‘Kama huamini hayo ninayoakuambia, ninaweza kuwathibitishia na kumweka hadharani
mchawi wenu…nitakuelezea sifa zake ili mmfahamu mbaya wenu…’ hiyo ilikuwa suati
ya ajabu ikitoka mdomono mwa mke wangu….
‘Mbaya
huo muda wa kukabidhi mikoba yake umefika, ndio maana alikuja na mkoba mweusi,
ambao hautakiwi kushikwa na mtu mwingine zaidi ya mrithi wake na mrithi wake,
na kikawaida mrithi wake anakuwa kipenzi chake, na kipenzi chake ndio hicho
kinachoumwa mara kwa mara, na kuumwa kwake ni sababu ya uchawi unangizwa mwilini mwake
ili mwisho wa siku mtoto anakuwa mwanga….’
‘Katika hatu za kuukabidhi huo uchawi,
inabidi kuwa karibu na mtu wake, na kila mara anatumia mkono wake wenye nguvu
ya uchawi, kwa kushika kichwa cha mrithi wake, hiyo ndiyo njia ya kumwingizia
madawa yake na kujifanya anamsomea kumbe anamwekea mazindiko yake, na yote hayo
yanafanywa ili mtoto arithi uchawi na mikoba hiyo. …je sio kweli?
‘Natumai kwa sifa hizi mtakuwa mumemjua
mbaya wenu, sasa kazi kwenu…’
Mara mke wangu akadondoka chini na kutulia
kimiya , akihema mhemo wa mtu aliye usingizini.
Tuendelee na kisa chetu…
*************
Akili mwanadamu ilivyo huwa
inaamini kirahisi pale inapoona mifano halisi, hata kama mifano hiyo ni viini
macho tu, sijui ni kwanini, kwani zile
dalili alizozitaja huyo mke wangu kwa kupitia hiyo sauti sijui ndio shetani
aliyemuingia mke wangu zilikuwa sawa sawa kabisa.
‘Au ni kwa vile mke wangu alimuona mama akifanya ndio maana ikawa
rahisi kusema hivyo’ nikasema moyoni, lakini ukumbuke aliyekuwa akiongea si mke
wangu nikiwa na maana sauti ilikuwa tofauti kabisa na ya mke wangu, je ina
maana mke wangu kafanga kuigiza hiyo sauti,
Akili ikaanza kutafakari upande wa pili, nikianzia kukumbuka kuwa
matatizo haya yalianza pale tu mama alipokuja kuishi na sisi, kabla ya hapo
kulikuwa hakuna matatizo, mtoto alikuwa haumwi, mke alikuwa hana hayo
mashetani, na kazini mambo yalikuwa sio mabaya, nilionekana mchapaakzi hodairi
japokuwa malipo hayakuwa mazuri saana ...
‘Mkoba mweusi…’
Ni kweli mama alikuja na mkoba fulani mweusi, hakutaka upokelewe, na hadi sasa sijui ulipo. Ina
maana kweli humo ndio kuna vitu alivyotaka mjukuu wake arithi, sizani,
nitamuuliza vyema kuhusu huo mkoba na wapi alipouweka,…hapo nikageuka
kumuangalia mama kutaka kumuuliza lakini nilihis kama nikimuuliza hivyo ataona
nimeamini hayo mambo.
Pia ni kweli kuwa mama ana tabia ya kumshika mtoto kichwa kama
vile anamuomba , na mimi sikuona ubaya wa hilo, na ni kweli pia mama ni kipenzi
cha mjukuu wake, kwani hapo kuna ubaya gani, lakini kwanini hayo yasemwe na
hilo sijui ni shetani au ni kitu gani...nikaanza kuhisi kitu kikinipa mtihani
kichwani.
Nikahema kwa muda halafu nikamwangalia mke wangu kuhakikisha kuwa
ile hali aliyokuwa nayo imekwisha, alikuwa katulia pale alipokuwa , haonyeshi
dalili ya kutingishwa tena, akili yangu ikazama kwenye mawazo….
Nikawa nawaza ni kwanini hayo yaongelewe kumuhusu mama, na sio mtu
mwingine je ni kwa ajili ya chuki, kama ni chuki ni chuki za nini kwa mama,
kwani mama ana kitu gani cha kufanya watu wamchukie, au ni kwasababu hatakiwi
humu ndani , kwanini hatakiwi wakati mimi ni mwanae, na mke wangu mwenyewe
ndiye alitoa pendekezo hilo kuwa mama aje kuishi na sisi, kw avile huko
kijijini anapata shida…!
‘Labda kuna mtu ana chuki na familia hii akapanga hayo yatokee,
sasa kama ni kupanga walipanga saa ngapi,, na jinsi gani waliweza kumfanya mke
wangu aweze kuigiza sauti kama hiyo ya kiume, ya kiume kweli...nilipofikia hapo
nikataka nimuulize mama maswali angalai akili yangu itulie huenda akanisaidia, taratibu
nikagauke kumuangalia mama ambaye kwa
muda huo alikuwa kainama chini, alikuwa kakiangalia chakula huku kijiko kikiwa
nusu kwenye sahani na nusu kwenye meza.
Nilitaka niwe mimi na mama tu waakti namuuliza, sikutaka mtu
mwingine, kwahiyo nikaona nitafute njia ya kumtoa hapo huyo shemeji yangu,
nikageuka kumuangalia shemeji, ambaye alikuwa akimtengeneza mtoto vizuri
asiumwe na mmbu.
Kabla sijasema lolote, mara mke wangu akainuka pale alipokuwa
amekaa akasimama, akatutizama akionyesha kushangaa, akakunja uso kama kujiuliza
kumetokea nini, akajikagua, akageuka kuangalia mlangoni, moyoni nikasema
anatafuta njia ya kukimbia, nikajiandaa kumdaka
Akageuka akamuangalia mama, alimuangalia mama kwa muda, halafu akageuza
kichwa huku na kule, kama anatafuta kitu, halafu taratibu akatembea kuelekea chumbani, tukaona
hakuna haja ya kumsumbua tena. Tulibaki mimi na mama na shemeji yangu na mtoto,
mtoto kwa muda huo alikuwa amepitiwa na usingizi.
Nikataka kuhakikisha kuwa hana homa, na kweli alikuwa hana homa,
alikuwa na hali ya kawaida ila mwili ulikuwa umelegea, hana nguvu, utafikiri
kanyweshwa madawa ya kulevya, alikuwa hapendi kula kabisa
Mama ndiye aliyeanza kuongea baada ya kimya kirefu, na kauli yake
ndiyo iliyonifanya nisinyae na yale mawimbi ambayo yalishatanda kichwani na
kuniweka njia panda yaliyeyuka ghafula. Mama alisema hivi;
‘Uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi, na mzazi ninayemzungumzia hapa
ni mama, sizani kama kuna mzazi anaweza kuyasahau machungu ya uzazi wake, hasa
ukiwa washida,…kwa mwanamke aliyezaa anaweza kunielewa haya ninayoyaongea.
‘Na uchungu wa uzazi unatofautiana, wengine wanaponea tundu la
sindani, kama ulivyokuwa uchungu wangu, wakati nahangaika kukuzaa wewe mwanangu....uchungu
huo humfanya kila mara mzazi ashituke pale mtoto wake anapopatwa na matatzo
hata kama yupo mbali vipi....’akahema na kutulia
‘Mwanangu nimekuzaa kwa shida sana, wakati mwingine nafikia kuwaza
kuwa hakuna mwanamke aliyepitia machungu hayo niliyopitia mimi. Kumbuka wakati
nakuzaa wewe ilikuwa ni maamuzi kuwa uzaliwe wewe mimi nife au wewe ufe mimi
nizaliwe,…nilivumilia machungu, nilijitahidi, na kwa uwezo wa mungu, mimi
nauita ni muujiza tulipona sote. Na baaada yaw ewe kutoka duniani nilipoteza
fahamu.
Mwaanngu nilipozindukana, nilijikuta nipo chumba cha upasuaji,
ilibidi wanifanyie upasuaji wa haraka, na kilichoamuliwa ni kutolewa kizazi,
ili niweze kuishi, wanajua wenyewe madakitari kuwa ilikuwa ni sababu
gani..kwangu mimi , muhimu ni kuwa wewe umezaliwa upo hai, hata nikifa tena,
basi...
Mwanangu, nilipokuzaa wewe, na mungu akahakikisha sitapata mtoto
mwingine tena, labda ni kwa manufaa yangu au labda ni kwa ajili ya mitihani mingine
ya ulimwengu huu. Je kama ningewazaa watoto wawili au watatu na umasikini
niliokuwa nao ningeliwalea vipi, labda …sijui labda, baba yako angeliweza
kumudu, hata hivyo, siwezi kujua mungu kwanini alipanga hivyo.....’akatulia
kidogo
‘Huenda ilitakiwa iwe hivyo ili niendelee kupata mitihani ya
dunia, kwani kutokuzaa tena ikawa ni tatizo kwangu, ndicho kilichofanya niachane
na baba yako kwasababu nilikuwa na uwezi wa kumpatia mtoto wmingine...mwanamke
gani asiyezaa.. binadamu hana shukurani.’akatulia kidogo
‘Hahaha, mwanangu, leo hii eti naambiwa, mimi nimekuwa mchawi, ninataka
kumuua mwanangu,…niiue damu yangu, kwanini
sikumuua wakati namzaa, kwanini sikumuua wakati nahangaika naye nikiwa sina
mbele wala nyuma, nije kumuua sasa hivi akiwa ndiye msaada wangu....hilo
lifikirie kwa makini mwanngu,….eti pia nataka kumuua mjukuu wangu, haah, hivi
kwel inaingia akilini…’akatulia mama
‘Mjukuu wangu nimemuona kama mtoto wangu wa pili, maana kizazi
kilishatoka kwa ajili yako mwanangu, na mungu akaona anipe mjukuu au wajukuu badili yake, sasa mimi niwaue,….ooh,
jamani, kweli hili limeniuma sana, sana, lakini nitafanyaje....’akatulia kidogo
‘Lakini huyo ni mke wako una haki ya kumsikiliza mwanangu, mimi ni
mama tu, huenda wakati wangu ulishapita, baada ya kubeba mimba miezi nane,
sijui, nikakuzaa kwa shida, nikakulea kwa shida, nani atayajua hayo, labda
yaliyopita si ndwele tugange yajayo, sisi tumeshapitwa na wakati, sasa ni zamu
ya mke wako, ....mapenzi sasa ni kwa mke, ...msikilize mke wako...’akasema mama
‘Nakumbuka kuna siku za mwanzoni, nilikuwa mara kwa ma ra nakupigia
simu kila nikikwama, mke wako akanipigia simu na kuniambia, nisizani kuwa nyie
huku mjini mnafaidi,...mnahangaika kutafuta, kwa shida, nipunguze kukupigia
simu kukuambia shida zangu, ...’akatulia
‘Baada ya kuupata ujumbe huo, ndio maana nikawa sihangaiki
kuwapigia simu tena, watu wenyewe , wale waliowhi kuja kwangu au kupita hapo
ninapoishi ndio waliokuja kuwasumbua, sikupenda kabisa mwanangu iwe hivyo, nitafanya
kazi kwanani kwa hali hii, shambani ukilima hakuna mavuno, na jembe lenyewe ni
jembe basi…ni maisha ya shida niliyoishi, ninabakia kuomba omba…
‘Kwahiyo mwanangu, sikupenda kuja kuwasumbua, msikilize mke
wako,..kwani hata wewe kuja kunichukua sikufurahia, najua nitawakwaza, lakini sio
kiasi cha kuniita mimi mchawi, ni chuki gani hiyo inayofikia hatu ya kumvunja
mzazi nguvu kiasi hicho, hivi mnaelewa, ni jinis gani mtu anavyojisikia akiitwa
mchawi, kitu ambacho hakijua, ….’akasema na mimi nikaingiwa na mshangao, ina
maana mke wangu aliwahi kumpigia mama simu na kumwambia hivyo.
‘Unajua mwanangu kuna muda natamani mungu aichukue roho yangu tu
nijifie nikaenda kupumzika tu, ili niaachane na haya mateso ya dunia, maana kila hatua ya
maisha yangu imekuwa ni mateso, sikumbuki kuiona raha yah ii dunia, labda
kipindi naishi na mama, naishi na wazazi wangu, baada ya hapo, dunia ikanitenga….sasa
nina mtoto nilitamani na mimi nipumzike, nile jasho langu, kumbe ndio bado
kabisa mambo yanaongezeka …’ akasema
mama.
Mama aliinama chini kama anaomba, halafu akainuka kuelekea
alipolala mtoto wetu, na akainua mkono wake kama kawaida yake akauweka juu ya
kichwani cha mtoto, sijui alikuwa akisema maneno gani, na kwa muda ule mke
wangu alikuwa anatokeza mlangoni,,,,,
Mimi kwa vile nilishamfahamu mama kuwa kila akitaka kulala huwa
anamfanyia mjukuu wake vile kama kumuombea dua ya usiku mwema, sikuwa na shaka,
kumbe kwa muda huo mke wangu alikuwa akitoka, kutokea chumbani alipokuwa, na wakati anafika mlangoni akakiona kile
kitendo cha mama kumshika mjuu wake kichwani.
Shemaji yangu aliyekuwa kambeba mtoto alikuwa akimuangalia mama
kwa chuki akitaka kumzuia, ….tahamaki, mke wangu akakurupuka kutoka pale
mlangoni na kumrukia mama, akamsukuma mama kwa nguvu zote, msukumo ambao ulimfanya mama adondoke chini na
kwa bahati mbaya kichwa chake kikagonga kwenye meza na mama akapoteza fahamu.
Niliduwa ghafla, nilimtizama mke wangu nilihisi labda alikuwa kapandisha,
kwani akipinadisha mashetani yake huwa
hivyo, na huwezi kumlaumu, lakini nikagundua kuwa yupo katika hali yake ya
kawaida, ila kilichoonekana pale ni chuki ya wazi machoni, na alionyesha kuwa
angeendelea kumuumiza mama kama angeinuka,
Kiukweli sikuweza kuvumilia, hapo hapo nikainuka kwenye kiti. Na
kumwangalia mama akiwa katulia kimya, na akilini nikajua mama keshakufa, mwili
ulinitetemekea kwa hasira, moyoni nikajua mke wangu keshamuua mama yangu, …nilimwendea
mke wangu kwa hasira na kumshika mabegani..
Hasira zilinipanda, sijui ni kwasababu ya yaliyotokea au ni
kwasababu ya kusukumwa kwa mama..na sijui kama mama yupo hai au vipi, …,ila
nakumbuka nilimzoazoa mke wangu na kumtupia pembeni ….kwanza sikutaka kuchukua
hatua ya kipigo, kwni ningelifanya hivyo ningeliua, subira ikanisaidia,…mimi
nikageuka kumuangalia mama pale alipolala, sijui nilipata nguvu wapi za kumbeba
mama, maana mama ni mnzitp…nilimuinua mama na kumweka kwenye sofa;
Nilimtikisa mama, kimiya,…ina maana mama kweli amekufa, nikaanza
kulia
‘Mama, mama, mama.. usife mama, bado nakuhitaji sana mwanao…’
Nililia kwa muda mrefu, huku namtingisha mama aamuke, nikiyaruidia
hayo maneno kuwa;
`Mama nakuomba usife bado
nakuhitaji sana mwanao…’
Unajua kulia, nililia, hadi machozi yakamlowesha mama, na kama
miujiza mama alifumbua macho nakuniangalia sana,na baadaye naye akaanza kulia,
nilimkumbatia kichwa chake kama mtu amkumbatia mtoto kifuani.
Mama baadaye aliinuka kwa shida huku akishika kichwa kuonyesha
kuwa kina maumivu, nilitafuta kidonge cha kutuliza maumivu nikampa akanywa.
Halafu nikachukua maji ya bairidi na kuanza kumkanda..baadaye akatulia .
Nilikaa kwenye sofa, nikaweka kichwa cha mama mapajani, mama
akatulia na nilihiai akiwa kapitiwa na usingizi, na mimi nikashikwa na
kauzingizi.
Nilipofumbua macho, mama alikuwa keshaamuka, kaka kwenye sofa
pembeni yangu, na aliponiona nimefumbua macho, akasema;
‘Mwanangu nitafutie nauli niondoke…sitaki niwakosanishe wewe na
mke wako, lakni kabla sijaondoka, nataka nikuhadithia maisha yangu yaliyopita,
ambayo hujawahi kuyasikia,….
‘Mama nilishakuambia huwezi kuondoka hapa nyumbani, ..huwezi
kuniacha..’nikasema
‘Hapa ilivyo mke wako keshatoa tamko, ama mimi ama yeye…je unahisi
hapo utafanya nini, …huwezi kumuacha mke kwasababu yangu mimi, hilo silikubali,
mke wako ni muhimu sana,….’akasema mama.
‘Mama, haya nitayamaliza kwa amani, wewe utaona tu, ninachoomba ni
wewe moyo wako utulia, utusamehe…najua haya yoye ni kwa ajili mama una kinyongo
na sisi….’nikamwambia mama.
‘Ningekuwa na kinyongo na nyie nisingalikubali kuja kuishi na nyie
hapa ….moyo wangu ulishasamehe kila kitu, na nilishawasahemeeh hata hao
walionifanyia niwe hivi…’akasema
‘Mama, mimi ni mwanao, na ukitaka kuondoka utaenda kuishije huko
kijijini, huoni utazidi kunifanya mimi nizidi kuteseka, mama haya na mke wangu
yatakwisha tu, najua ni mitihani tu, hali aliyo nayo ndiyo inamsumbua…’nikasema
‘Mwaanngu naomba utulie usikie kisa cha maisha yangu, ujue wapi
ulipotokea, na hao wanaosema mimi ni mchawi, …wajue kuwa mimi nilikuzaa vipi na
isingelikuwa mimi kukubali niteseke ili tu wewe uje uzaliwe, wasingelikuwa nawe
hii leo,…’akasema mama
Mimi nikaona kusikia hicho kisa ni kitu kingine, lakini kuondoka
kwa mama sitakubalina nako kamwe….
WAZO LA LEO . Ibilisi wa mtu ni mtu…watu wanaweza kuwa
chanzo cha mfarakano katika jamii, wakajenga fitina, wakitumia njia mbali mbali
ikiwemo ua ushirikina, Shiriki ni mbaya na adui mkubwa wa binadamu. Tujiepushe
kabisa na ushirikina, kwani tukifanya hivyo tutakuwa tunashindana na mungu, na
kuwa wakala wa shetani na shetani ni aadu wa mwenyezimungu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment