hivi wewe ni
tajiri, je katika misha yako ulishawahi kuikamata milioni kumi taslimu mkononi….?’
Akaniuliza na hapo nikakaa kimiya, nikijua kuwa hawo ni watu wanaoleta utani
kwenye mitandao ya simu, baadaye nikasema kwa kigugumizi.
‘Si-si-ja-jawahi …oh milioni kumi, hiyo elifu kumi naitafuta
kwa mbinde….milioni, hiyo ni ndoto ya….’nikasema na kukatisha maneno yangu, na
huyo mwanadada akacheka, ilionekana alikuwa na watu wengine pembeni yake, kwani
nilisikia na wao wakictuliaheka pia
‘Tunayo furaha kukufahamisha kuwa wewe umechaguliwa kuwa
mshindi wetu wa milioni kumi,…hureehe, ….’nikasikia wakisema kwenye simu na
kushangilia. Na mimi nikawa nimetulia nikiwaza je ni kweli au wananitania, na
huyo mwanadada akasema;
‘Unajisikiaje mpendwa kwa ushindi huo….’aksema na sikuweza
kusikia mengine, moyoni nilikuwa na furaha, lakini kwa upande mwingine nilikuwa
siamini. Baadaye wakakata simu wakisema watanipigia baadaye, hapo nikajua ni
wahuni tu walikuwa wakinitania. Nikaingia mitaani….`karanga karanga, pata
karanga kwa afya yako, ubuyu kwa hamu yako….’nikawa naendelea na wimbo wangu wa
biashara.
Ilipofika usiku simu ikapigwa, na nilipoangalia ni jina la
kampuni hiyo ya simu za mikononi, na huyo mwanadada akaanza kwa kujitambulisha
na kunihoji kama walivyofanya mchana, na baadaye wakakata simu na muda mchache
baadaye wakanipigia tena kuniuliza maswali mengine yanayonihusu mwenyewe na
wakanielekeza jinsi gani ya kwenda kuzipata hizo pesa.
Sikuweza kuamini kuwa kweli nimepata hizo pesa hadi pale
nilipofika kwenye hizo ofisi zao na kukabidhiwa hicho kitita, na kesho yake
nikafunga safari ya kurudi kwetu kijijini kuanza maisha ya kitajiri, nikiwa na
ndoto nyingi za kumuona mwanangu……’akasema mama, na hapo nikakumbuka maelezo ya
babu..
******
‘Mjukuu wangu, mama yako alipofika hapa, wengi tulishikwa na
butwaa na kujiuliza ni wapi kazipata hizo pesa, na kwa uwoni wa watu wengi, wakahisi
kuwa huenda ni hizo pesa alizokuwa kaiba huyo mwanaume wake, ndio anazitumia.
‘Tulikuja kufahamu kuwa alikuwa akiishi na huyo mwanaume,
pale tu huyo mwanaume wake alipofikishwa hapa na kufunguliwa mashitaka ya wizi
wa mamilioni ya pesa. Yeye hakutaka kuficha, kila aliyefika kumtembelea huko
jela, aliwaambia kuwa yeye keshao na mke wake ndio yule yule aliyewahi
kumtelekeza.
Mama yako alipofika kwanza alikuja kumchukua mtoto wake….na
baadaye, akanunua shamba na humo akajenga nyumba yake nzuri, na kuishi humo na
mtoto wake. Na akaanza kazi ya kufuatilia kesi ya mumewe, pesa inaongea bwana,
haikuchukua muda mume wake akatoka , wakidai kuwa katoka kwa dhamana…..
Tatizo lilianza kutokea tu alipomchukua mtoto wake, kwani
maradhi yakawa yakimuandama huyo mtoto, alikuwa kila siku anaumwa, …mtoto huyo akakonda
sana, kwani alikuwa hali. Tofauti na tulivyokuwa tukiishi naye,…alianza kuumwa
walipomchukua wao wenyewe. Na hapo watu wakamshauri mama yako ahangaike kwa
tiba mbadala.
Mtu aliyemshauri, akampeleka kwa mganga wa kienyeji, na huko
akaelezewa mengi, ya kuwa anayemfanya mtoto wake awe hivyo, ni mama mmoja
ambaye aliwahii kumlea huyo mtoto wake, na kafanya hivyo kwasababu ya wivu.
Unaona fitina zilivyopandikizwa, lakini nashukuru kuwa mama yako alikuwa
haamini sana mambo hayo
‘Siwezi kuamini hayo….mimi nimekuja hapa kupata dawa ya tiba
ya mwanangu, sio kumtafuta mchawi…..’akasema mama akiendelezea kule aliponihadithia
babu.
‘Tawire, ,…’akasema rafki yake aliyekwenda naye. Huyo rafiki yake, alikuwa mtoto wa mama mdogo
wa bibi yako, familia ambayo ilikuwa haimpendi kabisa bibi yako na pia, aliwahi
kuwa mpenzi wa baba yako kipindi hicho cha nyuma, wakaja kukosana, na huyo
mwanamke akaolewa na jamaa mwingine. Na walizoeana na mama yako kwa vile
walikuwa wakikaa majirani. …’alikumbuka babu yake alivyosema kumhuus huyo
rafiki wa mama, mama yeye hakumuelezea vyema huyo rafiki yake ni nani.
‘Na hata tulipotoka hapo, sikuwa naamini hayo niliyoambiwa,
haiwezekani huyo mama afanye hivyo,….kwasababu gani, eti kwa ajili ya wivu,
haiwezekani…..’nikamwambia huyo rafiki yangu
Uvumi ukasambaa, kuwa bibi yako ndiye aliyekufanya uwe
unaumwa wakati wote, na anataka kukufanya kitoweo kama alivyowafanya watoto
wengine. Na nasikia usiku mmoja wanakijiji walikutana kwani kulikuwa na mtoto
mmoja alifariki, na wao wakaambiwa kuwa mchawi ni bibi yako,kipindi hicho mama
yako alikuwa hayupo alikuwa kasafiri kwenda kununua mahtaji ya duka lao….’alikumbuka
alivyosema babu yake.
`Niliporudi nikakutana na kilio….’akaendelea kuongea mama
kwa huzuni
‘Mama yako aliporudi alinikuta nipo nyumbani kwake, na
kuniulizia mtoto wake yupo wapi, kwani alishaanza kuhisi kuna utofauti, na mimi
nikamwambia tupo kwenye msiba mnzito….’alikumbuka jinsi babu yake alivyomuhadithia.
‘Baba mbona upo,
umekuja kunitembelea ni nini, lakini mbona upo hivyo,…?’ akauliza mama yako
akiwa na mashaka.
‘Kuma msiba…’akasema babu huku akionyesha uso wa huzuni na
ailionekana hataki kuongea ila anajilazimisha.
‘Msiba wa nani,…baba, hapana, mtoto wangu hajafa baba, usija
ukasema hivyo…’akasema mama akionyesha uso wa kusikitika.
‘Sio mtoto wako aliyefariki…..’akasema babu
‘Sasa ni nani amekufa, na mtoto wangu yupo wapi?’ nikauliza.
‘Oh, wamemuua mke wangu..masikini, imani zao za kishirikina
zimewatuma kuja kumuua mke wangu bila hata kosa…’babu yako akasema huku akilia
kama mtoto mdogo.
‘Haiwezekani ….ni nani kafanya hivyo?’ akauliza mama yako.
‘Wanadai walitambua hilo toka kwa mganga, na pia wewe liwahi
kuongea nao kuhusu mtoto wako,na wewe uliwaambia wafanye wanalotaka…., na
kwasababu wana uhakika kuwa mke wangu ni mchawi, na walishamkanya, kuwa
akirudia watafanya hivyo, wao hawakuwa na njia nyingine ila ni kufanya hayo
mauaji, ya kinyama…’akasema babu.
‘Hii sio haki, ni lazima tukashitaki kwanini hawo watu wajichukuliwe
sheria mikononi mwao…wana ushahdi gani na mambo hayo ya kishirikina, mimi
sijawahi kuongea nao kuhusuiana na hayo, ….nakumbuka tulipokwenda kwa huyo
mganga, alisema kuwa mchawi wa mtoto ni mwanamke aliyemlea, mimi sikukubaliana
na hilo…..sasa oh, jamani, ….yaani mama wa watu alivyokuwa mpole kwa kila mtu,
anajituma kuwasaidia watu….leo hii wanamuua ….kweli dunia haina wema…kwakweli
mama yako alilia sana , tukawa tunalia wote hadi tukaishiwa…’akakumbuka
alivyosema babu.
‘Watu hawo wabaya sana, tangu siku nyingi wamekuwa
wakimsakama mke wangu, nilishawaambia kuwa hizo ni imani zao haba, dhana zisizo
na mshiko,….mimi ninayeishi na mke wangu namjua vyema kabisa, hahusiki kabisa
na hayo wanayofikiria, lakini hawakukubali….na nahisi kuna mtu alikuwa nyuma ya
haya yote….’akasema babu akimwambia mama.
‘Kwahiyo wakaja usiku na kumuua?’mama alimuuliza babu.
‘Walifika usiku, na kwanza kabisa, walitafuta njia za
kunitoa mimi, wakasema ninaitwa kwa mjumbe, kumbe sio kweli, nilipotoka usiku
huo kweda kwa mjumbe,….nikijua kuna tatizo kubwa, huku nyuma wakaja watu na
mafuta ya taa, wakaichoma nyumba yangu na bibi yako akiwa ndani…..’akasema babu
kwa huzuni.
‘Bibi yako alikuwa akiumwa, kwahiyo nilimuacha akiwa
amelala,…na moto ulimkuta akiwa usingizini, akaungua , na kuteketea
kabisa….’akasema babu kwa huzuni.
‘Unasema kweli babu…?’ mama yako akauliza huku machozi
yakiwa yamemjaa usoni.
‘Kama unabisha nenda ukaangalia nyumba yangu, yamebakia
majivu tu, kwani walihakikishia kuwa kila kitu kimeungua, na kubakia
majivu…’akasema babu.
‘Mjumbe na walinzi wa jadi walikuwa wapi?’ akauliza mama.
‘Hawakuwepo siku hiyo….kwani nilipofika kwa mjumbe
niliambiwa hayupo…, eti walikuwa wamekwenda kimuwinda simba ambaye inasemakana
alikuwa akila mifugo yetu, lakini hayo yote ilionekana kuwa ni jambo
walilolipanga pamoja….sina cha kufanya,….sitasahahu hilo, na nimeapa kama
sheria haitafuta mkondo wake, mimi mwenyewe nitalipiza kisasi cha mke
wangu….’akasema babu.
‘Namkumbuka sana mke wangu, utafikiri alijua ni nini kitamsibu,
kwani siku hiyo kabla ya kulala, aliniomba tumuombe mungu atulinde na
kutuepushia mabaya ya usiku, na kusema; `ni bora tumuombe mungu, kwani usiku ni
sawa na nusu kifo, na huenda ikawa ndio saa za mwisho za kuishi kwetu, kwahiyo
inakuwa vyema kuomba na kutakiana kila-laheri…’akasema babu kuwa aliambiwa
hivyo na bibi.
‘Na siku hiyo tuliongea sana, na aliniambai kuwa yeye
haogopi kufa, japokuwa watu wamekuwa wakimuandama kila siku, ….lakini yeye ana
imani kuwa mungu peke yake ndiye mlinzi wake…na kama atakufa kwa mikono ya hawo
watu basi imepangwa na mungu, iwe hivyo,…..’akasema.
‘Mke wangu mbona leo unaongea hivyo?’ nikamuuliza kwa
mashaka.
‘Usiwe na wasiwasi mume wangu, kama nikitangulia kufa hakikisha
unamsaidia mjukuu wetu, hakubahatika kuwa na mjukuu, huyo ndiye mpla
aliyetujalia naye, uwe unampa usia mwema wa maisha mema, kwanza awe mchapakazi,
awe anapenda kujitolea kama tulivyokuwa sisi …apende kuwaa mstari wa mbele, kwa
kila jambo la kujitolea natumai kujituma huko ndio itakuwa baraka katika maisha
yake….’
‘Aliniambia bibi yako nikuusie hivyo, kwahiyo kama unampenda
bibi yako fanya hivyo katika maisha yako yote…’akakumbuka jinsi babu yake
alivyomwambia
‘Na pia usije ukafanya lolote kama hawa watu watachukua
sheria mkononi mwao, usije ukalipiza kisasi, kwani mimi mungu wangu anatosha…kamwe
usije ukapandwa na jaziba, kwani hawa watu hawajui wanalolifanya, ni uhaba wa
kuwaza, na propaganda potofu zimechukua nafasi kwenye ubongo zao.’aliniamba.
‘Sasa kwanini ulitaka kulipiza kisasi?’ nilimuuliza babu.
‘Hasira mjukuu wangu, ………ilikuwa ni hasira mjukuu wangu,
unapofikwa na majanga kama haya, hasira zinatangulia ibilisi anakusimamia
mbele, kukushawishi ufanye lolote baya, kwa yoyote utakayemuhisi hivyo, hata
kama huna uhahidi naye …na kwa hali hiyo niliwaona wanakijiji wote ni adui
zangu, nikawa siongei na mtu yoyote, na hata walipofika kunipa pole,
sikuwakaribisha, niliwafukuza…’akasema babu.
‘Nilimkuta babu yako, akiwa peke yake, hakutaka kuongea na
mtu, lakini cha ajabu, mimi alinikaribisha na kuangua kilio mbele yangu, ….aliniona
kuwa sio kweli, kuhusu uvumi uliokuwepo kuwa mimi niliwashauri watu kufanya
hivyo, kitu ambachoo sio kweli….mambo yao hayo yalikuwepo hata kabla ya huyo
mtoto kuwepo, babu yako alijua hilo , …’alisema mama kuthibitisha maneno ya
babu.
‘Mimi ni lazima nichukue hatua….’mama alisema ndivyo
alivyomshauri babu kuwa ili haki itendeke inabidi wafungue kesi, wawashitaki
hawo waliofanya hivyo.
‘Nimeshakuambia nitalipiza kisasi mwenyewe….kwanza
utamshitaki nani …siwajui hawo waliofanya hivyo…ninachoweza kusema ni
wanakijiji wenzangu, sasa nitawashitaji wanakijiji wote…hapana, lazima nitafute
njia yangu ya kulipiza kisasi cha mke wangu…’hiyo ilikuwa kauli ya babu yako
NB: Je babu alilipiza kisasi na kukiuka maneno ya mkewe kuwa
asije akalipiza kisasi kama watu hao waliozamiria kumuua watafanya hivyo?
WAZO LA LEO: Ogopeni
sana dhana, ogopeni sana uvumi, ogopeni sana propaganda potofu, kwani hizo ni
sawa na imani za kishirikina, za kuamini jambo ambalo huna uhakika nalo. Ukifuata
hisia hizo bila ushahidi utakuwa umemfuata shetani, na mazara yake yanaweza
kuwa mabaya zaidi ya hilo lililotokea na kukusukuma kufanya hivyo. Tuwe makini,
tuwe na subira kwenye majanga na misiba, kwani subira huvuta heri.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment