Kisa kilivyoanzia:
Siku hiyo nilikuwa kituo cha basi nikisubiria usafiri, mara
kukatokea tukio la aina yake, pikipiki, ilikuwa inakatisha barakabara kwa kasi,
ikakoswakoswa kugongwa na daladala zilizokuwa zikifukuzana, watu wakabakia
mdomo wazi , na kila mmoja akawa anaongea lake.
Wakati hayo yakiendelea mimi nikasogea pembeni, nichelea ajali
maana madereva wa madala dala walikuwa wanasogeza magari hadi sehemu
wanaposimama abiria, mimi nikawa naingia
kwenye dunia ningine ya mawazo, nikiwazia jinsi ya kupata usafiri mara gari la kifahari likasimama hatua kidogo mbele
na pale niliposimama, na jamaa
akiendeshwa alikuwa akitabasamu na simu yake mkononi, mimi nikaliangalia kwa
macho ya hamasa, moyoni nikasema wenye nacho wana raha zao.
Wakati naendelea kuwaza, mlango wa lile gari ukafunguliwa, na
jamaa mmoja akatoka nje ya hilo gari, nahisi
kwa muonekano wake atakuwa muheshimiwa, au mkurugenzi fulani, kwani
alikuwa, pande la mtu, kitambi, suti ya maana, eeh, mungu kamjalia kama kipato
anachopata ni cha halali akafunga gari lake na ugeuka kutuangalia.
Nikawa nataka kuondoka ile sehemu maana watu walikuwa
wanasukumana, na kwa muda huo nikamun yule jamaa akiwa anakuja upande ule
niliosimama, mimi nikajua kuna mtu anamfuata kumsalimia…nikawa sina habari naye,
lakini machoyangu yalikuwa yanamtizama anavokuja pale tuliposimama.
Cha ajabu nikamuona huyu jamaa akinijia mimi, akanisogelea pale
niliposimama, na kwa muda ule sikujua ni nani, mpaka aliponikaribia akawa
anatabasamu na kuniangalia usoni, hakunysha mkono hapo hapo wa kunisalimia, na
mimi sikutaka kujibaragua, eti kwa vile ni tajiri, basi nianze kumsalimia, nikatulia
nikiwaza huyu mtu ni nani, mbona sura inakuja na kutoka.
Wakati huo alikuwa kasimama mkabala na mimi, ananikagua usoni,
kama nay eye anajiuliza, au kunisanifu,…sikupenda hiyo hali, nikataka nisogee
pembeni, lakini nikahis kama hiyo sura naifahamu, hata hivyo sikupenda kuwazia
huo, maana nikiwazia huko nahisi moyo ukinienda mbio …nikapepesa macho kama
siamini, bado akili haikubali kuwa huyo ndiye huyo huyo ninayemfikiria mimi au
ni mtu mwingine.,
‘Mjumbe habari yako….’akasema
Mjumbe ni neno tulilokuwa
tukilitumia tukiwa shuleni, tukimaanisha
mwenza katika msafara, maana kipindi cha likizo tulikuwa tunapangwa
mafungu mafungu kwa ajili ya usafiri wa kurudi makwetu, enzi za neema,
wanafunzi wanalipiwa usafri na serikali, kutoka shuleni na kurudi shuleni, sasa sisi tuliokuwa tunasafiri kwenda Dar,
tulikuwa tunaitana `mjumbe’
‘Mjumbe….!’nikasema kwa mashaka na sasa nikitafuta usawa wa
kumkwepa na ikibid kukimbia, kwani niliona ni mzuka, au kibwengo, lakini kama
ni mzuka au shetani sijui, halingelikuwa na hali ile, gari zuri, hali nzuri….nikajilaumu
kwanini nimesema hilo neno ‘mjumbe’ …
‘Habari yako, za siku nyingi….’akanyosha mkono sasa kunisalimia,
nikasita kuinua mkono wangu, sasa akili haikuwa swa, moyo unanienda mbio
naogopa, natafta usawa wakukimbilia, nikaanza kujivuta kinyume nyume, na watu
wakawa wanatuangalia, wakinishangaa, maana mwenzangu kanyosha mkono kunisalimia
tena mtu wa wadhifa, lakini mimi siupokei…
Jamaa akatabasamu,
akashusha mkono wake, na kunisogelea, akasema;
‘Mhh, mjumbe, unahisi umeona mzuka, mfu kafufuka au…..’akasema
Sikuamini macho yangu vyema, nikayapepesa mara mbili na kumbukumbu
zikanijia kuwa ni yule yule jamaa ninaye mfahamu, nikajikuta natikisa kichwa na
maneneo haya yakanitoka ;
‘Aisee ndio wewe…haiwezekani, Mungu kweli mkubwa …ume-ume…imekuwaje’
nilishikwa na kigugumizi, na kushindwa kutamka hayo maneno vizuri…..
‘Hahaha, ndio hivyo..hujakosea nimefufuka, na sasa unaongea na mzuka wa yule uliyemfahamu, mjumbe….lakini
ukumbuke kuwa mungu ni mkubwa, na yeye anajua siri za waja wake wote, leo na
kesho hadi mwisho wa dunia…najua umeshangaa sana kuniona na hata sasa huwezi
kuamini kuwa ni mimi, ni mimi, na wala sio ndugu yake huyo unayehisi alikufa….ndio
mimi `mjumbe’…’akasema
‘Ni kweli ni wewe au nafananisha…hapana, lakini mbona….?’
nikamuuliza
‘Ndio mimi bwana..usiumize kichwa kuwaza sana,….’akasema, na sasa
akanyosha mkono wake tukashikana mikono na kusaliamia saa nikiwa na uhakika
kuwa ndio yeye, na ni binadamu sio mzuka, .. lakini hata hivyo kichwani nilikuwa na maswali mengi yanayohitaji
majibu ya haraka , kwani kwa mara ya mwisho nilipoonana na huyu jamaa alikuwa
taabani, na baadaye nikasikia tetesi kuwa huyo jamaa keshafariki…
****
‘Unajua mjumbe, sijui nikuambije,..unaweza ukasema milima haikutani lakini wanadamu hukutana, hata
hivyo, mbona nilipata taarifa za kijabu ajabu ina maana wanadamu wanaweza
kukutana na wafu…’nikasema sasa kiutani japokuwa moyoni nilikuwa bado na
mashaka.
‘Hahaha, watu bwana, unajua wabongo tunapenda sana uvumi, mzaha,
na ushabiki bila tathimini au uchunguzi, na hili ni tatizo,…ni kweli nilikuw
anusu mfu, ndio maana watu walisema nimeshakufa au sivyo…?’ akauliza na kucheka
‘Ndio hivyo, …ningekuwa na imani haba ningeogopa hata kukusalimia,
hapa nilitaka kukimbia, lakini nikajipa moyo maana kuna watu wengi..’nikasema
‘Yaani imekuwa kama siku ile ulipokutana na mimi pale Lugalo Hospitalini,
ulivyoogopa hata kunishika mkono, ukijua nimeshaathirika, au….’akasema tukacheka.
Ni kweli siku nilipoonana na huyu ‘mjumbe’, ilikuwa ni hospitali ya Lugalo, alikuja kupata
matibabu, mimi nilifika hapo kumuona mgonjwa wetu aliyekuwa kalazwa hapo hospitalini.
Mara nikiwa naingia kwa haraka maana muda ulikuwa umekwisha wa
kuona wagonjwa, ghfala nikamuona mtu anatembea mwendo wa shida, kakonda,…ukomo
wa kukonda, binadamu akikonda hubadilika kabisa….anazeeka, hata kama alikuwa
kijana.
Mtu huyu akawa ananijia na huku akijaribu kuatabsamu, lakini uso
ulionyesha huzuni na labda machungu, nikawa naogopa, maana ni kile kipindi
ugonjwa wa ukimwi unaogopewa, moyoni nikajua ni muathirika tu.
Jamaa akanisogelea, akanyosha mono kunisalimia kiukweli mkonow
angu ulikuw amnzito kuitikia ile salamu, nikawa kama nimeshikwa na ganzi,
nikabakia kumuangalia huyo jamaa, kwangu bado sikuwa nimempata vyema, lakini
aliponinyoshea mkono kunisalimia, nikaanza kumtambua.
Jamani binadamu akikonda hubadilika,..na hasa kama alikuwa mnene,
na akaisha kihivyo….mabega yamepaa, mkono umekuwa mwembaba, binadamu
anabadilika, na akibadilika hata sura huwa nyingine kabisa, jamaa yangu alikuwa
hivyo, niliogopa hata kuitikia salamu ya kumshika mkono, lakini kiujasiri w
kujidanganya nikainua mkono wangu tukashikana,..mkono wangu ukawa unatetemeka.
‘Mjumbe, …..aheri nimekuona, maana hapa sina nguvu, naomba unipelekee hiki cheti pale mbele, ili
niweze kuingia kumuona dakitari,…..kuna majibu yangu ya damu na vipimo vingine….’akaniambia
‘Una matatizo gani mjumbe?’ nikajikuta namuuliza.
‘Sijui ….aheri ningelijua nikajua moja, lakini ngoja tusubiri
vipimo, ndivyo msema kweli, ni aheri
ningelijua kuwa naumwa ukimwi, ningelijua kuwa mimi ni muathirika, lakini hii
ni mara ya pili katika kipindi cha miezi mwili, ya kwanza niliambiwa sina
tatizo,watu hawakuamini…mimi najua ni kweli sina,..lakini kwanini nakonda,
kwanini mwili unaisha,..hiyo ni siri yangu, au labda madocta wananificha ..sijui
…’akasema.
‘Kiukweli sijakuelewa..unasema unajua kwanini unaisha hivyo na
hiyo ni siri yako…na bado umepimwa, huna tatizo, kwanini sasa husemi hiyo siri
yako, ili ukatafutiwa dawa, au ufumbuzi…..’nikamwambia
‘Hakuna atakayenielewa….ni adhabu mpaka iishe…….’akasema
Sikuweza kuongea naye zaidi, basi nikachukua kile cheti na
kukipeleka kwa dakitari kwa ajili ya kupewa majibu yake, nilitamani nimuombe
dakitari nifahamu ukweli, lakini haikuruhusiwa, hata hivyo, sikuwa na muda
zaidi, nikageuka, …kumuangalia jamaaa, nilimuona kaka kainama chini…,
Sikuwa na muda wa kurudi kuongea naye tena, maana muda wa kuona
wagonjwa ulikuwa umepita, na mimi nilihitajika kumuona mgonjwa wangu, nikatembea
uelekeo mwingine nikajua nitarudi
nitakuja kuonana naye nijua vipimo vyake vinasema nini, na wakati
nampita akainu uso akatikisa kama kunishukuru, ila niliona ajabu, kwani macho
yake yalikuwa yanatoa machozi, alikuwa analia...
Machozi yalikuwa yakitoka kwenye macho ambayo, yamemtoka kwa ajili
ya kukonda,.., uso wake ulikuwa umekunjamana, na hata nywele zilionekana kama
kunyonyoka, nikajikuta na mimi machozi yananitoka.
Wakati namuangalia nikakumbuak enzi zetu za shule tukiwa
sekondari ya Umbwe (mti safi wa matunda bora). Jamaa huyu alikuwa pandikizi, japokuwa kipindi hicho hakuwa na kitambi, na kipindi
hicho alikuwa na sura ya utoto, ujanaa …lakini siku hiyo nilipokutana naye
Lugalo, alikuwa kaisha kikomo cha kuisha, kazeeka, ….oh.
Machozi yalipomtoka, akachukua leso yake kwa mkono usio na nguvu, na
kuyafuta machoz yake kwa haraka, na mimi sijui kwanini, machozi yakinilenga lenga, nikijaribu kujizuia
nisiendelee kumtizama, na akilini moja kwa moja nikajua ni muathirika, huruma, ikanija, nikijua mwenzangu huyo
anahijia huduma, na nasaha ya hali ya juu, na sio kulia. Yeye akasema;.
‘Usijali rafiki yangu haya ndiyo majaribu ya dunia, lakini
sijambo, ujue nilipima hospitali moja, nikaambiwa sina tatizo, nikasema
haiwezekani, jamaa yangu mmoja akaniambia, hao walionipima, wamenidanganya, akanishauri nije hapa, ndio
nikaona nifika hapa nipime tena…’akasema
‘Usijali, yote ni heri na kuumwa sio kufa , na ukiumwa muhimu
nikutambua tatizo ni nini….’nikasema hata mimi kichwani nilijua ni lazima
kaathirika.
Nilitaka niwe nay eye hadi kwa dakitari, ili niwe na uhakika
lakini muda ulikuwa hautoshi kumsubiria, nikamuacha na kuelekea chumba cha
wagonjwa walilazwa, nikamuona jamaa yangu tukasalimiana kidogo, baadaye
nikaambiwa nitoke maana muda wa kuona wagonjwa umekwisha. Ikabidi sasa nirudi
kumuona huyo rafiki yangu.
Wakati natoka, nikamuona rafiki yangu akiwa ametoka kwa dakitari,
akiwa kashikilia kile cheti chake na karatsi nyingine ya majibu, akaniona
akatabasamu, halafu machoni nikamuhisi anataka kulia, nikamsogelea na kumshika,
nilijua analia kwasababu ya hayo majibu kuwa `kaathirika’ na kwahiyo anahitajia
ushawishi na kumpa moyo.
Nilipomshika kama kumkumbatia hivi, akaanza kulia, ile kulia kwa
kwikwi kwa kutikisika, hadi baadaye akatulia, na mimi hapo nilipo nguvu zikawa
hazipo,nikijua nimemshika muathirika na sijui..unajua siku hizo elimu japokuwa
nilikuwa nayo kuwa huwezi kuambuskizwa kwa kumshika mtu, lakini ila hali ya
udhaifu wa kibinadamu, ilinifanya niwe na mashaka, woga, na nikijua mwenzngu
sasa ndio anaanza safari ….nikawa nimetulia nikisubiria aniambie kaambiwa nini,
na moyo sikuwa na shaka, nilijua jibu ni moja, kuwa kasha-athirika.
‘Samahani rafiki yangu usione nalia,…nalia na mawili, kwanza nalia
kwa vile huenda kama wanavyosema watu madakitari wanaendelea kunificha,
wananiambia sina tatizo..wanasema damu yangu ni safi, na sina tatizo ..labda
nipime vipimo vingine vya `utra sound..’
lakini siumwi ndani, mimi siumwi hivyo wanavyofikiria wao, hata sasa…sielewi
rafiki yangu…’akasema.
‘Lakini pili ambalo ni baya zaidi, nalia kwa vile jamii na dunia
imeshanitenga, nalia kwa vile sina raha, sina ndugu sina….unakumbuka
nilishaona, niliamua kuoa mapema tu, nikijua nitajituliza, kama unijuavyo tamaa
za ujana ziliteka, na ushauri niliokuwa nimepewa ni kuoa, sasa mke kanikimbia….’akasema
na sasa akaanza kulia tena.
Alipotulia akanionyeshea karatasi yake ambayo kweli ilionyesha hana matatizo yoyote zaidi ya
udhaifu wa mwili na hakuwa na tatizo la maradhi mengine, damu , mkojo na kila
kitu hakina matatizo, moyoni nikajisemea, mara nyingi madakitari hawasemi moja
kwa moja una ukimwi watakuambia unaumwa homa, tumbo , kwahiyo labda walitumia
hekima hii kumficha huyu jamaa. Lakini hata hivyo mbona hata magonjwa mengine
hana!
‘Pole sana,natumai wamekupa dawa itakayokusaidia…, na vipi maisha
mengine, yanakwendaje?’ nikamdadisi, akaniangalia akajitahidi kutabsamu,
akainama chini na hakusema jambo hapo, alipoinua uso, jibu nikaliona… machozi…!
Machozi yale yaliashiria mengi, na kwa mwenye akili alijua kwanini
alitoa machozi yale. Na kabla hajanihadithia lolote nikaitwa na jamaa zangu
kuwa wanataka kuondoka, na mimi nilikwua nimedowea lifti , sasa nikajiona nipo
njia panda, nibakia hapo nimliwaze rafiki yangu na nisikia masahibu yake au
Wenzangu wakawa wananiita kwa ishara kuwa tunachelewa na mjumbe
akawaona, akasema;
‘Nenda tu rafiki yangu…mungu akipenda tutaonana, na kama labda
ndio siku ya mwisho kuoanana na wewe, usiache kuniombea duwa,….’akasema, basi Ikawa sina jinsi nikamuaga rafiki yangu huyo
kwa kumpa chochote mkononi.
Siku zikapita nikawa nimemsahau, na siku moja nikakutana na jamaa
yangu mmoja anayemfahamu huyo mjumbe, akaniambia, jamaa alikwisha fariki..
NB: Ndio tumeanza kisa chetu hivyo, kaeni mkao wa kula
WAZO LA LEO: Unapokutwa na matatizo ya dunia, usikate tamaa, japokuwa matatizo
yanazidiana, unaweza ukaandamwa na matatizo mfulululizo mpaka ukasema `kwanini
mimi’ ukafikia hata kukufuru na hata kuingia kwenye shiriki. Kumbuka matatizo
ni yetu wanadamu , na matatizo ni sehemu ya mitihani ya kimaisha, usikate
tamaa, zidi kumuomba mungu, huku ukijitahidi kupambana nayo, ipo siku utashinda
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment