Upande ule
waliokuwepo mwanadada kulionekana hakuna maelewano, lakini muda wa mahakama
ulipofika wakatulia, na mimi ile taswira ya yaliyotokea nyuma ikagota,
nikatuliza kichwa changu kusikia kinachoendelea leo mahakamani, lakini moyo
wangu haukuwa na amani kabisa.
Kesi ilianza
na kilichotawala siku hiyo ni mabishano ya mawakili hao wawili mtetezi na
muongoza mashitaka, mabishani hayo kwa sasa yalilenga ni nani asimamishwe kutoa
ushahidi, na watetezi waling’ang’ania kuwa mimi na mdada tusimamishwe kwanza,
kabla hawajamruhusu mtuhumiwa kutoa maelezo yake, na hapo mwendesha mashitaka,
akasema;
‘Mdada na
mhasibu ni mashahidi wangu na mimi ndiye ninayejua ni muda gani nitawasimamisha,
hamuwezi kunishurutisha kwa hilo,…’akasema mwendesha mashitaka na wakili
mtetezi akasema;
‘Sasa
kwanini wewe unang’ang’ania kuwa nimsimamishe mteja wangu, wakati unafahamu kuwa
hata mimi nina mpangilio wangu , kwanini ulianza kuniingilia mpangilio wa kazi
zangu. Ndugu muheshimiwa hakimu, mimi naona kuwa mdada na mhasibu ni mashahidi
muhimu sana, kwani wao ndio waliokuwepo humo ndani wakati mauaji yanatendeka…’akasema
wakili mtetezi
‘Hata ama
walikuwepo, lakini tendo hilo hawakuliona ...’akasema wakili muendesha
mashitaka
‘Hayo
unawasema wewe, ni muhimu wakasimama na kujieleza wenyewe ili haki itendeke,
sisi tunahisi kuna jambo mnaficha,...’akasema wakili mtetezi
‘Lakini hebu
rejea maelezo yako ya kesi iliyopita wewe mwenyewe ulisema leo ndio aambayo
mshitakiwa ataweza kutoa maelezo yake, lakini hadi sasa unawasimamisha
mashahidi wengine huoni kuwa unamyima haki mteja wako, wakati alishajiandaa
kutoa maelezo yake..’akasema muendesha mashitaka
‘Unajuaje kuwa
alikuwa kajiandaa kuongea leo hata kama ni hivyo, lakini mimi naweza kubadili
ratiba, kwa mpangilio wangu, na hilo halikuhusu wewe, yeye ni mteja wangu na
hao niliowasimamisha ni mashahidi wangu nikitaka kujenga hoja kuwa mteja wangu
hakuhusika na hayo mauaji, …’akasema wakili mtetezi
‘Ndugu muheshimiwa hakimu, sisi tulikuwa tumeshajiandaa kumsikiliza mshitakiwa, kama
ilivyokubalika katika siku ya kesi iliyopita, lakini cha ajabu tunashangaa leo
wanasimamishwa mashahidi wengine,nahisi
wenzetu wanamnyima haki mshitakiwa, na wanatufanya na sisi tuanze
kujipanag vingine,…’akasema wakili muendesha mashitaka
‘Kwahiyo
wewe upo upande gani?’ akauliza wakili mtetezi na wakili muendesha mashitaka
akatabasamu na kusema;
‘Mimi ni
muendesha mashitaka na lengo letu ni kuona haki inatendeka , sio kwamba kwa
vile ni muendesha mahitaka basi nitashikiza mshitakiwa kuchukuliwa adhabu tu,
hapana ni lazima hatua zote zifuatiliwe ikiwemo mshitakiwa kupewa nafasi ya
kujitetea, kama alivyoomba yeye mwenyewe...’akasema wakili huyo
‘Lakini
hakimu hajasema kuwa mshitakiwa ajitetee, na hili litafika atasimama na kufanya
hivyo, lakini kwa mpangilio wangu mimi kama mtetezi wake…’akasema wakili
mtetezi,na hapo hakimu ikabidi aingilie kati na kuuliza;
‘Je upande
wa utetezi, mnatarajia kumsimamisha
mshitakiwa lini, maana kwenye kumbukumbu zetu kweli ulitakiwa kumsimamisha
mshitakiwa leo kutoa maelezo yake, lakini muda unakwenda, hujamsimisha na sasa
unataka shahidi mwingine asimame kutoa maelezi,…?’ akaulizwa wakili mtetezi
‘Bado
naendelea na mashahidi wangu wa utetezi, na muda ukiruhusu nitamsimamisha
mshitakiwa muheshimiwa hakimu, nalifahamu hilo na hapa ninajenga hoja, ili
akisimama kila kitu kiwe wazi…’akasema wakili mtetezi na wakili muendesha
mashitaka akaingilia kwa hoja.
‘Tunaomba
sababu muhimu za kuendelea kumchelewesha huyo mshitakiwa... kwani kama ni
kujenga hoja, sio katika hatua hii, hatua hii ilikuwa ya kuiweka wazi hoja na
kutoa hitimisho’akasema
‘Ndugu
muheshimiwa hakimu, sisi tulitaka watu wawili wasimame kutoa ushahidi wao
kwanza kwa upande wao, lakini upande wa wenzetu wakadai hao ni mashahidi wao,
hatuna mamlaka ya kuwasimamisha mpaka waidhinishwe kama mashahidi wetu…'akasema na kuendelea kusema;
'Sasa
ninachoshangaa ni kuona wao wakitaka mtu wetu ndiye asimame, na ikionyesha kuwa
ni hitimisho,hili halitawezekana mpaka hao mashahidi wawili wasimamishwe, ili
na wao waeleze jindi ilivyotokea siku hiyo, tuna uhakika kuna ammbo mengi
hayajawekwa wazi, na wakisimama hao watu hayo mambo yatabainika.’akasema wakili
mtetezi.
‘Sisi tuna
mapangilio wetu, na tunafahamu kwanini hawa watu hawajasimamishwa, ..wao,
hawakuona tukio la mauaji, na kuna watu wameshatoa maelezo ambayo hata wao
wakisimamishwa watayatoa hay ohayo,....ni marudio tu..’akasema wakili
‘Lakini sisi
hatujarizika na hayo maelezo waliyotoa wengine, kwanini yatolewe na wengine
wakati wao wapo,....na kwanini muombe mshitaiwa asimame, je mshitaiwa ni
shahidi wenu?’ akauliza wakili mtetezi.
‘Sisi hatujasema
asimame kama shahidi wetu,...yeye mwenyewe aliomba kusimama kutoa maelezo yake,
baada ya kuona nyie mnatoa mashahidi wasiotosheleza kile alichokiona yeye….’akasema
wakili huyo na hapo hakimu akawaita mawakili hao wawili mbele na kuanza kuteta nao, walichukua muda kidogo na baadaye
hakimu akasema;
‘Kwa vile
muda uliobakia ni mchache, na tumeona kuwa mshitakiwa akianza kutoa maelezo
yake itachukua muda, kwahiyo upande wa waendesha mashitaka ni zamu yenu kutoa
mashahidi, na muda uliopo utatosha kutoa shahidi mmoja, ambaye hatachukua muda
sana…’akasema wakili na muendesha mashitaka akiwa kama hajajiandaa kwa hilo
akasema;
‘Japokuwa
sisi kwa upande wetu tulishajiandaa kumsikiliza mshitakiwa , lakini wenzetu kwa
namna yao wameendelea kumyima haki yake, hata hivyo sisi tupo makini wakati
wote na tumesha jitosheleza kwa hilo, na katika moja ya hoja za watetezi ni
kuwa wanawahitajia mdada na mhasibu kuja kutoa ushahidi wao, sisi hatuna
pingamizi kwa vile tunajiamini,na tunajua ni nini tunachokifanya …’akasema
muendesha mashitaka na wakili mtetezi akatoa pingamzi na kusema;
‘Ndugu
muheshimiwa hakimu, wakili muedesha mashitaka anapoteza muda, badala ya
kumsimisha shahidi wake, yeye anatoa maelezo, hiyo ni mbinu ya kupoteza muda,
na hakimu akasema;
‘Hiyo sio
kazi yako wakili mtetezi, ,....’akasema hakimu na kuangalia saa, halafu
akasema;
‘Wakili muendesha
mashitaka, msimamishe shahidi yako…’akasema hakimu na muedesha mashitaka
akasema;
‘Nitamsimamisha
mhasibu,aje kutoa ushahidi wake…’akasema.
Alipotamka
hilo, nikabakia mdomo wazi, sikutarajia, na nilijua kama ni kutoa ushahidi,
mdada angeitwa kwanza. Kwa muda ule, nilikuwa kamamtu aliyebebeshwa mzigo mzito
bila kujiandaa japokuwa tulishaarifiwa kuwa mimi na mdada wakati wote tunaweza
kusimamishwa kutoa ushahidi na ndio maana siku hiyo tulikuwa nje, upande wa
mashahidi.
‘Mhasibu unahitakiwa
kuingia ndani ukatoe ushahidi….’nikasikia sauti ikiita na mimi wakati huo
nilikuwa mbali nikiwazia tukio lililopita, nilikuwa nakumbuka kauli ya wale
waheshimiwa wakati nilipoitwa kwenye ofisi ambayo sasa inaitwa ofisi yangu, na
wale wakubwa na katika moja ya maelezo yao ni kuwa niwe makini wakati wa kutoa
usahhidi wangu, nisije kuongea mambo ambayo hayanihusu
‘Mambo kama
yapi ?’ nikauliza nikianza kuingiwa na wasiwasi kwani ilionyesha dhahiri kuwa
kesi ijayo nitasimamishwa kutoa ushahidi.
‘Unaweza
kuulizwa kuhusu marehemu na kazi
yake,ujue wewe hukuwahi kufanya kazi na marehemu
na kwahiyo hakuwahi kujua kiundani ni kitu gani alikuwa akikifanya, kwahiyo huwezi kujua lolote linalomuhusu yeye,
kwahiyo ukiulizwa mambo yake ni bora useme hujui lolote, usije ukaropoka tu...kwa
labda kuna mambo umeyaona humu ndani au umesikia lolote kuhusu yeye na ofisi
yake, ukifanya hivyo ni kosa maana utakuwa unatoa siri za ofisi ambazo
hazihusiani na hiyo kesi….’akasema mmoja wapo.
‘Sizani kama
wanaweza kuniuliza mambo kama hayo, na hata wakiniuliza hayo mimi nitakuwa
makini jinsi gani ya kujibu…’nikasema kwa kujiamini
‘Ufahamu mawakili
ni wajanja sana, wakiwa wanatafuta jambo wanaweza kutumia njia yoyote ya
kukupoteza akili yako, na unaweza ukayumbushwa na kujikuta umeropoka bila hata
kutarajia, sisi tuna uzoefu na hayo, ….’akasema huyo muheshimiwa.
‘Nitakuwa
makini kwa hilo...’nikasema
‘Na jingine
ni kuwa huu mkataba tunaokupa sasa hivi ndio utakaotambulikana rasimi...’akasema
‘Sizani kama ulishawahi kupewa mkataba wowote kabla,
ambao una orodha za vitu vyote vilivyokuwemo humu ndani na ambavyo unatakiwa
kuvifanyia kazi..’akauliza mwingine akiniangalia kwa makini.
‘Mkataba,..na
orodha, hapana...nakumbuka niliambiwa nisubiri hadi hapo kesi
itakapokwisha,..naona ajabu leo….’nikasema na kabla sijaendelea zaidi huyo
muheshimiwa akanikatisha na kusema;
‘Usione
ajabu, hii nafasi inahitajika mtu awepo, angalau afanye kazi ..., hatuwezi
kuacha shughuli ziende kienyeji japokuwa kuna watendaji wengine wanaendelea
kufanya zile kazi za marehemu, lakini hata hivyo, hapa kulikuwa na ofisi
maalumu, na kuna mambo ambayo yanahitaji mtu kuyasimamia, haya yaliyopo humu ni
mambo nyeti, hatuwezi kumpa mtu yoyote tu,, na kwa vile wewe umeaminiwa,ni
vyema ukayafanyia kazi...’akasema
‘Lakini ....’nikaamza
kujitetea
‘Hakuna cha
lakini, hakuna kitu kigeni, hakuna kitu kigumu, kinachohitajika kwa sasa ni
kuhakikisha kuwa kumbukumbu muhimu zipo mikononi mwa mtu mwaminifu, mengine
yapo kwenye mitandao, na hayawezi kupotea, lakini kuna kazi zipo humu, zilikuwa
hazijafanyiwa kazi, na nyaraka za siri ambazo hazitakiwi kusambaa ovyo...’akasema
‘Lakini orodha ya vitu hivi naona kama haijakamilisha
baadhi ya vitu, nakumbuka wakati walipokuwa wakinisaili wale waheshimiwa kuna
vitu walinionyesha, hapa sivioni….’nikasema
‘Vitu kama
vipi,...wewe huwezi kujua vitu gani unastahili kukabidhiwa na vitu gani
unastahili, sisi ndio tunaofahamu hilo,
kwahiyo wewe unachotakiwa kwasasa ni kupokea huu mkataba kama ulivyo, na vitu
vilivyomo,huna haja ya kudadisii kitu ambacho hakipohumu, umenielewa…’akasema
na mwenzake akaitikia kwa kichwa
‘Na hata
kwenye kesi ikatokea kuulizwa makabidhiano ya ofisi , wewe utasema ulikabidhiwa
kama inavyoonyesha hapa, kabla ya hapo, kama uliona kitu fulani , na sasa
hakipo, huna haja ya kuumiza kichwa chako, hivyo visahau katika kichwa chako,
…’akasema
‘Na je wewe
uliwahi kupitia kabla na kuangalia vitu vyote alivyoviacha marehemu humu
ndani?’ akauliza
‘Hapana
sikuwahi kufanya hivyo, maana nilikuwa sijakabidhiwa ofisi …’nikasema
‘Unaonaeeh...
, hilo ndilo jibu sahihi, na popote utakapoulizwa unatakiwa kusema hivyo,na kwa
vile umetuelewa, sisi hapa hatuna zaidi, kwa leo tunaishia hapa, lakini
tutaendelea kuja mara kwa mara kukuelekeza baadhi ya kazi kabla hujaanza kazi
rasimu...’akasema muheshimiwa.
‘Kiujumla
bado hujaajiriwa, kama unavyosoma huu mkataba ni ajira ya muda, ya
majaribio,...unachofanya kwasasa ni kushikilia ofisi hadi hapo kesi
itakapokwisha, ….natumai umetuelewa’akasema na wakasimama na kunyosha mikono
tukashikana na wakaondoka zao.
Walipoondoka
waheshimiwa hawa , nikawa nausoma ule mkataba, na mara mlango ukagingwa,akaingia
mdada, nilishasahau kabisa habari zao, na nilipomuona nikawa na hamu ya kujua
ni kitu gani kimetokea kati yake na mpelelezi, yeye akionyesha hasira usoni,
akasema;
‘Mumemalizana
na watu wako, ...?’ akauliza
‘Ndio, je na
wewe umemalizana vipi na ...’nikasita kuendelea na yeye akasema;
‘Nasikia
kesho mimi au wewe tutasimamishwa kutoa ushahidi, kwahiyo tunahitajika
kujiandaa…’akasema na alionyesha hakutaka kuongea yaliyotokea kati yake na
mpelelezi
‘Ni nani
kakuambia?’ nikamuuliza nikimuangalia usoni na yeye akaangalia ule mkataba,
akauchukua, na kabala haujaugusa akawa kama aumbuka jambo, akachukua kidude
chake wenye moba akatoa kitambaa cheupe, akapitisha juu juu kwenye ule mkataba
halafu akakiweka kile kitambaa kwenye kitufe fulani, akasubiri.
‘Yah, ndio
wao...hamna shaka...’akasema
‘Ndio wao
wamefanya nini?’ nikamuuliza
‘Mumeongea
nini na hao watu?’ akaniuliza badala ya kujibu swali langu
‘Kuhusu
makabidhiano ya ofisi na vilivyomo, na ya kuwa huu mkataba ndio unaoonyesha
kila kitu ninachotakiwa kuwa nacho, hakuna zaidi ya hayo yaliyoandikwa hapo...’nikasema
‘Nilijua
tu....’akasema
‘Kwahiyo
wewe umegundua nini?’ nikamuuliza nilipoona akiweka kile kidude kwenye mkoba
wake, nay eye bila kujali swali langu akasema;
‘Muendesha
mashitaka kasema wewe au mimi au wote wawili kesho kuna uwezekano mkubwa wa
kusimama kutoa ushahidi,….’akasema na kunifanya niishiwe nguvu, kwani nilijua
kikombe hicho kimeshapita kumbe mambo bado na hadi muda huo sikuwa nimefikia
uamuzi kuwa nisimamie upande gani...’nikasema
‘Sasa naona
muda umefika kusema ukweli wote maana siwezi kuapa kwa kitabu kitakatifu halafu
niseme uwongo, mimi siwezi hilo kabisa...’nikasema
‘Sawa, kwani
nani akuambia useme uwongo, ...sema ukweli, lakini uwe ukweli kwa masilahi
yako, ukisema ukweli wa kukuangamiza sijui kama hata mungu atakusamehe...’akasema
‘Mimi
sikuelewi, ina maana ninachotakiwa kusema ni ukweli wa kunipendelea, je kama
unanipendelea mimi na kukuweka wewe hatiani, nitafanyaje?’ nikamuuliza
‘Kama ni
ukweli, ....nijuavyo mimi, hakuna cha kuniweka mimi hatiani, labda uwe
hujatumia akili yako,...nimekuambai ukweli uwe ukweli kweli...siwezi
kukufundisha kila kitu cha muhimu,kwanza jua ni nini unachokifanya, na adui
yako ni nani, maana hapo ujue unapambana na adui...’akasema
‘Adui yetu
ni nani?’nikauliza
‘Hilo swali
la kuniuliza, wewe mwenyewe unawaona, watu ama hawa, ambao wanachukua vidhibiti
na kuvifisha, watu kama hao, ambao lengo lao ni kujijali wenyewe, ...hao ndio
uwaangalai kwa jicho jingine, na hao ndio wauwaji...’akasema
‘Lakini...’nikaanza
kujitetea
‘Hakuna cha
lakini hapa...ukifika sema kila kitu, wao wamekuja kuiba nyaraka, wamezipeleka
wapi...halafu wanakuabidhi mkataba kama huu, mimi ninao mkataba wa awali ambao
ulitakiwa upewe, na humo kuna kila kitu, ikibidi mimi nitautoa kama ushahidi,
wasitubabaishe,..unasikia sema kila kitu...’akasema
‘Mhh, mdada
huoni hapo tutajichanganya, mimi naona muda wa kufanya hivyo haujafika,....’nikasema
‘Wewe
unasubiria muda gani tena...mtu wa ajabu sana wewe, siri ya ushindi ni kuwa
kama unapambana na adui, na mara ukimpatia adui yako nafasi, ...mshindile makonde
ya nguvu ili aishiwe nguvu, ukimuachia hiyo nafasi, atakuja ufahamu udhaifu wako,
...na unakuwa umeshampa nafasi ya kuweza kukuzidi nguvu,....’akasema, na mimi nikawa imiya nikikumbuka maneno ya
mpelelezi
‘Kama
utasimamishwa kabla ya mshitakiwa hajatoa maelezo, uwe makini na ile utakachokielezea,
cha muhimu ni ukweli, huku ukivuta muda, kwani wakati muafaka wa kusema kila
kitu haujafika, ..
‘Wakati gani
muafaka wa kusema kila kitu...?’ nikamuuliza
‘Wakati
mshitakiwa akishamaliza kutoa maelezo yake, hapo utajua ukweli wake, je yupo na
kundi au na jamii,...’akasema
‘Mimi
kwakeli hapo sijui, maana tangu mwanzo unasema niseme ukweli na nafasi ya
kusema ukweli imeshafika, nab ado unaniambia nisubiri, ...mbona mnanichanganya...’nikasema
‘Unajichanganya
wewe mwenyewe, kwasababu kama ungeniambia ukweli wote toka awali mimi ningejua
nifanye nini, na huenda kesi hii ingelishamalizia, lakini wewe na mdada mna
ajenda ya siri,..sijui mna ajenda gani...’akasema
‘Hata mimi
sijui...’nikasema na mara sauti ikasema;
‘Mhasibu
pita mbele na inua mkono wako utoe kiapo cha kusema ukweli...’sauti ikanishitua
NB: Haya ukweli
utaanza kuelezewa
WAZO LA LEO: Ikitokea upo kati kati ya
sintofahamu, kila mtu anataka usimamie upande wake, na wewe unashindwa kujua
usimamie wapi, cha msingi ni kuangalia ukweli
na haki ipo wapi. Usiogope kulaumiwa, kwani lawama hizo ni za muda, ogopa
kujuta kwa kusema yasiyo kweli na haki, kwani majuto huja baada ya athari, na
huwezi kujua athari hiyo itadumu kwa muda gani na ni yupi ataumia.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment