Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, June 20, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-80


Haya tuje kwenye kesi yetu moja kwa moja, ni kwanini huyu mtoza ushuru aliuwawa, na aliuliwa na nani na kundi au...?’

‘Kabla sijajibu swali lako, kwanza ni vyema tukamtambua huyu marehemu, mtoza ushuru, alikuwa nani hadi kifo chake

‘Marehemu ni vijana wa mwanzo walioandaliwa na hilo kundi, na alipewa hiyo kazi mwanzoni kabisa, na hadi anafariki, alikuwa ameshafikia kiwango cha u-mwenzetu,...U-mwenzetu ni kiwango cha juu katika kundi, wana vyeo vyao wenyewe, na hadi anafariki, alishafikia hatua hiyo na akawa anaandaliwa kupewa cheo kikubwa...’

‘Huenda cheo hicho ndicho chanzo cha kifo chake, kwasababu migogoro ndani ya kundi, ilianzia ipindi hicho, wakati wanataka kumpata kiongozi muwakilishi wa kundi kwa hapa nchini, ukumbuke kundo hilo sasa ni la kimataifa,...’akasema

‘Katika kugombea vyeo, kila mtu akimtaa mtu wake,kukatokea mgongani, wenyewe kwa wenyewe wakaanza kupigana vita, na marehemu akaanza kushutumiwa kwa makosa mbali mbali, makosa ambayo hata wao wenyewe walikuwa nayo, lakini kwa mtizamo tofauti marehemu akaonekana kuwa anajijali mwenyewe, na hata baadaye kufikia kumshuku kuwa anasaliti kundi..na hi ilitokea kipindi akiwa na mahusiano na mdada...’akasema.....

Tuendelee na kisa chetu

                 ******
Ni wakati wakili mtetezi anataka kuanza kuuliza maswali , na ndipo kukatokea kitu muelekeo wa mlangoni, na hapo, kukatokea kama sauti ya watu kuhangaika, na kuanza kugeuka kuangalia muelekeo wa mlangoni...

Watu wote waligeuka kuangalia kule mlangoni,na hata mimi nikageuka kuangalia, na hakimu naye halikadhalika akawa anafanya hivyo hivyo, nikajiuliza kuna nini, ...na mimi nikageuka, lakini sikuona cha ajabu huenda aliyekuwa akiangaliwa alikuwa ameshapita, nikazidi kuangalia kama nitamuona aliyeingia au kitu gani cha ajabu lakini sikuweza kabisa kumuona,au kuona tukio lolote la ajabu,..

Watu sasa wakawa wananong’onezana hata yule ambaye hata hakuwahi kuona hicho kichotokea huko muelekeo wa mlangoni, naye akawa na lake jambo, ilimradi mdomo ufunguke, na mnongono wa watu wengi hugeuka kuwa ngurumo, na mimi nafsini nikawa najiuliza kuna nini, kumetokea jambo gani..lakini sikupata jibu

‘Utulivu, tunataka utulivu...’akasema hakimu akigonga kirungu chake mezani

‘Wakili mtetezi unaweza kuendelea kumuuliza shahidi maswali…’akasema hakimu, na wakili mtetezi akiwa kama kapigwa na butwaa, kwanza akatulia kama anawaza jambo na bado akiwa anaangalia muelekeo ule wa mlangoni, na baadaye akamgeukia hakimu na kusema;

‘Samahani sana Muheshimiwa hakimu, kwa sasa sina maswali, na hata wenzangu, hawana maswali kwa sasa, nilitaka kuliweka hili wazi tu muheshimiwa…’akasema na hakimu alionyesha mshangao, na alitaka kusema kitu lakini akawa kama anafikiria jambo, baadaye akamgeukia wakili muendesha mashitaka na kusema;

‘Wakili muendesha mashitaka unaweza kuendelea na mtu wako, maana naona upande wa utetezi wanaonekana kukosa maswali ya kuuliza, sijui ni kuelewa au bado wanatafakari,..tuendelee muendesha mashitaka ,maana naona muda hautusubiri...’

Wakili muendesha mashitaka naye akiwa kama haamini, maana alijua kunaweza kutokea maswali mengi upande wa utetezi, lakini aliona ajabu kwa watu hao kuwa kimiya, naye akageuka upande ule wa muelekeo wa mlangoni, akawa kama anaangalia jambo, huku uso wake ukimemeta kwa tabasamu, tofauti na uso wa wakili mtetezi, aliyekuweo hapo muda mfupi, wakili huyu akasema;

‘Ukweli umedhihiri muheshimiwa hakimu, ndio maana wenzetu wameshindwa hata kuuliza swali moja, sisi tunachotaka hapa ni haki itendeke....’akasema huku akiangalai upande ule wa utetezi, halafu akamgeukiwa shahidi wake, na kusema;

‘Sasa tutaendelea na shahidi wetu, tukumbuke kuwa huyu ni mtaalamu, kwahiyo yote anayoyaongea hapa kayafanyia kazi na tafiti yakinifu, na kila jambo lina ushahidi wake, hatuongea kwa maneno tu, tutakuja kuonyesha shahidi zote na mashahidi wengine kuthibitisha haya wapo,....’akasema na kuangalia kule muelekeo wa mlangoni, huku akitabasamu, na baadaye akamgeukiwa mpelelezi na kusema;

‘Shahidi wetu, mpelelezi, mtaalamu,  sasa ni wakati wa kutuelezea jinsi mtoza ushuru alivyouwawa kutokana na uchunguzi wako na jinsi kifo chake kinavyohusiana na hilo kundi….’akasema muendesha mashitaka

‘Kwanza hebu tueleze siku ile ya tukio , siku ile ambayo mtoza ushuru aliuwawa, wewe ulikuwa wapi?’ akaulizwa

‘Siku ile ya tukio, siku ambayo mtoza ushuru aliuwawa, mimi nilikuwepo hapo hapo kwenye eneo la nyumba ya mdada...’akasema na watu wakaguna, na kuanza kunongong’ona, na hata hakimu naye akaonyesha uso wa mshangao na kuuliza hilo swali tena

‘Ina maana ulikuwepo eneo hilo, kwa ndani au kwa nje...?’ hakimu akauliza hilo swali akiwa kama hajaelewa na alionyesha kushangaa kidogo.

‘Nilikuwepo ndani ya eneo la hiyo nyumba, yaani nilishaingia getini na kuwa kwenye sehemu ya nje ya nyumba, lakini sio ndani ya jengo la nyumba yenyewe,....’akasema shahidi

‘Ukisema ndani ya eneo, ina maana ni kwenye viwanja, inawezekana ni sehemu ya bustani, au sehemu yoyote ya nje, lakini sio ndani ya nyumba wanapoishi watu au sio?’ akauliza muendesha mahistaka

‘Ndio hivyo muheshimiwa,....’akasema

‘Ehe, hebu sasa endelea na maelezo yako sitaki kukuongoza natumai unajua jinsi gani ya 
kuyaweka maelezo yako sawa ili yaeleweke kwa muheshimiwa hakimu na mbele ya mahakama hii tukufu...’akasema wakili muendesha mashitaka.

‘Siku hiyo mimi nilikuwa na ahadi ya kukutana na mdada, ni ahadi isiyo rasimi, yaani yeye hakuwa na taarifa ya ujio wangu, na nilipofika karibu na eneo la makazi yake,nikaona kuna mishughuliko isiyo ya kawaida, baadaye niliona gari likija na mtu mmoja akatoka ndani ya gari, mtu huyo alikwenda kuongea na mlinzi....’akatulia kidogo

‘Mimi nikajongea hadi eneo la getini, nikawa nawaona mlinzi na huyo mtu wakiongea, na kwa muda huo gari alililokuja nalo huyo mtu lilishaondoka, mimi nikapata nafasi ya kuweza kusogea zaidi na niliona geti likiwa nusu wazi, na muda huo mlinzi akatoka kwenye lindo lake, na kumuacha yule mtu aliyefika hapo kwenye lindo...’akasema

‘Alitoka kwenye lindo kwa vipi, kutoka nje, au kuelekea wapi?’ akaulizwa

‘Alitoka kwenye kibanda chake cha ulinzi na kuelekea kwenye nyumba, na kumuacha yule mtu akiwa kasimama nje ya hicho kibanda cha huyo mlinzi,alikuwa kasimama kwa nje ya hicho kibanda huku akiwa anaongea na simu ya mkononi...’akasema

‘Nilimchunguza yule mtu kwa haraka nikagundua kuwa kwa muda huo huyo mtu mawazo yake yalionekana kumuangalia zaidi yule mlinzi, na huku anaongea na simu...’akatulia

‘Na kwa akili za kawaida, mtu huyu asingeliweza kuwa makini na kitu kinachotokea nyuma yake, na hapo mimi nikautumia hiyo nafasi, nikasukuma mlango wa pale getini , na kwa mwendo wa haraka wa kujificha, nikaambaa-ambaa, sambamba na michongoma, kuelekea sehemu ya maegesho ya magari, bila ya huyo mtu kuniona...’akasema

‘Na wakati huo mlinzi alikuwa ameshafika maeneo ya maegesho ya magari, hakuelekea mlangoni kama nilivyohisi , kuwa labda alitumwa ndani na huyo mtu,kuongea na bosi wake, lakini cha ajabu huyo mlinzi akaelekea maeneo ya maegesho ya magari, na kwa haraka akaingia kwenye gari la madada, na kwa muda huo mimi nilikuwa nimeshafika maeneo yale kwa kujificha, nikatulia sehemu huku nikiwa na simu yangu nikichukua matukio yote hayo...

‘Nilimuona akiingia kwenye gari la mdada, na hakukaa sana akatoka kwenye gari hilo akiwa kashika Nyundo mkononi...’alipotaja nyundo watu wakaguna, na hata hakimu akawa anaandika kitu huku akipitia pitia makabrasha yake...

‘Ilikuwa ni nyundo na pisipisi, akaelekea sehemu ya dirisha la nyuma, ...nilikuwa na nilijitahidi sana kuchukua matukio hayo kwenye simu yangu mkononi ambayo ina nguvu ya hali ya juu kuchukua matukio, kwahiyo hayo yote ninayoyaongea hapa yapo kwenye vielelezo vya ushahidi kama mnataka kuyaona kama ushahidi...’akasema

Wakili muendesha mashitaka akasogea na kuinua juu mfuko uliokuwa na kanda za video, na kusema

‘Ushahidi wote upo hapa....hamna shaka...’akasema

‘Endelea mtaalamu wetu...’akasema muendesha mashitaka

‘Kwahiyo mlinzi alipochukua nyundo na ile pisipisi, akatembea hadi kwenye dirisha la nyumba ya mdada, na nikamuona akitoa ile pisipisi akatumbukiza kwenye kona za dirisha na kuanza kufanya jambo, kumbe alikuwa akipachua dirisha, kwani baadaye niliona akilisukuma kwa mkono likafunguka na kwa haraka akaingia ndani kwa kupitia dirishani....’akasema na muendesha mashitaka akasema;

‘Hadi hapo tumeelewa, kuwa mlinzi aliingia ndani kwa kupitia dirishani sio mlangoni kama ilivyoelezewa awali, je wenzetu upande wa utetezi mna swali, ....?’ akauliza na upande ule ulikuwa kimiya

‘Sasa nikuulize mpelelezi, kabla hujaendelea nataka hili liwe wazi, wewe ulimuona mlinzi akiingia ndani kwa kupitia dirishani na je ulimuona wakati anatoka?’ akauliza

‘Ndio nilimuona wakati anatoka...’akasema

‘Wakati anaingia alikuwaje na wakati anatoka alitokaje...?’ akaulizwa

‘Wakati anaingia alikuwa hakuvaa gloves mikononi, yaani kinga za kuzuia alama za mikononi, ila wakati anatoka alikuwa amevalia hizo kinga za mikononi na akiwa kashikilia ile nyundo, pisipisi na mfuko wa bahasha kubwa, nahisi ndani kulikuwa na kitu...’akasema.
‘Bahasha hiyo ni kubwa, na ilionekana kuwa na vitu ndani yake, ni kubwa za kuweza kuweka faili hizo kubwa za kiofisi...mkiangalia kwenye hizo kanda, mtaona vyema...’akasema
‘Yule mlinzi alipotoka alitoka kwa haraka sana na kukimbilia muelekeo wa kuelekea huko getini....’akasema

‘Una uhakika kuwa kweli alielekea getini?’ akaulizwa

‘Nina uhakika maana nilitoka pale nilipojificha na kuangalia upande wa maelekeo huo japokuwa sikuweza kuona vyema kwa mbele,lakini kwa jinsi alivyokimbia alionekena kuelekea huko...’akasema.

‘Haya hebu tuambie wakati upo hapo nje, uliona nini kingine au kusikia kitu gani kingine?’ akaulizwa

‘Nilisikia mlio wa risasi...lakini haukuwa na nguvu sana, kwasababu ukiwa nje, huwezi kusikia sauti ya kutoka ndani kwa ukamlifu wake, na mimi nilitambua moja kwa moja kuwa huo ni mlio wa bastola, kwa vile nina uzoefu na vitu hivyo,lakini kwa mtu asiye na uzoefu wa milio kama hiyo asingeliweza kugundua hilo....’akasema

‘Ulifanya nini, uliposikia hivyo?’ nikamuuliza

‘Hakukuwa na muda wa kufanya lolote, zaidi ya kutafuta njia za kuondoka hapo kwani kwa muda huo mfupi polisi walishafika,...polisi walifika muda ule ule wakati mtu mmoja niliyemuona akitokea ndani akiwa anakuja muelekeo wa pale nilipokuwa nimejificha.

Mimi niliona kuendelea kukaa pale nistashindwa kuendelea na uchunguzi wangu ambao sikutaka kuingiliwa na polisi,...nilichofanya ni kutafuta njia ya kutoka ndio nikamuona yule mtu yupo mikononi mwa polisi, na muda huo nilishafika maeneo ya getini ...’akasema

‘Huyu uliyemuona akiwa mikononi mwa polisi ni nani, ni yule wa mwanzo au ni huyu aliyetokea ndani?’ akauliza

 ‘Ni huyu wa pili...’akasema

‘Okey, huyo wa mwanzo tutakuja kumuongelea baadaye, nataka kumjua huyu wa pili ni nani?’ akauliza

‘Huyu wa pili ni mhasibu,....’akasema na watu wakaguna na kuanza kunong’ona...hadi hakimu akasema

‘Utulivu....endelea na maelezo yako’ akasema hakimu

‘Huyu mtu alivyotoka mimi sikumuona kuwa ametokea wapi, ila alikuwa anakimbia kuja muelekeo huo wa maegesho ya magari, nilimuona wakati anakaribia maeneo hayo ndio polisi wakamuona maana muda huo polisi walishafika, na hapo hapo mimi nikatafuta muelekeo wa kutoka nje, sikutaka kukutana na askari polisi kwa muda huo.

‘Huyu mtu ulivyomuona kwa muda huo mfupi kabla hajaingia mikononi mwa polisi, alikuwa vipi, na je hukuona mtu mwingine aliyekuwa na ndevu..akitokea ndani kwa muda wote uliokuwepo hapo?’ akaulizwa

‘Huyu mtu aliyetokea ndani alikuwa na wasiwasi sana, na kitu nilichokigundua ni kuwa alikuwa akijipangusa kwenye kidevu,na ghafla akavamiwa na maaskari, akanyosha mikono juu na huku akionyesha kwa mikono kwa wasiwasi kuelekea mlangoni, lakini polisi hawakumpa muda wakawa wamemshika na kumuweka pingu.

‘Na muda huo nilikuwa nimeshapata upenyo nikawa sambamba na mlinzi,na mlinzi aliniona lakini yeye alijua kuwa mimi ni sehemu ya maaskari waliofika hapo,  mimi nikamnyoshea mkono kama kumsalimia, nikamsogelea na kumuuliza

‘Kumetokea nini hasa?’ nikamuuliza

‘Kumetokea kitu kama mlio wa bastola...ni, bastola, kimetokea huko ndani,  ndio polisi wameshafika, nashangaa kwa jinsi walivyofika kwa haraka , sijui zaidi...’akasema

‘Wakati wanafika wewe ulikuwa hapa getini?’ nikamuuliza na yeye akaniangalia kwa wasiwasi, halafu akasema

‘Nilikuwa nimekwenda kujisaidia na wakati narudi, ndio nikasikia huo mlio na polisi wakaanza kuingia....’akasema

‘Kwahiyo wakati wanaingia hukuwepo kwenye lindi lako...?’ nikamuuliza

‘Ndio.nilikwenda kujisaidia....’akasema sasa akionyesha wasiwasi uliodhahiri.

‘Na mwenzako kaenda wapi?’ nikamuuliza

‘Mwenzangu!, Mwenzangu gani, mimi nipo peke yangu....’akasema akionyesha kushangaa, huku akiniangalia kwa wasiwasi, na hapo nikapata picha kuwa mlinzi hataki huyo mtu mwingine aliyekuwepo hapo afahamike,...’akasema shahidi na wakili muendesha mashitaka akaingilia na kuuliza

‘Je wakati unatoka , ukitafuta upenyo wa kutoka nje, hukumuona huyo mtu mwingine aliyekuwa kaachwa hapo getini?’ akaulizwa

‘Sikumuona kabisa, inaonekana huyo mtu aliondoka haraka na mapema sana, na hata ile bahasha aliyokuwa nayo mlinzi sikuweza kuiona popote maana niliingia ndani na kuanza kufanya upekuzi sikuona kitu, kwahiyo hiyo bahasha ndicho alichokuwa kakifuata huyo mtu mwingine,alipokipata aliondoka...’akasema mpelelezi.

‘Na wakati unasikia mlio wa risasi ulikuwa bado sehemu ya nyuma, kwahiyo hukuona mtu mwingine yoyote akitoka?’ akaulizwa

‘Kwa muda huo hadi mlio wa risasi unasikika, nilikuwa upande wa nyuma, sehemu ya uficho ambayo huwezi kuona mbele ya nyumba hiyo, kwahiyo kwa huko mbele kama kulitoka au kuingia mtu nisingeliweza kuona, na hadi mlio wa risasi unasikika, bado nilikuwa sehemu ile ile, ila nilishaanza kusogea sehemu ninayoweza kuona kule dirishani alipoingilia huyo mlinzi.

‘Mlinzi alipotoka alionekana vipi?’ akaulizwa

‘Alionekana mwingi wa wasiwasi, nilimuona akihangaika hata kufunga dirisha ilikuwa ni kwa kuhangaika sana alionekana kutetemeka, hadi kuangisha ile pisipisi, ambayo hakukumbuka hata kuiokota, mimi niliwahi kuikota, ...’

‘Kwahiyo mlio wa risasi ulisikika mlinzi akiwa ndani ya hilo jengo?’ akaulizwa

‘Ndio alikuwa bado yupo ndani ya hilo jengo...’akasema

‘Na hukuona mtu mwingine kutoka zaidi ya mlinzi aliyetokea dirishani na mhasibu aliyetoka na kukamatwa na askari, je huyu mhasibu alitoka baada ya risasi au kabla ya mlio wa risasi kwa jinsi ulivyoona...’akaulizwa

‘Huyu mhasibu muda anatoka na ndio mlio unatokea....sizani kama alikuwa ndani, haingewezekana, ni muda anatoka, na mlio unasikika, nasema sizani, maana huyu mtu nilimuona akija muelekea wa maegesho muda mfupi sana baada ya huo mlio, ...’akasema

‘Haiwezekani kuwa alikuwa ndani wakati mlio unatokea na ndio akakimbia?’ akaulizwa

‘Hapana haiwezekani, ..kwa mpangilio wa muda, ni lazima mlio ulitokea wakati anatoka ukiangalia maheabu ya muda....’akasema

‘Na kule getini, ulisema kuliachwa mtu, je wewe wakati unatoka,hukumuona huyo mtu..?’ akaulizwa hilo swali tena

‘Sikumuona huyo mtu tena,..walikuwa wameshafika maaskari, ni muda mfupi sana,hao maaskari walifika mapema sana, ni kama vile walikuwa hapo nje wakisubiria tukio..’akasema mpelelezi

‘Sasa hebu tuambie kuhusu huyu mtu wa kwanza, huyu mtu uliyemuona akiongea na mlinzi akaachiwa ulinzi hebu tumfahamu alivyo, kabla hujatuambia jinsi gani kifo cha mtoza ushuru kinavyohusiana na hili kundi, je huyu mtu wa kwanza uliyemuacha getini ni nani,alionekana vipi?’ akaulizwa, na mara kukatokea ghasia upande wa nyuma, ilionekana kuna mtu alikuwa kaingia, na kusukuma watu...

‘Utulivu, kuna nini hapo maeneo ya mlangoni, ...walinzi hebu hakikisheni utulivu upo...’akasema hakimu na kukaonekana bado kuna mtu anataka kupita mbele, na walinzi sasa wakawa wanawaondoa watu ili kupatikane njia....

NB: Kuna nini zaidi, tuzidi kuwepo sehemu ijayo?

WAZO LA LEO:Ustaarabu wa mtu huonekana katika kauli na mateno. Kauli inaweza ikamfanya mtu aonekane jinsi alivyo...kwa,jisni gani anavyoweza kuongea na watu mbali mbali, wakubwa na wadogo, au jinsi gani anavyoweza kuelekeza jambo, au jinsi gani unavyoweza kutoa hoja mbele za watu.

Kuna watu hawana huo ustaarabu, hawajui waongee kauli gani kwa wakati gani, au waonyeshe adabu gani kwa watu wa iana gani. Ni muhimu sana watu tukajichunga kwa tabia hizi kwani vitu vidogo vidogo kama hivi vinaweza kusababisha mzozano, chuki, na hata maumivu kwa watu wengine, kwa kauli tu, tunazozitoa mdomoni.

Tukumbuke kuwa hulka na tabia njema, sio matendo tu bali ni pamoja na kauli zako kwa wenzako, na kwa jamii.

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Yasinta Ngonyani said...

kazi nzuri sana yaani..nasubiri mwendelezo wake