Kilikuwa ni kikao cha wanafamilia, akiwezo mzee, na mabinti zake, ambao
walishamua kuhakikisha baba yao anaondokana na mambo yote yanayomfanya
aathirike kiafya, na kwa mtizamo wao, waliona ni vyema kwanza wakasuluhishe tatizo la ndoa yao, ....
‘Sasa tufanyeje maana mama katoa masharti yake magumu,
ambayo baba hayakubali, na halikadhalika baba ni hivyo hivyo….?’ Akauliza binti
wakati wakimsubiri baba yao.
‘Dawa ni kuwakutanisha wote kwa pamoja, wakaongea
tukiwasikiliza,….lakini kabla ya hilo, inabidi tukae na mama , tumuelezee jinsi
gani anatakiwa kuongea na baba, hatakiwi aje na ukali, akimkasirisha baba,
inaweza ikaleta mshituko mwingine,…hapa tunaweza tukatatua tatizo la ndoa, na
ikawa tiketi ya kummaliza baba….’akasema mwenzake.
‘Nikuulize dada, ni kipi bora,kuwepo na ndoa ..hata kama hakuna
mapenzi, watu wanaishi wanaitwa mume na mke, lakini ndani hakuna amani wala
mapenzi, ….huoni hapo tutakuwa hatujasaidia,….mimi naona kazi kubwa ni kujenga
mapenzi, …hili tukifanikiwa kuliwezesha,kuijenga ndoa hakutakuwa na shida,….kwasababu
sioni umuhimu wa ndoa kama hakuna mapenzi ya kweli, ….unaonaje ndugu yangu?’
akauliza
‘Hilo ndilo swala gumu, ….sisi kama watoto raha yetu ni
kuona mama anarudi, na wanaishi pamoja na baba, lakini je hiyo raha ya ndoa
ipo,….amani ya moyoni, itakuwawepo, ni kweli wao ni wazee, hawana haja sana, ya
kufikiria hayo, ….lakujini nijuavyo uzeeni ndipo sehemu ya kuwa na mashikamano,
raha, na utulivu, kuliko anani….’akatulia.
‘Ni kweli, ujanani, ….unaweza ukaruka huku na kule, uzeeni
ni fainali,…na mwili, mishipa , fahamu zimeshachoka, zinahitaji
matulizo,..hazihitzji mihamaniko tena…hapo inabidi tuwe makini…’akasema.
‘Mimi kiukweli nionavyo, hata kama mama atarejea, baba
hatakuwa na raha…..atakuwa anaishi kwa ajili yetu tu, upendo kwake kwa mama ulishakwisha,
…sasa hapo naona kuna umuhimu wa kuonana na mama tujaribu kumuelezea hilo, kama
anaona ataweza kumshawishi baba arejeshe moyo wake kwake, basi,…kama hataweza,
mimi naona ili kuepusha shari, bora wakae hivi hivi, ila kuwe na ukaribu
fulani…’akasema.
‘Hapana mimi hilo sikubaliani nalo, mimi najua kama
watarudiana na wote wakakaa pamoja, watapendana tu, …umri huo walio nao ni wa
busara, ….hata kama sio ule upendo wa awali,lakini wataishi kama mke na
mume,…..haina haja kuwapa watu faida,….cha muhimu ni kuwakutanisha,….’akasema
mdogo mtu….na baadaye baba akaingia, na kukaa kwenye kiti chake,…
*******
‘Haya binti zangu, nipeni muhutasari wa kikao cha
leo,..maana nyie ni wasomi, kila kikao, hata kama ni cha kifamilia, ni lazima
kuwa na ajenda, …na ni muhimu kwangu ili nijipange, je ni kuhusu maendelea ya
shughuli zetu au kuna jipya?’ akauliza.
‘Baba tukikutana hapa, unajua kabisa hatuongelei, maswala ya
kazini, hapa ni maswala ya nyumbani, umesahau mwenyewe ulivyotupangia,
….’akasema.
‘Aaah, nilijua mumekuja na mambo ya kulaya ulaya, akili sasa
imeshaanza kuchoka, …..haya mambo gani ya kinyumbani?’ akauliza.
‘Ni swala la ndoa yako….’akasema dada mtu, na akamuona baba
akibadilika sura,
‘Baba hatuna nia mbaya na wewe, na nia yetu sio kukukwaza
kwa ajili ya kumrudisha mama, lakini hili lina umuhimu wake, kwani nyie ni
wazazi wetu, na dawa ya hili ni kutafuta suluhisho la kudumu na lenye manufaa
kwa pande zote, wewe na mama….’
‘Kwasababu sisi tukiongea na mama anakulaumu wewe, na
anakuona wewe ndiye unayechangia kuvunjika kwa ndoa yenu, kwa kutokumsikiliza
yeye….anadai hata kampuni , na utajiri uliopo sasa kama asingelikuwa yeye,
usingelipatikana, sasa mumetajirika, unamzarau….hayo ndio maneno yake kila
siku…’akatulia na mwenzake akaendeleza kwa kusema.
‘Na wewe baba tukiongea na wewe una madai yako pia,
tumeyasikia, … na kwa ujumla madai yako tukiyapima, tunayaona yote yana msingi
na hata ya mama yana msingi pia, hatuwezi kuyapuuza…sasa kwanini hamukai pamoja
mkaangalia wapi mumemkosea, mkasahihishana….’akasema huyo binti.
‘Baba nyie ni wazazi wetu, hadi sasa hakuna usahihi wa
kisheria kuwa wewe na mama mumeachana, au sio?’ akauliza binti mdogo,
alipomuona baba yake kakaa kimiya hasemi kitu, na baba yake akainua kichwa na
kuwaangalia wote wawili kila mmoja kwa sekunde chache, akasema;
‘Upo….unahitajika ushahidi gani tena, mnataka mpaka
tupelekane mahakamani kama wanavyofanya wazungu…..hapana, sisi tulishafikia
maafikiano, na mbele ya mwanasheria wetu huyo aliyetusalati, na ukinitajia
mwanasheria naona kama ni watu wakuja kula pesa zetu, na kuchunguza undani wa
watu ili waweze kuwatapeli….lakini hata hivyo, huyo mwanasheria alitushauri
kuwa, tukapeana muda wa kufikiria, kabla ya kufikia maamuzi ya kuandikiane
talaka…’akasema
‘Kwahiyo baba kwa ujumla talaka, haijatoka?’ akaulizwa.
‘Talaka….?...ndio talaka ya, kimaandishi haijatolewa, lakini
kwa kauli zetu, mimi na yeye, tulishaafikiana hivyo…lakini mwanasheria hakutaka
kukimbilia kuandika hiyo talaka kwa haraka, na akadai tupeane muda kwanza…na
mambo yalivyo, nimekuja kugundua kuwa , kumbe walikuwa kitu kimoja…walikuwa
wakinizunguka …..mungu amewaumbua.’akatulia.
‘Baba hayo mengine ni ya kusikia tu…naomba yasikuumize
kichwa….’akasema binti.
‘Wewe unasema tu, kwa vile ni mama yako, …lakini kama
ungelikuwa wewe kwenye nafasi yangu, nina imani ungelichhukua hatua kubwa
zaidi,…hakuna kitu kibaya kwenye ndoa kama kukosa umanifu,…kusalitiana, na
kuendekeza shiriki…mama yenu alikuwa na uazaifu wa hayo yote,…shiriki, kila
jambo mpaka kwa mganga, mimi sina hulka hiyo…msizani kuwa mimi maamuzi hayo
nimeyachukulia kwa hara…’akatulia.
‘Sitaki kuyaanika mabaya ya mama yenu, kama anavyoanika hayo
anayoyaona ni mabaya yangu, kwani haitanipa faida yoyote, lakini nimevumilia
mengi sana….kueni myaone, ….ndoa ina siri nyingi sana, watu wanatoka nje
wameshikana wakiitana mume na mke, lakini ndani ya nyumba zao kuna siri kubwa
sana….usione watu wanashikwa na viarusi,..ukichunguza kwa mapana, kisa ni
ndoa……oh, ….’akatulia.
‘Baba tunaomba usiyachukulie hayo kiundani sana, ….kama
unahisi yanakuumiza, ni bora tukatishe haya amzungumzo….;akasema huyo binti
pale alipomuona baba yake akihangaika .
‘Msiwe na wasiwasi…..’akasema na kutulia kwa muda, na yule
binti alipoona baba yake yupo sawa, akasema;
‘Hayo matatizo ya ndoa, ….ni kweli yapo, japokuwa hatujawahi
kuingia huko, lakini baba mimi nina imani kuwa wanandoa wakitaka maisha ya ya
ndoa yao yabadilike yawe wanavyotaka wao, wanaweza kufanya hivyo na
wakafanikiwa….tatizo ni ile hali ya kila mmoja kukubali ukweli, na kujiweka
katika nafasi yake….’akasema mmoja wa wale mabinti.
‘Ni kweli baba, na ukitaka maisha ya ndoa yenu, irejee
kwenye upendo, wa kweli mnaweza, na sisi tutahakikisha kuwa yanabadilika, ….amueni
kuwa mnarejea, na sis mtushirikishe, tuna uhakika, tukishirikiana pamoja
tutafanikiwa….., tuna imani kuwa mama atakua sio yule unayemfahamu tena’akasema
binti.
‘Wanangu, hayo ya mimi na mama yenu, ni sawa na kumpigia
gita mbuzi,…..sikuanza leo, na niliwahi hata kumtafuta dakitari bingwa, ajaribu
kukaa na mama yenu, ili arejeshwe kwenye msiamamo wa ndoa,…..lakini
haikusaidia,….kiukweli…mim sina imani na mama yenu tena…..sina mapenzi naye
tena….naombeni mnifikirie na mimi, na kama kweli mnanipenda na kunijali na
mimi….nipeni nafasi yangu, kumtafutia mwenzake, ambaye atanipa tulizo la
moyo…..’akasema.
‘Baba kwa umri huo,….na hata hivyo ni nani kwa umri huo,
atakubali aolewe na wewe…?’ akauliza.
‘Wapo wengi….lakini baada ya kufanya uchunguzi, nimempata
mmoja,…nitakuja kuwatambulisha kwenu, kama ndio mnataka iwe hivyo, …..’akasema.
‘Baba unamzungumzia, Maua ?’ wakauliza na kabla baba yao
hajajibu yule binti mkubwa akasema;
‘Baba kwa ushaidi tulioupata Maua kweli ana uja uzito, lakini
hiyo mimba sio yako….ni ya mpwa wako, na huenda kuna ujanja unataka kuchezwa
ili ubambikiwe hiyo mimba,….hilo hatutalikubalia. Cha muhimu tunajua kuwa mimba
ni ya mpwa wako, na kama unataka kutoa msaada ni shauri yako…’akasema binti.
‘Hilo niachieni mimi,…kama ni yangu au sio ya kwangu, hilo
haliwahusu, mimi ninayemuhitaji ni huyo binti, na nimeshawaambia kuwa yule ndio
dawa yangu, …kama isngelikuwa huyo binti, msingelinikuta hai …..mengine hayana
maneno ya kuelezea, niachienii mwenyewe…., mimi nitailea hiyo mimba na hata
kama mtoto sio wa kwangu…..lakini kama ni wangu, nitahakikisha nampata kwa kila
njia …..oh’akasema.
Wale mabinti walimuangalia baba yao kwa muda wakiwa
wametulia, kwani walimuona kama anaongea kitu ambacho hakieleweki, hiyo mimba,
itaingieje, wakati wao wanajua kuwa alishafanyiwa upasuaji wa kuzuia kuzaa….wakaangalia
na kukonyezana, na baba yako, alipowaona mabinti wake wapo kimiya akasema;
‘Kwahiyo hakuna mwenye taarifa yoyote mliyoipata ….?’
Akauliza huku akiwa kama anajisikia vibaya, akachukua maji akanywa na kutulia
kwa muda, ….akainama huku akiwa kashika kichwa, akionekana kuwaza sana, na wale
mabinti wakaogopa kuwa wakiendelea kuliongelea hoja iliyokuwa ikiongelewa
huenda likamuathiri baba yao,…..na ndipo mmojawapo akasema;
‘Baba usiwaze sana kuhusu hilo,…. hatujapata taarifa rasmi
kutoka hospitalini, ….tulipofika asubuhi, alikuwa bado hali yake ni ile
ile….’yule binti akasita kuendelea, kwani …walikuwa wakitafuta mwanya wa jinsi
ya kuleta taarifa waliyoipokea…ambayo ilikuwa sio nzuri kumwelezea baba yao.
‘Mimi sio mtoto mdogo, najua kuwa mpwa wangu hayupo tena duniani..dalili
zote nimeshaziona, …na nina njia nyingi za kupata taarifa,….nimeshajua yote,
…lakini….ni vigumu sana kuamini mpaka uone kwa macho yako….ooh, ndio dunia hii,
maisha ni kitu kidogo sana, ni kama ndoto tu, ….unalala unaota, unahangaika na
dunia, ukiamuka upo dunia nyingine, watu wanaanza kukuita marehemu….’akasema.
‘Baba …’akasema binti na mara simu ikalia.
Yule binti akaipokea na kuisikiliza kwa muda, halafu
akageuka kumwangalia baba yake, na ….hakuweza kuzuia machozi, …akageuka
kuangalia kwingine, na hapo akawa hana jinsi ila kusema ukweli..
‘Ni kweli baba..Tajiri hatupo naye duniani…..’akasema huyo
binti, na kumsogelea baba yake, akawa kamshikilia kama anamkumbatia kwa upande
upande na baba yake alikuwa kainama vila vile, baadaye akasema;
‘Nilijua…..tatizo ni kuwa kauwawa….sasa muuaji,
apatikane,….huyo muuaji,… huyo mwanamke, ….’akaseimama na akawa kama
anapepesuka.
‘Baba tulia unataka kwenda wapi..’yule binti mwingine
akasema an kumsogelea baba yakae.
‘Hasira….natamani ule ujana wangu ungelikuwepo….na sijui nikimuona
huyo binti, sijui…nitamfanya nini….na kama polisi watashindwa kumpata ,
nitatumia vijana wangu watamkamata tu, ….’akasema
‘Baba iachie sheria ifanye kazi yake, hilo lipo mikononi
mwao kwa hivi sasa, huwezi kuwaingilia…..’akasema binti yake.
‘Sheria itafanya kazi…mmh?....na ifanye kweli kwani kama
haitafanya hivyo, nitafanya hivyo mwenyewe…na wasipoangalia, vifo vingi
vitafutia…..ninavyowajua hawo watu……sijui, tatizo ni kuwa watu wakishaonja
kumwaga damu, wanabadilika kabisa, kwao wanaona ni kitu cha kawaida…kuua mtu
wanaona kama kuua ng’ombe…..’akatulia.
‘Basi baba ngoja tuangalie taratibu nyingine , za
mazishi…..wewe tulia, na jipe moyo’akasema binti.
‘Na …..wale akina mama na binti yao, wapo wapi,….kwani
nilisikia waliitwa na Mpwa wangu…..inawezekana bado wako huko huko,…namombeni
sana muwakaribishe hapa kama moja ya familia,…..na nahitajia sana kuongea na
wao….’akasema.
`Baba usiwe na shaka na hilo…’akasema mmoja wa wale mabinti
Na mara mlango ukagongwa, na ….
********
‘Wewe ndiye mama yake Maua..?’ sauti ikasema kwa nyuma yao,
wote wawili wakageuka, na kujikuta wakiwa wanaangaliana na mama mmoja aliyekuwa
kavaa mawani, na mkononi kashika simu, huku akiwa anataka kuongea na mtu.
‘Mama hebu twende, huoni mtu mwenyewe anaongea na
simu..’akasema Maua.
‘Subiri…naona kama namfahamu huyu mama’akasema mama Maua.
‘Subirini naongea na mtu muhimu sana…..nataka kuongea na
nyie,….’akasema yule mama alipoona Maua akamvuta mama yake.
Yule mama alipomaliza kuongea na simu akawasogelea, akavua
ile miwani, halafu akashika kiuono, akamwangalia mama Maua,halafu akamwangalia
Maua, halafu akasema;
‘Hivi kumbe upo hai, wewe si ulikimbilia msituni, na kwa
mara ya mwisho nilisikia kuwa umeuwawa na watu wa msituni…’akasema huyo mama.
‘Kama unavyoniona ndio mimi, hayo mengine yalikuwa ni maneno
tu…’akasema mama Maua.
‘Ohhh, na huyu ndiye binti yako…?’ akasema na kumwangalia
Maua
‘Ndio yeye, …’akasema mama.
‘Sasa wewe mama, hebu niambie, ….hivi kweli una uchungu na
mwanao, …kibinti kidogo hiki, kiende kiolewe na mzee,….sasa na babu yake, una
akili kweli, na hata hivyo hii, dunia inakwenda wapi, yaani binti mdogo kama
wewe unakwenda kufanya ufusuka na mzee kama yule….’akatema mate chini.
‘Wewe mama wewe nakuomba usinivunjie heshima
ynagu,…sijafanya hivyo unavyosema wewe..’akasema Maua.
‘Najua utasema hivyo, kuwa yule mzee, kakutaka…lakini kwa
kauli niliyoisikia ni kuwa una mimba, ..hehehe….hivi wewe huna aibu uende
kumbambikia yule mzee mimba, …yule mzee hazai, kwa taarifa yako, ….alifanyiwa
upasuaji …’akasema huyo mama.
‘Wewe mama, nakuambia tena, kuwa hayo unayozungumza hayana
ukweli….wewe yaache kama yalivyo…’akasema Maua.
‘Unasema niyaache kama yalivyo….?’ Akasema kwa sauti ya
ukali, akimwangalia Maua…
‘Wewe binti, niangalia hivi hivi….unajua nikuambia ukweli,
nyie ndio mumechangia huyo mzee, asinirejee….kama isingelikuwa nyie,
angenirudia tu, ile biashara yake, na miradi yake, mnajua jinsi
ilivyopatikana….ni mimi na juhudi zangu, sasa hali imekuwa nzuri, wanakuja watu
wa ajabu, ….na mabya yatawaandama, unaoana …..wameanza kuuana, na bado,
….’akasema huku akitaka kupokea simuiliyokuwa ikiitwa.
‘Mama hebu twende zetu….’akasema Maua.
‘Hebu subiri kidogo, sijatoa kauli yangu yoyote
kwake,…..’akasema Mama Maua.
Yule mama alimaliza kuongea na simu, akawageukiwa Maua na
mama yake, akasema;
‘Sikilizeni kwa makini, iacheni ile familia kama ilivyo,
kama mumekosa sehemu ya kwenda, rejeeni kijijini mkalime, kwani yoyote yule
atakayeingie pale, kwa namna yoyote, kama sio mwanafamilia,
hataishi…nawahakikishia, kama mimi sio mwanamke wa huko, kulikoogopewa,
jaribuni kuingia pale….’akasema huku akiwa kashika kiuono.
‘Mimi ni mama yake huyu, na nilikuja kuangalia jinsi gani ya
kuyaweka hayo mambo sawa, wewe kama mwanamke mwenzangu, nakuomba tukae tuongee
tuone jinsi gani ya kuyasawazisha, maana hakuna mtu anayeweza kukurupuka na
kwenda kudai kuwa mimba na huyu, bila kuwa na mahusiano naye,…..’akasema mama
Maua.
‘Kwahiyo wewe unaona ufahari, kusikia kuwa binti yako
katembea na mzee kama yule, ….hivi wewe unatoka kijiji gani, au ndio maana
walikutimua wazazi wako…’akasema huyo mama.
‘Sijafurahia hilo, na hilo halijakubalika kuwa kuna
mahusiano kati ya binti yangu na mzee wako..hayo ni maneno tu, …na ukiyajua
kiundani utaelewa kwanini imekuwa hivyo….na kama nitaamua kwenda polisi, huenda
huyo mzee wako na wote wanaohusika watakuwa hatiani, maana huko ni
kubaka….’akasema Mama Maua.
‘Hehehe….unatishia nyau eeh, nendeni polisi, maana huko ndio
mtaumbuka, nimeshawaambia yule mzee hazai , hiyo mimba …imetoka wapi, ….sawa
hata kama kwa uzinzi wake alikutana na huyo binti, na huyo binti bila aibu,
akamkubalia,…..maana hapo, ni kujiuza, ….lakini asisisingizie mimba,….hilo
litawaumbua’akasema yule mama.
‘Hayo tukikutana pamoja tutayaongelea, na ukweli
utajulikana..’akasema mama Maua.
‘Mkutane na nani….nawaombeni mondoke mrejee huko mlipotoka,
hakuna wa kukutana naye…..’mara simu ikalia tena. Alisikiliza kwa makini,
halafu akasema kwa hasira.
‘Nani aje huko, mwambieni, mimi sina muda wa kupoteza….na
hawo wanawake mnaowazungumzia ninao hapa, nimewaambia waondoke zao…..’akasema
‘Nimeshawaambia sina muda huo, yote nitayamaliza nijuavyo
mimi, kwanza wameanza kuuana, mwishoni waliobakia wataanza kuwehuka….hilo
nawaambia mlisikie, huyo baba yenu anajifanya hanisikilizi, atakuja kunipigia
magoti…’akasema huyo mama.
‘Nitakuja kwa wakati wangu, lakini siwezi kuongozana na hawa
wanawake, watanitia aibu….’akasema na kuanza kuondoka..
‘Mama twende zetu….’akasema Maua.
‘Twende wapi sasa?’ aakuliza Mama Maua
‘Twende huko huko, mimi mama siwezi kuondoka mpaka
nihakikishe nimepata haki yangu, …siwezi kuwaachia hivi hivi…’akasema Maua.
‘Haki gani , na wakati anayejua yote keshafariki?’ akauliza
mama Maua.
‘Hayo tutayajua huko huko…yule mzee ni mpwa wake, na…..na
huyo dakitari, ataelezea ukweli ulivyokuwa..’akasema Maua.
‘Kama ni hivyo, kwanini tusiende huko kwa huyo
dakitari…’akasema Mama Maua kama anauliza.
‘Twende kwanza huko tulipoitiwa….kwa huyo mzee’akasema Maua.
‘Aaah, na wewe na huyo mzee….nakuambia ukweli, mimi
sitakubaliana na hayo ya mama yako, kama wewe ni mwanangu kweli, achana na huyo
mzee, sitakubali kamwe uolewe na huyo mzee, kama unaogopa kuhusu kulea, twende
tukaishi pamoja, nilikulea wewe kwa shida, sitashindwa kumlea mjukuu wangu,….’akasema
Mama Maua.
‘Mama mimi ninachodai ni haki yangu, wameniharibia mpangilio
wa maisha yangu…na kwa maelezo ya Tajiri, Mzee anawajibika kwa hili…na hapo
hapo kwa mzee ndipo tunaweza kupata ukweli wote, na mwenye ujauzito huu tutamjulia hapo hapo…’akasema Maua.
‘Haya….twende ….na huyu mama yako mdogo kaenda wapi? ’akasema
Mama Maua, na kuangalia huku na kule.
‘Atakuwa katangulia kwa huyo mzee,….tutamkuta huko huko…’akasema
Maua.
Mara wakasikia sauti ikiita nyuma yao, walipogeuka wakamuona
ni mama mdogo akija kwa kasi, ….wakamsubiri hadi alipowafikia, akiwa bado ana
hema, akasema;
‘Mumesikia hiyo…msicheze na polisi,…msicheze na yule mzee,
niliwaambia ni mchawi,..ona sasa, nasikia yule wakili naye, ….’akaonyeshea kwa
kidole shingoni.
‘Unamaana gani kusema hivyo…’akauliza mama Maua.
‘Ngoja ninyamaze maana polisi hawana dogo, wewe sikilizia
tu,….’akasema huku akitembea kuongoza mwendo, akionyesha kuwa na wasiwasi ….mama
na mwanae wakaangalia na baadaye wakamfuatia nyuma.
NB: Msichoke,…tupo pamoja.
WAZO LA LEO:
Binadamu tulivyo, kila mmoja ana maono na hulka yake,…mnapokuwa kwenye ndoa, nyie
ni kitu kimoja, mnahitajika, maono na hulka hizo zilandane, kwa kuonyeshana, kuambizana
ukweli kuhusu maono hayo, jinsi gani unavyojisikia, au jinsi gani usivyopenda
iwe au isiwe…, kwani neno dogo tu linaweza likaleta tafsiri tofauti na kusababisha
kutokuelewana, hata kama mmoja alisema hivyo bila nia mbaya.
Ni vyema basi, tuwe wawazi, na tusiogope kuelezana huo
ukweli, na pia tukubali kusikiliza, tuondoe mfumo dume/jike ili kuepusha
migogoro isiyo ya lazima kwenye ndoa zetu.
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
Na pia katika ndoa ni lazima kuwasiliana ni kitu kikubwa sana ni kama vile kupalilia shamba...nimependa wazo la leo..na kazi yako hakika si mchezo..Hongera sana.
Wengi wakishapata shamba hawana muda wa kulihudumia, mpaka linaota majani. Ndoa kwao wanajua ni kutimiza wajibu na kupata sifa ya kuwa MWANANDOA.
Ndoa ina hitajika kuenziwa,kuhudumia kama lilivyo shamba, kwa kuelewana, kusikilizana, na kujadiliana pale mnapoona kuna tatizo.
Kuna tabia za kurithi, nyingine hazifai, ulizaneni kwanza, usijichukulie maamuzi yako mwenyewe, kwani mwenzako anaweza akakuchukia sana. Kwenye kisa chetu, tabia iliyojionyesha ni `ushirikina,' zipo nyingi.
Nashukuru sana dada yetu Yasinta, kwa mfano huo wa shamba.
Post a Comment