Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, December 12, 2014

NANI KAMA MAMA-5Zilishapita siku tano, nipo hospitalini hakuna hata ndugu yangu mmoja aliyejitokeza, huenda walikuwa hawajui nilipo,…, basi vipimo vilivyotoka na kuonekana sina tatizo, na mimi nikajitutumua kuwa sijambo, nikaruhusiwa mimi mwenyewe sikuona umuhimu wa kuendelea kukaa hapo hospitalini, dakitari alipopita akanikaruhusi na mimi sikupoteza muda nikaondoka kuelekea kituoni.

Inavyoonekana labda siku ile ya ajali hakuna mtu anayenifahamu aliyeshuhudia tukio hilo, ilikuwa ni ajabu basi yaani  hata wafanyakazi wanzengu hakuna aliyebahatika kuwepo eneo hilo, nahisi na wao walikuwa na mambo yao, hasa kwa wale waliopata Bahati mbaya kama yangu ya kupunguzwa kazi, kila mmoja alikuwa akiwaza lake, na kuhangaika kivyake.

Kwa hali hiyo hata nyumbani hawajui wapi nilipo, watakuwa wamehangaika sana, na sijui waliponiona sionekani  nyumbani hadi usiku sijui walichukua hatua gani. I Nikawa nawaza, na moyoni nikimshukuru mungu kuwa ni mzima, japo cha moto ninakipata. Hapo sijui hata pa kuanzia, pesa sina…nikashika mfukoni na kupata pesa kidogo niliyopewa na huyo mgonjwa jirani yangu na jamaa yake.

‘Hii ndio pesa ya mwanaume wa nyumbani,…sijui watanipkeaje, wakiuliza pesa ya mfao sijui nitawajibu nini…siwaambii kuwa nimeibiwa, …siri yangu….’nikawa naongea peke yangu.

Nilipotoka nje ya eneo la hospitalini,  nilitamani nipate mtu mwenye simu nipige nyumbani kwanza nijue hali ya wagonjwa maana siku  ile ya tukio nilimuacha mama akiwa na mtoto hospitalini , mtoto akiwa na hali mbaya, hata sijui ilikuwaje, nilipowaza hivyo miguu isiyo na nguvu ikachanganya kutembea.

Nilifika eneo yanaposiamama magari, nikapanda hilo gari na Bahati nzuri nikapata kiti, maana kama ingelikuwa kusimama kwa hali niyo nayo ningemdondokea mtu, niliona baadhi ya watu wakiniangalia kwa mashaka,..nahisi ni kwa jinsi nilivyokonda, au sijui kwanini walikuwa wakiniangalia hivyo, sikujali akili yangu ikazama kwenye mawazo..

Nauli ya dala dala aliyonisaidia mgonjwa aliyekuwa jirani yangu kwenye kitanda, ambaye nilimuelezea matatizo yangu akanionea huruma akanipa pesa inisaidia kwa kwa nauli na hata jamaa yake moja alipokuja kumuona yeye, sijui kama alimsimulia kuhusu mimi,  kwani wakati anatuaga, akaja akanipa pesa kidogo, nikashukuru sana.

Ajabu hata kondakita hakuniuliza nauli, nikashukuru kimoyo moyo, nikatoka nje ya gari na kuanza kutembea kuelekea maeneo ya hapo nilipoanga, kwanza kuna watu wa nyumba za jirani, niliona kupo kimiya, watu hawapo…nikahisi kuna jambo, nikawa natembea hivyo hivyo kukaribia eneo la nyumba niliyopanga.

Nikafika nyumbani, nilipokaribia nyumba yenyewe nikashangaa kuona watu wamejaa hapo nilipopanga, akili ikanipaa,  kwanza nikasimama na mawazo ya haraka yakakumbuka mtoto aliyekuwa akiumwa, lakini pia nikajipa moyo kuwa nyumba hiyo ni ya kupanga sipo peke yangu na familia yangu, huenda kuna kitu kimetokea kwa wapangaji wenzangu.

Nikavuta pumzi, na kutembea kwa tahadhari kuelekea hapo kwenye nyumba…

Tuendelee na kisa chetu…..

**********


Niliokutana nao awali ni watu ambao walikuwa  hawanifahamu vyema, nikaona wengine wakinisalimia na kunipa pole, mmoja akasema;

‘Huyu ni kaka yake nini, mbona wanafanana…’mmoja akasema mimi nikajiuliza moyoni kwanini wanasema hivyo,  nikasogea nikakutana na mtu wa kwanza anayenifahamu, akaniangalia, akanitolea jicho, akashika mdomo, akasogea kinyume nyume, akageuka na kutimia mbio…

Nikaduwaa, nikasimama, sielewi kitu….

Mara ghafala wakajitokeza watu wanaonifahamu ikawa hali ni ile ile, kile aliyeniona hakuniangalia mara mbili, hugeuka na kutimua mbio, watu waliokusanyika hapo wakawa wanakimbia kutoka eneo hilo, na kila niyemkaribia akawa anakimbia, na hadi kukabakia kweupe, nikabakia nimeshangaa kulikoni......

Nikatembea kuingia ndani, nikaona kimiya, waliobakia hapo ni mama , mke wangu na ndugu za mke wangu…mama akasimama na kuniangalia kwa makini, mke akakurupuka, nikajua ni yale yale mashetani nikageuka kumfuata mamamama, ikawa kama nimejichongea mke alitoka mlangoni na kutimua mbio

‘Mshikeni yule jamani atapotea tena..’nikasema hakuna aliyenisikiliza, wale jamaa zake na wao wakatoka mlangoni na kuanza kukimbia, nikabakia mimi na mama na mtoto…nikamtizama mtoto akiwa kalala chini, alikuwa bado kadhoofika lakini moyoni nikshukuru kuwa ni mzima, kwahiyo nikapumua

‘Kuna nini hapa mama?’ nikamuuliza mama ambaye alikuwa kasimama kaganda, hasemi kitu, nilipoona hivyo nikamfuata mwanangu pale alipolala, nikamuinua akafumbua macho, na kwanza aliniangalia kwa makini halafu akawa kama anawaza jambo , akasema;

‘Kumbe hujafa baba….’akasema
‘Sijafa, nani kasema nimekufa...?’ nikauliza na kumgeukia mama, mama alikuwa kainua mikono juu kama anaomba, akaniupia jicho akiniangalia kwa mshangao, na mara nyingi kukasikia kilio,…gari likasimama nje, nikachungulia kupitia dirishani, nikamuona mama akanisogelea na kunishika mkono akasema;
‘Ingia ndani ulale, utulie kimiya..’akasema, na mimi nikashangaa nikamuangalia mtoto , mtoto akasimama, akanishika mkono, tukaongozana kuelekea chumbani nikafika kitandani nikajilaza, nilishikwa na usingizi wa ajabu na ndani ya usingizi niliota nimekufa napelekwa kuzikwa..

Ilkuwa ni ndoto ya kutisha, maana nilijiona kabisa nimekufa, na nimeshaandaliwa kuzikwa, na wakati nimeshafikishwa kaburini na kunitumbukiza humo wakaanza kunifukia nikazindukana, nikakurupuka, watu walipoona hivyo,  wakaanza kukimbia…na mimi nikatoka mle kaburini kwa haraka na kuanza kukimbia, kuwafuata watu na watu wakazidi kunikimbia kama vile nawakimbiza wao, nikazindukana.

Nilipofungua macho, nikaona watu wamesimama karibu ya kitanda, alikuwepo dakitari ninayemfahamu, walikuwepo wazee, na ndugu ndugu upande wa mke wangu, na majirani, kila mmoja akiwa aknitolea macho, wakiwa hawaamini, nikakaa vyema kitandani na kuwauliza

‘Hivi kuna nini hapa nyumbani?’ nikauliza
‘Taarifa zilizokuja ni kuwa umepatwa na ajali na umekufa, na hapo ulivyotukuta tulikuwa tuansubiria mwili wako kwa ajili ya mazishi yako, mara unatokea, na wakati huo watu wamekwenda kuchukua mwili wako muchwari, muhimbili, na cha ajabu kabisa, watu wamepewa mwili unaofanana na wewe kabisa,….’akasema mzee mmoja

‘Kwahiyo mnasemaje, mnataka kuhakikisha kuwa mimi ndiye halisi au mimi ni mzuka…’nikauliza

‘Tumeamini kuwa wewe ni halisi, maana dakitari huyu hapa ambaye ni mmoja wa watu waliokupokea huko muhimbili, na pia maiti iliyoletwa haina majeraha, ina maana hiyo maiti ilikufakifo cha akwaida imesharudishwa na wenyewe wamaitambua..’akasema mzee huyo

‘Huu sasa ni uchuro, inabidi mkatambike kwenu..’akasema mzee mmoja akimuangalia mama yangu.

‘Ni Bahati mbaya tu, hakukuwa na mawasiliano maana mimi nilipata ajali nikapoteza kila kiu na hakuna aliyeweza kutambua au kuhangaika kutafuta jamaa zangu hata waliponiuliza sikuwa aili ya kusema waje huku, kwanza wengi walioniuliza ni wageni kwangu….ndio hivyo namshukuru mungu nimepona kiwmili lakini kiakili naona nipo mfu…’nikasema

‘Ina bidi msome duwa, na maombi kwa mungu, kuna tatizo kwenye hii nyumba…kwenye hiyo familia yenu…’akasema mzee mwingine, na wakati huo nikaona wakimuingiza mke wangu ambaye alisogea na kuniangalia kwa makini, akionyesha kuogopa, wakawa wamemshikilia bara bara, lakini alivyowatoka hutaamini wote walitupwa chini mke akatoka mbio, …

‘Wewe lala tu, hilo tuachieni sisi wenyewe….ila mwenye nyumba yupo hapo nje, alitaka kuja kuongea na wewe….sijui anasemaje’wakasema ndugu wa upande wa mke wangu.      

‘Anasema anataka huyu mpangaji, ahame kwenye nyumba yake haraka, maana eti ana mkosi, mara afe mara afufuke na kodi halipi,…’akasema jirani mmoja

‘Hayo ni ya kuongea tu, muhimu tumuacheni huyu mtu utulie kwanza, ndugu kutananie mliongee muone jinsi gani ya kuisaidia hii familia….’akasema docta aliyeitwa kunichunguza kama kweli ndiye mimi, na kweli watu wakatoka na kuniacha nikiwa nimeduwaa…hata sielewi nifanye nini, akili ilikuwa imesimama kwa muda.                    

************

 Mambo ndio hayo,  mke ana kinachoitwa mashetani, mtoto anaumwa magonjwa yasiyojulikana , kazi sina, pesa sina, mwenyenyumba anataak nihame, haraka iwezekanavyo, huku nimetambulikana kuwa nimekufa…..

Kutokana na matatizo ya mke wangu, na mtoto, mke wangu akapata ushauri kwa mashoga zake kuwa madude hayo yana wataalamu, ambao ni waganga wa kienyeji, na mmoja wa mashoga zake akamuelekeza kwa mtaalamu mmoja huko Temeke.

Basi siku hiyo, akaamua kuanza kumfuatilia mganga huyo aliyekezwa kwake. Kabla ya hapo hakuwa na tabia hiyo ya waganga wa kienyeji, kwani ni mmoja wa watu waliokuwa wakipinga imani hizo,lakini uvumilivu ukamshinda, baada ya kukumbana na mitihani hiyo.

Akaamua kujaribu njia hiyo, huenda atafanikiwa, akaaga kuwa kweli anakwenda kwa huyo mtaalamu, mimi nilimwambia huko siwezi kwenda kabisa, kwanza sikupenda kuonekana na watu, mwili wangu ulikuwa bado hauna nguvu, na muda mwingi nilikuwa nalala tu nikiwaza.

Mke wangu aliondoka na mdogo wake, Sisi tukabakia na mtoto na mama. Tulikuwa na hamu sana ya kusikia nini wataambiwa, kwani wenyewe tulishaanza kuhisi kupotoshwa, kama tujuavyo. Wengi wa waganga hawa ni wafitinishaji, ingawaje kweli wapo wenye dawa za kusaidia, lakini ukienda kwa wale wanapiga ramli, ujue umekwisha.
‘Mwanangu utakuja kusikia mabaya zaidi….na huenda na wewe ukanichukia, ..mimi naona nitafute nauli niondoke, lakini nashindwa kuondoka kwa hali kama hii, wewe ndio hivyo unaumwa, huna pesa…mjukuu anaumwa, mke ndiye huyo kachanganyikiwa,…’akasema mama

‘Mama wewe huendi popote, utakaa hapa hapa, kama nikuondoka tutaondoka wote, maana kama ulivyosikia mwenye nyumba hatutaki kwenye nyumba yake, hata mimi sipendi kukaa hapa tena,…’nikasema kumuambia mama

‘Ninachokiomba ni mkeo apate matibabu apone, lakini sio huko kudanganywa, na nina wasiwasi huko watamdanganya sana, na kuna dawa aliandikiwa mtoto za kununua hatujanunua, badala ya kuhangaika tupate pesa za kumibia mtoto wanahangaika na waganga wa kienyeji, ndugu zake wamelishikilia hilo kweli…’akasema mama

Mimi nilikuwa nikikuna kichwa kwa mawazo, kwani hali yandani ilikuwa ngumu, chakula kilikuwa cha shida, na dawa za mara kwa mara za mtoto zilikuwa zinahitajika, kwahiyo nilikuwa sina amani kabisa kichwani.

Hapo nikawa hata sijui niende kwanani, nilikuwa nimepungua sana kwa muda mfupi. Nilishukuru mungu kuwa sikuwahi kupata ,maradhi, la sivyo, ningekwisha kabisa. Nilishngaa nguo zangu zote nilizokuwa nikivaa, zikawa zinanipwaya, ilibidi kuongeza tundu nyuma ya mkanda, ili niweze kuzivaa baadhi ya suruali zangu.

 Huko walipokwenda mke wangu na mdogo wake, walichelewa kurudi hadi jioni, tukawa na wasiwasi hata simu yao ilikuwa haipatikani, tukadhania kuwa huenda kazidiwa, lakini tukaona tuvute subira.Na jioni ilipofika wakaingia wakiwa wamechoka, labda kutokana na usafiri au njaa. Walitusalimia kwa sauti ya kuchoka, na tukawaitikia, na wao wakakimbilia ndani kujipumzisha kwanza.

`Ndugu yangu,…nilipatwa na mtihani, katika maisha mtumainie mungu peke yake, usiwatumainie wanadamu, huo ni ushauri wangu kwako, kila siku muombe mola wako akulinde na vitimbwi vya shetani kwasababu shetani  akitaka kukupoteza atapenyeza mirija yake kupitia sehemu yoyote aipendayo, na baya zaidi anaweza akaitumia familia yako kama silaha yake.

‘Nikuambie ukweli mjumbe, watoto, mke na mali ni mtihani mkubwa hilo nakuthibitishia kivitendo. Anaweza asiwe mke, akawa mume pia kutegemeana na nani mwenye uthabiti ndani ya familia, hilo mimi limanipata na nimejifunza….’akasema mjumbe.


`Jioni  aliporudi mke wangu kutoka kwa mganga sikupenda hata kumsikiliza,lakini kwa vile tulitaraji huenda kafanikiwa kuileta dawa ya mtoto tukakaa pamoja mezani kumsikiliza, tulikuwepo mimi, mama yangu na mdogo wa mke wangu ambaye ilibidi abakia hpo kusaidia kazi. Mama mkwe alisema shemeji yangu huyo atabakia hapo ili awe msaada.

Mimi sikupenda mtu mwingine kubakia kutokana na hali za kiuchumi zilivyo atakuja kuteeka na njaa, ije kuwa lawama, nikasema kumuambia mama mkwe;

‘Kwa vile mama yangu yupo hapa, haina haja,…kama ni swala la kupata msaidizi wa kulea mtoto..’ nikamwambia mama mkwe, mke wangu akasema.

‘Siwezi kumtuma mama mkwe, nikiwa na shida, na mama ni mtu mzima, kazi za nyumbani hapa ataziweza zote, na kwanini usitake ndugu yangu kuja kuishi hapa…?’ akasema mke wangu kwa hasira. Ilibidi nikubali shingo upande, na mdogo wa mke wangu, akaja, na akawa analala na mama yangu.

Tukawa sasa tunasubiri kusikia taarifa ya kutoka huko kwa mganga wa kienyeji, kwanza tulitangulia kukaa mezani , mimi , mama na shemeji yangu …na mtoto, mke alibakia ndani kwa muda, labda alikuwa akinywa dawa , tukawa tunamshubiria.

Basi mke wangu alitoka chumbani na kuja kukaa nasi pale mezani, ilionekana akiwa na wasiwasi na anachotaka kutuambia. Mdogo mtu akawa anamtizama dada yake aanze kuongea, yeye hakutaka kusema wameambiwa nini kutoka huko kwa mganga wa kienyeji.
 Basi tukatulia kimya kumsikiliza mke wangu. Kitu cha kwanza kulichotutia hofu na pale waliporudi, walipofika tu, walifanya jambo la ajabu,  kwani walivyofika tu,walienda moja kwa moja alipokuwa amelala mama na mtoto. Mama yangu na mjukuu wake walikuwa wametandika mkeka nje na kujilaza huku wakipata upepo mwanana unaotoka kwenye mti uliopandwa hapo nje.

Wao walifika pale walipolala, ghafla wakamzoazoa mtoto . Mama akabakia kashanga, lakini hakusema kitu. Mara nyingi mtoto wangu alikuwa akimpenda sana bibi yake, kuliko hata mama yake, kwasababu hasa ya matatizo yaliyokuwa yakimtokea mara kwa mara mke wangu hadi mtoto akawa anamuogopa.

Mara nyingi mke wangu akichanganyikiwa, huwa hamtambui kabisa hata mwanae, anaweza akampiga hata kumuumiza, kwahiyo mtoto akawa kajenga umbali kati yake na mama yake akiogopa kipigo.

Walipofika muda huo  nilikuwa nimsimama mlangoni, niliona kitendo hicho, cha wao kumchukua mtoto wangu wangu pale alipokuwa kalala na mama, nikataka kuliingilai lakini niaona haina haja, ngoja nivite subira,  nilifikiria labda  ni sehemu ya dawa, ila nilimuona mama akisononoke kwa kutikisa kichwa. Nilimtizama nikamuashiria atulie kwa mkono, naye alitulia kama mimi.

Basi baadaye tukajiunga mezani kupata chakula cha usiku na kusubiri nini kimeletwa toka huko kwa mtaalamu. Wakati tumetulia kusikiliza nini wamekuja nacho, na wakati huo shemeji yangu ndiye aliyekuwa kambeba mtoto,tofauti na siku zilizopita ambapo bibi yake ndiye aliyekuwa mara nyingi anambeba huyo mtoto.

Ghafla mke wangu akaachia kijiko alichokuwa kakishika na kudondoka chini, sakafuni sote tukageuzo vichwa upande wake, tukajua mambo yameanza,….mke akawa pale chini na kama kawaida akaanza kutetemeka, kujibamiza

Nikamuangalia shemeji , nikamuashiria sogee mbali, kwa vile yeye ndiye aliyembeba mtoto, lakini hakufanya hivyo, akachukau chupa yenye maji akamwangaia dada yake kichwani.

Kwa kitendo kile tukajua mambo yamenza, huwa matatizo yake huanza hivyo hivyo. Anaweza akamrukia mtoto akataka kumkaba, au yoyote miongoni mwa waliopo mbele yake, na kwahiyo inatakiwa mtu amuwahi mapema, la sivyo anaweza akaleta madhara.

Mimi kwasababu nilishamjua, nikajua moja kwa moja kuwa keshapandisha yale maruheruhe yake, na hapo hapo ilibidi tufanye kazi ya ziada kumkamata na kumweka chini, hapo chini alianza kutingishwa na akawa anajibamiza chini kwa nguvu, na mdogo wake alipommwagia yale maji akatulia, akitulia hivyo ujue ana ujumbe fulani, anataka kuutoa, na akishautoa hunyamaza kimya na hali yake hurudi kama kawaida. Tukausubiri huo ujumbe, na kweli akainua kichwa na kwa muda halafu akawa anatutizama mmoja mmoja kwa zamu.

‘ Mnataka kumjua mbaya wa familia hii au siyo,…. basi ngoja niwapashe kuhusu , mbaya wenu, mbaya wenu hayupo mbali nanyi kabisaa…, mbaya wenu anataka kumpoteza huyo mtoto , anataka abakie ndani ya nyumba hii kama malikia na baadaye amuue hata mtoto wake wa kumzaa…mchawi hana ndugu mchawi hana mtoto….akitaka damu ya mtoto ni lazima aipate’ akainuka na sote tukajiandaa, tukijua anataka kukimbia

Alisimama akawa anatuangalia huku kashika kiuno na halafu akanigeukia mimi na kusema;

‘Wewe usiyeelewa kitu, nishakuambia familia yako itasambatarika kama vumbi kwenye upepo mkali. Heu angalia sasa hivi huna kazi, maisha magumu, mume gani usiyekuwa na kazi, hujiulizi tu, wewe hujui nini kinasababisha yote haya, basi yote hayo yanasababishwa na huyo mbaya wenu.

‘Alitaka kukua, alitaka kukugeuza ndondocha, lakini akaambiwa muda bado…kwanza, anataak damu changa, anataka damu changa….Nakuambia unielewe mapema, kwani mwishowe utamkosa mtoto wako huyo anayeumwa kila siku, na baadaye mkeo na mwishowe wewe utakuwa chakula cha wanga…., hahahaha.

‘Nimeshakuambia mbaya wako hayupo mbali nanyi ni mwanga, anakula watu usiku, kakimbia huki alipokuwepo, wanakijiji walitaka kumuua, hivi wewe unataka uambiwe nini…’ akacheka kwa dharau. Halafu akatugeukia kutuangalia mmoja mmoja kwa zamu, na kucheke tena na tena.

‘Lakini kiti wangu hatamuweza, kiti wangu nitamchukua mwenyewe siku ikifika, hamtamuona tena…hahahaha…atatokomoea kabisa….tutakwenda kuishi naye msipopajua…’ akasema mke wangu kwa sauti ambayo siyo yake kabisa ni sauti ya kidume dume yenye mkwaruzo, inayotetemeka.

Maneno haya sikuyapenda kabisa,  nikajua ni njama hizo za mganga wa kienyeji, sasa naona kaja na vitisho, nikajiuliza kwanini mke wangu yamtokee haya, na kwanini yaanze kipindi tu mama alipofika hapa. Na kauli hii ya kuwa mchawi wa familia yetu hayupo mbali na sisi, haikuwa ngeni, najua wanamuhis mama yangu hivyo, nikamwangalia tena, na yeye sijui alijua kuwa najiuliza maswala kama haya akaendelea kusema;

‘Kama huamini hayo ninayoakuambia,  ninaweza kuwathibitishia na kumweka hadharani mchawi wenu, lakini nitawaelezea kwanza kwa ishara zake ili mujue wenyewe…

Mbaya wenu huyu anachotaka ni mtu wa kumuachia mikoba yake ya uchawi wake. Je alipofika hapa hakuwa na mkoba mweusi j huo mkoba upo wapi…?’ akauliza nikakumbuka kuwa kweli mama alipofika hapa alikuwa na mkoba mweusi, na mama hakutaka mtu aushika, aliingia nao ndani na sijauona tena.

‘Mbaya huo muda wa kukabidhi mikoba yake umefika, ndio maana alikuja na mkoba wake huo, na kawaida ya watu hao, ni kukabidhi mikoba hiyo kwa watu wanaowapenda, na kipenzi chake ndio hicho kinachoumwa mara kwa mara, na hiyo ni sababu ya kumwingizia madawa yake ili mwisho wa siku muwe mnalea mwanga….’

‘Mkoba huo umeshaanza kukabidhiwa kwa anayetakiwa kurithi mambo hayo ya uchawi, lakini mimi nimekuwa nikimlinda, ndio maana kunatokea vita, na anayeumia ni mtoto….kazi mtapoteza, maisha yatakuwa magumu,..hamtaelewana..hadi hapo mbaya huyo atakaoshindwa, …..’akasema

‘Lakini keshajua kuwa ana mtu wa kutegemea, wewe…unayemlinda, wewe ndiye kikwazo…sasa muda umefika kuamua, je unataka mtoto wako arithi uchawi, au afe, ..je unataka mke wako afe…je unataka uwe masikini mpaka lini, je unataka kuteseka mpaka lini, ajali hiyo ilipangwa tu…na ule miwli uliofanana na wewe, ni wewe..ulishapelekwa kuzimu, lakini tukakuokoa..ili uje ujifunze, na usibadilika ukachukua hatua , yatakayofuata ni maba zaidi…

Aliendelea kusema mchawi wa mwanetu ndio yule yule aliyezoea kumshika mtoto kichwani, hiyo ni njia ya kumwingizia madawa yake na kujifanya anamsomea kumbe anamwekea mazindiko yake, na yote hayo yanafanywa ili mtoto arithi uchawi na mikoba hiyo. …je sio kweli?

Ni kweli mama kila siku mtoto akizidiwa anamuweka mkono wake kichwani kwa mtoto na huwa kama anamuombea hiyo imekuwa ni tabia yake, kila mtoto akizidiwa sana..

‘Natumai kwa sifa hizi mtakuwa mumemjua mbaya wenu, sasa kazi kwenu…’

Mara mke wangu akadondoka chini na kutilia kimiya , akihema mhemo wa mtu aliye usingizini.

NB: Mtihani

WAZO LA LEO: Maisha yakiwa magumu, na adui ujinga akaingilia kati, watu hufikia hatua wakawa na imani haba ya mungu, wakataliwa na shetani, wakaanza kuchukiana wenyewe kwa wenyewe, chuki , hadaa, fitina, shiriki zikatawala. Dawa ya hayo yote ni imani thabiti ya kuwa mungu yupo na muweza wa yote hayo ni mungu, na hayo hayataeleweka bila elimu, watu wasome waelimike, waijua dunia na mzingira yao. Wamjue mungu ni nani kwao.Ni mimi: emu-three

No comments :