Nilifika
mapema mahakamani, mdada na mpelelezi
walikuwa hawajafika, nikaona nitumie muda huo kusikia watu wanazungumziaje hiyo
kesi, nikasogea walipokuwa wamekaa watu wakiongea, nikaanza kusikia mazungumzo
yao, huku nikijifanya naandika kitu kwenye simu yangu.
‘Huyu mlinzi
wanamuonea tu, amekamatwa kama chambo tu, mapapa waliohusika na haya mauaji
wapo wanakula starejhe zao...’akasema jamaa mmoja
‘Ina kweli
huenda sio yeye aliyeua...ndivyo unavyoona wewe?’ akauliza mwenzake
‘Inawezakana
akawa yeye lakini kwa kutumwa, au sio yeye ila kwa vile inatakiwa mtu akamatwe,
basi wakamnyaka huyo mlinzi...ukiangalia kwa makini huyu mlinzi ni mnyonge tu,
hebu jiulize kwanini amuue huyo mtoza ushuru, ...’akasema mwenzake
‘Lakini
ushahidi unaonyesha wazi, labda useme katumwa, na yeye kama mlinzi aliweza
kufanya hivyo kwa ajili ya kumlinda bosi wake, kama alivyoelezea muendesha
mashitaka...’akasema mwenzake
‘Hebu niambie
kuna tetesi kuwa alifika mtu pale getini kwake, na kumtuma huyo mlinzi, lakini
maelezo yamegeuzwa kuwa mlinzi alisikia kelele, ndio akatoka mbio kuona ni kitu
gani kinaendelea na hapo akakuta huyo mtoza ushuru anataka kumzuru mdada,
akamuwahi kwa risasi...hivi huoni kama kuna utata hapo..’akasema
‘Lakini
ukiwasikiliza polisi na maelezo yao mbona mimi sioni tatizo hapo,...yeye kama
mlinzi alisikia kelele, akaona ni bora aende kumuona bosi wake, alipofika
akakuta hiyo hali unafkiri yeye angelifanya nini...’akawa kama anauliza
mwenzake.
‘Kama hayo
ni kweli, wanini toka awali huyu mlinzi asikamatwe, akafikishwa mahakamani,
kwanini aje kukamatwa sasa hivi?’ akauliza mwenzako.
‘Hiyo ni
kazi ya polisi, wanaweza kufanya hivyo kwa makusudi fulani, ili kutafuta kundi
nzima, kwa upande wangu mimi sioni tatizo kabisa...’akasema mwenzake
‘Hukusikia
kuwa kuna mtu alifika getini, akamtuma huyo mlinzi kuangalia ni kitu
kinachoendelea huko ndani, kwanini mpaka aje mtu kumutuma huyo mlinzi, na huyo
mtu ni nani, mbona kwenye maelezo ya kesi nzima sijasikia kutajwa....na
nikasikia kuna mtu aliyekuwa ndani, aliyewahi kukutana na huyo mlinzi mtu huyo
alikuwa an ndevu,.....unakumbuka mwanzoni kabisa kuna uvumi kama huo huyo mtu
alikuwa ni nani,..’akawa kama anauliza
‘Polisi
wanafahamu zaidi, hizo ni vumi za mitaani, na hizi huchochewa na watu wenye
masilahi yao, na wanasiasa wanapata mwanya wa kuweka sera zao, achana nazo
kabisa, tunachohitajia ni ushahidi ambao unaletwa hapa mahakamani...’akasema
mwenzake
‘Ushahidi
unaweza ukatengenezwa, na mashahidi wakafundishwa, hilo lipo na linafanyika
sana, nikuambie kweli, siku hizi wenye pesa , wenye utajiri ndio wanatawala,
wanaweza kucheza na vipngele vya sheria, kosa likawa sio kosa, na mtuhumiwa
akawekwa mtu baki kabisa...wewe utaona tu,...ngoja tusiseme mengi, maana hapa
ni mahakamani tusije tukafungwa kwa kuambiwa tumezua....’akasema na wakawa
kimiya na watu wakgeuka kuangalia waliokuwa wakiingia, alikuwa mdada, na
baadaye akaingia mpelelezi.
Muda wa kesi
ulikuwa bado, naona hakimu alichelewa kufika, na nikapata muda wa kuongea na
mpelelezi pembeni, mdada hakutaka kuwa na mimi karibi sijui ni kwanini, nikageuka
kumuangalia mpelelezi ambaye alikuwa akifungua makabrasha yake, alipoona
namuangalia akasema;
‘Vipi
mliwahi kuongea na mdada?’ akauliza huku akimtupia mdada jicho, mdada kwa muda
huo alikuwa anasoma kitu kwenye simu yake, hakuwa anawaangalia watu, na watu
wengi walikuwa wakimtupia jicho, sijui ni kwasababu ya urembo wake, au kuna
jingine linaloendelea vichwani mwao.
‘Nilimpigia
simu tukaongea naye, kiukweli sikuweza kuongea naye mengi, mdada mara nyingi
kwenye simu hataki kuongea sana, na majibu yake wakati wote ni ya makato mkato...’nikasema
‘Lakini nikuulize
swali, huyu mdada mpo vipi na yeye, sio kwamba naingilia mambo yenu binafsi,
lakini hebu niambie kuhusu urafiki wenu...’ akaniuliza swali na kunifanya
nisite kidogo kumjibu, nikasema;
‘Ndio ni
kweli ni rafiki yangu,siwezi kulipinga hilo, kuwa yeye ni rafiki yangu wa
karibu, lakini pia ukumbuke kuwa huyo ni mfanyakazi mwenzangu , kwahiyo tupo
karibu kama ilivyo kawaida ya wafanyakazi, mnapoishi pamoja mnazoeana,na mimi
na mdada tumezoeana sana mpaka watu wanatufikiria vibaya...lakini sio
kihivyo...kiukweli mnapokuwa ofisi moja
mengi yanaweza kutokea’nikasema
‘Yah, ni
kweli hata kufikia kuchumbiana,hiyo inatokea, hata kujihusisha mapenzi ya siri
hata kama mna wake au wachumba au sio, hili lipo wazi, lakini kuna hali
inayoendelea kati yako na mdada, ambayo inatiliwa mashaka, ...’akasema
‘Kama ipi,
kiukweli ndio kama nilivyokuambia, siwezi kupinga ukweli huo kuna mdada ni
rafiki yangu, tumezoeana sana, lakini sivyo kama watu wanavyoona, na mimi
siwezi kuwazuia wafikirie hivyo, au kutafuta njia ya kupinga wanavyohisi wao,
...kwasababu mimi nina mchumba wangu tayari...’nikasema.
‘Ndio maana
nikakuuliza hivyo, je unamfikiriaje huyo mchumba wako, wakati ukiwa na mdada,
kiukweli inavyoonekana wewe ni mdada mumefika mbali sana, na hata huyo mchumba
wako atakuwa analalamika, je huo uchumba wenu bado upo?’ akaniuliza
‘Uchumba
wetu bado upo, na nilitarajia kufunga ndoa karibuni, lakini haya yaliyotokea
yameharibu kila kitu, hata sijui jinsi gani ya kulimaliza hili tatizo, ...’nikasema
‘Kwanini,
kwani mchumba wako amesema nini?’ akaniuliza
‘Haniamini
tena...na wamefikia hatua ya wao kugombana, na hata baba mkwe kuingilia
kati,sijaweza kukaa na mchumba wangu kulimaliza hili, nimeona bora niliache
kwanza hadi haya matatizo yaishe, hata hivyo, ukweli utabakia pale pale,
kwasababu huyo ni mama watoto wangu...’nikasema.
‘Lakini hebu
sema ukweli wako, unampenda sana mdada kuliko hata huyo mchumba wako?’ akaniuliza
na mimi nikabakia kimiya, sikuweza kumjibu zaidi ya kuinama chini tu.
‘Ni kweli kwa
urembo wa mdada, mwanaume yoyote anaweza kughilibiwa hata kama ana mke
wake,...na mdada ni mjanja sana anaweza kutumia urembo wake kama mtaji, hata
hivyo, nina wasiwasi na huyu binti,nahisi kuna jambo analifanya sio bure, ndio
maana nakuuliza kuhusu huyu binti, je mnafahamiana kivipi, kuacha hayo maswala
ya kiurafiki?’ akauliza
‘Mimi na
mdada ...mmmh, zaidi ni kikazi, na kama ni kutoka nje ni ile hali ya kuondoa
mawazo ya kiofisi, na ...unajua mimi nilikuwa sinywi, lakini mdada
akanifundisha, nilikuja kuona ni maisha ya kuondoa mawazo, lakini ikizidi sana
inaharibu, na ni hatari...sirudiii tena...’nikasema
‘Nilijua tu,
mdada ni mjanja sana, ni lazima anaweza alikufanyia jambo ili kukunasa, hebu
niambie kuna lolote aliweza kukufanyia, ambalo hukupendezwa nalo, na huenda
likakuletea matatizo?’ akaniuliza na hilo swali nahisi alishalifanyia kazi na
aliuliza hivyo unitega.
‘Wakati
mwingine mdada anafanya mambo kwa mzaha, kuna mambo alinifanyia, lakini ilikuwa
ni utani, na nilikuja kumuelewa, sina kinyongo naye, kwanini umeniuliza haya,
nahisi kuna jambo unalifatuta au umeligundua...?’ nikamuuliza
‘Hebu
niambie ukweli, wewe na mdada mna mpango gani wa kamaisha?’ akaniuliza swali
ambalo sikulitegemea
‘Mpango wa
kimaisha kama upi?’ nikauliza
‘Uchumba,....urafiki
wa karibu, na vitu kama hivyo...’akasema
‘Aaah,
hapana huko umekwenda mbali, ni rafiki na mfanyakazi mwenzangu tu, hakuna
zaidi, na kama unavyomjua mdada, kweli anaweza kutulia kwa kuitwa mke wa mtu...’nikasema
kama ninauliza
‘Nakuuliza
hivi nikiwa na maana yangu,nina uhakika kama sio leo, lakini nijuavyo mimi,
haitachukua muda utasimamishwa kutoa ushahidi na maswali kama hayo yatakuja kuulizwa...’akasema
‘Kwani hayo
yanahusiana vipi na hayo mauaji?’ nikamuuliza
‘Kwao wao hayo
ni chanzo cha kila kitu,...wewe utaona tu, ...’akasema
‘Oh, lakini,
hapo naona watanitega, na sipo tayari kuyaongelea hayo, unafikiri wanaweza
kuniuliza hayo, ....hapana, ni lazima niongee na mdada...’nikasema
‘Uongee naye
kuhusu nini, kwani una wasiwasi gani, cha muhimu ni ukweli,...na kama
ungenifunulia japo kidogol ningelijua jinsi gani ya kukushauri, je upo tayari
kuniambia kila kitu kuhusu wewe na mdada?’ akaniuliza
‘Swali ni
hili je hayo sio maswala binafsi, na je yanahusiana vipi na hayo mauaji, ?’
nikauliza
‘Nikuambie
ukweli,...chanzo cha hayo mauaji sio kama inavyoonekana kwa sasa, nimefanya uchunguzi
wangu wa kina, alichokuwa akifanya mdada, ndio mbinu wanazotumia hawa watu, na
walimchukua mdada kwa nia hiyo...sasa kama ulitumbukizwa huko, ni lazima ndada
alikufanyia huo ujanja, ndio ukanaswa...’akasema
‘Sijakuelewa,....’nikasema
na kumtupia mdada jicho, tutajikuta tunaangaliana akaniminyia jicho, ikanibidi
niduwaee, ana maana gani kunifanyia vile, nikageuka kumuangalia mpelelezi, na ambaye
alikuwa ndio kainua kichwa, na akageuka kumuangalia mdada, mdada kwa muda ule
alikuwa keshainama kuendelea na kile alichokuwa akikifanya.
‘Mimi jana niliitwa na wakubwa zangu, kuna
msukumo wa kutaka hii kesi iunganishwe na upelelezi wangu, yaani mimi nitoe
ushirikiano kwa polisi, ili hili tatizo limalizike kabisa,kwahiyo mimi nikitoka
hapa natakiwa nikakae na hao polisi walioshughulikia hii kesi tuone
tutasaidiana kivipi...na hapo kuna mabadiliko makubwa yatatokea,...’akasema
‘Na wewe umekubali,
je ulishajiandaa kwa hilo...?’ nikamuuliza
‘Hili sio
swala la kukubali ni amri, na kama imefikia hapa, ujue kuna mtafutano hapo,
sasa ni wakati wa wewe kuongea kila linalofaa ili niweza kukusaidia vinginevyo,
usije kushangaa mimi ninakuwa adui wako mkubwa, kama unahusika, sizani kama
nitaongea na wewe kihivi..’akasema
‘Una maana
gani?’ nikauliza
‘Ok, mimi nimewaomba
muda kidogo, ili nimalizie kazi yangu, na huo muda nataka niongee na wewe na mdada,
kila mmoja kwa wakati wake, na safari hii nataka ukweli wote...’akasema
akiniangalia huku kakunja uso.
‘Ukweli upi
tena, mbona nimeshakuambia kila kitu...zaidi ya ...hebu niambie unataka
nikuambie kitu gani tena?’ nikauliza
‘Nataka
ukweli, jinsi gani ulivyojiunga na mdada, alikufanyia nini...je wewe na mdada
mlifanya nini hadi kupata mali kiasi hicho, ukaweza kujenga nyumba ...na yeye
akaweza hata kununua gari la bei mbaya,..usifikiri hilo halijulikani,
linajulikana sana, na usinidanganye kuwa ni pesa za mshahara, ...hilo
sitakubaliana nalo...’akasema
‘Ina maana
kila aliye na mali yake anahitajika kujieleza, basi waanza hao wakubwa, kwanini
mimi iwe ni tatizo....’nikasema
‘Ni tatizo,
hasa yanapotokea maswala kama haya, ...mauaji, amani inakosekana, watu
wanasumbuliwa,...dhuluma inazidi, ufisadi inakuwa ni sifa badala ya kuonekana
ni kosa..kwa watu wenye nia njema ni lazima tujiulize, ni lazima tujitolee
kuyatokomeza haya, hiyo ndio kazi yangu na lazima niifanye kwa moyo wangu
wote...’akasema
‘Kaanzie
huko kwa wakubwa, kwanini uanzie huku wa wanyonge?’ nikamuuliza
‘Unapotaka
kukata mti wenye matawi yaliogemea nyumba, kwanza unahitajika kuyakata hayo
matawi yaliyoegemea nyumba, kwani yanaweza kuwa ni hatari zaidi...halafu
unakwenda kukata shina,...baadaye unatoa mizizi, au sio?’ akawa kama anauliza
na wakati huo kesi ilishaanza.
Nikageuka kumuangalia mdada, na akanionyeshea
ishara kuwa anataka kuongea na mimi, na kwa muda ule mpelelezi alikuwa anaongea
na simu, alipomaliza akageuka kuniangalia, na kusema;
‘Wakubwa
wananiita,....kuna dharura imetokea huko...’akasema
‘Wakubwa
gani?’ nikauliza kwa mshangao, na muda ule nikaona mdada anainuka kuondoka.
NB: Naishia
hapa kwa leo
WAZO LA LEO: Ukiwa wewe ni kiongozi, boisi au
una wafanyakazi wako, hata wa majumbani, jaribu sana kujali haki za hao watu,
je wanapata mahitajio yao muhimu, kuachia mbali mshahara, na je huo mshahara
una kidhi haja ya kazi wanayoifanya, je wanavyo vitendea kazi stahiki, wana kinga
kwa ajili ya afya zao, je wanapata matibabu wao na familia zao, je upo karibu
nao kiutawala.Kama hatutajali haki za hawa watu basi hata utendaji wao
hautakuwa mnzuri, watafanya kazi kwa vile ni lazima wafanye, sio kwasababu
utendaji unaostahili, na hichi ndio chanzo kingine cha kukosa amani katika
jamii zetu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment