‘Masikini
mhasibu, nilikuona jinsi ulivyokuwa unajikanyaga pale mahakamani, hahahaha,
ujanja wa bure, kumbe huna kitu kabisa, hivi wewe uhasibu huo uliupata pata
vipi, au ndio nyie mlioenda shule kukariri tu...’akaanza kunitania mdada, huku
akicheka kwa dharau.
‘Yaani
badala ya kunipa pole na hongera wewe unanidhihaki...’nikasema
‘Nikupe
pole, wakati ulikuwa aribu uvurunde, huna maana kabisa wewe, kumbe wewe huwezi
kuwa mwanajeshi...’akasema
‘Kwanini
mimi nimekosea nini?’ nikauliza
‘Wewe ngoja
uone nitakavyowajibu siku wakinisimamisha kutoa ushahidi,labda wasifanye
hivyo...’akasema mdada kwa kujiamini.
‘Kwanini
unajiamini hivyo, nikuambie ukweli yoyote atakayesimamishwa pale mbele, ni
lazima atakuwa na wasiwasi, ujue pale hujui utaulizwa nini, na hicho
unachoulizwa huwezi kuwa na uhakika mwenzako ana lengo gani, sio swala la
kwenda shule...’nikasema
‘Nikuambie
siri moja ya kumshinda adui yako, usikubali akutishe kwa macho, pili usimpe
nafasi ya kuchambua kauli yako, tatu, usimsaidie kufikiri..na ukianza wewe
hakikisha hapati pumzi ya kukurudi...’akasema
‘Mhh, mdada
mbona kauli yako ni ya kibabe sana, utafikiri wewe ni askari...’nikasema
‘Hahaha,
masikini mhasibu, kila mtu ni askari bwana, cha muhimu ni kujiamini..ndio fani
hiyo ina wenyewe, kwani ni taaluma inayojitegemea lakini katika maisha ya
kawaida kila mtu ana ulinzi binafsi ambao ngao yake ni kujiamini...sasa wewe
hujiamini, ndio maana ukawa unajianyaga...’akasema
‘Lakini mdada
mimi nilijaribu sana kuwa upande wako, na nimefanya hayo kwa ajili yako,
nimeshindwa kusema ukweli wote kwa kukulinda wewe, ina maana mimi hapo
nimefanya kosa...?’nikasema kama namuuliza
‘Hahaha,
mhasibu usitake turudi nyuma kwenye kauli yangu ya mwanzo, na ujua nasubiri
jibu, na hilo jibu litoke kabla kesi hii haijaisha, ukichelewa tu, utakuja
kunikumbuka na utakuwa umeshachelewa...fikiria kwa makini na uwe na uhakika
nayo, kumbuka maisha yako ni wewe mwenyewe, usikubali kuwa mtumwa wa mtu
mwingine, jiamini....na kama kuna mtu unaona yupo upande wako, hakikisha kweli
anakutahamini..’akasema
‘Mhh, kweli
eeh, ndio maana uliona nilivyokuwa najaribu kuficha ukweli, ukweli ambao
ningeliusema wewe ungelikuwa hatiani...’nikasema
‘Mhh,
mhasibu, masikini...hata siku moja sifikirii kusaidiwa, mimi huwa anjipigania
mwenyewe,...ila ninapenda sana kusaidia watu...wewe unasema umeshindwa kusema
ukweli wote, ukweli upi huo, hebu niambie wewe ulitaka useme ukweli upi, ....?’
akaniuliza na kabla sijamjibu akasema;
‘Sikiliza
wewe mwanaume, Usije ukajifanya wewe unajua kuongea sana, uaongea tu, bila kuwa
na uhakia na hicho unachokiongea, mdomo, utatamka, ..lakini hebu chunga athari
ya kile utakachokitamka, linganisha matamshi yako na ukweli wa hicho kitu na
athari zake,...sione raha kuongea kitu ukitumaini kuwafurahisha watu, kumbe itu
hicho kitageuka kuwa kisu au sumu ya kukudhuru wewe mwenyewe, kuwa makini kwa
hilo hasa katika hii kesi, kuna mengi huyajui...’akasema na kutikisa kichwa.
‘Wewe
unajua, au unasema tu..’nikasema
‘Mhasibu,
usitake niongee sana, ila ninachokushauri ni kuwa makini sana katika kutoa
kauli zako hasa mbele ya mahakama, ni bora ukae kimiya au uongee yale uliyo na
uhakika nayo tu...’akasema.
‘Mdada mimi
inaniuma sana kusema uwongo, na baada ya kumaliza pale moyo wangu ulinisuta
sana, nikawa najiuliza ni kwanini wewe hupendi niseme ukweli ulivyokuwa, hasa
kwenye lile swala la ndevu, kwanini hutaki niseme kuwa wewe ndiye
uliyenivalisha zile ndevu za bandia...?’ nikauliza
‘Mhasibu
ngoja nikusaidie mpenzi wangu, hebu chukilia ukweli halisi, kwa mfano,uneglisema
hivyo, na ukaja kuulizwa ni kwanini ulifanya hivyo ungelisema nini?’ akaniuliza
‘Nitasema ni
wewe ulinishauri hivyo, ili mtoza ushuru asinielewe kuwa mimi ni
nani...’nikasema
‘Wewe
mwanaume kwanini hujiamini, hiyo kauli ya wewe ulisema, huoni kuwa ni ya kitoto
zaidi, jifunze jinsi ya kujitetea, haya, mfano wakakuuliza tena, ni kwanini
ujifiche sura yako, kama kweli ulikuwa katika usahihi?’ akaniuliza
‘Mdada, wewe
ndiye ulinishauri hivyo, mimi sikujua kusudio lao ni nini, ...’nikasema
‘Hapo
umeshaanza ujikanyaga, ...unaona hapo, wahiyo ni heri huo uwongo kuliko ungelisema ukweli,
kwani ukweli huo ungezua hisia nyingi, na wewe ungelionekana mtu wa ajabu sana,
bendera fuata upepo, mtu usiyejiamini, ....na uwe makini kwa hilo, kwani kama
utaendelea hivyo, basi mwisho wa siku wewe utashukiwa mhalafu,. Ni vyema hilo lisifahamike
kabisa kwa yoyote yule, hiyo iwe siri yangu mimi na wewe tu....’akasema na mimi
nikabakia kimiya nikiwaza na nikamuona mdada akitaka kusema kitu mimi
nikamuwahi kwa swali;
‘Hivi mdada,
nikuulize huyu mtu aliyenipiga nyundo mimi na wewe, ni nani?’ nikamuuliza na
yeye kwanza akatabasamu halafu akaangalia pembeni na kusema
‘Mimi sijui,
hiyo ni kazi yao wao kumtafuta...usipende kubeba mizigo ya wenzako yenye utata,
jiamini, nimeshakufundisha hilo’akasema mdada
‘Mimi naanza
kuhisi vinginevyo, huenda ikawa ni kweli....’nikasema
‘Ukweli upi
huo...?’ akaniuliza
‘Kuwa huenda
kweli ni wewe uliyenipiga na hiyo nyundo...’nikasema
‘Mimi sijui
hilo, na wala sijui kulitokea nini kipindi kile, ndio maana sipendi
kusimamishwa pale mahaamani, kwani ninaweza nikapandwa na hasira nikaiharibu
mahakama yote, ....’akasema
‘Ahaa
nimelewa kumbe ndio maana hawataki kukusimamisha weweckutoa ushahidi?’
nikamuuliza
‘Sijui, ....hilo
ni kazi yao, kama wapo tayari wafanye hivyo, mimi siogopi kabisa,ila
wakinisimamisha wajiandae...’akasema mdada akikunja uso kuashiria hasira.
‘Mdada, hivi
wewe unafanya haya yote kwa ajili ya nani?’ nikamuuliza na yeye akaniangalia na
kutabasamu akasema;
‘Nfanya
yaote hayo kwa ajili ya nani,...hahaha mhasibu, ina maana hujui, ni kwa ajili
yangu, ni kwa ajili ya maisha yangu,ni kwa ajili ya kuwakomoa hao wanaojiona
wamefika, mafisadi wakubwa, hao wanakula mali ya wananchi, wakavimba kama
vifutu, wakati wananchi wao wanakondeana, wakizidi kuambiwa wafunge mikanda na
ahadi za maisha bora ya kufikirika,..nilishakuambia hilo, na sijutii kabisa
kuwachukulia hao mafisadi mali yao, ...’akasema
‘Mimi nahisi
kuna mtu unayemfanyia kazi, sio kama unavyodai wewe, na mimi unanitumia kama
njia ya kufanikisha malengo yako...’nikasema na yeye akaniangalia kwa makini huku akichezesha chezesha macho,
halafu akataabsamu, na kusema;
‘Masikini
mhasibu,...kwanini unanifikiria hivyo, hivyo ina maana wewe hdi sasa
hujaniamini kuwa mimi nafanya haya kwa ajili ya watu kama nyie, na zaidi
nafanya haya kwa vile ninakupenda sana...nimefanya mengi wa ajili yako, hata
kuwa tayari kuivunja ndoa yako, ili tu uwe mchumba wangu, hebu jiulize wewe una
nini cha maana saana, ujue mimi nipo kwa ajili ya masilahi zaidi, sasa wewe una
masilahi gani, una nini cha kuitwa tajiri, hebu jiangalia una masilahi gani...’akasema
kwa dharau.
‘Mimi sijui,
yote hayo unasema wewe..’nikasema na akawa kaangalia mbele na uso wake
ulionyesha kuwazia jambo nahisi kuna
kitu kinamkera, halafu akatabasamu, akawa anasita kugeuka kuniangalia, na hali
hii ilikuwa ngeni kwa mdada, mdada mara zote tukiwa na mimi huwa anajiamini, na
anakuwa kama mtu wa kutoa amri kwangu, lakini leo nilimuona tofauti, akasema;
‘Ujue
nimefanya hayo yote kwa ajili yako, huwezi kuamini hilo lakini ipo siku
utanikumbuka, na nimefanya haya kwa vile ninakupenda kwa moyo wa dhati, na hao
wanaokudanganya , wakajifanya wanakupenda, wanafanya hivyo tu kwa vile tu,
imetokea hivyo ilivyotokea, hakuna kingine....’akatulia kidogo.
‘Hata hivyo
napenda kuumbusha kuwa mimi sitakubali mtu mwingine akuchukue hivihivi...yaani
mimi niumie, halafu niwe mshika pembe, hapana...., labda niwe maiti, labda
niondoke...’akasema na kutulia halafu akaniangalia na kusema;
‘Mhasibu,
natumai umeyasikia yangu ya moyoni, labda utaniona mwanamke wa ajabu sana, wa
kumulezea mwanaume hivyo, wakati mwanaume mwenyewe anajifanya hana habari...nimegundua
kitu hasa kutoka kwako, maana wanaume nyie mkipendwa mnajifanya kuringa...sasa ,
nikuulize na wewe, je unanipenda kama ninavyokupenda wewe?’ akaniuliza sasa akiniangalia
moja kwa moja usoni, akiwa hapepesi macho.
‘Mdada, mimi
siwezi kukujibu hilo swali, unataka nikujibu nini, kwasababu wewe unafahamu
fika mimi nina mchumba wangu tayari,...’nikasema na yeye akawa amaetulia kimiya
na nilipoona hasemi neni nikasema;
‘Hebu jaribu
kujiweka katika nafasi yake, halafu utendewe hivyo, hivyo unavyotaka wewe, hebu
jaribu kuhisi,...utajisikiaje,mdada nakuomba, tujaribu kuwa na moyo wa huruma,
namuonea huruma sana huyo binti, .....’nikasema na yeye akageuka na kuniangalia
usoni, nilihisi kama kitu kinapita usoni mwake, akatikisa kichwa, na niliona
machoni kukiwa na kitu kama machozi, lakini sio machozi, akahema.
Aliendelea
kukaa kimiya kama anawaza jambo, halafu akataabsamu, na taratibu lile tabasamu likaanza kuyeyuka,
na uso uliokuwa unavutia ukaanza kujenga sura nyingine, lakini kabla hajafikia
kukasirika kabisa akageuka pembeni na kusema;
‘Unanikatisha
tamaa mhasibu, kwanini hutaki kutoa kauli ya kunipa moyo, kwanini hutaki
kukubali ukweli kuwa hata wewe unanipenda..nafahamu fika kuwa moyo mwako
unanipenda na huyo mchumba wako ni kwa
vile tu, ilitokea hivyo, mkaonana kabla yangu,...kweli si kweli?’ akaniuliza na
mimi nikabakia kimiya halafu akaendelea kusema;
‘Mhasibu ni
vyema ukasema ukweli kabla hujachelewa,
nakuambia hili ili siku moja usije ukajuta, na wakati huo nitakuwa sipo nawe
tena,...’akasema na kutulia na kabla sijasema kitu akanisogelea na kuchukua
simu yake, akapiga picha tukiwa pamoja akasema;
‘Hebu
tabasamu nataka kuweka kumbukumbu ya siku ya leo...’akasema tukatabasamu na
akachukua picha, akawa anaiangalia, na mdada akasema;
‘Kwahiyo
mimi , nataka kusikia kauli yako, niambie moja kwa moja je kweli na wewe
unanipenda kama ninavyokupenda mimi,hebu angalia hii picha tunavyoendana,
nakuambia ukweli , utakuja kunikumbuka na unitafute usinione...’ akasema na
kuniangalia tena usoni
‘Mdada hilo
lipo dhahiri, kupenda kupo, siwezi kukataa, lakini kwa hali ilivyo, mimi sina
ujanja wa kufanya lolote, yule ni mchumba wangu tayari na ameshanizalia mtoto,
na tumeingia kwenye mkataba naye na ni mkataba mgumu ambao mimi siwezi kuuvunja,
unamfahamu vyema baba yake, sasa mimi hapo unataka nifanya nini...?’ nikamuuliza
‘Mhasibu, usitake
kunichefua, au wataka mimi nifanye
kweli, ili jamii ijue kuwa wewe na mimi ni wachumba wa siri, mimi nakustahi sana
wewe, ..baba mkwe wako niliongea naye, nikajaribu kumuelimisha, hilo na
mengineo, lakini kama alivyo, ni mgumu kuelewa, na shauri hilo lipo mikononi
mwako, wewe ndiye mwenye maamuzi, hata hivyo, mbona wao walishavunja huo
uchumba unaodai wewe, ‘akatulia na kuangalia saa yake.
‘Sijaongea
nao, sizani kama uchumba huo utavunjwa kirahisi hivyo, je huo mkataba
tuliowekeana nao utakuwaje, unataka nyumba yangu na kila kitu kiwe mikononi
mwao...huoni kuwa mimi nitakosa kila kitu...’nikasema
‘Mliandikishana
hivyo, unaona hawa watu walivyo..lakini kwa mzazi anaweza kufanya lolote, wewe
ulijifanya kijogoo, ukawa unaparamia mitetea, haya hiyo ndio faida yake...’akasema
na mimi nikainama chini na kusema;
‘Yametokea sasa
ningelifanya nini..hata hivyo hata kazi alinitafutia huyo baba mkwe, unaona
kulivyo pagumu hapo....’nikasema
‘Hahaha,
hata hii kazi ya mtoza ushuru ni yeye aliyekupigia debe,...alikuwa akikuvuta na
alijua akikuweka wewe utafanya kila anachokitaka yeye, lakini sasa maji
yamemfika shingoni,familia yake ina haha huku na kule hadi wa waganga wa
kienyeji, nasikia wanataka kunitupia juju mimi na wewe, una habari hiyo, sio
ajabu maana,kila mchumia janga hula na wa kwao, au sio.....’akasema
‘Nani aumbia
yote hayo?’ nikamuuliza
‘Kaa kama
ulivyo, na bakia na msimamo wako huo, mchumba mchumba, na safari hii
ukiwabembeleza ukamrudia huyo mtu, basi wewe utakuwa mume bwege,...hilo liweke
akilini, maana hapo itakuwa sio mapenzi tena, bali ni kulipa fadhila....’akasema
‘Mdada ni
lazima niongee na hao watu nijue msimamo wao upoje, siwezi kuamua lolote mpaka
sasa, hata kama nakupenda vipi, hata kama wewe unanipenda vipi, lakini ujue
kuna ndoani imenasa kooni mwangu...siwezi kumuacha mtoto wangu....’nikasema
‘Haaaah,
kumbe, ...nimekuelewa, mtoto ndio kikwazo, au?’ akauliza
‘Sio kikwazo
...ila...’nikasita
‘Mimi
nilikuwa nataka kusikia kauli yako tu, ili nijue nipo na mtu ambaye kweli
ananipenda kwa dhati, uchumba sio ndoa,...kama mngelikuwa mumefunga ndoa,
nisingeliweza kulifanya hili, ...sawa mumezaa mtoto, lakini hiyo ilikuwa kwa
bahati mbaya, na unataka kumuoa mtu ambaye huna mapenzi naye, huoni kuwa
utajitaia utumwani, maisha yako yatakuwa hayana raha, na ndio mwanzo, wa
kuchepuka chepuka...kuwa makini na hilo....’akasema
‘Sasa wewe
unataka mimi nifanye nini?’ nikamuuliza
‘Maamuzi ni
ya kwako, na ni bora uchukua maamuzi mapema kabla hujachelewa, wani kesi hii
ikiisha, utabakia kunikumbuka,...siku ya leo iweke akilini mwako, na uyakumbuke
maneno yangu, tuyaache haya, tuongee swala lililopo mbele yetu...’akaangalia
saa yake na mimi nikawa nawaza kauli yake hii ya mwisho ana maana gani kusema
hivyo;
‘Kwanini
unasema nitakuja kukumbuka, kwani una mipango gani?’ niamuuliza
‘Mpelelezi,
anataka kuongea na mimi, sijui anataka uniambia nini, na huyu mtu nimemuona ana
ajenda ya siri, badala ya ufanya kazi yake, anataka kutumia migongo ya watu,
mimi siwezi kumfanyia kazi yake, na kama ananishuku mimi, kwanini hanischukulii
hatua...’akasema
‘Kwani siku
ile hamukuongea naye?’ nikamuuliza
‘Wewe mtu,
kwanza siku ile ulinificha ...hukuniambia kuwa huyo mtu yupo ndani kwako, pili
inaonekaan mna ajenda ya siri nyie wawili, ndio hapo nakosa amani, ina maana
umeshaanza kunisaliti mimi, mhasibu unakumbuka tulipotoka, ...usitake nifanye
yale ambayo utakuja kuniona mbaya, usinilazimishe nifanye jambo nitakalokuja
kujijutia....’akasema
‘Pale
ilikuwa vigumu kukuelezea lolote maana ningelisema lolote angelisikia,
nilijaribu kuonyesha hisia kuwa humo kuna mtu, lakini ukawa hunielewi,
unafikiri mimi pale ningalifanya nini...’nikasema
‘Mimi sio
mtoto mdogo, kazi hii sikuianza leo, nafahamu kabisa kuwa mnakutana mara kwa
mara na huyo mtu, na ameshaupa kazi ya kufanya, kunichunguza mimi ...lakini
kwangu mimi hamtapata kitu, mimi natimiza wajibu wangu kwa jamii, ipo siku
utalijua hilo, ...kwahiyo msipoteze muda wenu sana kunifuatilia mimi, na nazidi
kukumbusha kuwa haya ninayoyafanya kwa namna moja au nyingine yatakuja
kukusaidia wewe...’akasema
‘Kwani
mliongea nini na mpelelezi?’ nikamuuliza na yeye akatabasamu na akatulia kama
anawaza jambo, halafu akaanza kunielezea
NB:
Alielezea nini, hebu tukutane sehemu ijayo
WAZO LA LEO: Kutamka nakupenda ni rahisi sana, na
wengi wanatamka tu, wakiona ni kauli ya kupita tu, lakini kauli hiyo inatakiwa
iwe ni ahadi inayotoka moyoni, ...tulitamke neno hilo tukiwa na yakini ya weli kuwa
kweli tumependa, hatuna shaka, vinginevyo, tutakuwa kwenye kundi la wanafiki,
ambao mara nyingi kauli zao ni za uwongo.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment