Siku zikapita nikawa nimemsahau, na siku moja nikakutana na jamaa yangu mmoja anayemfahamu huyo mjumbe, akaniambia, jamaa alikwisha fariki..
‘Keshafariki, una uhakika?’ nikamuuliza.
‘Hivi kwa hali ile unaliza una uhakika uliwahi kumuona siku za
karibu, akiwa kazidiwa, ameisha, anatembea utafikiri mzee aliyechoka, mwili
umekuwa kama skeletoni …..’akasita kuongea kwani aliona mdada akipita, na jamaa yangu huyu ni mwngi wa mambo hayo.
‘Nilimuona Lugalo hospitalini…’nikasema nami nikigeuza uso kuangalia huko anapoangalia
‘Pale walimdanganya kuwa hana tatizo,…alishaathirika
yule wakamficha kiaina…’akasema
‘Aaah, …wasingelimficha, wangelimuambia wakampa nasaha na jinsi
gani ya kuishi maisha ya matumaini, ..sizani kama alikuwa na tatizo hilo...mimi mwenyewe niliona cheti chake na majibu ya vipimo labda kama alikuwa na tatizo jingine..’nikasema.
‘Wewe niulize mimi,…keshaaga dunia yule…tusubiri zamu zetu maana
tatizo hilo sio la mmoja, tutakwenda wengi…’akasema akizidi kumuangalia huyo mdada, na vazi alilovaa huyo mdada lilizidi kumchanganya mwenzetu, kwani lilimkaa vyema mwilini, akawa anatembea kwa madawa,
na jamaa akawa anajilamba lamba mdomo.
‘Acha tamaa, hebu niambie ukweli…’nikasema.
‘Ukweli upi tena..nisubiri
hapa nitarudi, yule hawezi kupita hivi hivi, lazima nimpe neno, huwezi jua….’akasema na akamfuatilia huyo binti, mimi nikaendelea na
mambo yangu, nikijua kweli huyo jamaa ameshafariki, leo hii nakuatana naye akiwa hai na afya tele, na gari alilo nalo linashiria kuwa hali ni nzuri kweli sikuweza kuamini...!
Tuendelee na kisa chetu....
*******************
`Je rafiki yangu amepata bingo gani…’ nikamuuliza
Yeye akasema;
‘Hebu twende kwenye gari, maana hapo gari lilipo sipaamini sana umeona muda kulitaka kutokea ajali, ukiwa ndani ya gari unajishau, hasa madereva wasiojua nini maana ya kuwa dereva,
..’akasema na kunishika mkono, tukaenda, na kuingia ndani ya gari lake, hali
ya hewa, baridiii, nikajihisi nimeingia dunia nyingine,….wenzetu wana raha jamani acheni wazidi kuwa mafisadi…..,
`Ni siri gani ya maisha uliyoigundua, nami niitafute huenda
nikapata mafanikio kama yako…’ Nikaendelea kumuuliza yeye akaendelea kuwa kimia
huku akiendesha gari lake hadi sehemu nzuri, akalisimamisha
Akageuka na kuniangalia akatabasamu na akainua mkono na kunigonga
gonga mgongoni kwa nguvu alizo nazo, nilihsi maumivu, lakini sikusema kitu. Sio
ule mkono tena ambao niliogopa kuupokea siku ile, sasa ni mkono ambao una kilo nyingi!
Akauondoa mkono mgongoni kwangu, halafu akacheka, akaniangalia kwa muda kama
vile anatafakari jambo…mara nikamuona akama anataka kutoa machozi, …nikashikwa na mshangao,
ikabidi nimuulize
‘Vipi tena, maana kwa hali uliyo nayo sihisi kama unastahili kutoa
machozi...'nikasema na yeye akachukau leso yake na kuipitisha machoni, halafu akasema;
`Unanikumbusha siku ile, tulipokutana
pale Lugalo hospitali, unakumbuka, ulipoondoka na kuniacha, unajua nilizidiwa sana hadi kuchukuliwa kulazwa, hakuna hata ndugu aliyekuja kuniona, baadaye nikatoka, nikiambiwa
sina tatizo,ikabidi nihame mji, ndipo watu wakajua nimeshakufa…!’
‘Ooh, hata mimi niliskia hivyo ndio maana nakuwa na hamu sana ya
kutaka kujua historia ya yaliyokukuta, …ni maombezi, au ni miujiza gani
uliyokutana nayo, au ulipata tiba mbadala, maana nasikia kuna wataalamu wa
kutibu kila magonjwa siku hizi…’nikasema
`Ndugu yangu hebu tufike hapo hotelini tupate chochote ili nikupe
hadithi yangu , kiukweli ni hadithi ndefu, nikianza kuielezea hapa siku itaisha..’akasema huku akifungua mlango wa gari, nami nikafanya hivyo tukatoka na kuelekea kwenye hoteli iliyokuwa hapo karibu. Baada ya kuagiza vilivyoagizwa, akasema;
‘Kisa changu ni kirefu, nadhani kama nikutunga kitabu basi kitakuwa
kitabu kikubwa sana, na labda viwe zaidi ya vitabu viwili..ila nitajaribu kukupa kwa muhtasari tu,
kwani dunia hii ina mambo, lakini yote tisa, tuwaheshimu sana wazazi wetu, na
kila mara nikimukumbuka mama yangu, natamani kulia, lakini ndio maisha na
nikumbie kitu, ndugu yangu, ‘ hakuna kama mama..’ akatulia.
‘Mama!!, kwani mama yako yupo wapi?’ nikamuuliza nikiogopa kumuuliza
kuwa mama yake yupo hai au..
‘Rafiki yangu hivi kweli niambie ..Ni ' Ni nani kama mama '…katika hii
dunia?’ akaniuliza huku akianiangalia, na machoni nilimuona akijenga ukungu wa
machozi.
Nilimwangalia bila kumpa jibu ili aendelee na kisa chake, akatulia
kwa muda halafu akaniangalia tena, sasa akiwa na tabasamu usoni.
`Mimi katika maisha yangu kilichonisaidia na kufikia mafanikio
niliyo nayo hivi sasa, ni SU-BI-RA, na UCHA MUNGU... Alilitamka neno hili kwa
sauti kubwa, `subira’.na 'Ucha mungu'
`Hutaamini kuwa nilishaliona kaburi hilo...na watu walikuwa
wanahesabu masaa, wakisikilizia…lakini cha ajabu nilikuwa siumwi na ugonjwa
wowote, na siku ile nilipokutana na wewe pale lUGALO, sikujua naumwa nini....mwili tu ulikuwa
unaisha, udhaifu, sisikii kula….nikawa nakonda kwa mawazo.
Siku ile nilifika kupima tu, ili niwathibitishie walimwengu kuwa
siumwi ugonjwa huo wanoufikiria wao...., ila naumwa ugonjwa usioelezeka, ugonjwa wa mawazo na matatizo. hakuna ugonjwa mbaya kama mawazo,..., shida ziliniandama, na umasikini ukanijaa mwilini, laana ikawa imenifika….
Rafiki yangu, matatizo yaliniandama kama mvua, lakini nikakumbuka
kile kisa cha nabii Ayubu,jinsi alivyoteseka,.. na matatizo yaliyomkuta,
akakimbiwa na jamaa zake wote, lakini hakukata tama, kwasababu ya subira.
`Nadhani hata wewe uliyeniona kipindi kile usingeamini kuwa
siumwi, na wengi hata wewe walidhania kuwa nimeukwaa, nimeathirika, lakini kwa uhakika nilikuwa siumwi, watu
walinikimbia wakizani nina ukimwi, lakini yote nilimuachia mungu.
Matatizo niliyokuwa nayo
hakuna aliyejua kiini chake….Ni nani umgemwambia kipindi kile akuelewe..hakuna,
kila mmoja alikuwa akisema lake…unajua nilipozidiwa watu walifikia kusem;
‘Mwache afe si-amejitakia mwenyewe, mzinzi mkubwa huyo, …na
mengine mengi…’akatulia
'Jamani hivi kweli mimi nimekuwa mnzinzi zaidi ya wazinzi waliojaa humu duniani…ni kweli ujana una mambo yake,
lakini hayo waliyokuja kunipakazia jamii, hayakuwa na ukweli, ukweli wa hayo yaliyonkuta ni
tofauti kabisa, na hicho walichokuwa wakikifikiria wao…’akasema
‘ Lakini ya mungu mengi, yote hayo yalikuwa maneno ya wanadamu
wasiokuwa na simile, na raha yao kuona wengine wakitaabika...mimi nilikuwa na yangu makubwa ambayo kwa wenye kufikiri wataelewa na kujifunza...’ Akasema huku
anamimina kinywaji chake.
`Unajua kwa matatizo niliyokuwa nayo ilifikia hatua mke wangu mwenyewe
akanikimbia…jamaa na ndugu zangu wakawa hawaonekani tena….’akasema
‘Na kiukweli, matatizo haya yalianzia kwa mke wangu mwenyewe, na huyo huyo akanikimbia, …na matatizo hayo
yalianza pindi nilipoamua kumchukua mama yangu ili aje tuishi naye. ....hapo sasa nianze kukuhadithi vyema....'akasema akijiegemeza vyema kwenye kiti....
************* kisa kinaanzia hapa*************
Kama nilivyosema mimi niliamua kuoa mapema, ili kuhimili tamaa
zangu kama mlivyoniona kule shuleni nilikuwa situlii, nahisi ndio maana
nilipoanza kukonda watu wengi walikimbilia kusema nimathirika, ...lakini
kiukweli baada ya kuoa, mimi niliamua kutulia kabisa mimi na mke wangu, na uzuri,
mke alikuwa keshanijulia, kwahiyo sikuwa napata taabu.
Nilioa nikiwa bado kwenye nyumba ya kupanga yenye vyumba viwili
baadaye nilipopata mtoto nikachukua chumba cha tatu… kipato changu kilikuwa sio
kikubwa sana, kama ujuavyo mishahara yetu, lakini maisha nilikuwa nayamudu.
Tulipopata mtoto gharama zikaogezeka, ikabidi kujipanga vyema, mke
wangu naye akawa anabangaiza huku na kule, alikuwa muhangaikaji kweli,
anajituma, ili tuweze kuyamudu maisha,
maisha yakawa yanakwenda, japokuwa kiukweli kipato hakikuwa kinakidhi haja
saana, maana licha ya sisi weyewe, bado mwanzoni tulijitahidi kuwakumbuka
wazazi ....
Mama yangu alikuwa kijijini na maisha yake yalikuwa ni ya
kimasikini kweli, sikupenda kuoa mapema, ili niweze kumuhudumia mama yangu, lakini
mama ni mmoja wa watu walionishinikiza kuwa nioe mapema,....alisema, hataki
kuja kuathiriwa na tabia yangu, aliyoiita chafu, na pia anahitajia wajukuu,
kwahiyo niliamua kuoa kwa ridhaa yake.
Unajua ukishaoa, umeshakuwa na mwenza wa ushauri, kwahiyo huwi na
uhuru wa maamumuzi ya peke yako tena, pili kutegemeana na kipato changu kidogo ilibidi
nianze kuangalia maisha yangu na familia yangu kwanza, kwa hali hiyo nikajikuta
naanza kumsahau mama, kiukweli ikafika muda sikumbuki kumtumia mama pesa za
matumizi kama ilivyokuwa awali,...
Ni mke wangu ndiye aliyekuwa kwa asilimi kubwa akisaidia sana
familia, mshahara wangu wa mwezi ulikuwa ni mdogo, ukipata unalipa madeni,
umekwisha, ninabakia kutegema kile kidogo anachopata mke wangu kwenye biashara
zake, kwahiyo mke wangu akawa ni mtu muhimu sana.
Lakini kipato cha mke wangu ni cha mke wangu, na sio kwamba
alikuwa akipata pesa nyingi, hapana ni hela za kusaidia kula kwa siku hiyo,
kesho yake anajituma kupata nyingine, kwahiyo sikuweza kumwambia lolote mke wangu kuhusu
hali ya mama ….
Ikafikia muda watu wanaotoka kijijini wakawa wananiletea
malalamiko kuwa mama yangu anaishi kwa shida, na mimi nimemtelekeza mama, nimesahau
nilikotoka, na lawama nyingi tu na ni kweli kutokana na hali ya kimaisha na
kipato, nilikuwa nimeshamshau mama yangu, ningefanyeje.....
Kwa kuona hivyo, ikabidi niongee na mwenzangu kuwa tufanye nini
maana mama anateseka huko kijijini, yeye akanishauri tumchukue mama, aje tuishi
naye...wazo hilo sikukubaliana nalo, nikijua hali halisi tuliyo nayo,...na mama
yangu nimjuavyo hataweza kuivana na mke wangu.
Sio kwamba mama ni mkali, hapana mama ni mtu mpole sana, lakini
mke wangu ana tabia ya utegemezi, maamuzi ya kibinafsi, kujiona na msafi
sana....sasa akikutana na mama ambaye ni mpole , huruma....nahisi kuna hali
itafika nitakuwa upande wa mama, nikitaka hiki kifanyike kwa mama na mke wangu
anaweza akapinga, ni mawazo yalinijia tu, japokuwa sikuwa na uhakika nayo.
Lakini cha muhimu sana, ni hali ya kimaisha na kipato
tunachokipata je kitaweza kutuwezesha sote hata hivyo nikaona pia ni wazo jema ili kwa hicho kidogo
tunachokipata tunaweza tugawana hivyo hivyo,;
‘Kwanini tusiwe tunamtumia kidogo kidogo ....maisha tunayoishi ni
ya shida, akiongezeaka mtu mwingine tutazidi kuumia.....’nikamwambia mwenzangu
kuzidi kumpima, kama kweli ana nia hasa ya kuishi na mama yangu, nay eye akasema
‘Unajidnganya, mbona inapita miezi mitatu, hujamtumia mama yako
pesa, mimi naona ni bora aje tuishi naye hapa, hicho kidogo tunachopata akione, na aone maisha tunayoishi, sio
wanasema tunaishi kwa raha, sijui nini na nini, aje ajionee mwenyewe,
tunavyohangaika usiku na mchana....’akanishauri mwanzoni nikapuuza, nikatuma
vijisenti kidogo, ....
Haikupita muda watu walitoka huko kijijini wakaja na taaarifa kuwa
mama pamoja na hali ngumu, anaumwa, anateseka , kwahiyo nikapanga kwenda
kumchukua, nikaomba ruhusa ya siku kadhaa, na kukopa kiasi kidogo kazini
kinisaidie kwa nauli, nikasafiri kwenda kumchukua mama...
**********
Nikiwa njiani nilikumbuka jinsi gani mama yangu alivyonilea kwa
shida, unajua maisha ya kwetu kijijini na ukiwa na baba ambaye hajui umuhimu wa
familia, yeye anachopata ni kunywa, na kwenda kutangaza utajiri wa kufikirika
kwa marafiki zake, akirudi kalewa, ukali...basi mama akawa anabeba majukumu
yote.
Niliwaza mengi kuhusu Mama, mama yangu, nikajuta kwanini sikuweza
kumkumbuka, na hadi kufikia kiasi hicho. Hivi ni nani anastahili kufaidi
matunda na jash la mwanae, nilijiuliza
‘Kwanza ni mzazi wako, maana ndiye aliyekulea kwa shida,, na hasa
mama yako, na bahati nzuri mama yangu yupo hai kwanini nimtese, na ndio
nikakumbuka ule usemi, aliokuja kuniambia mmoja wa watu waliokuja kunipa
taarifa, aliniuliza swali
‘Ni nani kama mama yako...?’
‘Hakuna ‘ nikamwambia.
‘Sasa kwanini unamuacha mama yako ateseke mwenyewe huko kijijini..?’
akaniuliza
‘Ni kwasababu ya maisha magumu, kipato kidogo, sasa ninashindwa
kukigawa,...’nikajitete hivyo.
‘Hivi wewe unajiona ni bora zaidi ya mzazi wako, wewe ule ushibe
na mke wako wakati mama yako anateseka kijijini?’ akasema kama ananiuliza.
‘Sio hivyo, na sio lengo kufanya hivyo, ni hali halisi..’nikasema.
‘Fikiria sana...katika dunia hii wazazi ndio baada ya
mungu,..wakiteseka ujue na hali yako itakuwa ngumu,...mkumbuke mama yako,
kumbuka ulipotoka, hakuna kama wazazi wako, hakuna mama yako....’akaniambia.
‘Ni kweli hakuna mama.....’nikasema wakati nashikwa na usingizi na
nilipoamuka nikajiukuta nimeshafika kijijini.
Kwakweli hali niliyomkuta
nayo mama ilikuwa ya kusikitisha kweli, ...analalia mkeka, chakula cha shida,
...siku hiyo niliyokaa hapo nilitamani kupambazuke haraka tuondoke,
nilishasahau kuwa ndiyo maisha niliyokulia, ndipo nilipotoka.
Kweli kesho yake tukaondoka naye na kuelekea mjini, japokuwa mama
alinisihi kuwa nisichukulie haraka kuondoka naye, kwani hamjui huyo mke wangu
yupoje.
Kiukweli tangu nimuoe mke
wangu, hatukuwahi kuja kukaa hapo nyumbani, hata siku ya harusi, tuliifanya
kinamna yake, kwani tulifika mchana tukaenda kuoa, kufika kwa mke, kukawa na
shughuli iliyochukau muda mrefu, tukarudi hapo nyumbani usiku, kesho yake tukaondoka,.
‘Unajau mke wako hata sura yake siifahamu vyema, maana siku ile ya
ndoa yenu mlikuja usiku na mkaondok kesho yake alfajiri,, na hamjapata muda wa
kuja kunitembelea, mpaka mumepata mjukuu, hutaki hata kumleta mkeo, si vizuri
hivyo....’akalalamika mama.
‘Mama ni hali za maisha, yeye ananisaidia kutafuta maisha,
nikisema tuje wote huku, nani atahangaika huko, ndio maana nilikuwa nakuja
mwenyewe, ili yeye apate muda wa kutafuta kidogo kwa ajili ya kesho na
kumuhudumia mtoto..’nikajitetea
‘Haya twende huko mjini, sijui mkeo atanikubali na hali yenyewe
hii...’akasema mama akijiangalia nguo alizovaa, na moyoni nikawa nasononeka,
kuwa hata nguo ya maana sikuwahi kumnunulia mama.
‘Mama usijali yeye mwenyewe ndio katoa pendekezo hilo, muhimu ni
kusikilizana naye tu, kwani anajitahidi sana kunisaidia katika maisha, na
sizani kama atakufanyia ubaya wowote..’nikamwambia
Basi tukaondoka na kufika mjini, na tulifika usiku, baada ya mama
kuoga na kuandaliwa sehemu yake ya kulala, tukaongea kidogo, ...joto
lilimsumbua mama, kwahiyo kuna muda akawa kajifunua,...mama hapendi kabisa
kujifunua sehemu ya uso wake, muda wote kajitanda,na kuacha sehemu ndogo tu ya
usoni.
Mke wangu akawa kamuona mama vyema sasa, nikaona mke wangu akikunja sura yake, akawa kama kaona kitu cha kumtisha, sikujali
nikajua ni ile hali ya adabu kati ya mke na mama mkwe wake,..
Hata kesho yake, sikuona ule uchangamfu wa mke wangu kwa mama,
...tangu siku hiyo, mke wangu akawa kabadilika, akawa mara kwa mara akimtizama
mama kama anamuogopa....sikutaka kumuuliza, nikawa najua kuwa watakuja kuzoeana
tu.
Hata hivyo nikiwepo karibu, mke wangu alijitahidi kumnyenyekea
mama yangu kama ilivyo kuwa ada kwa wake kwa mama zao wakwe, maisha yakaenda
hivyo, japokuwa kiukweli sikuona ile hali niliyoitarajia kwa mke wangu kwa mama
yangu, kwani mke wangu ni mcheshi, tukiwa naye najisahau kwa ucheshi wake,..lakini
alipokuja mama, ikawa kama kuna kitu kimemuingia mke wangu akawa na ukimiya wa
ajabu.
Kwa mfani kama nipo naongea
naye , akitokea mama tu, yeye hubadilika, akawa kimiya, akawa kama anaogopa
kitu anakuwa hana raha kabisa, nikaanza
kuhisi vibaya, kuwa mke wangu hampendi mama, …nikjajifanya kama sijali, tukaendelea
kuishi hivyo hivyo, na masiku yakaendelea mbele na siku moja ambapo ndipo mambo
yalipoanzia likatokea la kutokea.
******
Siku hiyo ambayo sitaweza kuisahau, mke wangu alitoka kwenda
bafuni, wakati ameshaoga, anatoka mlango wa bafuni, ghafla akateleza na
kudondoka chini, Kabla hajainuka alisema kichwa kinamuuma, akaanza kulalamika
kichwa, kichwaaa,…
Ghalfa akakurupuka, na kuanza kutingishwa, unajua kutingishwa.
Yaani wewe chukua chupa kama hii ya soda uitingishe harakaharaka, ndivyo
alivyokuwa akitingishwa mke wangu. Na huku anaweweseka, na kutoa sauti ambayo
siyo yakwake…ilikuwa sio sauti yake, kabisaaa…
‘Kwa mtu yoyote atajua kuwa hayo ni matatizo ya mashetani
yamempanda, lakini kwa mke wangu tangu nimuoe hajawahi kutokewa na kitu kama
hicho, kwahiyo, nilivyotoka nje na kumuona katika hiyo hali, sikukimbilia moja
kwa moja kuamini hivyo, nilijua ana malaria au shinikizo la damu…nikamshikilia
kwa nguvu, hadi nikachemsha, na kwa muda huo mama alikuwa ndani akisaidia
kupika.
Mama aliposikia hiyo hali ikabidi aache shughuli, aje kuona kuna
tatizo gani,akanikuta napambana na mke wangu nikijaribu kusmhika, ili
asijiumize, maana alikuwa akijigonga gonga, sakafuni, mama akasogea na
kumuangalia mke wangu.
Mama ni mama, wanajua mengi zaidi yetu, akaanza kumuongelesha kwa
kumuuliza mke wangu,
‘Niambie wewe ni nani na una shida gani kwa mtoto wangu..?’ mama
akauliza
‘Unaniuliza mimi ni nani, mimi ndiye mwenye nyumba hii, na kuwepo
kwangu ni kwasababu yako wewe, unataka kuiharibu nyumba yangu…wewe ndiye mbaya
wangu…’ sauti ya ajabu ikatoka kwa mke wangu.
‘Hebu nieleze ubaya wangu kwako ni nini…’ mama akamuuliza
‘Sikutaki humu ndani, uondoke haraka, la sivyo nitakufanya kitu
mbaya, na wewe sio mtu mwema kabisa kwenye hii familia, toka,nakumabia
toka…toka, wewe ni mchawi, mwanga, toka humu ndani haraka, unataka kunai na
kumuua mtoto wangu….’ Akawa anayarudia haya maneno huku anamsukuma mama kwa
kidole chake.
Mama alikaa kimiya, ilikuwa kama kitu kimeshika , akawa hana
nguvu, akatulia kwa muda, na wakati huo mke wangu naye akalegea na kulala
chini, na hapo tukawa tunampepea mama akawa ananiangalia kwa makini, akiwa kama
anataka kujua nitasema nini, lakini mimi akilini sikuwa na mawazo yoyote mabaya
kwa mama yangu, nilijua hayo ni malaria kwa mke wangu, kapawa tu.
Baadaye akatulia , mke wangu akarejea katika hali yake, akasimama
na kuelekea ndani, na mimi nikamuuliza mama yale maneno ya maana gani, mama
akaniangalia machoni , akasema,
`Hayo ni mambo ya kiulimwengu, ukichukiwa na walimwengu, kila mtu
atakunyoshea kidole, sina zaidi ya kukueleza mwanagu, subiri umuulize vyema mkeo
yeye atakufafanulia zaidi…’ akasema mama na kusimama kwends kuendelea na
shughuli zake
Mimi nikamfuata mke wangu ndani, nilimkuta kajilaza kitandani,
nikamuuliza hali yake, akasema kichwa ndicho kinamsumbua, halafu yeye
akaniuliza;
‘Kwani kulitokea nini?’ akaniuliza
‘Ulishikwa na kitu kama mashetani, ukaanza kuongea ovyo,
sikukuelewa kabisa..’nikasema
‘Nilingea nini?’ akaniuliza
‘Aaahm hayo yaache tu, mimi naona ni heri ukapime malaria …’nikasema
‘Niambie niliongea kitu gani, nataka kujua….’akanisisitizia
‘Uliongea kwa sauti ya ajabu ukasema mbaya wako ni mama eti mama
ni mchawi….’nikasema
‘Oh, kumbe…nilijua tu, sasa mambo yametoka waziwazi, natumai mwenyewe umesikia hayo, mama yako ni
nani…umeyasikia mwenyewe, usija kusema ooh , mimi nimzua, sasa elewa kuwa
tunaishi na nyoka humu ndani…’akasema
‘Unasema nini?’ nikasema kwa hamaki.
‘Lakini si umesikia mwenyewe…sio mimi , kama ingelikuwa ni mimi
ungeliskiai mapema nikiongea, je sauti ilikuwa ya kwangu au ilikuwa sauti ya
mtu mwingine?’ akaniuliza
‘Kwahi hata ikiwa sauti ya mtu mwingine, huoni labda ni malaria
umechanganyikiwa tu…’nikasema
‘Sikilize mume wangu, hizo ni ishara zinakutkea ili umjue mama
yako vyema, siku ila tu nilipomona sura yake, nilihisi moyo ukinienda mbio,….nimekuwa
nikimuota ndoto mbaya, mara anataka kuniua,….mara anataak kumuua mtoto, sasa
hali imetokea dhahiri, ujue huo ukweli…..’akasema
‘Ujue huyo ni mama yangu, ndiye aliyenizaa…’nikasema
‘Sasa uamuzi ni wako, usubiri mabaya yatokee kwanza, au uanze
kuchukua uamuzi wa haraka,…kiufupi ni kuwa mama yako sio mtu mnzuri, na hali
ilivyo, mama yako hafai kuishi nasi hapa ndani…’akasema mke wangu.
Kwakweli sikuweza kusema kitu, kuna hali ikaanza kuniingia
akilini, nikiwazia hiyo hali liyomtokea mke wangu, nikakumbuka maneno ya watu
kuhusu hayo mashetani, kuwa yanaweza kukuelezea mambo usiyoyafahamu.
Lakini huyu ni mama yangu, hawezi kunifanyia hivi…’nikajikuta
nikijisema mwenyewe. Siku hiyo nzima ilikuwa kama kumingiwa na jambo kubwa sana
ndani ya familia yangu sote tulikuwa kimiya, hakuna kusemeshana, mke wangu akawa
haongeai na mimi, na mama halikadhalika.
Ilikuwa jambo la ajabu kwani tangu mama afike hapo sikuona dalili
ya mke wangu kumnyanyasa mama, ni ile hali ya kuwa kama anamuogopa tu, lakini
hakuwahi kumfanyia mama ubaya wowote, labda kama alikuwa akifanya hayo kisiri,
na hata mama sikumsikia akilalamika kuwa mke-mwana wake anamnyanyasa, kwahiyo
hiyo hali kutokea ikawa ni mshituko kwangu.
Mama alikuwa kipenzi change, nikikumbuka alivyonilea kwa shida,
sikutaka kabisa kutokea kitu cha kumuumiza zaidi ya hali mbaya iliyotokea
nikamuacha huko kijijini, nilipanga kuwa kwa vile tupo naye sasa, nitajitahidi
awe na maisha ya kawaida na sisi kutokana na kipato tunachokipata, mimi
nilikuwa mwana pekee kwake, leo hii mke wangu anadai kuwa mama ni mchawi na
hamtaki, kwanini, nilishindwa kupata jibu!
Hali ile ikamtokea tena, siki hiyo hiyo, ya kuweweseka, sasa hivi
nikakumbuka kuwa kama ni mashitani kweli kinachotakiwa ni kusoma vitabu
vitakatifu, nikawa namsomea mara kwa mara, nilimsomea na kumwagia maji , na
baadaye akatulia. Na ghafla akazindikuana, …
Alipozindukana, akanikodolea macho na kuniuliza kumetokea nini,
mimi nikamwambia kuwa kapandisha tena mambo hayo kama mashetani, akaniuliza kwa
kushangaa, mashetani?
‘Ndio kama yale ya mwanzoni, ulipodondoka ukitoka kuoga…’nikasema
‘Na hayo mshetani yanataka
nini?’ akaniuliza
‘Achana nayo bwana, eti yanadai hayamtaki mama, eti mama yangu ni
mchawi,kitu ambacho hakipo na hakiwezekani..hayo ni mashetani na mashetani haya
nia njema kwa wanadamu, ni bora yaangamie kabisa..’ nikasema huku naiunuka
kuondoka, kwani muda ulishaenda sana na nilitakuwa kwenda kubangaiza.
‘Sasa unakwenda wapi hili unaliona dogo sio, inabidi utafute
kwanini hili limetokea, wewe unaondoka, je likija tena nitafanyaje..’
akaniuliza mke wangu huku kanitolea macho.
‘ Nikuambie mke wangu, sasa hivi likija hili shetani liambie hilo
haliwezekani likafie mbali, hakuna kitu kama hicho mama yangu namafahamu sana,
mama yangu nimtu mwema sana..’Nikasema nakuondoka zangu
‘Huo ulikuwa ni mwanzo tu….’rafiki yangu…
WAZO LA LEO: Jamani tuacheni uzushi, kuna watu wengine wakisikia jambo tu, hata kama hawajalifanyia utafiti kuwa ni la kweli, wanaanza kulitangaza kila kona, bila kujali kuwa linaweza kuathiri au kuleta sintofahamu. Uzushi ni haufai, ulimi unaweza kuangamiza, tuwe makini kabla ya kutoa kauli zetu na kuwazushia watu wengine ubaya.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment