‘Kwanini wewe mwanaume hukutaka hukunipeleka chakula cha machana...?’
nilishitulia na swali kutoka kwa mwanadada wa mapokezi. Niliinua uso
kumwangalia mwanadada huyo, na kugeuza kichwa changu haraka, kuangalia upande mwingine, halafu nikageuka tena kumwangalia tena, safari hii kwa mashaka, na yeye alipona hivyo, akasimama ule mtindo wa niangalie tena.
Moyo wangu ukaanza kunienda mbio,hali hiyo imekuwa ikinitokea, maana tangu
nimuone huyu mdada siku ile ya kwanza , nimekuwa sina amani moyoni, na kila mara nikikutana naye, nahisi moyo
kunienda mbio, na kutokuwa na msimamo wa kimawazo, sizani kuwa ni muwasho washo
wa upendo, kuwa labda moyo wangu umetokea kumpenda, hilo halikubaliki akilini,
japokuwa kweli ni mrembo ana mvuto, lakini siwezi kusema nimeshampenda huyu
binti, ...
Sasa sijui kwanini nakosa raha, kila nikikutana na huyu
binti, na inavyoonekana hata yeye keshanifahamu hivyo,na ndio maana anataka kunichezea,
nikasema kimoyo moyo;
‘Hutaniweza wewe dada ushinde kabisa...mimi nina mchumba
wangu ambaye karibni nitafunga naye ndoa...’nikasema kumbe ile sauti ilitoka
bila kujijua.
‘Eti unasema nini..?’ nikasikia nikiulizwa
‘Hapana, nilikuwa njiuliza akilini kwanini mrembo kama wewe
hujaolewa...?’ nikasema
‘Kwasababu wanaume wa siku hizi wanaringa, wanachotaka wao
ni kuwaharibia wasichana maisha yao, lakini sio kwa nie njema...’akasema
‘Kwanini mkubali kirahisi?’ nikamuuliza
‘Kwasababu wanaume ni waongo, na wanawake ni waaminifu,
wanawaamini wanaume, kumbe wanaume hawaaminiki...’akasema
‘Swali bado lipo pale pale, kama mnafahamu hivyo kwanini
mkubali kirahisi?’ nikamuuliza
‘Achana na maswali yako yasiyo na tija, sogea huku nataka
kukuuliza swali moja...’akasema na mimi nikasogea hadi pale alipokuwa amekaa,
na mara akasimama, akawa kama anajiangali, nikafahamu kwanini anafanay hivyo,
alitaka nimsifie, mimi nikabakiwa nimeduwaa, mdomo ulikauka mate ghafla
Mwanadada huyu alikuwa kavaa nguo ambayo licha ya kumbana,
lakini ilikuwa ikionyesha sehemu zake za ndani kwa asilimia kubwa, nikageuka na
kuangalia pembeni. Yule mwana dada kuona hivyo akatoka pale kwenye kiti chake
na kuja hadi aple niliposimama, akanisgelea na tukawa sambamba, tumeangaliana
uso kwa uso;
‘Hivi wewe mwanaume gani, ..unyeogopa wanawake....?’ akasema
na kunipitisha kidole shavuni, taratibu.
‘Sikiliza dada yangu, sio wote wenye tabia kama
unavyofikiria wewe,mimi naheshimu sana kauli yako uliyoitoa mwanzoni...’nikasema.
‘Kauli gani?’ akaniuliza akionyesha uso wa mshangao
‘Kuwa wewe una mchumba wako...’nikasema na yeye akacheka
sana, hadi akainama, halafu akageuka kuniangalai usoni, ....halafu akasema;
‘Huo ni ushamba tu, ...hapa ni ofisini, unatakiwa uchangamke
na wenzako mtindo wa kujificha ofisini ukajifanya una chapa kazi sana
hautakufikisha popote, wangapi walifanya hivyo, na sasa hawapo,...’akasema.
‘Walifanya nini na wamekwenda wapi?’ nikamuuliza
‘Maswali maswali...mimi sipenzi tabia yako ya kuuliza uliza
maswali kama polisi...’akasema
‘Sinataka na mimi nifahamu....’nikasema
‘Walikuwa wakipendekeza kwa bosi, kazi na wao, ilipofika
siku ya kupunguzwa wafanyakazi, wakawa ni wa kwanza kwenye rodha ya kutolewa, ....waliokuja
kubakia kazini ni watoto wa wakubwa,na sisi tunaofahamu jinsi gani ya kuishi na
watu ....tuulize sisi tukufundishe mbinu za kufanya kazi..’akasema
‘Mbinu gani hizo za kufanya kazi?’ niiamuuliza
‘Fanyakazi, kukiwa na kazi na kama bosi anaihitajia hiyo
kazi, na kama bosi hayupo, huhitajiki kujiumiza kichwa, unapanga mambo yako,
hivi wewe huna mambo yako binafsi, miradi, utajiendeleza, maana mshahra wenyewe
hautoshi, sasa...lazima ujipange, na muda wa kupanga mambo yako ni wakati bosi
hayupo, akirudi aah, kama sio wewe unajibaragaua kama vile upo bize..., bosi anakuona unajituma,
kwanini ujiumize, kwanza bosi atajuaje kuwa unafanya kazi....kosa kubwa ni la
kwao, hawalipi wafanyakazi haki ya jasho lao....’akasema na mimi nikakumbuka
bosi alivyosema;
‘Mimi nataka ufanye
kazi kama kazi yako, kwa kujituma, hata kama mimi sipo, ufanye kazi, ukijua
kuwa kazi hiyo ni wajibu wako, au sio..?, ndivyo nilivyofanya mimi, nikajijenga
hivyo, hadi leo,...na ukiwa na hula ya kujituma bila kusimamiwa, utafanikiwa
sana katika maisha yako, hata ukiwa na kazi yako
‘Huo ni mtizamo wako, usio na tija,....kufanya kazi namna
hiyo ni sawa na kujipendekeza, huwei kuleta mafanikio katika malego ya utendaji
bora..’nikasema na yeye akaniangalia kwa makini, halafu akabenua mdomo wa dharau,
na kusema
‘Achana na upuuzi huo, unameshaanza kunichefua, Sasa
sikiliza, leo nimealikwa na rafiki yangu chakula cha jioni, nataka wewe uwe
mwenza wangu...’akananiambia
‘Kwanini usiende na mchumba wako?’ nikamuuliza
‘Mchumba, mchumba, mchumba...., mimi nimekuambia wewe,
...kwanini kila ninalokuambia kitu wewe unakimbilia kummtaja huyo unayemuita mchumba,
who is mchumba by the way, to hell with
him, offcourse, mnatakiwa mfahamu
hivyo mabwege kama nyie,.....’akaniambia na mimi nikamwagalia kwa mshangao kwa
kauli yake hiyo.
‘Kwani yule sio mchumba wako, kama ulivyosema siku ile....?’
nikamuuliza
‘Sitaki maswali, unanisikia, jiamini mwanaume.....nawachukia
sana wanaume wasiojiamini, kweli wewe utaweza kutoka na mwanamke mkaenda sehemu
, sehemu ambapo kuna wanaume wa kweli,...nina mashaka na wewe....jiamini
mwanaume...’akasema huku akitoboa na kidole kifuani.
‘Kwahiyo wewe unataka mimi nifanye nini?’ nikamuuliza
‘Sasa sikiliza kama wewe ni mwanaume kweli,....nataka haya
yafutayo, ...ujiamini, hasa ukiwa na mrembo kama mimi, pili usiwe bahili, tatu,
na ni muhimu, kama kweli unataka uendelee kuwepo kwenye hii kampuni, basi
nisikilize mimi, ...’akasema na kunisogelea uso wake ukawa karibu na wa kwangu,
nikageuza kichwa changu pembeni.
‘Wanaume wengine wa ajabu kweli, mnapendwa lakini
hampendeki....shiiit’akasema na kugeuka kutka kuondoka na mimi nikamuuliza.
‘Hebu nikuulize kitu, kwanini unafanya hivyo, maana siku ya
kwanza tu kufika, niliona wanaume wanagombana kwa ajili yako, na sasa
wamesimamishwa kazi kwa muda,...bado unanitaka na mimi na umeona tangazo la bosi
kuwa hataka maswala ya mapenzi kazini, inaonyesha una ajenda fulani ya siri, na
hata hivyo,wewe unataka kuwa na wanaume wangapi?’ nikamuuliza
‘Mimi sijaolewa, sina mipaka ya nani awe na mimi kwa muda
gani, hayo ni maamuzi yangu...na kwanini useme nitakuwa na wanaume
wangapi....mwanaume kwangu ni kama Banzoka, natafuta ikiisha utamau
naitema...unasikia sana....’akasema, na mara gari ambalo nafahamu ni la huyo mchumba
wa huyu mdada, likaja na kusimama, akatoka huyo jamaa ambaye nimesikia kuwa ni mchumba
wake, alikuwa na mfuko, nahisi kuna kitu anamleta huyo mchumba wake.
Alifika hadi pale tulipokuwa tumesimama, , akamsogelea huyu
mchumba wake akambusu kwenye shavu, halafu akageuka kuniangalia, aliniangalia
kwa muda mrefu, bila kusema neno,akakunja sura , na sura yake ilikuwa ya
kutisha, hasa macho yake, halafu
akamgeukia kwamwangalia mdada, na kusema;
‘Ndiye huyu eeh,..?’ akauliza na huyu binti hakusema neno, kwani mlango
ulifunguliwa na boasi akaingia, na yule jamaa alipomuona huyo bosi akageuka
kuondoka, na wakati huo huo huyo binti akakimbilia kwenye kiti chake na kuanza
kujifanya anafanya kazi, na mimi nikageuka na kutembea kuelekea ofisini kwangu
huku akilini nikijiuliza huyo jamaa ana maana gani kuuliza vile... ‘Ndiye huyu eeh,..?.
Bosi kumbe wakati anaingia alituona, tukiongea, kwani
baadaye aliniita na mangezi yake yalilenga huko.
‘Nakuona siku hizi upo karibu sana na huyo mdada, ...’akaniambia,
kama ananiuliza
‘Hapana, sivyo hivyo, ...tulikuwa tunaongea tu...’nikasema
‘Uwe makini sana na huyo mdada, ...nakupa kama onyo, sio
kwamba nakuonya kwa sababu ya sheria za kazi, au nataka kukuingilia katika
maisha yako binafsi, nakuonya kwa vile namfahamu sana huyo mdada,tabia yake, na
mtu wake,ambaye keshatambulikana kuwa ni mchumba wake, utakuja kuingia kwenye matatizo, na mimi
sitakuwa na nafasi ya kukufuatilia, ...’akasema.
‘Samahani bosi, kwahiyo akiniita au akitaka tuongee
nimkatalie?’ nikamuuliza
‘Sijasema hivyo, ila wewe kama mtu mwenye akili utafahamu
jinsi gani ya kumwambia, ...nikuambie jambo, maisha ya kazini, kila mtu ana
akili yake, na hapa kazini kila mtu kaja, na maombi yake na anajifahamu kwanini
yupo hapa, ....sasa usije ukamfuata mtu,
ambaye hujui nini lengo lake, hujui ana kusudio gani akilini mwake...’akaniambia
na mimi nikamuitikia kwa kichwa.
‘Maisha yalivyo, kuna watu ambao nia yao ni kuhakikisha wengina
wanaharibikiwa, au kutaka wengine wafanye watakavyo wao, hata kama wanafahamu
kuwa hicho wanachokushauri wewe hakina manufaa,au kitakuja kukuleta madhara...akilini
mwake, ana kauli ya shauri lako, sasa kama mtu uliyepevuka kiakili ni kazi yako
wewe unayeshauriwa kuchuja hayo mwenzako anayokushauri, kuna wengine wana
ushauri mzuri, lakini kuna wengine leng lao ni kama wachawi...’akaniambia.
‘Kama wachawi...?’ nikauliza kwa mshangao.
‘Wachawi, lengo lao ni kutaka wengine
wasifanikiwe,....kuwaharibia watu malengo yao...na tabia ya marafiki kama hao
ni hivyo hivyo...uwe makini ...’akasema.
‘Oh, kumbe...!?’ nikasema na kabla sijatoa kauli yangu
akasema;
‘Kuna watu walikuja hapa, wakajitahidi sana kufanya kazi,
lakini wakaja kuvutwa na ushauri wa kupotoshwa na wenzao, wakajiingiza kwenye
tabia chafu, za hadaa na hata wizi, anasa, starehe, sasa hivi wapo mitaani
wanajuta. Cha msingi unapokuwa kazini, kwanza fahamu wewe ni nani, na
unafanyanini, na kwanini ufanye hivyo,
ikiwa na maana unafahamu misingi na kanuni za kazi yako. Ukifahamu hivyo, hata
aje nani, hata kama ni bosi wako, hutayumba, kwani unajua ni nini
unachokifanya.
‘Ni kuambie ukweli kazi ndio msingi wa maisha yako, na
familia yako, na kila mtu ana malengo yake, huwezi kujua ni kwanini mwenzako
anakushauri hivi au vile, huenda anakushauri hivyo ili uharibikiwe, na
ukiharibikiwa, kimoyoni keshafanikiwa, maana yeye ni mchawi, ....ana roho na
tabia za kichwi, ukiwafuata hawo, mwisho wa siku utajua, na majuto ni mjukuu,
kwahiyo chunga sana ushauri wa watu wenye nia mbaya...’akaniambia
‘Bosi nashkuru sana kuwa na wewe, maana kila siku najifunza
maisha...’nikasema
*******
Kipindi cha machana, bosi akaniita, na kuniuliza nina kazi
kwa sasa, nikamwambia kazi nilizokuwa nikifanya nimemaliza, akasema;
‘Sasa basi, ngoja tuendelee na kile kisa cha masiha yangu,
kama unakumbuka, tuliishia pale mimi na kaka yangu tuliposafiri kwenda kwa mama
wa kambo, baada ya baba kuamua kuwa
tuondoke pale twende mjini, kwani maisha yetu kijijini yalikuwa magumu sana.
Tuliondoka kwa usafiri wa basi hadi mjini, ...ndio hapo
tulipoishia...
Ilikuwa ni muda wa jioni, na wakati tunafika, mama huyo wa
kambo alikuwa kakaa sebuleni, akisoma gazeti, alipotuona, akawa kainama huku
anaendelea kusoma, nikaona ajabu maana mama yangu akimuona mume wake anakuja
atamkimbilia na kumpokea mzig, lakini sivyo alivyofanya huyo mama.
‘Mke wangu hata kutupokea hutaki...’akasema baba.
‘Aaah, nimechoka, kazi za hapa nakuwa kama mtumishi wa
nyumba,...’akasema huku akiniangalia mimi na kaka yangu kuanzia kidole cha
mguuni hadi kichwani.
‘Hawa ndio nani, mbona wachafu hivi...’akasema akikunja pua,
kama vile kaona uchafu fulani.
‘Ina maana umewasahahu watoto wako....’akasema baba.
‘Watoto wangu,...mmh, sina watoto kama hawa, hebu wapite
maana harufu za majash yak zinanikera, hivi wanaoga kweli hawa....’akasema kwa
dharau.
‘Wametoka safari, safari za mabasi yetu unazifahamu,
wataoga, watatulia, ..ni watoto wako sasa,....’akasema
‘Yaani umeamua kwenda kunichukulia mizigo huko kijijini,
mimi ndio yaya wa kulea watoto wa wengine, yeye ake huko anastarehe, mimi
nahangaike kulea ...hapana sasa naona wewe
umenichoka, .....’akasema huku akisimama na mimi nikaazna kuingiwa na wasiwasi,
maana hata salamu hatujatoa tumeshaanza kusimangwa.
‘Mke wangu tulishaliongealea hili, hawa watoto, wanatakiwa
kusoma, na mimi nimeona ni bora niwe na hawa watoto karibu, ili nihakikishe
wanasoma, na wanakua katika maisha bora, kule kijijini watakuwa hawapati masomo
yanayostahili, na pili hawa ni wakubwa, sio watoto wa kukusumbua kichwa chako,
na wewe nakuamini utawalea vyema...’akasema baba.
‘Aaah kumbee, umeshaniona mimi ndiye mlezi wa machokoraa...,
haya tutaona...mimi ndio jalala la watoto wa wenzangu, ...tutaona,...’akasema
na kuinuka kuondoka, na sisi tulikuwa tumesimama wala hatujui tufanye nini.
Baba akatuambia tuingie ndani tuweke mizigo ndani,...
‘Huo uchafu wenu tafuteni pa kuuweka,...’mama akasema
alipona tunaingia na mizigo yetu, na baba akatuambia tuweke hiyo mizigo yetu
kwenye chumba ambacho kilikuwa ni stoo ya kuhifadhia vitu vibovu vibovu...
Mimi hapo hapo nikaanza kumkumbuka mama, nakaikumbuka ile
taswiara ya mama akionyesha uso wa huzuni, na kuniashiria kuwa mama alikuwa
hana raha kwa vile alifahamu huyu mama atakuwa hatupendi,...nikatamani nirudi
nyumbani, lakini isngeliwezekana tena.Mama huyu wa kambo alikuwa muda wote
katununia, hata ukimsalimia anaweza asikuitikie, hata akikuitikia anakuwa kama
kalazimishwa, tukajitahidi hivyo hivyo kujiweka karibu na yeye lakini ilikuwa
vigumu sana.
‘Huyo mama wa kambo hakuwa na watoto wengine?’ nikamuuliza
bosi wangu huyo.
‘Alikuwa nao, alikuwa na watoto watano, wakike watatu na
wakiume wawili..’akasema.
‘Na wewe kipindi hicho ulikuwa na miaka mingapi?’
nikamuuliza.
‘Kipindi hicho mimi nilikuwa na umri wa miaka saba, kwahiyo
nilikuwa mtoto mwenye akili timamu, na unavyofahamu watoto wa kijijini umri
kama wangu nilikuwa nafahamu kaz zote, kupika, kufagia na kzi zote muhimu, ..’akasema.
‘Mlipofika hukuwakuta hawo ndugu zako, na walikupokeeni vipi?’
nikamuuliza.
‘Mhh, hao ndugu zangu, walituona kama wavamizi, tulionekana
kama wakimbizi,, watu waliokuja kuvamia nyumba ya watu....hatukopokelewa kwa
amani, japokuwa watoto wakikutana haichukui muda kuzoeana, na kugombana kwa
hapa na pale.
‘Hawo ndugu zetu, walizoea kunipiga, lakini kaka yangu
alikuwepo kunitetea, na kila mara wanasema kwa mama yao, na mama yao anakuja
juu, kuniona mimi ndiye mkorofi.
‘Nyie washamba, njooni huku....’alikuwa mmoja wa ndugu zetu
tuliowakuta na mimi sikukubali nikamwambia
‘Mshamba nani?’ nikamuuliza kwa hasira.
‘Nyie si mumetoka kijijini huko, washamba tu...’akaniambia
na mimi sikukubali, nikaanza kujibishana naye, na yeye akanishika kutaka
kunipiga, sikukubali,...nikamjibisha, na kufanya vile ikawa kosa, kilio
kikasikika, cha nguvu, kama vile nimemuumiza.
Mama kwa haraka akaja na kuuliza kuna nini, yule mtoto
akasema mimi nimempiga, na kumuumiza jicho, akawa analifuta jicho kwa nguvu ili
lionekane jekundu, mama akanisogelea akashika shavu langu, akalivuta na
kuniinua juu, fikiria shavu linavuta mpaka unainuka juu, nikagugumia kwa
maumivu, na kilichofuata ni kibao kilichoziba masikio yangu, hadi nakahisi
ukiziwi.
'Mamaaaah,....upo wapi mama....'
Nikaanza kulia, nikiita mama yangu..
‘Kimiya wewe...kimiya kabisa, wewe una tabia mbaya,
nilishasikia sifa zako mkorofi sana wewe, na hapa umefika, nitahakikisha
unanyooka,...’akaniambia huku akisukuma na kidole machoni kwangu. Nikaanza
kumkumbuka mama, na sikuwahi kufikiria kuwa mama anaweza kukuchukia kiasi kile.
Na niliona dhahiri kuwa mama huyo hanipendi, na kwa ilivyo, alitakiwa kuuliza
tatiz lipo wapi, lakini yeye alikimbilia kunipiga mimi na kuniona mimi ni
mbaya, akamuona mtoto wake ndiye mkweli.
Siku zikaenda hali ilikuwa hiyo hiyo, na mimi nikageuzwa
mfanyakazi wa ndani, kila kazi ilikuwa ni mimi, kufagia kuosha vyombo, ndugu
zangu hawakugusa kitu, labda baba akiwemo, ndio wanajifanya wanajituma hata
mama anajifanya kuwatuma na kuwaambia wanisaidie kazi.
‘Nyie msaidieni dada yenu kazi...hamuoni dada yenu ni mvivu,
kila kazi mfanye nyie, tu, leo nay eye afanye hizo kazi, lakini msaidieni
kidogo’atawaambia na wao kama wanafahamu ishara hiyo toka kwa mama yao
watajifanya wanafanya kazi na kujifanya kunielekeza kazi, kama vile mimi sijui
hizo kazi, wakati muda wote nizifanaya mimi, na baba kama baab mwingine
akauliza
‘Vipi, hawa wanaendeleaje hapa...?’ akauliza akiniangalia
mimi na kaka yangu, na mimi nilimuangalia baba kwa jicho la huzuni, lakini
sizani kama alinielewa, yeye akageuka kumwangalia mpendwa wake.
‘Najitahidi kuwanyosha, maana inaonekana huko watoto huko walipotoka
walikuwa wanadekezwa sana, hawajui hata kazoo moja, kazi ni kunivunjia vyombo,
ndani kuchafu, kila ukifagia , dakika mbili hakutamaniki, sasa mimi hapa sitaki
mchezo, ni lazima wawe watoto wema, nitawanyosha kweli kweli...’mama anasema
akinitolea jicho mimi.
‘Lakini mama yao anasema ni watoto wema sana , wanajituma...na
mimi nimekaa nao wanajua akzi sana, hakuna kazi huyu mtoto asiyoifahamu kupika
kufagia ....sasa iweje abadilike kama unavyosema?’baba akasema.
‘Anawatetea tu,...na nyie wanaume muda mwingi mpo kwenye
kazi zenu, na vijiweni, mtafahamu vipi tunavyohangaika na watoto, watoto kama
hawa wanajifanya kufanya kazi wakiona baba yao yupo, kinafiki, lakini kama
haupo, utaongea weee mpaka sauti inakauka, nimewaambia ndugu zao, wawafaundishe
kazi, maana wanatoka kijijini, hawajui kazi nyingine, kuna kazi za kijijini,
lakini hapa ni mjini , kuna usafi wake, vyommbo vioshwe vikaushwe , viwekwe
kabatibi, si kusambaza samabza vyombo kama kijijini....’akasema.
‘Basi ni vyema, wafundisheni, ....’akasema halafu
akanigeukia mimi na kusema
‘Mnasikia nyie sitaki mdhama hapa, fanyeni kazi na wenzenu,
sikilizeni mama yenu anavyowaelekeza, ni lazima mfaham kazi zote, ili mkiwa
wakubwa muweze kujihudumia,...’akasema baba, na mimi sikuwa na la kusema nikawa
kimiya. Na myoni nikawa namkumbuka mama, na machozi yakawa yanakaribia kunitoka
‘Kaka yako alikuwa hakusaidii kazi hizo?’ nikamuuliza
‘Kaka yangu alikuwa akinionea huruma sana, alikuwa
akijitahidi kunisaidia kazi, lakini siunafahamu kazi nyingi za ndani kunai le kasumba
ya kusema ni kazi za kike, kwahiyo kwa asilimia kubwa kazi zote nilikuwa
nafanya mimi, kama msichana, kupika kuosha
vyombo, kufagia, ...’akasema
‘Sasa shule ulikuwa ukienda saa ngapi, au mlikuwa hamjaanza
kusoma?’ nikamuuliza.
‘Kipindi hicho nilikuwa nimeshaanza shule, kwahiyo mimi
ilinibidi niamuke asubuhi sana, nifanye usafi wa nyumbani, nioshe vyombo kabla
ya kwenda shuleni, nashukuru kaka yangu mkubwa alikuwa akinisaidia kazi, kama
za kufagia, lakini hata hivyo, kazi
karibu zote zilielekezwa kwangu...’akasema.
Basi maisha ndivyo yalivykuwa na ndivyo nilivyokaribishwa
hapo...’akaendelea kusimulia maisha yake.
‘Wewe mchafu sana, nilishakuambia ukiamuka asubuhi sitaki
kuona uchafu, uoshe vyomb vyote ufagie, na hakikisha nguo za ndugu zako ni
safi...’akaniambia mama, na mimi sikuwa na la kufanya ni kuitikia
‘Sawa mama...’ huku nikijitutumua, mwili hauna nguvu maana
kazi ni nyingi ukilinganisha na umri wangu, na baya zaidi unafanya kazi huku
unasimangwa, mateke, wakati mwingine fimbo, unafinywa, shavu na sikio lilijaa majeraha ya kufinywa, nikawa nalia ,
namkumbuka mama, hata hivyo ningefanya nini....
Hali ilivyozidi kuwa mbaya, ikabidi nimuulize kaka yangu ;
‘Kaka hivi tutaishije maisha haya mpaka lini, mbona sisi
tunanyanyaswa hivi...?’nikamuuliza kaka
‘Mdogo wangu inabidi tuvumilie tu, tutafanyeje na baba ndio huyo
sizani kama atatusikiliza hata tukimwambia,...’akasema na kweli baba hakuliona
hilo, maana muda mwingi yeye alikuwa huko kwenye shughuli zake, na tuliogopa
tukimwambia tutaonekana sisi ni wavivu. Ikabidi tuvumilia maisha hayo ya shida,
lakini hali ilivyozidi mimi nikamwambia kaka yangu.
‘Mimi nitamwambia baba, nimechoka...’nikasema
‘Wewe unajitakia matatizo, baba hatakuamini, ni bora
uvumilie tu, nitakuwa nikikusaidia kazi ...’akanionya kaka yangu.
‘Hapana ni lazima nimwambie baba..mimi nazidi kuumia, na
nachoka , hata shuleni naishai kusinzia,.....’nikasema
‘Vumilia tu...’akasema kaka yangu, na wakati tunaongea mara baba
akatokea..
Inaonekana siku hiyo alikuwa na mapumziko, au alikuja hap
nyumbani kwa dharura akatuona tukiwa tumesimama wawili, mimi nikawa naendelea
na kazi za usafi, nikisubiri wakati muafaka,nimwambie baba, nilishaamua ni
lazima nimwambie baba ukweli, kaka alikuwa kama anaogopa ogopa.
‘Mimi nitamwambia baba....’nikasema na kaka akanivuta tutoke
nje, lakini sikukubali, na ile halai baba akaiona na kutuuliza;
‘Nyie vipi mbona mumesimama hapa...hamna kazi ya kufanya?’
akauliza na tukawa tunaangaliana mimi na kaka yangu kila mmoja akimtegea
mwenzake aongee, na nilifahamu kaka hataongea kitu, mimi nikaamua kuongea...
NB: Je baba aliwasikiliza na je ni kitu gani kilitokea...
WAZO LA LEO:
Wazazi tuwe makini katika malezi ya watoto, ubaguzi wa watoto hujenga chuki
isiyoisha myoni, tuelewe kuwa unavyomtendea mtoto wa mwenzako vibaya ndivyo
hivyo hivyo mtoto wako atakuja kutendewa, kwani dhambi nyingi malipo yake ni
hapa hapa duniani.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Kisa hiki kina mafunzo mengi sana ningefurahi kama walezi wengi wangesoma ....najiuliza kwa sauti sijui ni kwa nini watu wanakuwa na chuki kiasi hiki? Tupo pamoja ...
Post a Comment