‘Ponda maisha rafiki yangu, huwezi jua ya kesho, mwenzako
sasa hivi yuko huko kikaoni, wakimaliza kikao tu, usiku wanajimwaga kwenye mabaa,
unajua nini kinachoendelea huko kama sio kunywa, kula nyoma choma na .....baada ya hapo utajaza mwenyewe..’hayo yalikuwa maneno ya shoga yangu, alipoanza
kunijaza hisia ambazo sikuwa nazo kabla.
Kutokana na hayo maneno, vishawishi, na hata kwenda kujionea mwenyewe, nikawa nimebadilika kabisa,na kuwa na tabia ambayo sikuwa nayo kabla,tabia ambayo
mpaka sasa naijutia, na kujiuliza kwanini nilifikia hapo,…na ni nini
nimekipata baada ya hapo, zaidi ni kuathirika kiakili , kimwilii na sijui kama afya yangu
itatengemaa tena, kama sio kuelekea kaburini….nimeshakata tamaa ya kuishi.
Tabia hii ilianzia kubadilika kidogo kidogo, hasa pale nilipokutana na shoga yangu huyu. Yeye ndiye aliyeanza kunijaza maneno, na ndiye
aliyenitoa kwenye tabia ya malezi ya wazazi wangu hadi kuwa mwanamke wa mafiga
matatu, ….najuata sana, na hata kama nilivutwa na hali ya mume wangu, lakini
sikustahili kujiingiza kwenye haya machafu…..hadi, hadi….’hapo alishindwa
kuongea akawa analia.
Yaani tabia hiyo ilianza kama
mchezo wa kuigiza,….naikumbuka sana siku ile nilipokutana na rafiki yangu huyu na hatimaye nikakutana na mke wa adui wa mume wangu, ilianza hivi....
***
Huyu rafiki yangu alikuwa akija kwangu mara kwa mara, na tulikuwa tukiagiza bidhaa pamoja toka nchi za nje, na tulifikia hatua ya kuaminiana sana. Kutokana na msimamo wangu, alishindwa kabisa kuniingiza kwenye mambo mengine nisiyoyataka,hadi pale aliponiletea hii taarifa kuwa kaipata kutoka vyanzo venye uhakika. Nilimkatalia kata kata na kusema;
‘Mimi siwezi kuamini hayo maneno yako maana
namjua vyema mume wangu, tunapendana na kuaminiana sana, na kazi yake hiyo
aliyojiingiza nayo inahitaji awe msafi, hawezi kujiingiza kwenye hayo
machafu’nikamwambia huyo shoga yangu.
‘Kama unabisha ipo siku nitakuleta ushahidi uone mwenyewe,
mimi mwenyewe nilikuwa nikimwamini sana mume wangu, lakini siku moja nikaifuma
barua toka kwa hawara wake wa nje, na hata nilipombana sana hakukubali ukweli,,
nikasema ngoja, basi siku moja walipoondoka tu, na mimi nikafunga safari,
nikawafuatilia nyuma…’akasema huyo shoga yangu.
‘Hayo mambo ndiyo siyataki kuyasikia, achana na hizo habari, kama huna kazi sema nikue kazi unisaidia kupanga haya marobota huku juu,....mimi najiuliza kwanini umfuatilie mume wako kwani hamuaminiani, huoni huko ni kujiumiza mwenyewe, na utajiweka katika hali mbaya ya kusononeka bure’nikamwambia huyo shiga yangu.
‘Ndio maana nakuambia kuwa na wewe usijifungie nyumbani, ukimaliza kazi hapa jichanganye na wenzako, katumie muda huu, maisha yeneywe mafupi, …kutana na wenzako hata ikibidi tafuta figa la pili na la tatu, pata rafiki wa siri wa
kuaminika, ambaye siku moja moja unakuwa naye,anakutoa upweke, …’hayo maneno yake, yalinifanya nimfukuze, hapo ofisini kwangu, na yeye akabakia kunicheka, na kusema.
‘Ipo siku utaamini maneno yangu, ..’akasema lakini sikutaka kabisa kumsikiliza, na nilijitahidi
sana kumkwepa kuongea naye nikijua huyo ni ibilisi wa kibinsadamu, ukimfuata anaweza ukapotea,
Lakini siku moja nikakutana na yule mke wa aliyekuwa
rafiki wa mume wangu,....huwa anakuja hapo dukanikwangu akihitaji nguo mpya. Siku ya kwanza alipokuja hapo kwangu nilimuheshimu sana,kwani yeye nilimuona kama mkombozi wangu, maana isingelikua yeye, ningelikuwa nimeshaolewa na huyu jamaa anayejifanay ni tajiri.
Ingawaje baadaye, baada ya mume wangu kujiingiza kwenye siasa, tulianza kujenga uadui na huyo mwanamke, hasa kipindi kile cha kampeni na uchaguzi,..tulifikia hadi kuwa maadui, kwasababu ya mambo hayo
ya kisiasa, kwahiyo kukutana kwetu ilikuwa sio kwa urafiki , ni kwa vile alihitaji nguo mpya, na mimi ndiye niliyekuwa nikileta nguo anazozipenda.
Siku hiyo nilikuwa kwenye duka langu la nguo, na humo ndani kuna vitu vingine vya urembo, nikiwa nimechoka na nilijiandaa kufunga duka, nikajipumzikie,kwani nilikuwa nimekata tamaa ya kupata wateja kwa siku hiyo ya jumapili.
Nikiwa nafunga funga amhesabu, mara mlangoni akaingia huyu mama, alikuja na wafanyakazi wake, wakasema wanahitaji nguo za harusi ya ndugu yao, na mapambo yake, nikaanza kuwahudumia. Na moyoni nilijua nitaingiza pesa ya maana , kwani mara nyingi
akija huyu mwanadada, huwa ananunua vitu vingi.
Kwa namna nyingine alikuwa mteja wangu
mzuri, licha ya upinzani wa kisiasa , na kwangu mimi, mteja ni mfalme, nikampokea kwa kunyenyeka, na yeye bila
hiana akajikaribisha, baada ya kuchagua alichokitaka, akaniomba tuongee ndani
ya ofisi yangu.
Nikashikwa na mshangao, maana sio kawaida yetu , yeye akija, na kununua alichokihitaji, analipa pesa nakuondoka zake,na alishanaimbia, kama hizo nguo zingelikuwa zinapatikana sehemu nyingine asingeliweza kuja hapo kwangu. Sasa leo kaja na mpya, anataka tuongee, na maongezi yenyewe anahitaji yafanyikiea kwenye ofisii, sehemu yenye faragha, nikaogopa.
`Kwani una maongezi gani na mimi hadi tuongelee hko ofisini...?' nikamuuliza.
'Usiwe na wasiwasi, ....ni maongezi ya akwaida tu ya akina mama, sina baya na wewe, mambo ya kisiasa yasitufanye tukose ubinadamu, sitachukau muda wako mwingi maana hata mimi nina kazi nyingi sana,....'akasema na kutangulia kuingia kwenye ofisi yangu ambapo huwa sikaribishi watu ovyo.
Tulipoingia na yeye kukaa kwenye kiti, akaanza mwenyewe kuongea;
‘Unajua kwa vyovyote iwavyo, kuna kitu kimoja
kinatuunganisha’akaanza kuongea pale alipohakikisha kuwa nimefunga mlango na
hakuna wa kutusikia hayo tunayoyangea, na moyoni nilijua kuna jambo kubwa
anataka kuniambia.
‘Kitu gani hicho cha kutuunganisha maana kisiasa sisi ni
maadui, labda kibiashara….nikuulize mapema, unahitaji nini kutoka kwangu, maana hali
ilivyo, wewe huna urafiki na mimi, ni kwa vile tu unahitaji bidhaa kwangu...ulishasema ni kwa vile nguo kama hizo zangu hujaweza kuzipata mahali pengine ungelikuwa hufiki hapa kwangu tena...una taka kuongea jambo gani....?’nikamuuliza huku nikiwa naogopa, asije akatokea mume wangu na kuniona nikiwa na huyu mtu, maana mume wangu alishanikanya kuwa nisiwe na ukaribu na hawa watu.
‘Mimi sina uadui na wewe, na wala sina urafiki na wewe, mimi
ni mteja wako tu, na kama ningelikuwa na dhana potofu, ningelikata kabisa mguu
kuja kwako, lakini kuna mambo mengine tunahitajika tuwe pamoja kama wanawake,
tukae tuongee na tuwe na mashirikiani,maana mimi ni mwanamke kama ulivyo wewe ,
kuna leo na kesho…’akaniambia na alinishangaza kwa kauli yake hiyo, nikatulia
kumskiliza.
‘Kuna jambo muhimu nataka nikuambie, hili usilichukulia
pupa, kwani ukichukulia puapa hutaweza kufanikiwa, unatakiwa uchunguze kwanza
mwenyewe ili ulthibitishe. Ni kuhusu hawa waume zetu…’aliposema hivyo, nikajua
ni yale yale.
‘Mimi nimesikia mengi, lakini mimi sijali, kama wana yao,
mimi siwezi kuvunja miiko yangu ya
ndoa’nikamwambia na yeye akasema kwa upole.
‘Ni kweli, najua hilo, na najua sana tabia yako, na
ulitakiwa unishukuru sana siku ile, nilipoamua kujitolea na kushika ile nafasi
yako. Kama isingelikuwa mimi , wewe sasa hivi ungelikuwa upo kwenye haya maisha
yangu, au umeshakufa kwa kihoro,….inahitaji moyo na ujasiri kama wakwangu, na
sio kwamab siumii, naumia sana…’akasema huku akizuia machozi.
‘Nikuambie ukweli, wakati mwingine najuta kwanini niling’ang’ania
kuolewa na yeye, maana mimi ndiye niliyelazimisha, na hata nikimlalamikia mtu,
nitaonekana mjinga, ndio maana nakomaa kiume, nitahakikisha tunakula sahani
moja hadii kieleweke, ingawaje najua huenda mwishoo wa siku nikaumuiamimi,
..hizi zote ni mbio za sakafuni,…’akasema na kutulia.
‘Haya ni yenu na mume wako, mimi wala sikukulazimisha ufanye
hayo uliyoyafanya, na wala sikujua mipango yenu, ‘nikamwambia.
‘Ni sawa…na nakubaliana na wewe, na msimamo huo ni mzuri
sana, lakini ni bora ukajua nini kinachoendelea mapema, kuliko kuja
kushitukiziwa…ni bora ukamjua adui yako mapemakabla hajakuingilia ndani….’akasema
na kuniangalia kwa makini.
‘Kwanini mnapenda kuingilia ndoa za wenzenu,….’nikalalamika.
‘Nani kakuingilia kwenye ndoa yako wewe!…’ akasema kwa jaziba, na baadaye
akatulia, na kusema kwa sauti ndogo ya unyenyekevu,
‘Sikiliza mpendwa, mimi sina mpago wowote wa kuingilia ndoa
yako, …niingilie ili iweje, yangu yenyewe inanishinda, ….mimi nimekuja kukusaidia
tu, kwa vile mimi yameshanikuta, …! Na kukuambia haya sio lazima ukaamini, kwasababu
hata mimi nilikuwa kama wewe mwanzoni, sikuwa naamini hayo,…’akasema na
kutabasamu kidogo.
Nilikuwa kama wewe, hivyohivyo, sikutaka kufuatilia kabisa
mambo ya mume wangu, hadi pale
nilipohakikisha kwa macho yangu mwenyewe…nikajua labda ni kwa vile
nililazimsiha hii ndoa, ndio maana ananifanyia hivi, sikujua kuwa kumbe avumaye
baharini ni papa kumbe wengine wapo…’akasema na kutabasamu, tabasamu la mbali.
Sikuamini macho yangu, na mpaka sasabado najiuliza, hivi ni
kweli au kuna kitu kimetumika…hapana, kweli tembea uone…’akasema na kuangalia
juu.
‘Macho hayana pazia…sikutaka kabisa, kukuambia hilo,lakini
limeniuma, na naona nikusanye nguvu kwa wenzangu kama tutaweza tuchukua hatua,
maana kumbe sipo peke yangu,….’akacheka kwa ile sauti ya juu kidogo.
‘Kumbe sio mimii tu, niliyetendewa huu unyama,….maana
kiukweli mwanzoni nilumia sana, niliteseka sana, nilijua ni kwangu tu, lakini nimekuja kugundua
kuwa hata kwako mambo ni hayo hayo, ila ni kwa vile hujui tu, …’akasema, na
mimi nikashituka na kutaka kujua anataka kusema nini.
‘Kama nilivyokuambia, wanaume wote wapo sawa, ni kama
shilingi ilivyo, ukiigeuza huku au huku kote ni sawa, kilichobadilika ni picha,
lakini shilingi ni ile ile,….hawa wenzetu hawariziki, hata kama wana malikia
nyumbani ambaye ana kila sifa ya uzuri,
wao wakipata mwanya wa kukutana na mwingine ambaye huenda hana hata hizo sifa alizo
nazo mke wake, lakini kwa vile kamlegezea tu,…basi keshalainika…’akasema huku
akikunja uso kuonyesha anakerwa na jambo fulani.
‘Kwani unataka kuniambia nini, mimi nimeshakuambia kuwa
sijali mambo yao, kama kuna mambo yao wanayafanya, waacha wayafanye wanavyotaka
, ni zambi zao wenyewe, ilimradi mimi sijui kwangu ni sawa tu….hayanihusu…’nikamwambia
lakini moyoni nikiwa na dukuduku,maana huyu ni mtu wa pili ananiambia mambo
kama hayo, huenda kuna ukweli.
‘Juzi nilikuwa huko Dodoma, huko wanapokutania, nilikwenda
kwa ajili ya mambo yangu ya kibiashara, huwa nakwenda mara kwa mara, lakini
mume wangu hajui, maana mimi na mume wangu ni jina tu, mke na mume,…na haya
yote labda niseme nilijitakiwa mwenyewe. Basi bwana wakiwa huko kwenye mambo ya
kisiasa, wakishamaliza yale waliyokusudia, kuna kitu kinaitwa utawala binafsi.….’akasema.
‘Mimi na wenzagu huwa tuna biashara zetu, na kunapokuwa na
vikao kama hivyo, tunapata wateja wengi, kuna biashara tuanpeleka huko kwa
ajili ya mahoteli, kwahiyo mambo mengi yanayotokea kwenye mahoteli
tunayajua,….’akasema na kutulia kidogo.
‘Ndio maananikakuambai kuwa wanaume wote ni sawa na
shilingi, unaweza ukasema mume wangu ni mtakatifu, hawezi kufanya mabaya,
…unajidanganya, kama anakunywa, ujua ulevi ulivyo,ni kishawishi chamambo
mengine, akilewa,anakuwa hajitambui, anaweza akafanay machafu hata na
mkwewe,….’akasema na kutulia.
‘Mimi sijakuelewa mpaka sasa…’nikamwambia.
‘Leo sitataka unielewe, lakini ipo siku utanielewa, …na
ukiwa tayari mimi nitakusaidia , tunaweza tukaongozana mimi na wewe mguu kwa
mguu, hadi huko, wakiwa kwenye vikao vyao ukajionea mwenyewe na hapo utajua
kuwa kumbe, niliyokuwanikiambiwa ni kweli, kumbe….mimi nilikuwa nafugwa tu ndani,
wenzangu wanaifaidi dunia,….sasa hebu angalai hii picha kwa makini, ….’akasema huku
akibonyeza ile simu yake na akanipa niangalia. Nilisita , lakini baadaye
nikasema kwani nikiangalai nitazurika na nini…
Mwanzoni sikuelewa vyema, maana niliangalia kwa papara,
lakini nilipotulia vyema, nakufautilia kile nilichokiona, ndipo nikagundua ni
nini…ilikuwa ni picha ya video, inaonyesha kabisa matendo, kwahiyo sio ile
picha ya kupiga mtu kasimama, unaweza kusema ni picha ya kugushi,, ….
Niliwaona watu wamekaa wawili wakinywa, huku wanaongea,
sauti zao zilikuwa zikisikika kwa shida maana kulikuwa na sauti za mziki wa
taratibu, na sauti zingine za watu wakiongea, kwahiyo sauti zilikuwa
zikiingiliana, na unashindwa kujua vyema wao walikuwa wakiongea nini….
Wale watu walikuwa wakinywa, na kula nyama, na ilionekana
kuwa wanaongea jambo muhimu sana, na haikupita muda, mara wakaja wanawake
wawili wakajiunga nao. Ilivyoonekana pale, ni kuwa wanajuana maana wala
wanawake hawakuonyesha kusita, kila mmoja alikwenda kukaa kwa mtu wake, na moja
kwa moja wakashikana mkono nyumba ya mgongo wa kila mmojawapo, kama wafanyavyp
wapenzi, wakabusiana kwa mahaba
‘Kwa muda ule niliwajua tu, kama wanaume, wakistarehe na
wawanwake wao, nilikuwa sijaweza kugundua ni akina nani, kwani hisia zangu
hazikuwa zinafikiria lolo te baya, …
Picha hiyo ilichukuliwa kwa mbali, lakini kila hatua ilikuwa
ikikuzwa, hadi sura za wale watu zikawa zikionekana wazi,…hapo mwili ukaanza
kunisisimuka, jaziba, hasira, zikatawala ubongi wangu, ..jasho likaanza
kunitoka.
‘Haiwezekani, huu ni ujanja wa mitandao, ….’nikasema, huku
nimetoa macho ya kushangaa, yule mwanamke hakusema kitu, alikuwa kama hayupo,
alikuwa akiangalia pembeni, kama anawaza mambo yake,hakutakahata kunisemesha au
kuniambia lolote, katulia kimiya. Nikaendelea kuangalia ile video kwenye hiyo
simu, akili kwa muda huo haikuwa yangu tena…..
Mara wale watu, kila mtu na wake, wakainuka na kuanza
kucheza mziki, na wakawa wanashikana shikana,…huku wakabadilishana, mara huyu
anacheza na huyu, na baadaye mwingine anacheza na mwingine, ilikuwa ni aibu
tupu, na uchafu mtupu, kwa watu kama hawa, ambao sikutegemea kabisa
wangelifanya mambo kama hayo, nilitamani niibamize ile simu, lakini akili
iliniambia nisubiri nione zaidi.
Baadaye nikawaona wakiondoka kila mtu na mwenzake, wakaingia
kwenye vyumba tofauti, kila mtu na wake,…na pale ile video ikasimama,….. Pale
nilipo mwili ulianza kuniishia nguvu,kwasababu kwa hali waliyoondoka nayo pale,
ilionyesha wazi kuwa hawo ni wapenzi wa siku nyingi, na huko kwenye vyumba kuna
mabaya yanakwenda kufanyika, kwani walionekana kama vile mke na mume…
‘Hayo mengine ya chumbani siwezi kukuonyesha kwa sasa, yapo
ymehifadhiwa kwa manufaa ya ubindamu, maana tuliamua kuchukua kila kitu, ila
najua wewe mwenyewe utajua ni nini
kilifanyika zaidi ya hapo,…’akasema yule mwanamke na kuinuka,huku akiangalia
saa yake, kuonyesha kuwa kachelewa anahitaji kuondoka haraka.
‘Haya niambie unanidai shilingi ngapi…?’ akaniuliza huyu
mwanamke huku akiweka simu yake kwenye mkoba wake,kama vile hakuwahi kuongea na
mimi.Mimi sikuwa na nguvu kabisa ya kumjibu, nilichofanay ni kumpa bili ya vitu
alivyonunua, na yeye bila kusema zaidi, akanilipa pesa yangu na taratibu, akaondoka
zake.
NB: Haya niambieni akina mama, kumbe ndivyo mnavyowaona waume zenu hivyo, sijui ukweli upoje, lakini ndiyo ilivyotokea kwenye hiki kisa,....tuzidi kuwepo.
WAZO LA LEO: Utofauti wa kiitkiadi, ziiwe za kisiasa, au za kijamii, zisitufanye tuwe maadui, tukasahau ubinadamu wetu, tukumbuke kuwa sote ni watoto wa baba na mama mmoja, Adam na Hawa(Eva).
Ni mimi:
emu-three
6 comments :
Tatizo ukiamini sana majungu , unaweza ukaingia mkenge.
Si wote wapo hivyo ..wazo la leo ni bonge la wazo..
Jibu ni kuwa je na wanaume wote mpo hivyo. Ujumbe umefika, kwa wenye kuelewa, twakupenda sana M3
napata mafunzo hapa angalia waume wenzio watakulaumu kutoa siri za 'vikao'
Wewe unatusaliti, mambo mengine hayazungumzwi, ....aaah, umeharibu m3
wazo la leo zuri sana,wanasiasa kama watalipata hili itakuwa poa sana.
Post a Comment