Niligeuza
kichwa huku na kule sikuona mwanaume hata mmoja katika mkutano huu nilioalikwa
nikashangaa na ilifikia hatua kutaka kutoka nje, lakini nikatulia kimiya,...nikikumbuka
ujumbe nilioupata toka kwa mwanadada mmoja, mwana dada huyu ndiye yule
niliyekutana naye kule hotelini akiwa mmoja wa wahudumu.
‘Nina
ujumbe wako,...nataka kukupa...’aliniambia.
‘Hata mimi
nilikuja hapa nikiwa na maongezi na wewe...kuna kitu nataka kukuuliza....’nikamwambia.
‘Hapana, nakushauri
kwanza angalia huo ujumbe na fuatilia....ni muhimu sana , ukitoka huko utakuja
uniambie nini unachotaka kuniambia,...kama nilivyokuambia unatakiwa uwe na
tahadhari na..na mke...wako, kwani upo ndani ya mtego mkubwa....’akaniambia
huku akiangalia huku na kule.
‘Mbona
hunifafanulii, kila tukikutana wewe unanipa mambo juu, juu, na ...mengi
nimeshaanza kukutana nayo, inaonekana unajau mengi kuhusu mke wangu sijui na
nani....’nikamwambia akacheka na kusema;
‘Sijui
mengi kuhusu mkeo,...tafadhali ondoka..nipo kazini...’akasema na kuondoka, mimi
nilichukua chakula nilichotumwa na bosi wangu nikarudi kazini, ...siku hizi
bosi wangu kabadilika kabisa, alikuwa hakai ofisini kama kawaida yake, au
kuniita ita ndani, ....na wala hakutaka kuongea na mimi, akija ananituma
chakula halafu anaondoka zake, nikashangaa kuna nini kikubwa kinaendeela, na
siku hiyo nikaamua kumuuliza;
‘Vipi bosi
mbona umebadilika sio kama ile mara ya kwanza...?’ nikauliza.
‘Nyie mitu
mibaya sana...sitaki hata kuongea na wewe, na ingelikuwa naweza ningelishafukuza
kazi weye, lakini.....ipo siku ..ondoka nenda fanya kazi ako...’akaniambia na
mimi sikubisha nikaondoka kufanya kazi yangu, huku nikiwaza,....kuna nini
kimetokea au ndio ile simu imeshafiksha yale yaliyofanyika siku ile....
Pamoja na
hili , nimekuwa nikitumishwa katika maswalamwengine, ambayo sikuyapenda,
nimejikuta kama changudoa wakiume,..wakutumwa, nikutane na mwanamke huyu na
yule na yanayotakiwa kufanywa nai yale yale niliyomfanyia bosi wangu, na hili
likafikia hatua nikaona sio vyema, ni bora tuongee vyema na mkewangu, kwangu
sasa imetosha, sasa basi...lakini kuna huu ujumbe natakiwa kuufuatilia....
*******
‘Hiki ni
kikao maalumu, ni kikao cha ushauri, kikao cha kukumbushana na
kuelimishana...hiki ni kikao maalumu cha akina mama,...cha kupeana majukumu,
mpo tayari...’akasema mwendesha kikao...na wakati watu wanajibii kuwa wapo
tayari, akanigeukia kuniangalia mimi;
‘Ingawaje
kuna mwanababa mmoja hapa tumemwalika hapa kwasababu maalumu...tunakuomba
mwanababa usijisikie vibaya tukitumia hiyo lugha ya kikao maalumu cha akina
mama, wewe hapa umealikwa kwa kazi
maalumu, ili ujue umuhimu wa akina mama na majukumu yao. Na baadaye tutakuwa
na mazungumzo maalumu na wewe...
Hapo kidogo
nikaingiwa na hamu ya kukaa kumbe nimealikwa kama mgeni maalum, sijui hayo
mazungumzo maalumu ni mazungumzo kwasababu gani. Nilikumbuka ule ujumbe ulikuwa
na masharti kuwa nisiende na simu au saa, na tulipofika hapo mlangoni
tulikaguliwa na vyombo maalumu.
‘Kama
mnavyojua sisi akina mama ndio walezi, tunaolea watoto na waume wetu, hilo ni
jukumu letu na kama yupo mwanamama hajui hilo,bas hajakamilika kuitwa
mwanamama. Hebu jiulize kwanini hakuna kitchen party ya wanaume...hilo ni jambo
dogo tu, wengine watadai ni kwasababu ya kukusanya vyombo vya jikoni...ukiwaza
hivyo utakuwa na ufinyu wa kutafakari, na wengine wakifika pale wanaleta mzahamzaah
tu, hasa wale ambao hata ndoa hawaijui, mnatia aibu na vitendo vichafu,
kwasababu waankuwepo hapo hawajui nini wanatakiwa wakifanye...’akasema huyo
kiongozi au mwenyekiti.
‘Mimi sio
msemaji hapa tuna wataalamu mbali mbali, kuna wataalamu kama madocta, kuna
wataalamu wa haki za akina mama ,jinsia na watoto, kuna kungwi , na kuna
wataalamu maalumu kwa hili tunalotaka kuliongelea hapa,na kabla ya kuongea
kwanza kuna kuhojiana, hilo tumelianza kimiya kimiya...kujuana na kuelezana
nini hasa kilichotuleta hapa nakama unakubaliana nalo, au vipi , na
ukikubaliana unakula kiapo..ndio maana ya kuandikishana palemlangoni..’akasema.
‘Sasa na
mkaribisha mama kungwi huyu tunataka atukumbushe kidogo majukumu ya kina mama
ambayo yameshahaulika na matokeao yake ndiyo haya, kunatokea watu wengine,
ambao mimi naweza kuwaita ni mawakala wa shetani, ..wengine wataona natumia
lugha chafu, lakini sioni neno jingine la kuwaita hawa watu. ...’akasema huku
akingalia huku na kule.
‘Kama mtu
unajifunza jambo sio kwa nia njema utaitwa nani, ....wewe unajifunza mambo ya
ndoa, lakini sio kwa ajili ya ndoa, ni kwa ajili ya kuharibu ndoa za watu, wewe
tutakuita nani,kama mtu unadiriki kufanya uchafu ili uje uwachafue wenzako wewe
tutakuita nani....lugha ya moja kwa moja wewe ni shetani tu...’wakina mama
waliopo hapo wakashangalia,
‘Karibu
sana mtaalamu wa mambo ya ndoa....tupashe kidogo kungwi wangu, maana mimi
nimefundwa na huyu mama, ndio maana ndoa yangu inapeta, tuna raha , tuna Baraka,
hatuna shida...’akamkaribisha mama mmoja ambaye lipoinuka ukumbi mzima
ukalipuka kwa shangwe, hapo ndipo nikajua kuwa kumbe wapo wakina mama wengi kwa
upnde wa juu, hapo nilipokuwa nimekaa nilikuwa siwaoni vyema.
‘Nashukuru
sana mwenyekiti, na nikianza moja kwa moja naweza kusema, wakina mama
tumechangia kwa kiasi kikubwa kuvunjika kwa ndoa zetu, hata kama nyingine
hazijavunjika, ila zipo mashanini, watu hawan raha, kila siku kulalamika,mume
wang hivi...kimpandakimeshuka....ndoazetu hazipo kama zilivyotakiwa ziwe ,
...ndoa ilitakiwa iwe sehemu ya raha, kuliwazana, kupendana, kuheshimiana,
...lakini je hiyo ipo kweli, siri ya mtungi aijua kata...tumekwepa majukumu
yetu....’akasema na kufungua makabrasha yake.
‘Sisi ndio
walenzi wa watoto na waume zetu ndio kauli mbiu ya kikao hiki, anzia kuchukua
maana halisi ya ulezi utaona kuwa muhusika mkuu ni mwanamke, mume ni kiongozi
tu wa familia, katibu ni mwanamke,.... lakini huyo kiongozi hataiweza kazi yake
kama hakulelewa vyema, ...hakutayarishwa vyema, ndio mama unaona katika picha za
video yupo muhusika mkuu, lakini hataiweza ile kazi yake kama hakuyatarishwa,
hakuongozwa vyema....sisi ndio watayarishaji, sio ndio walezi,sisi ndio familia
...’akatulia kidogo.
*******
Mimi nikiwa
nimetulia kimiya huku huyo mwanamama akiongea, nilijaribu kuwaza mambo
yanavyokwenda hadi hapo nilipofikia,ilishafikia mahali niamue kufanya unyama
niishie zangu kijijini, au hata nikifungwa basi, maana sina uhuru tena,
nimewekwa kwenye sehemu ambayo kazi yangu nikuamrishwa tu,leo nenda hapa
utakutana na mama mmoja, fanya hivi na vile, baadaye unaweza kusikia hiyo
mwanamama kadondoka na kuzimia au ana haha
huku na kule kutafuta pesa...
Jana tu
nilijikuta na wakati mgumu, nilipokamatishwa na mama mmoja wa muheshimwa,
nilipotoka hapo, yule mama alinipigia simu akaniambia kuwa akikutana na mama
ama zake ama zangu, nilijaribu kujitetea lakini alikata simu,....kwa hali kama
hiyo nikawa natembea kimashaka sijui itakuwaje baadaye licha ya kuthibitishiwa
kuwa ninalindwa kila mahali ninapokwenda.
‘Kila
unapokwenda hakikisha una simu yako , na hii saa ivae mahali popote kwa usalama
wako,kama ukiwa kwenye hatari ni rahisi sana kujulikana na kuokolewa mara
moja...’aliniambia mke wangu. Lakini leo sikuja na saa wala hiyo simu, nikifuata
maagizo niliyoambiwa. Mwanzoni nipopata huo ujumbe nilizania isije ikawa ni
mtego wa hawo watu wenye hasira na mimi.
Mawazo
yakarudi kikaoni tena kumsikiliza huyo mwanamama, maana alikuwa akiongea vitu
vizito...nikamsikiliza kidogo;
‘Imefikia
hatua sasa tunadai usawa,....hebu tuulize usawa ni upi tunaodai, usawa wa kuwa
sana na wanaume,..au usawa wakukwepa majukumu yetu kama wanawake, au usawa upi
huo tunaodai, wengi hatujui hilo, tunafuata
mkumbo tu, ...tunadai tu usawa, tukae kwenye viti tukunje nne, wanaume nao
waingie jikoni,au sio, tukae chini wanaume nao wafanye yale wanawake
wanaofanya, inawezekana kweli,...haya waambieni wakabebe mimba....sio ndio
usawa huo, wengi hatujui huo uswa unaotafutwa ni usawa wakitu gani...mnaujua
huoi usawa?’ akauliza na baadhi ya wanwake wakasema;
‘Tunaujua
na unawezekana....’halafu kikafuatia kicheko.
‘Hiyo ndio
kauli ya wengi inawezekana, na matokeo yetu ndio hayo yanayotokea sasa, kuwa
tunakwepa hata yale majukumu ya asili, ..majukumu ambayo mungu katuumba nayo,
ambayo tukiyafanya sisi kama wanawake, yanaleta tija ba Baraka, lakini
tukiwaachia wanaume, uwezekano wa kuwa kama ipasavyo ni nusu kwa nusu...matokea
nyumba zinabakia kama mahema na mashetani wanakuja kujipenyeza na hata kujenga
nyumba....’akasema na kutulia.
‘Ndugu
zanguni, ndoa inajengwa na mke na mume, na asilimia kubwa ya ndani ya ndoa,
inashikiliwa na mwanamke, ukitaka kujua hilo jaribu kuchunguza majukumu yote ya
ndani utaona muhusika mkuu ni mwanamke,...ndio maana nasema mwanamke ndiye
mlezi, ....sio ulezi kwa watoto tu, bali hata malezi kwa waume zetu...’akasema
na wanawake wengine wakaguna.
‘Mimi nina
miaka thelathini na mume wangu, watu wanasema labda nimempa mume wangu limbwata,
kwa jinsi gani mume wangu anavyokuwa karibu na mimi...kweli ninakiri kuwa nimempa
limbwata....’akasema na watu wakacheka.
‘Lakini sio
limbwata la dawa zenu za kiganguzi, ...ni limbwata la mapenzi..najua nini maana
ya ndoa, najua nini maana ya malezi ya familia, ....najua jinsi gani kama
mwanamke natakiwe niwe...sivyo hivyo mnavyojua nyie......’watu wakacheka.
‘Msicheke,hili
ni somo lenye uzoefu, na lengo langu ni kuwafunza wanawake wenzangu kutokana na
uchunguzi wangu huo ambao nimeufanya kimatendo, na kutokana na hayo nimegundua
mengi kuwa kama sisi wanawake tutafuata na kutimiza majukumu yetu ya asili, sio
tu kuwa ndoa zetu zitadumu, bali pia baraka za kipato zitaongezeka mara dufu
'Niwaambie ukweli, mnaniona mimi na mume wangu tuna hali nzuri, ....lakini wakati tunaoana, tulikuwa hohe hahe,
tukianza maisha,...lakini kwasababu kila mmoja lijua nini maana ya ndoa,
tukajituma, kila mmoja akitimiza majukumu yanayomstahili.....sasa wengi
wanatuonea gele...limbwata limbwata..hakuna limbwata hapa ni mapenzi ya
asili....’akaendelea kuelezea.
********
Mimi nikiwa
namsikiliza huyo mwanamana, nusu ya mawazo yangu yalikuwa mbali, na hapo, nikamuwaza
mke wangu wa kwanza maana taarifa nilizopata ni kuwa yeye sasa ni mwalimu, na
wamerudi toka Kenya, huko alikuwa akisoma, na wameamua rasmi kurudi kijijini yeye
na mume wake mume wake akiwa kafungua maduka ya jumla, na mke akiwa mwalimu,
...
Pamoja na kazi zao hizo, wamejichanganya kwenye jamii, ili kusaidia
kuendeleza kijiji, na mke wangu huyo wa kwanza ni mwenyekiti wa akina mama,na
moja ya majukumu yake ni kuwasaidia akina mama kujiajiri...
Nikiwa
nawaza haya, taswira ya aliyekuwa mke wangu huyo wa kwanza ikiniangalia kwa
huzuni,taswira hiyo ilikuwa siku ile ya mwisho wakati tunaagana,..kwakweli
nilipofika hapo nilijikuta nikijilaumu, nilijiona mtu asiye na bahati, ...kwani
sasa hivi najiuliza nini hasa nilichokuwa nikikitafuta kwa mke ....awe wa namna
gani...na mara nikasikia yule mwanamama akionga kama vile anajibu swali hilo
kama vile nimemuuliza yeye.
‘Wanaume
wengi wanatafuta mke mwema, ...je sisi tumejiandaa vipi ili tuwe katika hilo
kundi la wake wema, ...hebu tujiulize sifa hizo tunazo...sifa za mke mwema
tunazo, kama hatuna kwanini hatuzitafuti, kwani zina gharama gani....na cha
ajabu mtu huenda wakati anaolewa alikuwa nazo... kabla hajolewa, akishaolewa
zinachujuka...na matokeoa yake nyumba zake zinapwaya, wanakuja hawa wajamaa
wanatuchulia waume zetu, kwa uzembe wetu wenyewe....halafu unatumia
ubabe...unatafuta miti shamba....hakuna haja ya miti shamba, rudieni uasili
wetu...’watu wakashangailia.
‘Huyu mke
mwema ana sifa gani...’nikajiuliza, anatakiwa awe mzuri sawa, anatakiwa awe na
adabu sawa, anatakiwa awe mchapakazi sawa...na je kama vyote hivyo anavyo
lakini hajui ....hajui.....nikawa nawaza hapo hajui nini ...nikiwa namlenga mke
wangu wa kwanza...mapenzi...'akatulia kidogo.
Kwa hali niliyo nayo nikajikuta nikiwaza na hata kujiuliza, kwani mapenzi ni nini, ....hivi ni mapenzi gani
hayo anayotakiwa mke au mume awe nayo, mapenzi ya kisasa, ya ukweli na uwazi....mara
nikamsikia huyu mama akisema;
‘Hakuna
mapenzi ya kisasa na ya kizamani,...mapenzi yalikuwepo toka enzi za Adamu,...ni
yale yale...tatizo ni kuwa tunaolewa lakini hatujui tufanye nini kwa waume zetu,
tunasubiri kama magogo, ....mume akisogeze huku akuinue huku, wewe umekaa tu
kama gogo....umelala kama gogo...’hapo wanawake wakacheka na kushangilia..
‘Msicheke,
hiyo ni aibu, ...na aninapozungumzia kulala kama gogo, sio kule kulala kwa
kulala,ichukulieni hiyo kimapana, nazungumzia majukumu yote ya ndoa, ....’akasema
na wanawake waliokuwepo hapo wakicheka wakatulia kusikiliza na hata mimi
nikatulia kumsikiliza.
‘Mapenzi,
ni tafsiri ndefu, inatoka mbali, hadi hitimisho lake ni kule kunapoitwa ..mmmh, la
ndoa....ambapo wengi ndipo tunapogota, na kuzania kuwa huko ndipo penye maana ya mapenzi, ....mapenzi hayaanzii huko , yanaanzia mbali, toka nje,....hadi ndani, na baadaye ndio tunafika huko..hata huko kwenyewe, tumeshindwa....jamani mna nini nyie kizazi....?.’akasema kama anaguna huku akiniangalia mimi, naona kuwepo kwangu hapo
kumezuia hata ile kauli aliyotaka kuongea, kuikatisha, na mimi nikacheka.
‘Jamani hilo
lilikuwa ni jukumu letu, tumelikwepa, hivi huko kwenye `kitchen party’
tunaambiwa nini...tunafika pale kwa nia ya kuupeana zawadi tu....najua hapo
hapatoshi, muda ni mdogo sana hapo wakufundwa, na ukizingatia hapo mwanawali
aanwazia zawadi gani atapewa, hawazii ni majukumu gani anayokwenda kuyabeba,
maana hayajui.....atayajuaje wakati wameokotana barabarani,hata a hadi zedi ya
ndoa haijui, anachojua ni kuwa kapata mume.
‘Ni muhimu sana
mtu kabla hujaolewa ukajua nini maana ya ndoa, nini nahitajika kufanya,
...kwasababu wewe ndiye ulitakiwa kumuonyesha mume wako afanye nini, ...lakini
tumekuwa magogo...tuliiii...umelele kama gogo, tuliii...haya wajanja wameibuka
na mbinu mpya, wanatuibia, wanatuletea mgonjwa...wamgundua kuwa nyie mlioolewa,
hamjui nini maana ya ndoa, na wakati wao wanahitji kuolewa,sasa ujanja ni
kupata au ni kuwahi...wanawawahi mkiwa bado mumelala.....
‘Tunatakiwa
tubadilike,...amukeni wanawake na hili halitafanikwia kama sisi wenyewe hatutajituma, tukaondokana
na hiyo kasumba ya kutaka kujilinganisha na mwanaume, halafu tunasahau majukumu
yetu ya asili....kwanza hata kama umeolewa, jaribu kutafuta muda wako, soma,
siku hizi vipo vijarida, vitabu magazeti na hata mitandao, someni, jifunze
jinsi gani ya kuijenga ndoa yenye furaha,..jamani mnataka tuongee lugha gani...’akasemahuyu
mama kwa jaziba.
‘Jifunzeni,
jisni gani ya kulea watoto, jinsi gani
ya kulea waume zetu....hilo halihitaji shule ya kukaa darasani, lakini tuonavyo
sasa,..pengine kuna umuhimu huo, maana tumewazarau mashangazi, mabibi zetu
ambao sasa tunawaita wachawi...ajabu kabisa,.....labda tuanzishe hizo
shule....kama walivyokuwa wakifanya wazee wetu,....ziwe za kisasa kidogo,
badala ya msituni, tuingie darasani,....’akasema na kuonesha picha ya wanawake
wapo darasani.
‘Tunaona
aibu kupelewa msituni,...au kwa bibi, au kwa shangazi, ....maana zamani kabla
ya kuwa ndani ya ndoa, ulihitajika kwenda unyango, kulikuwa na majina mengi
yaliyotumika, lakini lengo lilikuwa ni kumfunda mke ili ajue majukumu yake ya
ndoa, sasa hiyo haipo, tunakwenda na wakati, huku wakati umetuacha mbali ajabu,
maana wenzetu wajanja, wale ambao ndoa imewashidna ndio hawo wanapiga parapanda
la haki sawa...haya haki sawa, sijui kwa vipi...
‘Tunadai
haki, ..sawa si sawa, ....?’ akauliza pale alipona watu wanaguna, ...na hapo watu
wakasema `sawa, haki sawa kwa wote...’
‘Ni haki
yenu kudai hiyo haki,...lakini tunapodai haki , tudai haki za msingi,sio haki
za asili yetu, tusidai kile tusichokijua...maana sasa tunataka wafanyaakzi wa
ndani, bustanini, na hata kitandani....’akasema an watu wakacheka.
‘Ndivyo
ilivyo, tumekuwa wavivu hata kitandani...tunatia aibu....maana kila siku watu
wanapiga mayowe, mume katembea na mfanyaazi wa ndani, ..kwasababu ya uvivu
wetu, ....uzembe wetu, tukubali susikubali huo ni uzemeb wetu...’akasemana
kuangalia huku na kule.
‘Uzembe
wetu ndio uliotufanya kuwaachia wafanyakazi
wa ndani hadi yale majukumu ya msingi ambayo yanafikia hadi hawo wafanyakazi wa
ndani wanatembea na waume zetu, yeye ale wapi, kila mtu anakula ofisini kwake...ukiona
mfanyakazi wako wa ndani katembea na
mume wako,jiulze mara mbili kosa lipo wapi....ujilaumu wewe mwenyewe kwasababu
umeshindwa majukumu yako....ukiona mume wako anatemeba nje, jiulize wewe
mwenyewe kosa lipo wapi....maana umeshindwa majukumu yako....!
‘Namaliza kwa kusema...sawa tudai haki zetu
tupambane na mfumo dume, ...kama nilivyoona hiyo fulana aliyovaa mwenzetu hapa,
kuwa haki sawa kwa wanaume na wanawake,...lakini tuwe makini na hicho
tunachokidai, kwanza tuwe tumetimiza wajibu wetu, ...je mnatimiza wajibu
wenu....?’ akauliza na wanawake wakasema;
`Ndioooooooo’
‘Sasa
kwanini waume zenu wanatembea na wafanyaakzi wa ndani, kwanini waume zenu
wanatembea na mahawara, uliwahi kukaa chini ukatafakari, ukafanyia uchunguzi wa
kisayansi, au unachukulia jaziba, na kulipiza kisasi, na wewe unakwenda
kutembea na mtunza bustani,...ndivyo tulivyo, hasira hasara, badala ya kujenga
tunabomoa, tunajiau wenyewe....?’ akauliza swali ambalo hakutaka jibu, kwani
aliendelea kuongea kwa haraka ili kwenda na muda....
‘Nimewauliza
hilo swali, je ni kwanini, inakuwa hivyo....?’ akauliza tena.
‘Ni tamaaaa
zaaaoooh wanaume....’wakasema kwa sauti.
‘Je mna
uhakika na hilo mnalolisema, kuwa ni tamaa zao ...mumefanya utafiti wa
kisayansi mkaona kuwa kweli sababu ni tama zao....?’ akauliza na watu wakawa
kimiya.
‘Sikilizeni,
ndugu zanguni, mimi nimefanya utafiti wa kisayansi, nimegundua kuwa asilimia
kubwa tatizo lipo kwetu sisi wanawake, ndio wenye mataizo, najua wengi
hawatakubaliana na mimi, lakini ndio ukweli ulivyo...ndio maana tumeamua wale
ambao tumeligundua hili tuanze mchakato wa kufundishana hatua kwa hatua, na
ikibidi tufungue shule,...’akasema huku watu wakiwa wametulia.
‘Ingelikuwa
amri yangu, na hili linawezekana ni kuwa kabla mwanamke hujaolewa ni lazima upitie hizo shule,apitie
mafundisho, afundwe kiukweli...’ aliposema hivyo wanawake wengine wakaguna.
‘Hilo ndilo
tatizo, kuwa hatutaki kujifunza, utakuwaje dakitari bila kwenda shule ya
udakitari, utakuwaje mwananda bila kuisomea hiyo ndoa, mbona mnaizalilisha hii
sehemu muhimu ya maisha yetu, ...kama hutaki , kama unajifanya unajua haya
kaolewe, lakini ukiumwa an manyigu usipige ukulele....’watu wakacheka.
‘Tatizo ni
kuwa tunataka na sisi tuwe kama wanaume,
sio mbaya..., lakini tujue kuwa hata siku moja wewe hutakuwa mwanaume,
kama wewe umezaliwa kuwa mwanamke, ...usikwepe majukumu, usikimbie umbile lako,
maana hata hao wanaojibadili ipo siku watajuta,...maana sisi ni wanadamu tu,
...leo tupo kesho tutarudi kwa huyo aliyetuumba, na ukiuliza nani alikuumba
hivyo sijuii utakuwa na jibuu gani la kumjibu muumbaji....’akasema huyo mama.
‘Narudia
tena kama kweli tunataka ndoa zetu zidumu tusikwepe majukumu ambayo ni ya asili, aliyotujalia
mwenyezi mungu, kiuzoefu wangu na utafiti wangu hayo majukumu ukimuachia
mwanaume ulezi wa familia hautatekelezwa
kama inavyopasavyo, amini usiamini,...’akasema huku akifunga funga makabrsha
yake kuonyesha kuwa anamalizia.
‘Majukumu
ya asili ni swala nyeti la wanawake,
sisi ndio tuaoijua hiyo kazi, kulea watoto na kuwalea wanaume,tusikwepe haya majukumu
jamani kwa masilahi ya familia zetu, kwa masilahi ya vizazi vijavyo na kwa baraka
za riziki zetu...’akamalizia huyo mama na kuashangaliwa sana, halafu akaingia
mwanamama mwingine,...huyu alivaa kabisa fulana imeandikwa `haki sawa kwa
mwanaume na mwanamke, ...’ moyoni nikasema hapo kuna kazi, ....
Mimi akili
ikawa inahama nusu nipo hapo nusu nipo nje nikiwazia matatizo yangu,...ni
kijiuliza hivi hayo aliyoongea huyo mwanamama yameeleweka, ....hivi kweli sisi
wanaume hatuji malezi, ....na mara akili yangu ikahama na kumwazia mke wangu, nikijua kabisa huko sasa natufutwa, nitakuwa
natafutwa na bosi, sijui nikikutana naye nitamwambia nini,....Bosi wangu.
*******
‘Umesema
hujamuona tangu asubuhi na hakuwahi kukuagana kuwa anakwenda wapi, ....mbona
siamini hayo maneno....’akasema na kumkodoleamacho Kimwana.
Kimwana
alitulia kimiya akiwa nawasiwasi,kwani tangu asubuhi alipoachana na mume wake,
hawajawasiliana naye na hata alipojaribi kumpigia simu ikawa haipatikani, na
aalipoona hivyo alikwenda nyumbani, na huko hakumkuta..
‘Huyu mtu
kaenda wapi, ..mbona ananiingiza kwenye matatizo...’akajikuta akiongea peke
yake,alijua nini kitafuta kama mume wake huyu atakuwa kafanya kinyume na
inavyotakiwa.
‘Akawasha
chombo chake maalumu cha kumtafuta, na kilipowaka akakuta mwanga wake ni mkali
zaidi kuonyesha kuwa kitu anachokitafuta kipo hapo hapo karibu, ...akafuatilia
hadi akafika kwenye kabati la nguo, na
humo akaikuta simu ya mume wake ikiwa kwenye mfuko wa suruali, na
saa...akavitoa na kuviangalia, simu ilikuwa imezimwa.
‘Huyu mtu
kafanya nini...?’ akajiuliza. Vifaa vile aliambiwa asiachane navyo, kila
anapokwenda, kwani ukiwa na hivyo vifaa unaonekana moja kwa moja katika mitambo
yao, na wao walimwamia kuwa kuwa akiwa an hivyo vifaa atakuwa analindwa aili
asije akazurika na maadui wanaomtafuta.
‘Hapa kuna
jambo, huenda huyu mume wangu akgundua jambo, ndio maana kaamua kuviacha hivi
vifaa,hata simu..hapana kuna jambo, sasa nitamtafutia wapi....?’ akajiuliza na
wakati anahngaika mara simu ya mama ikaita.
‘Natakauje
hapa na mumeo haraka...’sauti ya mama ikasema.
‘Mume
wangu...ooh, shajarudi bado..’akajikuta akijiuma uma.
‘Ndio maana
huku haonekani, alikuwa akzima simu yake, ..mtafute haraka uje naye, nakupa
nusu saa uwe uemshafika hapa, na yeye...’sauti ya amri ikasema.
‘Haya,
ngoja nimtafute...’akasema lakini hakujua amtafutie wapi.
Alijaribu
kumtafuta kila mahali anapohisi kuwa anaweza kumpata, lakini hakufanikiwa, na
baadaye akjipeka mwenyewe kwa mama.
‘Una maana
gani kusema hivyo,...haonekani....sikusikii vyema, kwasabubu huyu tulikuambia
ni mtu wako, halafu ni mumeo,...ndivyo nilivyowafundisha hivyo, ndio jinsi ya
kuishi na mume hivyo, mume atoke bila kukuaga, ina maana mnaishi vipi, na huyo mume wako au ...umekiuka yale
niliyokufundisha kwasababu wewe ni bosi wake...wewe ni mke wake...kama unafanya
jinsi mke anatakiwa kuishi na mumewe, hilo lisingelitokea kamwe...nieleze kuna
tatizo gani..?’ Mama Docta akawa anongea kwa jaziba.
‘Hapana
mimi sijakiuka kabisa miiko ya ndoa kama ulivyotufundisha,....ila naoana kuna
jambo linaloendelea ambalo huenda silifahamu, kwasababu kaacha simu na ile saa,
hii ni kuonyesha kuwa huenda keshagundua kuwa hivyo vifaa vinamuonyesha kila
anapokwenda....’akajitetea mke wangu.
‘Hapo
hujaniambia kitu, maana mimi nawajua wanaume ipasavyo,kama ungelifuatilia kama
nilivyowafundisha huyo mwanaume asingelishawishika na kitu chochote, huenda
umejifanya wewe ni kidume, na hili litakutokea puani...sitaki utani kwenye hii
kazi,....’akagonga meza kwajaziba.
‘Unajua
nyie mnafanya itani, nimewekeza hela
yangu nyingi sana, na hivi sasa ni muda wa kuirudisha, ...mimi nimetumia hela
nyingi sana kuwafanya muonekane hapa mjini ...mnatamba mnaitwa wasichana
warembo,..hamjui yote hiyo ni gharama, na nani wa kurudiha hiyo gharama kama
sio waume zenu, leo hii unakwenda kinyume....sasa nakupa masaa mawili nataka
huyu mtu apatikane...na akipatana nataka umlete hapa..kuna kazi muhimu
sana...’akasema mama.
*********
‘Hebu
niambie ulikuwa wapi mume wangu..?’ nikaulizwa kwa sauti ya kinamna, sauti ya
kumnasa ndege tunduni, nikamtupia jicho mara moja na kuangalia pembeni, maana
nilitarajia ile sauti ya ubosi, maana mke wangu ni bosi ...alishaniambai hilo,
na kweli sehemu kubwa ya mambo yetu alikuwa yeye ndiye mweney amri, Mume kama
huna pesa una usemi gani.
‘Nilitoka
kidogo ....kupoteza mawazo, ....kuna jamaa yangu mmoja aliniita , huyo jamaa ni
rafiki yangu mkubwa, nilishaongea naye kuhusu maswala ya kunitafutia kazi, na
leo alivyoniita nilijua kapata kazi mahali, tumeongea wee, nikajisahau kabisa
..’nikasema uwongo.
‘Mume wangu
unajua ukisema ukweli ninafahamu na ukisema uwongo ninafahamu pia, ndio tatizo
la kusomea haya masomo ya hulka za binadamu, nilishakuambia katika shughuli
zetu hizi, ilibidi niyasoem hayo masomo, ....’akasemahuku akiniangali machono
moja kwa moja.
‘Hata hivyo
usijali, mimi ninakuamini mume wangu, ...kwasababu nakupenda sana...fanya
ufanyalo lakini usije ukadanganyika kunisaliti....maana ninavyokupenda
sitafurahi nikikusa moja kwa moja...unajua hilo...’akasema mke wangu na yale
madoido yake akanifanya niwe katika dunia nyingine, lakini hata hivyo akilini
mwangu nikajua kuna jambo linakuja. Sio bure ,ingelikuwa siku zile za mwanzo
ningesema ni mahaba yake, lakini tangu alivyonitamkia kuwa yeye ni bosi wangu ,
nimekuwa nikijihami kwa kila jambo,ingawaje
imekuwa kama mbwa mbele ya chatu.
‘Sikiliza
mume wangu, najua kabisa unavyojisikia, lakini yote ni mitahani ya misha, najua
kabisa wewe ulitakiwa uwe kwenye ofisini yako , au umeajiriwa mahali, katika
wadhifa wa meneja, au sio.....’akasema kama ananiuliza huku akifanya mambo
yake. Nikuambie ukweli huyu dada alijua nini akifanye kwa wakati gani, na ni
mjanja wa kughilibu akili, ....kwanii mimi hapo sikuwa najielewa,zaidi ya
kumuona yeye ni kila kitu. Huku namuitikia kila kitu anachosema;
‘Kweli
kabisa mke wangu, ....hivi kweli unanijali kiasi hicho, ....kama umeligundua
hilo, nakushukuru sana, maana imefikia hatua naadhirika sana, unajua
kuadhirika, hali iliyopo sasa naadhirika, katika maisha yangu sikutegemea kuwa
ningelifanya haya niliyoyafanya...hata hvyo mke wangu mengi ni wewe
unanikamatisha,...unajua mimi sipendi mambo hayo....sasa naogopa hata kukutana
na wanzangu, na wakiniuliza upo wapi siku hizi inabidi
niwadanganye...’nikasema.
‘Pole sana
mume wangu, wakati mwingine nakufanya hivyo ili ufunuke macho na
masikioa,..uijue dunie ilivyo, ....Sasa mume wangu wakati umefika, ...kuna
sehemu nimeshakutafutia, utakuwa meneja....unasemaje.?’ akaniuliza na mimi
nikashituka kwa hamasa.
‘Eti nini
kazi, halafu niwe meneja....unasema kweli au unanitania...?’ nikauliza.
‘Toka lini
nikakutania mume wangu, mimi nakupenda sana mume wangu ndio maana naishi na
wewe kwa dhida na raha nikujua sasa itakuja,na najua sasa raha ndiyo hiyo
ushindwe mwenyewe, .....unajua mume wangu, kufanikiwa kwako ndio mafanikio
yangu pia,kwahiyo usiku na mchana nakuhangaiia wewe ili na wewe ufanikiwe...’akasema
na kuniangalia mchoni.
‘Nchi hii
ukiijulia huwezi kufa njaa, nchi hii ukiIjulia unaweza ukafanya lolote
lile...na hilo limafanikiwa , ila kama ujuavyo nchi hii ili ufanikiwe jambo,
lazime upenyeze rupia....na ni pesa nyingi kidogo, maana unakwenda kuwa meneja,
ambapo utalipwa mshahara mkubwa, gari na gharama zake, utapewa nyumba...kama
sio nyumba,utalipwa pesa sawa na kulipia nyumba....sasa ili kulifanikisha hilo,
kuna jambo dogo linahitajika kufanyika...’akasema na hapo nikajua ni yale yale.
‘Jambo gani
tena hilo wakati umeshasema kazi imepatikana, au ndio danganay toto...’nikasema
kwa hasira.
‘Sikiliza
nimeshakuambia ili upate kitu, ni lazima ufanye kitu, na hali ilivyo wanasema
penye uzia ufanye nini,..penyeze rupia! Sio rahisi rahisi tu kama unavyozania,
utatemeba mpaka umalize ofisi zote usipate kitu, lakini ukiijulia hii dunia,
hupati shida...’akasema na kutabasamu.
‘Lakini
mimi nikaona ili uondokane na huu utumwa,..utumwa wa kuwa tegemezi, ni lazima ufanya jambo kwa jasho lako
mwenyewe...sitaki utafutiwe kazi na hapo hapo zile gharama za kuipata hiyo kazi
pia ulipiwe....wewe uuna onaje, maana nimemwambia huyo mtu kuwa utalipa
mwenyewe....’akanimabia.
‘Ningependa
iwe hivyo, lakini kwa pesa gani, pesa ninayopata niya kuniwezesha kula
tu...sasa huoni hapo unanitega, nitapaat wapi pesa za kulipia hiyo gharama na
je ni kiasi gani,,,,?’ nikauliza.
‘Ina maana
huniamini...mimi nimebuni njia ya kupata hizo pesa, unafanya kazi na alzima
ulipwe kiasi kizuri, na kazi hiyo ni nyepesi tu, ...kuna kazi ndogo ambayo ukiifanikisha
tunapata mshiko mzuri, na mshiko huo utakuwezesha
kumlipa huyo wakala ...kama ujuavyo, kila kitu lazima kiwe na wakala siku hizi,
...’akainuka pale alipokuwa amekaa huku na kusimama akasema’
‘Unajau
wakala wanalipwa sawa na mshahara wako
wa hiyo kazi....ndio gharama zao....lakini pia kuna watu wengine wameingiahapo,
na wao wanahitajika kulipwa, watu waliosuka huo mpango ili uingizwe kwenye hiyo
ofisi kwani wewe kutokana na historia yako hakuna kampuni ingelikukubali
....’akasema.
Niliwaza
mengi, ni kweli ofisi nyingi nilizokwenda kuombakazi kila inapofikia hatu ya
kujielezea wananiambia nikasubiri nikirudi mara ya pili wanakuja na hoja kuwa
baaada ya kuchunguz ahistoria ya kazi wameona hawanihitaji...nikiuliza historia
yangu ina ubaya gani, wanasema hawana haja ya kuniambi, ila kama watanihitaji
wataniita..na hapo imeshatoka...
Nilihangaika
kila ofisi kuomba kazi mpaka nikakata tamaa na kusema huenda ofisi zote
wameshawasilina kuhusu mimi, au kuna mtu ambaye kila anapoulizwa kutoa habari zangu
huko nilipoanzia kufanya kazi ananipakazia ubaya..basi nikaona nikubali ukweli,
na kujituma kwenye kazi za kuwa kibarua,...sasa leo naletewa habari kama hii, kuwa
imepatikana kazi ambayo inaendana kabisa na kiwango cha elimu
yangu,....nitafanya lolote ili niipate, nikasema moyoni...
WAZO LA LEO: Tukumbuke kuwa kila mtu ni marehemu mtarajiwa, na kila kifo hakikosi sababu, kwani sote ni mavumbi, tumetoka kwa udongo tutarudi kwa udongo. na kazi ya mungu haina makosa. Blog yenu hii inaungana na wengine kutoa mkono wa pole kwa familia, ya jirani yetu mwanablog mwenzetu, na muigizaji mashuhuri Marehemu Steven Kanumba, Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. AMIN
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
Darasa hili ni tamu mno kila nikiingia hapa natoka na maarifa kibao..Ahsante sana na kumbuka tupo Daima pamoja.
Yani huwa natamani hata weekend uwe unaupdate ,kutaka tu kujua nini kinaendelea. Kweli maisha ni safari,pia njiani kuna milima na mabonde.
Post a Comment