Ilikuwa usiku wa maneno, sikumbuki ni saa
ngapi, simu yangu ikawa inaita, sikutaka kuipokea, maana nilikuwa nimechoka
sana, kwani nilipotoka kazini, ili kumkwepa yule mdada, nilipitiliza hadi
uwanja wa mpira nikajiunga na wenzangu wengine kwenye mazoezi, na nilipotoka
hapo nikapitia sehemu nyingine, kuangalia mpira ligi za Ulaya,hadi saa tano,
nikarudi nyumbani na kulala.
Niliiwasha simu yangu ambayo nilikuwa
nimeizima makudi, ili huyo mdada asinisumbue, na ilipowaka tu, milio ya kuingia
ujumbe wa maneno, ikaanza kuingia kwa mfululizo, sikutaka kusoma huo ujumbe kwani
nilifahamu ni kitu gani anataka, nikaiweka simu pembeni, na mra simu ikaanza
kuita. Nikaangalia mpigani ni nani nikaona ni namba ngeni
Nikaacha ikalia mpaka ikakatika, baadaye kwa
kupoteza muda, nikaanza kusoma ujumbe alionitumia huyo binti, zilikuwa nyingi,
nikawa nasoma kwa haraka haraka, hadi nikafikia ujumbe ambao ulinitia wasiwasi
‘Nimekusubiri sana, bahati kaja huyu muhuni,
tumesihia kugombana, naomba uje unisaidie niondoke hapa...’
‘Oh, njoo haraka kuna tatizo kubwa, nakuomba
ufike haraka, ...la sivyo naituma ile picha kwa bosi wako.
‘Njoo, uniokoe, kama kweli unanipenda njoo, ....kuna
tatizo kubwa sana na wewe peke yako ndiye utaweza kunisaidia, usipofika,
utakuja kujijutia...’ na ikawa mwisho wa ujumbe.
Mara simu ikaanza kuita, nilipoangalia nikaona
ni namba nyingine ngeni, safari hii nikaamua kuipokea, na sauti ya mwanaume
ikasema;
‘Wewe ndiye Mosi?’ akauliza.
‘Kwani wewe ni nani?’ nikauliza kwa sauti
kali.
‘Ni muhimu, kuna dada mmoja yupo hapa,
amekunywa kupitiliza, hawezi hata kutembea, na amesema anakusubiria wewe,
hatuwezi kumuacha aendelee kukaa hapa, kasema tukupigie wewe uje kumchukua vinginevyo,
sisi tutamtoa na kumtupia kwenye mtaro wa maji machafu, hatulazi walevi humu
ndani....’akasema na kukata simu.
Mimi
niliwaza sana, huenda huo ni mtego, wamefanya hivyo makusudi ili nifike kwa
huyo mwanamke. Lakini kama ni kweli, kuwa huyo binti kalewa sana, na alitarajia
kuwa mimi ndiye nitaenda kumchukua, na balaa likimtokea, huoni kuwa nitakuja
kulaumiwa mimi na jamii, hapana, huu sasa sio ubinadamu
Kwa vile sio mbali sana, ngoja niende
nihakikishe mwenyewe....’nikasema
Tatizo kwenye nyumba hii ninayokaa mwenye
nyumba ni matata, kwani hufuatilia sana wapangaji wake, na hasa akikuona
ukitoka usiku, lakini sikujali, nikijua kuwa hiyo ni dharura.
Basi
nikawaza saana mwisho nikasema ngoja tu niende, kwani kutaharibika nini, mimi
nitakwenda, kama ni kweli kalewa mimi nitambeba hadi kwake na kwa vile anaishi
na mdogo wake, itakuwa rahisi, huyo mdogo wake, atamsaidia kumlaza kitandani,
na mimi nitarudi kwangu, sitataka kuongea naye
.
Nikatoka nje, na kuifuata pikipiki yangu na
wakati natoka mwenye nyumba akatokeza na kuniuliza;
‘Saa hizi unakwenda wapi?’ akaniuliza nikishangaa,
nikijiuliza huyu mtu huwa halali , ina maana muda wote yupo macho kuangalia
usalama wa nyumba yake.
‘Kuna mtu kanipigia simu ananihitajia
anaumwa’nikasema
‘Hiyo miito ya muda kama hii sio mizuri, kama
ingelikuwa mimi nisingelikwenda huko, nakushauri achana naye, puuzia huo muito,
kwa manufaa yako, rudi kalale, huyo mtu utamuona kesho.’akaniambia.
‘Hapana hiyo ni dharura, atakuwa mgonjwa, ni
muhumi niende tu’nikasema nay eye akaguna na kusema.
‘Haya utakuja kukumbuka ushauri wangu, ukirudi
hakikisha kufunga mlango wa nje...’akasema na mimi sikumsikiliza kwani akili yangu
ilikuwa ikimuwazia huyo mdada, huenda keshatupwa nje , na wahuni wanaweza
kumfanya vibaya.
‘Utakuwa ni uonevu, kwanini binti mrembo kama
huyu anajizalilisha hivyo...’nikawa najiuliza huku nikiendesha pikipiki langu
kwa mwendo kasi, kwani muda kama huo barabara ilikuwa nyeupe, sikuwa na
wasiwasi wa kukutana na magari.
Kwa vile kulikuwa sio mbali sana, nikawa
nimefika kwenye hilo jengo, nasikia mwanzoni ilikuwa ni nyumba ndogo tu ya
wageni,lakini baadaye imeboreshwa na kujengwa kuwa hoteli kubwa, lakini bado
watu wanapaita `nyumba ya wageni.
Nilifika hapo, sikupitia mlango wa kawaida,
nikapitia kwa nyuma,kwenye jengo hilo kuna mlango wa nyuma, mimi naufahamu
sana, unaweza kupenya, na kuingia ndani bila kupitia mlango mkuu.Sikutaka watu
wanione, maana huenda kuna watu bado wanasterehe zao, nikaingia kwenye mlango
wa nyuma hadi ndani sehemu ninayofahamu watu maalumu hukaa.
Nilishawahi kukaa kwenye hiyo nyumba ya
wageni, ni hoteli kubwa tu, ina sehemu za kulaza wageni, na mimi nilipofika
hapa kwa mara ya kwanza, nilipanga hapo, kabla sijapata chumba, kwahiyo kuna
sehemu za kupenya kama hutaki mtu akuone, na unachotakiwa ni kumpa yule mlinzi
kitu kidogo, kama akikuona.
Nashukuru sikuonekana, nikatembea hadi sehemu
ambayo nafahamu atakuwepo huyo mdada, lakini kulikuwa hakuna mtu, nikageuka
kutaka kwenda kumuona mmoja wa wahudumu wa hapo, kabla sijafanya hivyo, nikaona
ujumbe wa maneno.
‘Kama ukifika, nipo chumba 233, nimeamua
kulala hapa hapa....’
Nikajiuliza nifanye nini, maana huo sasa ni
mtego, nikageuka kutaka kuondoka na mara jamaa mmoja anayefanya kazi hum ndani
akaniona, ananifahamu akanijia na kusema;
‘Mimi ndiye niliyekupigia simu, huyu Mdada,
amefanya vurugu na jamaa yake, kumbe hawaelewani siku hizi, mimi nikaona kwa
vile kalewa sana, nimpele juu, kwenye chumba cha wageni, ...kwani hawezi kabisa
kutembea,...’akasema.
‘Oh, huyo jamaa yake yupo wapi?’ nikamuuliza.
‘Alitolewa na walinzi, kakasirika kwelikweli
...na kama angelikuwa na silaha angeliua mtu, ...’akasema.
‘Sasa kama huyo dada kalala, mimi naondoka,
...maana nikionana naye kwa sasa sitaelewana naye.’ Nikasema.
‘Kwanza nifahamu ni nani atalipia hicho
chumba, maana mimi nimetoa msaada tu...tumehangaika kumbeba hadi huko, na bosi
akifahamu tumefanya hivyo, bila malipo ya awali, tunaweza kufukuzwa kazi,
kwahiyo nakuomba kesho ufike na pesa....mimi nitakudhamini...?’ akasema baada
ya kuuliza.
‘Tutaongea kesho, anaweza kulipa mwenyewe,....
, hata mimi nitalipa lakini sasa hivi sikuja na pesa, tufanye kesho, ...’nikasema.
‘Ok, lakini ni vyema ukaenda kumuona,maana
alikuwa akikutaja sana kuwa tukuitie...’akasema huku akiniangalia na tabasamu
mdomoni, kuonyesha mzaha.
‘Hapana....’nikasema lakini kimoyo moyo,
nikaona ni vyema nifike nimuone huyo binti kama yupo salama, lakini sikutaka
huyo jamaa afahamu. Kwahiyo yule jamaa alipoondoka kuendelea na shughuli zake
mimi kwanza nikaangalia huku na kule kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayeniona, na
kwa haraka nikapanda juu, hadi kwenye hicho chumba nikagonga, kimiya, nikagonga
tena kimiya, nikazungusha kitasa cha mlango mlango ukafunguka....
**********
Mpendwa aliendelea kunisimulia kisa chake,
‘Lakini leo nakuona haupo sawa, kama mtu
ambaye hajapata usingizi....’Bosi akaniuliza
‘Aaah, nimechoka tu...’nikasema, huku akilini
nikiwazia yaliyotokea jana, sikutaka hata kuyakumbuka.
‘Nikuambie kitu, katika maisha yako penda
kujenga ratiba na mpangilia wa nyendo zako, na katika ratiba yako hakikisha
unakuwa na sehemu ya kutosha ya kulala, kulala ni muhimu sana kwa afya ya
mwanadamu, usipolala, unaweza kujiathiri afya yako, na hata utendaji wako wa
kazi ukawa mbovu.
‘Siku hizi nawashangaa watu badala ya kulala,
wanakalia kuchat. Wanatumia muda
muhimu wa kulala kwa kuongea na wenzao kwenye simu, na wanachoongea hakina
tija, kwanza unatumia gharama ya simu kwa hasara, kwanini mtu hujiulize gharama
hiyo niliyotumia kwa kuchat, ina marejesho gani yenye faida...’akatulia na
kuniangalia.
‘Kama mtu mwenye hekima, jenga tabia yenye
manufaa, kuwa kila gharama ina marejesho yake yenye faida, usikubali kupoteza
muda wak bure, ambayo ni gharama, muda ni gharama, kama usipoutumia vyema,
ukazalisha jambo basi ni hasara, na muda kamwe harudi nyuma, ni kama maji
ukiyamwaga aridhini yanapotea, ..muda haurudi nyuma, umri unakwenda mbele,
usija ukajutia muda wako ukiwa mzee, hautasaidia kitu...’akaniambia.
‘Kwahiyo muda wa kulala, hakikisha unalala,
ili kuuweka mwili wako sawa, gharama ya kulala, inalipwa kwa kuboresha afya
yako, usipolala, unaifanya ile gharama isiwe na marejesho kwahiyo ni hasara
kwako...sijui unanielewa...?’ akaniuliza pale aliponiona nimeduwaa.
‘Nimekuelewa bosi.....’nikasema huku nikiwa
kama mtu aliyezindukana kutoka kwenye usingizi, kwakeli nilikuwa nimechoka,
kimwili na kiakili, na moyoni nilikuwa ninajijutia kwa yale yaliyotokea jana,
....
‘Haya, leo kwa vile nina kikao baadaye,ngoja
nikuhadithie sehemu ya kisa cahangu, kwani hata hivyo, nakuona akili yako haipo
sawa, lakini kazi niliykupa jana umemaliza...?’akaniuliza.
‘Nimeshamaliza bosi, nimeshakutumia kwa barua
pepe....’nikasema.
‘Ok, sawa, ...nakumbuka kwenye kisa chetu, tuliishia
pale nilipoingia kidato cha pili, kidato hicho nakikumbuka sana, kutokana na
machungu yake...’akasema
‘Haya tuendelee na kisa chetu....’akasema
‘
‘Kidato cha pili kilifungua ukurasa mwingine
wa maisha yangu, kama nilivyokuambia, mdogo wangu ambaye tulikuwa tunasoma
naye, alishajenga chuki dhidi yangu, kwahiyo akishirikiana na mama yake wakawa
wananifitinisha mimi kwa baba, na kwa vile baba alikuwa haniamini tena, akawa
anaamini kila analoambiwa.
Siki
hiyo niliporudi nyumbani, nikawakuta mama na baba wanaongea, kumbe walikuwa
wakinijadili mimi, hawakunipa hata muda wa kupumzika, wakaanza;
‘Haya tuambie huyo mwalimu unayetembea naye ni
nani, ...?’ akauliza mama
‘Mwalimu gani ninatembea naye?’ nikauliza kwa
mshangao.
‘Ina maana na wewe unatuuliza swali, unafikiri
hatufahamu yote yanayotokea huko shuleni, kumbe kufaulu kwako kote huko ni
maksi za hongo,..’akasema baba.
‘Baba mbona mimi sielewi hicho mnachongea, ni
mwalimu gani huyo ambaye atakubali kunipa maksi, na mimi sina mazoea na mwalimu
yoyote,.....zaidi ya kimasomi darasani...’nikasema
‘Ndio tunafahamu kuwa mahusiano yenu yameanzia
kimasomo, na baadaye yamekwenda kimapenzi, unafikiri sisi hatujui ni kitu gani
kinachoendelea huko shuleni..’akasema baba.
‘Sio kweli, mimi sina mahusiano na walimu,
....kama ni kuonana nao ni kwenye masomo tu...’nikasema
‘Juzi ulikwenda kwa mwalimu wako wa hisabati
ulifuata nini?’ akauliza baba, ni kweli nilikwenda kwake, kwasababu yeye
aliniagiza nikachukue madaftari, na wakati huo yeye alibakia shuleni,
nikayafikisha, sasa sijui taarifa hizo zilikujaje nyumbani tena kwa kupotoshwa.
‘Ni kweli nilikwenda kwa huyo mwalimu,
alinituma madaftari yetu, nikamkuta mke wake..yeye alibakia
shuleni...’nikajitetea.
‘Unaonaeeh, ulikwenda nyumbani kwake, na sio
mara ya kwanza, na somo hilo unafaulu sana, na mwalimu huyo nasikia yupo karibu
sana na wewe. ...’akasema baba.
‘Mwalimu huyo ananifahamu na kunituma kwa vile
nafaulu sana somo lake....’nikajitetea.
‘Unaanza kusema mwenyewe, sasa sikiliza,
nimeyachunguza haya yote na wewe mwenyewe umenithibitishia hivyo kuwa
unafahamiana na huyo mwalimu, adhabu yako utabakai hapa nyumbani hakuna kwenda
shule...’akasema baba.
‘Lakini baba mitihani inakaribia na mimi sina
kosa lolote, kwanini msiwaulize walimu kama kweli mnayosema ni
sahihi...’nikawaambia.
‘Siwezi kupeleka kesi ya tumbili kwa ngedere,
hawo hawo ndio mnaofanya nao umalaya, halafu nikawaulize, nimeshasema utabakia
hapa nyumbani, hakuna kwenda shule, tuone huo umalaya wako utapeleka wapi..’akasema
baba, na mama akasema;
‘Na humu nyumbani hakuna kutoka, utakuwa
ukifanya kazi za hapa nyumbani, kutoka kwako ni mpaka mimi nikutume, na
utakwenda na mtu...’akasema mama.
Mimi nikaona nitumie mbinu, kwani mitihani
inakaribia, na wao nia yao labda ni kunikomoa ili nisifaulu mitihani, na
nilifahamu hizo ni mbinu za huyo mdogo wangu, ili nisifaulu mitihani,
nilichofanya ni kuwaomba majirani zangu ambao nasoma nao, wanipatie madaftari
yao, nikawa naandika nikiwa nyumbani na kujisomea.
Majirani na watu wakaanza kumsema baba kuwa
anachofanya si sahihi, ni kumnyima mtoto haki yake, na hata serikali ikijua
atachukuliwa hatua za kisheria, hapo akalegeza kamba, na kuniruhusu niende
shuleni. Nilipofika shuleni, nikaamua kutulia, na kusoma yale yote waliyofundishwa
wenzangu, na mtihani wa taifa ulipokuja nikaweza kuufanya na mungu akanijalia
nikafaulu kuingia kidato cha tatu.
Mdogo wangu kwa tabia yake mbaya , hata walimu
wakamfahamu, na alishapewa onyo, lakini hakusikia, hata mtihani huo akawa
hakufaulu, kwahiyo hakuweza kuingia kidato cha tatu, na kwa utukutu wake,
walimu wakaamua kumfukuza, mimi nikaendelea na masomo yangu nikiwa kidato cha
tatu, nikijiuliza je wazazi watasemaje maana huyo ndiye waliyemtegemea kama
mlinzi wangu.
Maisha ya shule kama unavyoyafahamu, kuna ile
hali ya wanafunzi kuwa marafiki, wakike na wa kiume, na mimi nikawa naandamwa
na wanaume, kila mmoja akitaka urafiki na mimi, nilijitahidi sana
kutokujishughulisha na mambo hayo, lakini kama binadamu inafikia mahali unasema
ngoja na mimi niwe na rafiki tu, japo tu wa kuongea naye, kama walivyo wenzangu
, sikuwa na nia ya kuwa na urafiki wa mapenzi ya ndani.
Ushawishi huo ukaniteka akili yangu, na marafiki
zangu wakawa wananishawishi kuwa ukiwa na rafiki wa kiume, ataweza pia
kukulinda na mabaya mengine, kwani wakati mwingine uantembea sehemu yenye
hatari, lakini ukiwa na rafiki wa kiume karibu yako, unakuwa na usalama zadi,
na mimi hilo nikaliona lina umuhimu wake, japokuwa kwa umri wangu, nilikwa
siogpi sana.
Kazi ikawa kumpata rafiki wa kweli, ambaye
atanielewa, walikuwepo wengi wanaofaa, lakini sikuwa na mazoea nao ya karibu
sana, lakini siku moja, nikakutana na kijana moja ambaye alinionyesha upendo
dhati, ilitokea tu, hata siwezi kueleza ilikuwaje, akawa karibu na mimi sana, kila
nikiwa mnyonge anakuwa karibu kuniliwaza, na kunipa moyo, nikiwa na shida ya
kimsomo, anakuwa karibu name, tunasaidiana.
Kwakeli kijana huyo akaiteka nafsi yangu, na
akili yangu ikatokea kumpenda, nikaona huyo anafaa kuwa rafiki yangu wa karibu,
kwanza alikuwa sio muhuni, hakuwa kwenye yale makundi mabaya, na katika
maongezi yetu,alikuwa akiweka mkazo sana swala la masomo, nikaona huyu
atanifaa, kwani hataniharibia maisha yangu. Kwa ujumla nikapmenda sana na niliendelea
na masomo yangu vizuri tu huku nikiwa na uhusiano na huyo kijana, wa maongezi
tu.
Kumbe mdogo wangu alikuwa anatumwa kuja
kunichunguza, na alipogundua kuwa nina rafiki wa kiume, ambaye mara kwa mara
nipo naye, akaenda kutoa taarifa huko nyumbani, na kuwaambia wazazi wangu kuwa
nina mwanaume, na ameshanifuma nikifanya mapenzi na huyo mwanaume, kitu ambacho
sio kweli.
‘Baba mimi nina uhakika nimewaona kwa macho
yangu...’akasema huyo mdogo wangu akiwaambia baba na mama.Na niliporudi
shuleni, kabla sijaweka vifaa vyangu nikaitwa na kuanza kuhojiwa.
‘Haya tuambie huyo mwanaume wako ni nani?’
akauliza baba.
‘Mwanaume gani baba?!’ nikauliza kwa mshangao.
‘Huyo uliyekuwa ukifanya umalaya naye,..kila
siku upo naye, haya bisha kuwa huna mwanaume shuleni ambaye kila siku
mnaonekana naye’akasema mama.
‘Hao ni wanafunzi wenzangu, tunakuwa na
vikundi vya kujisomea, hakuna lolote baya nimelifanya..’nikajitetea
‘Hivyo vikundi ni vya kwako wewe mwenyewe, na
huyo mwanaume, na hizo kazi mlizopewa ni za kufanya mapenzi, mnafundishwa hivyo...’akasema
mama kutilia chumvi
‘Mapenzi!!?’...nikauliza kwa mshangao.
‘Unajifanya hujui,..hujui maana ya mapenzi,
wakati wewe ni mwalimu wao, nasikia unaongoza kwa umalaya hpo
shuleni...’akasema mama
‘Jamani hayo yametoka wapi, kwanini
mnawasikiliza watu, kwanini hamfiki shuleni mkawauliza walimu, watawaambia
tabia yangu ilivyo, huo ni uwongo...’nikasema.
‘Tatizo lako wewe ni mbishi, muhuni, na
unatufanay sisi ni watoto wadogo, huko ulipofika sisi tulipitia, tunafahamu
sana ..lakini sisi hatukuwa Malaya kama wewe, tulivumilia hadi tukaolewa, sasa
wewe unaona umefika,....’akasema mama, na wakati huo baba alikuwa anasikiliza,
macho yalionyesha chuki, hasira, na kama angelikuwa na kitu kibaya angeniumiza
kabisa,...baadaye baba akasema;
‘Mnaona wenyewe sasa...mimi nilipoamua huyu
mtu asisome mkanina mimi ni mbaya, mkaniatangazia kwa majirani kuwa sipendi
maendelea ya watoto wa kike, sasa mumeyaona wenyewe,... sasa haya yamethibitika
waziwazi umeonekana ukifanya umalaya wako na huyo mwanaume wako, ...’akasema baba
kwa hasira huku akitafuta fimbo.
‘Baba sio kweli, sijawahi kufanya mapenzi na
mtu yoyote, huyu ni muongo tu..’nikasema lakini baba hakusikiliza, alichukua
fimbo na kuanza kuniadhibu kwa viboko huku nikiwa nimefungwa kamba, kichwa
chini miguu juu.
Na hiyo haikutosha chini, kwa pale waliponining’iniza,
kichwa chini , miguu juu, wakaweka jiko la mkaa, likiwa karibu sana, joto
likawa linanipandia usoni, na hapo nikaachwa nikae hapo hapo, usiku kucha, na
ni baada ya kupigwa na fimbo hadi fimbo kukatika katika na kuishia mwilini.
Nililia na kuomba msamaha, japo sikufanya
kosa, lakini hakuna aliyenisikiliza, na baba alipochoka kuniadhibu akasema;
‘Sasa nakusimamisha shule kabisa, wewe si
unataka kufanya uhuni kunidhalilisha mimi huko shuleni,nasikia umeamua kufanya
hivyo, ili unizalilishe mimi, nionekane sijui baba asiyejua kulea watoto, .... sasa mimi nakusimamisha kabisa shule, sahau kabisa kuhusu shule, maana wewe shule ilikuwa sehemu ya kujifundishia uhuni, huko hutaenda
tena...’akasema baba kwa hasira.
Iliniuma sana kwa vile ilikuwa imebakia muda mchache
sana, wa kufanya mitihani ya kuingia kidato cha nne, na kwa hali ilivyo,
ilionekana dhahiri kuwa kweli baba kadhamiria nisiendelee na shule,hata sikujua
nifanye nini...
NB: Je niliruhusiwa kufanya mtihani, au ndio
ilikuwa mwisho wa masomo yangu,...tukutane sehemu ijayo
WAZO LA LEO:.Unapoletewa
taarifa zenye dalili ya fitina na uwongo, usizichukulie kama zilivyo , kwanza
zichunguze kabla hujaamua lolote, kwani sio watu wote wanaokutakia mema.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment