Maua alitoka nje , na kule nje aliwaona mama yake akiongea
na mama mdogo, walionekana hawaelewani kuhusu jambo fulani, na walipomuona Maua
wakakatisha yale mazungumzo yao, na kujifanya hakuna kilichokuwa kikiendelea
kati yao, wakamsogelea Maua. Wakwanza kuongea alikuwa ni mama mdogo akasema;
‘Ehe tuambie, amewahi kukuandikia chochote, au kukuelekeza
wapi pa kupatia pesa?’ akauliza mama mdogo, na mama Maua akashika mdomo akionyesha
kushangaa kwa kauli hiyo, akamwangalai ndugu yake huku akiwa kamtolea macho
akasema;
‘Hivi ndivyo unavyoishi na mwanangu hivyo…..?’ akauliza mama
yake Maua akimwangalia huyo mama mdogo sasa kwa hasira.
‘Kama nisingelimfudisha jinsi gani ya kuishi unafikiri
mngeliweza kuijenga ile nyumba, ….mnakaa kwenye nyumba ya maana mnasifika kule
kijijini kuwa mna nyumba nzuri, hamjui
jinsi gani pesa zilivyopatikana….sio rahisi kihivyo..’akasema mama mdogo huku
akiwa kashika kiuno.
‘Acha kutusimanga, hizo pesa hazikutoka kwako, zimetoka kwa
mwanangu, hata hivyo…pesa zinatafutwa kwa njia nyingi za halali, zipo njia za
heri, na watu wanafanikiwa, unafikiri wote wanaojenga wamepata pesa kwa njia mbaya
mbaya kama hizo…, hiyo ni tabia yako, umejijengea mwenyewe tu,….usimpoteze mtoto
wanguu kwa tabia hizo chafu,….’akasema mama Maua.
‘Tabia chafu eeh, sasa na ile nyumba imejengwa kwa mambo
hayo, ya tabia chafu, ondokeni mle……kama kweli mna imani hiyo, kuanzia leo
tokeni kwenye ile nyumba, mkajenge nyumba yenu kwa pesa za kubangaiza,….kwa biashara
zenu za magengeni kama mtaweza…..nawaambieni ukweli nishukuruni sana, kwa
kumuelimisha huyo bnti yenu, japokuwa bado hajaiva, …..’akamwangalia Maua.
‘Hivi mnaongea nini, maana mumejisahau kuwa mpo hospitalini
na watu wanawasikiliza….mtafukuzwa hapa sasa hivi’akasema Maua.
Mama akageuka huku na kule kwa aibu, lakini mama mdogo,
akanyesha mikono kwa kuzarau, akasema;
‘Mambo ya kijijini bwana….tumeongea nini cha ajbu, hayo ni
mambo ya kawaida tu.’akageuka kuelekea barabarani, baada ya kusikia mngurumo wa
gari likikaribia, na kusimama sehemu inayoegeshwa magari, lilikuwa gari la
kifahari, akawa analiangalia kwa muda, halafu akageuka kumwangalia Maua.
‘Mambo yakienda shwari nataka uwe na gari kama lile…..kama
utafuta ninavyotaka mimi, …lakini kama ukizubaa, nitaliwahi mimi, …..nitahakikisha
nalipta gari kama hilo,….hilo liweke akilini…’akasema huku akishika kidevu.
‘Kwa pesa gani?’ akauliza mama Maua.
‘Kwa pesa gani,….pesa za urithi, huyo jamaa, kama keshakufa,
ni lazima Maua apate sehemu yako, kwa ajili ya huyo mtoto……mtoto ana haki ya
kurithi mali ya baba yake, na kwa vile bado hajazaliwa haki zote zinasimamiwa
na mama yake,….pili nina mambo yake kibao ya siri, wakijifanya kuleta nyodo,
nitawatishia…..lakini tatizo wewe bado ni mshamba…unamfuata huyo mama yako, …fuata
ninavyokuagiza….kuanzia sasa, mambo yote nitayasimamia mimi..’akasema huku
akipiga kifua.
‘Hivi wewe mama,….umesahau ulivyoniambia mwanzoni,.., wakati
nilivyoitwa kuja kumuona huyo mgonjwa ulinielekeza nini na sasa unaongea nini?’
akauliza Maua.
‘Sijasahau…., ila kila kitu kwa mpangilio maalumu, ukifika
huku unadai haki ya mtoto, ukienda kwa mzee, unambambikia mzigo….unapata huku
na kule, dunia ndivyo inavyokwenda, wewe niachie huu mpira, tatizo lenu,
mnaleta ….imani zenu za njaa, dini, dini…dini huku unakufa njaa,….dini iwekwe
kwanza pembeni, ili upate masilahi, ukifanikiwa, eeh, sasa unaanza kutubu,….utazubaa
wenzako wananyakua cha juu, unabakiwa na hasara…..’akatulia akiangalia lile
gari, na kutikisa kichwa.
‘Maua hebu tuambie huyo mgonjwa anaendeleaje?’ akauliza mama
Maua.
‘Mgonjwa, au marehemu……’akasema mama mdogo
‘Nani kasema ni Marehemu,….wewe mmama wewe, ni nani ni
marehemu?’ akauliza Maua kwa kushangaa.
‘Huyu ndugu yangu kumbe ndivyo alivyo….ina maana nimemtupia
mwanangu she..ta…ni. Hivi wewe ndugu yangu, unafikiri wewe utaishi milele….maana
unakimbilia kuona wenzake wamekufa,…eti
wafe ili urithi, …utarithije kitu sio halali yako….kila mtu ni marehemu
mtarajiwa’akasema mama Maua.
‘Kumbe mnajau hilo, ….kuwa kila mtu ni marehemu mtarajiwa….eehe,…..sasa
kwanini mnilaumu, kila mtu ni marehemu mtarajiwa ehe, sawa kabisa,…, kwahiyo
hata huyo mgonjwa, ni ishara kuwa anakaribia kufa, au keshakuwa marehemu,
….sisi, tunajongelea, kama ni hivyo, basi tusipoteze muda, tufaidi wakati bado
upo’akasema na kuwaangalia mama Maua na Maua.
‘Mama hali ya Tajiri ni mbaya, …..nashindwa hata kusimulia,
na sikuweza kuamini kuwa angeliweza hata kuongea na mimi kwa muda wote
ule…..kanielezea mengi,….ambayo sikuwa nayajua, na nimegundua kuwa wanadamu
wanaweza wakamchafua mtu akaonekana takataka,…..wakati sio, na wengine
wakajipamba kwa shari jeupe, kumbe ndani wameoza….mama naogopa sana.’akasema
Maua.
‘Acha mafumbo, elezea ulivyoulizwa….unaogopa nini, kama wana
yao, sisi tutachukua hizo pesa, ili zisiendelee kukaa kwao, zije kwetu
tuzitumie kwenye mambo masafi….unaona mambo yanavyokwenda….’akasema mama mdogo.
‘Ndio hivyo….., kwa ujumla Tajiri hali yake sio shwari,
nimetolewa wakati …..kazidiwa na anashindwa hata kuhema, wakati naondoka
walikuwa wakimuwekea vifaa vya kumsaidia….yeye mwenyewe aliniambia kuwa hataweza
kumaliza siku ya leo..’akasema Maua kwa huzuni.
‘Unaona,…mimi ni mtabiri, haiwezekani mtu apigwe risasi,
iingie ndani ya mwili, na bado apone, na mpigaji akiwa na lengo la kuua…..hapo
anatapatapa tu, lakini sasa hivi utasikia,….’akasema huku akiangalia watu
wakiingia kule kwenye wodi ya watu mahututi. Mama akamwangalia mwanae kwa
huruma, halafu akasema;
‘Sasa mwanangu, hebu niwekwe wazi, maana huyu mama yako
ananielezea mambo mengine ambayo hayaingii akilini,….mnataka nielewe vipi,
maana mimi nimeshamvaa yule mzee, na kumdai kuwa kaniharibia binti yangu, sasa
hapa tena nasikia mengine, mwanangu una wanaume wangapi,…..?’ akauliza mama
Maua.
‘Mama naomba usimsikilize mama mdogo,…..yeye anaweza
akamsingizia kila mwanaume kuwa ndiye aliyenipa mimba kama anaona huyo mwanaume
ana pesa, inavyoonekana hii mimba ni kitega uchumi chake….naona hata aibu,
…’akasema Maua na mama yake akamwangalia ndugu yake kwa jicho baya, halafu
akamgeukia mwanae, na kumwangalia kwa macho ya huruma.
‘Mwanangu,….sijui hata nifanye nini, maana hii sasa ni
aibu,….sijui nitaongeaje na huyo mzee, maana nilishahamaki, na kumtishia,….sasa
kumbe tena oh,…lakini bado sijaelewa, kwani hamjaniweka wazi, …ni huyo mzee, au
ni huyo mgonjwa, anayehusika na hiyo mimba….au kuna mwingine na hawa watu
mnawasingizia kwa ajili ya kupata pesa?’ Akauliza tena mama Maua.
‘Mama……’kabla hajasema kitu, docta akatokea na wote
wakatulia na kumwangalia huyo docta….Yule docta akawasogelea na kusema;
‘Nani anaitwa Maua?’ akauliza
‘Ni mimi docta….’akasema Maua na huku akimsogelea yule docta
na mama yake akawa yupo nyuma yake, mama mdogo, akasita , akawa amesimama pale
pale.
‘Mgonjwa anataka kuongea na Maua, ….na naomba msimuuliza
maswali mengi, …acheni yeye aongee anachotaka kuongea, na …..’akawa anaongea
huku akiondoka kuelekea huko kwenye chumba cha wagonjwa mahututi. Maua na mama
yake wakamfuatilia nyuma.
‘Mama wewe usiende huko…., hayo hayakuhusu, usijiingize
kwenye matatizo..’akasema Maua.
‘Mimi safari hii sikuachii, mimi na wewe kila mahali, na
tukitoka hapa tunaondoka wote…hawa watu sio watu wema, watakutumbukiza kwenye
shimo la giza….’akasema mama yake, na wakawa wameshaingia chumba hicho cha watu
mahututi, wakavalishwa vile vifaa vya mdomoni.
‘Huyo mgonjwa anasema anataka kuongea na Maua,….wewe mama
ungelibakia nje..’akasema dakitari mwingine waliyemkuta huko ndani.
‘Hapana ni lazima niwe karibu na mwanangu,…..’akasema mama
Maua,. Na docta hakutaka kubishana naye zaidi, akawafungulia chumba maalumu
alicholazwa huyo mgonjwa , wakaingia…..
*******
‘Maua umekuja na nani,…haya nikuambiayo ni mimi na wewe tu,…
na utajua mwenyewe jinsi gani ya kuyafanyia kazi, sikutaka mtu mwingine
aingilie kati, ni nani huyo uliyekuja naye?’ akauliza Tajiri bila hata ya
kuwaangalia, ilikuwa ni ajabu kabisa, kwani huyo mgonjwa alikuwa kalala huku
kaangalia juu, hakuwahi kugeuza kichwa wakatii wanaingia, lakini alijua kuwa
Maua kafuatana na mtu mwingine.
‘Huyu ni mama yangu mzazi,….’akasema Maua.
‘Oh, mama yako mzazi,…yule ambaye tulitakiwa kwenda kwake
kwa ajili ya kujitambulisha,…ndio amekuja,haya nitambue mama, lakini ndio hivyo
tena…. bahati mbaya, maana sizani kama huo utambulisho una maana tena,…mungu
mwenyewe ndiye ajuaye….ishara zote za kuondoka zimeshatimia….’akatulia na
baadaye akageuza kichwa kwa shida.
‘Nawaomba msogee hapa karibu, huenda, na mama yako
atafurahia kuyasikia haya nitakayokuambia, japokuwa nia na lengo langu ni
kukuambia wewe mwenyewe,…lakini ….nijuavyo mama mzazi haweze kumtelekeza mwanae,
kama kweli anajua uchungu wa uzazi, wanaofanya hivyo, ni kwa vile hawajui
uchungu na thamani ya uzazi….’akatulia.
‘Mhh, sijui, kama….’akasema huku akijitahidi kumwangalia
Mama Maua , halafu akasema;
‘Mama yako Maua…sura yake sio ngeni kwangu,…na sijui, kama
ni niliwahi kumuona kabla, sina uhakika na hilo, …..na sio wewe niliyekutana
nawe siku ile….nakumbuka hilo, ooh, siku ile nilihangaika sana nikutane na wewe
nilijaribu kukufuatilia lakini sikukuwahi….na sasa upo mbele yangu, …lakini
macho hayana nguvu tena ya kukutambua vyema, naona giza giza…., kilichobakia
kwangu ni macho ya moyoni, ambayo yanaona mambo ya ughaibuni…’akatulia.
‘Hebu niambie wewe ni nani, na je uliwahi kukutana na mimi
kabla?’ akauliza huku akijaribu kumwangalia mama Maua. Mama Maua akakumbuka
walivyoambia wa na docta kuwa wasiongee chochote, wamuache mgonjwa aongee
mwenyewe, ili wasimpe wakati mgumu wa kufikiria;
‘Najua huwezi kukumbuka, lakini…akili na moyo wangu
unanielezea kuwa wewe niliwahi kukuta na wewe, sura yako sio ngeni….’akatulia
na akawa kama anatikisika ….
‘Msimuulize swali au
kumfanya awaze jambo jingine, ana maneno yake anataka kuongea, na hahitjiki
kuwaza mengine zaidi…’wakakumbuka docta alivyowaambia.
‘Usijali kuhusu mimi, wewe ongea hilo ulilomuitia Maua’akasema
mama Maua.
‘Oh, naanza hata kusahau niliyotaka kumwambia Maua….oh,
Maua, nakumbuka nilikuahidi kuwa nitakuambia ni nani aliyekupa huo uja
uzito….’akasema na kutulia kwa muda, hadi Maua na mama yake wakahisi huenda
huyo mgonjwa hataongea tena.
*******
‘Rejea siku ile ya tukio…..’mara sauti ikasikika, ilikuwa
sauti ya shida,, lakini kila hatua ile sauti ikawa inaongezeka na kuwa na uhai
, kama vile mtu anayeongeza sauti kwenye redio.
‘Mimi nilikuwa nimeshalewa kupitiliza,….maana nilishindwa
kufanya kile nilichokuwa nikikitamani siku nyingi….Maua ulikuwa umeuteka moyo
wangu, nilikuwa kila mara nikikuwaza wewe….natamani niruke kutoka Arusha hadi
Dar,… tangu siku ile niliyokuona awali ulikuja kuwa sehemu ya akili yangu…
‘Maua sio siri, katika maisha yangu, niliwahi kumpenda mtu
mmoja tu…mambo ya ujanani tena, ambaye nilikuja kutengwanishwa naye, kwasababu
ya mambo ya kizamani, nikakimbilia huku machimboni kutafuta mali, na yeye sijui
alikimbilia wapi, lakini nilisikia alipotolea msituni…..basi tena, huko alipo
mungu amlinde….
Maua akageuka kumwangali mama yake, na mama yake alikuwa
kakodoa macho kumwangalia huyo mgonjwa,…hakuna aliyesema neno, wote wakabakia
kusikiliza …..
`Huyo msichana, kipindi hiicho, …ndiye aliyewahi kuuteka
moyo, wangu, na cha ajabu, yale niliyokuwa nikiyasikia, kwa huyo aliyewahi
kuuteka moyo wangu, yalikuja kutokezea kwako, ….ajabu kabisa, kwa umri
niliokuwa nao, kuja kupata kisebu sebu cha mapenzi, kwa binti mdogo, kama wewe….ni
aibu, lakini ndivyo ilivyokuwa…’akatulia.
‘Lakini huo ndio ukweli,siwezi kukuficha kwa sasa..maana
sina cha kukudanganya, …ukweli ni huo, na nilijaribu kila mbinu za kukuvuta
karibu, ili uweza kuyafahamu hayo….kuwa mimi nilikuhitajia sana, na niliapa
kuwa ni lazima wewe uje kuwa mke wangu…., lakini kila hatua ilikuwa na
vikwazao,..na ndipo nikaongea na mama yako mdogo, akanipa mbinu..
‘Mama yako mdogo…sizani kama anakuthamini kama
mwanae,..naomba anisamehe kwa hilo, sina nia mbaya ya kuwachinganisha…, na kama
angelikuwepo hapa ningelisema haya haya, na nilishamwambia hivyo..kuwa
alichokuwa akikufanyia wewe sio halali…najuta kuwa na mimi tamaa zangu za
kimwili,…zilinizidi, japokuwa sikufanikiwa,..’akatulia.
`Maua, siku ile, nilijiandaa kweli kweli…na yaliyofanywa na
mama yako mdogo, sikuwa nimeyafahamu, ila nilichokuja kushuhudia na pale
ulipozidiwa, ….nayajua hayo madawa, nisikufiche, hayo madawa ukiyanywa, unakuwa
na akili tofauti na akili zako za kawaida, utajikuta unafanya mambo ambayo
huwezi kuyafanya ukiwa na akili zako….
‘Ulianza kufanya mambo ambayo…ooh, sikuamini , na mimi kwa
vile ndivyo nilivyokuwa nikitaka, nikawa nimezidiwa…..na kama
ilivyopangwa,ukapelekwa chumbani….nayaongea haya ili mama yako ayasikie, ili
ajue kuwa binti yake, hakufanya makusudi, ili wasije
wakakudanganya,……’akatulia.
‘Binti yako, alikuwa mwali….sijui….kwani mimi sikuweza
kufanya hilo nililokuwa nimekusudia….ila ilibidi nidanganye, ili kuficha ila
aibu niliyoipata….najua aliyenifanyia hivyo, ambaye ndiye kaniwahi ….lakini na
yeye atanifuata tu,….nahisi hivyo’akatulia.
‘Mama binti yako, hakuwa Malaya , kama wanavyodai
wengine…mimi na wenzangu ndio tuliomtumbukiza kwenye lindi la mtihani huo….na
siku hiyo, ilitakiwa mimi nikutane naye, ili ….oh, unajua mama kuna mambo ya
kishirikiana katika biashara zetu, na mimi nilitakiwa kila mara kukutana na
binti…mwali….lakini kama Malikia hakupenda, sikuweza kutimiza hayo…na safari
hiyo ya Dar, aliipinga sana, ….’akatulia huku akijaribu kumwangalia mama Maua.
‘Nakumbuka siku naondoka, aliniambia wazi wazi, kuwa
sitafanikiwa hayo niliyoyapanga, na kama ni mambo ya zindiko,….hilo hakulirizia,
na halitafanikiwa……nitaishia kuumbuka..na kweli niliumbuka,
sikufanikiwa,…..nikaishia kulewa, nikalala fofofo…..nilipozindukana nilikuwa
wameshafanya mambo yao, wakaniambia mambo tayari, …sikupenda kuwauliza zaidi,
kwani nilikuwa nimetahayari…..
‘Sasa ni nani aliyewahi kufanya yale niliyoyakusudia?’
akauliza huku akiangalia juu.
‘Katika mambo haya ya kiimani za kimila, kuna kitu kinaitwa
zindiko,….lakini mambo hayo, ….yalikuwa mageni kwangu, …na zaidi ya zindiko,
mimi nitayaita mambo ya kishetani’akakohoa, halafu akasema.
‘Mwanzoni nilikuwa na shauku sana, kwahiyo sikujali,….nilikubali
kila kitu, na ilikuwa kama mchezo wa kuigiza, nikajikuta nimeingia na kutimiza
karibu kila kitu,…lakini siku zilivyozidi kwenda, moyo wa kibinadamu ukaanza
kunisuta, nikawa silali, mawazo, na hata ndoto za kutisha zilianza kuniandama,…’akakohoa
tena.
'Ilibidi kila mara kufanyike kitu kinachoitwa Zindiko, na
siku ile, ndio ilikuwa siku ya kufanikisha hilo, japokuwa Malikia alipinga ,
alipinga kwa vile alishanihisi vibaya, na alitaka kila kukifanyika hilo jambo,
awepo, ili nisiende zaidi ya ….siwezi kuyaelezea hapo, ni mambo yao, na naona
muelewe hivyo….kwani yanatisha,…sijui kwanini wanadamu tunajipeleka huko….’akakohoa
tena.
`Kwahiyo kwa makubaliano ya wanachama wengine, wahusika
wakuu, ikapita kuwa hilo jambo lifanyike huko Dar , kwani nilishawahakikishia
kuwa nimempata mwanawali, ambaye nilithibitishiwa na mama yake mdogo kuwa ni
mwali kweli….na moyoni nilishaingiwa na tamaa naye, ninaweza kusema,
nilishampenda mwanao, samhani sana mama….mama Maua.’akakohoa tena.
‘Maua haya nayasema yanatoka moyoni mwangu,…unielewe hivyo,
na unisamehe, sikuwa na jinsi, kwa hali niliyokuwa nayo, na mazingira mazima
yaliyovyokuwa,mama na wewe unisamehe kwa hilo, kwani sisi wanadamu ni wepesi
sana kudanganyika na mbinu za ibilisi, na hasa inapohusu jambo la mali, utajiri….’akatulia
halafu akasema.
‘Safari ikapangwa, ikabidi tufike kwa siri Dar, na kila
mmoja aliingia Dar kwa siri kwa namna yake….na wahusika wakuu waote walikuwepo,
kasoro Malikia tu…’akakohoa mfulululizo, na baadaye akatulia.
‘Zindiko lilitakiwa kufanyika,…na waliotakiwa kulifanikisha
hilo ni wale waliokabidhiwa huo mkoba….nikimaanisha mimi, au mjomba au mkewe,
na ukumbuke mjomba keshajitenga, mambo
ya kishirikina, yaliyochukuliwa kwa mganga, na mganga aliyakabidhi mambo hayo
kwa mjomba wangu, ambaye alikuja kunikabidhi huo mkoba na huyo mganga keshapotea,
na hakuna wa kubadili lolote…kwahiyo ili lifanikiwe hilo zindiko, mimi
nahitajika….
Ukumbuke kuwa Mjomba keshaniachia kila kitu, mkewe
keshaondolea kwenye kikundi, kwahiyo, mzigo mzima uliangukia kwangu, na wote
wakawa wananiangalia mimi, na nisipofanya hilo kuna mambo yanakwama, biashara, kupata
madini, ni imani za kishetani, lakini gharama yake ni kubwa kuliko watu
wanavyozania, zinaumiza , zinatesa, na zinahusisha watu wasistahili, kwa
maslahi ya watu wengine…
‘Mimi siku hiyo, nilikuwa sijisikii vyema, hata hivyo
ilibidi niwajibike, na kwa vile nilishakupenda Maua nikaona hiyo ni nafasi
yangu kubwa sana, ….nikasahau kuwa malikia alikuwa na nguvu zake za giza, …..msimuone
vile, yule mwanamke ni kiboko wa mambo hayo….yeye alisema kama hakuna
mwanawali, tufanye njia nyingine, ambayo ni ya kumwaga damu….ikiwa na maana
kuua….’akatulia
‘Siku ile alinifanya vibaya, akasahau kuwa hayo niliyotakiwa
kuyafanikisha sio kwa ajili yangu tu, ilikuwa kwa ajili ya kundi zima, na kwa
manufaa ya mambo yetu ya kupata madini…..akaweka ubinafsi wake mbele…ushetani
ndani ya ushetani…
`Sijui mnanielewa hapo?’ akawa kama anauliza.
‘Kama hamnielewi basi ndivyo hivyo….. hivyo ndivyo ilivyokuwa….imani
za kishirikina zimeshika kasi sana…’akatulia,
‘Tena wasomi, wakubwa, matajiri, wakuu wa dini ndio wanazo
sana….lakini kwa kujificha…’akatulia.
`Siku ile mambo ya zindiko yalitakiwa kufanyika, na wahusika
waliyashapanga vitu vyao….na kazi ikabakia kwangu, lakini nikashindwa, na
washirika, wakawa wakiniuliza kila mara kuwa tayari, ile wachukue ile damu….damu
inayotoka kwa mwanawali, ambaye hajawahi kukutana na mwanaume…..natumai hapo mnanielewa…
‘Kama isingelifanikiwa siku hiyo, kuna mambo yalitakiwa
yafanyike,…damu ya mtu ingelitakiwa ichukue nafasi yake….na hilo nilishaanza
kuliogopa,…hayo siwezi kuyaongelea zaidi maana yanatisha, ….maana kwa hayo, napata
taabu sana nikiyawazia…..jamani kuua ni laana, mimi hapa nilipo naona shida,
Napata mteso, damu za watu zinaniandama….najuta najuta…..’akawa anongea hivyo
huku akionyesha kusikia maumivu makali.
‘Ogopeni sana kuua, damu za watu zinatesa, wote niliowaua kila
mara wananijia na kudai haki yao, wananitesa,..kila nikipoteza fahamu Napata
mateso makali sana….ogoeni sana kuua ….hivi sasa nateseka, nateseka….sana sana….naomba
roho itoke haraka, nikakuate na huo moto, maana sina ..sijui kama nitaweza
kusamehewa’akawa analalamika maumivu…akaanza kukohoa kwa mfulululizo.
‘Maua…naona muda umefika,…ila ili ujue ni nani alifanya hayo
niliyoyashindwa…ooh, nenda kamuone dakitari wa mjomba….huenda, nahisi hivyo,
kwa vile yeye kumbe anajua mengi ya hayo, na …nilikuja kugundua hayo jana tu,
alipokuja kuniomba huo mkoba, sikuamini….’akatulia.
Na nikikumbuka siku ile, ….nilipozidiwa na pombe, nilisikia
wenzangu wakisema …muiteni docta, sikujua ni docta gani huyo…..ooh, sasa,
naanza kuelewa, ….lakini siwezi kuelezea zaidi, muda naona umefika, kwaherini…..’akaanza
kutikiswa kwa nguvu, na baadaye akaanza kukoroma, ….akatulia,…..na yale mashine
ya kuonyesha mapigo ya moyo yakawa kama yanaanza kunyooka, lakini ghafla,
yakajirudi.
‘Oh,…naona kuna kitu, …..nimeota…..mungu nisamehe, ..ooh,
eti nini, hapana..haiwezekani, ina maana ni damu yangu, haiwezekani,..oh, Maua
ina maana wewe ni ni….oh, oh, oh, kamuone docta atakuelezea, ….’akaanza kutikiswa kwa nguvu,hadi kitanda
kizima kikawa kinatetemeka.
Mara Docta anayemuhudumia akaingia kwa haraka na kuwaambia
akina Maua na mama yake watoke nje,…. na wakaingia madakitari wengine, kusaidia....
Maua akawa anasita kuondoka….mama yake akawa anamvuta mkono…..na
Maua akatupa macho kwenye yale mashine ya kuangalia mapigo ya moyo,….mishale
ilishaanza kunyooka, na mara mlio wa ishara ya hatari ikaanza kulia.
Yule docta akachukua vifaa vya kushinikiza mapigo ya moyo na
kukiweka kifuani, na mwili wa Tajiri, ukaruka juu, …alifanya hivyo tena, lakini
haikusaidia kitu, ….akaviweka pembeni, akchukua vifaa vyake, akasikilizia
masikioni,….akawageukiwa wengine, na hakusema neno, akavua vile vifaa alivyokuwa navyo masikioni...na wenzake wakaanza kuondoa vifaa kutoka kwa yule mgonjwa.
Yule docta, akageuka kuondoka na alipofika mlangoni, ...,akawaona Maua na mama yake, wakiwa wanavutana kuondoka, mama akimvuta binti yake, na binti yake, akiwa kama kaganda,…
‘Oh, nyie bado mpo?’ akauliza
‘Ina maakeshafariki..?’ akauliza Maua huku machozi yakiwa
yameshaanza kumtoka.
‘Nasikistika kusema kuwa ndio hivyo….lakini, nawaombeni
msubiri nje, kama ni kweli nitawaambie, ngojeni niwaite waenzangu kwanza,
huenda kuna ujuzi wa ziada….’akasema huku akiandika kitu kwenye cheti chake na
alipohakikisha kuwa hawo akina mama wameondoka, akachukua shuka jeupa na
kuufunika ule mwili, …
NB:Amini usiamini, dunia hii imejaa mambo ya ajabu,
ushirikiana sasa hivi umekita kwenye mioyo ya watu, wakubwa kwa wadogo,...hadi kwa viongozi wa dini ambao tulikuwa tunawategemea, ...na hata wasomi, ambao tulijua kuwa watasaidia ....sijui huko tunapokwenda kama
imani za dini zenyewe zinapigwa vita…
WAZO LA LEO:
Dhambi ya kuua ni kubwa sana, na ukiua, usizanie kuwa unaweza ukaifukia ile
damu kwa mguu, ukasema oooh, hawatanijua, nimeokoka…damu ile itakuandama mpaka
kufa kwako.Tuepuke dhambi hiyo, na ili kufanikiwa kwa hilo, ni wote kupendana, tuondoe
chuki, …chuki ni tabia ya ibilisi,….ni vyema tukusaidiana…tukashirikiana, na haki ya kila mtu ikaheshimiwa.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
This is mу firѕt time рay
a νisіt at hегe and i am rеally ρleаssant to rеad all
at sіngle ρlаce.
Μy blog post :: instant payday loans
my web site :: instant payday loans
Post a Comment