Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, March 15, 2013

Uchungu wa mwana Aujuaye ni mzazi-72



Maua alitoka nje , na kule nje aliwaona mama yake akiongea na mama mdogo, walionekana hawaelewani kuhusu jambo fulani, na walipomuona Maua wakakatisha yale mazungumzo yao, na kujifanya hakuna kilichokuwa kikiendelea kati yao, wakamsogelea Maua. Wakwanza kuongea alikuwa ni mama mdogo akasema;

‘Ehe tuambie, amewahi kukuandikia chochote, au kukuelekeza wapi pa kupatia pesa?’ akauliza mama mdogo, na mama Maua akashika mdomo akionyesha kushangaa kwa kauli hiyo, akamwangalai ndugu yake huku akiwa kamtolea macho akasema;

‘Hivi ndivyo unavyoishi na mwanangu hivyo…..?’ akauliza mama yake Maua akimwangalia huyo mama mdogo sasa kwa hasira.

‘Kama nisingelimfudisha jinsi gani ya kuishi unafikiri mngeliweza kuijenga ile nyumba, ….mnakaa kwenye nyumba ya maana mnasifika kule kijijini  kuwa mna nyumba nzuri, hamjui jinsi gani pesa zilivyopatikana….sio rahisi kihivyo..’akasema mama mdogo huku akiwa kashika kiuno.

‘Acha kutusimanga, hizo pesa hazikutoka kwako, zimetoka kwa mwanangu, hata hivyo…pesa zinatafutwa kwa njia nyingi za halali, zipo njia za heri, na watu wanafanikiwa, unafikiri wote wanaojenga wamepata pesa kwa njia mbaya mbaya kama hizo…, hiyo ni tabia yako, umejijengea mwenyewe tu,….usimpoteze mtoto wanguu kwa tabia hizo chafu,….’akasema mama Maua.

‘Tabia chafu eeh, sasa na ile nyumba imejengwa kwa mambo hayo, ya tabia chafu, ondokeni mle……kama kweli mna imani hiyo, kuanzia leo tokeni kwenye ile nyumba, mkajenge nyumba yenu kwa pesa za kubangaiza,….kwa biashara zenu za magengeni kama mtaweza…..nawaambieni ukweli nishukuruni sana, kwa kumuelimisha huyo bnti yenu, japokuwa bado hajaiva, …..’akamwangalia Maua.

‘Hivi mnaongea nini, maana mumejisahau kuwa mpo hospitalini na watu wanawasikiliza….mtafukuzwa hapa sasa hivi’akasema Maua.
Mama akageuka huku na kule kwa aibu, lakini mama mdogo, akanyesha mikono kwa kuzarau, akasema;

‘Mambo ya kijijini bwana….tumeongea nini cha ajbu, hayo ni mambo ya kawaida tu.’akageuka kuelekea barabarani, baada ya kusikia mngurumo wa gari likikaribia, na kusimama sehemu inayoegeshwa magari, lilikuwa gari la kifahari, akawa analiangalia kwa muda, halafu akageuka kumwangalia Maua.

‘Mambo yakienda shwari nataka uwe na gari kama lile…..kama utafuta ninavyotaka mimi, …lakini kama ukizubaa, nitaliwahi mimi, …..nitahakikisha nalipta gari kama hilo,….hilo liweke akilini…’akasema huku akishika kidevu.

‘Kwa pesa gani?’ akauliza mama Maua.

‘Kwa pesa gani,….pesa za urithi, huyo jamaa, kama keshakufa, ni lazima Maua apate sehemu yako, kwa ajili ya huyo mtoto……mtoto ana haki ya kurithi mali ya baba yake, na kwa vile bado hajazaliwa haki zote zinasimamiwa na mama yake,….pili nina mambo yake kibao ya siri, wakijifanya kuleta nyodo, nitawatishia…..lakini tatizo wewe bado ni mshamba…unamfuata huyo mama yako, …fuata ninavyokuagiza….kuanzia sasa, mambo yote nitayasimamia mimi..’akasema huku akipiga kifua.

‘Hivi wewe mama,….umesahau ulivyoniambia mwanzoni,.., wakati nilivyoitwa kuja kumuona huyo mgonjwa ulinielekeza nini na sasa unaongea nini?’ akauliza Maua.

‘Sijasahau…., ila kila kitu kwa mpangilio maalumu, ukifika huku unadai haki ya mtoto, ukienda kwa mzee, unambambikia mzigo….unapata huku na kule, dunia ndivyo inavyokwenda, wewe niachie huu mpira, tatizo lenu, mnaleta ….imani zenu za njaa, dini, dini…dini huku unakufa njaa,….dini iwekwe kwanza pembeni, ili upate masilahi, ukifanikiwa, eeh, sasa unaanza kutubu,….utazubaa wenzako wananyakua cha juu, unabakiwa na hasara…..’akatulia akiangalia lile gari, na kutikisa kichwa.

‘Maua hebu tuambie huyo mgonjwa anaendeleaje?’ akauliza mama Maua.

‘Mgonjwa, au marehemu……’akasema mama mdogo

‘Nani kasema ni Marehemu,….wewe mmama wewe, ni nani ni marehemu?’ akauliza Maua kwa kushangaa.

‘Huyu ndugu yangu kumbe ndivyo alivyo….ina maana nimemtupia mwanangu she..ta…ni. Hivi wewe ndugu yangu, unafikiri wewe utaishi milele….maana unakimbilia kuona  wenzake wamekufa,…eti wafe ili urithi, …utarithije kitu sio halali yako….kila mtu ni marehemu mtarajiwa’akasema mama Maua.

‘Kumbe mnajau hilo, ….kuwa kila mtu ni marehemu mtarajiwa….eehe,…..sasa kwanini mnilaumu, kila mtu ni marehemu mtarajiwa ehe, sawa kabisa,…, kwahiyo hata huyo mgonjwa, ni ishara kuwa anakaribia kufa, au keshakuwa marehemu, ….sisi, tunajongelea, kama ni hivyo, basi tusipoteze muda, tufaidi wakati bado upo’akasema na kuwaangalia mama Maua na Maua.

‘Mama hali ya Tajiri ni mbaya, …..nashindwa hata kusimulia, na sikuweza kuamini kuwa angeliweza hata kuongea na mimi kwa muda wote ule…..kanielezea mengi,….ambayo sikuwa nayajua, na nimegundua kuwa wanadamu wanaweza wakamchafua mtu akaonekana takataka,…..wakati sio, na wengine wakajipamba kwa shari jeupe, kumbe ndani wameoza….mama naogopa sana.’akasema Maua.

‘Acha mafumbo, elezea ulivyoulizwa….unaogopa nini, kama wana yao, sisi tutachukua hizo pesa, ili zisiendelee kukaa kwao, zije kwetu tuzitumie kwenye mambo masafi….unaona mambo yanavyokwenda….’akasema mama mdogo.

‘Ndio hivyo….., kwa ujumla Tajiri hali yake sio shwari, nimetolewa wakati …..kazidiwa na anashindwa hata kuhema, wakati naondoka walikuwa wakimuwekea vifaa vya kumsaidia….yeye mwenyewe aliniambia kuwa hataweza kumaliza siku ya leo..’akasema Maua kwa huzuni.

‘Unaona,…mimi ni mtabiri, haiwezekani mtu apigwe risasi, iingie ndani ya mwili, na bado apone, na mpigaji akiwa na lengo la kuua…..hapo anatapatapa tu, lakini sasa hivi utasikia,….’akasema huku akiangalia watu wakiingia kule kwenye wodi ya watu mahututi. Mama akamwangalia mwanae kwa huruma, halafu akasema;

‘Sasa mwanangu, hebu niwekwe wazi, maana huyu mama yako ananielezea mambo mengine ambayo hayaingii akilini,….mnataka nielewe vipi, maana mimi nimeshamvaa yule mzee, na kumdai kuwa kaniharibia binti yangu, sasa hapa tena nasikia mengine, mwanangu una wanaume wangapi,…..?’ akauliza mama Maua.

‘Mama naomba usimsikilize mama mdogo,…..yeye anaweza akamsingizia kila mwanaume kuwa ndiye aliyenipa mimba kama anaona huyo mwanaume ana pesa, inavyoonekana hii mimba ni kitega uchumi chake….naona hata aibu, …’akasema Maua na mama yake akamwangalia ndugu yake kwa jicho baya, halafu akamgeukia mwanae, na kumwangalia kwa macho ya huruma.

‘Mwanangu,….sijui hata nifanye nini, maana hii sasa ni aibu,….sijui nitaongeaje na huyo mzee, maana nilishahamaki, na kumtishia,….sasa kumbe tena oh,…lakini bado sijaelewa, kwani hamjaniweka wazi, …ni huyo mzee, au ni huyo mgonjwa, anayehusika na hiyo mimba….au kuna mwingine na hawa watu mnawasingizia kwa ajili ya kupata pesa?’ Akauliza tena mama Maua.

‘Mama……’kabla hajasema kitu, docta akatokea na wote wakatulia na kumwangalia huyo docta….Yule docta akawasogelea na kusema;

‘Nani anaitwa Maua?’ akauliza

‘Ni mimi docta….’akasema Maua na huku akimsogelea yule docta na mama yake akawa yupo nyuma yake, mama mdogo, akasita , akawa amesimama pale pale.

‘Mgonjwa anataka kuongea na Maua, ….na naomba msimuuliza maswali mengi, …acheni yeye aongee anachotaka kuongea, na …..’akawa anaongea huku akiondoka kuelekea huko kwenye chumba cha wagonjwa mahututi. Maua na mama yake wakamfuatilia nyuma.

‘Mama wewe usiende huko…., hayo hayakuhusu, usijiingize kwenye matatizo..’akasema Maua.

‘Mimi safari hii sikuachii, mimi na wewe kila mahali, na tukitoka hapa tunaondoka wote…hawa watu sio watu wema, watakutumbukiza kwenye shimo la giza….’akasema mama yake, na wakawa wameshaingia chumba hicho cha watu mahututi, wakavalishwa vile vifaa vya mdomoni.

‘Huyo mgonjwa anasema anataka kuongea na Maua,….wewe mama ungelibakia nje..’akasema dakitari mwingine waliyemkuta huko ndani.

‘Hapana ni lazima niwe karibu na mwanangu,…..’akasema mama Maua,. Na docta hakutaka kubishana naye zaidi, akawafungulia chumba maalumu alicholazwa huyo mgonjwa ,  wakaingia…..

*******

‘Maua umekuja na nani,…haya nikuambiayo ni mimi na wewe tu,… na utajua mwenyewe jinsi gani ya kuyafanyia kazi, sikutaka mtu mwingine aingilie kati, ni nani huyo uliyekuja naye?’ akauliza Tajiri bila hata ya kuwaangalia, ilikuwa ni ajabu kabisa, kwani huyo mgonjwa alikuwa kalala huku kaangalia juu, hakuwahi kugeuza kichwa wakatii wanaingia, lakini alijua kuwa Maua kafuatana na mtu mwingine.

‘Huyu ni mama yangu mzazi,….’akasema Maua.

‘Oh, mama yako mzazi,…yule ambaye tulitakiwa kwenda kwake kwa ajili ya kujitambulisha,…ndio amekuja,haya nitambue mama, lakini ndio hivyo tena…. bahati mbaya, maana sizani kama huo utambulisho una maana tena,…mungu mwenyewe ndiye ajuaye….ishara zote za kuondoka zimeshatimia….’akatulia na baadaye akageuza kichwa kwa shida.

‘Nawaomba msogee hapa karibu, huenda, na mama yako atafurahia kuyasikia haya nitakayokuambia, japokuwa nia na lengo langu ni kukuambia wewe mwenyewe,…lakini ….nijuavyo mama mzazi haweze kumtelekeza mwanae, kama kweli anajua uchungu wa uzazi, wanaofanya hivyo, ni kwa vile hawajui uchungu na thamani ya uzazi….’akatulia.

‘Mhh, sijui, kama….’akasema huku akijitahidi kumwangalia Mama Maua , halafu akasema;

‘Mama yako Maua…sura yake sio ngeni kwangu,…na sijui, kama ni niliwahi kumuona kabla, sina uhakika na hilo, …..na sio wewe niliyekutana nawe siku ile….nakumbuka hilo, ooh, siku ile nilihangaika sana nikutane na wewe nilijaribu kukufuatilia lakini sikukuwahi….na sasa upo mbele yangu, …lakini macho hayana nguvu tena ya kukutambua vyema, naona giza giza…., kilichobakia kwangu ni macho ya moyoni, ambayo yanaona mambo ya ughaibuni…’akatulia.

‘Hebu niambie wewe ni nani, na je uliwahi kukutana na mimi kabla?’ akauliza huku akijaribu kumwangalia mama Maua. Mama Maua akakumbuka walivyoambia wa na docta kuwa wasiongee chochote, wamuache mgonjwa aongee mwenyewe, ili wasimpe wakati mgumu wa kufikiria;

‘Najua huwezi kukumbuka, lakini…akili na moyo wangu unanielezea kuwa wewe niliwahi kukuta na wewe, sura yako sio ngeni….’akatulia na akawa kama anatikisika ….

‘Msimuulize swali au kumfanya awaze jambo jingine, ana maneno yake anataka kuongea, na hahitjiki kuwaza mengine zaidi…’wakakumbuka docta alivyowaambia.

‘Usijali kuhusu mimi, wewe ongea hilo ulilomuitia Maua’akasema mama Maua.

‘Oh, naanza hata kusahau niliyotaka kumwambia Maua….oh, Maua, nakumbuka nilikuahidi kuwa nitakuambia ni nani aliyekupa huo uja uzito….’akasema na kutulia kwa muda, hadi Maua na mama yake wakahisi huenda huyo mgonjwa hataongea tena.

*******

‘Rejea siku ile ya tukio…..’mara sauti ikasikika, ilikuwa sauti ya shida,, lakini kila hatua ile sauti ikawa inaongezeka na kuwa na uhai , kama vile mtu anayeongeza sauti kwenye redio.

‘Mimi nilikuwa nimeshalewa kupitiliza,….maana nilishindwa kufanya kile nilichokuwa nikikitamani siku nyingi….Maua ulikuwa umeuteka moyo wangu, nilikuwa kila mara nikikuwaza wewe….natamani niruke kutoka Arusha hadi Dar,… tangu siku ile niliyokuona awali ulikuja kuwa sehemu ya akili yangu…

‘Maua sio siri, katika maisha yangu, niliwahi kumpenda mtu mmoja tu…mambo ya ujanani tena, ambaye nilikuja kutengwanishwa naye, kwasababu ya mambo ya kizamani, nikakimbilia huku machimboni kutafuta mali, na yeye sijui alikimbilia wapi, lakini nilisikia alipotolea msituni…..basi tena, huko alipo mungu amlinde….

Maua akageuka kumwangali mama yake, na mama yake alikuwa kakodoa macho kumwangalia huyo mgonjwa,…hakuna aliyesema neno, wote wakabakia kusikiliza …..

`Huyo msichana, kipindi hiicho, …ndiye aliyewahi kuuteka moyo, wangu, na cha ajabu, yale niliyokuwa nikiyasikia, kwa huyo aliyewahi kuuteka moyo wangu, yalikuja kutokezea kwako, ….ajabu kabisa, kwa umri niliokuwa nao, kuja kupata kisebu sebu cha mapenzi, kwa binti mdogo, kama wewe….ni aibu, lakini ndivyo ilivyokuwa…’akatulia.

‘Lakini huo ndio ukweli,siwezi kukuficha kwa sasa..maana sina cha kukudanganya, …ukweli ni huo, na nilijaribu kila mbinu za kukuvuta karibu, ili uweza kuyafahamu hayo….kuwa mimi nilikuhitajia sana, na niliapa kuwa ni lazima wewe uje kuwa mke wangu…., lakini kila hatua ilikuwa na vikwazao,..na ndipo nikaongea na mama yako mdogo, akanipa mbinu..

‘Mama yako mdogo…sizani kama anakuthamini kama mwanae,..naomba anisamehe kwa hilo, sina nia mbaya ya kuwachinganisha…, na kama angelikuwepo hapa ningelisema haya haya, na nilishamwambia hivyo..kuwa alichokuwa akikufanyia wewe sio halali…najuta kuwa na mimi tamaa zangu za kimwili,…zilinizidi, japokuwa sikufanikiwa,..’akatulia.

`Maua, siku ile, nilijiandaa kweli kweli…na yaliyofanywa na mama yako mdogo, sikuwa nimeyafahamu, ila nilichokuja kushuhudia na pale ulipozidiwa, ….nayajua hayo madawa, nisikufiche, hayo madawa ukiyanywa, unakuwa na akili tofauti na akili zako za kawaida, utajikuta unafanya mambo ambayo huwezi kuyafanya ukiwa na akili zako….

‘Ulianza kufanya mambo ambayo…ooh, sikuamini , na mimi kwa vile ndivyo nilivyokuwa nikitaka, nikawa nimezidiwa…..na kama ilivyopangwa,ukapelekwa chumbani….nayaongea haya ili mama yako ayasikie, ili ajue kuwa binti yake, hakufanya makusudi, ili wasije wakakudanganya,……’akatulia.

‘Binti yako, alikuwa mwali….sijui….kwani mimi sikuweza kufanya hilo nililokuwa nimekusudia….ila ilibidi nidanganye, ili kuficha ila aibu niliyoipata….najua aliyenifanyia hivyo, ambaye ndiye kaniwahi ….lakini na yeye atanifuata tu,….nahisi hivyo’akatulia.

‘Mama binti yako, hakuwa Malaya , kama wanavyodai wengine…mimi na wenzangu ndio tuliomtumbukiza kwenye lindi la mtihani huo….na siku hiyo, ilitakiwa mimi nikutane naye, ili ….oh, unajua mama kuna mambo ya kishirikiana katika biashara zetu, na mimi nilitakiwa kila mara kukutana na binti…mwali….lakini kama Malikia hakupenda, sikuweza kutimiza hayo…na safari hiyo ya Dar, aliipinga sana, ….’akatulia huku akijaribu kumwangalia mama Maua.

‘Nakumbuka siku naondoka, aliniambia wazi wazi, kuwa sitafanikiwa hayo niliyoyapanga, na kama ni mambo ya zindiko,….hilo hakulirizia, na halitafanikiwa……nitaishia kuumbuka..na kweli niliumbuka, sikufanikiwa,…..nikaishia kulewa, nikalala fofofo…..nilipozindukana nilikuwa wameshafanya mambo yao, wakaniambia mambo tayari, …sikupenda kuwauliza zaidi, kwani nilikuwa nimetahayari…..

‘Sasa ni nani aliyewahi kufanya yale niliyoyakusudia?’ akauliza huku akiangalia juu.

‘Katika mambo haya ya kiimani za kimila, kuna kitu kinaitwa zindiko,….lakini mambo hayo, ….yalikuwa mageni kwangu, …na zaidi ya zindiko, mimi nitayaita mambo ya kishetani’akakohoa, halafu akasema.

‘Mwanzoni nilikuwa na shauku sana, kwahiyo sikujali,….nilikubali kila kitu, na ilikuwa kama mchezo wa kuigiza, nikajikuta nimeingia na kutimiza karibu kila kitu,…lakini siku zilivyozidi kwenda, moyo wa kibinadamu ukaanza kunisuta, nikawa silali, mawazo, na hata ndoto za kutisha zilianza kuniandama,…’akakohoa tena.

'Ilibidi kila mara kufanyike kitu kinachoitwa Zindiko, na siku ile, ndio ilikuwa siku ya kufanikisha hilo, japokuwa Malikia alipinga , alipinga kwa vile alishanihisi vibaya, na alitaka kila kukifanyika hilo jambo, awepo, ili nisiende zaidi ya ….siwezi kuyaelezea hapo, ni mambo yao, na naona muelewe hivyo….kwani yanatisha,…sijui kwanini wanadamu tunajipeleka huko….’akakohoa tena.

`Kwahiyo kwa makubaliano ya wanachama wengine, wahusika wakuu, ikapita kuwa hilo jambo lifanyike huko Dar , kwani nilishawahakikishia kuwa nimempata mwanawali, ambaye nilithibitishiwa na mama yake mdogo kuwa ni mwali kweli….na moyoni nilishaingiwa na tamaa naye, ninaweza kusema, nilishampenda mwanao, samhani sana mama….mama Maua.’akakohoa tena.

‘Maua haya nayasema yanatoka moyoni mwangu,…unielewe hivyo, na unisamehe, sikuwa na jinsi, kwa hali niliyokuwa nayo, na mazingira mazima yaliyovyokuwa,mama na wewe unisamehe kwa hilo, kwani sisi wanadamu ni wepesi sana kudanganyika na mbinu za ibilisi, na hasa inapohusu jambo la mali, utajiri….’akatulia halafu akasema.

‘Safari ikapangwa, ikabidi tufike kwa siri Dar, na kila mmoja aliingia Dar kwa siri kwa namna yake….na wahusika wakuu waote walikuwepo, kasoro Malikia tu…’akakohoa mfulululizo, na baadaye akatulia.

‘Zindiko lilitakiwa kufanyika,…na waliotakiwa kulifanikisha hilo ni wale waliokabidhiwa huo mkoba….nikimaanisha mimi, au mjomba au mkewe, na ukumbuke mjomba keshajitenga,  mambo ya kishirikina, yaliyochukuliwa kwa mganga, na mganga aliyakabidhi mambo hayo kwa mjomba wangu, ambaye alikuja kunikabidhi huo mkoba na huyo mganga keshapotea, na hakuna wa kubadili lolote…kwahiyo ili lifanikiwe hilo zindiko, mimi nahitajika….

Ukumbuke kuwa Mjomba keshaniachia kila kitu, mkewe keshaondolea kwenye kikundi, kwahiyo, mzigo mzima uliangukia kwangu, na wote wakawa wananiangalia mimi, na nisipofanya hilo kuna mambo yanakwama, biashara, kupata madini, ni imani za kishetani, lakini gharama yake ni kubwa kuliko watu wanavyozania, zinaumiza , zinatesa, na zinahusisha watu wasistahili, kwa maslahi ya watu wengine…

‘Mimi siku hiyo, nilikuwa sijisikii vyema, hata hivyo ilibidi niwajibike, na kwa vile nilishakupenda Maua nikaona hiyo ni nafasi yangu kubwa sana, ….nikasahau kuwa malikia alikuwa na nguvu zake za giza, …..msimuone vile, yule mwanamke ni kiboko wa mambo hayo….yeye alisema kama hakuna mwanawali, tufanye njia nyingine, ambayo ni ya kumwaga damu….ikiwa na maana kuua….’akatulia

‘Siku ile alinifanya vibaya, akasahau kuwa hayo niliyotakiwa kuyafanikisha sio kwa ajili yangu tu, ilikuwa kwa ajili ya kundi zima, na kwa manufaa ya mambo yetu ya kupata madini…..akaweka ubinafsi wake mbele…ushetani ndani ya ushetani…

`Sijui mnanielewa hapo?’ akawa kama anauliza.

‘Kama hamnielewi basi ndivyo hivyo….. hivyo ndivyo ilivyokuwa….imani za kishirikina zimeshika kasi sana…’akatulia,

‘Tena wasomi, wakubwa, matajiri, wakuu wa dini ndio wanazo sana….lakini kwa kujificha…’akatulia.

`Siku ile mambo ya zindiko yalitakiwa kufanyika, na wahusika waliyashapanga vitu vyao….na kazi ikabakia kwangu, lakini nikashindwa, na washirika, wakawa wakiniuliza kila mara kuwa tayari, ile wachukue ile damu….damu inayotoka kwa mwanawali, ambaye hajawahi kukutana na mwanaume…..natumai hapo mnanielewa…

‘Kama isingelifanikiwa siku hiyo, kuna mambo yalitakiwa yafanyike,…damu ya mtu ingelitakiwa ichukue nafasi yake….na hilo nilishaanza kuliogopa,…hayo siwezi kuyaongelea zaidi maana yanatisha, ….maana kwa hayo, napata taabu sana nikiyawazia…..jamani kuua ni laana, mimi hapa nilipo naona shida, Napata mteso, damu za watu zinaniandama….najuta najuta…..’akawa anongea hivyo huku akionyesha kusikia maumivu makali.

‘Ogopeni sana kuua, damu za watu zinatesa, wote niliowaua kila mara wananijia na kudai haki yao, wananitesa,..kila nikipoteza fahamu Napata mateso makali sana….ogoeni sana kuua ….hivi sasa nateseka, nateseka….sana sana….naomba roho itoke haraka, nikakuate na huo moto, maana sina ..sijui kama nitaweza kusamehewa’akawa analalamika maumivu…akaanza kukohoa kwa mfulululizo.

‘Maua…naona muda umefika,…ila ili ujue ni nani alifanya hayo niliyoyashindwa…ooh, nenda kamuone dakitari wa mjomba….huenda, nahisi hivyo, kwa vile yeye kumbe anajua mengi ya hayo, na …nilikuja kugundua hayo jana tu, alipokuja kuniomba huo mkoba, sikuamini….’akatulia.

Na nikikumbuka siku ile, ….nilipozidiwa na pombe, nilisikia wenzangu wakisema …muiteni docta, sikujua ni docta gani huyo…..ooh, sasa, naanza kuelewa, ….lakini siwezi kuelezea zaidi, muda naona umefika, kwaherini…..’akaanza kutikiswa kwa nguvu, na baadaye akaanza kukoroma, ….akatulia,…..na yale mashine ya kuonyesha mapigo ya moyo yakawa kama yanaanza kunyooka, lakini ghafla, yakajirudi.

‘Oh,…naona kuna kitu, …..nimeota…..mungu nisamehe, ..ooh, eti nini, hapana..haiwezekani, ina maana ni damu yangu, haiwezekani,..oh, Maua ina maana wewe ni ni….oh, oh, oh, kamuone docta atakuelezea,  ….’akaanza kutikiswa kwa nguvu,hadi kitanda kizima kikawa kinatetemeka.

Mara Docta anayemuhudumia akaingia kwa haraka na kuwaambia akina Maua na mama yake watoke nje,…. na wakaingia madakitari wengine, kusaidia....

Maua akawa anasita kuondoka….mama yake akawa anamvuta mkono…..na Maua akatupa macho kwenye yale mashine ya kuangalia mapigo ya moyo,….mishale ilishaanza kunyooka, na mara mlio wa ishara ya hatari ikaanza kulia.

Yule docta akachukua vifaa vya kushinikiza mapigo ya moyo na kukiweka kifuani, na mwili wa Tajiri, ukaruka juu, …alifanya hivyo tena, lakini haikusaidia kitu, ….akaviweka pembeni, akchukua vifaa vyake, akasikilizia masikioni,….akawageukiwa wengine, na hakusema neno, akavua vile vifaa alivyokuwa navyo masikioni...na wenzake wakaanza kuondoa vifaa kutoka kwa yule mgonjwa.

Yule docta, akageuka kuondoka na alipofika mlangoni, ...,akawaona Maua na mama yake, wakiwa wanavutana kuondoka, mama akimvuta binti yake, na binti yake, akiwa kama kaganda,…

‘Oh, nyie bado mpo?’ akauliza

‘Ina maakeshafariki..?’ akauliza Maua huku machozi yakiwa yameshaanza kumtoka.

‘Nasikistika kusema kuwa ndio hivyo….lakini, nawaombeni msubiri nje, kama ni kweli nitawaambie, ngojeni niwaite waenzangu kwanza, huenda kuna ujuzi wa ziada….’akasema huku akiandika kitu kwenye cheti chake na alipohakikisha kuwa hawo akina mama wameondoka, akachukua shuka jeupa na kuufunika ule mwili, …

NB:Amini usiamini, dunia hii imejaa mambo ya ajabu, ushirikiana sasa hivi umekita kwenye mioyo ya watu, wakubwa kwa wadogo,...hadi kwa viongozi wa dini ambao tulikuwa tunawategemea, ...na hata wasomi, ambao tulijua kuwa watasaidia ....sijui huko tunapokwenda kama imani za dini zenyewe zinapigwa vita…

WAZO LA LEO: Dhambi ya kuua ni kubwa sana, na ukiua, usizanie kuwa unaweza ukaifukia ile damu kwa mguu, ukasema oooh, hawatanijua, nimeokoka…damu ile itakuandama mpaka kufa kwako.Tuepuke dhambi hiyo, na ili kufanikiwa kwa hilo, ni wote kupendana, tuondoe chuki, …chuki ni tabia ya ibilisi,….ni vyema tukusaidiana…tukashirikiana,  na haki ya kila mtu ikaheshimiwa.


Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

This is mу firѕt time рay
a νisіt at hегe and i am rеally ρleаssant to rеad all
at sіngle ρlаce.

Μy blog post :: instant payday loans
my web site :: instant payday loans