Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, March 18, 2013

Uchungu wa Mwana Aujuye ni mzazi -73



Kilikuwa ni kikao cha wanafamilia, akiwezo mzee, na mabinti zake, ambao walishamua kuhakikisha baba yao anaondokana na mambo yote yanayomfanya aathirike kiafya, na kwa mtizamo wao, waliona ni vyema kwanza wakasuluhishe tatizo la ndoa yao, ....

‘Sasa tufanyeje maana mama katoa masharti yake magumu, ambayo baba hayakubali, na halikadhalika baba ni hivyo hivyo….?’ Akauliza binti wakati wakimsubiri baba yao.

‘Dawa ni kuwakutanisha wote kwa pamoja, wakaongea tukiwasikiliza,….lakini kabla ya hilo, inabidi tukae na mama , tumuelezee jinsi gani anatakiwa kuongea na baba, hatakiwi aje na ukali, akimkasirisha baba, inaweza ikaleta mshituko mwingine,…hapa tunaweza tukatatua tatizo la ndoa, na ikawa tiketi ya kummaliza baba….’akasema mwenzake.

‘Nikuulize dada, ni kipi bora,kuwepo na ndoa ..hata kama hakuna mapenzi, watu wanaishi wanaitwa mume na mke, lakini ndani hakuna amani wala mapenzi, ….huoni hapo tutakuwa hatujasaidia,….mimi naona kazi kubwa ni kujenga mapenzi, …hili tukifanikiwa kuliwezesha,kuijenga ndoa hakutakuwa na shida,….kwasababu sioni umuhimu wa ndoa kama hakuna mapenzi ya kweli, ….unaonaje ndugu yangu?’ akauliza

‘Hilo ndilo swala gumu, ….sisi kama watoto raha yetu ni kuona mama anarudi, na wanaishi pamoja na baba, lakini je hiyo raha ya ndoa ipo,….amani ya moyoni, itakuwawepo, ni kweli wao ni wazee, hawana haja sana, ya kufikiria hayo, ….lakujini nijuavyo uzeeni ndipo sehemu ya kuwa na mashikamano, raha, na utulivu, kuliko anani….’akatulia.

‘Ni kweli, ujanani, ….unaweza ukaruka huku na kule, uzeeni ni fainali,…na mwili, mishipa , fahamu zimeshachoka, zinahitaji matulizo,..hazihitzji mihamaniko tena…hapo inabidi tuwe makini…’akasema.

‘Mimi kiukweli nionavyo, hata kama mama atarejea, baba hatakuwa na raha…..atakuwa anaishi kwa ajili yetu tu, upendo kwake kwa mama ulishakwisha, …sasa hapo naona kuna umuhimu wa kuonana na mama tujaribu kumuelezea hilo, kama anaona ataweza kumshawishi baba arejeshe moyo wake kwake, basi,…kama hataweza, mimi naona ili kuepusha shari, bora wakae hivi hivi, ila kuwe na ukaribu fulani…’akasema.

‘Hapana mimi hilo sikubaliani nalo, mimi najua kama watarudiana na wote wakakaa pamoja, watapendana tu, …umri huo walio nao ni wa busara, ….hata kama sio ule upendo wa awali,lakini wataishi kama mke na mume,…..haina haja kuwapa watu faida,….cha muhimu ni kuwakutanisha,….’akasema mdogo mtu….na baadaye baba akaingia, na kukaa kwenye kiti chake,…

*******

‘Haya binti zangu, nipeni muhutasari wa kikao cha leo,..maana nyie ni wasomi, kila kikao, hata kama ni cha kifamilia, ni lazima kuwa na ajenda, …na ni muhimu kwangu ili nijipange, je ni kuhusu maendelea ya shughuli zetu au kuna jipya?’ akauliza.

‘Baba tukikutana hapa, unajua kabisa hatuongelei, maswala ya kazini, hapa ni maswala ya nyumbani, umesahau mwenyewe ulivyotupangia, ….’akasema.

‘Aaah, nilijua mumekuja na mambo ya kulaya ulaya, akili sasa imeshaanza kuchoka, …..haya mambo gani ya kinyumbani?’ akauliza.

‘Ni swala la ndoa yako….’akasema dada mtu, na akamuona baba akibadilika sura,

‘Baba hatuna nia mbaya na wewe, na nia yetu sio kukukwaza kwa ajili ya kumrudisha mama, lakini hili lina umuhimu wake, kwani nyie ni wazazi wetu, na dawa ya hili ni kutafuta suluhisho la kudumu na lenye manufaa kwa pande zote, wewe na mama….’

‘Kwasababu sisi tukiongea na mama anakulaumu wewe, na anakuona wewe ndiye unayechangia kuvunjika kwa ndoa yenu, kwa kutokumsikiliza yeye….anadai hata kampuni , na utajiri uliopo sasa kama asingelikuwa yeye, usingelipatikana, sasa mumetajirika, unamzarau….hayo ndio maneno yake kila siku…’akatulia na mwenzake akaendeleza kwa kusema.

‘Na wewe baba tukiongea na wewe una madai yako pia, tumeyasikia, … na kwa ujumla madai yako tukiyapima, tunayaona yote yana msingi na hata ya mama yana msingi pia, hatuwezi kuyapuuza…sasa kwanini hamukai pamoja mkaangalia wapi mumemkosea, mkasahihishana….’akasema huyo binti.

‘Baba nyie ni wazazi wetu, hadi sasa hakuna usahihi wa kisheria kuwa wewe na mama mumeachana, au sio?’ akauliza binti mdogo, alipomuona baba yake kakaa kimiya hasemi kitu, na baba yake akainua kichwa na kuwaangalia wote wawili kila mmoja kwa sekunde chache, akasema;

‘Upo….unahitajika ushahidi gani tena, mnataka mpaka tupelekane mahakamani kama wanavyofanya wazungu…..hapana, sisi tulishafikia maafikiano, na mbele ya mwanasheria wetu huyo aliyetusalati, na ukinitajia mwanasheria naona kama ni watu wakuja kula pesa zetu, na kuchunguza undani wa watu ili waweze kuwatapeli….lakini hata hivyo, huyo mwanasheria alitushauri kuwa, tukapeana muda wa kufikiria, kabla ya kufikia maamuzi ya kuandikiane talaka…’akasema

‘Kwahiyo baba kwa ujumla talaka, haijatoka?’ akaulizwa.

‘Talaka….?...ndio talaka ya, kimaandishi haijatolewa, lakini kwa kauli zetu, mimi na yeye, tulishaafikiana hivyo…lakini mwanasheria hakutaka kukimbilia kuandika hiyo talaka kwa haraka, na akadai tupeane muda kwanza…na mambo yalivyo, nimekuja kugundua kuwa , kumbe walikuwa kitu kimoja…walikuwa wakinizunguka …..mungu amewaumbua.’akatulia.

‘Baba hayo mengine ni ya kusikia tu…naomba yasikuumize kichwa….’akasema binti.

‘Wewe unasema tu, kwa vile ni mama yako, …lakini kama ungelikuwa wewe kwenye nafasi yangu, nina imani ungelichhukua hatua kubwa zaidi,…hakuna kitu kibaya kwenye ndoa kama kukosa umanifu,…kusalitiana, na kuendekeza shiriki…mama yenu alikuwa na uazaifu wa hayo yote,…shiriki, kila jambo mpaka kwa mganga, mimi sina hulka hiyo…msizani kuwa mimi maamuzi hayo nimeyachukulia kwa hara…’akatulia.

‘Sitaki kuyaanika mabaya ya mama yenu, kama anavyoanika hayo anayoyaona ni mabaya yangu, kwani haitanipa faida yoyote, lakini nimevumilia mengi sana….kueni myaone, ….ndoa ina siri nyingi sana, watu wanatoka nje wameshikana wakiitana mume na mke, lakini ndani ya nyumba zao kuna siri kubwa sana….usione watu wanashikwa na viarusi,..ukichunguza kwa mapana, kisa ni ndoa……oh, ….’akatulia.

‘Baba tunaomba usiyachukulie hayo kiundani sana, ….kama unahisi yanakuumiza, ni bora tukatishe haya amzungumzo….;akasema huyo binti pale alipomuona baba yake akihangaika .

‘Msiwe na wasiwasi…..’akasema na kutulia kwa muda, na yule binti alipoona baba yake yupo sawa, akasema;

‘Hayo matatizo ya ndoa, ….ni kweli yapo, japokuwa hatujawahi kuingia huko, lakini baba mimi nina imani kuwa wanandoa wakitaka maisha ya ya ndoa yao yabadilike yawe wanavyotaka wao, wanaweza kufanya hivyo na wakafanikiwa….tatizo ni ile hali ya kila mmoja kukubali ukweli, na kujiweka katika nafasi yake….’akasema mmoja wa wale mabinti.

‘Ni kweli baba, na ukitaka maisha ya ndoa yenu, irejee kwenye upendo, wa kweli mnaweza, na sisi tutahakikisha kuwa yanabadilika, ….amueni kuwa mnarejea, na sis mtushirikishe, tuna uhakika, tukishirikiana pamoja tutafanikiwa….., tuna imani kuwa mama atakua sio yule unayemfahamu tena’akasema binti.

‘Wanangu, hayo ya mimi na mama yenu, ni sawa na kumpigia gita mbuzi,…..sikuanza leo, na niliwahi hata kumtafuta dakitari bingwa, ajaribu kukaa na mama yenu, ili arejeshwe kwenye msiamamo wa ndoa,…..lakini haikusaidia,….kiukweli…mim sina imani na mama yenu tena…..sina mapenzi naye tena….naombeni mnifikirie na mimi, na kama kweli mnanipenda na kunijali na mimi….nipeni nafasi yangu, kumtafutia mwenzake, ambaye atanipa tulizo la moyo…..’akasema.

‘Baba kwa umri huo,….na hata hivyo ni nani kwa umri huo, atakubali aolewe na wewe…?’ akauliza.

‘Wapo wengi….lakini baada ya kufanya uchunguzi, nimempata mmoja,…nitakuja kuwatambulisha kwenu, kama ndio mnataka iwe hivyo, …..’akasema.

‘Baba unamzungumzia, Maua ?’ wakauliza na kabla baba yao hajajibu yule binti mkubwa akasema;

‘Baba kwa ushaidi tulioupata Maua kweli ana uja uzito, lakini hiyo mimba sio yako….ni ya mpwa wako, na huenda kuna ujanja unataka kuchezwa ili ubambikiwe hiyo mimba,….hilo hatutalikubalia. Cha muhimu tunajua kuwa mimba ni ya mpwa wako, na kama unataka kutoa msaada ni shauri yako…’akasema binti.

‘Hilo niachieni mimi,…kama ni yangu au sio ya kwangu, hilo haliwahusu, mimi ninayemuhitaji ni huyo binti, na nimeshawaambia kuwa yule ndio dawa yangu, …kama isngelikuwa huyo binti, msingelinikuta hai …..mengine hayana maneno ya kuelezea, niachienii mwenyewe…., mimi nitailea hiyo mimba na hata kama mtoto sio wa kwangu…..lakini kama ni wangu, nitahakikisha nampata kwa kila njia …..oh’akasema.

Wale mabinti walimuangalia baba yao kwa muda wakiwa wametulia, kwani walimuona kama anaongea kitu ambacho hakieleweki, hiyo mimba, itaingieje, wakati wao wanajua kuwa alishafanyiwa upasuaji wa kuzuia kuzaa….wakaangalia na kukonyezana, na baba yako, alipowaona mabinti wake wapo kimiya akasema;

‘Kwahiyo hakuna mwenye taarifa yoyote mliyoipata ….?’ Akauliza huku akiwa kama anajisikia vibaya, akachukua maji akanywa na kutulia kwa muda, ….akainama huku akiwa kashika kichwa, akionekana kuwaza sana, na wale mabinti wakaogopa kuwa wakiendelea kuliongelea hoja iliyokuwa ikiongelewa huenda likamuathiri baba yao,…..na ndipo mmojawapo akasema;

‘Baba usiwaze sana kuhusu hilo,…. hatujapata taarifa rasmi kutoka hospitalini, ….tulipofika asubuhi, alikuwa bado hali yake ni ile ile….’yule binti akasita kuendelea, kwani …walikuwa wakitafuta mwanya wa jinsi ya kuleta taarifa waliyoipokea…ambayo ilikuwa sio nzuri kumwelezea baba yao.

‘Mimi sio mtoto mdogo, najua kuwa mpwa wangu hayupo tena duniani..dalili zote nimeshaziona, …na nina njia nyingi za kupata taarifa,….nimeshajua yote, …lakini….ni vigumu sana kuamini mpaka uone kwa macho yako….ooh, ndio dunia hii, maisha ni kitu kidogo sana, ni kama ndoto tu, ….unalala unaota, unahangaika na dunia, ukiamuka upo dunia nyingine, watu wanaanza kukuita marehemu….’akasema.

‘Baba …’akasema binti na mara simu ikalia.

Yule binti akaipokea na kuisikiliza kwa muda, halafu akageuka kumwangalia baba yake, na ….hakuweza kuzuia machozi, …akageuka kuangalia kwingine, na hapo akawa hana jinsi ila kusema ukweli..

‘Ni kweli baba..Tajiri hatupo naye duniani…..’akasema huyo binti, na kumsogelea baba yake, akawa kamshikilia kama anamkumbatia kwa upande upande na baba yake alikuwa kainama vila vile, baadaye akasema;

‘Nilijua…..tatizo ni kuwa kauwawa….sasa muuaji, apatikane,….huyo muuaji,… huyo mwanamke, ….’akaseimama na akawa kama anapepesuka.

‘Baba tulia unataka kwenda wapi..’yule binti mwingine akasema an kumsogelea baba yakae.

‘Hasira….natamani ule ujana wangu ungelikuwepo….na sijui nikimuona huyo binti, sijui…nitamfanya nini….na kama polisi watashindwa kumpata , nitatumia vijana wangu watamkamata tu, ….’akasema

‘Baba iachie sheria ifanye kazi yake, hilo lipo mikononi mwao kwa hivi sasa, huwezi kuwaingilia…..’akasema binti yake.

‘Sheria itafanya kazi…mmh?....na ifanye kweli kwani kama haitafanya hivyo, nitafanya hivyo mwenyewe…na wasipoangalia, vifo vingi vitafutia…..ninavyowajua hawo watu……sijui, tatizo ni kuwa watu wakishaonja kumwaga damu, wanabadilika kabisa, kwao wanaona ni kitu cha kawaida…kuua mtu wanaona kama kuua ng’ombe…..’akatulia.

‘Basi baba ngoja tuangalie taratibu nyingine , za mazishi…..wewe tulia, na jipe moyo’akasema binti.

‘Na …..wale akina mama na binti yao, wapo wapi,….kwani nilisikia waliitwa na Mpwa wangu…..inawezekana bado wako huko huko,…namombeni sana muwakaribishe hapa kama moja ya familia,…..na nahitajia sana kuongea na wao….’akasema.

`Baba usiwe na shaka na hilo…’akasema mmoja wa wale mabinti

Na mara mlango ukagongwa, na ….

********

‘Wewe ndiye mama yake Maua..?’ sauti ikasema kwa nyuma yao, wote wawili wakageuka, na kujikuta wakiwa wanaangaliana na mama mmoja aliyekuwa kavaa mawani, na mkononi kashika simu, huku akiwa anataka kuongea na mtu.

‘Mama hebu twende, huoni mtu mwenyewe anaongea na simu..’akasema Maua.

‘Subiri…naona kama namfahamu huyu mama’akasema mama Maua.

‘Subirini naongea na mtu muhimu sana…..nataka kuongea na nyie,….’akasema yule mama alipoona Maua akamvuta mama yake.

Yule mama alipomaliza kuongea na simu akawasogelea, akavua ile miwani, halafu akashika kiuono, akamwangalia mama Maua,halafu akamwangalia Maua, halafu akasema;

‘Hivi kumbe upo hai, wewe si ulikimbilia msituni, na kwa mara ya mwisho nilisikia kuwa umeuwawa na watu wa msituni…’akasema huyo mama.

‘Kama unavyoniona ndio mimi, hayo mengine yalikuwa ni maneno tu…’akasema mama Maua.

‘Ohhh, na huyu ndiye binti yako…?’ akasema na kumwangalia Maua

‘Ndio yeye, …’akasema mama.

‘Sasa wewe mama, hebu niambie, ….hivi kweli una uchungu na mwanao, …kibinti kidogo hiki, kiende kiolewe na mzee,….sasa na babu yake, una akili kweli, na hata hivyo hii, dunia inakwenda wapi, yaani binti mdogo kama wewe unakwenda kufanya ufusuka na mzee kama yule….’akatema mate chini.

‘Wewe mama wewe nakuomba usinivunjie heshima ynagu,…sijafanya hivyo unavyosema wewe..’akasema Maua.

‘Najua utasema hivyo, kuwa yule mzee, kakutaka…lakini kwa kauli niliyoisikia ni kuwa una mimba, ..hehehe….hivi wewe huna aibu uende kumbambikia yule mzee mimba, …yule mzee hazai, kwa taarifa yako, ….alifanyiwa upasuaji …’akasema huyo mama.

‘Wewe mama, nakuambia tena, kuwa hayo unayozungumza hayana ukweli….wewe yaache kama yalivyo…’akasema Maua.

‘Unasema niyaache kama yalivyo….?’ Akasema kwa sauti ya ukali, akimwangalia Maua…

‘Wewe binti, niangalia hivi hivi….unajua nikuambia ukweli, nyie ndio mumechangia huyo mzee, asinirejee….kama isingelikuwa nyie, angenirudia tu, ile biashara yake, na miradi yake, mnajua jinsi ilivyopatikana….ni mimi na juhudi zangu, sasa hali imekuwa nzuri, wanakuja watu wa ajabu, ….na mabya yatawaandama, unaoana …..wameanza kuuana, na bado, ….’akasema huku akitaka kupokea simuiliyokuwa ikiitwa.

‘Mama hebu twende zetu….’akasema Maua.

‘Hebu subiri kidogo, sijatoa kauli yangu yoyote kwake,…..’akasema Mama Maua.
Yule mama alimaliza kuongea na simu, akawageukiwa Maua na mama yake, akasema;

‘Sikilizeni kwa makini, iacheni ile familia kama ilivyo, kama mumekosa sehemu ya kwenda, rejeeni kijijini mkalime, kwani yoyote yule atakayeingie pale, kwa namna yoyote, kama sio mwanafamilia, hataishi…nawahakikishia, kama mimi sio mwanamke wa huko, kulikoogopewa, jaribuni kuingia pale….’akasema huku akiwa kashika kiuono.

‘Mimi ni mama yake huyu, na nilikuja kuangalia jinsi gani ya kuyaweka hayo mambo sawa, wewe kama mwanamke mwenzangu, nakuomba tukae tuongee tuone jinsi gani ya kuyasawazisha, maana hakuna mtu anayeweza kukurupuka na kwenda kudai kuwa mimba na huyu, bila kuwa na mahusiano naye,…..’akasema mama Maua.

‘Kwahiyo wewe unaona ufahari, kusikia kuwa binti yako katembea na mzee kama yule, ….hivi wewe unatoka kijiji gani, au ndio maana walikutimua wazazi wako…’akasema huyo mama.

‘Sijafurahia hilo, na hilo halijakubalika kuwa kuna mahusiano kati ya binti yangu na mzee wako..hayo ni maneno tu, …na ukiyajua kiundani utaelewa kwanini imekuwa hivyo….na kama nitaamua kwenda polisi, huenda huyo mzee wako na wote wanaohusika watakuwa hatiani, maana huko ni kubaka….’akasema Mama Maua.

‘Hehehe….unatishia nyau eeh, nendeni polisi, maana huko ndio mtaumbuka, nimeshawaambia yule mzee hazai , hiyo mimba …imetoka wapi, ….sawa hata kama kwa uzinzi wake alikutana na huyo binti, na huyo binti bila aibu, akamkubalia,…..maana hapo, ni kujiuza, ….lakini asisisingizie mimba,….hilo litawaumbua’akasema yule mama.

‘Hayo tukikutana pamoja tutayaongelea, na ukweli utajulikana..’akasema mama Maua.

‘Mkutane na nani….nawaombeni mondoke mrejee huko mlipotoka, hakuna wa kukutana naye…..’mara simu ikalia tena. Alisikiliza kwa makini, halafu akasema kwa hasira.

‘Nani aje huko, mwambieni, mimi sina muda wa kupoteza….na hawo wanawake mnaowazungumzia ninao hapa, nimewaambia waondoke zao…..’akasema

‘Nimeshawaambia sina muda huo, yote nitayamaliza nijuavyo mimi, kwanza wameanza kuuana, mwishoni waliobakia wataanza kuwehuka….hilo nawaambia mlisikie, huyo baba yenu anajifanya hanisikilizi, atakuja kunipigia magoti…’akasema huyo mama.

‘Nitakuja kwa wakati wangu, lakini siwezi kuongozana na hawa wanawake, watanitia aibu….’akasema na kuanza kuondoka..

‘Mama twende zetu….’akasema Maua.

‘Twende wapi sasa?’ aakuliza Mama Maua

‘Twende huko huko, mimi mama siwezi kuondoka mpaka nihakikishe nimepata haki yangu, …siwezi kuwaachia hivi hivi…’akasema Maua.

‘Haki gani , na wakati anayejua yote keshafariki?’ akauliza mama Maua.

‘Hayo tutayajua huko huko…yule mzee ni mpwa wake, na…..na huyo dakitari, ataelezea ukweli ulivyokuwa..’akasema Maua.

‘Kama ni hivyo, kwanini tusiende huko kwa huyo dakitari…’akasema Mama Maua kama anauliza.

‘Twende kwanza huko tulipoitiwa….kwa huyo mzee’akasema Maua.

‘Aaah, na wewe na huyo mzee….nakuambia ukweli, mimi sitakubaliana na hayo ya mama yako, kama wewe ni mwanangu kweli, achana na huyo mzee, sitakubali kamwe uolewe na huyo mzee, kama unaogopa kuhusu kulea, twende tukaishi pamoja, nilikulea wewe kwa shida, sitashindwa kumlea mjukuu wangu,….’akasema Mama Maua.

‘Mama mimi ninachodai ni haki yangu, wameniharibia mpangilio wa maisha yangu…na kwa maelezo ya Tajiri, Mzee anawajibika kwa hili…na hapo hapo kwa mzee ndipo tunaweza kupata ukweli wote, na mwenye ujauzito  huu tutamjulia hapo hapo…’akasema Maua.

‘Haya….twende ….na huyu mama yako mdogo kaenda wapi? ’akasema Mama Maua, na kuangalia huku na kule.

‘Atakuwa katangulia kwa huyo mzee,….tutamkuta huko huko…’akasema Maua.

Mara wakasikia sauti ikiita nyuma yao, walipogeuka wakamuona ni mama mdogo akija kwa kasi, ….wakamsubiri hadi alipowafikia, akiwa bado ana hema, akasema;

‘Mumesikia hiyo…msicheze na polisi,…msicheze na yule mzee, niliwaambia ni mchawi,..ona sasa, nasikia yule wakili naye, ….’akaonyeshea kwa kidole shingoni.

‘Unamaana gani kusema hivyo…’akauliza mama Maua.

‘Ngoja ninyamaze maana polisi hawana dogo, wewe sikilizia tu,….’akasema huku akitembea kuongoza mwendo, akionyesha kuwa na wasiwasi ….mama na mwanae wakaangalia na baadaye wakamfuatia nyuma.

NB: Msichoke,…tupo pamoja.

WAZO LA LEO: Binadamu tulivyo, kila mmoja ana maono na hulka yake,…mnapokuwa kwenye ndoa, nyie ni kitu kimoja, mnahitajika, maono na hulka hizo zilandane, kwa kuonyeshana, kuambizana ukweli kuhusu maono hayo, jinsi gani unavyojisikia, au jinsi gani usivyopenda iwe au isiwe…, kwani neno dogo tu linaweza likaleta tafsiri tofauti na kusababisha kutokuelewana, hata kama mmoja alisema hivyo bila nia mbaya.

Ni vyema basi, tuwe wawazi, na tusiogope kuelezana huo ukweli, na pia tukubali kusikiliza, tuondoe mfumo dume/jike ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima kwenye ndoa zetu. 

Ni mimi: emu-three

2 comments :

Yasinta Ngonyani said...

Na pia katika ndoa ni lazima kuwasiliana ni kitu kikubwa sana ni kama vile kupalilia shamba...nimependa wazo la leo..na kazi yako hakika si mchezo..Hongera sana.

emuthree said...

Wengi wakishapata shamba hawana muda wa kulihudumia, mpaka linaota majani. Ndoa kwao wanajua ni kutimiza wajibu na kupata sifa ya kuwa MWANANDOA.

Ndoa ina hitajika kuenziwa,kuhudumia kama lilivyo shamba, kwa kuelewana, kusikilizana, na kujadiliana pale mnapoona kuna tatizo.

Kuna tabia za kurithi, nyingine hazifai, ulizaneni kwanza, usijichukulie maamuzi yako mwenyewe, kwani mwenzako anaweza akakuchukia sana. Kwenye kisa chetu, tabia iliyojionyesha ni `ushirikina,' zipo nyingi.

Nashukuru sana dada yetu Yasinta, kwa mfano huo wa shamba.