Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, June 4, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-70


Mahakama ilikuwa imejaa watu isivyo kawaida, ilibidi askari wa usalama wafanye kazi ya ziada kuwazuia watu wasiendelee kuingia kwenye ukumbi huo wa mahakama, kwani ndani kulishajaa watu na bado watu walikuwa wakizdi kuja kusikiliza kesi, na kesi iliyovutia wengi ni hiyo ya mauaji ya mtoza ushuru, japokuwa kulikuwa na kesi nyingine iliyopangwa kusikilizwa siku hiyo hiyo.

Penye wengi pana mengi, kila mwenye mdomo hapakosi la kuongea, hata kama halina uhakika, kwani kwa mbali niliwasikia watu wawili wakiongea kwa sauti ya juu kidogo, bila kujali kuwa wapo mahakamani, mmoja akasema;

‘Leo tutaona ukweli kama kweli wanasiasa wana nguvu zaidi ya sheria…’

‘Lakini uonavyo wewe kweli ni hivyo kuwa wanasiasa ndio wakosaji, mimi naona ni uzembe wa watendaji wenyewe?’ akauliza mtu mwingine

‘Watendaji gani, unaozungumzia wewe, hivi kama bosi ambaye ni mtu wa siasa akitoa amri, hili lisifanyike, au lifanyike hivi, hao watendaji watakaidi, hawawezi kumpinga bosi wao hata siku moja, ....wafanye hivyo kama hawataki kazi,…’akasema jamaa wa kwanza

‘Ndivyo ilivyo, mimi sioni ajabu, maana mengine tumejitakia wenyewe, hao wanasiasa tumewachagua wenyewe, wapo hapo kwenye nyadhifa zao kutokana na kura zetu, na sasa wanatuonyesha jeuri yao,wanasema ukitaka kumjua mtu tabia yake muache apate, akipata tu, utaijua tabia yake ipoje, lakini wakati hana atanyenyekea utafikiri ni mtu mwema sana....’akasema

‘Kura yako ina thamani pale inapotafutwa, lakini baada ya kuhesabiwa, haina thamani tena, kwani yule uliyemchagua anakuwa ndiye bosi wako,…..na hatajali kuwa wewe ndiye uliyempa hicho cheo,ndio mchezo wa siasa ulivyo….’akasema

‘Lakini hawa watendaji hasa watu wa usalama,kwanini wawaogope wanasiasa wakati wao ndio walinzi wa dola….?’ Akauliza

‘Kawaulize wenyewe…chunga mdomo wako, mimi sijawataja hao,...’akasema mwenzake akitaka kumkatisha kwani kesi ilishaanza, na mara watu wakatulia pale hakimu alipoanza kuitaja hiyo kesi,na baada taratibu zote za kimahakama, na kuelezea kesi hiyo inavyokwenda ikafikia hatua ya kuitwa shahidi aliyetakiwa kutoa ushahidi wake siku hiyo, hapo hakimu akasema;

‘Upande wa wanaoshitaki, muiteni shahidi wenu,…’hakimu akasema na muendesha mashitaka akasema;

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, nitamsimamisha shahidi wangu, lakini nawaomba upande wa utetezi wawe makini katika uulizaji wao wa maswali, kama tulivyoongea nao,kwani hatutaki mahakama hii ikageuka sehemu ya kutuliza fujo…’akasema na kauli hii iliwafanya watu wagune, na wakili mtetezi akasema;

‘Mheshimiwa hakimu,muendesha mashitaka, anataka kututisha, hiyo kauli yake inaonyesha jinsi wenzetu walivyo, nia na lengo lao ni kutufanya sisi tusitimize wajibu wetu….’ Na hapo kukatokea malumabano ya mawakili hao wawili hadi hakimu alipoingilia kati

‘Nimesema shahidi anayestahiki kutoa ushahidi wake aitwe nasikusema muanze kulumbuana,nawaonya tena ….’akasema hakimu akigonga kirungu chake na mahakama ikawa kimya,na muendesha mashitaka akasema

‘Shahidi wangu atakayekuja kutoa ushaidi wake ni Mdada Binti Majivuno…..’akasema na mara minong’ono ya watu ikasikika, na minong’ono ya kundi la watu hugeuka kuwa mngurumo, na ndipo hakimu akagonga kirungu chake na kusema;

‘Kama hakutakuwa na utulivu hatutaruhusu tena wasikilizaji, watu wa usalama hakikisheni sheria za mahakama zinafuatwa na kama hakuna utulivu tutawatoa wote nje…’akasema hakimu na kukawa kimi wakati huo mdada alishafika sehemu wanaposimama mashahidi na kuanza kutoa kiapo, na taratibu nyingine zikafuatwa.

Mimi pale nilipokaa nikiwa na askari usalama nyuma yangu nilihisi mwili ukinisisimuka, hasa nilipomuona mdada akiwa kasimama pale mbele, nilianza kuingiwa na wasiwasi hasa hapo wakili mtetezi atakapoanza kumuhoji mdada.

Akili yangu ilirejea nyuma siku ile nilivyoshuhudia akimtupa mtu kama katoto, umbile la mtoza ushuru ni kubwa, lakini kwa mdada ilionekana kama katoto...sikuamini, ni nguvu gani hizo zinazoweza kumuingia mtu awe na nguvu kama za tembo, ndio hayo mashetani au kuna nini cha zaidi...nikaendelea kuwaza huku mdada akitoa maelezo yake huku akiongozwa na msimamizi wa kesi hii.

‘Haiwezekani mtu awe na nguvu za namna hiyo, aweze kumrusha mtu kama mtu anayerusha gunia lisilo na uzito…’nikasema siku nilipomuahdithia mpelelezi

‘Hizo ni imani tu,hakuna kitu kama hicho,kitaalamu mdada anajulikana kaathirika na msongo wa mawazo kutokana na madhila aliyoyapata, hayo mengine ni uvumi tu wa watu…’akasema mpelelezi.

‘Ipo siku utashuhudia mwenyewe na wewe utakuja kuniambia,….hata mimi nilikuwa siamini hayo,lakini siku ile niliposhuhudia mwenye kwa macho yangu,nimeanza kuamini kidogo kuwa kuna mambo yanayozungumzwa mengine yapo…’nikasema.

‘Kwahiyo wewe unasema mdada ana mashetani?’ akaniuliza mpelelezi, na hapo nikashituka toka kwenye mawazo nilipomuona mdada akiulizwa swali na muendesha mashitaka;

‘Mdada binti Majivuno hebu tuambie siku ya tarehe ambayo marehemu aliuwawa wewe ulikuwa wapi?’ akaulizwa mdada.

‘Nilikuwa nyumbani kwangu muheshimiwa…’akasema mdada

‘Ulikuwa ukifanya nini?’ akaulizwa

‘Nilikuwa nipo kwenye mapumziko maana nilikuwa naumwa,…’akasema mdada

‘Ulikuwa unaumwa nini,unaweza kutuambia tatizo gani lilikuwa linakusumbua?’ akaulizwa

‘Mimi huwa nina matatizo yanayotokana na msongo wa mawazo,japokuwa wengine wanasema nimekubwa na mashetani lakini kitaalamu wanasemani ni tatizo linatokana na mgandamizo wa mawazo yaliyotokana na matatizo yaliyowahi kunikuta kipindi cha nyuma….’akasema mdada

‘Inatosha haina haja kuelezea zaidi, Muheshimiwa hakimu, nia ya kumuuliza hivyo ni ili mahakama yako tukufu ielewe tatizo alilo nalo mdada,ili wenzetu wakianza kumuhoji wawe na tahadhari hiyo,na sikuwa na makusudio ya kuwatisha….’akasema wakili muendesha mashitaka,na wakili mtetezi akataka kuweka pingamizi lakini katulia

‘Hebu tuambie siku hiyo ambayo marehemu aliuwawa, ulikuwa na nani?’ akaulizwa

‘Alikuwepo Mhasibu na kabla ya hapo alikuwepo bosi wa kampuni yangu niliyokuwa nikifanyia kazi…’akasema

‘Walifika hapo kufanya nini?’ akaulizwa

‘Walifika kuja kunijulia hali,na katika hali waliyonikuta nayo,ikabidi wapeane zamu ya kunilinda,….’akasema

‘Je kipindi marehemu anafika wewe ulikuwa wapi?’ akaulizwa

‘Mimi nilikuwa ndani chumbani kwangu, kama nilivyosema nilikuwa naumwa,…’akasema

‘Kwahiyo wakati marehemu anaingia wewe ulimuona?’ akaulizwa

‘Wakati  marehemu anaingia mimi sikumuona, nilimuona wakati nimetokea chooni, na nilipofika pale alipokuwa amesimama nilishangaa kumuona amemshikia bastola mhasibu,….’akasema

‘Wewe ukafanya nini?’ akaulizwa

‘Kwanza nilishituka sana,pili nikajua kuna hatari,kwahiyo ni lazima nijihami,na kwa vile mtoza ushuru ambaye ni marehamu alikuwa hajaniona, nikaona nichukua nafasi hiyo kumgonga mkono wa huyo marehemu,mkono uliokuwa umeshika silaha, na nilifanya hivyo, na silaha ikamtoka mononi……’akasema mdada

‘Ehe ikawaje?’ akaulizwa, na mdada akasema;

‘Wakati huo hali ilishaanza kunibadilika, nikawa sijitambui tena...’akasema

‘Una maana gani kusema ulikuwa hujitambui tena ….?’ Akauliza

‘Akili ya kawaida ilinitoka, nikawa mtu mwingine, sijui inavyokuwa ila nakuwa sina kumbukumbu zangu za kawaida,…’akasema mdada

‘Kwahiyo wakati unamgonga huyo mtoza ushuru mkono, ulikuwa bado unajitambua, baada ya hapo hali ikabadilika ukawa hujitambui tena...?’ akaulizwa

‘Ndio muheshimiwa, ninachokumbua hapo ni kuwa nilimuona mtoza ushuru akiwa na bastola, nikamgonga mkono na bastola ikamtoka, na wakati huo mwili wangu ukawa unasisimukwa, kichwa kikawa kinaniuma sana, na mara nikahisi kama kitu kimeziba aili yangu, nikawa sijitambui tena.....’akasema

 ‘Ulizindukana kutoka kwenye hali hiyo wakati gani?’akaulizwa

‘Kipindi polisi wameshafika nilizindukana na kujikuta nipo sakafuni nimelala….na nilipoamuka dakitari wangu akanituliza na kuniambia nisiwe na wasiwasi….’akasema

‘Ulpozindukana uliona nini?’ akaulizwa

‘Niliwaona askari wakipima huku na kule,na baadaye macho yangu yakamuona mtu kalala sakafuni, akiwa kafunikwa,nikamuuliza dakitari wangu kumetokea nini,akaniambia mtoza ushuru kauwawa….nilishituka sana, na kwa vile alikuwa mtu wangu wa karibu niliumia sana…..’akasema

‘Hebu niambie ukweli,kabla hujapoteza fahamu, ulimuona mtoza ushuru akiingia, kwanini aliingia nyumbani kwako?’ akaulizwa

‘Mtoza ushuru alifika kwangu akinilitea kazi yangu,zilikuwa nyaraka za gari langu ambazo zilikuwa zinahitajia kukamilishwa, na ilitakiwa nizione mimi kwanza,na niweke sahihi yangu na baadaye nimalizie malipo yangu niliyokuwa nadaiwa..’akasema

‘Sasa kwanini mtoza ushuru ageuka na kumuwekea silaha mhasibu,..?’ akaulizwa

‘Mhasibu hana mahusiano na mtoza ushuru, na siku alipoleta huo mzigo bado nilikuwa naumwa,na sikuweza kupata hizo pesa zote alizokuwa akizihitajia huyo mtu, nahisi baada ya kupewa kiasi pungufu, akahisi anataka kudhulumiwa ndio maana akaamua kutumia vitisho….’akasema mdada.

‘Hebu tuambie,unapopoteza fahamu unaweza kujijua baadaye kuwa ulifanya nini?’ akaulizwa

‘Hapana siwezi kujua kabisa,mengi nafanya kuambiwa…’akasema na muongoza mashitaka akasema;

‘Panapokuja mgeni kwako utaratibu wako upoje?’ akaulizwa

‘Mlinzi anakuja kunipa taarifa, na mimi namuambia huyo mgeni aingie au namuelekeza jinsi gani ya kumuambia....’akasema

‘Siku hiyo ya tukio, alipofika huyo mgeni, uliongea na mlinzi wako , akikupa taarifa kuwa kuna mgeni?’ akaulizwa

‘Hapana kwa vile nilikuwa naumwa, sikuweza kuongea naye, nilimuomba mhasibu ambaye alikuwepo kwa muda huo, ili aonane na huyo mtu....’akasema

‘Kwahiyo kazi yote alifanya mhasibu?’ akaulizwa

‘Ndio...’akasema mdada

‘Kwahiyo mhasibu ndiye aliyeonana na mtoza ushuru baada ya kuongea na mlinzi?’ akauliza hilo swali tena

‘Ndio...’akasema

‘Na huwezi kujua ni kitu gani waliongea hao watu, hukuweza kusikia walichokuwa wakiongea?’ akaulizwa

‘Hapana, sikuweza kusikia, nilikuwa nimepumzika chumbani ...’akasema

‘Kwa namna hiyo watu waliokuwepo hapo kwa muda huo ni mlinzi akiwa getini, na ndani akawa yupo mtoza ushuru na mhasibu?’ akaulizwa

‘Ndio....

‘Kwa sasa nawaachia watetezi wamuhoji shahidi nitaendelea naye sehemu ya pili…..’akasema muongoza mashitaka na wakili wa utetezi akasogea hadi pale aliposimama mdada, akamuangalia kwa macho makali,na kusema;

‘Kama wewe una shetani, ushindwe na hilo shetani lishindwe na liangamie kwa nguvu za mwenyezi mungu….’akasema na watu wakacheka, na hakimu akasema;

‘Wakili usilete mchezo mahakamani….’akasema hakimu

‘Ndugu muheshimiwa,mimi nilitaka kuliondoa hilo shetani nililosikia linamsumbua huyo shahidi, na kuondoa wasiwasi kwa watu, samahani sana, natumai shetani limeondoka,…’akasema na watu wakacheka,

‘Samahami muheshimiwa hakimu, nataka kumuuliza huyu shahidi anayesema kuwa yeye hakujua kilichoendelea kipindi chote hadi polisi walipoingia….’akatulia

‘Huyu mtu anadai alipotewa na akili, na tunaweza kusema kwa muda huo alikuwa mwendawazimu na aliweza kufanya lolote bila kujitambua…’wakili muongoza mashitaka akaweka pingamizi kwa kauli ya wakili mtetezi,na maelezo yake na hakimu akakubaliana napingamizi hilo.

‘Mdada,unasema hali hiyo ikikutokea unakuwa hujitambui, sawa si sawa?’ akaulizwa

‘Sawa..’akasema mdada

‘Kwahiyo unakuwa huna akili za kibinadamu za kawaida?’ akauliza

‘Mimi sijui kwasababu sijitambui..’akasema mdada

‘Kwahiyo unaweza kufanya mambo kinyume na hali halisi ya kibinadamu..?’ akaulizwa

‘Mimi sijui kwasababu ninakuwa sijitambui…’akasema mdada

‘Kwahiyo kwa vile hujitambui,kwa vile akili ya kibinadamu haipo,unakuwa wewe sio binadamu wa kawaida, na unaweza kufanya mambo ambayo hata mnyama anaweza kufanya, au wale waliotindikiwa na akili wanavyofanya….’akasema na wakili muendesha mashitaka akaweka pingamizi.

‘Muheshmiwa hakimu, mimi namuuliza shahidi anavyokuwa kipindi hicho, na hali kama hiyo haina tofauti na wale waliotindikiwa na ubongo, na kwa majina mengine japo hatuyapendi wakiitwa watu, majina kama vichaa, au wendawazimu, mimi hapo nina kosa gani?’ akauliza wakili mtetezi.

‘Hebu niambie mdada, hali kama hiyo hukutokea wakati gani?’ akaulizwa

‘Hali kama hiyo hunitokea mara chache sana...’akasema mdada

‘Hata kama ni mara chache, ieleze mahakama hali hiyo hukutokea wakati gani, natumai swali langu lipo wazi...’akasema wakili

‘Ni wakati nimetingwa na msongo mkubwa wa mawazo na kupandwa na hasira,...’akasema

‘Na ni kwa watu wote wanaoweza kukufanya hali hiyo itokee?’ akaulizwa

‘Hapana, sio kwa watu wote, mara nyingi ni kwa wanaume, ..na ni kutokana na....’ kabla hajaendelea wakili huyo akasema;

‘Kwahiyo ugomvi wako mkubwa ni kwa wanaume....?’ akaulizwa

‘Nahisi hivyo, kutokana na hayo waliyowahi kunifanyia....’akasema

‘Na mtoza ushuru alikuwa mwanaume,...au sio? ’akasema na muendesha mashitaka akasema wakili anahitimisha kulazimishia hoja yake...’na hakimu akakubali pingamizi

‘Wakati mtoza ushuru anaingia na bastola wewe ulikuwa wapi?’ akaulizwa

‘Nilikuwa nimetoka pale nilipolala na kwenda chooni...’akasema

‘Na wakati huo akili zako zilikuwa sawa?’ akaulizwa

‘Ndio...’akasema

‘Na ulipomuona mtoza ushuru akili zako zikabadilika...?’akasema

‘Hapana, zilibadilika pale nilipomuona kashika bastola, na nilipomgonga mkononi, na yeye akaanza kuja juu kupambana na mimi na hapo hasira zikapanda, hali ikaanza kunibadilikia, na fahamu zikawa sio zangu, sikujua kilichoendelea....’akasema

‘Umesema hali hiyo ikikutoka unakuwa hujitambui, na kwahiyo unaweza kufanya lolote bila kujijua au sio?’ akauliza na kabla shahidi hajajibu akaendelea kusema;

‘Na umesema ulipomuona mtoza ushuru, akiwa  na bastola, ukamgonga na bastola ikamtoka, lakini yeye akaja juu kupambana na wewe, na hasira zikakupanda, ukawa hujitambui tena, na umesema, hasira zako zinakuwa zaidi kwa wanaume, si ndivyo ulivyosema

‘Ndio...’akasema

‘Ulimgonga mtoza ushuru mkononi, silaha ikamtoka, na unasema hapo akili ikawa sio yako, na kawaida ukimdhibiti mtu asiye na silaha na silaha ikimtoka unachofanya ni kuhakikisha kuwa haipati tena hiyo silaha, au kuichukua hiyo silaha, na kwa vile wewe ulikuwa huna fahamu za kibinadami na umeshika hiyo silaha, ...kilichofuatia ni nini...’akawa kama anauliza na wakili akaweka pingamizi kuwa wakili anahitimisha ...

‘Tuendelee sehemu ya pili....’akasema wakili mtetezi na wakili muendesha mashitaka akafika, na muda huo vielelezi kadhaa vikaletwa mezani kuonyesha kuwa sehemu hiyo inayofuata inahitajia vielelezi na moja kati ya vielelezo hivyo ni ule mfuko ukiwa na mkoba uliokuwa na bastola....na kwa muda huo nikamuona mpelelezi akisogea na kuteta na muendesha mashitaka.

NB : Mambo yameanza kuiva

WAZO LA LEO: Utu na ubinadamu ni pamoja na kujali afya zao, sasa hivi Dar, kuna 
msongamano mkubwa wa magari, na foleni zinakuwa ndefu sana na magari yanasimama kwa muda mrefu zaidi ya msaa manne. Humo ndani ya magari kunakuwa na wagonjwa, watu wasijiweza, watoto, na watu wamebanana.


Kiafya sio salama mtu kusimama ndani ya daladala lililojaa kwa masaa zaidi ya matatu. Najua foleni kwasasa inatokana na matengenezo ya barabara, lakini wakati mwingine ni kutokana na misafara ya waheshimiwa, ...ratiba za hao wakubwa zinajulikana , kuwa muda fulani watapita barabara fulani, basi ingelifaa magari yaambiwe mapema, kuwa kuanzia saa fulani kutapita msafara, kwahiyo magari hayo yapitishwe njia nyingine mbadala, au kwenye barabara zisizo rasimi, ili kupunguza foleni na watu kuathirika kiafya....


Ni mimi: emu-three

No comments :