Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, July 27, 2012

Hujafa hujaumbika-76 Hitimisho-34
‘Ulimjuaje huyo Kimwana?’ nikamuuliza huyo binti, akiwa katulia , lakini hata hivyo alionekana kuwa na wasiwasi sana, kinyume na kawaida yake tunapokutana.

‘Nani aisiyemjua Kimwana, kila mtu anamjue yeye, kwa uzuri wake kila msichana anatamani kuwa mnzuri kama yeye, lakini uzuri wake kumbe ni sumu kwa maisha ya watu, na badala ya watu kuupenda uzuri wake kwa wema, umegeuka kuwa uzuri wa ubaya, na kila mmoja anataka kumharibu…’akasema huyo binti.

‘Lakini wewe alikufanyia kitu gani kibaya kwako?’ nikamuuliza.

‘Kama ana ukimwi, na mimi nimeshaupata huo ukimwi, lakini kwa ajili yake, na….na, sijui nimewakosea nini…binadamu wenzangu,….mimi ni masikini, sina baba, sina mama,…. Niliokuwa nikiwategemea kama wazazi wangu ….ooh, angalia huyu baba akaja kunigeuka kuwa na kuwa sumu ya kunimaliza mimi. Sasa mimi nina thamani gani tena katika hii dunia. Usichana wangu una maana gani tena, …’akaanza kulia.

Nilitaka kumkatiza kwa kumbembeleza, lakini nikaona nimpemuda wakumaliza machungu yake, nimuache alie kidogo, na akaendelea kusema;

‘Eti dada, mimi ni nani atanioa tena akisikia kuwa nina ukimwi, …nilitamani sana mume wa kwanza kuugusa mwili wangu ndiye atakaye kuwa mume wangu…ndio maana huyu baba aliponifanyia kitu kibaya, niliona ni heri …..ni heri niwe tu mke wake, sasa ina  maana gani,..hebu niambie mimi nimewakosea nini wanadamu wenzangu, ina maana umasikini na laana…..’akawa analia kwa kwikwi, kiasi kwamba hata mimi niliyekuwa nikimsikiliza nikawa sina amani tena moyoni

Baadaye alitulia na kwa muda huo sikutamani kumuuliza tena maswali, nikamwambia kwa upole;

‘Unajua mdogo wangu, sio kweli kuwa kila ukitembea na mwenye ukimwi na wewe utakuwa nao, na pia sio kweli kuwa ukitembea na mwenye ukimwi hutakuwa nao,…. cha muhimu ni kwenda kupima , ukipima utajua afya yako,….na utajijua wewe mwenyewe kuwa usalama au la…ni kama ikiumwa na mbu, sio lazima kuwa na malaria,lakini pia unaweza ukaambukizwa malaria,na ili ujue kuwa huna au unao ni kupima kwanza……’nikamwambia.

‘Usinidanganye kwa hilo, mimi najua ninao, lakini kabla sijatangulia, …..mmh,..we niache tu, ila dada nakuomba kitu, nakuomba nipo chini ya miguu yako..’akasimama na kuja kunipigia magoti, na mimi sikupenda kabisa hilo tendo, nikasimama na kumsimamisha.

‘Unafanya nini, mimi nilishakuambia kuwa kama una shida yoyote niambie tu, nitakusaidia, sio mpaka kunipigia magoti, unashida gani nyingine…hebu niambie mdogo wangu?’ nikamuuliza.

‘Nataka kwenda kijijini kwetu, nasikia kuna mtaalamu wa huu ugonjwa, naomba nipo chini ya miguu yako…nipe nauli, mimi huwa naoteshwa na kuelekezwa nini nifanye, …na kila inapotokea inakuwa kweli, nikipuuza najikuta kwenye matatizo, kama hayo aliyonifanyia baba, kama ningelifuatilia nilivyoelekezwa nisingelikutana na hayo matatizo…’akasema.

‘Ni nani huyo anakuelekeza?’ nikamuuliza.

‘Mimi sijui, huwa kuna hali inanijia nakuniashiria kuwa uafanye hivi, au uende mahali fulani utapata hiki, na sasa imeniambia kuwa nisipokwenda huko kijijini, nitaangamia kwa ugonjwa mbaya, na najua utakuwa huo ukimwi….’akasema akionyesha wasiwasi .

‘Unataka kwenda kijijini kwa ajili ya kutibiwa ugonjwa ambao hujajua kuwa unao, usiwe hivyo, sikia ,kesho mwambie mama kuwa unataka ukapime kwanza, ukijijua nitakuambia nini cha kufanya,…’nikamwambia,

‘Je wewe siumesema kuwa upo tayari kunisaidia, sasa nimekuomba huo msaada, wa nauli tu ….kama huwezi basi, ngoja nitatafuta kwa wengine,  lakini sio kwa huyu baba au kwa mama wa watu…’akasema.

‘Kwani unataka kuondoka bila kuaga?’ nikamuuliza

‘Baba siwezi kumuomba lolote,…sitaki hata kumuona tena, mama siwezi kumuomba kitu,kwasababu namsikitikia sana, mama wa watu mpole hana hatia leo hii watu kwa tamaa zao wanamuangamiza, yeye sitaki kabisa kumuumiza tena, na sitakuwa na raha tena nikimwangalia usoni, ..siwezi, na kama dada usiponipa hiyo nauli, basi, …labda njia nyingine, ili nisimuona huyo mama akiwa an huzuni , ….nitakunywa sumu, nife….’akasema na kuniacha nikiwa  nimeduwaa.

‘Eti nini..?’ nikasema kwa hamaki.

‘Dada hilo nimedhamiria,kama hutanipa nauli, basi …nitajua la kufanya, ….siwezi, najua nimemkosea sana mama, ingawaje sio dhamira yangu, najua …na nimejitahidi kumsaidia sana,lakini huenda isiiwe na tija, naona bado sijaweza kumsaidia itakiwavyo, sitaona raha nikimuona akiteseka, ….hapana…’akasema na hapo akaingia ndani na kuniacha nikiwa nimekaa pale sebuleni, nikiwaza.

Niliwaza sana, niliwaza hii familia, na kumuwaza mama mwenye hii familia, sijui anajua nini zaidi , sijui alipojua kuwa mume wake katembea na huyo Kimwana ambaye alikuja kugundua kuwa Kimwana kaathirika…sijui alijiskiaje. Nikaona ni bora tu nimpe huyu msichana hiyo nauli, lakini lazima nihakikishe kuwa anakwenda kupima kwanza.

Baadaye alitoka akiwa kabeba nguo zake ,akaniambia anataka kufua nguo zake, kama nitampa hiyo nauli, basi ataondoka,..kwani alishaambiwa kuwamimi ndiye ninaweza kumsadia , ..ila kama sitampa atajaribu kuomba kwa yoyote mwingine, lakini hatakubali kukaa tena kwenye hiyo nyumba,….

‘Mimi nitakupa nauli lakini mpaka unihakikishie kuwa utakwenda kupima kwanza…’nikamwambia.

‘Hilo la kupima usipoteze muda wako, ..siendi huko,…nilishaambiwa kuwa nikipima tu,basi, sitaokoka tena, hawo watu nisiowajua wamesema watainyonya hiyo damu yangu kama ina wadudu, na itaingia damu nyingine isiyo na wadudu, wewe utaona tukikutana tena….’akasema akionyesha kuwa kweli anaamini hivyo.

‘Lakini huoni kuwa hizo ni njozi tu, ni vyema ukawaona madakitari wenye vipimo halisi..’nikjaribu kumshawishi.

‘Eti nini , madakitari,  hawo madakitari wenyewe siwaamini tena, mimi nikifika huko kijijini nitajua wapi pa kwenda,….huko najua nitaweza kuwalilia wazazi wangu huko walipo, huko ndipo nilipozaliwa na kama ni kufa nifie huko huko nilipotokea, ….najua nimeshamaliza kazi yangu hapa mjini…na hata hivyo hawo watu wameshaniahidi kuwa huko nakwenda kuchukua Baraka zao, uniamini tu dada yangu…’akasema.

‘Je uliwahi kwenda kumuona nesi?’ nikamuuliza ili kupoteza lengo kwanza.

‘Hapana,…nampenda sana huyo dada, na huenda yupo kwenye wakati mgumu, lakini sina la kufanya, yeye alikuwa kama mmoja wa ndugu zangu wakaribu kama ulivyo wewe, lakini nimeshindwa hata kwenda kumpa pole….najua hana hatia…, kama nitarudi tena nitampa pole,lakini kwa sasa, mimi nataka nifike kijini kwetu….’akasema.

Nilitaka kumdadidi zaidi, lakini akatoka nje na nguo zake, alionyesha kuwa hataki kuongea zaidi bila ya kumpa hiyo nauli, ….

 Basi nilimpa nauli nikiona ndilo jambo ninaloweza kumsaidia na kumuomba sana ajitahidi kwanza akapime, na nilimwambia kwanza aongee na mama yake, kwani yeye alimchukulia kama binti yake.Hakunijibu kitu, akawa anaendelea kufanya usafi wa guo zake, na mimi nikaona sina la kufanya nikaondoka zangu.

Kesho yake nikapata taarifa toka kwa mke wa wakili mkuu kuwa huyo binti keshaondoka, na mkononi alikuw akashika barua, sikujua ni barua ya nini, nikamkaribisha na tukaanza kuongea …

‘Nilijua tu huyu binti atakuja kuondoka,lakini sikujua kuwa ataondoka kwa njia hii, nilimchukulia kama binti yangu, nikamlea nakumpa kila ambacho anastahili kupewa binti yangu,leo hii anaondoka kama tumekosana…’akalalamika mke wa wakili mkuu.

‘Ni kuchanganyikiwa  tu, naomba umsamehe…’nikasema.

‘Mimi sina kinyongo naye, ila imeniuma sana, maana sasa huko kijijini atakwenda kuishi na nani, hana wazazi kwa sasa, hana baba, wala mama, ….na nilishangaa sana,..nilishamwambia kuwa pale mimi nitamlinda hatasumbuliwa tena na mume wangu baada ay lile tukio, , lakini kumbe, mwenzangu alikuja kunigeuka, nilikuja kusikia kuwa alikuwa bado anatoka na mume wangu….’akasema kwa uchungu.

‘Ulisikia kwa nani….?’ nikamuuliza.

‘Dunia hii ina siri….na huyu nesi, alikuwa shoga yake mkubwa, nilishamkanay sana aiwe na mazoea na watu kama hawo, lakini hakunali, sasa hebu angalia hawa watu wasio na huruma na binti wa watu kama huyo, …wamekuja kumwangamiza binti wa watu akiwa bado mdogo…’akaniambia.

‘Kumwangamiza kwa vipi?’ nikamuuliza nikijifanya sijui lolote.

‘Yaani kuna watu wanyama hapao duniani, na sijui kama watakuja kusamehewa, hilo tuliache tu, maana kabla hujafa utakumbana na mengi, …’akasema na hakutaka kuniambia lolote hata nilipomdadisi sana, na mwisho wake nikamuuliza.

‘Wewe kama dakitari uliwahi kumshauri huyo binti yako akapime, …..baada ya lile tukio ?’ nikamuuliza.

‘Nilitumia kila mbinu lakini hakukubali kabisa….nilitaka kama inawezekana nimpe dawa za usingizi nimchukue damu lakini kila mbinu nilizojaribu nilikuta anajua lengo langu ni nini, sikufanikiwa…ana kitu kama mashetani, akama anvyodai yeye, kuwa yanamuelekeza, ….yaani huyo binti ana maajabu, sasa sijui kwanini hayo mashetani hayakumsaida wakati anabakwa na huyo mmwanaume….’akaniambia.

‘Na wewe je ulishapima, maana hili tunashauriana kila mtu..’?’nikamuuliza.

‘Siku nyingi, sana mimi ni dakitari, na huenda watu watashangaa, na wengine wamekuwa wakitunyoshea vidole kwanini hatuna watoto, ….niliwaficha mwanzoni, na ilitakiwa iwe siri yangu, ….lakini hata hivyo, hili nililiona mapema,….ukiishi na mume utamjua tabia yake, mimi kama dakitari, nikawa namechukua tahadhari mapema, namshukru mungu kuwa nilifanikiwa, sijui labda itokee jingine….’akaniambia.

‘Ina maana wewe umeshapima na kuwa  huna tatizo la huo ugonjwa….maana siku hizi maambukizi yapo ya iana nyingi ?’ nikamuuliza.

‘Amini usiamini mimi  sina,mungu alininyowekea mkono wake wa ulinzi mapema,…..namshukuru sana mungu,….ila niliona kuwa huyo muambukizaji ni bora aondoke hapa duniani maana hana huruma na watu kama huyo binti yangu, lakini sikupata bahati ya kumuondoa mimi dunia, ila aliyefanikiwa kumuondoa, naona kafanya kwa niaba yangu…’akasema na alisituka pale alipogundua kuwa kaongea lile alilokuwa akilikataa.

‘Una maana gani kusema hivyo, huyo muambukizaji ni nani, na kamuambukiza nani, naomba uliweke hili wazi, mimi ni wakili wako…?’ nikamuuliza.

‘Tafadhali,sana na unisamehe sana, hilotuliache kwanza..ipo siku nitakusimulia lakini sio leo…’akaniambia

‘Na unahisi ni nani muuaji wa Kimwana, maana kila mmoja anakataa kuwa sio yeye…hata nesi keshakataa kuwa sio yeye?’nikamuuliza.

‘Akate asikatae ni huyo huyo nesi, na hawara yake….hilo sina shaka nalo’akasema huku akionyesha kuwa kweli ana hasira fulani moyoni, na ana maana hiyo.

‘Je kwa kauli yako hiyo kwa kumuita mume hawara yake,….inaonyesha kuwa hujamsamehe mume wako, ..na hii nikuonyesha kuwa ndoa yenu ipo matatani, au unataka kusemaje kuhusu ndoa yenu na majaliwa yake?’ nikamuuliza.

‘Najua wengi watasema namnyanyapaa mume wangu, lakini tungalia ukweli na hali halisi,  mimi nimeamua na sitaangalia nyuma tena, ….nitakachofanya ni kuvuta subiri apone, na akitoka, naibariki ndoa yao na nesi, kwani wao wanastahiliana, na kweli wanapendana ,maana haina haja kuishi na mtu ambaye ana mtu wake wa siri, wanayependana,…mimi nimevumilia mengi kwa upande wangu, na imetosha..’akaniambia.

‘Unasema kuwa watu watasema kuwa unamnyanyapaa mume wako kwanini ufikirie hivyo..?’nikamuliza

‘Wewe ni wakili wangu, lakini siwezi kukuambia kila kitu, kuna mambo  mengine yakitaaluma yangu, nahitajiwa kutoyasema, hilo najua hata wewe unalifahamu, kama ipo siku utastahili kuambiwa utaambiwa lakini sio kwa sasa, nakuomba unielewe kwa hilo, wewe chukua hii barua yako toka kwa huyu binti, sijui kakuandikia nini,labda kuna jambo linanihusu, kama lipo naomba uniambie ili nijue kwanini kaamua kunikimbia….’akaniambia.

‘Ina maana wewe ulipoiona hii barua hukutaka kabisa kuisoma kwanza…ili ujue kwanini kaondoka, na ina maanahakuacha ujumbe wowote kwako….,?’nikamuuliza.

‘Mimi sina tabia hiyo,…hiyo barua unaona jinsi ilivyofungwa, na imeandikwa jina lako…huyo muandikaji alitaka hii barua ikufikia wewe mwenyewe, anakuamini sana kuliko hata mimi,na mimi sina tabia ya kupkenyua viti vya watu kama kweli havinihusu, naheshimu sana maadili yangu…’akasema na mimi nikaifungua ile barua na kuanza kuisoma.

Ilikuwa barua ndefu, na sijui alianza kuiandika lini, maana ilielezea mambo mengi sana, maisha yake hapo kwenye hiyo nyumba, na mengine ambayo alishawahi kunielezea, na kuna sehemu alianiagiza kuwa nikapate uhakika kwa nesi, yeye ataniambia zaidi, na nilipofika sehemu ya mwisho wa hiyo barua ndipo nikakutana na maelezo ambayo yalinifanya mwili mzima usisimukwe,….nilihisi kizunguzungu,…sikuamni hadi nilipokutana na nesi,ambaye aliniithibitishia hilo.

‘Kweli nesi, alikuwa mtu wa pekee sana…..’

NB Natamani niendelee lakini muda hautoshi, tukutane tena kwenye sehemu iliyobakia.

WAZO LA LEO: Siku zite hazilingani,…usiwaze sana ukiona mambo yako hayaendi vyema, ujua kuwa katika kuhangaika kote kuna kupata na kukosa. Ukipata mshukuru mungu, na halikadhalika ukikosa mshukuru mungu wako.

**********************************************************************************


KUTOKA KWA WAZEE WETU: Hili nimeipata kutoka kwa mzee wetu mstaafu, ambaye katika maisha yake yote amekuwa kazini, kutoka ujanani hadi akaja kustaafu, na alipostaafu, kaingia kwenye kazi ya ulinzi,…kwa umri huo alio nao, asingelistahili kufanya hiyo kazi, ilitakiwa kukaa na kula pensheni yake…lakini hiyo pensheni ipo wapi?’

‘Sio kwamba napenda kuifanya hii kazi, bali ni hali halisi ilivyo, miaka mingi nilikuwa kazini, mtiifu ,mchapakazi hodari, na hata nilipotoka pale kazini niliacha jina langu likiwa ni maarufu, lakini nini nilichokipata baada ya kupewa ile barua ya kuwa nimestaafu, ni mishahara yangu miwili, na kuambiwa nikachukue pensheni yangu.

Hela iliyokuwa ikikatwa kwenye mshahara miaka yote hiyo, haikunisaidia kitu, kwasababu ilikuwa ni pesa ndogo kutokana na mshahara wangu, kama ningeliitumia muda ule ilikuwa na thamani, angalau ingenunua kitu, lakini kila muda unavyokwenda thamani yake hushuka….mia ya jana sio sawa nay a leo.

Haya nikahangaika mpaka nikaipata hiyo inayoitwa penshion,  niifanyie nini..ikawa ni tatizo jingine,kwani haiwezi kufanya lolote, ….na ukumbuke kuwa mimi wakati wote nilikuwa mtu wa kutumikishwa kwenye maofisi, sijui biashara na wapi pa kuanzia,…lakini haina jinsi nikaamua kufungua kigenge,…balaa likaniandama, wakaja hawa watu wa city na kuvunjwa hilo genge na watu wa jiji, na vitu vyote, mtaji wote, ukaguduka, sina mbele wala nyuma, watoto wengine bado wanahitaji ada, wanasoma, nifanyeje,…nikaona ndio nitafute kazi hii ya ulinzi.

`Wazo langu kwa wenye makampuni,..matajiri …’akamalizia huyo mzee kwa kusema, `Angalieni sana wazee waliotumikia makampuni yenu, wajalini wanapoondoka,wao walijitolea sana…angalau wapeni kitu cha kuanzia maisha, hiyo mishahara miwili na hiyo pensheni haitawasaidi lolote….wazee ndio Baraka ya mafanikio yenu…au ndio tusubiri pension ya kuzikiwa, kwani ndio ilikuwa lengo langu kuwa nifanye kazi kwa ajili ya kuja kuzikiwa?


Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Hii imetumwa kwenye e-mail na mpendwa mmoja,anasema;

Hongera sana mkuu, haya mawazo yako kama yangelikuwa yanapitiwa na hawo jamaa mbona ingesaidia.

Akauliza hivi;

Hivi mkuu hivi visa unaviandika saa ngapi na je ni vya kweli, na hizo picha zao unazipata wapi, na je ni wahusika kwenye hivyo visa?

Mpenzi wa blog yako