Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, May 15, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-58


‘Mhasibu wewe na mdada mna mahusiano gani?’ nikaulizwa swali  hilo baada ya kutoa maelezo yangu nikisimamiwa na muendesha mashitaka, nilijitahidi kuelezea yote ninayoyakumbuka siku ile, na nilipomaliza, akasimama wakili mtetezi na uniuliza maswali mengi na baadaye akaniuliza hilo swali la mtego;

‘Ni mfanyakazi mwenzangu...’nikajibu kwani nilishajiandaa nalo na sikutaka kuelezea zaidi.

‘Ina maana mkiwa wafanyakazi mnakuwa huru, au wewe ni tabia yako ya kumtembelea mdada, muda wowote, hata kwenda kulala pamoja ...’akasema wakili na wakili wangu akaingilia kati kulipinga hilo kuwa hayo ni maswala binafsi na hayana ukweli

‘Kama likesha humo, alifanya nini, hakulala humo, hawaulala humo , yeye na mdada, ukumbuke bosi alishaondoka, wakabakia wawili unafikiri kilitokea nini, walikaa macho,...ni ukweli usipingika kuwa walilala, ...nimekosea nini hapo...’akasema wakili mtetezi

‘Kauli yako ya mwanzo umesema nililala naye...’nikajitetea

‘Hukulala naye?’ akauliza

‘Sikulala naye, kwasababu alikuwa mgonjwa, na kazi yangu ilikuwa kuhakikisha yupo salama, na akiamuka niweze kumsaidia...’nikasema

‘Swali ni kuwa muda wote huo mlikuwa macho hamkulala?’ akauliza

‘Kuna muda tulilala..’nikasema

‘Sasa unakataa nini, inaonekana wewe una tabia ya kukataa ukweli..’aasema huyo wakili, na kabla sijajitetea akauliza;

‘Turudi siku ya tukio, waati mlipokuwa na mfanyakazi mwenzako, mkakesha usiku kucha,unasema kuna muda mlilala, au sio, nyie wawili au sio, nakushangaa kweli, maaan  kwenye maelezo yako umesema una mchumba wako...’aasema na watu wakacheka.

‘Hebu niambie, je siku hiyo unasema alifika marehemu mkaongea naye, akakupa mzigo wa mdada, na wakati unaelekea ndani , marehemu akatokea kwa nyuma akiwa an bastola..sawa?' akauliza na mimi kabla sijajibu swali akaendelea kusema;

'Kwahiyo kumbe ni wewe uliyeongea na mlinzi, au baada ya mlinzi kuongea na mtu mwingine, wewe ndio ukatoka kwenda kukutana na marehemu, maana kutokana na maelezo ya mlinzi, yeye  anasema  aliongea na mtu aliyekuwa na ndevu, na alikuwa mtu tofauti na wewe hebu tuambie humu ndani mlikuwa watu wangapi?’ nikaulizwa.

‘Ni kweli mimi ndiye niliyeongea na mlinzi, na hakukuwa na mtu mwingine, na mlinzi akaniambia kuwa kuna mgeni wa mdada nje, na mimi nikaenda kuonana na huyo mgeni, na huyo mgeni alikuwa ni ndio huyo marehemu,akanipa huo mzigo wa mdada, na wakati naelekea ndani, ndio marahemu akatokea kwa nyuma akiwa an bastola, haukuwa na mtu mwingine,....’nikasema

‘Lakini mlinzi kasema aliongea na mtu aliyekuwa na ndevu, sio wewe, je huyo mtu mwingine ni nani?’ akaniuliza

‘Mimi simjui, ...’nikasema na moyoni nilijihisi vibaya, kwani sikuweza kusema ukweli, na kwa mbali kitaswira nikamuona mdada, akitabasamu huku kashika shavu akinisanifu na kusema; 'masikini mhasibu...'.

‘Hebu sema ukweli wako, wewe siku hiyo ulikuwa na ndevu?’ akauliza wakili huyo

‘Hapana, sikuwa na ndevu , na hata nikiwa nazo huwa nazikata, huwa zinaota kidogo sana, lakini sio kwa kiasi hicho mlichosema nyie....na sina tabia ya kufuga ndevu...’nikasema

‘Ukumbuke upo chini ya kiapo, tena cha dini yako, je ni kweli kuwa siku hiyo hukuwa na ndevu, na kwanini mlinzi anasema kuwa yeye aliongea na mtu mwenye ndevu, ina maana yeye anasema uwongo, je sio wewe unayesema uwongo, wakati umeshaapa, hivi wewe kweli unamuamini mungu wako?’ akaniuliza

‘Ndio namuamini mungu wangu,...’nikasema

‘Na unakiri uweli kuwa haya unayotuambia ni ya kweli yote, kuwa wewe siku hiyo hukuwa na ndevu?’ akauliza na kabla sijajibu wakili wangu akaingilia kati kuwa wakili huyo analazimisha nitoe jibu kwa vitisho

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, simuulizi kwa vitisho, hapa tunachohitajia ni ukweli, na ukweli ulivyo ni kuwa huyu jamaa ndiye aliyekuwa humo ndani, na kwa kauli yake mwenyewe amesema hakuna mtu mwingine aliyeongea na mllinzi zaidi yake, ina maana ni yeye aliyeongea na mlinzi, na mlinzi anasema mtu aliyeongea naye alikuwa na ndevu,..je huyo mtu ni nani, mwenzetu huyu anasema hamjui, ...sasa tutaelewaje, na huyo mtu mwingine ni nani....’akasema kama anauliza

‘Ina maana kulikuwa na mtu mwingine, ambaye wao hawakumuona, ...je huyo mtu mwingine ambaye wao hawakumuona ni nani,  ...?’ akauliza swali na kuniangalia machoni

‘Mimi simjui huyo mtu mwingine....’nikasema nikionyesha udhaifu wa sauti

‘Muheshimiwa hakimu, hii inaonyesha jinsi gani huyu sivyo mkweli na nahisi anataka kuficha ukweli, ni kwa amsilahi ya nani,...kwa mtizamo huo tunaweza kumuhukumu mtu asiye na kosa,  ..’akasema wakili mtetezi, na wakili akaambiwa athibitishe hilo.

‘Mimi nitalithibitisha hilo kuwa mshitakiwa kakamatwa kimakosa , kuna mtu mwingine ambaye anastahili kukamatwa kwa kosa hilo, lakini hajapatikana...’akasema na kunigeukia mimi, akauliza;

‘Mhasibu, wakati ukiwa humo ndani, wakati marehemu alipokulazimisha uingie naye ndani mkiwa na huo mzigo, ni kitu gani kiliendelea?’ nikaulizwa

‘Niliingia na marehemu akiwa nyuma yangu akiwa kanielekezea bastola, na tulipofika chumbani mdada hakuwepo, hakuwa kalala chumbani kwake, alitoka, na ndiyo ilikuwa nusura yake kwani marehemu alishajiandaa kumfanya lolote, na mara mdada akatokea akiwa keshabadilika, akaweza kumdhibiti marehemu, na marehemu akawa hamuwezi tena mdada, mimi baadaye nikapigwa na kitu kichwani,....’nikasema

‘Unasema mdada alikuwa keshabadilika, kwa vipi?’ nikaulizwa

‘Alikuwa kapagawa ,kashikwa na mashetani, huwa hali hiyo humtokea mara kwa mara, na akiwa hivyo anakuwa na nguvu za ajabu....’nikasema

‘Umesema mdada aliweza kumdhibi marehemu na bastola ikawa imemtoka mikononi,na unasema kuna muda ulipigwa na kitu kichwani, je ulipigwa na kitu gani?’ nikaulizwa

‘Nahisi ni nyundo..’nikasema

‘Unahisi lakini huna uhakika?’ akauliza huyo wakili

‘Ndio nahisi maana sikuona hicho kitu..’nikasema na wakili mtetezi akamuangalia wakili muendesha mashitaka aliyeonyesha kama anataka kuingilia kati, lakini wakili huyo akabakia kimiya na wakili mtetezi akauliza.

‘Kwanini wewe ulihisi kuwa ni nyundo, na sio jiwe au kitu kingine?’ akaniuliza

‘Kwasababu nyundo inafahamika, mtu akikugonga nayo ni tofauti na jiwe, kwa mtu unayefahamu nyundo utajua kabisa hiyo ni nyundo iliyonigonga..’nikasema

‘Lakini hukuwa na uhakika kabisa kuwa hicho ulichopigwa nacho ni nyundo, inawezekana ikawa kitu kingine kinachofanana na nyundo?’ akauliza wakili mtetezi

‘Inawezekana lakini kiwe na mfano huo ....’nikasema

‘Je ulimuona huyo aliyekupiga na hiyo nyundo?’ akauliza

‘Sikumuona kabisa...’nikasema

‘Je wakati upo hapo, akili yako ilikuwa sawa, kuwa ulikuwa na uwezo wa kuona vyema, na kuangalia huku na kule?’akauliza

‘Ndio sikuwa nimepoteza akili, niliweza kuona vyema, siwezi kusema niligeuka sehemu zote, hapana, kwasababu muda mwingi, na hasa kwa muda huo nilikuwa namuangalia mdada, na wakati mwingine marehemu, kwani muda huo alikuwa hai...’nikatulia kidogo

‘Nilikuwa namuangalia mdada, kwani alikuwa sio yeye tena, na nilikuwa natafuta mwanya wa kukimbia lakini pia, niliogopa marehemu anaweza kuiwahi ile bastola na kumpiga nayo mdada...’nikasema

‘Kwahiyo muda wote huo, humo ndani mlikuwa wewe, mdada na marehemu?’ akaulizwa

‘Kwa ufahamu wangu ndio tulikuwa sisi watatu tu...’nikasema

‘Kwanini unasema kwa ufahamu wako, na nimekuuliza swali la kupambanua ufahamu wako, kuwa je ulikuwa na akili timamu, ulikuwa na akili ya kwueza kujua kinacotokea humo ndani,ukakubali kuwa ulikuwa na akili timamu, au nikuulize tena hilo swali, kuwa je wakati huo, akili yako ilikuwa sawa,..?’ akauliza

‘Nimesema kwa ufahamu wangu kwasababu, inavyoonyesha, kulikuwa na mtu mwingine aliyeweza kuja , kuingia bila mimi kumuona, na ndiye aliyenipiga na nyundo kichwani...’nikasema

‘Huyo mtu alitokea wapi?’ akauliza kama anajiuliza , lakini akawa kaniangalia mimi

‘Siwezi kujua...’nikasema

‘Kwahiyo unahisi tu kuwa huenda kulikuwa na mtu mwingine...inawezekana hakukuwa na mtu mwingine wakati huo, inawezekana kuwa mdada ndiye aliyekupiga na hicho kitu kama nyundo?’ akasema huku kaniangalia, na sikujua ni swali au anatoa maelezo na mimi nilipoona ananiangalia tu, nikasema;

‘Nyundo ingetoka wapi, hakukuwa na nyundo humo ndani..’nikasema kwa mshangao

‘Una uhakika gani, ina maana wakati umo humo ndani uliweza kukagua nyumba yote na ukahakikisha kuwa humo ndani kulikuwa hakuna nyundo..mmmh, kumbe kweli, ...’akasema na watu wakacheka na mimi niksema

‘Sio kweli, hizo ni dhana zako tu, mimi nilifika hapo nikiwa mgeni kabisa, na nia na lengo letu, ilikuwa kumsaidia mdada...’nikasema

‘Kama sio kweli, hebu niambie wewe umesema ulikuwepo hapo kama mgeni, ulifika tu kumsaidia mgonjwa...sasa una uhakika gani kuwa sio mdada aliyechukua nyundo, iliyokuwa mahali anapopajua yeye akakugonga nayo kichwani? Akauliza

‘Nina uhakika maana muda mwingi nilikuwa namuangalia mdada, kwani kwa muda huo ndiye aliyekuwa ni tishia kwangu, kwahiyo inawezekana wakati naangalai hivyo, huyo mtu alikuja kwa nyuma na kunigonga kichwani na nyundo, atakuwa alikuja kwa nyuma akafanya hivyo..’nikasema

‘Wakati unapigwa na hicho kitu kama nyundo ulikuwa umeangalia wapi?’ akauliza

‘Tulikuwa tumeelekea mlango wa kutokea nje,....’nikasema

‘Kwahiyo aliyekupiga na hiyo nyundo alikuwa katokea nyuma, ...iwe ni chumbani au chumba chochote, sio kutokea nje....?’ akauliza wakili muendesha mashitaka

‘Ni kweli, kama angelitokea mlango wa nje, wa kutoka nje ningelimuona,...’nikasema

‘Kwahiyo wewe unakiri kuwa wakati wote ulipokwua humo ndani hukuwahi kumuona mtu mwingine zaidi ya mdada na marehemu, ?’ akauliza

‘Ni kweli, sikumuona mtu mwingine..’nikasema

‘Na mlinzi alikuwa getini akilinda, na kama angeliingia ungelimuona akiingia pale mlangoni, sawa au sio sawa?’ akauliza

‘Ndio nigelimuona akiingia labda awe ameingia kwa kupitia sehemu nyingine...’nikasema

‘Kwani kuna mlango mwingine wa nyuma wa kuingilia kwenye hiyo nyumba?’ akauliza

‘Hapana nijuavyo mimi upo mlango mmoja tu wa kuingilia ndani...’nikasema

‘Unamuona huyo mtuhumiwa hapo mbele, hukuwahi kumuona akiingia humo ndani?’ nikaulizwa

‘Sikuwahi kumuona wakati huo, ...’nikasema na wakili mtetezi akageuka kumuangalia wakili muendesha mashitaka kama ana swali, na wakili muendesha mashitaka akasimama na kuanza kuniuliza maswali.

‘Umesema kuwa muda wote wewe ulikuwa unamuangalia mdada, na kwa namna hiyo mdada alikuwa keshatoka upande wa muelekeo wa chumbani, alikuwa muelekeo wa mlango wa kutokea nje, akitaka kuwazuia, ...?’ akauliza

‘Ndio...’nikasema

‘Na pia wakati huo, ulikuwa ukimuangalia marehemu asije akachukua hiyo bastola, kwahiyo kuna wakati unamuangalia mdada, na kuna wakati unamuangalia marehemu ...?’ akauliza

‘Ndio...’nikasema

‘Kwahiyo inawezekana wakati unamuangalia marehemu ambaye lengo lake ilikuwa kuichukua hiyo bastola, huyo mtu aliyekuwa na nyundo, aliweza uingia kwa haraka, bila yaw ewe kumuona?’ akauliza

‘Inawezekana, lakini awe ni mtu mwenye uzoefu, na uharaka wa hali ya juu, ...’nikasema

‘Pia huyo mtu anaweza kutoka chumbani au chumba chochote humo ndani,..’akauliza wakili muendesha mashitaka na wakili mtetezi akapinga hilo swali kuwa yeye anamulekeza shahidi kusema aonavyo yeye, na hakimu akakubali hilo pingamizi, na wakili muendesha mashitaka akasema hana swali jingine na wakili mtetezi akaendelea na maswali yake;

‘Wewe muda huo ulikuwa sakafuni, ulikuwa umeangalia wapi?’ akaulizwa

‘Nilikuwa nimeangalia muelekeo wa mdada, na wakati huo huo namuangalia marehemu...’nikasema

‘Na mdada kwa muda huo alikuwa wapi?’ nikauliza,

‘Yeye alikuwa anatemba mwendo ule kama wa kunyata, akitutafuta na alipotuona akawa anakuja uelekeo wetu, nahisi alijua kuwa tumekimbilia nje, kwahiyo kwa muda ule akawa kasimama nusu muelekeo wa mlango na nusu muelekeo wa kutokea nje..’nikasema

‘Kwa nyuma yako kulikuwa na nini?’ nikaulizwa

‘Kwa nyuma yetu kulikuwa ni muelekeo wa chumba cha mdada, na upande mwingine ni dirisha kubwa la nje..’nikasema

‘Kwahiyo huyo aliyekupiga na nyundo, alitokea kwa nyuma yako?’ nikaulizwa wakili muendesha mashitaka

‘Ndio kwani angelitokea kwa mbele yangu ningelimuona, na mdada angelimuona..’nikasema na wakili mtetezi akataka kuniuliza swali lakini akasita na kuangalia saaa, na hakimu naye akavutika na hali hiyo, akaangalia saa yake na kusema;

‘Muda umekwisha, kama mna maswali zaidi dhidi ya huyu shahidi mtamuuliza siku ya kesi ijayo, ...’akasema na mimi nikaweza kupumua, nikatoka na mbele yangu nikakutana na mpelelezi, ambaye alionekana na furaha usoni, akasema;

‘Bado unaendelea kuficha ukweli, sijui kwa masilahi ya nani’akasema

‘Nimeficha ukweli gani?’ nikauliza

‘Akisimama mtuhumiwa ukweli wote utajulikana na wewe hutaaminika tena, ...hilo ni kosa kubwa umefanya, wewe unaongea kumlinda mdada, na mdada hana masilahi na wewe, nikuambie ukweli, mwisho wa siku mdada atakuwa kamaliza kazi yake, na kupata ajira yake, wewe utakuwa wapi?’ akaniuliza na mimi nikabakia kimiya.

‘Unajua mdada anafanya hivyo kutokana na shinikizo la watu wake..na wewe anakutumia tu..’akasema kama ananiuliza

‘Akina nani hao watu wake?’ nikauliza nikionyesha mshangao, nikikumbuka kuwa siku hile huenda mdada alipoingia na kukutana na huyu mpelelezi watakuwa waliongea...

NB: Tuishie hapa kwa leo

WAZO LA LEO: Kosa ni pale unapojua kuwa unalotenda ni kosa na bado ukarudia hilo kosa, au kuukana ukweli pale unapojua ni ukweli, lakini kwa sababu zako binafasi au sababu za masilahi, au shinikizo la watu fulani,wewe ukaukana ukweli. Kumbuka kuwa msema kweli wakati wote ni mpenzi wa mungu, je msema uwongo ni mpenzi wa nani....




Ni mimi: emu-three

No comments :