Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, May 6, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-51


Nilifika mapema mahakamani,  mdada na mpelelezi walikuwa hawajafika, nikaona nitumie muda huo kusikia watu wanazungumziaje hiyo kesi, nikasogea walipokuwa wamekaa watu wakiongea, nikaanza kusikia mazungumzo yao, huku nikijifanya naandika kitu kwenye simu yangu.

‘Huyu mlinzi wanamuonea tu, amekamatwa kama chambo tu, mapapa waliohusika na haya mauaji wapo wanakula starejhe zao...’akasema jamaa mmoja

‘Ina kweli huenda sio yeye aliyeua...ndivyo unavyoona wewe?’ akauliza mwenzake

‘Inawezakana akawa yeye lakini kwa kutumwa, au sio yeye ila kwa vile inatakiwa mtu akamatwe, basi wakamnyaka huyo mlinzi...ukiangalia kwa makini huyu mlinzi ni mnyonge tu, hebu jiulize kwanini amuue huyo mtoza ushuru, ...’akasema mwenzake

‘Lakini ushahidi unaonyesha wazi, labda useme katumwa, na yeye kama mlinzi aliweza kufanya hivyo kwa ajili ya kumlinda bosi wake, kama alivyoelezea muendesha mashitaka...’akasema mwenzake

‘Hebu niambie kuna tetesi kuwa alifika mtu pale getini kwake, na kumtuma huyo mlinzi, lakini maelezo yamegeuzwa kuwa mlinzi alisikia kelele, ndio akatoka mbio kuona ni kitu gani kinaendelea na hapo akakuta huyo mtoza ushuru anataka kumzuru mdada, akamuwahi kwa risasi...hivi huoni kama kuna utata hapo..’akasema

‘Lakini ukiwasikiliza polisi na maelezo yao mbona mimi sioni tatizo hapo,...yeye kama mlinzi alisikia kelele, akaona ni bora aende kumuona bosi wake, alipofika akakuta hiyo hali unafkiri yeye angelifanya nini...’akawa kama anauliza mwenzake.

‘Kama hayo ni kweli, wanini toka awali huyu mlinzi asikamatwe, akafikishwa mahakamani, kwanini aje kukamatwa sasa hivi?’ akauliza mwenzako.

‘Hiyo ni kazi ya polisi, wanaweza kufanya hivyo kwa makusudi fulani, ili kutafuta kundi nzima, kwa upande wangu mimi sioni tatizo kabisa...’akasema mwenzake

‘Hukusikia kuwa kuna mtu alifika getini, akamtuma huyo mlinzi kuangalia ni kitu kinachoendelea huko ndani, kwanini mpaka aje mtu kumutuma huyo mlinzi, na huyo mtu ni nani, mbona kwenye maelezo ya kesi nzima sijasikia kutajwa....na nikasikia kuna mtu aliyekuwa ndani, aliyewahi kukutana na huyo mlinzi mtu huyo alikuwa an ndevu,.....unakumbuka mwanzoni kabisa kuna uvumi kama huo huyo mtu alikuwa ni nani,..’akawa kama anauliza

‘Polisi wanafahamu zaidi, hizo ni vumi za mitaani, na hizi huchochewa na watu wenye masilahi yao, na wanasiasa wanapata mwanya wa kuweka sera zao, achana nazo kabisa, tunachohitajia ni ushahidi ambao unaletwa hapa mahakamani...’akasema mwenzake

‘Ushahidi unaweza ukatengenezwa, na mashahidi wakafundishwa, hilo lipo na linafanyika sana, nikuambie kweli, siku hizi wenye pesa , wenye utajiri ndio wanatawala, wanaweza kucheza na vipngele vya sheria, kosa likawa sio kosa, na mtuhumiwa akawekwa mtu baki kabisa...wewe utaona tu,...ngoja tusiseme mengi, maana hapa ni mahakamani tusije tukafungwa kwa kuambiwa tumezua....’akasema na wakawa kimiya na watu wakgeuka kuangalia waliokuwa wakiingia, alikuwa mdada, na baadaye akaingia mpelelezi.

Muda wa kesi ulikuwa bado, naona hakimu alichelewa kufika, na nikapata muda wa kuongea na mpelelezi pembeni, mdada hakutaka kuwa na mimi karibi sijui ni kwanini, nikageuka kumuangalia mpelelezi ambaye alikuwa akifungua makabrasha yake, alipoona namuangalia akasema;

‘Vipi mliwahi kuongea na mdada?’ akauliza huku akimtupia mdada jicho, mdada kwa muda huo alikuwa anasoma kitu kwenye simu yake, hakuwa anawaangalia watu, na watu wengi walikuwa wakimtupia jicho, sijui ni kwasababu ya urembo wake, au kuna jingine linaloendelea vichwani mwao.

‘Nilimpigia simu tukaongea naye, kiukweli sikuweza kuongea naye mengi, mdada mara nyingi kwenye simu hataki kuongea sana, na majibu yake wakati wote ni ya makato mkato...’nikasema

‘Lakini nikuulize swali, huyu mdada mpo vipi na yeye, sio kwamba naingilia mambo yenu binafsi, lakini hebu niambie kuhusu urafiki wenu...’ akaniuliza swali na kunifanya nisite kidogo kumjibu, nikasema;

‘Ndio ni kweli ni rafiki yangu,siwezi kulipinga hilo, kuwa yeye ni rafiki yangu wa karibu, lakini pia ukumbuke kuwa huyo ni mfanyakazi mwenzangu , kwahiyo tupo karibu kama ilivyo kawaida ya wafanyakazi, mnapoishi pamoja mnazoeana,na mimi na mdada tumezoeana sana mpaka watu wanatufikiria vibaya...lakini sio kihivyo...kiukweli mnapokuwa ofisi  moja mengi yanaweza kutokea’nikasema

‘Yah, ni kweli hata kufikia kuchumbiana,hiyo inatokea, hata kujihusisha mapenzi ya siri hata kama mna wake au wachumba au sio, hili lipo wazi, lakini kuna hali inayoendelea kati yako na mdada, ambayo inatiliwa mashaka, ...’akasema

‘Kama ipi, kiukweli ndio kama nilivyokuambia, siwezi kupinga ukweli huo kuna mdada ni rafiki yangu, tumezoeana sana, lakini sivyo kama watu wanavyoona, na mimi siwezi kuwazuia wafikirie hivyo, au kutafuta njia ya kupinga wanavyohisi wao, ...kwasababu mimi nina mchumba wangu tayari...’nikasema.

‘Ndio maana nikakuuliza hivyo, je unamfikiriaje huyo mchumba wako, wakati ukiwa na mdada, kiukweli inavyoonekana wewe ni mdada mumefika mbali sana, na hata huyo mchumba wako atakuwa analalamika, je huo uchumba wenu bado upo?’ akaniuliza

‘Uchumba wetu bado upo, na nilitarajia kufunga ndoa karibuni, lakini haya yaliyotokea yameharibu kila kitu, hata sijui jinsi gani ya kulimaliza hili tatizo, ...’nikasema

‘Kwanini, kwani mchumba wako amesema nini?’ akaniuliza

‘Haniamini tena...na wamefikia hatua ya wao kugombana, na hata baba mkwe kuingilia kati,sijaweza kukaa na mchumba wangu kulimaliza hili, nimeona bora niliache kwanza hadi haya matatizo yaishe, hata hivyo, ukweli utabakia pale pale, kwasababu huyo ni mama watoto wangu...’nikasema.

‘Lakini hebu sema ukweli wako, unampenda sana mdada kuliko hata huyo mchumba wako?’ akaniuliza na mimi nikabakia kimiya, sikuweza kumjibu zaidi ya kuinama chini tu.

‘Ni kweli kwa urembo wa mdada, mwanaume yoyote anaweza kughilibiwa hata kama ana mke wake,...na mdada ni mjanja sana anaweza kutumia urembo wake kama mtaji, hata hivyo, nina wasiwasi na huyu binti,nahisi kuna jambo analifanya sio bure, ndio maana nakuuliza kuhusu huyu binti, je mnafahamiana kivipi, kuacha hayo maswala ya kiurafiki?’ akauliza

‘Mimi na mdada ...mmmh, zaidi ni kikazi, na kama ni kutoka nje ni ile hali ya kuondoa mawazo ya kiofisi, na ...unajua mimi nilikuwa sinywi, lakini mdada akanifundisha, nilikuja kuona ni maisha ya kuondoa mawazo, lakini ikizidi sana inaharibu, na ni hatari...sirudiii tena...’nikasema

‘Nilijua tu, mdada ni mjanja sana, ni lazima anaweza alikufanyia jambo ili kukunasa, hebu niambie kuna lolote aliweza kukufanyia, ambalo hukupendezwa nalo, na huenda likakuletea matatizo?’ akaniuliza na hilo swali nahisi alishalifanyia kazi na aliuliza hivyo unitega.

‘Wakati mwingine mdada anafanya mambo kwa mzaha, kuna mambo alinifanyia, lakini ilikuwa ni utani, na nilikuja kumuelewa, sina kinyongo naye, kwanini umeniuliza haya, nahisi kuna jambo unalifatuta au umeligundua...?’ nikamuuliza

‘Hebu niambie ukweli, wewe na mdada mna mpango gani wa kamaisha?’ akaniuliza swali ambalo sikulitegemea

‘Mpango wa kimaisha kama upi?’ nikauliza

‘Uchumba,....urafiki wa karibu, na vitu kama hivyo...’akasema

‘Aaah, hapana huko umekwenda mbali, ni rafiki na mfanyakazi mwenzangu tu, hakuna zaidi, na kama unavyomjua mdada, kweli anaweza kutulia kwa kuitwa mke wa mtu...’nikasema kama ninauliza

‘Nakuuliza hivi nikiwa na maana yangu,nina uhakika kama sio leo, lakini nijuavyo mimi, haitachukua muda utasimamishwa kutoa ushahidi na maswali kama hayo yatakuja kuulizwa...’akasema

‘Kwani hayo yanahusiana vipi na hayo mauaji?’ nikamuuliza

‘Kwao wao hayo ni chanzo cha kila kitu,...wewe utaona tu, ...’akasema

‘Oh, lakini, hapo naona watanitega, na sipo tayari kuyaongelea hayo, unafikiri wanaweza kuniuliza hayo, ....hapana, ni lazima niongee na mdada...’nikasema

‘Uongee naye kuhusu nini, kwani una wasiwasi gani, cha muhimu ni ukweli,...na kama ungenifunulia japo kidogol ningelijua jinsi gani ya kukushauri, je upo tayari kuniambia kila kitu kuhusu wewe na mdada?’ akaniuliza

‘Swali ni hili je hayo sio maswala binafsi, na je yanahusiana vipi na hayo mauaji, ?’ nikauliza

‘Nikuambie ukweli,...chanzo cha hayo mauaji sio kama inavyoonekana kwa sasa, nimefanya uchunguzi wangu wa kina, alichokuwa akifanya mdada, ndio mbinu wanazotumia hawa watu, na walimchukua mdada kwa nia hiyo...sasa kama ulitumbukizwa huko, ni lazima ndada alikufanyia huo ujanja, ndio ukanaswa...’akasema

‘Sijakuelewa,....’nikasema na kumtupia mdada jicho, tutajikuta tunaangaliana akaniminyia jicho, ikanibidi niduwaee, ana maana gani kunifanyia vile, nikageuka kumuangalia mpelelezi, na ambaye alikuwa ndio kainua kichwa, na akageuka kumuangalia mdada, mdada kwa muda ule alikuwa keshainama kuendelea na kile alichokuwa akikifanya.

 ‘Mimi jana niliitwa na wakubwa zangu, kuna msukumo wa kutaka hii kesi iunganishwe na upelelezi wangu, yaani mimi nitoe ushirikiano kwa polisi, ili hili tatizo limalizike kabisa,kwahiyo mimi nikitoka hapa natakiwa nikakae na hao polisi walioshughulikia hii kesi tuone tutasaidiana kivipi...na hapo kuna mabadiliko makubwa yatatokea,...’akasema

‘Na wewe umekubali, je ulishajiandaa kwa hilo...?’ nikamuuliza

‘Hili sio swala la kukubali ni amri, na kama imefikia hapa, ujue kuna mtafutano hapo, sasa ni wakati wa wewe kuongea kila linalofaa ili niweza kukusaidia vinginevyo, usije kushangaa mimi ninakuwa adui wako mkubwa, kama unahusika, sizani kama nitaongea na wewe kihivi..’akasema

‘Una maana gani?’ nikauliza

‘Ok, mimi nimewaomba muda kidogo, ili nimalizie kazi yangu, na huo muda nataka niongee na wewe na mdada, kila mmoja kwa wakati wake, na safari hii nataka ukweli wote...’akasema akiniangalia huku kakunja uso.

‘Ukweli upi tena, mbona nimeshakuambia kila kitu...zaidi ya ...hebu niambie unataka nikuambie kitu gani tena?’ nikauliza

‘Nataka ukweli, jinsi gani ulivyojiunga na mdada, alikufanyia nini...je wewe na mdada mlifanya nini hadi kupata mali kiasi hicho, ukaweza kujenga nyumba ...na yeye akaweza hata kununua gari la bei mbaya,..usifikiri hilo halijulikani, linajulikana sana, na usinidanganye kuwa ni pesa za mshahara, ...hilo sitakubaliana nalo...’akasema

‘Ina maana kila aliye na mali yake anahitajika kujieleza, basi waanza hao wakubwa, kwanini mimi iwe ni tatizo....’nikasema

‘Ni tatizo, hasa yanapotokea maswala kama haya, ...mauaji, amani inakosekana, watu wanasumbuliwa,...dhuluma inazidi, ufisadi inakuwa ni sifa badala ya kuonekana ni kosa..kwa watu wenye nia njema ni lazima tujiulize, ni lazima tujitolee kuyatokomeza haya, hiyo ndio kazi yangu na lazima niifanye kwa moyo wangu wote...’akasema

‘Kaanzie huko kwa wakubwa, kwanini uanzie huku wa wanyonge?’ nikamuuliza

‘Unapotaka kukata mti wenye matawi yaliogemea nyumba, kwanza unahitajika kuyakata hayo matawi yaliyoegemea nyumba, kwani yanaweza kuwa ni hatari zaidi...halafu unakwenda kukata shina,...baadaye unatoa mizizi, au sio?’ akawa kama anauliza na wakati huo kesi ilishaanza.

 Nikageuka kumuangalia mdada, na akanionyeshea ishara kuwa anataka kuongea na mimi, na kwa muda ule mpelelezi alikuwa anaongea na simu, alipomaliza akageuka kuniangalia, na kusema;

‘Wakubwa wananiita,....kuna dharura imetokea huko...’akasema

‘Wakubwa gani?’ nikauliza kwa mshangao, na muda ule nikaona mdada anainuka kuondoka.

NB: Naishia hapa kwa leo


WAZO LA LEO: Ukiwa wewe ni kiongozi, boisi au una wafanyakazi wako, hata wa majumbani, jaribu sana kujali haki za hao watu, je wanapata mahitajio yao muhimu, kuachia mbali mshahara, na je huo mshahara una kidhi haja ya kazi wanayoifanya, je wanavyo vitendea kazi stahiki, wana kinga kwa ajili ya afya zao, je wanapata matibabu wao na familia zao, je upo karibu nao kiutawala.Kama hatutajali haki za hawa watu basi hata utendaji wao hautakuwa mnzuri, watafanya kazi kwa vile ni lazima wafanye, sio kwasababu utendaji unaostahili, na hichi ndio chanzo kingine cha kukosa amani katika jamii zetu.

Ni mimi: emu-three

No comments :