Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, January 24, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-1


Basi nikapata ajira kirahisi, na kila tukipata nafasi, bosi wangu huyu akawa akinisimulia maisha yake, huko alipotokea na madhila aliykutana nayo, hadi kufikia hapo alipo, akiwa mumiliki wa kampuni yenye wafanyakazi wa kila idara.

Siku  ya kwanza, siku ya pili, siku ya tatu nikawa sasa ni mwenyeji, na mtu niliyeanza kuzoeana naye mapema alikuwa yule dada wa mapokezi, alianza kuniachangamkia sana, kiasi kwamba wengi wakahisi tofauti, hata hivyo kwa yale niliywahi kuyaona siku ile ya kwanza, sikutaka kuwa naye kwa urafiki wa ndani, kwanza alishaniambia ana mchumba, na pili wanaume wanapigana kwa ajili yake.

‘Kaka leo nakuomba unitoe chakula cha mchana.....’nilishitushwa na sauti hiyo, wakati nasubiria ofisi ifunguliwe, nilifahamu kuwa na yeeye ameshafika, lakini sikutegemea yeye kuniomba hivyo.

‘Mhh!, leo?.... hapana, nina kikao na bosi.....’nikamwambia.

‘Lakini kaka kwanini unakuwa kama unanikwepa, kwani unaninaje...?’ akaniuliza.

‘Hapana, unafahamu mimi bado mgeni kwenye kampuni hii, isitoshe mimi sina kawaida ya kuwa karibu sana, na wachumba wa watu....’nikasema na yeye akacheka, sana, na kunisogelea akawa kama ananinong’oneza.

‘Mimi nataka niwe rafiki wako wa karibu, maana unafaa sana...usijali ile kauli yangu kuwa nina mchumba, huyo ni geresha, ....’akasema na mimi nikamwangalia kwa macho yakutahayari. Kwakweli msichana huyu ni mrembo, nahisi ndio maana wanaume wengi walikuwa wakijigonga kwake, lakini mimi sio mtu wa kugombea mapenzi, sikutaka kabisa kuwa na urafiki naye, na nilishakanywa na bosi, kuwa hataki urafiki wowote wa kimapenzi kwenye kampuni yake.

Wafanyakazi wakaanza kuja mmoja mmoja, na mazungumzo yetu yakakatishwa, lakini kabla hatujaachana naye, akanisogelea na kusema;

‘Kumbuka nataka unitoe chakula cha mchana, tafuta njia za kumkwepa bosi wako, bosi, bosi...sio bosi wa kila kitu, ..sisi tunamjulia yule, ana wivu sana...kuna kitu muhimu nataka kukuambia, ...muhimu sana...’akasema na kuondoka.

*********

Siku hiyo kweli nilikuwa na miadi na bosi wa hiyo kampuni, na ya baada ya kazi za ofisini za asubuhi, bosi akaniita ofisini kwake, tulikaa huku tunapata maji, na hapo akaanza kuongea na mimi, ili kuniweka sawa. 

Kwakweli kwa kipindi hicho kifupi, mimi nilimuona ni mtu anayejali wafanyakazi, tofauti na wanavyomuongelea pembeni, sijui labda ilikuwa mimi kwa vile ni mgeni, lakini sikuona hu ubaya wake.

‘Mgeni vipi, naona sasa umeshakuwa mwenyeji, au sio?’ akaniuliza na mimi nikasema.

‘Ni kweli nimeshaanza kuzoea hali ya hapa, ...sio mgeni tena...’nikasema.

‘Kwahiyo nisikuite mgeni, nitakuita mhasibu wangu, inatosha...’akasema huku akinywa maji kidgo.

‘Sawa an mimi nitakuita bosi wangu....’nikasema

‘Tukiwa kazini, nione kama mwenzako, usiniogope kama bosi wako, nawashangaa  sana wafanyakazi wangu, wakiniona utafikiri wameona simba, huo sio utendaji mnzuri wa kazi,kufanya kazi kwa kuogopana ni kutokujiamini,...hali kama hiy inakufanya uwe kama mtumwa, badala ya kuwa mtendaji wa kazi. Mimi huwa najiuliza sana, kwanini ufanye kazi pale unapomuona bosi katokea wakati  hukuwa na mipango hiyo,...

‘Mimi nijuavyo, kabla ya kazi yoyote unakuwa umeshajipanga, nitaanza hiki na kile, kwa utaratibu au ratiba fulani kichwani mwako, nifanye hiki kwanza, halafu kitafuatia hiki, na taratibu hizo hazitakiwi ziseme mpaka bosi atokee, au sio, sasa iweje, umekaa, bosi katokea, mbio mbio, unashika makaratasi, unajifanya unawajibika, huko ni kujidanganya, na matokeo yake ni kuwa ukiondoka watu hawafanyi kazi maana wamezoea kusimamiwa...

‘Mimi nataka ufanye kazi kama kazi yako, kwa kujituma, hata kama mimi sipo, ufanye kazi, ukijua kuwa kazi hiyo ni wajibu wako, au sio..?, ndivyo nilivyofanya mimi, nikajijenga hivyo, hadi leo,...na ukiwa na hula ya kujituma bila kusimamiwa, utafanikiwa sana katika maisha yako, hata ukiwa na kazi yako mwenyewe hutapata shida...vinginevyo, kufanya kazi kwa kuonyesha kuwa unafanya, huo ni unafiki wa kujidanganya mwenyewe...’akasema.

‘Mhh, ni kweli...’nikasema

‘Unaona wale waliopigana siku ile ulipofika, niliwapa barua ya kuwasimamisha kwa muda,  kwasababu walipigana kazini hiyo ni kinyume cha sheria za kazi, lakini pia hawakutaka kusema ukweli, lakini tetesi zikanifikia kuwa kumbe wawili hao, walikuwa wakigombea msichana, ni aibu kabisa...'akasema akitikisa kichwa.

'Mimi nawashangaa watu, yaani watu wazima  na akili zao wanagambana kwasababu ya mapenzi, mapenzi hayagombewi bwana,....mapenzi yanakuja yenyewe, ukiona watu wanagombana kwa ajili ya mapenzi, watu hawo wana walakini, ....halafu cha ajabu msichana mwenyewe  ana mchumba wake, na huyo jamaa yake ni mkali kama nini, ana hasira , ni watu wa huko Mara, sasa sijui, akisikia kuwa kuna mtu anamsogelea mpenzi wake, itakuwaje,...kuna mtu atakuja kupigwa risasi, na jamaa mwenyewe ni askari, lakini aliyekwenda shule.

Sasa wale jamaa,nimesimamisha kwa muda wakajifikirie wanataka kazi au wanataka mapenzi, sisemi kuwa wasiwe na wapenzi, lakini hayo ni nje , baada ya kazi, pili ni makosa kabisa kupigana kazini...’akasema nikijua kafanya hilo kama onyo kwangu.

‘Na huyo binti nimempa barua kali, kuwa maswala ya mapenzi mkiwa kazini ni marufuku, haya yanasababisha watu wasifanye kazi...’akatulia

‘Lakini hawo uliwasimamisha kwa muda, umewasaidia vipi, maana naona kama uhasama wao ni zaii ya mapenzi, mimi nilisikia watu wakisema,  uhasama wao umegusia hata imani zao za dini na siasa...?’ nikamuuliza

‘Nilifahamu kuwa nikiwafanyia hivyo, kutatokea nini, maana haikupita muda nimepokea simu toka kwa waheshimiwa, mmojawapo baba yake ni muheshimiwa fulani , kaanza kwa kunilaumu, hata bila kujua chanzo ni nini...’akasema bila kujibu swali langu, sijui hakunielewa au ana malengo yake mengine, na mimi kama kawaida yangu nikamuuliza swali.

‘Anakulaumu nini huyo muheshimiwa?’ nikamuuliza.

‘Kwanza kaanza kusema kuwa kampuni yangu ina ubaguzi,...’akasema

‘Ubaguzi gani.?’nikamuuliza kwa kushangaa

‘Hakusema ubaguzi gani hata nilipomuuliza, yeye aliendelea kuongea tu.

‘Wewe inaonekana unakiuka taratibu za kazi na ajira,....’akasema

‘Taratibu gani nimekiuka muheshimiwa...’nikamuuliza

‘Unawezaje kuwafukuza kazi watu bila barua za maonyo, uliwahi kuwapa barua za maonyo,hujawahi, kwahiyo wewe hufuati taratibu za ajira na kazi,...’akaniambia.

‘Lakini muheshimiwa mimi sijawafukuza, nilichofanya ni kuwasimamisha kwa muda, kwa amkosa waliyofanya, wakirudi tutakaa nao, ili wajifunze, kama ni maonyo nimeshawaonya sana, kama wamekuambia sijawahi kufanya hivyo, wamekudanganya muheshimiwa..’nikamwambia

‘Eeeh, huyo ni muheshimiwa halafu ukamwambia nini....?’ nikamuuliza pale nilipomuona yupo kimia kwa muda.

‘Usipowarejesha hawo wafanyakazi baada ya siku tatu, nitahakikisha kampuni yako inafungiwa..’akaniambia hivyo.

‘Mhh, sasa hilo balaa, sasa utafanya nini, warudishe kazini?’ nikamuuliza na kumwambia nay eye akaniangalia machoni  kwa muda, halafu akasema;

‘Nakumabia haya ili na wewe ujifunze, kuwa kila jambo lina mitihani yake, usione kuwa mimi ni bosi nina wafanyakazi, ..nina pesa, ukafikiri utakuwa salama, hutakutana na mitihani kama hiyo, ...watu kama hawo wapo sana, na sio kwamba hawafahamu taratibu na sheria, wanafahamu, lakini hulka na siliak zao ni hivyo, kusigishana...’akasema.

‘Eti unaniuliza nitafanya nini, nimeshafanya nilichofanya, hakuna kurudi nyuma, ...nawasubiri hao wafanyakazi warudi kwa muda niliowaambia, na wakirudi nataka barua ya maelezo kwanini walifanya hivyo, na kama hawatatajieleza vyema, nitajua cha kufanya...mimi sigopi, maana nafuata sheria, hii ni kazi , hii ni ajira kama mtu anataka kufanya kazi basi afanye kazi kwa taratibu na sheria,vinginevyo, mimi sitasita kuchukua hatua,...’akasema akonyesha sauti ya ubosi.

‘Mhh, mimi bado nina mashaka, kuhusu huo ubaguzi  aliokuambia huyo muheshimiwa, huoni kuwa labda, ni mambo ya malumbano yao ya kidini na siasa, na huyo muheshimiwa ana chama chake au sio....?’nikamuuliza.

‘Unafahamu jamii yetu kwa sasa inaharibika, na chanzo kikubwa ni kutokuwa makini na mambo yetu, tumekuwa bebdera fuata upepo, ...na hili linanikumbusha ile kauli ya adui ujinga...,  mtu anaweza akawa amesoma vizuri tu, akapata cheti, ...,lakini akili hajaelimika...alisoma akakariri nadharia za wenzake, lakini hakuziingiza kwenye utendaji akaona kweli zinafanya kazi...hili ni tatizo.

‘Sasa basi, kama mtu angelisoma akaelimika hayo yote yasingelitokea, nikuambie ukweli, dini ni sheria za mungu, ni kama sheria hizi za kidunia, lakini dini inagusa sana moyoni, sasa usipokuwa makini ukajua ni kitu gani unatakiwa ufanye kwa wakati gani, wewe utaitikia tu amiini....’ akatabasamu.

Nikuambie ukweli, sio kila mtu mwenye dini anaifahamu dini yake vyema, na sio kila mwanachama wa siasa anaifahamu siasa ya chama chake vyema, na hili ni kosa, wengi wanaufahamu wa juu kwa juu, sio ule wa mapana yake, ndio maana kwenye sheria kuna wanasheria, japokuwa tuna ufahamu kidogo wa sheria, lakini wapo waliobobea  kwenye sheria, wameisomea hiyo nyanja kwa undani zaidi, halikadhalika kwenye dini kuna wanazuoni wake, wameiosomea dini kwa nafasi yake...sasa sisi kila mtu ni mwanasiasa, kila mtu ni mtaalamu wa dini, tunajidanganya,...

‘Mimi ninashangaa sana iweje kila mtu anafahamu sheria za dini, anajinadi na kulumbama hata kitabu cha dini chenyewe hakijui , hakipo mkononi, unaongea unabishana,..halafu upo ofisini, mnabishana , mnalumbana, na mwenzako, unapoteza muda wa kazi amba utakuja kulipwa, huoni hapo unamnyinya mwajiri wako, hil hatulioni.

‘Sikatai watu wasiulizane mambo ya dini, ni kawaida, hata mimi naweza kukuhoji kutaka kujua,..na kila mtu ana ufahamu wake wa yale mambo ya kawaida  ya dini yako na utendaji wa ibada na matendo mema, lakini sio kwenye malumbano,sio kwenye hukumu, huko kuna utaalamu wake, hiyo kazi wanatakiwa waifanye viongozi wa dini..nimewaambia wafanyakazi wangu, na nakuambia na wewe malumbano ya kidini sehemu ya kazi ni marufuku...’akasema.

‘Sasa hawa watu wameanza kunitishia,  kuwa watanionyesha jeuri yangu..kuwa eti ni mbaguzi, kuwa eti....hata siwaelewi.’akasema huku akionyesha kutahayari usoni

‘Wamekuambia watakuonyesha Jeuri gani..na ni akina nani hao?’ nikamuuliza

‘Sijui ...nmeona karatasi imeandikiwa, labda wanataka kunishitaki au kunivizia nyumbani wanipige, lakini mimi siogopi mtu, kwa vile nafahamu fika nipo kwenye sheria, sijamfanyia mtu ubaya...’akasema

‘Nimekuelewa bosi, pole sana...’nikasema

*********

‘Sasa ngoja nikuelezee kidogo historia yangu;

‘Mimi ni wa pili katika familia ya baba aliyekuwa na wake watatu, na mama yangu mzazi  alikuwa mfanyakazi wa hospitalini na akiwa kazini akakutana na baba wakapendana wakaoana. Mama akabatika kupata watoto wanne, wa kwanza akiwa mwanaume, wa pili mimi na wawili chini yangu, wote wakiume. 

Kwahiyo katika tumbo la mama yangu nilikuwa mwanamke peke yangu.

‘Ulijisikiaje kuwa mwanamke peke yako?’ nikamuuliza

‘Wakati mwingine kiutoto, unaona kama umeonewa vile, kwani utaona watoto wa kiume wakiwa na michezo yao ya kiume kama mpira wa miguu, na mimi nataka nicheze, wananikataza, ...kuna kazi nyingine unaambiwa ni zako wewe mwanamke, wanaume wanakuwa hawazifanyi...

‘Wewe ni mwanamke, huwezi,...’wananiambia, nikitaka kucheza mpira na wao, lakini mimi naona naweza, kwahiyo wakati mwingine inakuwa ni ugomvi, lakini kaka zangu walinipenda

 ‘Maisha ya kuanza kuishi mbali na mama yangu mzazi, yalianzia pale nilipokuwa na umri wa mwaka na nusu, kwa jinsi nilivyohadithiwa na mama yangu  mkubwa, maana yeye ndiye aliyenilea nikiwa mdogo hadi miaka minne...’akasema.

‘Nasikia mama wa kambo ni wabaya sana vipi mama yako huyo wa kambo?’ nikamuuliza.

‘Kwa jinsi mama yangu huyo mkubwa alivyonilea siwezi kumtofautisha na mama yangu mzazi, na sikuweza kufahamu kuwa mama wa kamb ni wabaya. Mama yangu huyo, alinipenda sana kama malikia ndani ya nyuma...’akasema.

‘Hukutamani kurudi kwa mama yako, maana ulikuwa mdogo sana?’ nikamuuliza.

‘Kwakweli mwanzoni kabisa ule uhali wa kumkosa mama ulikuwepo, lakini sio sana kutokana na mama huyo alivyotulea,kwahiyo nilipapenda sana nyumbani kwa mama mkubwa kuliko hata sehemu yangu niliyozaliwa, na hii ni kawaida kwa mtoto,hujenga mapenzi na kupazoea pale alipolelewa zaidi ya pale alipozaliwa....’akasema.

‘Sasa kwanini mlichukuliwa kwenda kuishi na mama yenu mkubwa?’ nikamuuliza

‘Mimi na ndugu zangu, tulichukuliwa kwenda kuishi na mama mkubwa kwasababu mama alishikwa na ujauzito, na mimi nilikuwa mdogo sana, umri wa mwaka mmoja na nusu, kwahiyo nilihitajia mtu wa kunilea, siwezi kukumbuka vyema maisha ya udogo wangu, zaidi ya kuwa mama mkubwa alikuwa mama mzuri sana, na hakuwahi kutunyanyasa, hata siku moja, hadi nikafikisha miaka minne.

Nikiwa na umri wa miaka minne, baba akatuchukua na kwenda kuishi tena na mama yangu mzazi, na kwa vile nilishazoea maisha ya nyumbani kwa mama mkubwa, ilinipa taabu sana kuyazoea maisha mengine, japokuwa huko ni kwa mama yangu mzazi,...Maisha yalikuwa magumu sana kipindi hicho, maana kipato cha mama, na sisi wanne, hakikudhi haja, ilikuwa ni hali ngumu kwa ujumla, lakini tulizoea maana ni kwetu ni kwetu.

‘Kwani baba alikuwa hatoi pesa ya matumizi....?’ nikamuuliza

‘Alikuwa akitoa, lakini kilikuwa kiasi kidogo, shughuli zake hazikuwa kubwa sana,...’akasema

‘Baba alikuwa na mke mwingine wa tatu, yeye alikuwa na afadhali kidogo ya maisha,,,’akasema , na kusubiria kama nitauliza swali, na alipona sijauliza swali akaendelea kuongea;

Maisha ya uke wenza yana mitihani yake, hasa pale wanawake wanapokuwa na tabia za ubinafsi, ,mama mwingine, mke wa tatu wa baba, alikuwa na tabia yake mwenyewe, sikuwa nimemfahamu vyema kabla, mwanzoni nilikuwa nahisi mama wote wana tabia moja, tabia ya upendo kwa watoto, kama alivyokuwa mama mkubwa.

Mimi niliombea na mama yetu huyo mwingine awe na tabia kama za mama mkubwa. Na kwa vile pale kwa mama tulikuwa tunaishi maisha ya shida hali ngumu , baba akasema  mimi na kaka yangu mkubwa twende tukaishi na mama yetu huyo.

Sikufurahia sana kumuacha mama, na wadogo zangu wengine, maana mama ni mama yako, lakini kutokana na nakama za kimaisha tukaona aheri twende huko tukabadili mazingira, nikiwa na kumbukumbu za mama mkubwa , kuwa hata mama huyo huenda akawa mnzuri kama mama mkubwa.

‘Unaposema mlikwenda ina maana mama zako hao walikuwa wakiishi mbali mbali sana, kiasi cha kusafiri?’ nikamuuliza.

‘Ndio, ... mama mkubwa alikuwa akiishi huko mikoani kusini, mama huyo mdogo alikuwa akiishi hapa kwenye mka huu,  lakini mjini, na sisi tulikuwa tukiishi huko kijijini ,  mwanzoni tulikuwa pamoja na baba, lakini baadaye baba akaenda kuishi na mama huyo mdogo mjini, ambapo wana mgahawa na biashara nyingine.

*********

‘Mama sisi tunakwenda kwa mama wa kambo....’nikamwambia mama yangu siku tuliyoambiwa kuwa tunakwenda kuishi na mama huyo wa kambo, mke wa baba yangu. Nilishangaa kumuona mama hana raha usoni, sio kawaida yake, ikabidi nimuulize mama.

‘Mama mbona huna  raha, ...kwasababu tunaondoka au kuna tatizo jingine?’ nikamuuliza
‘Wanangu nimeongea na baba yenu na yeye akaona iwe hivyo, muende mkaishi  huko mjini, ili muweze kusoma vyema, kama mnavyoiona hii hali hapa nyumbani, chakula chenyewe ni cha shida, na mnatakiwa kusoma, ...’akasema mama akionyesha uso wa huzuni.

‘Lakini mama mbona unaonekana kama huna furaha, ?’ nikamuuliza mama.

‘Aaah, wanangu, siwezi kuamini kuwa huko mtaishi kwa amani,na inanisikitisha kuwa watoto wangu mumekuwa wakutangatanga,leo hapa kesho kule, na mnapoondaka hapa, mimi nitabakia niwaza sijui huko mtaishije, sijui mnafanywa nini, ni kawaida kwa mzazi...’akasema mama.

‘Mimi usiwe na wasi wasi na sisi...’akasema kaka

‘Lakini yote maisha, na ninachotakiwa kukifanya ni kumkabidhi mungu, yeye atawalinda, nyie jitahidini sana kuishi vyema na mama yenu huyo, muheshimuni  na ishini vyema na wenzenu...’akatuambia.

‘Mama usiwe na huzuni, mimi nafahamu mama huyo atakuwa mzuri tu, mbona mama mkubwa alitulea vizuri sana..’nikasema nikikumbuka maisha yetu na mama mkubwa ambaye alitulea kama watoto wake wa kuzaa.

‘Wanangu binadamu wote sio sawa....lakini msiwe na wasiwasi, mungu atawasaidia..’akatuambia
Basi safari ikafika tukaagana na nilimuona mama akitokwa na machozi, lakini kwa kipindi kile sikujua mama ana maana gani, mimi na kaka yangu tukaondoka.

Unafahamu tena utoto, furaha yetu ilikuwa kusafiri, na sehemu yenyewe  tunayokwenda ni mjini,bsi mioyoni mwetu tulikuwa na hamasa tele, ...hata wadogo zangu walikuwa wakililia na wao waende, lakini baba alisema tunaotakiwa kwenda  ni sisi wawili tu. Mimi na kaka yangu .

Tukaingia kwenye basi, tukaondoka, tukiwa hatuna ufahamu ni maisha gani tunykwenda kukabiliana nayo huko mbele, na mara kwa mara nilikuwa naiona taswira ya mama yangu akiwa na huzuni, lakini baadaye usingizi ukanishika, nilijikuta naamusha na kuambiwa tumeshafika...

NB: Karibuni kwenye kisa hiki kipya , natumai tutajifunza mengi


WAZO LA LEO: Tusipende kubishana na kuingia kwenye malumbano kwa mambo tusiyokuwa na ufahamu nayo vyema, kwani kila jambo lina taratibu zake, na misingi yake, na watu wake wa kuyasemea.Ndio maana kuna wanasheria, madakitari wahasibu, wanasiasa nk, sio kila mtu ana ufahamu wa kila nyanja. Ukijiafanya unajua sana, 
Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Keep this going please, great job!

Stop by my web site - their website (rayfordmpvk.blogs.experienceproject.com)