Mtoto
akajua kuwa mama yake kumbukumbu zake zimeshaanza kuleta shida, na kweli
kipindi hicho mama huyu alikuwa ameshaanza kujiwa na hali kama ya kuchanganyikiwa
akawa anaanza kuropoka ovyo, kusahau, na kuna muda anamkana mtoto wake huyo,
anamwambia yeye sio mtoto wake, mtoto wake hana sura kama hiyo….
‘Kwa
hali ile ikaonekana kuwa mama huyu anaweza kufichua siri, ukatoboa siri,
…lakini hana la kumfanya, kwani huyo ni mama yake bila yeye, hayo yote aliyo
nayo mali, cheo,…..asingelikuwa navyo…
‘Hali
hiyo kwa ujumla sasa ikawa nayo inampa shida, ikabidi mama huyo awe na ulinzi
wa ziada, hakutakiwa kutoka nje kuonana na watu japokuwa mama huyo alikuwa
mkaidi hakubali, ....
‘Unajua
kiukweli binadamu hachungiki, hasa mtu mzima kama huyo, ikawa ni taabu, mama
analalamika,…na akawa anaahidi kuwa ataenda polisi na kusema kila kitu…kwanini
mnanitesa, kwanini mnanifunga ndani kama mfungwa, kama mtoto wangu angelikuwepo
mngelifanyia hivi….hamji mali hii imetoka wapi…. mama akawa analalamika sana…ikawa
ni ugomvi…
Je
mtoto atafanya nini….
Tuendelee
na kumalizia kisa chetu.....
***************
Mtoto akajaribu kila njia kuona mama yake anatulia, na pia
kutaka kujua wapi alipoweka hicho kifaa chenye kumbukumbu, lakini mama akawa
hakumbuki, na majibu yake kwa huyo mtoto yalikuwa yale yale kuwa yeye sio mtoto
wake…
‘Wewe sio mtoto wangu siwezi kukuambia hata kama
ningelikuwa nakumbuka,…’akasema wazi wazi.
Ukumbuke kwa muda huo Moto alishatakiwa kuuwawa, akaponea
chupuchupu kwa kupitia kwa yule mtaalamu wa tiba mbadala, nilipewa sumu mbaya
nife, lakini nikawahiwa na mganga wa kienyejei akanitibu….’akaendelea kuongea.
‘Waliposikia kuwa nimepona hawakuamini, haijatokea, sumu
hiyo ukipewa huponi, iweje mimi nipone..jamani kuna wataalamu,…msiwadharau hawa
wataalamuw a tiba mabadala, huyo jamaa alinitibia katoa smu yote mwilini.
‘Hawa jamaa wakasikia nimepona, na mkuu huyu haraka
akajifanya ananijali, akatoa amri niwe nafanya kazi makao makuu, nia ili niwe
karibu naye, …na wajue imekuwaje,…muda huo sikuwa nafahamu lolote, sikuwa
nafahamu kuwa huyu mtu ni nyoka, najua tu, yeye ni bosi wangu, na kweli
ananijali.
‘Kuna muda nilikuwa napata mashaka, maana nikiwa karibu
naye, alikuwa akinituma kazi maalumu, na nikifika kwenye kazi nakutana na
mitihani mikubwa, taarifa zimeshafika kwa hao watu, na mara nyingi nikawa
naponea chupuchupu kuuwawa, nikawa
najiuliza, ni nani anatoa siri za kazi zangu na ni nani ametoa taarifa
zangu, wakati ilitakiwa nisifahamika kuwa bado nipo hai…..
‘Kipindi hicho baada ya kulipuka hilo bomu, tukawa
tumewachukua wale wataalamu wote, tukawaweka chumba cha siri, chumba hicho
alikifahamu mimi na muendesha mashitaka tu, hatukutaka mtu mwingine afahamu,…tulishahisi
kuna mdudu mtu, tukaona tubahatishe, ikawa siri yangu mimi na muendesha
mashitaka na vijana waaminifu wachache,
‘Mkuu alishapata taarifa kuwa wataalamu hao hawajafa, na
wapo mahali, lakini akawa hawajui ni wapi, mitandao yake tulishainasa, na
mtendaji wake wa mitandao tunaye, japokuwa alikuwa hajiwezi lakini akawa
anatuelekeza kwa shida, na uliweza kudhibiti sehemu kubwa ya mtandao wake,
lakini hatukuwa tunaelewa ni nani kiongozi… hapo tukaanza kutokuelewana na mkuu
wangu, akawa analalamika kuwa nafanya kazi bila kumuarifu yeye, na muda huo
yupo anatibiwa, tunawasiliana kwa ujumbe wa simu
‘Nimesikia wale wataalamu wapo hai, …wapo wapi?’
akaniuliza
‘Kuna sehemu wapo mkuu, usijali…’nikasema
‘Nauliza wapo wapi?’ akaniuliza kwa ukali na mimi sikumjibu
ujumbe wake huo, kitendo hiki kilimkwaza sana, hata akatoa taarifa makao makuu
kuwa mimi nakiuka utendaji wa kazi, siwajibi kwake, kwahiyo anapendekeza mimi
nisifanye kazi hiyo maalumu, apewe mtu mwingine. Maneno agalikuwepo angalipewa
yeye, lakini kwa mud huo alikuwa hajitambui kwani nay eye alikuwa miongoni mwa
wale waathirika wa kutaka kuuwawa na wale wataalamu.
‘Kwa muda huo mimi na muendesha mashitaka tulishaongea
na makao makuu, kuwa kazi hiyo ifanikiwe, ili tuweze kulinasa hilo kundi na kiongozi
wake basi watuachie hiyo kazi, na viongozi wote wa kiengo wasihusishwe, makao
makuu wakanielewa.
Siku moja tukamtembelea huyo kwa mama kwa kushitukizia,
na siku hiyo, akawa yupo vyema, kiasi, ila waliyoyaongea, yakatupa mashaka,
kwanza analalamika kuwa amefungwa, hana kosa, pili, anadai mtoto wake yupo
hajafa,….
‘Huyu mama anaweza kutusaidia,…’nikasema
‘Lakini kachanganyikiwa…’akasema mwenzangu
‘Tumchukue, atatusaidia mengi, …’
Mimi na muendesha mashitaka tukakubaliana kuwa tumchukue
huyo mama, tuwe naye karibu, huenda tukapata mengi. Kazi hii ilifanyika kwa
siri, na mama akijua tunamtoa kwa kile alichokiita kifungo, akakubali,
tukampeleka sehemu nyingine, lakini chini ya ulinzi wa kuhakikisha hatoroki.
Mkuu aliposikia kuwa mama huyo kachukuliwa, alikuja juu,
kwanza alidai tunakiuka sheria, za kumshika mtu asiyeruhusiwa kisheri, mama
huyo kachanganyikiwa,sisi tunamkamata , tunakiuka sheria na haki za binadamu,
lakini hatukujali hayo sisi kimiya.
‘Kiukweli tulijua hilo ni kosa kisheria, sasa tufanyeje,
hapo tukaona tuendelee kufanya kosa jingine dogo ili tuweze kufanikiwa,
tukatafuta mbinu za kidakitari ili huyu mama aonekane hajachanganyikiwa, …kuna
muda mama huyu yupo safi kabisa, mnaongea kama kawaida, lakini kuna muda
anakuwa kama sio yeye, unaweza ukahisi akajisingizia …
Kitendo cha mama huyo kuchukuliwa, kilimuathiri sana mkuu,
akawa anatuma ujumbe wa kauli kali, japokuwa haonyeshi kuwa ana uhusiano gani
na huyo mama, lakini ilionyesha wazi kuwa hakufurahishwa na hicho kitendo,
akatuma barua kwa wakuu akiwa huko huko hospitalini kuwaambia kuwa kama hawamuamini
basi wamuambie ….wakuu wakamwambia hilo litafanyiwa kazi , nia ya wakuu hao ni
kupoteza muda, ili sisi tuweze kufanikiwa na wao walishahisi kuna jambo, na
kikulacho kipo nguoni mwako, ila nani ni nani ilikuwa bado kitendawili.
Siku ile tukamfikisha mama mahakamani tukijua kuwa hapo
ataongea kila kitu na mahakama itachukua kauli yake kama ushahidi..na kweli siku
ile mahakamani akaongea mambo ambayo kidogo, yaliwafungua watu masikio hasa
hakimu na jpo lake, ndio maana hata tulipotaka kufanya mambo mengi, tukawa
tunapata ushirikiano wa kimahakama.
‘Siku ile huyo mama alipouwawa na bomu, niliumia sana
maana sisi ndio tuliomtoa huko alipokuwa na tukamfikisha hapo mahakamani
tukihakikishia usalama wake, bomu lile lilinivunja nguvu, nikajua kuwa sasa
tunapambana na jitu lisilojali, lipo tayari hata kuwaua wazee kama huyo…
Kutokana na ushahidi uliopatikana baadaye nia ya bomu
hilo ilikuwa sio kumuua huyo mama, halikukusudiwa kwake kabisa, ilikusudiwa
kuwa liniue mimi, maana mimi ndiye nilitakiwa niwe kwenye hilo gari la huyo mama
yeye ana gari lake hataki liguswe na mtu mwingine…kiusalama, tukapanga kuwa
baada ya kesi, mama huyo atachukuliwa na gari jingine,mimi nitatumia gari la
huyo mama, na pia tukitoka hapo mama huyo anapelekwa sehemu nyingine kiusalama.
Hawa watu wakitafuta njia za kunimaliza, wakaliweka hilo
bomu kwenye gari la mama, wakijua mimi ndiye nitalitumia, waliweka tukiwa
mahakamani, ujue kundi hilo kuna watu wao ndani ya watu wa usalama, kwahiyo
hata walipoingia ndani ya hilo gari, hakuna mtu aliyewashuku.
Bomu likawekwa kwenye hilo gari,..na ukumbuke kipindi
hicho mkuu wao wa mitandao alikuwa mikononi mwetu kwahiyo ule mtandao wao wa
mawasiliano kujua huyu yupo wapi, haukuwa unafanya kazi tena….
Mungu kama hakupanga kifo kitokee, hakitokei, na mama
kwa ubishi wake akasema hataki kuingia gari lolote zaidi ya gari lake..tukaona
haina haja kubishana naye, basi yeye na
walinzi wake anaowaamini wakaingia kwenye hilo gari, na bomu likawaua
wote,..kifo hiki kilimuumiza sana.
Kwa namna fulani, huyu jamaa japokuwa kwa namna fulani, kingemsaidia
kuondoa watu wote wanafahamu usiri wake, kwani mama alishaanza kuvujisha siri.
Mkuu akawa magonjwa kabisa siku ilipofikishiwa taarifa
hiyo, wanasema jamaa alizidiwa sana siku hiyo, japokuwa alikuwa jasiri. Lakini
hali ilibadilika ghafla, akapoteza fahamu.
Alipotulia na kuwa vyema, akaanza
kutulaumu sisi kuwa ndio tumechangia kifo cha huyo mama, na tunahitajika
kuwajibika kwa hilo…wakuu wakapelekewa taarifa, lakini wakuu walijua ni kitu
tunakifanya kauli ao ikawa ile ile kuwa wanalifanyia kazi.
Kwa ujumla makao makuu walishakosa imani na huyo mtu ,
lakini walikuwa hawana ushahidi na hawawezi kumuingilia kwani ni mtendaji wao
mkuu, anafahamika, ana sifa zote…., wakawa wanatuachia sisi tufanye kazi ili
tuweze kuonyesha kuwa jamaa huyo hafai au unahusika kwa namna moja au nyingine
na hilo kundi haramu, walihitaji ushahidi wenye nguvu…
Kama ilivyokuwa kwa wakosaji wote, kuwa za mwizi ni
arubaini, na kama ilivyosema kuhusu dhuluma, dhuluma haidumu…ikidumu
inaangamiza…, mwisho wa kundi hili ukafikia tamati,….mimi ndio nikakipata hicho
kifaa, chenye siri, niliamini kuwa kina siri kubwa sana, kwani huyo mama
marehemu kuna muda alitamka kitu kama hicho, kuna siku alisema ;
‘Mkitaka kujua siri ya mtoto wangu kuna kifaaa cha
komputa mkikipata mtajua kuwa mtoto wangu hajafa …’akasema
‘Hicho kifaa kipo wapi?’ nikamuuliza
‘Sijui, kama ningelijua,….ningelifurahi,…..’akasema na
ilitokea siku hiyo moja akaongea hivyo, ha hakuweza kuongea kauli hiyo tena,
hata tulipojaribu kumuhoji hadi anauwawa na hilo bomu.
‘Na niliposikia mkuu huyu akimuagiza nesi kuwa kuna
kifaa ninacho, nimekipeleka kwa fundi kifaa hicho ni muhimu sana kwake ,
nikajua kweli sasa tutagundua siri ambayo imejificha, …mara nesi akakiiba hicho
kifaa, akitaka kupata utajiri kwa huyu jamaaa.
Kipindi hicho mkuu alishatoroka hospitalini,
akijihami,..akikitafuta hicho kifaa,
akijua mwisho wake unakaribia,…nesi akaingia mkataba na huyo jamaa kuwa
atakitoa hicho kifaa kwa kupewa hisa na baadhi ya miradi ya huyo jamaa, nesi
akaona hilo ni kazi rahisi kwake, akaona hiyo ndio nafasi yake ya mwisho
kutajirika,.
Na kweli nesi akakipata hicho kifaa, na hakutaka
kuwapa polisi, kwani polisi hawana pesa, ndio akapanga mpango wa kukikabidhi
hicho kifaa kwa mtu mmoja ambaye alikuwa akitumika sana na hili kundi, kupelekea na
kutoa taarifa za mahabusu…
Mimi kwa Bahati nzuri nikawanasa wakati wanakabidhiana,
chombo kikapatikana na siri ikawa imefichuliwa , kwahiyo dunia yangu, ikafikia
tamati. Mashahidi waliotakiwa kuuwawa, yaani wataalamu baada ya tiba ya mganga wa tiba mbadala, wakawa na uwezo wa kuelezea kila kitu kuthibitisha hayo mbele ya hakimu, mzee mzima akazidi
kuchanganyikiwa.
Kiukweli kama angelifanikiwa kukipata hicho kifaa akakiharibu siri kubwa ya yeye ni nani ingelibakia kichwani mwake tu...lakini ya mungu mengi dhuluma haidumu, siri ikajulikana mbele ya mahakamani, na hapo ikawa mwisho wa dunia yangu
'Ama kuhusu hali ya mtuhumiwa huyo, alipoona kila kitu kipo wazi, alishindwa kuvumilia, akadondoka na kupoteza fahamu, na ana tatizo, kutokana na kuungua na moto wa lile bomu, uso wake umeharibika sana, ukimwangalia kwa sasa hayupo vizuri, kuna hali kama ya kuoza, docta aliyekuwa akimtibia anasema kuna dalili ya kansa, hebu fikiria kansa imejitokeza kwa muda mfupi tu...kwahiyo hatumuombei baya, ila adhabu mara nyingi zinaanzia humu humu duniani, ogopeni sana dhuluma
'Ni hayo
niliyotakiwa kuwaambia….ahsanteni sana.’
Moto akasema na kuanza kuondoka kuelekea kwenye gari
lake, lakini waandishi wakwa wanamzonga kwa maswali mengi hadi askari
waipoingilia kati.
‘Ni hayo ndiyo niliyotakiwa kuwaambia…..’ Moto akasema
na kuanza kuondoka kuelekea kwenye gari lake, lakini waandishi wakawa bado wanamzonga
kwa maswali mengi hadi askari walipoingilia kati.
‘Mengine suburini , mtayajua zaidi baada ya hukumu, cha
msingi ni kuwa dunia yangu imesambaratika, na muhusika mkuu
keshapatikana….’akasema Moto sasa akitembea kuondoka eneo lile akiwa anasindikizwa na askari
kuhakikisha hakuna mtu anayemsumbua tena, akaelekea kwenye gari lake kuondoka.
********
Tamati
Baada ya kumaliza kuongea na waandishi wahabari, Inspecta Moto, akatoka eneo hilo na kuelekea pale lilipokuwepo gari
lake, kila mmoja akimuangalia kama shujaa, yeye hakugeuka nyuma kuwaangalia
watu.
Akafungua mlango wa gari lake na kuingia ndani, lakini
kabla hajaondoa gari, akaona mdada akija kwa kasi, akiwapita askari kwa
kuwakwepa, huku akipunga mkono wake kama
kunisimamisha nisiondoke…askari wakamfuata kumzuia, Inspecta akafungua dirisha
la gari lake, kujua huyo mdada ni nani, mbona kama anamfahamu.
‘Hebu muachieni huyo mdada aje…’inspecta akawaambia
askari kwa sauti, na yule binti akasogea hadi pale kwenye gari na macho ya
Inspecta yakakutana na yule mdada, akamkumbuka,
akatabasamu, alikuwa yule binti wa mtaalamu wa tiba mbadala, akakumbuka fadhila
zao, akayakumbuka mawazo yake… akasema;
‘Vipi unahitaji lifti.....?’ akauliza akitamani huyo
binti asema ndio
‘Mhh,… lifti hapana,…sikuwa na nia ya kuomba lifti, ila
hawa askari wenu wamenikwaza unajua kukwazwa, ….basi ndio hivyo,
siwapendi,….mbona wana roho mbaya, hata kuingia ndani kusikiliza kesi
walinizuia, kwanini lakini….’akawa analalamika
‘Inabidi wafanye hivyo, maana watu ni wengi, na wengine
sio wastaarabu, wanaweza kuanzisha vurugu, …’akasema Moto
‘Sawa kama hata mimi sio mstaarabu, ….’akasema
akionyesha kuhuzunika
‘Sio kwamba na wewe upo hivyo, ningelijua ningewaambia
wakuruhusu , lakini wao watajuaje nani ni nani….usiwalaumu sana, hata wewe
ungekuwa kwenye kazi yao ungelifanya hivyo…’akasema Moto.
‘Najua kesi ya ngedere nimempelekea tumbili, tuyaache
hayo, …baba kanipigia simu kuwa anakuja kwako, nimemwambia upo kwenye kesi,
akasema ukitoka tu ni mwambie, maana anajiandaa kurudi kijijini, lakini hao
askari hawakutaka kunipa nafasi ya kukuona, na simu yako sijui imekuwaje, sijui
nilikosea namba, nikipiga inasema nimekosea...’akasema
‘Unasema baba yako eeh, anataka kuonana na mimi, kwa
kusalimia au kuna jambo jingine…..?’ akauliza Inspecta akiwa na wasiwasi.
‘Anasema ile sumu uliyowekewa mwilini inahitaji
kusafishwa kabisa, isije kukuletea madhara baadaye, kuna dawa kaja nazo, hataki
kurudi kijijini bila kuhakikisha kuwa wewe umezitumia, na awe na uhakika kuwa upo
salama...’akasema huyo binti.
‘Mhhh, ama kweli nyie ni watu wema sana, sijui kama
nitaweza kuwalipa wema wenu huo,, na hajaniambia gharama yake mpaka sasa,sijui
atanielewaje, lakini kwa vile mambo yamekwisha, nilizima nimlipe…’akasema Moto
‘Hahitaji umlipe chochote, sio kusudio lake,…yeye
anachotaka ni kukamilisha tiba yake tu…’akasema mdada.
‘Yah, hilo sio lazima aniambie mimi mwenyewe nafahamu
nifanye nini,….’akasema na kumuangalia yule binti kwa makini, akaona jinsi gani
anavyozidi kupendeza, kwa kipindi kifupi keshanawiri, akajikuta akitabasamu,
akasema;
‘Kuna kitu,nataka kwanza niongee na wewe , halafu
baadaye nitaongea na baba yako, ni muhimu sana, kwa vile nimekuona hapa, naona nisipoteze
muda huo, ....ingia ndani ya gari twende…’akasema
‘Hapana….’akasema Binti
‘Tafadhali, kuna kitu nataka kuongea na wewe kama
hutojali...’akasema na yule binti kwanza akasita kuingia akainua uso
kuwaangalia watu, sijui alikuwa akiwaza nini, na Inspecta akasema;
‘Vipi tena, mbona unasita kuingia kuna sehemu unakwenda
au kuna mtu anakusubiria, ingia tu usiwe na wasiwasi, na kwa vile baba yako
yupo kwangu, itakuwa vyema, nikaongea na yeye pia, au…?’akasema Moto akiangalia
watu kama kuna mtu anayemsubiria huyo binti.
Yule binti akafungua mlango wa gari na kuingia ndani ya
hilo gari, akiwa na aibu nyingi usoni..
‘Kitu gani unataka kuongea na mimi…unajua baba yeye
anasema anahitaji kukuonyesha kuwa yeye hafanyi kazi yake kwa pesa, kwani watu
walivumisha kuwa alirubuniwa na hao watu wabaya kwa kuthamini pesa kumbe sio
kweli….’akasema
‘Najua ….mimi nafahamu fika kuwa baba yako ni mtu mwema
tu, hilo wala lisikusumbue kichwa na hata baba yako nitaongea naye wala asiwe
na wasiwasi, yeye ni mtu mwema sana…’akasema Moto.
‘Ndio hivyo, ila kiukweli kuna muda anakwama, kuna muda
baba anakuwa hana pesa kabisa hata hivyo haachi kuwasaidia watu…watu bado
wanahitaji huduma zake, anajitolea bure, na wengine wana uwezo, lakini ile hali
ya kufikiria kuwa mzee huyu kawaisaidia na wao wamsaidia chochote, hawafikirii
hivyo, kazi ni kumsfia tu…’akasema
‘Kwanini asifungue kitu kama kliniki akajisajili, akawa analipwa tu…unajua watu wengine hawawezi
kujituma, wanapenda bure tu, na hawajali wewe mtoaji unaumia vipi, umetumia
gharama kiasi gani hilo hawalijui, na ni wepesi kusfikia, na hata kukashifu
pia….’akasema Moto.
‘Hilo la kufungua kilikini na kujisajili, ….mmh baba
hataki,…anasema hataki usumbufu kwani nia yake ni kusaidia, sio
kujitangaza..hataki hata kusikia mambo hayo, yeye anasema kapewa kipaji na
mungu, cha kusaidia watu hilo kwake linatosha…ni kama wewe unavojituma kwenye
kazi yako…’akatulia
‘Kwenye kazi yako, hufanyi tu kwa vile unalipwa
mashahara, sizani kama mshahara unaopata unalingana na kazi unayofanya, wenyewe
wataishia kukusifia tu, ukirudi nyumbani kama una watoto, hawawezi kushiba hizo
sifa….angalia kazi uliyofanya, ulijiweka hatarini, mpaka mke wako kauwawa…ni wito tu, kuna nini
utapata hapo, sifa…hahaha, sifa zinashibisha, sifa zitakuondolea machungu,
nikujitolewa tu, tenda wema uende zako…’akasema binti, na Inspecta akawa
anawaza jinsi gani bintu huyu alivyo na hekima.
‘Kweli …hilo ni
jukumu la kila mmoja wetu kwa nafasi yake…unajua baada ya kufa mke wangu,
sikutaka kabisa kuoa,..lakini kila mara nawaza, je ni sahihi kufanya hivyo,
nahitaji familia, nahitaji watoto…ili waje kuendeleza kizazi chetu, japokuwa
nilimpenda sana mke wangu, lakini keshaondoka, keshatangulia mbele ya haki, na
sote ndio njia yetu, sasa niombeleze mpaka lini,…nahisi nitakuwa nakufuru, sina
jinsi..’akasema Moto akionyesha kusononeka.
‘Pole sana, …wewe ni mume bora, na mke wako alipata
Bahati sana kuwa na wewe, japokuwa mitihani ilimpitia,lakini yote ndiyo
kidunia, yote yameumbiwa sisi wanadamu, najua huko alipo keshaingia peponi,
kwani alishindw kuvumilia, aliona akizidi kuwepo atazidi kuingia kwenye
madhambi, mungu amsamehe makosa yake…ila sasa wewe ni muhimu utafute mwenzako
…’akasema huyo bonti akimtupia jicho la aibu
‘Ni kweli kwa hali hii, nilizoea nikirudi nyumbani kuna
mtu wa kunipokea, tunasaidiana kazi,…yani wakati mwingine naogopa hata kuingia
chumbani, …kwakweli sijui, nimemkosa mtu niliyempenda sana…mmh….’akatulia
kidogo halafu akasema
‘Unajua mke na mume kuna siri kubwa sana, mnahangaika,
lakini mwishowe mnatakiwa kupumzika, mkiwa wawili mnakuwa kwenye dunia
nyingine, mambo ya kazi, mataizo mauzi ya dunia yote mnayasahau,mmmh, sasa leo
mwenzangu hayupo, inanipa shida sana, najihisi mpweke , na kuna muda namuota
mke wangu akiniambia nitafute mke ili roho yake iwe na amani..hebu fikiria
anafikia hata kunipigia magoti kuwa nitafute mke…..’akasema
‘Anakuambia hivyo kwenye ndoto, sasa kwanini huoi, hujui
unamtesa mwenzako….?’ akauliza binti akionyesha kama hamasa fulani.
‘Tatizo sio kuoa, tatio ni nani wa kuoa, mtu ambaye
kweli ataweza kuziba pengo la mke wangu, naogopa kuja kuumia, naogopa mitihani
hii ya maisha, nimeshaumwa na nyoka, naogopa hata unyasi, lakini……’akasema Moto na kugeuka kumuangalia huyo binti.
‘Mhh, ni uamuzi wako lakini,… ila kama umemuota mke wako
anakushauri hivyo, na anasema roho yake inataabika kwa vile hujaoa, ni vyema
uoe, ndoto nyingine ni ishara anakupa ujumbe na ukiutimiza, atakujia akiwa
amefrahia, na huenda hilo linampa adhabu, na kuoa kwako kutafanya awe kwenye
heri, nakushauri kama kaka yangu tafuta mke uoe……’akasema huyo binti na
kutulia.
‘Unajua kila nikikuangalia namuona mke wangu, ni kama
vile nyie ni ndugu, umefanana sana na mke wangu…isingelikuwa mnatoka mikoa
tofauti ningelisema nyie ni ndugu….’akasema Moto na huyo binti akamuangalia
Moto, na macho yao yakakutana, kuna hali iliwatokea wote, na binti akakwepesha
macho yake na kuangalia nje kwa kupitia dirishani akasema;
‘Binadamu hufanana…imetokea tu, mimi na yeye tukafanana,
kama unavyodai wewe, japokuwa mimi sioni kama tumefanana naye…na hata nikimuangalia
yeye ni mzuri sana, sizani kama mimi ni mnzuri kama alivyokuwa mke wako, ile
picha yake niliyoiona, nimemuona alivyokuwa mrembo,…’akasema huyo binti
akishusha sauti kama vile aliongea kitu kisichostahili.
‘Kiukweli mnafana kila kitu uzuri, tabia, unavyoongea,
na hata kila nikimuota mke wangu mwishoni nakuona wewe, mpaka najiuliza kuna
nini hapa…..’akasema
‘Hiyo ni kwamba, unahitajika upate mwenzako, tafuta mke
mimi nitafurahia kama ukiwa na wifi, nafika nyumbani siogopi, najua nitamkuta
wifi, lakini ukiwa hivyo peke yako naogopa kuja, midomo ya watu itabwabwaja
ovyo,…’akasema Binti.
‘Hahaha, wewe unahitajia wifi, kwanini wifi, kwanini
usiseme dada, au …..kiujumla ni kweli kwa hali ilivyo na mimi sasa naona …ooh,
ni kweli nahitaji mtu…wa kunisaidia majukumu,….’akasema Moto
‘Majukumu!?, ina maana unahitaji mfanyakazi wa ndani,
mimi nilijua unahitajia mke..?’ akauliza huyo binti
‘Hapana, sihitaji mfanyakazi wa ndani, nahitaji
mwenzangu,akiwepo majukumu tunasaidiana, au sio ...na mtu ambaye naona anaweza
kuziba pengo la mke wangu, mmh, hayupo
mbali, ….’akatulia na muda huo alikuwa kaangalia mbele, hakuwa amemuangalia
huyo binti, ila binti alikuwa akimuangalia yeye.
‘Kumbe umeshampata mtu mwenyewe tayari, kwanini sasa
unazunguka, sema harusi ni lini , mimi nitafurahia kweli nikimpata wifi yangu
niwe nafika kumtembelea…’akasema Binti kwa sauti ya kinyonge.
‘Mhh, kiukweli sijawahi kumwambia, ila amekuwa akilini
mwangu….’akasema
‘Na wewe bwana, mimi nijuavyo askari ni watu majasiri
sana, hawaogopi kufanya jambo, sasa kwanini hujamwambia, unaogopa nini,….?’
Akauliza binti, kwa sauti ile ile a kingonge, na akaongezea kwa kusema;
‘Au huna uhakika, humpendi….?’ Akauliza binti sasa
akimtupia jicho la siri Inspecta.
‘Inafikia maswala kama haya, hakuna cha uaskari, au
nani, …ni hulka ya kibinadamu, kwani hujui mwenzako anawaza nini….na kila jambp
lina muda wake, na ndio maana nikataka tuongee mimi na wewe kwanza..’akasema
‘Hahaha, usinichekeshe, mimi bado mdogo, siwezi kwenda
kukuelezea kwa huyo mtu, nitaanzaje, hapana, mimi iswezi, labda ingeikuwa
shangazi yangu, au…’akatulia
‘Binti naomba unielewe,….kama nilivyokuambia wewe
unafanana sana na mke wangu, kwahiyo nimeona ...lakini kama upo radhi, nakuomba
wewe ukubali uwe mke wangu....’akasema Moto na kugeuka kumuangalia yule binti,
na macho yao sasa yakawa yamekutana, binti akapandisha mkono na kushika
mdomoni, mdomo ukafunguka kwa mshangao, na kusema;
‘Khaaah, eti nini....mmh, mimi niwe mke wako, mmmh,
najua unanitania…najua utampata mwenzako tu anayekufaa…sizani mimi nastahili kuwa
mke wako…’akasema yule binti kwa mshangao, huku sasa akiianama chini kwa aibu.
‘Sikutanii Binti,…..nataka wewe uwe mke wangu, kama upo
tayari, na kama kweli unanipenda, maana maswala ya kuoana kitu kikubwa ni
upendo na upendo uwe wa dhati, kutoka moyoni,…sio tu kwasababu unataka au
ninataka kukuoa, niambie ukweli kama upo tayari, mimi sitaki kuchelewesha, nitaongea
na baba yako…’akasema Moto
‘Kama
nilivyokuambia wewe unafanana sana na mke wangu, nikimuota mke wangu, nakuona
wewe, … kwahiyo nimeona kuwa wewe unafaa kuziba pengp la mke wangu,..’akasema
Moto sasa akiwa kasimamisha gari.
‘Mhh, mbona unahitaji jibwa kwa haraka hivyo, unajua
umeni…mmh, hata siwezi kusema..’akasema Binti.
‘Nikuulize swali wewe unanipenda, upo radhi kuwa na
mimi..sitaki kukulazimisha, kama una mtu wako mwingine, niambie ukweli, kama
unaona sikufai, uniambie ukweli…sitaki kuja uje ujute au nije kupata matatizo
mbeleni, yaliyopita kwangu na makubwa, sasa hivi nahitaji faraja, …’akasema
moto na yule binti alikwa kama kapigwa na shoti ya umeme, alikuwa katulia
kimiya, huku akainama.
‘Nahisi unanitania..siamini….’akasema
‘Sikutanii…..nakuomba unikubalie uwe mke wangu, kama upo
tayari, na unanipenda, maana maswala ya kuoana kitu kikubwa ni upendo na upendo
uwe wa dhati, na sihitaji maswala ya mlolongo, sijui uchumba….hapana, kama upo
tayari, mimi sitaki kuchelewesha, nitaongea na baba yako, tufunge ndoa haraka
iwezekanavyo…’akasema Moto
‘Mhhh, …ni kama ndoto, siamini. Ahsante mungu, mmmh,
sina hata la kusema, zaidi ya kukuambia nakupenda, nilikupenda toka siku ile
ukiwa mgonjwa, nipo tayari niwe mke
wako, uwe mume wangu…..’akasema binti.
MWISHO.
********************************************************************
Nawashukuruni nyote
mliokuwa nami kwenye kisa hiki, na kama kuna lolote, maoni, tumeni kwa email
address ya mtandao: mira.com@gmail.com.
Kumbekeni mwisho wa kisa
hiki ndio mwanzo wa kisa kingine,
Na kama nimewachosha kusubiria
hitimisho, samahanini sana…kuna mambo yalikuw juu ya uwezo wangu, na kama ni
kisa kizuri umekifurahia, basi nashukuru, `like ‘ sana kwenye facebook, au
ingia ndani ya diary yangu, toa neno la shukurani. Zaidi sina, tupo pamoja,
tumuombe mungu atupe wasaa, afya tuweze kuanza kisa kingine.
TUPO PAMOJA
**************************
WAZO
LA LEO: Unapodhuluma, mali ya umma, mali ya watu, jasho la watu, ujue
umedhulumu vizazi na vizazi vya jamii, na kwa kudhulumu huko , ujue pia wewe
umsababisha hata vifo vya jamii hiyo,….angalia watu wanavyoteseka, masikini wasiojiweza,
wagonjwa wanakosa dawa, yote ni kutokana na dhuluma zako.
Ukumbuke pesa na mali
hiyo ya umma uliyodhulumu, ingelisaidia kununua madawa, kutoa huduma mbali mbali za kijamii, lakini wewe ukaamua kujali tumbo lako. ukajitajirisha....ni kweli, utashiba utatajirika, lakini ukumbuke, mwili wako utakuwa unanuka dhambi.
Kama una moyo wa imani
unamjua mungu kuwa yupo, basi kumbuka kuwa yote ni mapito, yalikwepo na
yatakuwepo, umeyakuta na utayaacha, wangapi wangapi walidhulumu, sasa wapo
wapi, siku itafika na wewe utarejea kwa mola wako mjuzi mwenye hekima,
anayefahamu kila kitu, atakuhukumu kwa dhuluma zako hizo, hakuna pa kujificha…kumbuka, kila mtu ataubeba mzigo
wake mwenyewe, muhimu, tubia, acha kula mali ya dhuluma, kama umedhulumu, umechukua mali ya umma, rejesha mali hiyo kwa wenyewe.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Keep it up, y'a number one
Post a Comment