Hali ya ofisi ikatulia kidogo maana bosi alikuwa
kachachamaa na wafanyakazi wakawa kila mmoja anajituma kwenye meza yake, na ile
tabia ya urafiki wa kimapenzi, ukapungua, kama ilitokea inakuwa nje ya ofisi,hata
tabia kutoana chakula cha mchana haipo tena, ikawa kazi ni kazi.
Baada ya wiki moja, Mdada, akarudi kazini, uso
ukiwa na makovu, akawa kavalia mawani makubwa kujaribu kuficha uso wake.
Siku
alipofika bosi akamuita ofisini kwake wakaongea kwa muda mrefu, halafu akatoka,
na alipopita kwenye meza yangu akaniachia ujumbe kwenye karatasi
‘Nataka tuongee baadaye....’nikasoma na kwa
hasira nikakichana kile kikaratasi huku nikisema huyu mwanamke hajakoma tu,
sitaki kuonana naye.
Ilipofika jioni nikpata ujumbe kwenye simu
yangu, kutoka kwa huyo binti, ukisema;
‘Nitakusubiri unipe lifti ya piki piki
yako,...’
Na mimi hapo hapo nikamjibu
‘Samhani kuna mtu kaniwahi, ..’ yeye akaandika
ujumbe mwingine,
‘Basi njoo mara moja nataka tuongea na wewe ni
muhimu sana, ni kuhusu yule jamaa, alivyoniambia, nimeshavunja uchumba na yeye
kwa ajili yako....’akaandika.
‘Mimi hayo hayanihusu, nakuomba tujuane kikazi
si zaidi ya hayo...’nikaandika.
‘Mimi nimeongea na bosi nikamwambia ukweli....’akaandika.
‘Ukweli gani?’ nikamuuliza
‘Kuwa mimi
kweli ninakupenda wewe, ...’akaandika.
‘Mimi sitaki mahusiani na wewe...’nikamjibu.
‘‘Ina maana hunipendi?’ akauliza.
‘Mimi sio aina yako, sikuwezi...’nikaandika
‘Wewe sio mwanaume?’ akauliza.
‘Hata kama mimi ni mwanaume, lakini sio kwa
ajili yako...’nikamjibu.
‘Basi mimi nitakufundisha uwe wa aina yangu,kama
kweli wewe ni mwanaume ...’akaandika.
‘Sitaki, urafiki na wewe nakuomba tafadhali...’nikamwandikia.
‘Sikiliza wewe mwanaume, kazi ni nzuri,
unaonaje ukienda mitaani, bila kazi,...’akaandika
‘Una maana gani?’ nikamuuliza kwenye ujumbe wa
simu
‘Unaelewa vyema, ...sasa tuonane tuongee,
...kama unamuogopa bosi wako basi tukutane nyumba ya wageni ya
kajificheni..’akaandika bila aibu.
‘Sina nafasi hiyo na mimi sina tabia ya kwenda
nyumba za wageni..’nikaandika.
‘Mimi nitafika huko kukusubiri na usipofika,
nitamwambia bosi wako yote yaliyotokea siku ile kuhusu wewe....’akasema.
‘Kuhusu mimi! Mimi nimefanya nini, wakati wewe
ndiye uliyetaka kuniingiza kwenye matatizo?’ nikamuuliza.
‘Nina siri zako nyingi, nikimuonyesha bosi wako,
sizani kama atakuvumilia, ...ulipokuwa ofisini siku ile, kuna picha nimechukua
tukiwa tumekumbatiana,...au nikutumia...’akaandika.
Mimi nakumbuka kabisa siku ile hakuwa na
kamera wala simu yake, je picha hizo alizichukua muda gani, na wakati nawaza
hivyo, ujumbe ukaingia kwenye simu,
‘Hebu angalia hiyo picha, je unaweza kusema
mimi ndiye niliyetaka kukuingiza kwenye majaribu...’akaandika, na mara ujumbe
wa kuonyesha kuwa kuna picha ukaingia. Nilianza kuhisi wasiwasi, huku
nikifungua hu ujumbe.
Picha
iliyonekana ilikuwa ni wakati ule Mdada huyu akajiribu kunibusu, na kweli kwa
jinsi alivyoichukua, inaonyesha kabisa na mimi nilitaka kufanya hivyo, sijui
alichukuaje, kwani ilionyesha wazi nilikuwa nataka kumbusu, hapo nikahisi mwili
ukiisha nguvu, nikazima simu yangu kwa
hasira.
Siku
hiyo kabla muda wa kuaondoka kazini haujafika, bosi akaniita ofisini kwake, na
alihisi sipo sawa akaniuliza nina tatizo, nikamwambia hakuna tatizo.
Yeye akaniambia;
‘Unafahamu Mdada alikiri kuwa anakupenda sana
na ampepanga kuachana na mchumba wake, ili muwe marafiki,..’akaniambia
‘Haiwezekani, mbona mimi nimemkatalia..hatujawahi
kuongea hilo, hapana bosi kakudanganya’nikasema.
‘Sema ukweli wako ina maana na wewe humpendi
huyo binti...?’ akaniuliza
‘Huyo si aina yangu, ni mkorofi, sitawezana
naye...wewe mwenyewe unafahamu hilo...’nikasema.
‘Huyo atatulia tu, ...huo ni wakati wake wa
kuruka ruka, lakini atakuja kutulia, ...’akasema.
‘Bosi kwanini unasema hivyo, mimi sizani, kama
nitawezana nay eye, nimeshamuona hanifai...’nikasema.
‘Umeshamuona, hakufai, ulimuonaje hakufai
wakati huna mahusiano nay eye?’ akaniuliza
‘Kwa jinsi nilivyomuona tu, na kwa tabia zake,
nilivyosikia kwa watu, hata wewe bosi unamfahamu hivyo..’nikasema
‘Kasema usimpomkubalia yeye, hatahitajia
mwanaume mwingine .....anaonyesha wazi kuwa anakupenda sana...’akaniambia bosi.
‘Bosi hivi kweli hata wewe unanishauri niwe na
mwanamke kama huyo , kweli ndi ushauri wako huo, nilitarajia wewe kunikanya nisiwe
karibu naye,kama ulivyonishauri mwanzoni!’ nikasema kwa mshangao.
Mimi sijakushauri hivyo, ila nakuelezea
alivyosema mwenzako, ..nashukuru hata hivyo, kuwa ofisi sasa kumetulia,mimi
nilikuwa nakupima uoni wako na je upo tayari na huyo binti, na kwa jinsi
ulivyonijibu inaonyesha wazi hata wewe una kitu moyoni kuhusu huyo binti, ila
nakuonyeni, fuateni sheria na taratibu za kazi ...’akasema bosi.
‘Bosi tutafanya hivyo,...’nikasema kwa sauti
ya unyonge.
‘Na wale jamaa niliowasimamisha kwa muda walifika
jana na barua zako za kujieleza, wewe ulikuwa umetoka, ...wakaniomba msamaha,
kwahiyo kesho watakuwepo ofisini...’akasema.
‘Mhh, sijui kama kutakuwa na amani, labda
wakifika wataendeleza ushindani wao...’nikawa kama najiuliza.
‘Ndio maana nikakuuliza kuwa unampenda huyo
binti, kwani sitavumilia mapigano na mvutano wa kimapenzi kwenye ofisi yangu,
kama mpo na uhakika wa kweli,wa kuwa wachumba, naomba mliweke wazi, tuwachumbie..mimi nitakusaidia
ili muweze kuishi kama mke na mume....’akaniambia.
‘Bosi....’ nikataka kujitetea na yeye
akaniangalia huku akitabasamu kimzaha
‘Kama huna nia na yeye kiukweli, basi haina
haja ya kushindana na wenzako kwani nina imani wenzako wakija, kutakuwa na
ushindani dhidi ya huyo binti, na hiyo ndio furaha yake...’akasema
Moyoni nilianza kuhisi wivu, ina maana hao
jamaa wakija, binti huyo hatakuwa na urafiki na mimi tena, nikikumbuka msimamo
wake wa mwenye kisu kikali ndiye atakaye kula nyama, na kama nilivyosikia kwa
wafanyakazi, jamaa hawo wana pesa na wanajua kuzitumia, kwahiyo mimi sitakuwa
na nafasi tena na huyo binti.
‘Sijui kwanini nilijisia hivyo, ina maana
kweli nilishampenda huyo binti au ni tamaa tu za kimwili?’ nikajiuliza kimoyo
moyo na aliyenishitua kwenye dimbwi hilo la mawazo alikuwa bosi.
‘Naona una mawazo sana, unawaza nini,
unamuwazia huyo mdada,umeshapenda wewe,....’akasema huku akicheka.
‘Hapana bosi....’nikasema
‘Ninachokuasa ni kuwa achana na mawazo ya
namna hiyo, waza mambo ya maendeleo ambayo ukiyafanya watu watakupenda hata
bila ya kushindana, watu watakuthamini na kila mmoja atatamani kuwa na wewe.
Hata siku moja usipende kuwaza mambo ya anasa kabla hujafanikiwa ...anasa
inakuja kwa ziada...
‘Ukweli ulivyo, huwezi kuwaza anasa kabla
hujachuma, anasa kabla ya machumo ni uzembe, na uzembe ni sumu ya maendeleo.
Maendeleo hutokana na juhudi sio kuota ndoto za mchana,..nikuambie ukweli
ukifanikiwa kila kitu kitajileta chenyewe, kwahiyo hakuna haja ya kuota ndoto,
fanya kazi,kwa bidii utafanikiwa,...’akasema na mimi nikaitikia kwa kichwa
‘Haya ngoja tuendelee na kisa chetu...’akasema
bosi
‘Unakumbuka pale tulipoishia, wakati mimi na
mdogo wangu tuliporejeshwa tena kwa mama wa kambo, na sisi kama watoto
tusingeliweza kupinga amri ya wazazi, lakini mimi sikupendelea kabisa kurudi
tena huko mjini, mama akatuambia baba kaahidi kuwa safari hii atahakikisha
hatunyanyaswi au kuteswa.
‘Je ni kweli baba alitimiza ahadi yake,...?’
nikamuuliza bosi na bosi akanitizama halafu akasema;
`Tuendelee kuanzia hapo, utajionea mwenyewe...’
********
Sijui ilkuwaje, kweli tulipofika kwa mama akatupokea
kwa shangwe, na tulimuona kama kabadilika, akatuonyesha sehemu ya kulala, na
kutuandalia chakula,
‘Wanangu karibu sana mjisikie mpo nyumbani, ..’akasema.
‘Tunashukuru sana mama, naona umebadilika
sana...’nikamwambia
‘Kwanini mwanangu, mimi ni mama yenu,
nawapenda sana, msisikilize maneno ya wambea kuwa nawatesa, mimi ninachofanya
ni kuwajenga ili muwe watoto wema, nawaonyesha jinsi gani ya kuishi maisha
mema..’akasema.
Kwakweli tulimuona kabadilika kidogo,akawa
anatulea vizuri,siku za mwanzoni, sio kama ilivyokuwa awali, lakini siku
zilivyozidi kwenda akaanza kubadilika, kumbe ilikuwa ni kama geresha, ubinafsi wa huyo mama haukupotea,
bado alikuwa na kinyongo na mimi na wala sikufahamu kwanini alikuwa akinichukia
kiasi hicho.
Ile hali ya utumishi na kufanya kazi ikawa ipo
pale pale, na ile hali ya kusingiziwa makosa hata kama sijayafanya ikawa ipo
pale pale, maisha ya dhiki, dhahama kusimangwa, ikawa ndio tabia ya nyumba
hiyo,na baba akawa kama anamwamini mke wake kuliko hata utetezi wangu,, mama
akisema jambo, baba anakimbilia kuniadhibu tu, watoto wake wakikosa,
wananisukumia mimi kuwa ndiye niliyefanya hilo kosa, na sikusikilizwa hata pale
nilipojaribu kujitetea.
Nakumbuka ni kipindi tulipomaliza mtihani wa
darasa la saba wa taifa nimemaliza na kuelekea nyumbani nilivyoingia tu
nikaanza kupewa kipigo na baba bila kuambiwa napigwa kwa kosa gani,baba siku
hiyo alinipiga sana, kama vile mtu anayepiga mnyama, na alipotosheka an kipigo
hicho, akaniambia nindoke mbele yake.
‘Huyu adhabu yake, asipewe chakula, atabakia
hivyo hivyo...mimi siwezi kukaribisha udanganyifu katika nyumba hii...’akasema
‘Jamani kwani mimi nimefanya nini....mbona
mnanipiga hata bila kujua kosa langu ni nini...?’ nikauliza na hakuna
aliyeniambia kosa langu ni nini.
‘Unajifanya hujui eeh, kwa vile umezoea
kufanya hivyo, unamdanganay nani, unafikiri siri zako zitajificha...’akasema
mama
Baada ya kukaa masaa kama ma nne nikiskilizia
maumivu na njaa ndio napata habari kuwa baba ameambiwa eti nilikua nameibia
kwenye mtihani, na hiyo ndio tabia yangu nikiwa darasani, nikashikwa na
mshangao mkubwa, mbona hilo alipo na halijawahi kutendeka, mimi huwa natumai
akili zangu. Nikajaribu kujitetea nilivyoweza lakini sikusikilizwa, baba
alikataa kabisa kunisikiliza.
Mambo hayakuishia hapo, kwani mama aliona njia
nzuri ya kunipata ni kunisingizia uwongo, anatuma watu wanakuja na uwongo huu
au ule, hapo nyumbani kesi zikawa haziishi kila siku natungiwa jipya na kuzidi
kuchukiwa na baba.Baba akawa sasa ananichukia kama vile mimi sio mtoto wake,
akawa haniamini tena, ikawa sasa ni
kipigo kejeli, masimango.
Siku ikafika ya mahafali ya kutuaga darasa la
saba ambayo kila mtu alikua anafuraha ya kipekee isipokua mimi maana hata
ruhusa ya kuhudhuria sherehe za mahafali hayo sikuweza kuipata kirahisi, baba
alikuja kuamua baadaye kuwa na mimi niende, na hata hivyo hakuniamini, ikabidi
nipewe na walinzi. Japokuwa ilikua siku ya furaha kweli kwa kila mwanafunzi lakini
haikuwa kwangu mimi.
Wenzangu walinionea huruma sana, hasa wale
wanaofahamu maisha yangu na familia yangu, hata walipjaribu kuniliwaza, niliona
kama wananizishia machungu, nikawa nipo peke yangu nimejikunyata kama mkiwa.
Niliwaangalai wenzangu wakicheza na kufurahi na kujiuliza moyoni, hivi mimi
nimekosa nini katika hii dunia, kwanini nabeba mateso nisiyokuwa na sababu
nayo, nimewakosea nini hawa watu.
Nikiwa nimekaa peke yangu, machozi yakaanza
kunitoka huku nikimkumbuka mama yangu, ambaye hakuweza hata kufika kuja
kunipongeza kutokana na nakama za kimaisha. Nilikaa hivyo hivyo, hadi ikafika
muda wa kukabidhiwa vyeti, na nilipokipokea tu, wale walinzi kwa kufuata
masharti waliopewa, wakaniambai turudi nyumbani haraka. Wenzangu wakaendelea
kushereheka. Nilirudi jela, maana nyumbani kwangu ilikuwa kama jela, sina raha,
sina uhuru.
Kwa kawaida wazazi humpongeza mtoto wao
anapomaliza darasa la saba, nilitarajia itakuwa hivyo kwa wazazi pale
nilipowaonyesha cheti changu, lakini hawakutaka hata kukiangalia, baba ndio
kabisa aligeuka pembeni akisema;
‘Huyu ni kupoteza muda tu, sijui kama
atafaulu, mtihani wenyewe nasikia umefanya kwa kuibia, umenitia aibu sana,...’akasema
akikumbushia siku ile alipoletewa taarifa za uwongo kuwa mimi nilionekana
nikiibia kwenye mtihanii huo wa kumaliza darasa la saba, kitu ambacho sio
kweli, na sikujua ni nani alileta uwongo huo, nikamuachia mungu, maana sikujua
nijitetee vipi.
‘Atabakia hapa nyumbani, afanye kazi za
nyumbani akipata mume aolewe, kama basi atampta huyo mume, kwani kwa tabia yake
hii ya uhuni, hakuna mwanaume atakaye mtaka, wanaume wanataka wanawake wenye
tabia nzuri, wachapakazi, lakini wewe uvivu, mzembe, muhuni, tabia zote chafu,...’akasema
mama wa kambo
Marafiki zangu waliwahi kunitembea waliumia
sana na walitaka kujua tatizo ni nini mbona sina raha, nipo kama mkiwa, lakini
sikuweza kuwaambia ni nini kinachoendelea ndani ya familia yangu, niliwaambia
ni mambo ya kawaida tu.
Siku zikaenda na muda wa matokea ya mitihani
ukafika, na taarifa zikaja kuwa nimefaulu, nilikimbia kwa haraka kuwafahamisha
wazazi wangu, nikitarajia furaha na kupongezwa, lakini sura niliyoiona
ilinikatisha tamaa, kumbe wao walishajua hayo matokea lakini hawakunifahamisha,
walikuwa na yao mengine kichwani.
‘Wewe hatukuamini, hata kama umefaulu, ukienda
huko sekondari pake yako utazidi kututia aibu....’akasema baba
‘Kwanini baba?’ nikauliza.
‘Wewe ni muhuni, huna adabu, nafahamu kabisa
ukipata mwanya kama huo, utautumia vibaya na kufanikisha mambo yako ya kihuni, na
mimi kama mzazi nitakuja kuaibika, na kuizalilisha hii familia...’akasema baba,
na sikumuelewa ni kwanini aniite mimi muhuni, ni uhuni gani huo niliowahi
kuufanya, maana mimi sina tabia kama hiyo, sijawahi kuwa na mpenzi, nab ado nilikuwa
mdogo wa kuwazia hayo..
Muda wa kujiunga na sekondari ukafika baba
akaendelea na msimamo wake huo huo, kuwa mimi sitaenda kusoma sekondari, akasema;
‘Huwezi kwenda sekondari peke yako, ni lazima
uwe na mtu wa kukuchunga, kwahiyo utasubiri hadi mdogo wako akimaliza shule ya
msingi, akifaulu mtaenda naye,sikuamini,...ina maana nikae mwaka mnzima hadi
mdogo wangu huyo, mtoto wa mama wa kambo, amabye walimuamini, amalize darasa la
saba, kwani muda huo yeye alikuwa darasa la saba.
‘Baba mimi sio muhuni, nitasoma kwa bidii,
....’nikasema.
‘Mimi nimeshasema, itakwua hivyo, sisi
tunakufahamu kuliko wewe unavyojifahamu, tabia yako hiyo, inahitaji uwe na
ndugu yako karibu, ukiwa peke yako utafanya mabaya zaidi...’akasema na kweli
akashikilia msimamo wake huo. Nilimuwazia mama yangu huko kijijini, kama angelikuwa
hapa, angelinitetea, lakini mama yangu wa kambo, akawa na msimamo huo wa baba,
na kusema.
‘Na hata huko kusoma ni kupoteza muda tu, ni
aheri akae hapa nyumbani, akipata mume ataolewa..’akasema mama huyo wa kambo.
Ukawa ndio msimamo wa wazazi wangu hao, na
kweli nilikaa nyumbani, nikifanywa mfanyakazi wa nyumbani hadi mdogo wangu alipomaliza
darasa la saba, na kweli akafaulu kujiunga na sekondari ndipo hapo nikaruhusiwa
na mimi kujiunga na sekondari kidato cha kwanza, baada ya wao kuniombea na
kukubaliwa.
Kwasababu maksi zangu za ufaulu zilikuwa za
juu kuliko hata za huyo mdogo wangu, mimi niliwekwa chumba cha watoto werevu,
kutokana na walimu wenyewe walivyopanga, na mdogo wangu huyo, ambaye alikuwa
mtoto wa mama wa kambo, akawekwa chumba kutokana na maksi zake, hali hii
ilijenga chuki fulani kwa ndugu yangu huyo, na alipomwambia mama yake , mama
yake akasema ni uhuni wangu ndio uliofanya walimu wanipendelee.
Pamoja na yote hayo, maisha magumu, kusakamwa,
kunyanyapawa, lakini hata hivyo, bado nilikuwa napenda sana kusoma, na darasani
nilikuwa na juhudi sana, na nilikuwa miongoni mwa wanafunzi walikuwa wakifanya
vyema darasani, na hali hiyo ilijitokeza pale tulipofanya mtihani wa kuingia
kidato cha pili, kwa kuwa miongoni mwa wanafunzi waliofanya vizuri.
Matokeo ya kuingia kidato cha pili yalipotoka,
nilikuwa miongoni mwa wanafunzi waliofanya vyema, tofauti na mdogo wangu, yaani
mtoto wa mama wa kambo, yeye japokuwa aliweza kuingia kidato cha pili, lakini
alama za ufaulu wake zilikuwa za chini, na hali hiyo ilimfanya mdogo wangu huyo
azidi kujenga chuki ya chini kwa chini dhidi yangu, akawa ananipalilia fitina, iliyokuja kuharibu maisha maisha yangu.....
NB: Je ni nini kitatokea kwa mpendwa huyu
WAZO LA SIKU: Tunapoishi na watoto wa wenzetu, tuwatimizie mahitaji sawa na
watoto wako, ukiwatendea watoto wa wenzako vibaya, ukawadekeza watoto wako,
ujue unaowaharibu ni watoto wako, kwani unawajengea maisha mabaya siku zijazo,kumbuka
mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment