Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, December 3, 2014

DUNIA YANGU-70 MWISHOMtoto akajua kuwa mama yake kumbukumbu zake zimeshaanza kuleta shida, na kweli kipindi hicho mama huyu alikuwa ameshaanza kujiwa na hali kama ya kuchanganyikiwa akawa anaanza kuropoka ovyo, kusahau, na kuna muda anamkana mtoto wake huyo, anamwambia yeye sio mtoto wake, mtoto wake hana sura kama hiyo….

‘Kwa hali ile ikaonekana kuwa mama huyu anaweza kufichua siri, ukatoboa siri, …lakini hana la kumfanya, kwani huyo ni mama yake bila yeye, hayo yote aliyo nayo mali, cheo,…..asingelikuwa navyo…

‘Hali hiyo kwa ujumla sasa ikawa nayo inampa shida, ikabidi mama huyo awe na ulinzi wa ziada, hakutakiwa kutoka nje kuonana na watu japokuwa mama huyo alikuwa mkaidi hakubali, ....

‘Unajua kiukweli binadamu hachungiki, hasa mtu mzima kama huyo, ikawa ni taabu, mama analalamika,…na akawa anaahidi kuwa ataenda polisi na kusema kila kitu…kwanini mnanitesa, kwanini mnanifunga ndani kama mfungwa, kama mtoto wangu angelikuwepo mngelifanyia hivi….hamji mali hii imetoka wapi…. mama akawa analalamika sana…ikawa ni ugomvi…

Je mtoto atafanya nini….

Tuendelee na kumalizia kisa chetu.....

***************

Mtoto akajaribu kila njia kuona mama yake anatulia, na pia kutaka kujua wapi alipoweka hicho kifaa chenye kumbukumbu, lakini mama akawa hakumbuki, na majibu yake kwa huyo mtoto yalikuwa yale yale kuwa yeye sio mtoto wake…

‘Wewe sio mtoto wangu siwezi kukuambia hata kama ningelikuwa nakumbuka,…’akasema wazi wazi.

Ukumbuke kwa muda huo Moto alishatakiwa kuuwawa, akaponea chupuchupu kwa kupitia kwa yule mtaalamu wa tiba mbadala, nilipewa sumu mbaya nife, lakini nikawahiwa na mganga wa kienyejei akanitibu….’akaendelea kuongea.

‘Waliposikia kuwa nimepona hawakuamini, haijatokea, sumu hiyo ukipewa huponi, iweje mimi nipone..jamani kuna wataalamu,…msiwadharau hawa wataalamuw a tiba mabadala, huyo jamaa alinitibia katoa smu yote mwilini.

‘Hawa jamaa wakasikia nimepona, na mkuu huyu haraka akajifanya ananijali, akatoa amri niwe nafanya kazi makao makuu, nia ili niwe karibu naye, …na wajue imekuwaje,…muda huo sikuwa nafahamu lolote, sikuwa nafahamu kuwa huyu mtu ni nyoka, najua tu, yeye ni bosi wangu, na kweli ananijali.

‘Kuna muda nilikuwa napata mashaka, maana nikiwa karibu naye, alikuwa akinituma kazi maalumu, na nikifika kwenye kazi nakutana na mitihani mikubwa, taarifa zimeshafika kwa hao watu, na mara nyingi nikawa naponea chupuchupu kuuwawa, nikawa  najiuliza, ni nani anatoa siri za kazi zangu na ni nani ametoa taarifa zangu, wakati ilitakiwa nisifahamika kuwa bado nipo hai…..

‘Kipindi hicho baada ya kulipuka hilo bomu, tukawa tumewachukua wale wataalamu wote, tukawaweka chumba cha siri, chumba hicho alikifahamu mimi na muendesha mashitaka tu, hatukutaka mtu mwingine afahamu,…tulishahisi kuna mdudu mtu, tukaona tubahatishe, ikawa siri yangu mimi na muendesha mashitaka na vijana waaminifu wachache,

‘Mkuu alishapata taarifa kuwa wataalamu hao hawajafa, na wapo mahali, lakini akawa hawajui ni wapi, mitandao yake tulishainasa, na mtendaji wake wa mitandao tunaye, japokuwa alikuwa hajiwezi lakini akawa anatuelekeza kwa shida, na uliweza kudhibiti sehemu kubwa ya mtandao wake, lakini hatukuwa tunaelewa ni nani kiongozi… hapo tukaanza kutokuelewana na mkuu wangu, akawa analalamika kuwa nafanya kazi bila kumuarifu yeye, na muda huo yupo anatibiwa, tunawasiliana kwa ujumbe wa simu

‘Nimesikia wale wataalamu wapo hai, …wapo wapi?’ akaniuliza

‘Kuna sehemu wapo mkuu, usijali…’nikasema

‘Nauliza wapo wapi?’ akaniuliza kwa ukali na mimi sikumjibu ujumbe wake huo, kitendo hiki kilimkwaza sana, hata akatoa taarifa makao makuu kuwa mimi nakiuka utendaji wa kazi, siwajibi kwake, kwahiyo anapendekeza mimi nisifanye kazi hiyo maalumu, apewe mtu mwingine. Maneno agalikuwepo angalipewa yeye, lakini kwa mud huo alikuwa hajitambui kwani nay eye alikuwa miongoni mwa wale waathirika wa kutaka kuuwawa na wale wataalamu.

‘Kwa muda huo mimi na muendesha mashitaka tulishaongea na makao makuu, kuwa kazi hiyo ifanikiwe, ili tuweze kulinasa hilo kundi na kiongozi wake basi watuachie hiyo kazi, na viongozi wote wa kiengo wasihusishwe, makao makuu wakanielewa.

Siku moja tukamtembelea huyo kwa mama kwa kushitukizia, na siku hiyo, akawa yupo vyema, kiasi, ila waliyoyaongea, yakatupa mashaka, kwanza analalamika kuwa amefungwa, hana kosa, pili, anadai mtoto wake yupo hajafa,….

‘Huyu mama anaweza kutusaidia,…’nikasema

‘Lakini kachanganyikiwa…’akasema mwenzangu

‘Tumchukue, atatusaidia mengi, …’

Mimi na muendesha mashitaka tukakubaliana kuwa tumchukue huyo mama, tuwe naye karibu, huenda tukapata mengi. Kazi hii ilifanyika kwa siri, na mama akijua tunamtoa kwa kile alichokiita kifungo, akakubali, tukampeleka sehemu nyingine, lakini chini ya ulinzi wa kuhakikisha hatoroki.

Mkuu aliposikia kuwa mama huyo kachukuliwa, alikuja juu, kwanza alidai tunakiuka sheria, za kumshika mtu asiyeruhusiwa kisheri, mama huyo kachanganyikiwa,sisi tunamkamata , tunakiuka sheria na haki za binadamu, lakini hatukujali hayo sisi kimiya.

‘Kiukweli tulijua hilo ni kosa kisheria, sasa tufanyeje, hapo tukaona tuendelee kufanya kosa jingine dogo ili tuweze kufanikiwa, tukatafuta mbinu za kidakitari ili huyu mama aonekane hajachanganyikiwa, …kuna muda mama huyu yupo safi kabisa, mnaongea kama kawaida, lakini kuna muda anakuwa kama sio yeye, unaweza ukahisi akajisingizia …

Kitendo cha mama huyo kuchukuliwa, kilimuathiri sana mkuu, akawa anatuma ujumbe wa kauli kali, japokuwa haonyeshi kuwa ana uhusiano gani na huyo mama, lakini ilionyesha wazi kuwa hakufurahishwa na hicho kitendo, akatuma barua kwa wakuu akiwa huko huko hospitalini kuwaambia kuwa kama hawamuamini basi wamuambie ….wakuu wakamwambia hilo litafanyiwa kazi , nia ya wakuu hao ni kupoteza muda, ili sisi tuweze kufanikiwa na wao walishahisi kuna jambo, na kikulacho kipo nguoni mwako, ila nani ni nani ilikuwa bado kitendawili.

Siku ile tukamfikisha mama mahakamani tukijua kuwa hapo ataongea kila kitu na mahakama itachukua kauli yake kama ushahidi..na kweli siku ile mahakamani akaongea mambo ambayo kidogo, yaliwafungua watu masikio hasa hakimu na jpo lake, ndio maana hata tulipotaka kufanya mambo mengi, tukawa tunapata ushirikiano wa kimahakama.

‘Siku ile huyo mama alipouwawa na bomu, niliumia sana maana sisi ndio tuliomtoa huko alipokuwa na tukamfikisha hapo mahakamani tukihakikishia usalama wake, bomu lile lilinivunja nguvu, nikajua kuwa sasa tunapambana na jitu lisilojali, lipo tayari hata kuwaua wazee kama huyo…

Kutokana na ushahidi uliopatikana baadaye nia ya bomu hilo ilikuwa sio kumuua huyo mama, halikukusudiwa kwake kabisa, ilikusudiwa kuwa liniue mimi, maana mimi ndiye  nilitakiwa niwe kwenye hilo gari la huyo mama yeye ana gari lake hataki liguswe na mtu mwingine…kiusalama, tukapanga kuwa baada ya kesi, mama huyo atachukuliwa na gari jingine,mimi nitatumia gari la huyo mama, na pia tukitoka hapo mama huyo anapelekwa sehemu nyingine kiusalama.

Hawa watu wakitafuta njia za kunimaliza, wakaliweka hilo bomu kwenye gari la mama, wakijua mimi ndiye nitalitumia, waliweka tukiwa mahakamani, ujue kundi hilo kuna watu wao ndani ya watu wa usalama, kwahiyo hata walipoingia ndani ya hilo gari, hakuna mtu aliyewashuku.

Bomu likawekwa kwenye hilo gari,..na ukumbuke kipindi hicho mkuu wao wa mitandao alikuwa mikononi mwetu kwahiyo ule mtandao wao wa mawasiliano kujua huyu yupo wapi, haukuwa unafanya kazi tena….

Mungu kama hakupanga kifo kitokee, hakitokei, na mama kwa ubishi wake akasema hataki kuingia gari lolote zaidi ya gari lake..tukaona haina haja kubishana naye, basi yeye na  walinzi wake anaowaamini wakaingia kwenye hilo gari, na bomu likawaua wote,..kifo hiki kilimuumiza sana.

Kwa namna fulani, huyu jamaa japokuwa kwa namna fulani, kingemsaidia kuondoa watu wote wanafahamu usiri wake, kwani mama alishaanza kuvujisha siri.

Mkuu akawa magonjwa kabisa siku ilipofikishiwa taarifa hiyo, wanasema jamaa alizidiwa sana siku hiyo, japokuwa alikuwa jasiri. Lakini hali ilibadilika ghafla, akapoteza fahamu. 
Alipotulia na kuwa vyema, akaanza kutulaumu sisi kuwa ndio tumechangia kifo cha huyo mama, na tunahitajika kuwajibika kwa hilo…wakuu wakapelekewa taarifa, lakini wakuu walijua ni kitu tunakifanya kauli ao ikawa ile ile kuwa wanalifanyia kazi.

Kwa ujumla makao makuu walishakosa imani na huyo mtu , lakini walikuwa hawana ushahidi na hawawezi kumuingilia kwani ni mtendaji wao mkuu, anafahamika, ana sifa zote…., wakawa wanatuachia sisi tufanye kazi ili tuweze kuonyesha kuwa jamaa huyo hafai au unahusika kwa namna moja au nyingine na hilo kundi haramu, walihitaji ushahidi wenye nguvu…

Kama ilivyokuwa kwa wakosaji wote, kuwa za mwizi ni arubaini, na kama ilivyosema kuhusu dhuluma, dhuluma haidumu…ikidumu inaangamiza…, mwisho wa kundi hili ukafikia tamati,….mimi ndio nikakipata hicho kifaa, chenye siri, niliamini kuwa kina siri kubwa sana, kwani huyo mama marehemu kuna muda alitamka kitu kama hicho, kuna siku alisema ;

‘Mkitaka kujua siri ya mtoto wangu kuna kifaaa cha komputa mkikipata mtajua kuwa mtoto wangu hajafa …’akasema

‘Hicho kifaa kipo wapi?’ nikamuuliza

‘Sijui, kama ningelijua,….ningelifurahi,…..’akasema na ilitokea siku hiyo moja akaongea hivyo, ha hakuweza kuongea kauli hiyo tena, hata tulipojaribu kumuhoji hadi anauwawa na hilo bomu.

‘Na niliposikia mkuu huyu akimuagiza nesi kuwa kuna kifaa ninacho, nimekipeleka kwa fundi kifaa hicho ni muhimu sana kwake , nikajua kweli sasa tutagundua siri ambayo imejificha, …mara nesi akakiiba hicho kifaa, akitaka kupata utajiri kwa huyu jamaaa.
Kipindi hicho mkuu alishatoroka hospitalini, akijihami,..akikitafuta hicho  kifaa, akijua mwisho wake unakaribia,…nesi akaingia mkataba na huyo jamaa kuwa atakitoa hicho kifaa kwa kupewa hisa na baadhi ya miradi ya huyo jamaa, nesi akaona hilo ni kazi rahisi kwake, akaona hiyo ndio nafasi yake ya mwisho kutajirika,.

Na kweli nesi akakipata hicho kifaa, na hakutaka kuwapa polisi, kwani polisi hawana pesa, ndio akapanga mpango wa kukikabidhi hicho kifaa kwa mtu mmoja ambaye alikuwa akitumika sana na hili kundi, kupelekea na kutoa taarifa za mahabusu…

Mimi kwa Bahati nzuri nikawanasa wakati wanakabidhiana, chombo kikapatikana na siri ikawa imefichuliwa , kwahiyo dunia yangu, ikafikia tamati. Mashahidi waliotakiwa kuuwawa, yaani wataalamu baada ya tiba ya mganga wa tiba mbadala, wakawa na uwezo wa kuelezea kila kitu kuthibitisha hayo mbele ya hakimu, mzee mzima akazidi kuchanganyikiwa.

Kiukweli kama angelifanikiwa kukipata hicho kifaa akakiharibu siri  kubwa ya yeye ni nani ingelibakia kichwani mwake tu...lakini ya mungu mengi dhuluma haidumu, siri ikajulikana mbele ya mahakamani, na hapo ikawa mwisho wa dunia yangu

'Ama kuhusu hali ya mtuhumiwa huyo, alipoona kila kitu kipo wazi, alishindwa kuvumilia, akadondoka na kupoteza fahamu, na ana tatizo, kutokana na kuungua na moto wa lile bomu, uso wake umeharibika sana, ukimwangalia kwa sasa hayupo vizuri, kuna hali kama ya kuoza,  docta aliyekuwa akimtibia anasema kuna dalili ya kansa, hebu fikiria kansa imejitokeza kwa muda mfupi tu...kwahiyo hatumuombei baya, ila adhabu mara nyingi zinaanzia humu humu duniani, ogopeni sana dhuluma

'Ni hayo niliyotakiwa kuwaambia….ahsanteni sana.’

Moto akasema na kuanza kuondoka kuelekea kwenye gari lake, lakini waandishi wakwa wanamzonga kwa maswali mengi hadi askari waipoingilia kati.

‘Ni hayo ndiyo niliyotakiwa kuwaambia…..’ Moto akasema na kuanza kuondoka kuelekea kwenye gari lake, lakini waandishi wakawa bado wanamzonga kwa maswali mengi hadi askari walipoingilia kati.

‘Mengine suburini , mtayajua zaidi baada ya hukumu, cha msingi ni kuwa dunia yangu imesambaratika, na muhusika mkuu keshapatikana….’akasema Moto sasa akitembea kuondoka eneo lile akiwa anasindikizwa na askari kuhakikisha hakuna mtu anayemsumbua tena, akaelekea kwenye gari lake kuondoka.

                                                     ********
Tamati
 Baada ya  kumaliza kuongea na waandishi wahabari,  Inspecta Moto, akatoka  eneo hilo na kuelekea pale lilipokuwepo gari lake, kila mmoja akimuangalia kama shujaa, yeye hakugeuka nyuma kuwaangalia watu.

Akafungua mlango wa gari lake na kuingia ndani, lakini kabla hajaondoa gari, akaona mdada akija kwa kasi, akiwapita askari kwa kuwakwepa,  huku akipunga mkono wake kama kunisimamisha nisiondoke…askari wakamfuata kumzuia, Inspecta akafungua dirisha la gari lake, kujua huyo mdada ni nani, mbona kama anamfahamu.

‘Hebu muachieni huyo mdada aje…’inspecta akawaambia askari kwa sauti, na yule binti akasogea hadi pale kwenye gari na macho ya Inspecta yakakutana na  yule mdada, akamkumbuka, akatabasamu, alikuwa yule binti wa mtaalamu wa tiba mbadala, akakumbuka fadhila zao, akayakumbuka mawazo yake… akasema;

‘Vipi unahitaji lifti.....?’ akauliza akitamani huyo binti asema ndio

‘Mhh,… lifti hapana,…sikuwa na nia ya kuomba lifti, ila hawa askari wenu wamenikwaza unajua kukwazwa, ….basi ndio hivyo, siwapendi,….mbona wana roho mbaya, hata kuingia ndani kusikiliza kesi walinizuia, kwanini lakini….’akawa analalamika

‘Inabidi wafanye hivyo, maana watu ni wengi, na wengine sio wastaarabu, wanaweza kuanzisha vurugu, …’akasema Moto

‘Sawa kama hata mimi sio mstaarabu, ….’akasema akionyesha kuhuzunika

‘Sio kwamba na wewe upo hivyo, ningelijua ningewaambia wakuruhusu , lakini wao watajuaje nani ni nani….usiwalaumu sana, hata wewe ungekuwa kwenye kazi yao ungelifanya hivyo…’akasema Moto.

‘Najua kesi ya ngedere nimempelekea tumbili, tuyaache hayo, …baba kanipigia simu kuwa anakuja kwako, nimemwambia upo kwenye kesi, akasema ukitoka tu ni mwambie, maana anajiandaa kurudi kijijini, lakini hao askari hawakutaka kunipa nafasi ya kukuona, na simu yako sijui imekuwaje, sijui nilikosea namba, nikipiga inasema nimekosea...’akasema

‘Unasema baba yako eeh, anataka kuonana na mimi, kwa kusalimia au kuna jambo jingine…..?’ akauliza Inspecta akiwa na wasiwasi.

‘Anasema ile sumu uliyowekewa mwilini inahitaji kusafishwa kabisa, isije kukuletea madhara baadaye, kuna dawa kaja nazo, hataki kurudi kijijini bila kuhakikisha kuwa wewe umezitumia, na awe na uhakika kuwa upo salama...’akasema huyo binti.

‘Mhhh, ama kweli nyie ni watu wema sana, sijui kama nitaweza kuwalipa wema wenu huo,, na hajaniambia gharama yake mpaka sasa,sijui atanielewaje, lakini kwa vile mambo yamekwisha, nilizima nimlipe…’akasema Moto

‘Hahitaji umlipe chochote, sio kusudio lake,…yeye anachotaka ni kukamilisha tiba yake tu…’akasema mdada.

‘Yah, hilo sio lazima aniambie mimi mwenyewe nafahamu nifanye nini,….’akasema na kumuangalia yule binti kwa makini, akaona jinsi gani anavyozidi kupendeza, kwa kipindi kifupi keshanawiri, akajikuta akitabasamu, akasema;

‘Kuna kitu,nataka kwanza niongee na wewe , halafu baadaye nitaongea na baba yako, ni muhimu sana, kwa vile nimekuona hapa, naona nisipoteze muda huo, ....ingia ndani ya gari twende…’akasema

‘Hapana….’akasema Binti

‘Tafadhali, kuna kitu nataka kuongea na wewe kama hutojali...’akasema na yule binti kwanza akasita kuingia akainua uso kuwaangalia watu, sijui alikuwa akiwaza nini, na Inspecta akasema;

‘Vipi tena, mbona unasita kuingia kuna sehemu unakwenda au kuna mtu anakusubiria, ingia tu usiwe na wasiwasi, na kwa vile baba yako yupo kwangu, itakuwa vyema, nikaongea na yeye pia, au…?’akasema Moto akiangalia watu kama kuna mtu anayemsubiria huyo binti.

Yule binti akafungua mlango wa gari na kuingia ndani ya hilo gari, akiwa na aibu nyingi usoni..

‘Kitu gani unataka kuongea na mimi…unajua baba yeye anasema anahitaji kukuonyesha kuwa yeye hafanyi kazi yake kwa pesa, kwani watu walivumisha kuwa alirubuniwa na hao watu wabaya kwa kuthamini pesa kumbe sio kweli….’akasema

‘Najua ….mimi nafahamu fika kuwa baba yako ni mtu mwema tu, hilo wala lisikusumbue kichwa na hata baba yako nitaongea naye wala asiwe na wasiwasi, yeye ni mtu mwema sana…’akasema Moto.

‘Ndio hivyo, ila kiukweli kuna muda anakwama, kuna muda baba anakuwa hana pesa kabisa hata hivyo haachi kuwasaidia watu…watu bado wanahitaji huduma zake, anajitolea bure, na wengine wana uwezo, lakini ile hali ya kufikiria kuwa mzee huyu kawaisaidia na wao wamsaidia chochote, hawafikirii hivyo, kazi ni kumsfia tu…’akasema

‘Kwanini asifungue kitu kama kliniki akajisajili, akawa analipwa tu…unajua watu wengine hawawezi kujituma, wanapenda bure tu, na hawajali wewe mtoaji unaumia vipi, umetumia gharama kiasi gani hilo hawalijui, na ni wepesi kusfikia, na hata kukashifu pia….’akasema Moto.

‘Hilo la kufungua kilikini na kujisajili, ….mmh baba hataki,…anasema hataki usumbufu kwani nia yake ni kusaidia, sio kujitangaza..hataki hata kusikia mambo hayo, yeye anasema kapewa kipaji na mungu, cha kusaidia watu hilo kwake linatosha…ni kama wewe unavojituma kwenye kazi yako…’akatulia

‘Kwenye kazi yako, hufanyi tu kwa vile unalipwa mashahara, sizani kama mshahara unaopata unalingana na kazi unayofanya, wenyewe wataishia kukusifia tu, ukirudi nyumbani kama una watoto, hawawezi kushiba hizo sifa….angalia kazi uliyofanya, ulijiweka hatarini,  mpaka mke wako kauwawa…ni wito tu, kuna nini utapata hapo, sifa…hahaha, sifa zinashibisha, sifa zitakuondolea machungu, nikujitolewa tu, tenda wema uende zako…’akasema binti, na Inspecta akawa anawaza jinsi gani bintu huyu alivyo na hekima.

 ‘Kweli …hilo ni jukumu la kila mmoja wetu kwa nafasi yake…unajua baada ya kufa mke wangu, sikutaka kabisa kuoa,..lakini kila mara nawaza, je ni sahihi kufanya hivyo, nahitaji familia, nahitaji watoto…ili waje kuendeleza kizazi chetu, japokuwa nilimpenda sana mke wangu, lakini keshaondoka, keshatangulia mbele ya haki, na sote ndio njia yetu, sasa niombeleze mpaka lini,…nahisi nitakuwa nakufuru, sina jinsi..’akasema Moto akionyesha kusononeka.

‘Pole sana, …wewe ni mume bora, na mke wako alipata Bahati sana kuwa na wewe, japokuwa mitihani ilimpitia,lakini yote ndiyo kidunia, yote yameumbiwa sisi wanadamu, najua huko alipo keshaingia peponi, kwani alishindw kuvumilia, aliona akizidi kuwepo atazidi kuingia kwenye madhambi, mungu amsamehe makosa yake…ila sasa wewe ni muhimu utafute mwenzako …’akasema huyo bonti akimtupia jicho la aibu

‘Ni kweli kwa hali hii, nilizoea nikirudi nyumbani kuna mtu wa kunipokea, tunasaidiana kazi,…yani wakati mwingine naogopa hata kuingia chumbani, …kwakweli sijui, nimemkosa mtu niliyempenda sana…mmh….’akatulia kidogo halafu akasema

‘Unajua mke na mume kuna siri kubwa sana, mnahangaika, lakini mwishowe mnatakiwa kupumzika, mkiwa wawili mnakuwa kwenye dunia nyingine, mambo ya kazi, mataizo mauzi ya dunia yote mnayasahau,mmmh, sasa leo mwenzangu hayupo, inanipa shida sana, najihisi mpweke , na kuna muda namuota mke wangu akiniambia nitafute mke ili roho yake iwe na amani..hebu fikiria anafikia hata kunipigia magoti kuwa nitafute mke…..’akasema

‘Anakuambia hivyo kwenye ndoto, sasa kwanini huoi, hujui unamtesa mwenzako….?’ akauliza binti akionyesha kama hamasa fulani.

‘Tatizo sio kuoa, tatio ni nani wa kuoa, mtu ambaye kweli ataweza kuziba pengo la mke wangu, naogopa kuja kuumia, naogopa mitihani hii ya maisha, nimeshaumwa na nyoka, naogopa hata unyasi, lakini……’akasema  Moto na kugeuka kumuangalia huyo binti.

‘Mhh, ni uamuzi wako lakini,… ila kama umemuota mke wako anakushauri hivyo, na anasema roho yake inataabika kwa vile hujaoa, ni vyema uoe, ndoto nyingine ni ishara anakupa ujumbe na ukiutimiza, atakujia akiwa amefrahia, na huenda hilo linampa adhabu, na kuoa kwako kutafanya awe kwenye heri, nakushauri kama kaka yangu tafuta mke uoe……’akasema huyo binti na kutulia.

‘Unajua kila nikikuangalia namuona mke wangu, ni kama vile nyie ni ndugu, umefanana sana na mke wangu…isingelikuwa mnatoka mikoa tofauti ningelisema nyie ni ndugu….’akasema Moto na huyo binti akamuangalia Moto, na macho yao yakakutana, kuna hali iliwatokea wote, na binti akakwepesha macho yake na kuangalia nje kwa kupitia dirishani akasema;

‘Binadamu hufanana…imetokea tu, mimi na yeye tukafanana, kama unavyodai wewe, japokuwa mimi sioni kama tumefanana naye…na hata nikimuangalia yeye ni mzuri sana, sizani kama mimi ni mnzuri kama alivyokuwa mke wako, ile picha yake niliyoiona, nimemuona alivyokuwa mrembo,…’akasema huyo binti akishusha sauti kama vile aliongea kitu kisichostahili.

‘Kiukweli mnafana kila kitu uzuri, tabia, unavyoongea, na hata kila nikimuota mke wangu mwishoni nakuona wewe, mpaka najiuliza kuna nini hapa…..’akasema

‘Hiyo ni kwamba, unahitajika upate mwenzako, tafuta mke mimi nitafurahia kama ukiwa na wifi, nafika nyumbani siogopi, najua nitamkuta wifi, lakini ukiwa hivyo peke yako naogopa kuja, midomo ya watu itabwabwaja ovyo,…’akasema Binti.

‘Hahaha, wewe unahitajia wifi, kwanini wifi, kwanini usiseme dada, au …..kiujumla ni kweli kwa hali ilivyo na mimi sasa naona …ooh, ni kweli nahitaji mtu…wa kunisaidia majukumu,….’akasema Moto

‘Majukumu!?, ina maana unahitaji mfanyakazi wa ndani, mimi nilijua unahitajia mke..?’ akauliza huyo binti

‘Hapana, sihitaji mfanyakazi wa ndani, nahitaji mwenzangu,akiwepo majukumu tunasaidiana, au sio ...na mtu ambaye naona anaweza kuziba pengo  la mke wangu, mmh, hayupo mbali, ….’akatulia na muda huo alikuwa kaangalia mbele, hakuwa amemuangalia huyo binti, ila binti alikuwa akimuangalia yeye.

‘Kumbe umeshampata mtu mwenyewe tayari, kwanini sasa unazunguka, sema harusi ni lini , mimi nitafurahia kweli nikimpata wifi yangu niwe nafika kumtembelea…’akasema Binti kwa sauti ya kinyonge.

‘Mhh, kiukweli sijawahi kumwambia, ila amekuwa akilini mwangu….’akasema

‘Na wewe bwana, mimi nijuavyo askari ni watu majasiri sana, hawaogopi kufanya jambo, sasa kwanini hujamwambia, unaogopa nini,….?’ Akauliza binti, kwa sauti ile ile a kingonge, na akaongezea kwa kusema;

‘Au huna uhakika, humpendi….?’ Akauliza binti sasa akimtupia jicho la siri Inspecta.

‘Inafikia maswala kama haya, hakuna cha uaskari, au nani, …ni hulka ya kibinadamu, kwani hujui mwenzako anawaza nini….na kila jambp lina muda wake, na ndio maana nikataka tuongee mimi na wewe kwanza..’akasema

‘Hahaha, usinichekeshe, mimi bado mdogo, siwezi kwenda kukuelezea kwa huyo mtu, nitaanzaje, hapana, mimi iswezi, labda ingeikuwa shangazi yangu, au…’akatulia

‘Binti naomba unielewe,….kama nilivyokuambia wewe unafanana sana na mke wangu, kwahiyo nimeona ...lakini kama upo radhi, nakuomba wewe ukubali uwe mke wangu....’akasema Moto na kugeuka kumuangalia yule binti, na macho yao sasa yakawa yamekutana, binti akapandisha mkono na kushika mdomoni, mdomo ukafunguka kwa mshangao, na kusema;

‘Khaaah, eti nini....mmh, mimi niwe mke wako, mmmh, najua unanitania…najua utampata mwenzako tu anayekufaa…sizani mimi nastahili kuwa mke wako…’akasema yule binti kwa mshangao, huku sasa akiianama chini kwa aibu.

‘Sikutanii Binti,…..nataka wewe uwe mke wangu, kama upo tayari, na kama kweli unanipenda, maana maswala ya kuoana kitu kikubwa ni upendo na upendo uwe wa dhati, kutoka moyoni,…sio tu kwasababu unataka au ninataka kukuoa, niambie ukweli kama upo tayari, mimi sitaki kuchelewesha, nitaongea na baba yako…’akasema Moto

 ‘Kama nilivyokuambia wewe unafanana sana na mke wangu, nikimuota mke wangu, nakuona wewe, … kwahiyo nimeona kuwa wewe unafaa kuziba pengp la mke wangu,..’akasema Moto sasa akiwa kasimamisha gari.

‘Mhh, mbona unahitaji jibwa kwa haraka hivyo, unajua umeni…mmh, hata siwezi kusema..’akasema Binti.

‘Nikuulize swali wewe unanipenda, upo radhi kuwa na mimi..sitaki kukulazimisha, kama una mtu wako mwingine, niambie ukweli, kama unaona sikufai, uniambie ukweli…sitaki kuja uje ujute au nije kupata matatizo mbeleni, yaliyopita kwangu na makubwa, sasa hivi nahitaji faraja, …’akasema moto na yule binti alikwa kama kapigwa na shoti ya umeme, alikuwa katulia kimiya, huku akainama.

‘Nahisi unanitania..siamini….’akasema

‘Sikutanii…..nakuomba unikubalie uwe mke wangu, kama upo tayari, na unanipenda, maana maswala ya kuoana kitu kikubwa ni upendo na upendo uwe wa dhati, na sihitaji maswala ya mlolongo, sijui uchumba….hapana, kama upo tayari, mimi sitaki kuchelewesha, nitaongea na baba yako, tufunge ndoa haraka iwezekanavyo…’akasema Moto

‘Mhhh, …ni kama ndoto, siamini. Ahsante mungu, mmmh, sina hata la kusema, zaidi ya kukuambia nakupenda, nilikupenda toka siku ile ukiwa mgonjwa,  nipo tayari niwe mke wako, uwe mume wangu…..’akasema binti.

                                            MWISHO.

********************************************************************
Nawashukuruni nyote mliokuwa nami kwenye kisa hiki, na kama kuna lolote, maoni, tumeni kwa email address ya mtandao:  mira.com@gmail.com.
Kumbekeni mwisho wa kisa hiki ndio mwanzo wa kisa kingine,
Na kama nimewachosha kusubiria hitimisho, samahanini sana…kuna mambo yalikuw juu ya uwezo wangu, na kama ni kisa kizuri umekifurahia, basi nashukuru, `like ‘ sana kwenye facebook, au ingia ndani ya diary yangu, toa neno la shukurani. Zaidi sina, tupo pamoja, tumuombe mungu atupe wasaa, afya tuweze kuanza kisa kingine.
TUPO PAMOJA

                                       **************************


WAZO LA LEO: Unapodhuluma, mali ya umma, mali ya watu, jasho la watu, ujue umedhulumu vizazi na vizazi vya jamii, na kwa kudhulumu huko , ujue pia wewe umsababisha hata vifo vya jamii hiyo,….angalia watu wanavyoteseka, masikini wasiojiweza, wagonjwa wanakosa dawa, yote ni kutokana na dhuluma zako.

Ukumbuke pesa na mali hiyo ya umma uliyodhulumu,  ingelisaidia kununua madawa, kutoa huduma mbali mbali za kijamii,  lakini wewe ukaamua kujali tumbo lako. ukajitajirisha....ni kweli, utashiba utatajirika, lakini ukumbuke, mwili wako utakuwa  unanuka dhambi. 

Kama una moyo wa imani unamjua mungu kuwa yupo, basi kumbuka kuwa yote ni mapito, yalikwepo na yatakuwepo, umeyakuta na utayaacha, wangapi wangapi walidhulumu, sasa wapo wapi, siku itafika na wewe utarejea kwa mola wako mjuzi mwenye hekima, anayefahamu kila kitu, atakuhukumu kwa dhuluma zako hizo, hakuna pa kujificha…kumbuka, kila mtu ataubeba mzigo wake mwenyewe, muhimu, tubia, acha kula mali ya dhuluma, kama umedhulumu, umechukua mali ya umma, rejesha mali hiyo kwa wenyewe.

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Keep it up, y'a number one