Mtoto mmoja wa tajiri
alijikuta akiokolewa kufa baada ya kunywa sumu, ili apendwe zaidi na wazazi
wake akiwa marehemu: Je ilikuwaje,…
Wazazi tuna mtihani mkubwa wa kulea watoto wetu. Unaweza ukalea ukijua
unapenda, kumbe unamponda mtoto wako mwenyewe. Tuwe makini sana.
Mzazi mwenzetu huyu, baada ya kuhangaika miaka mingi,
baadaye akabahatika kupata mtoto, na furaha iliyoje kwenye familia, wewe
fikiria watu walihangaika miaka saba, ili wapate mtoto, ikafikia sehemu
wakakata tamaa kabisa. Mungu akasikia kilio chao, na kuwajalia mtoto binti,
mrembo kweli kweli.
Hebu fikiria furaha iliyokuwa ndani ya ya hiyo familia,
furaha hiyo ilizidi ile furaha ya mgumba
kupata mtoto, au kibogoyo kuota meno…. Wazazi hawa wakawa wanamlea mtoto wao
kama malikia. Huduma zote muhimu akawa anapatiwa, hadi akakua akiwa na afya
njema furaha na kujiamini kuwa ninapendwa zaidi ya kitu kingine , kwani Kila
atakacho anakipata.
Mungu mkubwa, akawajali mtoto mwingine wa kiume. Sasa yule
wa kwanza keshakua kidogo, …..ana miaka minne,
kwahiyo mapenzi yakawa sasa yanaeleka kidogo kwa mdogo wake. Hali hii ikawa
inamuuma sana dada mtu, yaani kifungua mimba, kwahiyo akawa anajaribu kufanya
kile anachoona mdogo wake anakifanya ili na yeye aendelee kupendwa zaidi.
*******
Siku moja mdogo wake alijikata kidole kwa bahati mbaya,
wazazi wakawa na pikila pilika za kumsaidia huyo mtoto. Ilimradi mtoto
asiendelee kulia, akapakwa dawa, na kununuliwa hiki na kile. Dada mtu akaona
hayo matendo, kwani kwa muda huo hakuna aliyekuwa akimjali, hata pake alipoomba
kitu, aliona kama wazazi wake hawamsikilizi, wao na mdogo wake tu…kuona hivyo, akaingia
ndani kwake, anapolala, akachukua wembe, akajikata mkono.
Tatizo hakujali wapi ajikate, yeye alipochukua wembe kwa
hasira akajikata kwenye mkono sehemu ile, yenye mshipa mkubwa, kwahiyo damu
ikawa inamtoka kwa wingi sana, na wakati anafanya hilo tukio alikuwa chumbani
kwake, na wazazi wake walikuwa barazani
wakihangaika na mdogo wake. Hakuna aliyekuwa na mawazo naye kwa muda huo.
Ilikuja kubainika baadaye kuwa binti hayupo, na
walipohangaika kumtafuta ndio wakamkuta yupo chumbani keshapoteza fahamu
kutokana na kupoteza damu nyingi,
akakimbizwa hospitalini.
Ilikuwa huzuni kweli siku hiyo kwenye familia hiyo, maana
ajali mbili kwa wakati mmoja, na alipoulizwa binti ilikuwaje, yeye akajibu bila
aibu kuwa alijaribu kuangalai jinsi mdogo wake alivyojkata ili na yeye asikie
maumivu kama mdogo wake, kwa kumuonea huruma, na ili pia nay eye apendwe kama
mdogo wake.
‘Hivi huoni ulikuwa unajiua,….?’akaambiwa.
‘Mbona mdogo wangu hakufa, na badala yake mlimpenda kuliko
mimi….’akasema.
‘Wewe mjinga kweli kweli…usifanye hivyo tena…..’kauli hiyo
aliiweka kichwani, kumbe yeye sasa ni mjinga, hajui, ina maana hapendwi tena….
*********
Hali ile ikaisha, na tabia ile ya kuona mdogo wake anapendwa
zaidi ikawa inaendelea kumnyong’onyesha sana. Na siku moja wakati wanapita
mitaa ya jirani wakitoka shule ya chekechea, wakakutana na msiba. Pale kwenye
msiba, waliwaona wazazi wa mtoto aliyefariki wakilia kwa huzuni kubwa, na yeye
akauliza;
‘Kwanini wanalia vile?’ akauliza
‘Kwasababu kipenzi cha hawa wazazi kimefariki, …ndio maana wazazi
wa huyo mtoto wanalia hivyo. Yeye
akilini mwake ikamwiingia sana, kumbe mtu akifa anapendwa kiasi hicho, watu
wanakuja kwa wingi, wanamlilia, na wazazi wanaonyesha upendo wa hali ya juu.
‘Itabidi na mimi nifanye kitu, ili nife, …lakini nikifa
itakuwaje?’ akajiuliza. Hapo akafanya utafiti wa haraka, akaambiwa ukifa
unakwenda kuzikwa, na unawekwa kwenye
jeneza nzuri la kifahari….
‘Oh, kumbe….basi nimelewa. ..’akasema na jioni ile akatafuta
sumu ya kuulia panya, akaikoroga na kuiweka kabatini.
Muda ukafika, na akijua sasa wazazi wake wote wapo nyumbani,
wakiwa na mdogo wake, yeye alikaa pembani, akiwaza alichopanga kichwani,
baadaye akaingia chumbani kwake, na kuinywa ile sumu ….Tumbo likaanza kuuma, maumivi
aliyoyasikia hapo, alijuta kwanini alikunywa hivyo…na wazazi wakasikia hilo
yowe na kukimblia chumbani kwake.
Yule mtoto alikimbizwa hospitalini, baada ya kupewa maziwa, …aliponea
chupuchupu,..na toka siku hiyo hakutaka tena kujidekeza, akajua kuwa kumbe kila
jambo lina wakati wake, faida na hasara zake. Na sasa hivi tunaposimulia hiki
kisa ni muheshimiwa fulani, akiwa na majukumu ya kulea.
Wanajamii, yaliyotokea kwa watoto hawa, huenda hata sisi tunaojiona
ni wazima wazima tunayo kasumba hiyo, kuwa kila wanalofanyiwa wengine , hasa
likifanyika huko majuu tunaliona ni bora zaidi, huenda na sisi tukilifanya
tunaweza kuwa maarufu na kupendwa na watu. Sio kweli kuwa kila lilofanywa na
wengine lina maana kwetu, mengine ni sumu, tunaweza tukajikuta tunajiua
wenyewe, na tuombe mungu, itokee bahati, wawepo watu wa karibuni wa kutuokoa.
Tuweni makini sana na maisha yetu, maisha ni kitu chenye
thamani kubwa sana, tukichezea maisha yetu, hatari yake ni mara mbili ya hivyo
tunavyofikiria, kwani hali zetu ni ngumu, maisha ni magumu, sasa uongezee na
hayo matatizo, kweli tutaweza kuji,mudu.
Tujiulize ni nini tunachotaka katika uhai huu mfupi, kumbuka
ni kama jana tu walikuwepo watu
mashuhuri, sasa hivi tumeshaanza kuwasahahu, wameshaondoka, na ni nini
walichoondoka nacho, hakuna ….sasa tujiulize huo umashuhiri tunaoutaka kwa
wanadamu wenzetu , utaweza kutuweka milele,..jibu lake ni kuwa haiwezekani
kuishi milele.
Tufanyeni mambo kwa utaratibu wake, tukiwa na malengo
chanya, tuache kuiga vitu tusivyokuwa na uhakika navyo, hasa kwenye afya zetu, madawa ya kulevya, kulewa, kuvuta bangi na umalaya, haya yote ni sumu katika maisha yetu. Pia tusikimbilie kuiga mambo ya kisiasa ambayo sio hulika yetu, tuwe makini na ukoloni mambo leo, ni hatari sana kwenye usalama wa nchi zetu, ili mwisho wa siku tuwe na kitu cha
kujivunia, sio cha kujijutia.
Tukumbuke
kuwa majuto ni mjukuu huja baada ya kitendo....
NB: Badi nipo kwenye changamoto za hapa na pale, na hili linanipa wakati mgumu kukiendeleza kisa chetu, lakini nitajitahidi tu, tuombeane heri.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment