BAADA
YA DHIKI FARAJA
Utangulizi
Nikiwa na barua yangu mkononi, nilifika kwenye ofisi
niliyoelekezwa, muda hu nilishachoka kutokana na jua kali na kutembea kwa miguu,
ajira siku hizi ngumu kweli, unaweza ukamaliza kiatu kwa kutembea kila ukifika
kwenye ofisi unachona na kiratasi za kupunguzwa wafanyakazi, hata hivyo
sikukata tamaa nikajua kazi nitapata tu.
Leo hii nikaamukia kwenye ofisi mojawapo, ambayo kwa taarifa
za haraka inamilikiwa na mzawa, ni mtu aliyejiwekeza, hadi akafanikiwa, na
alikuwa akitafuta mhasibu. Niliamuka asubuhi sana, nikijua usafiri ni wa shida,
nikaingia kwenye dala dala hadi kwenye hizo ofisi, nilipofika zikutaka
kuulizia, maana ofisi yenyewe ilikuwa ikionekana, jina la ile kampuni lilionekana wazi, kwenye
jengo hilo, ilikuwa sio kubwa sana, na
kama nilivyoelekezwa, ni kampuni ya mtu binafsi.
Nikagonga geti, na mlinzi akanifungulia, akaniuliza wewe ni
nani na umekuja kufanya nini, nikamweleza, akanionyesha wapi nielekee,
nikakatembea hadi kwenye jengo lenyewe la ofisi, nikafungua mlango na kuingia
kwenye hiyo ofisi, cha kwanza kukutana nacho ilikuwa kelele za..
‘Piga, ua,...kata mtama, oooh, ..., nitakuua, huna adabu
wewe...huniwezi...’
Mbele yangu kulikuwa na baadhi ya wafanyakazi, niliona
wakiwa kwenye heka heka za kuamua ugomvi, kulikuwa na jamaa wawili walikuwa
wakipigana, kwa nguvu zote, hadi makoti yao ya suti, yakawa yamechanika,
hawakuwa wakijali, nikashikwa na mshangao,
hakuna aliyejali kuniuliza wewe ni nani na unataka nini, maana kila mmoja
alikuwa akitafuta upenyo wa kuangalia pambano la majamaa wawili ambao walivalia
suti za ofisi, japokuwa sasa mashati ya ndani yalikuwa yamelowa majasho.
Hata ,mimi nikaingiwa na hamasa ya kuona lile pambano,
nikatembea hadi pale, jamaa walikuwa wamepigana miereka, wapo chini, na moja
damu zilishaanza kumvuja puani, huyu wa juu,akawa ana msindilia mwenzake magumi
ya nguvu kama anataka kuua, na mwenzake akawa akijaribu kujizuia,kwa muda ule hakuna
aliyeweza kuwaamulia, watu walishachoka kuwaamua, wakaona wawaachie watwangane
hadi hamu zai ziishe.
‘Jamani hawa watu si watauwana?’ nikauliza kwa mshangao.
‘Waache wauwane, tumewaamulia lakini hakuna anayetujali,kisa
kidogo tu kimewafanya wapigane hivyo,mapenzi, yamegukia siasa, mara imani zao
za dini...’akasema mmoja wapo akiwa haniangalii, ila anaangalia hilo pambano.
‘Yule atashinda tu kwa jina la Yesu,...’akasema mmoja wapo
na mwingine akadakia
‘Na yule atashinda kwa nguvu za Allah...’akadakia mwingine
aliyekuwa pembeni yake
Nikashikwa na butwaa, dini hapa zimeingiaje tena, nikatulia,
na mara kukazuka mabishano ya wale waliotaja imani za dini zao kuwa hawo
wanaopigana watashinda kwa nguvu za imani zao, kwani haw wanaopigana walikuwa
na imani tofauti, kwahiyo hata washabiki wakawa wanamtetea kila mmja kutokana
na imani ya dini yake...
Hutaamini hawa wenzao, wakaanza kubishana kwa maneno makali,kila
mmoja akitetea nguvu za imani yake, ikawa kama vurugu tena, ..mzozo ukazidi na
watu wakaanza kushikana mashati, na wale waliokuwa wakipigana awali walikuwa
wamechoka, wakiwa kama majogoo, waliopigana muda mrefu.
Lakini pambano lao lilikuwa halina nguvu tena, kilichokuwa
na nguvu ni huu mvutano uliotokea kwa watazamaji, ambao walikuwa wakitupiana
maneno makali kukashifiana, kila mmoja akiongea yake, na ilionyesha wazi, hawa
wanaopingana kwa maneno makali ya chuki na kashifa wakieleza kwenye imani za
dini za mwenzake, hawakuwa wakizielewa dini zao vyema, kutokana na hoja
walizokuwa wakizitoa, lakini jaziba, zilikuwa zimewapanda, na mara fujo
ikaanza....
‘Nyie kuna nini hapa....’sauti kali ya kike ikasikika, na
mara watu wakatawanyika, mbio mbio kila mmoja akikimbilia sehemu yake ya kazi,
kumbe alikuwa ndio bosi mwenyewe kaingia, nikageuka taratibu kumwangalia huyo
bosi, ....nilishangaa, maana nilipokuwa nikiwasiliana naye nilijua ni mswahili,
kutokana na Kiswahili chake kizuri, lakini hapa namuona kama ni asili ya nje,
lakini nilivyomchunguza vyema, nikaona ni damu mchanganyiko, inaweza ikawa
wazazi wao walikuwa na asili mbili, sikujali sana.
Na mimi kwa haraka nikaenda kuonana na mpokea wageni, ambaye
wakati huo alikuwa akihangaika kuweka meza yake sawa, inaonekana alikuwa nje,
maana niliona kaweka bahasha yanye kitu kama vitafunio pembeni, na alikuwa
keshajisahau, hadi bosi wao alipoingia, na sasa anajiweka sawa kuonekana
kiofisi zaidi.
‘Samahani dada, mimi naomba kumuona meneja uajiri...’nikajitambulisha.
‘Hakuna meneja uajiri hapa, huyo aliyeingia ndiye mwenye
kampuni, na ndiye bosi wa kila kitu...’akasema huyo mwanadada akijiangalia
kwenye kiyoo, hakutaka hata kuniangalia.
‘Nimeleta barua yangu , niliwasiliana naye kwa barua pepe,
akasema nije nionane naye...’nikasema
‘Subiri, kaa hapo kwenye kiti, huoni ndio kaingia, na mambo
yenyewe leo yamekuwa ni vurugu vurugu, watu wanataka kuuana, kisa ni mapenzi,
....’akasema
‘Mapenzi ina maana haw watu walikuwa wakigombana kwasababu
ya mapenzi, wanamgombea nani!...?’ nikamuuliza
‘Eti mimi, ...mimi nimewaambia mwenye kisu kikali ndiye mla
nyama, ...wakaanza kuzozana, mara wakashikana mashati, mara ngumi, mimi
taratibu nikatoka zangu nje kutafuta vitafunio, nasikia huku nyuma wamepigana
hadi kuuana...shauri lao’akasema
‘Mbona nimekuta watu wakibishana na maswala ya dini na siasa...?’
nikauliza
‘Hawa watu ndivyo walivyo, kitu kidogo, kikitokea badala ya
kukizungumzia hicho kitu, na kuangalia chanzo chake wanakimbilia kukiingiza kwenye
kubishana kuhusu imani zao,...mimi nawashangaa sana, maana hata dini zao
wenyewe hawazijui vyema, kuswali hawaswali, kutwa ulevini, kamarii, na
vijiweni, kazini kwenyewe ndio hivyo, wanasubiri bosi aje ndio wanakimbilia
kujifanya wanafanya kazi, kweli imani za dini zinasema hivyo...’akawa kama
anaiuliza na mimi nikataka kumuuliza wewe je hujioni....
‘Kwahiyo aliyeshinda ndiye atakuwa mpenzi wako?’ nikamuuliza
‘Thubutu, ni nani awe na mpenzi njaa, kali kama hawa, mawazo
yao ya kufikiri finyu kabisa ...mimi nina mchumba wangu kila siku ananileta na
gari, sema tu mkiwa ofisini kuna ile hali ya kupitisha muda, unapata mpenzi wa
muda, unakuwa na rafiki wa hapa na pale, ili mambo yaende sawa, lakini sina
shida ya mtu....’akasema na mara mlango wa bosi ukafunguliwa
‘Unaongea na nani wewe badala ya kufanya kazi..’sauti kali ya
kike ikatanda hewani, hutaamini, yule dada alikaa kwenye meza yake na kuangalia
kwenye komputa yake na kujifanya anaandika kitu, huku akifunua funua
makaratasi, utafikiri kweli alikuwa akiandika jambo kwa kuangalia ile karatasi
anayoifunua, ...nilimwangalia kwa mshangao mkubwa, anavyoigiza kufanya kazi.
‘Wewe ni nani mbona umesimama hapo, unahitaji nini...’sauti
ya huyo mwanadada ikaniuliza.
‘Mimi nimekuja kuleta barua yangu ya maombi ya
kazi,...nilikuwa nawasiliana na wewe...’kabla sijamaliza akaja pale
niliposimama na kuichukua ile barua yangu na kuniambia
‘Njoo ofisini kwangu, ....’akasema na mimi nikamfuata huko
fisini kwake, na alipofungua mlango, tukajikuta kwenye ofisi nyingine kubwa, ambapo
kulikuwa na wafanyakazi kama watano, kila mmoja alikuwa kimiya kwenye kazi zake
na wawili wao walikuwa wale waliokuwa wakipigana, walikuwa wameinamisha vichwa
chini, nahisi ni kuficha uvimbe kwenye nyuso zao, ...na mbele yao ndio kulikuwa
na mlango mwingine wa kuingia kwenye hiy ofisi ya huyo bosi.
‘Karibu nikusaidie nini.....’akaniuliza huy mwanadada, baada
ya kukaa kwenye meza yake, huku akiifungua ile barua.
‘Mimi ndiye niliyekuwa nikiwasiliana nawe kwa barua pepe
kuhusu kuomba ajira hapa, katika idara ya uhasibu, na mara ya mwisho tuliongea
na simu ukasema nije leo....’nikamwambia
‘Ohoo, ndio wewe...ok, sasa niambie una jua nini katika
uhasibu?’ akaniuliza
‘Karibu kila kitu, kuanzia ukarani hadi kutoa taarifa kuu za
kimahesabu...’nikamwambia.
‘Safi kabisa, nataka watu wa namna yako, watu wanajua kazi,
kuanzia chini, sio mtu anakuja katoka shule au chuo anataka kuwa meneja,
anataka kuwa bosi hataki kwanza kujifunza mambo ya chini, hajui kazi za chini
zipoje, huyu mtu atawezaje kuwasimamia watu wa chini kama hajui wanafanya
nini...mimi nikuambie ukweli, nimetoka mbali sana....hutaweza kuamini, hapa
nilipo ni mmumiliki ya hii kampuni, lakini huwezi amini kuwa nimefanya kazi
hata ndani, ...’ akaniangalia kwa macho makali.
Nilimuona kama ananitania, nikatulia kumsikiliza na yeye
alipoona namwangalia huku natabasamu, akahisi simuamini, akarudia kwa kusema;
‘Nimefanyakazi kama mfanyakazi wa ndani, nimezalilika, ...nimetaabika, hadi kufikia kutaka kujiua,
...kwa kusingiziwa machafu ambayo sijawahi kuyafanya, na anayekusingizia, ni
baba yako mzazi,...leo hii namiliki kampuni hii na nina wafanyakazi ambao
wanataka niwalipe pesa nyingi tu huku hawafanyi kazi...muda mwingi hawafanyi
kazi...’akageuka kuangalia wafanyakazi wake kwa kupitia kwenye dirisha la
viyoo.
‘Lakini watu hawa hawajui jinsi gani nilivyotaabika, hadi
kufikia kiwango hiki, wanafikiri hali hii imetoka mawinguni, ukiondoka kidogo
tu, wapo kwenye magumzo, ubishani wa mipira, mara siasa, mara dini, umbea
mtupu, mabishano yao yasiyo na maana
yoyote, angalia mfano, leo nimefika nakuta watu wanapigana, sasa kweli tufika kwa
mtindo huu, nataka kuisafisha hii ofisi na kuajiri watendaji kazi wazuri,
sitaki ujinga...’akawa kama ananiuliza.
‘Mhh, bosi ina maana wewe uliwahi kufanya kazi za ndani, house girl?’ nikamuuliza
‘Ndio maana yake, huwezi amini, lakini ndio ukweli wenyewe, maisha yangu yamepitia hali ngumu, ambayo
naweza kusema ni wachache sana waliowahi kupitia maisha niliyowahi kupitia mimi,...nimeitwa
malaya na baba yangu mwenyewe mzazi, wakati huo simfahamu hata
mume...nikapigiwa nikisingiziwa kuwa ninafanya umalaya, na huenda nina mimba,
wakati hu sijawahi kutembea na mwanamume yoyote, nikakatizwa masomo, nimefungwa,...ikafikia
muda nikachoka, nikaamua kujiua.....’nikaona machoni yakimlenga lenga machoni,.
‘Usinikumbushe, maana watu hawajui tulipotoka, na wengi
nikiwasimulia wanaona ni uwongo ....mwenyewe nikikumbuka maisha yangu
yaliyopita nataka hata kulia,.....lakini leo hii unaona,nina kampuni, ninaajiri
watu, na kunifanya niamini kwa vitendo kuwa, baada ya dhiki kweli ni faraja, ...’akachukua leso yake na kufuta
usoni, nahisi ni kufuta yale machozi yaliyoanza kumtoka.
‘Karibu kwenye ofisi yangu, nitakusimulia kisa changu,
mwenyewe utashangaa, kwani yote ni maisha,lakini mimi ninaamini kuwa
ukivumilia, ukajitahidi, ukafanya kazi kwa bidii,utafanikiwa....ni kweli kabisa
utafanikiwa, lakini ukikaa na kulia, na kulaani, huku hufanyi jitihada, utashia
kubaya,...kama methali hiyo inayosema, baada ya dhiki, huja faraja, na mimi
sasa nimefarijika,....
********
NB: Ndugu wapenzi wa blog hii, nimediriki kukileta kisa hiki
kwani wengi sasa hivi wanapitia katika mitihani ya kimaisha, maisha kweli ni magumu
sana, hali za uchumi zinazidi kuwa tete, watu wanafikia hatua ya kukata tamaa,
na baya zaidi, hakuna anayetaka kufanya utafiti wa kisayansi akaona tatizo hasa
ni nini...
Kinachofuata ni kutafutana uchawi, kila mmoja anamtafatia ubaya mwenzake , kwa kutupiana
lawama, chuki za ndani kwa ndani zinaanza kujiejenga na kutafuta visingizio
hata kusipofaa, wengine tunawalaumu viongozi , tunailaumu serikali, tulioiajiri
wenyewe, kama ulimuajiri kiongozi mbovu, ni nani wa kulaumiwa, ni wewe uliyemuajiri
na kumpa kura yako, sasa tujiulize kihekima,...ni kwanini hali kama hizi
zinafikia hapa..
Swali la kujiuliza kama umemuajiri mfanyakazi mbovu unatakiwa ufanye nini....?
Kisa hiki kipya pamoja na kuangalia maisha magumu aliyopambana
nayo huyu mwanadada, tutajaribu pia kuangalia jinsi gani tunaweza kujikwamua,
japokuwa ni kwa shida,...badala ya kukaa na kumlaumu huyu au yule, kutokana na
madhila ya kimaisha,...ni kweli, maisha ni magumu, mtu unaamuka hujui atakula
nini,...anashindia kitumbua na kipande cha muhogo....
‘Lakini je ni sahihi kukaa na kubishana, na baya zaidi tunageuza
ubishani wetu hata kule kusipostahili. kwenye imani zetu za dini,..nafikiri kama tungelitumia vyema
imani zetu za dini, kusingelikuwa na ugomvi, na maisha yangelikuwa ni ya amani,...
‘Tatizo, tunageuza hisia za hulka zetu za asili za ubinafsi,
chuki za umimi, husada za kwanini, imani za kishirikiana, na kuzipandikiza kusikofaa,
maana dini zote zinafundisha amani na upendo, kama wewe unaingiza chuki, ushirikiana
husuda, na uhasama kwenye imani yako ya dini, huo ni ubinafsi , basi hiyo sio
imani sahihi ya dini, hizo ni tabia zetu za asili.
WAZO LA LEO:
Tusipende kuingiza mambo yetu binafsi, chuki zetu za asili, utofauti wetu wa
kimaisha , utofauti wetu wa kisiasa kwa kutumia mgongo wa dini. Dini zipo kwa
ajili ya kuzisafisha nyoyo zetu ili zijae upendo, amani na kuvumiliana, hazipo
kwa ajili ya kujenga chuki, ...
Tukitumia dini ili tupate wafuasi, ili tufanikiwe jambo
fulani, kwa njia ya chuki, propaganda potofu, tunafanya makosa hiyo ni dhambi
kubwa sana, kwani fitina ni mbaya kuliko hata uchawi, kwani matokea yake ni
mabaya sana, watu watauana, na wakiuana ujue wewe ndiye unayebeba hizo dhambi.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment