Nikiwa nimejipumzisha
kwenye hoteli baada ya shughuli nzito ya mahakamani, nilijilaza kitandani, na
kiuweli akili yangu yote kwa muda huo ilikuwa ikimuwaza mdada, mdada ambaye
alitaka tuongee naye kipindi kesi ikiendelea lakini ikashindikana kwani
mpelelezi naye alikuwa na mazungumzo na mimi, ikabidi nimtumie mdada ujumbe wa
maneno kuwa nipo na mpelelezi,ana maongezi na mimi na akajibu.
‘Fanya
uonavyo, ila uwe makini...’basi hatukuweza kuongea naye tena kwa siku hiyo, kwani
yeye aliondoka mapema, na sikujua anakwenda wapi, au litaka kunimbia nini,
nikabakia kwenye mahakama nikifuatilia hiyo kesi kwani hata mpelelezi naye aliondoka
kama alivyoniambia kuwa kaitwa na wakubwa zake, nikawa najaribu kukumbuka
mazungumzo yangu na mpelelezi huyo;
‘Hawa watu
siwaelewi, wanataka nini, ...ukweli umeshabainika, wao wanaufukia, hii kweli sio
haki, mambo kama haya hayataki siasa....’akasema
‘Ukweli upi
huo bosi unaotaka kufukiwa, wakati mahakama ipo kwa ajili ya hilo?’ nikamuuliza
na hilo neno bosi likamfanya aniangalie machoni na kusema
‘Bosi wako
sio mimi bwana,...’akasema huku akionyesha kwa mkono kuwa niache hilo neno.
‘Aaah,...kwa
hivi sasa wewe ni bosi wangu, ila mimi nauliza kuhusu hiyo kauli yako,
ulivyosema wanataka kuufukia ukweli, ni akina nani na ni ukweli gani huo?’
nikamuuliza
‘We acha
tu,...lakini anyway, nitajua huko
mbele kwa mbele, usijali, kazi zetu hizi zinakutana na mitihani mingi, unaweza
kupoteza muda wangu mwingi, halafu watu wengine wanakuja kuingilia na kusema
hayo mambo yamalizwe kienyeji..., ‘akasema
‘Watu kama
akina nani...?’ nikauliza
‘Unajua kwa
hali kama hii udhalimu hautaisha,...ni lazime tufike mahali tuseme sasa basi,
wadhalimu washugulikiwe, bila kujali huyu ni nani,vinginevyo tukiendelea hivi,
kupindisha-pindisha mambo tutaleta mtafaruku katika jamii, na wananchi
hawatakuwa na imani na viongozi wao...’akasema
‘Kwanini
unasema hivyo, kwani hao wakubwa wako ni akina nani, sio hao hao polisi?’
nikamuuliza
‘Mimi ni
mpelelezi wa kazi maalumu, sio lazima nishirikiane na polisi...ngoja mimi
niende, ila ule mpango wangu wa kuongea mimi na wewe, bado upo pale pale, ni
vyema, tukawa kitu kimoja, ili kuukomesha huu udhalimu, nafahamu ni kazi nzito,
hasa pale siasa zinapojichomeka, lakini, haki ni haki tu, kama sheria inasema
hivi huwezi ukasema sio hivi kwa vile huyu ni mwenzetu, hilo halipo...’akasema
‘Oh, unajua
nimekuwa na wakati mgumu sana mimi, maana watu ninaokuwa nao karibu, ambao
nawaona ni marafiki zangu , wamekuwa kama wananitega, hakuna anayetaka kuniambia
ukweli wa moja kwa moja...inafikia mahali hata sijui ninachokifanya, mwisho wa
siku nashindwa hata kujua nimwambia nani nini...’nikasema
‘Tumia akili
yako, ...na kagua nafsi yako kwanza, kwa kujiuliza je hilo ninaloambiwa ni
sahihi,...kama sio sahihi nahitajika kufanya nini, pili, je hilo nitakalofanya
mimi ni la haki, je ningelitendewa mimi ingekuwaje, je jamii itaneemeka nini na
hilo...cha muhimu usiwe mbinafsi wa maamuzi ya kijamii...’akasema
‘Sijakuelewa
mkuu...’nikasema
‘Utanielewa tu,
cha muhimu, tuwe pamoja, kivitendo, tenda kwanza niliyokuambia, na majibu yake
utayaona baadaye.....’akasema na kuangalia pale alipokuwa ameketi mdada, ambaye
kwa muda huo alikuwa hayupo akasema;
‘Nilikuona
kama mlikuwa mnawasiliana na mdada kwa macho, kuna miadi ya kukutana naye leo?’
akaniuliza
‘Hapana,...alinionyesha
ishara kuwa anatoka, ...’nikasema
‘Hivyo tu
basi...?’ akaniuliza
‘Ndio hivyo
tu mkuu, kwani vipi, ...’nikasema
‘Sawa, kama
unahitajia kuonana naye nenda mkaonane, lakini naona yeye keshaondoka, mtakutana huko hotelini au....?’akasema
kama anauliza
‘Hapana sina
cha kuongea naye kwasasa,...na sijui kama atakuja hotelini, siku hizi ana mambo
yake mengi, hatunani mara kwa mara, ...sasa ngoja mimi nikasikilize kinachoendelea
kwenye hii kesi maana naona itachukua muda, tofauti na nilivyofikiria...’nikasema
‘Yah, ndio
hivyo, tatizo ni kuwa hii kesi imeshaingiliwa, maana imegusa masilahi ya watu,
na hapo hapo siasa imeingia na kuweka kambi,itikadi zimeshika hatamu, na hili
litamfanya huyo mlinzi aozee jela, huenda bila hata hatia,...’akasema
‘Siasa za
chama gani, maana hapo sioni mtizamo wowote wa kisiasa...’nikasema
‘Kwenye
masilahi, kila mtu anatafuta kinga, na hao mafisadi, kinga yao kubwa ni kwenye
siasa, sio lazima awe wa chama fulani, lakini porojo zikizidi, na sheria
ikawekwa pembeni, hiyo ni siasa, ...’akasema
‘Kumbe ni
hivyo...’nikasema
‘Hapo tatizo
ni ubinafsi, kwa mtizamo wa hao watu kwa vile wapo majumbani kwao, wanapulizwa
na viyoyozi,wanaona hayo wanayoyaamua ni rahisi tu,...huyo si atakaa jela tu, baadaye
tutamtoa, lakini hawaoni athari za kibinadamu, huyu mtu ana familia yake
inahangaika huku na kule...haya huyo mtu mwenyewe ana-athirika kisaikolojia,
kiafya..hilo halionekani kwasasa maana mwenye
shibe katu hatamtambua mwenye njaa...’akasema
‘Je hakimu
hana mamlaka ya kuingilia kati na kuona haki ikitendeka haraka iwezekanavyo?’
nikauliza
‘Hakimu
anakwenda kutokana na muendesha mashitaka, kazi yake ni kuona haki inatendeka
kwa ushahidi, vielelezo na mashahidi, ...kama muendesha mashitaka atakuwa
ananunua muda, kutokana na shinikizo fulani, yeye anaweza asijue lolote, na
hataweza kuhukumu tu...’akasema
‘Je wewe una
mpango gani kwa hili, kama hao wakubwa zako wakiamua watakavyo, na sio kwa
jinsi haki ilivyo, kutokana na uchunguzi wako wewe utafanya nini, kwanini
usisimame mahakamani na kutoa huo ushahidi wako ili haki itendeke?’ nikamuuliza
‘Nitajua
huko mbele...kwa hivi sasa ni lazima nikamlishe upelelezi wangu haraka
iwezekanavyo, nikimaliza hiyo kazi, ninachohitajika ni kuwakilisha kazi hiyo kwa
mkubwa wangu, kazi yangu imekwisha,...’akasema
‘Oh, kumbe
huwezi kuuatilia tena kuwa hayo uliyogundua yamefanyiwa kazi..’nikasema
‘Majukumu
yangu yana mipaka yake, mimi nimetimiza wajibu wangu, hata hivyo, nitauma sana,
kama watafanya kinyume cha uchunguzi wangu, lakini siwezi kuingilia kati,..hata
hivyo mimi nina imani kuwa haki na ukweli wakati wote una nguvu, zaidi ya dhuluma...’akasema
‘ Ni kweli
lakini mimi nina mashaka na hilo....maana pesa na utajiri unaweza ukaitengeneza
haki ikawa vingine, na ukweli ukawa tofauti....’nikasema
‘Ni swala la
muda, ..sikukatalii kwa hilo...siku hizi propaganda potofu zinasikika sana
kuliko ukweli..., ni kweli, na ndio maana hadi sasa dunia haina amani, watu
wanauwana ovyo, na kila anayepata mwanya wa kujaribu kuelezea kilio chake,
anajikuta kwenye wakati mgumu, ndio maana wengine wanaamua kutumia kinga za
namna kwa namna wengine hufikia kutumia hata imani zao za dini kufikisha ujumbe
wao...na ukiangalia ni mambo yao binafsi tu, sio dini, lakini wameona ndio
sehemu sahihi ya kufikisha ujumbe wao, na wale wahusikaa kama sio sahihi...’akasema
‘Ndio wengine
wanafikia kuua watu wasio na hatia....?’ nikamuuliza
‘Hilo ni
kosa kubwa sana wanalolifanya,...dhuluma inamfanya mtu aingiwe na chuki,...keshakata
tamaa, anachotaka yeye kwa muda huo ni kulipiza kisasi, na hali hiyo inamgeuza
mtu kuwa mnyama na hata kufanya unyama zaidi ya yale aliyofanyiwa...’akasema
‘Haiwezekani,
...ili iweje sasa?’ nikauliza
‘Ndio hivyo,
kwa muda huo akili imeshaganda,..hasira, chuki, ndivyo vimemtawala, hajali
atakachokifanya, na hapo jamii haitaweza kumuelewa tena na hilo ndilo kosa
kubwa, katika harakati zozote, unatakiwa uweke jamii yako mbele, ufanye jambo
kwa masilahi yao,...baadaye watakuelewa tu, japokuwa jamii inaweza kupotoshwa
na propaganda potofu, na hata kukuona wewe unayetetea masilahi yao ni mbaya....’akasema
‘Sawa bosi,
naona wewe ni mwanaharakati sasa, ngoja mimi niende ndani kusikia ni nini
kinachoendelea kwenye hii kesi...’nikasema
‘Sawa wewe
sikiliza tutapashana habari, japokuwa mimi nafahamu ni kitu gani kitaongelewa hapo
leo na mamuzi ya leo ni nini...’akasema huku akiondoka.
‘Nakusikiliza
wewe...’nikasema
‘Sawa tupo
pamoja...ila ukumbuke ahadi yetu...’akasema
‘Ahadi gani...?’
nikamuuliza
‘Ya
kuniambia ukweli wote, tukikutana mimi na wewe ujiandae kwa hilo, kama utaongea
na mdada kwanza, mimi sijui, cha muhimu ni kuniambia ukweli, sizani kama wewe utafurahi
mtu ateseke au ahukumiwe kisivyo halali,..hata kama kuna shinikizo la namna
gani, lakini sheria ni lazima ishike mkondo wake...’ akasema na kundoka.
************
Nikiwa bado
kitandani nikiwaza , mara bosi akanipigia simu kuwa anataka tuonane naye
ofisini kwake kesho yake...nilifurahi sana kusikia sauti yake, na hakuwa na
muda mwingi wa kuongea naye kwenye simu, na mimi nikamkubalia kuwa nitafika
ofisini kwake kesho yake asubuhi, ili baadaye nikitoka hapo nikutane na mpelelezi.
Kesho yake
asubuhi nikajiandaa kama mtu anayekwenda kazini, na walinzi wakaniuliza na
kwenda wapi, nikawaambia nimeitwa na bosi wangu, ikabidi wawasiliane na
wahusika, na baadaye nikaruhusiwa nikisindikizwa na walinzi wawili, ili
kuhakikisha kuwa kweli nakwenda huko kulikohitajika.
Nilipofika
ofisini , wafanyakazi wengi waliniangalia kwa bashasha, na hata hivyo, sikuweza
kuongea nao, kwani ratiba na muda haukuniruhusu, nikaingia moja kwa moja kwa
bosi wangu, ..kabla ya hapo nilikutana na mhasibu aliyepewa kukaimu nafasi
yangu, tukabadilishana maneno mawili , matatu , halafu nikaingia ofisini kwa bosi.
‘Mhasibu
pole sana na matatizo yaliyokukuta, kiukweli yamenikwaza sana hata mimi, kama
ujuavyo mimi nilishakuandaa uwe mtu wangu, lakini ghafla, haya
yanatokea,....siwezi kukulaumu sana,lakini kwa namna nyingine, wewe mwenyewe
umechangia ...’akasema
‘Kwa vipi
bosi?’ nikauliza
‘Hujiamini,
na huna msimamo,...nikuambie ukweli, kwenye maisha ya kujitegemea, kujiamini na
kuwa na msimamo ni kitu muhimu sana, maana wewe sasa hivi utakuwa na familia
yako, sasa kama hujiamini, kama huna msimamo hutaweza kuiendesha fanilia
yako,...na halikadhalika, katika kazi, utakuwa kiongozi wa kampuni au kundi
fulani, kama hujiamini, na kama huna msimamo, utayumba, na kampuni au kundi
hilo halitaweza kusimama kwenye lengo lenu...unanielewa hapo...’akasema
‘Kwahiyo
mimi siwezi hayo, au?’ nikauliza
‘Kuweza
unaweza, ila kuthubutu, inakuwa ngumu kwako...wengi wanapoteza muda wao,
wanahindwa kuendelea kwasabbu ya kuogopa kuthubutu...naona hata wewe ni hivyo
hivyo...amua,pale unapoona ni sahihi, na utajuaje kuwa ni sahihi, ni kutoana na
taaluma yako...au sio, kama huna utaalamu na hicho kitu unauliza, utaelewa, na
hapo utaweza kufanya jambo kwa kujiamini...matokeao yake utayaona au sio...’akasema
‘Sawa bosi,
naona mimi nina bahati ya kukutana na walimu, kila hatua nakutana na wakufunzi
wa namna moja au nyingine, nashukuru sana bosi....’nikasema
‘Nimekukosa
sana, tena sana, wewe na mdada, hasa niliposikia mumepata akzi nzuri, japokuwa
mdada alinificha kuwa na yeye atakuwa kwenye kazi kwenye vitengo hivyo hivyo,
lakini nilikuja kuambiwa...’akasema
‘Mbona mimi
hilo sijui...’nikasema
‘Kazi siku
hizi ni kujuana,...kubebana,....’akasema huku akicheka, na akainua kichwa
kuniangalia, huku akisema;
‘Niliposikia
hivyo kuwa mumepata kazi sehemu nyeti kama hizo nilifurahi sana, niliona kuwa huenda itakuwa ni neema kwenu,lakini
kwa taarifa nilizozipata baadaye inaonekana kama kuna mchezo mchafu unaotaka kuchezwa, kwa
kukutumia wewe, ..hebu niambie vyema ni kitu gani kinachoendelea?’ akaniuliza
bosi huku akiniangalia moja kwa moja usoni.
‘Bosi
kiukweli hata mimi hadi sasa sijaelewa ni kitu gani hasa kinachoendelea na
zaidi ya hayo, hadi sasa sijaelewa mustakabali wa maisha yangu, kwani hata hiyo
ajira yenyewe niliyoahidiwa,bado sijakabidhiwa na nilichoambiwa hivi karibuni
ni kuwa hilo litafanyika baada ya kesi inayotukabidli kuisha kwani kuna watu
wameweka pingamizi….’nikasema
‘Mhasibu
unakumbuka toka awali nilishakuambia uwe makini na mdada,....sio kwamba namuona
mdada ni mtu mbaya, hapana, yeye ni mtu mzuri, licha ya mapungufu yake
kibinadamu,....unajua nikuambie ukweli, hata mimi bado sijamuelewa sana mdada,
japokuwa nimeishi naye, na ni mfanyakazi wangu, lakini ana mambo mengi ya chini
kwa chini, mpaka unafikia mahali simuaminiamini ni kweni ni mfanyakazi wangu na baba yake ni mwenza wangu katika
biashara…lakini kwa hali ilivyo sasa, naona ni heri aende huko anapokwenda,
sitamuweza tena...’akasema
‘Kwahiyo
hata mimi umefurahia kuondoka kwangu?’ nikamuuliza
‘Wewe
hapana, ...nilishakufahamu na nilijua nikikaa na wewe hatua kwa hatua
nitakujenga, uwe mtu wa kuweza kushika hatamu, lakini mdada akakuteka
mawazo....nikajaribu kukushauri, lakini hukutaka kunisikia, ndio tatizo hapo...’akasema
‘Bosi mbona
mimi nilijaribu sana kukusikia na nikajitahidi kufanya hivyo, lakini mengi
yaliyotokea naweza kusema sio kusudio langu....yametokea tu ili iwe sababu..’nikasema
na bosi akatikisa kichwa kama kukataa, na mimi nikaendelea kuongea,
‘Bosi kwa
ushahidi wa kutetea hoja yangu, hebu angalia kifo cha mtoza ushuru
kilivyotokea, je mimi nilijua hilo litatokea, mimi na wewe tulikwenda kumsaidia
mdada,...,kama unakumbuka kwenda kwangu kwa mdada ni kutokana na makubaliano
yangu mimi na wewe, kwa nia kumsaidia mdada, na tulikwenda wote, ulipoondoa tu
ndio hayo yakatokea,…’nikasema.
‘Hayo ni
matokea ya matendo yenu ya nyuma...na kama hayo mauaji yansingelitokea nahisi
kuwa ungebadilika kabisa, ukawa kama atakavyo mdada....lakini mauaji hayo,
yamezuia kila kitu...’akasema
‘Bosi mbona
uanaongea kama unafahamu mambo mengi kumhusu mdada...’nikasema
‘Mhasibu
hebu niambie kuna kitu gani alichokufanyia mdada hadi ukawa mtumwa wake,sizani
kama unafanya yote hayo anayoyataka yeye uyafanye kwa utashi wako,nahisi kuna
shinikizo jingine, hebu niambie ili tuweze kwenda sawa kama bado unaniamini
kama mshauri wako?’ akaniuliza
‘Bosi hakuna
kitu, mimi na mdada tumezoeana kikawaida tu,na mengi aliyonifanyia baadaye nilikuja
kugundua kuwa ulikuwa ni mzaha tu,ili niwe karibu na yeye, nahisi alinihitaji
mimi niwe mwenza wake, ndivyo mtizamo wangu ulivyo, hata hivyo, bado
sijakubaliana na yeye….’nikasema na bosi akawa ananiangalia tu hasemi neno,
nikaendelea kuonga
‘Bosi
nikuambie ukweli, ukiwa na mdada kama humjulii vyema , unaweza kuhisi
vinginevyo, kuwa huyu binti ni muhuni, ana tabia mbaya, anaringa,...lakini
sivyo hivyo, nimekuja kugundua kuwa mdada ni binti mnzuri tu,...ana utani
mwingi, na ni mtu wa kuona mbali kimaendeleo...bosi kiukweli mdada hajanifanyia
kitu kibaya, cha kunifanya hivyo, kuwa niwe mtumwa wake, hapana, mengi
ninayofanya, nayafanya kwa hiari yangu tu …’nikasema
‘Siamini...hayo
ninayoyasikia, kweli kupenda ni kubaya,...unajua mhasibu, nakuuliza haya
kwasababu nimeongea na baba mkwe wako, na kanilalamikia sana, kuwa wewe
umebadilika kabisa tofauti na jinsi alivyokuwa akikuamini, na hata hicho cheo
yeye ndiye aliyekuhangaikia,...unalielewa hilo..’ akawa kama ananiuliza
‘Baba mkwe
wako alitegemea kuwa utakuwa upande wake, ndio maana akakupigia debe ili
ukipate, lakini umemgeuka na kumsaliti…umekuwa upande wa mdada, ...mdada ambaye
kutokana na kauli ya baba mkwe wako mdada kawa adui ayke mkubwa...sijui kwa
vipi...’akasema
‘Bosi mimi
sijafanya lolote baya, ninachoshangaa ni baba mkwe wangu kuyasema hayo kwa watu
wengine badala ya kuniita mimi mwenyewe
tukayaongea,nikamueleza yangu kwa upande wangu….mimi bado namthamini kama baba
mkwe wangu na ninajali juhudi zake,ndio maana nikakubali hicho cheo…’nikasema
‘Je ni kweli
kuwa wewe na mtoto wake mumeshavunja uchumba wenu?’ akaniuliza
‘Nani kakuambia
kuwa tumevunja uchumba wetu mimi na Binti….bado mimi nafahamu kuwa huyo binti
ni mchumba wangu ikizingatiwa kuwa Binti ni mama wa mtoto wangu…’nikasema
‘Walioniambia
ni baba mkwe wako,na pia nikiwa naongea na mdada alisema hivyo hivyo, niliongea
nao kwa wakati tofauti,kwahiyo hata kama wewe hutaki kuniambia ukweli, lakini
ukweli nimeshaufahamu…sijui ni kitu gani kinachoendelea kati yenu watatu, wewe
mdada na huyo binti, lakini kwa hayo mnayoyafanya mjue mnamuumiza sana huyo
mzee...’akasema
‘Lakini mimi
siyafahamu lolote baya,….’nikasema kiunyonge
‘Sajajua
zaidi, nilitaka kupata ukweli kutoka kwako, lakini naona hilo halitawezekana,
hamna shida...’akasema
‘Bosi ukweli
ndio huo, mimi sijavunja uchumba wangu na huyo binti, kama wamefanya wao, mimi
sijui..’nikasema
‘Haya hamna
shida ila ninachotaka kukuambia kwa sasa ni kuwa kutokana na hali inavyoendelea
kwasasa, na sijui ni nini hatima ya kesi yetu, mimi nimeonelea tufikie hatua
nikutambue kuwa wewe sio mfanyakazi wangu tena, japokuwa hilo tulishaliongelea
kwa mdomo…lakini sasa nataak tulifanye kisheria, unafahamu tena taratibu za
kikasi, ningelifurahi uwe nami, lakini hilo naona halitawezekana tena’akasema
‘Bosi mimi
naona unipe muda...mimi bado nataka kufanya kazi hapa kwako, huko wanapotaka
kunipeleka naona kama wanataka kunitega tu...’nikasema
‘Usijali,
....cha muhimu ni nini kesi yenu itasema...zaidi siwezi kukubeba, maana hata
mzazi hubeba mtoto wake, mwisho wake, anashindwa kumbeba tena, anahitajia huyo
mtoto atembee mwenyewe...sasa naona umekuwa, unaweza kutembea mwenyewe, au
sio..’akasema
‘Bosi,
sikatai, na nisamehe sana kwa kutokuwa mtiifu sana kwako, lakini kiukweli mimi
nimejitahidi sana na nimekuwa nikifanya yote yale uliyonishauri, hata hivyo,
nakiri kila binadamu ana mapungufu yake, huenda mimi kutokana na udhaifi wangu
sikuweza kufikia lengo kama ulivyotaka, ...nahitajia muda, nilikuwa naomba
usichukue hatua zaidi,hadi hii kesi iishe....maana hata hicho cheo cheneywe
kina mizengwe....’nikasema
‘Mhasibu
kama ingelikuwa ni mimi mwenyewe, nisingelichukua maamuzi haya, lakini ujue
kampuni yangu, sipo mwenyewe, nina wenzangu, wawekezaji wenza, na wao wana
kauli zao, na kwa pamoja kwa nia njema wameamua hivyo,...kwahiyo siwezi kwenda
kinyume na wao...wewe kwasasa pigania haki yako, na kesi hiyo ipite, mengine
yatafuata baadaye....’akasema
‘Oh, naona
kama naanza kutupwa, maana kama baba mkwe keshaanza kunishutumu na kuniona
sifai, na hata kuvunja uchumba wangu na binti yake, nahisi mabaya zaidi
yataniandama....sasa na wewe tena ambaye nilishakuona kama mzazi wangu, umeamua
kunitupa, sijui hatima ya haya yote itakuwaje...’nikasema
‘Cha muhimu
ni kupambana, vumilia shida, vumilia matatizo, ukiwa katika msimamo thabiti wa
haki na ukweli...jitahidi sana kusimamia hayo, ..nina uhakika, kama kweli upo
kwenye kutenda haki, ukawa mkweli, utafanikiwa, kwani walisema wahenga, baaada
ya dhiki mara nyingi huwa ni nini....?’ akauliza na mimi nikamwangalia huku nikitamani kulia, na
mwishowe nikasema
‘Ni
faraja....’na hapo simu yangu ikalia,...alikuwa mdada akinipigia.
NB: Tumalize
tusimalize..
WAZO LA LEO: Mungu hana kasoro katika uumbaji
wake, na kila jambo kalifanya kwa makadirio yake, inakuwa ni ajabu binadamu
kuanza kukashifiana kutokana na maumbile ambayo mtu hakuyaomba, kazaliwa hivyo,
kajikuta yupo hivyo, wewe unamcheka, wewe unamkashifu, ...ina maana gani hapo,
ni kuwa wewe unampinga mwenyezimungu. Kumbuka aliyekupa wewe ndiye huyo huyo
aliyemnyima huyo unayemcheka, na kumkashifu, utakuja kuulizwa mbele ya hukumu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment