Siku hiyo
mimi nilichelewa kidogo , kwani kuna kazi nilipewa na bosi, kwahiyo nikajikuta
nipo mwenyewe ofisini, nikaharakisha mpaka nikamaliza ile kazi, nilipomaliza,
simu yangu ya mezani ikalia, na ni ilionyesha ni namba za humo humo ofisini, kuashiria
kuwa kuna mtu mwingine yupo ofisini nikapokea nijua pengine ni walinzi wanataka
kujua kuwa bado nipo na wanakagua usalama.
‘Hujamaliza
kazi zako wewe mwanaume, mimi nakusubiria....’sauti ile ilinishitua na
kunifanya mwili uishiwe na nguvu, sikutarajia kabisa kuisikia sauti hiyo kwa muda
kama huo, kwani nilijua siku hiyo
imepita salama, na nimeshaikwepa ile ahadi ya mdada kuwa tuwe naye kwenye
chakula cha usiku, nilishamwambia kuwa haitawezekana kwa vile nina kazi
nimepewa na bosi.
‘Kazi gani
hiyo ya kufanya hadi usiku wa manane?’ akaniuliza
‘Kazi za
kawaida, nikitoka hapo nitakuwa nimechoka, sitataka kwenda mahali popote...’nikamwambia.
‘Tutaona,
...ukimaliza mapema ni lazima tuonane...’akasema
‘Sijui...’nikasema
nay eye akasonya na kukata simu.
Nilipoiskia
hiyo sauti, ikavuruga ubongo wangu, nikawa sipo kawaida, na hapo hapo nikaanza
kujiuma uma na kuongea kwa kigugumizi.
‘Ina maana
na wewe ..ba-bado..u-upo ofi-sini, unafanya nini?’ nikauliza nikishikwa na
kigugumizi.
‘Haya yote
nimeyafanya kwa ajili yako, leo mwili wangu unakuwaza wewe, siwezi siku hii
ipite hivi hivi, bila kuguswa na wewe,...’akasema.
‘Sasa unafanya
nini ofisini muda kama huu, yaani umekaa hapa ofisini kwa ajili yangu?’
nikamuliza.
‘Wewe usiwe
mjinga, mimi sio mtoto kiasi hich, kulikuwa na kazi ya bosi kanipa niifanye,nikaichelewesha
makusudi, niliposikia kuwa wewe una kazi umepewa...kwahiyo leo upo na mimi wewe
mshamba...’akasema na kucheka kwa dharau.
‘Hivi wewe
kwanini unanitakia matatizo...?’ nikauliza.
‘Matatizo
gani wewe, ...ina maana wewe hunitamani huu mwili wangu wenzako wanapigana hata
kutaka kujiua kwa ajili yangu, ina maana wewe hujisikii lolote kwangu,
usinidanganye, nakuona jinsi gani unavyopata taabu ukiniona, sasa, unaonaje
mipango ilivyojileta yenyewe, nataka kuuona huo uanaume wako, maana
nilishakutilia mashaka...mshamba mkubwa wewe’akaniambia huku akiendelea kucheka
kwa kulainisha sauti.
‘Kwahiyo unataka
kufanya nini, ina maana kweli umedhamiria mambo yako ya ajabu ajabu, kweli wewe
mwanamke, wanawake wenzako wanajiheshimu, mbona wewe upo hivyo...usinitakie
balaa....’nikajitetea huku nikianza kuwazia sura ya huyo mchumba wake, na kauli
ya bosi kuwa huyo jamaa sio mtu wa mchezo, ikinijia akilini. Nilikaa kimiya mara
huyo binti akasema;
‘Umemaliza
kazi nije huko, au unakuja hapa nilipo..?’ akauliza na mimi nikajikuta
nikimuuliza
‘Kwani wewe
upo wapi....?’ nikamuuliza nikitaka kujua yupo ofisi ipi, ili nitafute upenyo
wa kumtoroka, kwani nilifahamu kabisa hayupo sehemu yake ya mapokezi, lakini
nafahamu anahitajika nimchukue na pikipiki yangu hadi kwake, kama hajamuambia
mchumba wake ampitie.
‘Nipo chumba
cha mikutano, kuna kazi nilikuwa naifanya kwa ajili ya mkutano wa kesho, wewe
unaweza ukaja tukakiwekea baraka hiki chumba, nimefanya kazi kubwa sana, na
sasa hivi nimetoka kuoga, nilikuwa najiweka sawa, ili ...mmh, ushindwe mwenyewe...’akasema
kwa sauti ya kulegeza.
‘Wewe
mwanamke una balaa...’nikasema huku nikiharakisha ili nitoke haraka mle ofisini
nikimbilie nje, nikamsubiria huko,nafahamu huko walinzi wapo, hataweza
kunifanyia vituko vyake, na nilipohakikisha nimezima taa na kila kitu kipo
sawa, nikafungua mlango wa ofisi yetu na kutoka nje, kulikuwa kimiya, ni kama muda
wa saa moja moja moja hivi kwahiyo huko nje giza lilishatanda.
Nilipomaliza
kufunga mlango nikageuka kwa haraka sasa nikijiandaa kukimbilia nje, nikajikuta
naangaliana uso kwa uso na huyu mdada, akiwa kajiiremba sijui hiyo kazi kaifanya
muda gani, na ajabu alikuwa kavaa khanga moja, sijui kama hiyo khanga alikuwa
nayo, au ndio hizo alizokuwa akiztumia kwa ajili ya kupambia huko ukumbi wa
mikutano.
‘Hivi
wewe..wewe. ...mbona umevaa hivyo, kama
upo nyumbani kwako, huoni kama ukionekana hivyo, utafikiriwa vibaya, na kwanini
unafanya hivyo..?’ nikauliza huku macho yakivinjari ule mwili uliokuwa
unaonekana kupitia kwenye ile khanga nyepesi. Macho yakawa ya kwanza kutekwa na
ibilisi.
‘Nimeshakuambia
siku ya leo nimejiandaa kwa ajili yako, ....ushindwe mwenyewe, kama wewe ni
mwanaume kweli...’akasema akinisogelea, nilikuwa kama nimeshikwa na bumbuwazi, sikuweza hata kusogea nyuma, na wakati huo
mdomo ukawa mkavu, nikapitisha ulimi kwa haraka,na lile tendo likamfanya huyo
binti atoe taabsamu lake ambalo lilikuwa likizidi kuniumiza.
Sio siri
huyu binti alikuwa kajaliwa uzuri wa hali ya juu, ni kama wale warembo wa dunia,
kaumbika vyema, na kila anachokifanya ni kama kimepangiliwa, ..nashindwa
kuelewa kwanini msichana mrembo kama huyu anafanya mambo ya aibu kama hayo.
Tabasamu
lake likanitoa akili ya kawaida ya kibinadamu, ni kama alifahamu kuwa akifanya
hivyo, atakuwa kanilogezea, akili ikawa sio yangu, na kwa muda huo akawa ananisogelea karibu na taratibu akaweka
mikono yake laini kunishika kiunoni, na mkono wake ukawa umegusa mkono wangu
kabla haujashika kiun changu, ule mguso wake, ulinifanya niwe kama mtu
aliyeguswa na umeme, nikatetemeshwa mwili mnzima, nikazidi kupotewa na ufahamu
wa kupambana na majairibu hayo,..
Huyu binti alipoona
nimetulia, akatoa mikono yake kiuononi, akaanza kunifungua shati langu vifungo,
huku analivuta kulitoa nje, nilikuwa nimechomekea vizuri shati langu, na mara nyingi nipo hivyo,wakati
huo akili ilikuwa sio yangu, nilikuwa kama nimezama kwenye giza nene, na akili
haikuwa inafanya kazi.
Wakati
ibilisi anataka kuniteka akili yangu, mara mlango wa nje ukagongwa, kwa haraka
akili ikanirejea, nikawa kaam nimezindukana kutoka kwenye ndoto ya ajabu, na kwa
haraka nikageuka na kutizama huku na kule, na yule mdada, akawa ananitzama
usoni kwa macho yake malegevu, hakujali huyo aliyegonga mlango.
Mimi kwa
haraka kama mtu aliyefumaniwa japokuwa hatukuwa tumefika mbali, lakini shati
langu lilikuwa limeshafunguliwa vifungo, na sehemu kubwa ilikuwa imechomolewa, kwahiyo
nikawa nafanya akzi ya kuichomeka vyema huku nahangaika kufunga shati langu
vifungo, lakini kabla sijafika mbali ule
mlango ukafunguliwa, na aliyekwua kasimama mlangoni ni yule yule mchumba wa
huyo binti, akiwa na mavazi yake ya kikazi na mknoni kashika silaha..
********
Kumbe jamaa
huyu ni polisi kweli, siku zote akija hapa ofisini kumleta huyu binti anakuwa
kavalia kiraia, na uutamfahamu kuwa anafanya akzi hiyo kutokana na gari lake,
na ukakamavu wake, alikuwa na mwili ulioshupaa, na kuonyesha misuli yenye
nguvu, na macho makali...
Mimi nikawa
nimesimama kama mtu aliyepigwa na ganzi, nilijikuta natoa macho ya uwoga, yule
jamaa hakusema neno, akasogea kati kati ya chumba, kwanza akanitupia mimi jicho,
huku akinishangaa kwa jinsi nilivyokuwa nimemuangalia kwa macho ya uwoga, halafu akageuka kuangalia kule alipkuwa
kasimama mchumba wake, na alipomuona jinsi alivyovaa, akageuka kuniangalia,
akasema;
‘Hebu
niambieni ni kitu gani kinaendelea humu ndani, ndiyo kazi mliyokuwa mnafanya..eeh,
ni uvaaji gani huo, kama watu wapo chumbani, angalia hili lijamaa, linaonekana
kabisa limetokea kufanya ufusuka...?’ akauliza huku akiniangalia halafu akageuka
kumwangalia huyo mchumba wake.
‘Mimi
nilikuwa na kazi zangu bwana sivyo kama unavyofikiria wewe, sio kila mtu ni
fusuka, naomba uniombe radhi....’nikasema.
‘Nikuombe
radhi, ...nikuombe radhi wewe, fusuka mkubwa wewe, angalia shati lak linavyokuhukum, hata vifungo vyako hujavifunga vyema umefunga juu chini kama mtu aliyefumaniwa...utanitambua,subiri hapo,niongee na huyu malaya....’akasema
akimuendea huyo binti huku silaha yake kaiweka begani.
‘Sikiliza
mkuu, mimi nilikuwa ofisini kwangu, nimemaliza kazi zangu, na nilikuwa antoka ,
...na kwa vile kuna joto, nilikuwa nimeacah shati kifua nje, sikujua kabisa
kuwa nitaweza kumkuta huyo binti, na wakati nataka kundoka, na huyo mchumba wako akatokea kama alivyo.....’nikageuka
kumwangalia mdada, ambaye alikuwa anatikisa mguu kama vile anafuata mdundo
fulani, huku kaangalia chini, na mikono yake kaweka kiunoni, akionyesha hana
wasiwasi.
‘Na ndio mkaona
mjipongeze kidogo, kazi na dawa au sio...aah, mimi
sina neno,...ninachotaka ni ukweli, kwasabbu siku nyingi nimekuona ukimwangalia
mchumba wangu kama fisi aliyona mfupa,...sasa leo nimakufuma kwa macho yangu
mwenyewe,huna cha kujitetea hapa, ninachotaka kwasasa ni ukweli, niambie ukweli mlikuwa mnafanay nini?’ akauliza huyu jamaa akinikagua
shati langu lilikuwa nusu wazi, na limechomolewa, na huo ulikuwa ushahidi kuwa
kuna lolote lilikuwa linaendelea kati yangu na huyo binti.
Kwa kweli,
moyoni nikawa najilaumu kwanini nilishindwa kuyakabili hayo majaribu japokwua
sikuwa nimefanya lolote baya, zaidi ya huyo binti, kuanza kunifungua shati na
kulivuta nje, na akilini nikawaza isije huyo binti alifanya hivyo makusudi ili
huyo jamaa yake aje anifume, lakini kwa ajili gani....
‘Hapana,
huyo ana mamb yake, alikuwa akifanya kazi ya kusafisha chumba cha mkutano ndio
maana unamuona hivyo, hata mimi nilipomuna hivyo nikashituka ndio maana nikawa
natoka nje kwa haraka ...’nikasema na yule jamaa akawa anamwangalai yule binti
huku anatabasamu, na kusema;
‘Hivi alivyo
, alikuwa anafanya usafi, kwanini unamtetea, acha aongee mwenyewe, au mumepanga
kusema hivyo,....’akasema akitoa sauti ya mzaha, na watu husema huyo jamaa
akiongea utafikiri anakutania kumbe mwenzako kakasirika, na kipigo chake ni
lazima ulazwe hospitalini, kama hujavunjika kiungo cha mwili.
‘Nilipoona
anamsogelea yule binti, mimi nikachukua mwanya huo kuanza kutoka kuelekea nje, na
kabla sijaufikia mlango, nikasikia sauti ya kipigo,...
‘Wewe
malaya, ulikuwa unafanay nini na huyo malaya mwenzako...?’ sauti ikauliza.
‘Malaya ni wewe mwenyewe, wewe mwenyewe hujioni, unabadili wanawake kama nguo, au unafikiri mimi sifahamu siri zako, kwanza kwanini unanipiga, mimi sio mke wako,..kuwa mchumba wako isiwe taabu,
ninaweza kuvunja huo uchumba...’akasema kwa sauti ya kukasirika.
‘Unasema nini, unataka
kuvunja huo uchumba kwasababu ya huyo malaya mwenzako, ngoja niiharibu hii sura yako unayojivunia nayo, tuone kama kuna mwanaume atakupenda,...’sauti ikasema na
mlio kwa kibau ukasikika, na kilio cha huyo mdada kikatawa.
‘Mamaaa,
kwani unanipiga, mimi sio mke wako, shetani mkubwa wewe nenda kampige mkeo na
kuanzia leo tusijuane...’akasema na wakawa wanashikana kupigana, na mimi
nikaingiwa na moyo wa huruma nikataka kugeuka kwenda kuwasaidia,
‘Samahani
ndugu yangu yangu acha ghadhabu huyo binti hajafanya kitu kama unavyofikiria wewe...’nikasema
nikiwa nimewakaribia, kilichoniziba mdomo ilikuwa ni teke lililonipata vyema
tumboni, jamaa alikuwa mwepesi ajabu maana teke hilo lilikuja kama umeme, na hata kabla sijaka vyema nikigugumia maumivu, nikapigwa kigoto cha puani,damu na kamasi vikaruka hewani,
Sijui hivyo vitendo vilitendwa vipi kwa haraka kiasi hicho, maana muda huo huo nikajiona nipo hwani, nikazungushwa kama
gurudumu la gari na kutua chini, kama gunia la mkaa na kabla sijatulia, nikasindiliwa na buti la
tumboni, karibu nitapike vyote nilivyokuwa nimekula,...na kama asingelikwua
huyo mdada kumpiga kichwani huyu jamaa na mashine ndogo ya kutobolea karatasi,
nahsi huyo jamaa angeliniua.
Ile mashine
ilimpata bara bara, akapepesuka, na kabla hajadondoka chini akayumba huku
akionyesha tabasamu la dharau,la kiuaji, na akayumba akapiga magoti, akashika
kichwa, kilikuwa kinavuja damu, mimi nilipoona huo mwanya nikasimama, na kwa
haraka nikakimbilia nje na walati natoka nje nikakukutana na walinzi, wakija
kwani walishasikia kilio cha huy binti.
‘Kuna nini
huko ndani?’ wakauliza.
‘Sijui naona
huyo mwanaume kaingia na kuanza kutupiga, yeye anafikiria huenda nilikuwa na
nia mbaya na mchumba wake...’nikasema na huy mlinzi kwa haraka akanikagua shati
langu lilivyokuwa, limetoka nusu na vifungo havijafungwa vyema,.....’nikasema
huku nikiharakisha kwenda kuchukua pikipiki langu, na kuliwasha na kuondoka kwa
mwendo wa kasi, sikugeuka nyuma hadi nyumbani kwangu, nilipofika kabla
sijafungua mlango simu yangu ikaita, nilipoangalia nikaona ni namba ya bosi
wangu.
‘Bosi habari
za saa hizi ..’nikasalimia huku nikihema.
‘Upo ofisini
au upo nyumbani ?’ akauliza
‘Nipo
nyumbani...’nikasema
‘Mbona nimesikia
kuwa upo ofisini, mnapigana na yule mchumba wa mtu?’ akauliza
‘Hapana,
mimi niliondoka mapema tu, nilipomuona huyo jamaa akiingia , nilijua akiniona
humo ofisini na mchumba wake atanifikiria vibaya..’nikasema
‘Ina maana
muda wote mlikuwa na huyo mwanamke, alikuwa hajamaliza ile kazi, nilimwambia
ikifika saa kumi na mbili kama hajamaliza aondoke?’ akaniuliza
‘Mimi
nilikuwa sijui kama yupo humo ofisini, wakati natoka ndio nikakutana
naye..’nikasema
‘Mkaanza
maongezi, au mapenzi?’ akaniuliza
‘Alianza
kunisemesha, na mimi nikaona sio muda mnzuri wa kuongea naye, na wakati naondoka
ndio huyo mchumba wake akaingia’nikasema
‘Lakini
nimeambiwa huyo mwanamke amevaa nguo za kuashiria mabaya, ...sikiliza
nimeshakukanya maswala ya mapenzi ofisini, na hili litakuwa mara ya pili
linatokea ofisini kwangu, mimi nimesema
sitaki uchafu huo ofisini kwangu, ...mimi kesho nitafanya uchunguzi wa kina kama nikagundua kuwa kulikuwa na jambo
kama hilo, utawajibika..’akasema kwa hasira.
‘Bosi
natumai unaniamini, mimi sijawazia kufanya hilo, ninachokuambia ndio ukweli wenyewe,
kama ningelifahamu kuwa huyo binti yupo humo ofisini, nisingelikaa humo,
ningelikwenda kuifanyia hiyo kazi nyumbani..’nikasema
‘Sawa,
tutaongea kesho, ila nimesikia kuwa, huyo mwanadada kaumizwa vibaya sana yupo mahututi hospitalini, na jamaa yake,
kashikiliwa na wenzake,... sasa sijui, kesi ya ngedere kupelekewa
tumbili,...sijui ni kitu gani kilitokea, siwezi kukifuatilia kwasasa hadi
kesho.....’akasema
‘Saw bosi tutaongea
kesho....’nikasema na bosi akakata simu.
***********
Asubuhi
kukawa na kikao kikali, bosi alikuwa kakasirika sana, na bila kuficha akaniita
mbele ya wafanyakazi na kunihoji, mimi nikajieleza kama ilivyotokea, na kwa
vile yule binti alikuwa hayupo, kukawa na hakuna maswali mengi zaidi, lakini
walinzi walisema kuwa, dalili walizoziona ziliashiria kuwa mimi na huy binti
tulikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi.
‘Bosi
nakuomba uniamini, mimi sijafanya kama wanavyodai hawo walinzi, huyo binti
alifanya hivyo kwa nia ya kunitega, na nahisi alifanya hivyo, ili bwana wake
aje anifume, lakini mimi nikamshitukia, na shati langu lilichomoka tu, na kwa
vile nilifahamu nipo peke yangu sikujali kuliweka sawa...’nikasema.
‘Kama unasema
wawili hawo walipanga iwe hivyo, mbona basi
huyo bwana wake alimpiga huyo binti, ...sizani kama walipanga hivyo, lakini
nitalifanyia uchunguzi wa kina, na nakuonya tena, ikitokea mara ya pili, mimi
sitavumilia nitakufukuza kazi kwa kukiuka sheria na mkataba wako wa
ajira...’akasema na mimi nikamuahidi kuwa nitajitahidi kuwa mbali kabisa na
huyo binti, kwani naona hana nia njema na mimi.
‘Na iwe
hivyo kweli..vingenavyo utamsikia kwenye bomba wakati upo mitaani, au jela ukinyea kopo, na ukikiuka ahadi yako hapa kwangu,nitahakikisha unasota mitaani, au jela, kwani sifa zako zitakuwa zimesharibika...’akasema.
Hali hiyo
ikapita ikabakia minong’ono, na wengi wakidai kuwa nimefumwa, nikizini na
mchumba wa watu, lakini sikuyatilia maanani na wala sikutaka kubishana na watu
nikawa kimiya nikimuachia mungu anisaidie.
‘Ngoja
tuendelee na kisa changu, hayo ya mapenzi yenu tuyaache kwanza, nitalifanyia
uchunguzi,..’akasema aliponiita ofisini kwake,.
‘Kinachonishangaza
ni hii tabia chafu inayoendelea kwenye ofisi yangu, hili sasa linakuwa ni
tatizo, na nikigundua kuwa huyo binti ndiye chanzo cha hay a yote itabidi
nimsimamishe kazi kwa muda, hata kama
baba yake ana hisa na mimi..’akasema
‘Ina maana
kumbe baba yake ana hisa kwenye kampuni yako?’ nikamuuliza
‘Ilibidi
nifanye hivyo, kwa ajili ya kibiashara zaidi, lakini sio kwamba kwa vile ni
mtot o wa mshirika wangu wa biashar ndio niache afanye atakavyo, mwenyewe
anamfahamu vyema mzazi wake huyo hana mzaha kwenye kazi, ...’akasema
‘Sawa bosi
tuendelee na kisa chetu, au?’ nikasema na bosi akaniangalia kwanza kwa makini
na kuniuliza swali.
‘Umempenda
sana huyo binti?’ akaniuliza
‘Hapana
bosi,..niamini bosi..’nikasema.
*********
‘Sehemu
iliypita ulianza kuona masiha yangu na mama wa kambo, sasa tutaingia zaidi kuona masiha hayo, na
jinsi gani nilivyotaabika na mama wa kambo,na siku ile nilishaamua kumwambia
baba kuhusu mateso hay japokuwa kaka yangu alinizuia nisimuambie baba, akijua
kuwa baba hatatusikiliza.
‘Mdogo wangu
jaribu kuvumilia, ..’aliniambia kaka yangu lakini kwa vile mimi ndiye
niliyekuwa nikiteseka zaidi nikaamua kumwambia baba.
‘Baba , kazi
za hapa nyumbani zimekuwa nyingi sana, tunasoma kwa shida, inabidi kuamuka
asubuhi kufanya kazi za ndani kabla ya kwenda shule na ukurudi nyumbani
halikadhalika, hata kazi za masomo ya nyumbani sipati muda wa
kuzifanya..’nikaanza kulalamika
‘Mbona mama
yenu anasema nyie hamfanyi kazi, sana sana wanaofanya kazi ni ndugu zenu tu, na
nyie mnakuja kuongea mambo mengine kabisa..’akasema baba
‘Mama
anasema kuwatetea watoto wake tu, lakini wao hawafanyi kazi kabisa, kazi zote
tunazifanya sisi, akinisaidai kaka yangu ..’nikasema
‘Ngoja
nitamuuliza mama yenu na kama ni uwongo, nitawadhibu kweli kweli..’akasema na
kabla hajamaliza mara mama akatokea na alipotuoa tunaongea na baba akahisi kuna
jambo, kwanza akauliza
‘Wenzenu
wapo wapi?’ akauliza
‘Wanacheza
nyumba ya jirani..’akasema kaka
‘Ina maana
ile kazi waliyokuwa wakiifanya wameshaimaliza ..’akauliza na hapo nilijua
ananiuliza mimi kazi aliyoniambia niifanye nimeshaimaliza , na mimi nikasema
‘Nimeshaimaliza
mama ile kazi, sio wao....’nikasema
‘Sasa
mnafanya nini hapa?’ akauliza huku akimwangalia baba , halafu akaniangalia
mimi.
‘Watoto
wanalalamika kuwa unawafanyisha wao kazi nyingi, na watoto wengine kazi ya ni
kucheza tu hawafanyi kazi, kazi anayefanya ni huyu na kaka yake tu...’akasema
baba.
‘Ndivyo
walivyokuambia ehe, na ukawaamini ....?’ akauliza huku kashika mikono kiuononi,
na kabla mume wake haajsema neno, akaendelea kuomngea.
‘Watoto hawa
ni wanafaiki wakubwa, siumesikia
nikiwauliza wenzao wako wapi, ina maana kuna akzi niliwapa kila mmoja na kazi
yake, na unaona wenzao wameshamaliza kazi zao,na hawa kwa uvivu wao walikuwa
bado waanjivuta vuta....’akasema mama .
‘Huyu mtoto
ni mvivu, wenzao walishamaliza kazi zao, sasa yeye anajifanya kuwa alikuwa akiifanya
hiyo kazi peke yake, sio kweli, ..ukiwasikiliza hawa watoto, tutakuja kukosana
wenyewe humu ndani...watoto hawa, ni wanafiki hawana lolote..’akasema na baba
akatuambia tuondoke mbele yake, maana eti sisi ni waongo.
Maisha
yakawa hivyo, na muda wetu wa kupumzika ni ule tu wa kwenda shule, na mara
nyingi tulikuwa tukitamani kukaa huko huko shuleni, japokuwa mchana tulikuwa tuna
muda wa kurudi nyumbani kupata chakula cha mchana, lakini mimi niliona ni bora
nikae shuleni na njaa yangu kuliko kurudi nyumbani, kwani hata nikirudi
nyumbani chakula chenyewe naweza nisikipate, nitaishia kufanya kazi, na hata
shuleni naweza kuzuiwa nisirudi tena.
**********
Baba muda mwingi alikuwa
kwenye mgahawa wake, ambapo kulikuwa na biashara ya chai, na vitafunio vyake kama maandazi, vitumbua, chapatti na sambusa,
ikatokea siku moja pesa ikapotea na aliyepoteza alikuwa ni dada yangu wa kambo,
na dada yangu huyo akanisingizia mimi kama
kawaida yao, kuwa mimi ndiye niliyepoteza;
Mama alikuwa
amekasirika, na baba akawa yupo wanatuuliza kwa pamoja
‘Huyu atakuwa kaziiba, na sasa anasingizia
kupoteza....’akasema mama na kunifanya nibakie mdomo wazi, kwani katika maisha
yangu sijawahi kuiba, mama alishatukanya kabisa tusje kuchukua pesa bila idhini
ya wazazi, na sisi wote tunalifahamu hilo.
‘Mama mbona mimi
sijachukua hizo pesa, aliyekuwa nazo ni huyo...’nikamtaja dada yangu huyo wa
kambo, akiwa pembeni yangu na haraka bila aibu huyo dada yangu akasema;
‘Muongo huyu, nilimuona
akiziiba akaondoka nazo, ananisingizia tu...’akasema huyo dada wa kambo, na
mama aliposikia hivyo akasema;
‘Mbona mlipokuwa hampo
haijawahi kupotea pesa, huoni kwamba nyie ndio mumeanzisha hii tabia, na huyu
mtoto mtoto anatabia mbaya sana ya wizi, nilikuwa sijamuamboa baba yako aheri
leo kajionea mwenyewe ...’akasema mama.
‘Mimi sijachukua
pesa....nilikwenda huko mgahani mara moja, tukiwa na mwenzangu na yeye ndiye
aliyechukua hizo pesa akisema wewe ndiye uliyemtuma...’nikasema.
‘Unaona jinsi gani
alivyo muongo,sasa anasema mimi ndiye niliyemtuma huyo ndugu yake, kwanza
tukuulize huko mgahawani ulifuata nini?’akaniuliza mama na baba wakati huo
alikuwa kakasirika kweli.
‘Nilikwenda kuchukua
ufagio...’nikajitetea
‘Unaona hebu muulize toka lini ufagio wa huko mgahawani
ukatumika huku nyumbani, huku kuna ufagio wake, kwanini ulikwenda kuchukua huo
ufagio wa huko,...ni ujanja wako wa kupata mwanya wa kudokoa pesa, mimi
nilishakuambia huyu mtoto ana tabia mbaya, na kila siku nalalamika pesa
zinapotea, kumbe ni mwizi wet yupo humu humu ndani....’akasema mama
‘Hebu niambie vizuri
pesa hiyo umeipeleka wapi?’ akauliza baba kwa hasira akinitolea macho yaliyojaa
hasira...mimi nikaanza kulia, niliona ninaonewa, sikuweza hata kujitetea zaidi,
sikujua hata niongee nini tena, nikajikuta nalia tu huku nikuita mama yangu;
‘Mama yangu njoo
nisaidie, nimekosa nini , mimi mama,hawa watu hawanipendi , kila siku
wananisingizia uwongo, mimi sijaiba jamani ...’nikawa nalia.
‘Mama yako ndiye
aliyekutuma uje uuibe pesa, unaiba ili umtumie hizo pesa...?.’akasema huyo mama
wa kambo kwa hasira.
‘Baba mimi sijachukua
pesa,..mbona hamniamini mimi, sijawahi kuiba katika maisha yangu, kwanini nije kuiba
huku...’nikajitetea, lakini baba hakuniamini tena, akaanza kuniadhibu, kwa
kunichapa, na alipomaliza mama akaona hiyo haitoashi akanichukua, sikujua
ananipeleka wapi, wakati huo nalia sana, maana naonewa, sijafanya kosa
naadhibiwa tu, na wadogo zangu, yaani watoto wa mama wa kambo wakawa wanashangilia
wakisema
‘MwIzi huyo mwizi
huyo....’hata yule ambaye ndiye aliyepoteza hizo pesa akawa ndiye anashabikia
zaidi...’
Mama alipoona kuwa baba kanichapa kidogo tu,
yeye kwa hasira akanishika mkono huku akisema;
‘Huyu tusipo mpa fundisho, tabia hii
hataiacha, wewe uanmgusa gusa na fimbo, watu kama hawa wana adhabu yao...’akasema
huku akivuta kunipeleka ndani wanaposagia nyama ya sambusa kisha akachukua
kidole changu na kukitumbukiza ndani kisha akaanza kusaga japo hakikusagika
sana, kilichofika juu, juu, ulikuwa huu mkono wa kushoto, unana hapa kidole
changu hakipo sawa.
Baba muda huo alikuwa karudi kwenye mgahawa
wake, mama akawa anaendelea na adhabu zake akaona hiyo haitoshi, akachukua
pasi, akaiwasha ikapata moto
‘Mama mimi sijaiba mbona mnanionea...’nikawa
nalia hata kaka yangu nilimuona machozi yakimtoa, lakini hakuwa na la kufanya,
mama akachukua ile pasi yenye moto, akashusha nguo, yangu na mara pasi
ikabadika mgongoni, maumivu niliyyasikia, ilikuwa karibu kupoteza fahamu
nikadndoka chini, huku hata sauti ya kulia haipo tena
Mama alipoona nimedondoka chini, akahisi
nimekufa, akaichukau ile pasi na kuweka pembeni, akakimbilia nje, na aliyetoka
haraka kwenda kumtafuta baba alikuwa kaka yangu, na baba akaja haraka na
kuuliza;
‘Kuna nini tena,....’akaniona nipo sakafuni,
nimetulia nikiwa nimeishiwa nguvu kabisa ya kulia tena, nilikuwa kama mtu
aliyepoteza fahamu.
‘Amaefanya nini huyu...?’ akauliza baba, na
mara mama akaja kwa haraka, na yeye akauliza
‘Kwani kafanya nini...?’ akauliza
‘Kaungua na pasi...’akasema binti wa mama huyo
‘Kaungua vipi mgongoni,?’ akauliza baba
akionyesha mshangao huku akiangalai lile jeraha, naona hata yeye aliingiwa na
wasiwasi maana lilikuwa ni jeraha kubwa.
‘Hawa watoto bwana, hapa nikumpeleka
hospitalini, hakuna haja ya kuuliza uliza tumuwahishe hspitalini...’akasema
mama na haraka wakaniinua na kunibeba na kunikimbiza hspitalini
Walipofika haspitalini wakadai kuwa ni utoto,
tuliunguzana wakati tunachezea pasi ya umeme. Docta alinikagua lile jereha, na
kusema jereha hilo ni kubwa sana, ni lazima nilazwe.
‘Watoto hawa watundu kweli kweli, wakati wanajifanya
wananyosha nguo na mwenzake kwa bahati mbaya mwenzake akapitisha pasi mgongoni
mwa huyu ndio akaungua kiasi hiki..’akasema mama akimwambia dakitari, na mimi
sikuwa na la kusema, niliogopa sana kusema mama ni muongo, nikanyamaza kimiya
huku nikimshukuru mungu tu.
‘Lakini jereha hili linaonyesha ni kama mtu
alidhamiria, akawa kaikandamiza pasi, huoni limeenda ndani sana..’akasema
docta.
‘Ni utoto, nafikiri sasa watakoma ubishi kuchezea
pasi tena...’akasema mama.
Nilikaa hospitali kama wiki mbili mpaka hapo
nilipopata nafuu nikaruhusiwa. Baba akajaribu kutafuta undani wa tukio zima na
ukweli ukadhiri, baba mzazi akajua ukweli ulivyokuwa,hapo baba akaona ili
kuepusha shari ni bora turudishwa tena kwa mama yetu mzazi huko kijijini.
Siku ya pili yake ,tulirudi mimi na kaka yangu,mama
aliptona jinsi tulivyokonda na kumuhadithia yaliyotukuta, akakasirika sana, na
kusema hata siku moja hatarusu mtoto wake kwenda huko mjini tena, mama akaendelea
na kazi sisi huku ndugu wa tatu tunaendelea na masomo katika shule ya serikali
ya hapo kijijini.
Kwa vile kwa asilimia kubwa mama alikuwa ndiye
anayetulisha kwa kiasi kidogo anachopata kwenye mshahara wake, maisha yalikuwa
ni magumu sana, lakini hata hivyo, mama hakukata tamaa, akawa anajitahidi kwa
hicho kidogo anachokipata.
Maisha huko mjini kwa mama wa kambo yakawa ni
ya shida, ikabidi baba na mama huyo warudi hapo kijijini kwa muda, na mama
akawa ndiye anayetegemewa na kipato chake kidogo cha mshahara wake anachopata,
na kwahiyo maisha yakazidi kuwa mabaya zaidi. Na mama huyo wa kambo alipokuwa
hapo, utafikiri kama sio yeye, alikuwa mpole, anajifanya anatupenda.
Baadaye baba akahangaika, na akafanikiwa tena
kuweza kufufua ile biashara yake huyo mjini, kwahiyo wakaondoka na mke wake,
yaani huyo mama wa kambo.
Maisha huko mjini yakawa mazuri, na baba akaja
na kuongea na mama, akamwambia kwa vile maisha huko mjini ni mauri na hapo
kijijini hali ni ngumu, basi ni bora mimi na mdogo wangu wa mwisho twende
tukasomee mjini.
‘Watot wangu waende huko mjini tena, hapana,
...’akasema mama, lakini baba akasema mama kesabadilika, baada ya kumsema sana,
hawezi kuwatesa watoto tena, na yeye mwenye atahakikisha tunaishi bila shida.
Mwisho wa siku mama akakubali, apo tena ikaamuliwa
kwenda kuishi huko mjini,, safari hii alinichukua mimi na mdogo wangu wa mwisho
na kutupeleka tukasomea huko mjini, na kipindi hicho mimi nipo darasa la sita.
‘Mama mimi siendi huko mjini...’nikasema
nikikumbuka yaliyonipata kipindi kile.
‘Mimi nitakwenda kama hutaki,...’akasema mdogo
wangu, yeye alikuwa mdogo sana, hakuwa anafahamu ni nini anakwenda kupambana
nacho huko, hata hivyo huyo mama hakuwa akiwanyanyasa sana watoto wa kiume ni
mimi tu alikuwa akiniandama sana sijui ni kwanini.
Mama akaniagalia na kuniambia,
‘Mtoto wangu mimi nataka ukasomee huko mjini,
ili ufaulu masomo yako, shule hii ya hapa kijijini hutaweza kufaulu, na masmo
ni muhimu sana katika maisha yenu...’akasema mama.
‘Lakini mama , huko mjini ninvyofahmu mimi, naenda
kufanyizwa kazi tu, sitapata hata muda wa kusoma...’nikalalamika.
‘Nimeongea hilo na baba yako, kasema safari
hii atahakikisha hamteseki tena, usiwe na wasiwasi mwanangu ni muhimu sana
mkawa mnamtii baba yenu...’akaniambia, japokuwa ilionekana kabisa hakupenda iwe
hivyo, hakutaka kabisa kuachana na watoto wake hasa huyo mdogo wetu, lakini
hakukuwa na jinsi ikabidi twende tena huko mjini. Nikimuomba mungu hali ile ya
mateso isirejee tena...
NB: Je hali ni ile ile, au kutakuwepo na
mabadiliko kama alivyoahidi baba
WAZO LA LEO: Majaribu na mitihani ya kimaisha
ni mingi, ya kila namna kwa wanadamu, yanapotukuta tunahitajika kupambana nayo, tusikate tamaa, wala kuyakimbia kwa visingizio mbali mbali, kwani yote hiyo yapo kwa ajili ya kupima, taaluma zetu, imani na misimamo yetu,
tujitahidi kupambana nayo, na silaha yetu kubwa iwe ni elimu, elimu ndiyo silaha ya
mambo mengi ya kimaisha. Tusome, tufanya utafiti wa kina, kabla ya kufikia maamuzi...
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment