Zilishapita siku tano, nipo hospitalini
hakuna hata ndugu yangu mmoja aliyejitokeza, huenda walikuwa hawajui nilipo,…,
basi vipimo vilivyotoka na kuonekana sina tatizo, na mimi nikajitutumua kuwa
sijambo, nikaruhusiwa mimi mwenyewe sikuona umuhimu wa kuendelea kukaa hapo
hospitalini, dakitari alipopita akanikaruhusi na mimi sikupoteza muda
nikaondoka kuelekea kituoni.
Inavyoonekana labda siku ile ya ajali
hakuna mtu anayenifahamu aliyeshuhudia tukio hilo, ilikuwa ni ajabu basi yaani hata wafanyakazi wanzengu hakuna aliyebahatika
kuwepo eneo hilo, nahisi na wao walikuwa na mambo yao, hasa kwa wale waliopata
Bahati mbaya kama yangu ya kupunguzwa kazi, kila mmoja alikuwa akiwaza lake, na
kuhangaika kivyake.
Kwa hali hiyo hata nyumbani hawajui wapi
nilipo, watakuwa wamehangaika sana, na sijui waliponiona sionekani nyumbani hadi usiku sijui walichukua hatua
gani. I Nikawa nawaza, na moyoni nikimshukuru mungu kuwa ni mzima, japo cha
moto ninakipata. Hapo sijui hata pa kuanzia, pesa sina…nikashika mfukoni na
kupata pesa kidogo niliyopewa na huyo mgonjwa jirani yangu na jamaa yake.
‘Hii ndio pesa ya mwanaume wa nyumbani,…sijui
watanipkeaje, wakiuliza pesa ya mfao sijui nitawajibu nini…siwaambii kuwa
nimeibiwa, …siri yangu….’nikawa naongea peke yangu.
Nilipotoka nje ya eneo la hospitalini, nilitamani nipate mtu mwenye simu nipige
nyumbani kwanza nijue hali ya wagonjwa maana siku ile ya tukio nilimuacha mama akiwa na mtoto
hospitalini , mtoto akiwa na hali mbaya, hata sijui ilikuwaje, nilipowaza hivyo
miguu isiyo na nguvu ikachanganya kutembea.
Nilifika eneo yanaposiamama magari,
nikapanda hilo gari na Bahati nzuri nikapata kiti, maana kama ingelikuwa
kusimama kwa hali niyo nayo ningemdondokea mtu, niliona baadhi ya watu
wakiniangalia kwa mashaka,..nahisi ni kwa jinsi nilivyokonda, au sijui kwanini
walikuwa wakiniangalia hivyo, sikujali akili yangu ikazama kwenye mawazo..
Nauli ya dala dala aliyonisaidia mgonjwa
aliyekuwa jirani yangu kwenye kitanda, ambaye nilimuelezea matatizo yangu
akanionea huruma akanipa pesa inisaidia kwa kwa nauli na hata jamaa yake moja
alipokuja kumuona yeye, sijui kama alimsimulia kuhusu mimi, kwani wakati anatuaga, akaja akanipa pesa
kidogo, nikashukuru sana.
Ajabu hata kondakita hakuniuliza nauli,
nikashukuru kimoyo moyo, nikatoka nje ya gari na kuanza kutembea kuelekea maeneo
ya hapo nilipoanga, kwanza kuna watu wa nyumba za jirani, niliona kupo kimiya,
watu hawapo…nikahisi kuna jambo, nikawa natembea hivyo hivyo kukaribia eneo la
nyumba niliyopanga.
Nikafika nyumbani, nilipokaribia nyumba
yenyewe nikashangaa kuona watu wamejaa hapo nilipopanga, akili ikanipaa, kwanza nikasimama na mawazo ya haraka
yakakumbuka mtoto aliyekuwa akiumwa, lakini pia nikajipa moyo kuwa nyumba hiyo
ni ya kupanga sipo peke yangu na familia yangu, huenda kuna kitu kimetokea kwa
wapangaji wenzangu.
Nikavuta pumzi, na kutembea kwa tahadhari
kuelekea hapo kwenye nyumba…
Tuendelee na kisa chetu…..
**********
Niliokutana nao awali ni watu ambao walikuwa hawanifahamu vyema, nikaona wengine
wakinisalimia na kunipa pole, mmoja akasema;
‘Huyu ni kaka yake nini, mbona wanafanana…’mmoja akasema mimi
nikajiuliza moyoni kwanini wanasema hivyo, nikasogea nikakutana na mtu wa kwanza
anayenifahamu, akaniangalia, akanitolea jicho, akashika mdomo, akasogea kinyume
nyume, akageuka na kutimia mbio…
Nikaduwaa, nikasimama, sielewi kitu….
Mara ghafala wakajitokeza watu wanaonifahamu ikawa hali ni ile
ile, kile aliyeniona hakuniangalia mara mbili, hugeuka na kutimua mbio, watu
waliokusanyika hapo wakawa wanakimbia kutoka eneo hilo, na kila niyemkaribia
akawa anakimbia, na hadi kukabakia kweupe, nikabakia nimeshangaa kulikoni......
Nikatembea kuingia ndani, nikaona kimiya, waliobakia hapo ni mama
, mke wangu na ndugu za mke wangu…mama akasimama na kuniangalia kwa makini, mke
akakurupuka, nikajua ni yale yale mashetani nikageuka kumfuata mamamama, ikawa
kama nimejichongea mke alitoka mlangoni na kutimua mbio
‘Mshikeni yule jamani atapotea tena..’nikasema hakuna
aliyenisikiliza, wale jamaa zake na wao wakatoka mlangoni na kuanza kukimbia,
nikabakia mimi na mama na mtoto…nikamtizama mtoto akiwa kalala chini, alikuwa
bado kadhoofika lakini moyoni nikshukuru kuwa ni mzima, kwahiyo nikapumua
‘Kuna nini hapa mama?’ nikamuuliza mama ambaye alikuwa kasimama
kaganda, hasemi kitu, nilipoona hivyo nikamfuata mwanangu pale alipolala,
nikamuinua akafumbua macho, na kwanza aliniangalia kwa makini halafu akawa kama
anawaza jambo , akasema;
‘Kumbe hujafa baba….’akasema
‘Sijafa, nani kasema nimekufa...?’ nikauliza na kumgeukia mama,
mama alikuwa kainua mikono juu kama anaomba, akaniupia jicho akiniangalia kwa
mshangao, na mara nyingi kukasikia kilio,…gari likasimama nje, nikachungulia
kupitia dirishani, nikamuona mama akanisogelea na kunishika mkono akasema;
‘Ingia ndani ulale, utulie kimiya..’akasema, na mimi nikashangaa
nikamuangalia mtoto , mtoto akasimama, akanishika mkono, tukaongozana kuelekea
chumbani nikafika kitandani nikajilaza, nilishikwa na usingizi wa ajabu na
ndani ya usingizi niliota nimekufa napelekwa kuzikwa..
Ilkuwa ni ndoto ya kutisha, maana nilijiona kabisa nimekufa, na
nimeshaandaliwa kuzikwa, na wakati nimeshafikishwa kaburini na kunitumbukiza
humo wakaanza kunifukia nikazindukana, nikakurupuka, watu walipoona hivyo, wakaanza kukimbia…na mimi nikatoka mle
kaburini kwa haraka na kuanza kukimbia, kuwafuata watu na watu wakazidi
kunikimbia kama vile nawakimbiza wao, nikazindukana.
Nilipofungua macho, nikaona watu wamesimama karibu ya kitanda,
alikuwepo dakitari ninayemfahamu, walikuwepo wazee, na ndugu ndugu upande wa
mke wangu, na majirani, kila mmoja akiwa aknitolea macho, wakiwa hawaamini,
nikakaa vyema kitandani na kuwauliza
‘Hivi kuna nini hapa nyumbani?’ nikauliza
‘Taarifa zilizokuja ni kuwa umepatwa na ajali na umekufa, na hapo
ulivyotukuta tulikuwa tuansubiria mwili wako kwa ajili ya mazishi yako, mara
unatokea, na wakati huo watu wamekwenda kuchukua mwili wako muchwari,
muhimbili, na cha ajabu kabisa, watu wamepewa mwili unaofanana na wewe kabisa,….’akasema
mzee mmoja
‘Kwahiyo mnasemaje, mnataka kuhakikisha kuwa mimi ndiye halisi au
mimi ni mzuka…’nikauliza
‘Tumeamini kuwa wewe ni halisi, maana dakitari huyu hapa ambaye ni
mmoja wa watu waliokupokea huko muhimbili, na pia maiti iliyoletwa haina
majeraha, ina maana hiyo maiti ilikufakifo cha akwaida imesharudishwa na
wenyewe wamaitambua..’akasema mzee huyo
‘Huu sasa ni uchuro, inabidi mkatambike kwenu..’akasema mzee mmoja
akimuangalia mama yangu.
‘Ni Bahati mbaya tu, hakukuwa na mawasiliano maana mimi nilipata
ajali nikapoteza kila kiu na hakuna aliyeweza kutambua au kuhangaika kutafuta
jamaa zangu hata waliponiuliza sikuwa aili ya kusema waje huku, kwanza wengi
walioniuliza ni wageni kwangu….ndio hivyo namshukuru mungu nimepona kiwmili
lakini kiakili naona nipo mfu…’nikasema
‘Ina bidi msome duwa, na maombi kwa mungu, kuna tatizo kwenye hii
nyumba…kwenye hiyo familia yenu…’akasema mzee mwingine, na wakati huo nikaona
wakimuingiza mke wangu ambaye alisogea na kuniangalia kwa makini, akionyesha
kuogopa, wakawa wamemshikilia bara bara, lakini alivyowatoka hutaamini wote
walitupwa chini mke akatoka mbio, …
‘Wewe lala tu, hilo tuachieni sisi wenyewe….ila mwenye nyumba yupo
hapo nje, alitaka kuja kuongea na wewe….sijui anasemaje’wakasema ndugu wa
upande wa mke wangu.
‘Anasema anataka huyu mpangaji, ahame kwenye nyumba yake haraka, maana
eti ana mkosi, mara afe mara afufuke na kodi halipi,…’akasema jirani mmoja
‘Hayo ni ya kuongea tu, muhimu tumuacheni huyu mtu utulie kwanza,
ndugu kutananie mliongee muone jinsi gani ya kuisaidia hii familia….’akasema docta
aliyeitwa kunichunguza kama kweli ndiye mimi, na kweli watu wakatoka na
kuniacha nikiwa nimeduwaa…hata sielewi nifanye nini, akili ilikuwa imesimama
kwa muda.
************
Mambo ndio hayo, mke
ana kinachoitwa mashetani, mtoto anaumwa magonjwa yasiyojulikana , kazi sina,
pesa sina, mwenyenyumba anataak nihame, haraka iwezekanavyo, huku nimetambulikana
kuwa nimekufa…..
Kutokana na matatizo ya mke wangu, na mtoto, mke wangu akapata ushauri
kwa mashoga zake kuwa madude hayo yana wataalamu, ambao ni waganga wa kienyeji,
na mmoja wa mashoga zake akamuelekeza kwa mtaalamu mmoja huko Temeke.
Basi siku hiyo, akaamua kuanza kumfuatilia mganga huyo aliyekezwa
kwake. Kabla ya hapo hakuwa na tabia hiyo ya waganga wa kienyeji, kwani ni
mmoja wa watu waliokuwa wakipinga imani hizo,lakini uvumilivu ukamshinda, baada
ya kukumbana na mitihani hiyo.
Akaamua kujaribu njia hiyo, huenda atafanikiwa, akaaga kuwa kweli
anakwenda kwa huyo mtaalamu, mimi nilimwambia huko siwezi kwenda kabisa, kwanza
sikupenda kuonekana na watu, mwili wangu ulikuwa bado hauna nguvu, na muda
mwingi nilikuwa nalala tu nikiwaza.
Mke wangu aliondoka na mdogo wake, Sisi tukabakia na mtoto na
mama. Tulikuwa na hamu sana ya kusikia nini wataambiwa, kwani wenyewe
tulishaanza kuhisi kupotoshwa, kama tujuavyo. Wengi wa waganga hawa ni wafitinishaji,
ingawaje kweli wapo wenye dawa za kusaidia, lakini ukienda kwa wale wanapiga
ramli, ujue umekwisha.
‘Mwanangu utakuja kusikia mabaya zaidi….na huenda na wewe
ukanichukia, ..mimi naona nitafute nauli niondoke, lakini nashindwa kuondoka
kwa hali kama hii, wewe ndio hivyo unaumwa, huna pesa…mjukuu anaumwa, mke ndiye
huyo kachanganyikiwa,…’akasema mama
‘Mama wewe huendi popote, utakaa hapa hapa, kama nikuondoka
tutaondoka wote, maana kama ulivyosikia mwenye nyumba hatutaki kwenye nyumba
yake, hata mimi sipendi kukaa hapa tena,…’nikasema kumuambia mama
‘Ninachokiomba ni mkeo apate matibabu apone, lakini sio huko
kudanganywa, na nina wasiwasi huko watamdanganya sana, na kuna dawa aliandikiwa
mtoto za kununua hatujanunua, badala ya kuhangaika tupate pesa za kumibia mtoto
wanahangaika na waganga wa kienyeji, ndugu zake wamelishikilia hilo kweli…’akasema
mama
Mimi nilikuwa nikikuna kichwa kwa mawazo, kwani hali yandani
ilikuwa ngumu, chakula kilikuwa cha shida, na dawa za mara kwa mara za mtoto
zilikuwa zinahitajika, kwahiyo nilikuwa sina amani kabisa kichwani.
Hapo nikawa hata sijui niende kwanani, nilikuwa nimepungua sana
kwa muda mfupi. Nilishukuru mungu kuwa sikuwahi kupata ,maradhi, la sivyo,
ningekwisha kabisa. Nilishngaa nguo zangu zote nilizokuwa nikivaa, zikawa
zinanipwaya, ilibidi kuongeza tundu nyuma ya mkanda, ili niweze kuzivaa baadhi
ya suruali zangu.
Huko walipokwenda mke wangu
na mdogo wake, walichelewa kurudi hadi jioni, tukawa na wasiwasi hata simu yao
ilikuwa haipatikani, tukadhania kuwa huenda kazidiwa, lakini tukaona tuvute
subira.Na jioni ilipofika wakaingia wakiwa wamechoka, labda kutokana na usafiri
au njaa. Walitusalimia kwa sauti ya kuchoka, na tukawaitikia, na wao
wakakimbilia ndani kujipumzisha kwanza.
`Ndugu yangu,…nilipatwa na mtihani, katika maisha mtumainie mungu
peke yake, usiwatumainie wanadamu, huo ni ushauri wangu kwako, kila siku muombe
mola wako akulinde na vitimbwi vya shetani kwasababu shetani akitaka kukupoteza atapenyeza mirija yake
kupitia sehemu yoyote aipendayo, na baya zaidi anaweza akaitumia familia yako
kama silaha yake.
‘Nikuambie ukweli mjumbe, watoto, mke na mali ni mtihani mkubwa
hilo nakuthibitishia kivitendo. Anaweza asiwe mke, akawa mume pia kutegemeana
na nani mwenye uthabiti ndani ya familia, hilo mimi limanipata na nimejifunza….’akasema
mjumbe.
`Jioni aliporudi mke wangu
kutoka kwa mganga sikupenda hata kumsikiliza,lakini kwa vile tulitaraji huenda
kafanikiwa kuileta dawa ya mtoto tukakaa pamoja mezani kumsikiliza, tulikuwepo
mimi, mama yangu na mdogo wa mke wangu ambaye ilibidi abakia hpo kusaidia kazi.
Mama mkwe alisema shemeji yangu huyo atabakia hapo ili awe msaada.
Mimi sikupenda mtu mwingine kubakia kutokana na hali za kiuchumi
zilivyo atakuja kuteeka na njaa, ije kuwa lawama, nikasema kumuambia mama mkwe;
‘Kwa vile mama yangu yupo hapa, haina haja,…kama ni swala la
kupata msaidizi wa kulea mtoto..’ nikamwambia mama mkwe, mke wangu akasema.
‘Siwezi kumtuma mama mkwe, nikiwa na shida, na mama ni mtu mzima,
kazi za nyumbani hapa ataziweza zote, na kwanini usitake ndugu yangu kuja
kuishi hapa…?’ akasema mke wangu kwa hasira. Ilibidi nikubali shingo upande, na
mdogo wa mke wangu, akaja, na akawa analala na mama yangu.
Tukawa sasa tunasubiri kusikia taarifa ya kutoka huko kwa mganga
wa kienyeji, kwanza tulitangulia kukaa mezani , mimi , mama na shemeji yangu …na
mtoto, mke alibakia ndani kwa muda, labda alikuwa akinywa dawa , tukawa
tunamshubiria.
Basi mke wangu alitoka chumbani na kuja kukaa nasi pale mezani,
ilionekana akiwa na wasiwasi na anachotaka kutuambia. Mdogo mtu akawa
anamtizama dada yake aanze kuongea, yeye hakutaka kusema wameambiwa nini kutoka
huko kwa mganga wa kienyeji.
Basi tukatulia kimya
kumsikiliza mke wangu. Kitu cha kwanza kulichotutia hofu na pale waliporudi, walipofika
tu, walifanya jambo la ajabu, kwani
walivyofika tu,walienda moja kwa moja alipokuwa amelala mama na mtoto. Mama
yangu na mjukuu wake walikuwa wametandika mkeka nje na kujilaza huku wakipata
upepo mwanana unaotoka kwenye mti uliopandwa hapo nje.
Wao walifika pale walipolala, ghafla wakamzoazoa mtoto . Mama
akabakia kashanga, lakini hakusema kitu. Mara nyingi mtoto wangu alikuwa
akimpenda sana bibi yake, kuliko hata mama yake, kwasababu hasa ya matatizo
yaliyokuwa yakimtokea mara kwa mara mke wangu hadi mtoto akawa anamuogopa.
Mara nyingi mke wangu akichanganyikiwa, huwa hamtambui kabisa hata
mwanae, anaweza akampiga hata kumuumiza, kwahiyo mtoto akawa kajenga umbali
kati yake na mama yake akiogopa kipigo.
Walipofika muda huo nilikuwa nimsimama mlangoni, niliona kitendo
hicho, cha wao kumchukua mtoto wangu wangu pale alipokuwa kalala na mama,
nikataka kuliingilai lakini niaona haina haja, ngoja nivite subira, nilifikiria labda ni sehemu ya dawa, ila nilimuona mama
akisononoke kwa kutikisa kichwa. Nilimtizama nikamuashiria atulie kwa mkono,
naye alitulia kama mimi.
Basi baadaye tukajiunga mezani kupata chakula cha usiku na
kusubiri nini kimeletwa toka huko kwa mtaalamu. Wakati tumetulia kusikiliza
nini wamekuja nacho, na wakati huo shemeji yangu ndiye aliyekuwa kambeba
mtoto,tofauti na siku zilizopita ambapo bibi yake ndiye aliyekuwa mara nyingi
anambeba huyo mtoto.
Ghafla mke wangu akaachia kijiko alichokuwa kakishika na kudondoka
chini, sakafuni sote tukageuzo vichwa upande wake, tukajua mambo yameanza,….mke
akawa pale chini na kama kawaida akaanza kutetemeka, kujibamiza
Nikamuangalia shemeji , nikamuashiria sogee mbali, kwa vile yeye
ndiye aliyembeba mtoto, lakini hakufanya hivyo, akachukau chupa yenye maji
akamwangaia dada yake kichwani.
Kwa kitendo kile tukajua mambo yamenza, huwa matatizo yake huanza
hivyo hivyo. Anaweza akamrukia mtoto akataka kumkaba, au yoyote miongoni mwa
waliopo mbele yake, na kwahiyo inatakiwa mtu amuwahi mapema, la sivyo anaweza
akaleta madhara.
Mimi kwasababu nilishamjua, nikajua moja kwa moja kuwa
keshapandisha yale maruheruhe yake, na hapo hapo ilibidi tufanye kazi ya ziada
kumkamata na kumweka chini, hapo chini alianza kutingishwa na akawa anajibamiza
chini kwa nguvu, na mdogo wake alipommwagia yale maji akatulia, akitulia hivyo
ujue ana ujumbe fulani, anataka kuutoa, na akishautoa hunyamaza kimya na hali
yake hurudi kama kawaida. Tukausubiri huo ujumbe, na kweli akainua kichwa na
kwa muda halafu akawa anatutizama mmoja mmoja kwa zamu.
‘ Mnataka kumjua mbaya wa familia hii au siyo,…. basi ngoja
niwapashe kuhusu , mbaya wenu, mbaya wenu hayupo mbali nanyi kabisaa…, mbaya
wenu anataka kumpoteza huyo mtoto , anataka abakie ndani ya nyumba hii kama
malikia na baadaye amuue hata mtoto wake wa kumzaa…mchawi hana ndugu mchawi
hana mtoto….akitaka damu ya mtoto ni lazima aipate’ akainuka na sote
tukajiandaa, tukijua anataka kukimbia
Alisimama akawa anatuangalia huku kashika kiuno na halafu
akanigeukia mimi na kusema;
‘Wewe usiyeelewa kitu, nishakuambia familia yako itasambatarika
kama vumbi kwenye upepo mkali. Heu angalia sasa hivi huna kazi, maisha magumu,
mume gani usiyekuwa na kazi, hujiulizi tu, wewe hujui nini kinasababisha yote
haya, basi yote hayo yanasababishwa na huyo mbaya wenu.
‘Alitaka kukua, alitaka kukugeuza ndondocha, lakini akaambiwa muda
bado…kwanza, anataak damu changa, anataka damu changa….Nakuambia unielewe
mapema, kwani mwishowe utamkosa mtoto wako huyo anayeumwa kila siku, na baadaye
mkeo na mwishowe wewe utakuwa chakula cha wanga…., hahahaha.
‘Nimeshakuambia mbaya wako hayupo mbali nanyi ni mwanga, anakula
watu usiku, kakimbia huki alipokuwepo, wanakijiji walitaka kumuua, hivi wewe
unataka uambiwe nini…’ akacheka kwa dharau. Halafu akatugeukia kutuangalia
mmoja mmoja kwa zamu, na kucheke tena na tena.
‘Lakini kiti wangu hatamuweza, kiti wangu nitamchukua mwenyewe
siku ikifika, hamtamuona tena…hahahaha…atatokomoea kabisa….tutakwenda kuishi
naye msipopajua…’ akasema mke wangu kwa sauti ambayo siyo yake kabisa ni sauti
ya kidume dume yenye mkwaruzo, inayotetemeka.
Maneno haya sikuyapenda kabisa, nikajua ni njama hizo za mganga wa kienyeji,
sasa naona kaja na vitisho, nikajiuliza kwanini mke wangu yamtokee haya, na
kwanini yaanze kipindi tu mama alipofika hapa. Na kauli hii ya kuwa mchawi wa
familia yetu hayupo mbali na sisi, haikuwa ngeni, najua wanamuhis mama yangu
hivyo, nikamwangalia tena, na yeye sijui alijua kuwa najiuliza maswala kama
haya akaendelea kusema;
‘Kama huamini hayo ninayoakuambia, ninaweza kuwathibitishia na kumweka hadharani
mchawi wenu, lakini nitawaelezea kwanza kwa ishara zake ili mujue wenyewe…
Mbaya wenu huyu anachotaka ni mtu wa kumuachia mikoba yake ya
uchawi wake. Je alipofika hapa hakuwa na mkoba mweusi j huo mkoba upo wapi…?’
akauliza nikakumbuka kuwa kweli mama alipofika hapa alikuwa na mkoba mweusi, na
mama hakutaka mtu aushika, aliingia nao ndani na sijauona tena.
‘Mbaya huo muda wa kukabidhi mikoba yake umefika, ndio maana
alikuja na mkoba wake huo, na kawaida ya watu hao, ni kukabidhi mikoba hiyo kwa
watu wanaowapenda, na kipenzi chake ndio hicho kinachoumwa mara kwa mara, na
hiyo ni sababu ya kumwingizia madawa yake ili mwisho wa siku muwe mnalea
mwanga….’
‘Mkoba huo umeshaanza kukabidhiwa kwa anayetakiwa kurithi mambo
hayo ya uchawi, lakini mimi nimekuwa nikimlinda, ndio maana kunatokea vita, na
anayeumia ni mtoto….kazi mtapoteza, maisha yatakuwa magumu,..hamtaelewana..hadi
hapo mbaya huyo atakaoshindwa, …..’akasema
‘Lakini keshajua kuwa ana mtu wa kutegemea, wewe…unayemlinda, wewe
ndiye kikwazo…sasa muda umefika kuamua, je unataka mtoto wako arithi uchawi, au
afe, ..je unataka mke wako afe…je unataka uwe masikini mpaka lini, je unataka
kuteseka mpaka lini, ajali hiyo ilipangwa tu…na ule miwli uliofanana na wewe,
ni wewe..ulishapelekwa kuzimu, lakini tukakuokoa..ili uje ujifunze, na
usibadilika ukachukua hatua , yatakayofuata ni maba zaidi…
Aliendelea kusema mchawi wa mwanetu ndio yule yule aliyezoea
kumshika mtoto kichwani, hiyo ni njia ya kumwingizia madawa yake na kujifanya
anamsomea kumbe anamwekea mazindiko yake, na yote hayo yanafanywa ili mtoto
arithi uchawi na mikoba hiyo. …je sio kweli?
Ni kweli mama kila siku mtoto akizidiwa anamuweka mkono wake
kichwani kwa mtoto na huwa kama anamuombea hiyo imekuwa ni tabia yake, kila
mtoto akizidiwa sana..
‘Natumai kwa sifa hizi mtakuwa mumemjua mbaya wenu, sasa kazi
kwenu…’
Mara mke wangu akadondoka chini na kutilia kimiya , akihema mhemo
wa mtu aliye usingizini.
NB: Mtihani
WAZO LA LEO: Maisha yakiwa magumu, na adui ujinga
akaingilia kati, watu hufikia hatua wakawa na imani haba ya mungu, wakataliwa
na shetani, wakaanza kuchukiana wenyewe kwa wenyewe, chuki , hadaa, fitina,
shiriki zikatawala. Dawa ya hayo yote ni imani thabiti ya kuwa mungu yupo na
muweza wa yote hayo ni mungu, na hayo hayataeleweka bila elimu, watu wasome
waelimike, waijua dunia na mzingira yao. Wamjue mungu ni nani kwao.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment