Kila nilipotaka kutuliza kichwa cahangu, sikuweza,maana ile
kauli niliyoisikia toka kwa yule dada iliniandama na kunifanya nijione kuwa
huenda mimi ndiye mkosaji, ingawajesilijui kosa langu, nikawa nahangaika kuutafuta
usingizi, lakini kama niliupata ukawa wa mang’amung’amu.
Na baadaye nikapata
usingizi lakini ndani ya usingizi huo nikajikuta nikiwa situlii, mandoto ya ajabu, ajabu ya kutisha, na mwishini
kabisa, nikaota naelea hewani,kama ndege, huku nikitafuta sehemu ya kutua.
Nikiwa hewani zile nguvu za kukaa hewani zikawa zinapungua,
na ghafla nikatua kwenye paa la nyumba. Nilipotua nikajikuta nikiteleza kuelekea
chini , maana paa lenyewe ni la bati, na lina umande wa usiku, kama vile
kulinyesha mvua.
Kwahiyo nikawa na akzi nyingine, ya kujizuia nisiteleze
nakuserereka kwenda huko chini ambapo sipajui papoje,na nikawa nahangaika
kutafuta sehemu ya kushika ili niweze kutafuta mwanya wa kushikilia na baadaye
nishuke chini taratibu, na wakati nahangaika hivyo, nikaweza kuangalia chini
aridhini.
Kule chini kulikuwa na miiba mirefu, kama vile miti
iliyochomekwa na juu yake kuna ncha kali kama ya mishale, ambayo kama ningeliachia pale juu na
kuporomoka chini, nikaangukia kwenye hiyo miba, basi mimi ningelichomwa na ile miba na kuwa
kama mshikaki ulichomekwa kwenye miti,
…nilipoona hivyo, nikaingiwa na wasiwasi mkubwa, nikawa najitahidi
kushika huku na kule,….na mikano sasa ikawa anachoka kushikilia sehemu ile
ndogo niliyoipata.
Nilihangaika kwa muda, na jinsi muda ulivyokuwa ukienda
ndivyo name mwili ulivyozidi kukosa nguvu,nikawa nimechoka, na hali ilivyokuwa
ilionyesha dhahiri kuwa sitaweza kushikilia tena, kwa vyovyote vile nitaanguka
chini, …nikajaribu kutafuta sehemu ambayo hata nikiangukia nisije nikachomwa
sana, …..na hapo hapo mikono ikawa imeshachoka, na sikuweza kushikilia tena,
nikaachia na kuanza kuserereka….
Nikiwa sasa nipo hewani, naeleeka chini, nikawa namuomba
mungu anisaidie ili nikitua chini, nisije nikachomwa na roho ikawa haitoki
haraka , na kuanza kuteseka na maumivu, yaani kama inawezekana nife haraka hata kabla
sijapambanana hayo machungu ya kubanikwa kama mshikaki, na mara nikasikia sauti
ikisema;
‘Wewe unaomba upate huruma ya mola wako, mbona wewe huna
huruma na wenzako?’ sauti ikiniuliza.
‘Huruma kwa watu gani?’ nikauliza huku nikiahangaika
kuangalia chini, ….lakini sikuweza maana ilionekana kuwa sehemu ile ndefu hadi
kutua chini.
‘Unatakiwa kwanza uwaharumie wenzako, kama unavyojihurumia
wewe mwenyewe, je hilo unafanya, hebu chunguza katika maisha yako, ni mangapi mabaya
uliyoyafanya yakasababisha wenzako kuumia, hebu jiulize hakuna mtu yoyote
uliyewahi kumuumiza katika maisha yako, wewe unaogopa jeraha, je hakuna lolote
baya ambalo kwa kulitenda kwako, kwa nafsi yako, likawa ni jeraha kwa wengine,,?’
nikaulizwa
‘Kwakweli sikumbuki,…. je ni nani niyeliyemuumiza hivyo?’
nikauliza.
‘Hebu jiulize mwenyewe , kweli hakuna katika maisha yako,
uliyemuumiza sana moyo wake, na kila siku anateseka kwa ajili yako, ….’ile
sauti ikasema.
‘Ni nani huyo…mbona mimi simuelewi,…..ni nani huyo?’
nikauliza.
‘Mara ni wepesi sana kujiona hatuna makosa, na wepesi sana
kuone wenzetu wana makosa, kama ilivyo wepesi sana kumnyoshea mwenzako kidole.
Na pale inapofikia sehemu ya kummwangalia mwenzko kwa jicho la kumsaidia
inakuwa ni uzito sana, lakini inapokuja kuwa unataka wewe kusaidiwa kwako
inakuwa ni wepesi sana….’ila sautiikasema.
‘Sijaelewa…kwanza ni nani huyo niliyemfanyia hayo mabaya…?’nikajitetea
na kuuliza.
‘Ni yule anayeumia ndani ya moyo wake, maumivu ambayo
hayadhihiri wazi, lakini maumivu hayo ni makali kwake,kama kuchomwa na miiba
mwili mzima,na kubanikwa kama mshikaki,…kutokana na hayo maumivu amekuwa kama
mfu,aanyeelea hewani, akitafuta wapi pa kutua, lakini kila anapojaribu anakuta
kuna miiba ile ile…
‘Haiwezekani, niwe mnyama kiasi hicho…ni nani niliyemfanyia
hivyo….?’ Nikauliza.
‘Hebu jiulize wewe umeonja angalau shida kidogoo tu,
ukatamani kufa, ..na sasa hapo ulipo unaomba ufe haraka kabla ya kupata hayo
maumivu, umesahau kuwa kuna mtu ambaye amekuwa akiumia miaka mingi,…wapo ambao
hawana hili wala lile, hawana macho, hawana masikio, hawana kiwiliwili, na kuna
ambao waanteseka mioyoni mwao, mika mingi , hawapati lepe la usingizi, ..na
hata kufikia kutaka kujiua ….’ila sauti ikasema.
‘Ni nani hawo ?’ nikauliza.
‘Wapo watu, lakini pia
yupo mtu ambaye amekuwa akiumia moyoni mwake toka udogo wake, hadi sasa,
bado anaumia,…akiwa anahangaika kutunza
ahadi yake,… lakini wewe hukuweza kabisa kuitunza ahadi yako,….unakumuka hilo?’
ile sauti ikaniuliza.
‘Sikumbuki….naomba unikumbushe ?’ nikasema.
‘Ni rahisi kwa mtu kusahau wema aliotendewa, hasa pale
anapokutana na raha za dunia , ambazo ni za kupita tu, kumbuka kuwa wema katu
hauozi, na mtenda mema…aghalabu hana thamani kweney uso wa dunia, lakini….’ila
sauti ikawa kama inapotea.
‘Nani huyo alinitendea wema…?’nikauliza.
‘Ni yule anayetunza ahadi yake, anayetunza dhamana,
aliyokabidhiwa, na huyo alifanya kwa ajili yako, cha ajabu wewe sasa huna habari
na yeye, wewe unachojali ni hisia zao,
je yeye hisia zake atazijali nani….ujue kabisa ili dua za mja zikubaliwe kwa
mola wake, inabidi moyo wa muombaji uwe safi, utubu dhambi zako,na ukiri kabisa
kuwa hutarudia tena,….je wewe umeshafanya hayo….?’ Akaniuliza.
‘Dhambi gani hizo na nimemfanyia nani…mbona unazidi
kunichanganya?’ nikauliza huku nikiangalia chini, na kujikuta ninakaribi akutua…nikasema.
‘Naomba kwanza uniokoe na hili janga,…ninakiri kuwa nitatubu
dhambi nzangu, naomba msamaha kwa wale wote niliowakosea, na kama nikipata
nafasi nitawapitia mmoja mmoja, niwaombe msamaha….naomba…..’nikawa nalia pale
nilipohisi nikigusa ncha moja ya zile miiba, na ule uchungu wake ukanifanya nipige ukulele…..
Na ghafla nikashituka na kuruka kitandani, …nilijikuta mwili
mzima umelowana jasho, nikajpapasa ubavuni pale nilipohisi ile ncha ikinichoma,
na kwa mbali nilihisi maumivu, na nilipochunguza pale kitandani nikagundua kuwa
kulikuwa na sindani ya kushonea nilikuwa nimeishahu hapo kitandani, na ndiyo
iliyonichoma.
‘Kumbe ni ndoto tu bwana,…nikajipa matumaini, lakini nfasini
nilikuwa nikiwaza mengi, nikijua kabisa hiyo ndoto ina ujumbe maalumu, ambao
natakiwa kuufanyia kazi,.
Nikawa najiuliza ni nani huyo aliyekuwa akinipa huo ujumbe,
ni mwenyezinungu,….nikawaza sana bilakupata jibu, na hapo hapo nikajiuliza tena,
na ni dhambi gani nilizofanya,na nilimfanyia nani, ….hadi inafikia hatu hii,
maana kweli nihisi kuwa ni mkosaji, haiwezekani niwe katika maisha ya dhiki
kama hayo, na baadaye nikajiandaa maana kulikuwa na kikao nyumbani kwa wakili
mwanadada. Alinihitaji niwepo.
Nikiwa najiandaa ndio nikakumbuka tukio la jana, wakati
nikiwa nyumbani kwa mwanadada, ujio wa
yule dada rafiki wa mke wa wakili mkuu. Ilikuwa ni tukio nisilolitarajia, ingawaje
nilikuwa na hamu ya kumuona huyo mwanadada, lakini alipokuja hapo hakuwa na
muda wa kuongea na mimi, alikuja kwa ajili ya kukutana na wakili mwanadada kwa
ajili ya kesi yao.
******
‘Ohh, pole sana nilikuwa nakuja huko kukuona,….’nikasema
baada ya kuduwaa kwa muda pale nilipofungua mlango, na kujikuta sina neno la
kusema kwa sekunde kadhaa. Yeye alikuwa kasimama pale mlangoni akiniangalia kwa
makini, huku akionyesha dhahiri kuwa amechoka, uso wake ulionyesha kuliochoka,
na ilionyesha wazi kuwa ana usingizi, …na yela macho..oh.
‘Wakili mwanadada nimemkuta?’ akaniuliza baada ya kuniona
nimeduwaa na sisemi kitu kwake.
‘Ndio ume-me-mkuta yuuu-po ndani, karibu..kari---ribu
nikuitieee?’ nikasema.
‘Hivi wewe huwa unashida hapa kwake…?’ akaniuliza huku
akionyesha kushangaa.
‘Hapana mimi nilikuja mara moja kwa ajili ya kujua nini
kinaendelea huko mahakamani’nikasema.
‘Kwanini usifike mwenyewe , unasubiri kuulizia ina maana
huna uchungu na hawo wenzako, hujui kuwa mengi yanaweza kuwa wewe ndiye msababishaji
….’akasema na kukumbuka kauli inayofanana na hii aliyowahi kuniambia siku za
nyuma.
‘Samahani kama nitakuuliza swali ambalo linaweza kukukazwa,
maana nakumbuka uliwahi kusema kauli kama hiyo hiyo, siku za nyuma. Ukanituhumu
kuwa mimi na wakili mkuu tunahusika kwa anmna moja au nyingine na sisi ndiye tuliyesababisha
haya yote, lakini sijui kuhusika kwangu kukoje, naomba unifahamishe ili nisiwe
nawaza jambo nilislolijua…’nikasema.
‘Kama hulijua mpaka sasa, ina maana halikuumizi akilini, na
kama hujui lolote mpaka sasa, basi haina maana hata kukuambia lolote,maana
haikugusi moyoni,…mimi ninashangaa kabisa,ina maana wewe hunalolote unalolijua
kuhusu hii kesi, ..huna lolote unalolijua kuhusu mtu yoyote mle kwenye hiyo
kesi, hakuna mtu anayekugusa katika hii kesi,…’akawa kama anapepesuka,….
‘Ooh, ingia ukae naona una kizunguzungu…’nikasema na kutaka
kumsogelea lakini akanyiosha mkono kama kunizua nisimsogelee.
Akasema;
‘Ina maana kweli wewe …..hunikumbuki hata mimi,….hapana
najua ni kwasababu huna lolote kunihusu mimi….sawa, lakini hata kiubinadamu,….ulitakiwa
kufika kuangalia nini kitaamuliwa,?’akasema kwa huzuni, na nikaona kama machozi
yanamlenga lenga.
‘Sio kwamba hainiumi kuhusu hii kesi, inaniuma sana,..na
nawajali wote,… na ningelifurahi kusaidia kadri ya uwezo wangu, lakini kwa
mfano leo, nilikuwa na mzigo naumalizia kama ujuavyo mimi sina kazi, kazi yangu
sasa ni pale ninapopata mzigo naufanyia kazi, …., nauuza ukiisha naagiza
mwingine, na pesa ninayofanyia hivyo ni ya mkopo, nikizubaa, nitashindwa hata
kulipa mkopo wa watu..kwahiyo….’nikatulia nilipomuona wakili mwanadada akitokea.
‘Oh,samahanini, sikujua kuwa kuna mgeni, ooh, endeleeni
kuongea… lakini kwanini mnaongelea mlangoni, mkaribishe mwenzako ndani, maana
namuona kachoka, ingia ndani muongee kwa nafasi….’akasema.
‘Aaah,mimi sina muda, nitaongeaje na huyu mgeni…., mtu
ambaye anajifanya hanijui, hanikumbuki…haina haja, na hata hivyo akili yangu
hapa imechoka, nina usingizi wa kupindukia, naomba tu, nijue nini kitaendelea
baada ya hii dhamana, maana tumeipata hiyo dhamana, na mimi nimekuja kwako kwa
ombi moja kuwa kama inawezekana uwe wakili wangu,…..nitajitahidi
kukulipa…’akasema na kuonyesha kweli amechoka, maana hata kuingia pale ndani
alikuwa akipepesuka.
‘Upo safi lakini..nakuona kama unapepesuka…..oooh, unaona…upo
safi kweli wewe?’akauliza wakili mwanadada huku akikimbilia kumshika.
‘Ni usingizi na uchomvu….’akasema nikiwa mimi nimeshamuwahi,
kablahajanguka, akawa mikononi mwangu, nilimuwahi na kumdaka,…na nilivyomsika, akawa kama kanilalia, na ile hali ilinifanya
moyo wangu uzidishe mapigo ya moyo….
‘Oh, samhani….naona hali yako sio shwari..l’nikasema.
‘Hali yangu haina shaka, nahitaji kulala kidogo…’akasema
huku akijitoa mikononi mwangu na ikawa kama vile ananisukuma nisimshike.
‘Kwa ajili ya afya yako ni vyema ukajipumzishe, hata kama
ukitaka unaweza ukajipumzisha hapa kwangu, …’akasema wakili mwanadada.
‘Hapana nakwenda kwangu, siku ya ngapi sasa sijaweza kuingia
kwangu,…nilifika nyumbani mara moja, halafu nikakimbilia kuja huku…kwahiyo
ngoja nikaangalia usalama wa sehemu yangu,….hata hivyo bahitaji kujipumzisha
nikiwa huru…. usijali mpendwa…’akasema na huku akijiandaa kuondoka.
‘Wewe kakusanye
nguvu, maana kesi yenu ni kesho kutwa, tumeomba ifanyike haraka iwezekanavyo
,maana kila kitu kipo tayari, na hatutaki ipoteze muda tena na matokea yake
lolote linaweza kutokea, kwahiyo leo na kesho una muda wakujipumzika,cha muhimu
ni masharti ya dhamana, kuwa hutakiwi kusafiri…’akasema wakili mwanadada.
‘Usiwe na sahaka, na je kuhusu wewe kuwa wakili wangu
unasemaje?’ akauliza huku akiniangalia kwa jicho la kujiiba.
‘Hilo usijali,na usiwe na shaka, kila kitu kitakwenda
shwari, wewe usiwe na wasiwasi wowote,mambo yote yapo shwari,…huhitaji wakili…nakuhakikishia
hilo’akasema wakili mwanadada na kuniangalia mimi kama nina la kusema, na mimi
nikafungua mdomo na kusema;
‘Ngoja nikusindikize, maana ulivyochoka,unaweza ukalala
njiani..’nikasema.
‘Hapana, tafadhali, ninachohitaji sasa ni kufika nyumbani na
kulala, sio kuongea na mtu, na wala sihitaji kuwa na mawazo na mtu, nitakunywa
dawa zitakazinisaidia nilale vyema, wewe endelea na mambo yako, siku ya kuongea
na mimi tutaongea kiukweli, na nahitaji majibu ya maswali yote….’akasema na kuanza
kuondoka.
‘Maswali….’nikasema nay eye akageuka na kuniangalia, safari
hii alionyesha uso wa kucgangamka, akasema;
‘Ndio maswali…..umeyasahau eehe…kwaheri….’akaondoka.
Majibu ya maswali gani…’nikajiuliza.
‘Unalo hilo, tafuta majibu ya maswali yote uliyowahi
kuulizwa,…’akasema wakili mwanadada huku akitabasamu.
‘Maswali gani hayo?’ nikauliza.
‘Utakuwa unayajua ni maswali gani, …ni swala la kutulia na
kutafakari kwa makini, wewe nenda katafakari kwa makini,…..’akaniambia huku
akinisindikiza nitoke nje,maana na yeye ailionekana kuchoka, alikuwa akihitaji
muda wa kupumzika,…nikawa najivuta kutoka nje.
Nikawa sina jinsi, nikatoka nje,na badala ya kuondoka moja
kwa moja, nikawa nimesimama pale nje ya mlango, nikijiuliza mwenyewe kichwani, hayo
maswali ni maswali gani, na kwanini kila nikikutana na huyu mwanadada ananiacha
nikiwa na mawazo mengi,na kwanini iniwie vigumu kwangu kumjua, wakati yeye
inaonyesha wazi kuwa ananifahamu….kama ni kweli ndiye huyoo ninayemfahamu,
kwanini asiniambie moja kwa moja.
Nikafika nyumbani kwangu,na mwenye nyumba yangu, akaniambia
kuna mgeni alifika hapo akiniulizia
‘Mgeni gani na yupoje?’ nikamuuliza.
‘Ni msichana mmoja anasema anatoka kijijini kwenu…’
‘Msichana?’ nikauliza.
‘Ndio…mnzuri kweli, lakini alionekana kuchoka sana sijui ni
kwasababua safari ndefu,…aansema atakutafuta kesho…’akaniambia.
‘Yupoje…anafananaje..?’ nikauliza
‘Nimekuambia ni mrembo, mnzuri….siwezi kumueelzea sana, …hata
hivyo mtaonana nye kesho, jina lake hakuniambi, ila anasema wewe mnajuana toka
utotoni…’akasema.
‘Anasemaanatokea kijijini?’nikauliza.
`Ndio, na alikuwa na begi la safari kabisa….’akaniambia.
Nikaingia ndani
nikiwa an mawazo mengi, huyu mgeni ni nani ambaye tulikuwa tukijuana naye toka
utotoni, …isije akawa ndiye Tausi binti Maringo halisi,….
NB: Hii ni sehemu ndogo ambayo inatukaribisha katika
kumalizia hiki kisa, nahisi mengi yatakuwa yameeleweka, kilichobakai na
hitimisho kamili.
WAZO LA LEO: Mapenzi
ya kweli hutoka kwenye nafsi, umbo na sura ni vichachizo vya kuvuta hamasa,
lakini matendo mema,na tabia njema ndiyo dira ya mapenzi ya kweli.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment