Wakati bosi ananisimulia kisa chake akili
yangu ilikuwa mbali kabisa, ikinipeleka kwenye tukio la usiku wa jana, ilikuwa
kama ndoto ndani ya kisiwa cha ajabu, ambacho sijawahi kukifika, ni kweli sina
tabia hiyo, na kwa siku hiyo ilikuwa ni kwa mara ya kwanza.
Katika
maisha yangu nimekuwa nikijaribu kuishi maisha mema, bila kujiingiza kwenye
matatizo, na siku zote nimekuwa nikifanikiwa, lakini nilipojiunga kwenye
kampuni hii nimejikuta nikitekwa na majaribu makubwa na chanzo kimekuwa ni huyu dada ambaye alijulikana kama Mdada.
Kwakweli nilishindwa kujua ni kwanini, namuwaza yeye tu, na nikimuoma moyo wangu unanienda mbio, na akinikaribu ndio basi tena, nakuwa kama mtu aliyepagawa,...sijui kanifanyia nini. Nimejaribu sana kuishinda nafsi, na kujaribu kutokumuwaza yeye, lakini imekuwa ni vigumu.
Sasa tukio la jana ndio likaharibu kila kitu,.....
‘Naona Mdada anaumwa, kanitumia ujumbe, kasema anaumwa leo hataweza kuja
ofisini, na kaniomba, wewe uende kumsaidia kumpeleka hospitalini....’akasema bosi
‘Kwanini mimi bosi, dereva wetu si yupo...?!’ nikauliza kwa mshangao.
‘Mimi sijui, labda kwa vile mlikuwa naye
jana...’akasema bosi na kunifanya nishangae bosi kafahamia vipi kuwa nilikuwa
na huyu mtu jana, na hapo hapo nikamuuliza;
‘Unasema tulikuwa naye jana, wapi....?!, mimi nakumbuka tulikuwa naye hapa ofisini, akatoka na mimi nilitoka baadaye, nikaenda mazoezini,
lakini mbona sifahamu kuwa anaumwa?’ nikawa najiuma uma, na bosi akaniangalia kwa mashana na kusema;
‘Je utaweza kwenda kumpeleka hospitalini au
nimtume dereva wetu ampeleke, lakini ningeshauri kwa vile hakuna kazi nyingi
nenda kampeleke, ili nihakikishe kuwa kweli anaumwa..’akasema bosi
‘Kwani mimi ndio nitakuwa kipimo kizuri cha
kumtambua kuwa kweli anaumwa, anaweza akaigiza kuwa anaumwa, na wala mimi nisifahamu ukweli, si uamfahamu anavyojua kuigiza jambo, utafikiri ni kweli..’nikasema
‘Na ndipo maana nakutuma wewe ili niufahamu uaminifu wako..’akasema
‘Ina maana bosi huniamini mpaka sasa?’
nikamuuliza kwa mshangao
‘Kwenye swala la mapenzi, ni nadra sana kumuamini
mtu, hata mume au mke wako nyumbani, huwezi kumwamini mia kwa mia, kwasababu mengi yanayofanyika katika nyanja hiyo hufanyika kwa siri, ...na
siri kubwa ni ile iliyopo moyoni,...kwahiyo kwa kifupi sijaweza kukuamini katika
swala kama hilo...’akasema bosi.
‘Sasa nifanye nini ili uweze kuniamini?’
nikamuuliza
‘Kwa sawala kama hilo, ni vigumu, na naweza kusema hilo halinihusu sana, hayo ni maswala binafsi,
ila nakutuma uende kwa huyo binti, nataka kufahamu kama kweli anaumwa, na kama
anaumwa uweze kumsaidia...ni hivyo tu, mengine niachie mwenyewe....’akaniambia na mimi akilini nikawa najiuliza bosi
anataka kunipima kitu gani hasa, je anafahamu nini kuhusu jana, mbona ni kama anafahamu yaliyotokea jana, je nikikataa kwenda atanifikiriaje....
‘Kwani bosi huyu binti unamfahamu kivipi,
zaidi ya kikazi,...?’ nikamuuliza na yeye akaniangalia huku akionyesha uso wa kushangaa
'Kwanini leo unaniuliza hivyo, jana umeingia kwenye msimamo gani, maana nakuona una waza sana, na pili ni kama kuna jambo umelitenda na unajishuku...?' akaniuliza
'Hapana bosi hakuna kitu, ila inanipa mashaka sana kuhusu huyu binti, naona kama ananiweka kwenye wakati mgumu, ...'nikasema, na yeye akaniangalia kwa makini halafu akasema
'Katika maswala ya mapenzi, kuna mambo unatakiw auwe makini nayo, kuna mshawasho wa kutamani,na kuna kupenda. Nafasi inaweza ikaona kitu, na kukitamani, na hapo unatakiwa uweze kuitawala ile nafsi kwa kujiuliza je kuna faida gani, au kuna uhalali w hicho kitu, ukiona kina madhara, unatakiwa kuikataza hiyo nafsi kwa haraka, ...ndio kama vile unapoona pombe au sigara, kwa mara ya kwanza, .....'akatulia.
'Ukianza kuvuta sigara au kunywa pombe, ni kwamba umeshaikubali ile hali ya nafsi yako, lakini kumbe ungeliweza kuikataza na ukaishinda, ...ukiendekeza hiyo hali, ndio unakuwa mlevi, mzinzi, mwizi na kadhalika...
'Sasa basi hapo ulipo, unapambana na nafsi yako, umeona kitu nafsi imekitamani, je kinafaa, je ni halali, ...unatakiwa uiulize nafsi yako , na muda wa kujiuliza ni sasa...ukifanya makosa, utakuja kujijutia, ....'akasema na kuniangalia machoni.
'Ndio maana nataka kumfahamu vyema huyo binti.....'nikasema
'Ili iweje, ....kwanza iulize nafsi yako, ichanganue kwa yale uliyoyaona, sawa, ...kama umempenda, na sio mshawasha wa kutamani, una haki ya kumchunguza vyema, ...kupenda ni mtihani, ...'akatulia na kuniangalia kwa makini.
‘Unauliza namuelewaje huyo binti, huyo binti namuelewa kama ninavyokufahamu wewe, ..., nikuambie
ukweli, huyo binti, nilipompokea hapa kazini, nilimtendea kama binti yangu,
nikawa najaribu kumsaidia, kwa jinsi nilivyoona mimi inafaa...lakini mimi ni muajiri wake tu, sina mamlaka ya undani zaidi kama mzazi....'akatulia kidogo.
'Kwanza nilimuona kama mtu mwenye matatizo, ambaye kaishi kwenye mateso au kukosa haki za mtoto, lakini nikagundua kuwa tabia aliyo nayo ni ya kwake binafsi, ni ya kujiingiza kwa tamaa, ...nikajaribu kadri ya uwezo wangu kumnyosha, lakini kama wanavyosema wahenga samaki umkunje akiwa mbichi, akishakauka ...mmh....'akatulia kidogo.
'Una maana huyo binti hana tabia nzuri,...hanifai...mbona jana ulinishawishi....'nikatulia.
'Sijasema hana tabia nzuri, hilo halipo akilini mwangu, nimesema kuna mambo anayaendekeza, na anaweza kuyaacha akiamau, ni mnzuri tu, tatizo lake anaona kuwa labda wanaume ndio wataweza kumsaidia, nilimkanya kuhusu hilo, nikamwambia kuwa kila
mtu ana mattizo yake, na msaada mkubwa wa matatizo ni mtu mwenyewe, kama
mwenyewe hutaweza kujisaidia usitegemee mtu mwingine akaja kufanya
miujiza...’akaniambia.
‘Mhh, umesema huyo binti alionekana kama ana matatizo, kwani ulivyoona wewe, huyo binti ana matatizo gani?’
nikamuuliza
‘Kama kweli anakupenda kama anavyodai, ipo
siku mwenyewe atakuambia, utamuona na kila kitu kama utakuwa mwangalifu, kitajionyesha cheyewe, cha muhimu uwe mwangalifu, uwe makini kwa kila hatua, maana yeye anaonekana kuwa mjanja kuliko hata wewe...’akaniambia na kuniangalia machoni, na mimi nikawa
nimetulia nikiwa nimetingwa na mawazo, hasa nikiwazia tukio la jana..
'Mhh...'nikaguna na kushika kichwa, na bosi aliponiona hivyo akawa anaandika ujumbe kwenye simu yake halafu akaniangalia na kusema;
‘Ngoja sasa nikusimulie kidogo sehemu ya
maisha yangu, nikimaliza, nitakuruhusu uende umpeleke huyo binti hospitalini ,
nimeshamwambia aanze kujiandaa, ukifika mnandoka, sio tena unafika ndio anaanza
kujiandaa, siunafahamu akina mama tulivyo.
‘Japokua hisia zangu zinanituma kuwa huenda
jana atakuwa alilewa sana, kwani kuna siku huyu binti anakunywa, ....kupitiliza, nimejaribu
sana kumkanya hiyo tabia, kuwa mawazo hayandolewi kwa kuyaahirisha kwa kulewa, lakini ..mmh, ni sikio la kufa halisikii dawa,..sasa kama
kweli anaumwa, ni muhimu uhakikishe anafika hospitalini.
'Kama ukirudi mapema tutaendelea na sehemu
nyingine ya maisha yangu...lakini kwa sasa ngoja nikusimulie sehemu hii ndogo ya yaliyotokea baada ya baba kutoa maamuzi yake,....’akaniambia na mimi sikuweza kupinga tena, nikakaa
kimiya nikimsikiliza bosi kuhusu maisha yake, huku moyoni nafahamu vyema, huyo
binti sio mgonjwa, bali ni kutokana na tukio la jana, sikutaka kumwambai bosi
ukweli,..
******
Ni kweli baba akanisimamisha shule, hakutaka
tena kuwasikiliza watu, si majirani wala ndugu zake, waliokuja kumshauri, yeye
akasema ameamua na hataki mtu kumuingilia maisha yake na familia yake;
‘Mimi nimeshaamua, sitaki kusikia upuuzi
wowote, nafahamu kabisa huyu binti akienda kubeba mimba huko shuleni mtakuja
kunilaumu mimi,....’akasema pale alipokuja kaka yake kumuomba aniruhusu kwenda
shule.
‘Lakini broo, hata akiwa nyumbani anaweza pia
akafanya hayo unayohisi anayafanya huko shuleni, cha muhimu ni elimu, elimu ni
wajibu kwa mzazi kumpatia mtoto wake, awe wa kike au wa kiume, hata dini
zinatushauri hivyo...’akamwambia kaka yake.
‘Hiyo elimu aliyoipata inamtosha kabisa, kwa
mtoto wa kike anataka nini zaidi, akizidi kusoma anakuwa na kiburi, angalia tangu
alipofika hicho kidato cha tatu, akirudi hafanyi kazi anasingizia kuwa eti ana
hiyo wanaita homework, kila siku homework, ni ujanja ujanja wa kipuuzi, ili
asifanye kazi, hapo ni mwanzo tu, je akifika huko juu, itakuwaje,...’akawa kama
anauliza na ndugu yake akawa anatikisa kichwa kwa kusikitika.
‘Sasa mimi nimeamua sitaki kusikia lolote,
atabakia hapa hapa nyumbani kama ndugu zake wengine, hawo mabinti wengine wapo
nyumbani, wana maadili mema, sijasikia maswala ya uhuni au umalaya, huyu kaenda
shule, ndio kila siku kesi, kafumaniwa, kaonekana, sasa nitakuwa kazi yangu ni
kesi, nitafanya kazi saa ngapi...’akasema baba .
‘Ndugu yangu, hayo ya kesi, ugomvi, ni
majukumu ya wazazi wote, sio kwamba wengine hawakumbani na majukumu kama
hayo,yapo, lakini wewe maamuzi yako sio ya hekima, kumzuia mtoto asisome, na
wakati kafaulu, ni makosa makubwa sana, unamdhulumu mtoto haki yake...’akasema
ndugu yake huyo.
‘Nimeshasema tusiingiliane katika maswala ya
kulea watoto, sijafika kwako na kukulaumu kuhusu mambo yako, haya niachieni
mwenyewe, nafikiri tumelewana, sina zaidi..’akasema kwa hasira na ndugu yake
akashindwa na kuondoka.
Kwakweli hatua hiyo ya kukatazwa kabisa kwenda
shule, iliniuma sana, nikawa mtu wa majonzi, hata machozi yakawa hayatoki tena,
kwani kila nilipowaona wenzangu wakienda shule,niliumia sana moyoni, nikabakia kumuomba mungu ashushe ehema zake,
huenda baba akabadili msimamo wake, lakini hilo halikuwahi kutokea, na kila
siku iliyopita ilikuwa ni aheri ya jana,..
‘Hivi mimi nina kosa gani hadi nitendewe hivi?’
nikajiuliza nikiwa nimejikunyata baada ya kuchoka na kazi za nyumbani, nilikuwa
nimekonda, nguo ni zile zile, sitamaniki,....
‘Au ni kwa vile mama yangu hayupo hapa?’
nikazidi kujiuliza, lakini hakukuwa na majibu ya haraka, kwani huko mama alipo
anapelekewa taarifa kuwa mimi bado nasoma.
Basi tena, ikabidi nikubali hali ilivyo,
nikukijua tena mimi shule ndio basi, na kwahiyo hata maisha yangu ya baadaye
yamefikia kikomo, kwani ni nani angelinioa mimi, kama wanavyodai wao,kuwa mimi
ni muhuni malaya sina adabu, ni mwanaume gani atapenda kuoa mtu kama mimi, kila
sehemu watu wameshaniona mimi ni mbaya, malaya muhuni, kwani mama alikuwa
akimuhadithia kile aliyefika hapo nyumbani;
‘Mtoto huyu mimi amenishinda, ana tabia chafu,
sijui kamfundisha nani, labda huko alipotoka, maana ni muhuni malaya, akifika
shuleni yeye ndiye mwalimu wao...’akasema mama.
‘Lakini una uhakika na hayo unayoyasema mama
nanihii....?’ akauliza jirani yake akitaka kunitetea.
‘Nafahamu yote, si alikuwa akisoma na huyo
ndugu yake darasa moja, alikuwa akimuona. Kaka yake alikuwa akijaribu kumkanya,
lakini hakusikia, yeye alimuona kwa mcho yake akimuona akitembea na wavulana
hapo shuleni, na kwasaabbu ni kaka yake amdogo wake kikamponza kwa kusema siri
za ndugu yake huyo, maana mtoto huyu alishafikia hatua ya kutembea na walimu...’akasema
mama wa kambo.
‘Oh, ilishafikia huko, mbona bado mdogo sana, na
haonekani kuwa hivyo...!’ akashangaa huyo jirani.
‘Ana udogo gani huyo, mwali mzima wa kuolewa,
udogo ni wa umri tu, lakini kwa matendo hata mimi simfikii, anafahamu kila
kitu, hebu muulize hapo, mamb anayoyajua ya mapenzi, uzazi, hutaamini....’akasema
mama.
‘Lakini hayo ya uzazi, ni masomo yao
wanayofundishwa mashuleni, ....mimi nijuavyo, watoto wa sekondari,
wanafundishwa mambo ya uzazi, ni sehemu ya masomo yao, sio uhuni huo...’akasema
huy jirani.
‘Wanafundishwa wakafanye mapenzi, vichakani na
madarasani na walimu wao, mbona wenzao hawafanyi hivyo, ni tabia yake chafu tu,
huenda ni ya kurithi toka huko alipotoka, yeye akifika shuleni, mazungumzo,
matendo yake ni hayo, umalaya uhuni...’akasema mama.
‘Mhh, hayo makubwa, hata siamini, ni mtoto
huyu huyu ninayemfahamu mimi, ...?’ akauliza
‘Sasa unahisi sisi tunamsingizia, ili tupate
nini, angalia kaka yake huyo, wanayesoma darasa moja kafukuzwa shule, kisa eti kwa
vile katoa siri za mahusiano ya dada yake na walimu wake. Ikabidi wamsingizie
mtoto wangu huyo kuwa kafeli mitihani, wakati mtoto wangu ana akili, na wakati
mwingine yeye ndiye aliyekuwa akimfundisha huyo dada yake...sasa na huyo naye utasema
tunamsingizia, na akae nyumbani kama ndugu yake...’akasema mama.
Baada
ya mda nilikubaliana na matokeo nikamua kuendelea kutii amri ya baba,hata ule
mtindo wa kuomba madaftari kwa wenzangu nijisomee, kuwa huenda baba akabadili
msimamo wake nikarudishwa shule ukasimama, kwani waliligundua hilo nikapigwa
amrufuku kuonekana nimeshaika madaftari, basi nikaona haina haja, ngoja nikae
kama wanavyotaka wao.
Hata baada ya kutii kila wanachokitaka bado
haikusaidia kitu, kwani mitihani iliendelea kuniandama,baba akaamua kabisa
kutokuaongea na mimi, akanitenga, akiniona ni mimi ni kama kaona takataka
fulani.Mwanzoni nilifikiria baba ananichukia kwa vile mimi ni mtoto wa kike,
lakini mbona hakuwafanyia hivyo, watoto wa mama huyo wa kambo, kwanini hayo
ananifanyia mimi tu.
‘Watoto wangu wenyewe wapo hapa nyumbani,
hawasomi, wanasingiziwa hawa akili shuleni, ...’siku hiyo akasema mama.
‘Lakini kwenye mitihani yao ulikuwa
ukifuatilia kama kweli wamefelishwa kwa makusudi...?’ akaulizwa.
‘Muda huo wa kufuatilia sina, waache wote
wakae hapa nyumbani, kinachonisumbua ni watu kuniona eti mimi namnyanyasa huyu
binti, kwa vile haendi shule, mbona hawaulizi kuhusu watoto wangu ambao wapo
hapa nyumbani...’akasema.
Ikafika siku ya sikukuu, ambapo watoto
wanatakiwa kuvaa vizuri na kufurahi na wenzao, baba hakutaka hata kuniona kabisa,
kitu ambacho kiliniuma sana kuona baba ananitenga kiasi hicho. Nilihuzunika
sana kuona,wenzangu wakiwa na furaha na shangwe, wananunulia hiki na kile
lakini mimi nilikuwa kama sio mtoto wake wa kumzaa, nikabakia chumbani na
kulia, hadi nikashikwa na usingizi.
Kwakweli nilijiuliza sababu ya msingi ya baba
yangu kufanya hivyo sikuweza kuijua mpaka sasa nimekaa kwa shida sana na kutengwa
na asilimia kubwa katika familia bila kujua sababu ila sikutaka kufanya kitu
chochote cha ajabu maana nilikua nampenda sana baba yangu. Nilijua baba
anachofanya sio yeye, ni kutokana na mama, mama alijitahidi kupandikiza fitina,
hadi moyo wa baba ukajaa chuki zidi yangu, kwahiyo, moyoni nikawa sina kinyongo
na baba yangu.
Pamoja na yote hayo sikukata tamaa, maisha yakawa
yanasonga mbele, hata hivyo kila siku mamb yalikuwa yakizidi, kila siku
kunazuka jipya kubwa zaidi ya la jana, shida nazo zikawa zinazidi, mateso
yakawa yanaongezeka, na kulikuwa hakuna wa kunitetea hata pale nilipojaribu
kujitetea, hakuna aliyenisikiliza kabisa, ni kama vile walikuwa hawanitaki
kabisa nionekane kwenye hii dunia,....
Siku moja nilitoka kwenda nyumba ya jirani
nikiwa na mtoto wa kaka yangu wa kambo , nikiwa huko , mara akaja msichana wa
kazi;
‘Dada unaitwa haraka nyumbani...’akasema huku
akihema.
‘Kuna nini tena ...?’ nikauliza nikiwa na
wasiwasi, na mwili ukaanza kuogopa.
‘Mimi sijui , nimeambiwa nikuite haraka uende
nyumbani...’akasema
Nikawaaga
jirani zangu na kukimbilia nyumbani, nilipofika sikumuona mama wala baba, na
hata yule mfanyakazi alikuwa hayupo ili nimuulize ni nani aliyeniita, na wakati
naangalai huku na kule, mara ghafla kaka zangu wawili wakaanza kunipiga bila
kujua sababu ya kipigo hicho.
Wakanibeba na kunipeleka chumbani, na wote
wakaanza kunipiga bila huruma utafikiri wanapiga mwizi, hawakuangalia wanapiga
wapi, kichwani, mwilini, ni kama wanataak kuniua, kwasababu ya kipigo cha muda
mrefu nilianza ku tokakwa na damu, puani mdomoni, hadi sehemu za siri, hadi nikapoteza fahamu....
NB: Je kuna kitu gani
kilitokea,
WAZO LA LEO:
Ukiwa peke yako jaribu kufikiri hekima ya
mawazo yako, na uwaze kadri ya uwezo wako, na wakati unaongea na watu chunga sana
maneno yako, kwani kauli ikitoka mdomono ni sawa na risasi, inaweza ikaua ,
ikajeruhi au ikaleta kitoweo, kitoweo ni mambo mema kutokana na hekima ya kauli
yako. Twawatakia Ijumaa njema.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment