‘Mume wangu najua nimekuwa mbaya kwako, na huenda yote niliyowahi
kukufanyia hayana maana tena kwako…tenda wema uende zako. Lakini hata kama
hujali wema wangu, sio sababu ya kutaka kuoa mjukuu wako, hii ni fedheha kwa
familia yako, na sijui unataka watoto wako wajisikieje….’Maua akasikia sauti ya
mwanamama ikiongea, …mlango ulikuwa haujafungwa vyema, kwahiyo watu wakiongea
ndani unawasikia.
Maua akasimama ghafla, na kutulia, na wenzake waliokuwa
wamesimama kwa mbali wakisubiria kukaribishwa kwanza, wakawa wanamwangalia
Maua. Na mama Mdogo alipoona Maua kaduwaa pale mlangoni, akasema;
‘Kwanini tusiingie ndani, hamuona mlango upo wazi..’akasema
mama mdogo huku akitembea kuelekea pale aliposimama Maua akitaka kuingia ndani,
lakini Maua akamzuia.
‘Hebu subirini
kidogo, kuna kitu nasikiliza….’akasema Maua na mama yake akasogea karibu na
aliposimama binti yake, na kumfanya mama mdogo arudi nyuma, akisonya kwa
hasira. Maua akawa katega sikio kusikiliza kinachoongelewa huko ndani.
‘Mimi sioni ubaya wa mzee kama mimi kumuoa binti sawa na
mjukuu wangu, na hata kama wewe umempata kijana uliyependezewa naye, ninakupa ruhusa
nenda ukaolewe..’akasema Mzee na yule mama alimwangalia yule mzee kwa jicho
baya, akasema;
‘Mimi sina laana hiyo….siwezi kujishushia hadhi yangu, kwa
kujizalilisha kwa watoto…kwanza ili iweje, nitapata nini kwa huyo kijana, kama
sio kujivunjia heshima’akasema yule mwanamama.
‘Kwasababu gani,….ngoja nikuambie kwa nini mtu kama mimi
nifanya hivyo, ni kwa kuwa huyo binti ameweza kuyafanya yale ambayo mke wangu…wewe
uliyekuwa mke wangu, hakuweza kunifanyia, kwanini nisimchukue binti hata kama
ana umri mdogo,…..’wakasikia Mzee akisema.
‘Hahaha….unanichekesha kweli, yepi aliyokufanyia ambayo mimi
nilishindwa kukufanyia, tatizo lako ni kuwa tamaa zimekuzidi, hakuna lolote na
pia wewe ulitaka niwe kama mtumwa wako, kila utakalo mimi nikubali tu, nikae
ndani kama mfungwa, hivi dunia ya leo ni ya kumweka ndani mke kama kitanda, ili
ukija unakilalia tu….hiyo ni aibu kwako, wewe na uzee huo unamezea mate vibinti
vidogo huna hata haya, hamuoni kuwa ni kujizalilisha, ….’wakasikia sauti ya
mwanamke ikiongea.
‘Kwangu mimi sioni kuwa najizalilisha,….kwasabbu sijafanya
ubaya, nimeamua kufuata taratibu zote, na sijawahi kusikia popote wakisema
mzee, hawezi kumuoa kijana-binti mdogo, au kijana, binti mdogo hawezi kuolewa
na mzee, hizo ni hisia zenu…..na sio kwamba mtu anapenda kufanya hivyo bila
sababu, hali halisi inamsukuma mtu afanye hivyo….’akasema Mzee.
‘Kwahiyo kama hiyo hali halisi ikiondolewa, hutakuwa na haja
ya kumuoa huyo binti?’ sauti ikauliza, ilikuwa ni sauti ya mmoja wa binti.
‘Sio rahisi kama unavyosema wewe,…. moyo ukipenda, au
ukikinai jambo, kuurejesha kwenye hali nyingine inakuwa vigumu, sana sana ukilazimisha
mtokeo yake ni kujiumiza…mimi hali iliyofikia kama ningeendelea kuwa na mama
yenu mngekuwa mumeshanisahau,…..’akasema huku akimwangalia yule mwanamke,
aliyekuwa kaangalia pembeni akiwa kama hataki kuangaliana na huyo mwanaume.
‘Angalieni, binti wa watu nimekaa naye siku mbili tu…., na
sio siku mbili, maana amekuwa akija kwa muda tu, na kuondoka, angalieni
mabadiliko niliyoyapata….hamuyafurahii haya mabadiliko?’akatulia.
‘Mabadiliko gani, mimi sioni ulichobadilika nacho….ni uzee
tu,….hakuna jingine, na zaidi ni ufinyu
wa kufikiria kwani ukizeeka sana na akili zinasinyaa…, jiheshimu mzee, hiyo
unayotaka kufanya ni aibu,..na huoni kuwa unamnyima haki huyo binti, kwani
alihitajika kuolewa na kijana mwenzake, wewe umemkatili….hiyo ni
dhuluma…’akasema huyo mama.
‘Unauliza mabadiliko gani,…wewe ulipoondoka uliniacha
wapi,….si uliniacha nikiwa kitandani, sijiwezi,….hebu ulizia yaliyotokea hapa,
walishafikia hatua wananisubiria ili wakanizike,…lakini akaja huyo binti,…ooh,
jamani, …kwanini hamunielewi’akasema huyo mzee.
‘Nilikuacha kitandani kwa vile ulinifukuza, kama
usingelinifukuza ningeliendelea kuwa nawe, na kukuhudumia,…..kama kufa siku
zikifika utakufa tu, hata akiwepo dakitari, …..sioni kwanini umtukuze huyo
binti, na nakuapia ole wake….’akatulia.
‘Mama usiseme hivyo, tulishakuomba, na ukakubali kuwa
utaongea kwa amani na busara, sasa…hayo ya kuapiza yanatoka wapi tena..mama
sisi tungelifurahia kama ungekuja na kuishi na baba tena, kwanini usimuonyeshe
kuwa upo tayari….’akasema mmoja wa binti.
‘Inabidi nimuambie ukweli huyu baba yenu, maana itaniuma
sana, kuona mzee kama huyu anaoa kibinti, na wakati nyie ni watoto wangu, eti mnaishi
na binti ambaye huenda kawazidi umri, ,mnafikiria nini kitatokea, nyie hamuyajui
hayo, msifikirie huku ni ulaya…’akasema na kutulia kidogo, na baadaye akasema;
‘Akiolewa huyo,….hamtaweza kumuheshimu kwa vile ni mdogo, na
yeye ataona mumemzarau, ataanza kuwachongea kwa huyo mzee, na kwa vile mzee
keshapenda, …unafikiri nini kitatokea…atamasikiliza yeye, na nyie mnaweza hata
kutimuliwa kwenye nyumba yenu…kwa mtaji huo mimi sikubali, katu sitakubalina na
hilo,…kama hanitaki mimi atakaaa hivyo hivyo, hadi atakapokufa…na nyie make hapa
mlinde mali zenu’akasema huyo mama.
‘Wewe mwanamke,….hukubali nini, unahusika na nini hapa
ndani,…kwanza hayo maswala na kunitisha tisha, sitai kuyasikia , maana mimi
sitishiki….ndio nakujua tabia zako,na hizo ndizo zinanifanya nisiwe na amani na
wewe…una imani za kishirikina , hapo ulipo unafikiria kumloga binti wa
watu…nakuambia ukweli, uchawi wako hauwezi kumzuru yoyote…ni ibilisi tu,…’yule
mzee akawa anasema kwa sauti.
‘Mimi nimeshasema, wewe utaamua mwenyewe, lakini sitaweza
kuona watoto wangu wanaishi na huyo binti, eti ni mama yao, hilo
halitakubalika na nitalipiga vita kwa
nguvu zangu zote…’akasema huyo mwanamke.
‘Tutaona, ….’akasema Mzee, na kukatishwa na simu, binti yake
akaipokea na kusikiliza na baadaye akasema, akiongea na huyo aliyepiga simu;
‘Lakini iweje mtu atoreke kwenye kituo chenu, hamuoni kuwa
kuna udhaifu…..’akatulia na kusikiliza na baadaye akaweka simu na kuwageukia
wenzake akasema;
‘Wanasema wakili naye katoroka, na kuna wenzao wengine
wameuwawa, wakati wanatoroka, …..’akasema huyo binti.
‘Mnaona, …..ndivyo itakavyokuwa hivyo, watakimbia watauwana,
lakini hawatakuwa na amani,….hawawezi kuingilia anga zangu….haki yangu
itawaangamiza mmoja baada ya mwingine…’akasema yule mwanamke.
Kukatulia kidogo, na baadaye, yule mzee, akasema;
‘Mbona hawa watu hawaonekani, hebu jaribu kuwapigia simu…..’akasema
Mzee, na akina Maua walivyosikia hivyo, wakasogea mbali na mlango, wakawa kama
wanatoka nje, na mama yake Maua akasema;
‘Kuna haja kweli ya kuingia humo ndani,…binti yangu,
tuondoke hapa kabisa, hii ni familia ya watu, utajiingiza kwenye matatizo yasiyo na maana
kwako,….huyo mwanamke nimeshamfahamu, ukoo wao unaogopewa sana kule kijijini,
..tuondokeni zetu’akasema mama Mua.
Maua akainama kidogo., halafu kweli akaanza kuondoka, mama
mdogo akamuwahi na kumshika mkono, akasema;
‘Haondoki mtu hapa mpaka kieleweke, kwanini nyie mnaogopa
nini, …mtoto wa majini halogeki, wanaologwa ni wale wanaoamini mambo hayo….mimi
siyaamini,..japokuwa nayasikia,….hatuondoki hapa hivi hivi….’akasema.
‘Wewe kama unataka nenda, kaongee nao, sisi tunaondoka…’akasema
Maua na wakaondoka na mama yake. Mama mdogo, alisita kidogo na baadaye
akawafuata huko nje, huku akilaani, kwa kitendo hicho.
‘Haiwezekani, ina maana ndoto zangu zote zipotee hivi hivi,….hapana,
lazima nitafanya jambo,..’akasema na kutoka nje, na huko nje aliwaona wenzake
wakielekea getini, kuondoka kabisa kwenye eneo hilo, akawakimbilia na
kuwauliza;
‘Sasa mnataka twende wapi?’ akauliza huku wakiwa
wameshaingia mitaani , kwenye watu wengi.
‘Tunaenda kumtafuta dakitari aliyekuwa akimtibia huyo mzee’akasema
Maua.
‘Wa nini,ni nani anaumwa hapa…na kama ni maswala ya Maua,
haumwi, ni mambo ya uja uzito hayo,….au kuna nini kwa huyo dakitari, madakitari
mara nyingi hawana pesa..’akasema mama mdogo huku akiwafuatia kwa nyuma.
‘Hatuendi kwake kwa ajili ya kutafuta pesa,…tunahitajia
kujua ukweli, je huu uja uzito ni wa nani?’ akasema mama Maua, na kumfanya mama
mdogo, awaangalie kwa mashaka na kusema;
‘Hivi nyie, ….manataka kuthibitisha nini…mimba hiyo
inajulikana ni ya nani,…na kama alimpa hiyo mimba keshakufa, basi wa kubeba huo
mzigo ni mjomba mtu, tunatakiwa tucheze karata vyema, tukizubaa hatutapata kitu
hapa…..mimi nawashangaa mnataka kumuona dakitari ili iweje?’ akauliza.
‘Hayo utakuja kuyajua baadaye….maana mdomo wake hauwezi
kufungwa,..ni bora uelewe hivyo hivyo…’akasema Maua akawa kama anatabasamu,
lakini myoni, alikuwa akiumia kuona binti yake anaishi ya huyo ndugu yake.
‘Tatizo lenu hamuoni mbali, na kwa mtaji huo, mtaendelea
kuwa masikini,…na naona nifanye mpango wa kupata pesa nirejee bongo,…’akasema
huku akichukua simu yake, na kuanza kupiga namba, na wenzake hawakumsubiri
wakaondoka.
*******
‘Dakitari yupo Dar,…kafungua ofisi yake huko, na anakuja kwa
dharura tu, je mlikuwa na shida gani nay eye,…?’ akauliza mmoja wa wahaudumu wa
hiyo hospitali, ambayo anaimiliki huyo dakitari waliemfuata.
‘Tuna shida kubwa na yeye, ….kama yupo Dar, tutamfuata huko
huko,….umesema hiyoo hospitali yake kaifungua sehemu gani?’ akauliza.
‘Maeneo ya Sinza….ukifika hpo ukiuliza jina lake,
wanamfahamu sana, kwani ni dakitari bingwa…’akasema huyo mhudumu …
‘Sawa tunashukuru….’akasema Maua na wakaondoka na mama yake,
hadi kwenye hoteli wanayoishi.
‘Mwanangu mimi naonatuondoke, twende tukaishi pamoja
kijijini..’akasema mama Maua.
‘Mama mimi mpaka nimjua baba wa huyu mtoto, kama Tajiri,
alisema yeye sio aliyenipa hii mimba, basi yupo mtu mwingine…..ni lazima
nimfahamu’akasema mama Maua.
‘Halafu itasaidia nini…na kama ni mmoja wa walinzi wa
Tajiri, maana kama alizidiwa na ulevi, na wewe kutokana na hayo madawa ulikuwa
hujitambui, basi lolote liliweza kufanyika….katika wasadizi wake yupo mmoja
alifanya hivyo….’akasema mama Maua.
‘Ni lazima nimfahamu……na nitafanya kila aina ya uchunguzi
mpaka nimfahamu….swali kubwa, ni kwanini Tajiri akasema tumuone dakitari, je
yeye anahusika nini na huu uja uzito….’akajiuliza Maua.
‘Au labda yeye ndiye aliyekupa huo ujauzito..’akasema Mama
yake.
‘Haiji akilini, maana siku ile kwa kumbukumbu zangu,
sikuweza kumuona, ina maana alikuja baadaye, au ni mmoja wa kundi lao….?’ Akawa
anajiuliza.
‘Ingelikuwa mimi ni wewe…nisingelisumbuka kabisa, na kwa
vile hata aliyekupa mimba hajulikani, basi, mtoto utamwambia baba yake alikufa,…yamekwisha,…..nani
atakuuliza, maana kweli humjui, tatizo na pale unapomfahamu…hutaweza kumficha
mtoto…’akasema mama yake.
‘Mbona mimi umenificha, wakati unafahamu fika kuwa baba
yangu ni nani?’ akauliza Maua, na hapo akamfanya mama yake atulie, na kujikuta
akitingwa na mawazo, akasimama na kutembea hadi kwenye dirisha, akawa
anaangalia nje, na kumbukumbu zikaanza kumrejea, siku ile alipoamua kwenda
hospitali mwenyewe.
*********
‘Oh,…naona kuna kitu,
…..nimeota…..mungu nisamehe, ..ooh, eti nini, hapana..haiwezekani, ina maana ni
damu yangu, haiwezekani,..oh, Maua ina maana wewe ni ni….oh, oh, oh, kamuone
docta atakuelezea, ….’ Maneno haya
yalimrejea mama Maua, na siku ile ile aliamua kurejea hospitalini, na alipofika
akaambiwa kuwa huo mwili ulishahifadhiwa.
‘Docta samhani sana,….nina mashaka kuwa huyo mtu ni ndugu
yangu, alipotea kijijini muda mrefu uliopita, naomba niutambue…’akasema.
‘Mbona ndugu zake wameshafika ….’akasema docta kwa mashaka.
‘Waliofika nawafahamu, na watoto wa mjomba wake, …..mimi
nilikuwepo wakati anakata roho, akatuagiza jambo, na kauli aliyoiongea
inaashiria kuwa ni mmoja wa ndugu zangu…nahitaji nimuone, na kuna alama
nikiiona nitajua ni yeye, ….’akasema.
‘Lakini sio utaratibu,….’akasema docta, na hakutaka
kubishana na huyo mama akamchukua huyo mama hadi pale ulipohiofadhiwa huo
mwili, na kumwangalia huyo mama.
‘Mwili wenyewe ndio huo, ….nikuachie, au unahitaji msaada
wangu?’ akauliza.
‘Nomba msaada wako, ..alama hiyo ipo shingoni,…kwenye shingo
yake, kuna sehemu aliumia akashonwa…kulibakia kitu kama mstari, …..’akasema na kabla hajamaliza, yule
dakiatari akawa keshamfunua yule maiti.
Mama akamsogelea na kumwangalia vyema usoni…na hisia za
kumbukumbu zikaanza kumrejea, japokuwa
sura ilikuwa imebadilika…lakini akawa
anahisi kama ndio huyo mtu anatemfahamu…
‘Hii alama ndio hapa?’ akauliza docta
Mama akasogea na kuiona,…alama ilikuwepo, lakini ilikuwa
ndogo sana, sio kama ile aliyokuwa akiifahamu,…hata hivyo alishangaa kujishia
mwili ukiishiwa na nguvu, …kitu ambacho kilimjia ghafla,akajikaza na kuinama
kuichunguza vyema ile alama, lakini labda kwasababu ya unene, alama ile ilikuwa
imefifia..hata hivyo, alijikuta machozi yakianza kumjia machoni, akasema;
‘Oh, inawezekana sio yeye……’akasema huku moyoni akiomba asio
ndio yeye, kwani itamuumiza sana, na ni kama mkosi,….
‘Nitashukuru sana akiwa sio yeye, maana ni aibu,…je kama
aliwahi kutembea na ….mungu naomba siwe ndio yeye….na kama angelikuwa ndio
yeye, wakazaa na binti ….ya..yake..hapaan sio yeye…’akawa anasema kwa sauti
ndogo ambayo huyo dakitari hakuwahi kumsikia, na yule dakitari akajua huenda
huyo mama alikuwa akimuombea huyo marehemu, akawa anafanya shughuli zake
nyingine, na Mama Maua akawa anaondoka, na yule dakitari akasema;
‘Kwani mama wewe ni mwenyeji wa wapi, inaonekana sura yako
sio ngeni kwangu?’
‘Natokea Singida…’akasema huku akitamani atoke hapo ndani
haraka.
‘Basi nimeshawahi kukuona hata kama sio huko, lakini
nimeshawahi kukuona mahali….inaonekana kabisa ninakufahamu….Hata mimi natokea
huko huko Singida, hata huyu marehemu namfahamu..’akasema.
‘Unamfahamu…..ooh, unamfahamu vipi?’ akauliza.
‘Marehemu anatokea huko huko kijijini, alikuja huku
Mererani, na bahati nzuri, hali ikamnyookea,…na Tajiri akawa Tajiri kweli….na
hata jina lake la asili, likasahaulika kabisa..’akasema.
‘Mimi wasiwasi wangu ni hilo jina,..Tajiri, ..mbona majina
kama hayo hayopo kule kwetu Singida,….na hata huyo niliyekuambia kuwa ninammfahamu,
hata nikamfananisha na huyu hakuwa na jina hilo la Tajiri, ndio maana naona sio
yeye…..’akasema mama Maua.
‘Wengi wanabadili majina yao kwasababu zao binafsi….wengine
eti wakitafuta nyota ya bahati,kwa ajili ya kupata madini ….’akasema huyo
dakitari huku akicheka.
‘Hizo ni imani zao…’akasema Maua.
‘Ni imani tu,…...na hata huyu marehemu aliabadili jina,
kwasababu namfahamu kwa jina lake la asili...na hutaamini wenyeji wengi wa hapa
hawamfahamu kwa jina lake la asili,…’akasema huyo dakirai na kumfanya mama Maua
ageuka na kumwangalia yule dakitari hata ile haraka ya kuondoka ikapungua.
‘Huyu Marehemu alipofika hapa, akawa haonekani onekani…alikuwa
mtu wa kujificha ficha, akipambana na polisi, maana alikuwa akishirikiana na
binti mmoja matata, waliokuwa karibu naye walimkanya kuwa huyo binti, ni uzuri
wa sura tu, lakini kiundani sio mwema, lakini hakusikia.
‘Kuna kipindi alitafutwa sana na polisi, ….na akawa kama
kapotea kabisa,… na nalipoonekana tena,akawa kabadilika kabisa, kawa mnene,
tofauti na umbo lake, la awali….alikuwa mwembamba sana huyo jamaa….na alikuja
kwa jina hilo jipya la Tajiri….akawa anagawa pesa, na kuhakikisha kuwa kila mtu
anamuita kwa jina hilo….la Tajiri., likajulikana na likawa ndio jina lake….’akasema
huyo dakitari
‘Ina maana hilo sio jina lake hasa la asili…?’ akauliza mama
Maua akiwa na moyo wa shauku, hadi akawa kama anajisikia kudondoka.
‘Hapana sio jina lake la asili,…mimi namfahamu sana…..japokuwa
kiukweli amebadilika sana, kwa tunaomjua …..tunaweza kumkumbuka, lakini kwa mtu
ambaye alionana naye mara moja, hawezi kusema huyu ndiye yule aliyetoka
kijijini, akiwa hana mbele wala nyuma….’akasema huyo dakitari.
‘Kwahiyo jina lake la asili anaitwa nani?’ akauliza Mama
Maua.
‘Marehemu jina lake
la asili anaitwa Adam….’akasema huyo docta, na mama Maua akaziba mdomo, safari
hii hakuweza kuvumilia, akajikuta akilia kwa kwikwi, hadi yule dakitari
akashangaa, akamsogelea yule mama na kumliwaza.
‘Pole sana…naona sasa umemfahamu vyema….’akasema
‘Ndio nimemfahamu vyema….’akasema huku akijikaza kutaka
kuondoka, na hakuweza kumwangalia yule dakitari tena, akatoka kwa haraka haraka
huku akijifuta machozi, hadi kule alipomuacha Maua kwenye hoteli waliyofikia.Na
siku hiyo hakutaka kuongea, na hata Maua laipomuuliza mbona amebadilika hivyo,
yeye alisema;
‘Mwanangu nina wasiwasi na maisha yako, hali hii inatia
wasiwasi, ikizingatia kuwa mimi ndiye mama na baba yako, ……ukumbuke kuwa huna
baba, …na kama alikuwepo, hayupo hai tena…’akasema mama Maua.
‘Mama umeshaanza maneno yako…nilishakuambia kuwa mimi
simuhitaji huyo baba, ..baba wa nini kwangu, kama hakunitafuta wakati nikiwa
mtoto hadi nimefikia umri huu, atanitafuta sasa ili iweje…na hata nikikutana
naye, sitakuwa na haja naye tena, ….mungu amepanga iwe hivyo….achana na
kumbukumbu hizo…’akasema Maua.
‘Hutaweza kukutana naye tena mwanangu....msahau kabisa….sahau
kabisa ujue kuwa wewe hukuwa na baba….’akasema mama yake na Maua akamwangalia mama
yake kwa mashaka, alitaka kumuuliza mengi zaidi lakini mama yake mdogo akafika
na mazungumzo yao yakakatishwa, na hawakuweza kuliongelea hilo, hadi leo,
wakati Maua aliposema;
‘Mbona mimi
umenificha, wakati unafahamu fika kuwa baba yangu ni nani?’
‘Maua ni bora usimjue kabisa….huyo aliyeitwa baba yako,
kwani ukimjua utaumia sana..naomba usiwe na shauku hiyo…’akasema Mama yake.
Maua akahisi kuna jambo,….inaonekana mama yake kagundua kitu ambacho
kinahusiana na baba yake, akaona ni lazima akifahamu.
‘Mama kama baba yupo, na unafahamu wapi alipo, naona kwa
haya yaliyotokea ni bora nikaonana naye, ili nizitoe hasira zangu kwake, maana
kama angelikuwepo, akatimiza wajibu wake kama mzazi huenda haya yaliyonikuta
yasingelitokea tena….hata kama mlifukuzwa kijiji, lakini alikuwa akifahamu
kakuacha na ujauzito, kwanini asihanganike kukutafuta, ili ajue kama
umejifungua mtoto wake yupo wapi, …’akatulia kidogo, halafu kama vile kakumbuka
jambo, akasema;
‘Halafu mama, ehee, nimekumbuka,….kama sikosei ulisema baba,
au huyo mwanaume alikupa uja uzito wangu,….alikimbilia huku…au sio?’ akauliza
na hakusubiri mama yake aseme kitu, akaendelea kusema.
‘Ulisema alikuja kuishi huku Arusha Mererani, ….na leo
ulivyobadilika hivyo, nahisi kama umekutana naye, niambie mama ukweli maana
hayo mabadilko uliyonionyesha leo, inaashiria kitu…naomba mama unieleze, kama
umekutana naye, au kama yupo hapa, ni wapi anaishi, usijali, mimi sitakwenda
kumsumbua kabisa….ila nataka tu kujua hilo…’akasema Maua.
‘Mwanangu,…baba yako hayupo hai….nilishakuambia hilo, je
unahitaji ukaone kaburi lake?’ akauliza Mama Maua.
‘Kama hilo kaburi lipo, nitafurahia kuliona…na nikiliona
moyo wangu utatulia,..na kwa hilo, inabidi niache mambo mengine yote, hadi
nilione hilo kaburi, au nimuone huyo baba kama yupo hai,….angalau hata kwa
mbali tu….’akasema Maua. Mama Maua alimwangalia binti yake kwa muda, na hakuweza
kujizuia, akajikuta machozi yakianza
kumtoka.
*********
NB: Najaribu kukumbuka kitu gani tumesahau, maana ndio
tunaishia kwenye kisa chetu hiki.
WAO LA LEO:
Unapolima shamba, ukapanda mbegu, utarajie kuwa kuna mmea utaota, na mmea huo
ili ukuwe vyema, unahitajia matunzo.
Siku hizi wimbi la watoto wa mitaani linaongezeka, na ajabu
kabisa, kuna akina mama wenye mtindio wa ubongo, ….wengine ni wazima, lakini
hali zao, kiafya, zimewafanya wawe kama wametengwa na jamii, kuna wasiojiweza
kiviuongo, …wamepewa ujauzito, na hata kujifungua, lakini wanaume waliotenda
hayo hawaonekani,….
Wewe mwanaume, uliyetenda hivyo, unatumai nini…kama kweli
una ubinadamu nenda kamchukue mwanao, hiyo ni damu yako, na utahukumiwa kwa
hilo,…nenda kamchukue mtoto wako umlee…kwani ulipopanda mbegu ulitarajia nini?
*********
NB: Najaribu kukumbuka kitu gani tumesahau, maana ndio
tunaishia kwenye kisa chetu hiki.
WAO LA LEO:
Unapolima shamba, ukapanda mbegu, unatarajia kuwa kuna mmea utaota, na mmea huo
ili ukuwe vyema, unahitajia matunzo.
Siku hizi wimbi la watoto wa mitaani linaongezeka, na ajabu
kabisa, kuna akina mama wenye mtindio wa ubongo, ….wengine ni wazima, lakini
hali zao, kiafya, zimewafanya wawe kama wametengwa na jamii, kuna wasiojiweza
kiviuongo, …wamepewa ujauzito, na hata kujifungua, lakini wanaume waliotenda
hayo hawaonekani,….
Wewe mwanaume, uliyetenda hivyo, unatumai nini…kama kweli
una ubinadamu nenda kamchukue mwanao, hiyo ni damu yako, na utahukumiwa kwa
hilo,…nenda kamchukue mtoto wako umlee…kwani ulipopanda mbegu ulitajia nini?
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment