Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, August 7, 2013

WEMA HAUOZI-46


Hakimu akiwa bado kashikilia kirungu chake juu akageuka kuwaangalia wenzake, huku akiwa bado na mshangao machoni , na wenzake wakiwa na wao wanaangalia kule alipotokea shahidi, bila kujali kuwa muheshimiwa alikuwa akiwaangalia, kutaka kuongea jambo,  na kwa muda huo yule shahidi alishafika sehemu ya mbele akisubiri amri nyingine.

Muheshimiwa hakimu, akajiweka sawa, na kumwangalia wakili mwanadada, kabla hajasema kitu, na akiwa na uso ule ule wa kushangaa akawageukiwa wenzake na kuwauliza

‘Haya ndio tuliyokuwa tukiongea kwenye kikao chetu cha mahakimu,…unajua kila mahala kuna utaratibu wake, hata kama una mambo yako….’akasema , halafu akageuka kumwangalia wakili mwanadada, na kusema;

‘Mbona mnarudia makosa yale yale, niliwaambia nini nilipowaita?’ akauliza.

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, ulituambia tuheshimu mahakama kwa kuvalia mavazi rasmi, kwani hapa pana adabu yake, lakini tukumbuke kuwa kuna watu wana tamaduni zao, kama walivyo wamasai, huwezi kuwalazimisha wavue mavazi yako na kuvaa suti, au nguo za kawaida wakiingia hapa mahakamani, , ndio ni taratibu za kimahakama, kutukujionyesha wewe ni nani, lakini na wao wana haki yao,ndivyo ilivyo kwa shahidi huyu, kutokana na imani yake, ya kiitikadi,harushusiwi kuondokana na mavazi yake hayo aliyoyavaa….’akasema wakili mwanadada.

Hakimu akainama na kuandika kitu kwenye makabrasha yake, na alipoamliza akaangalia saa yake, na kusema;

‘Tunaweza kuendelea…..

**********

Baada ya taratibu zote za kimahakama kukamilika kwa shahidi huyo, wakili mwanadada alimsogelea yule shahidi, na kuanza kumuelekeza juu ya ushahidi wake, akasema;

‘Ndugu shahidi, hebu tuelezee wewe ni nani na kazi zako hasa ni zipi?’ akaulizwa . Na yule shahidi kwanza akainua kirungu chake kilichotengenezwa kwa mkia wa mnyama, na kuzungushiwa shanga za hariri za rangi mbali mbali, kwanza alianza kutaja jina lake halisi halafu akaendelea kwa kusema;

‘Mimi najulikana kama `mtaalamu,’ na ndivyo wengi wanavyonitambua hivyo…’akasema na kabla hajaendelea wakili mwanadada akageuka upande ule wa wapinzani, ..

Upande ule, ulikuwa kimiya, na safari hii, aliyekuwa kainama, na hata hakutaka kuongea kitu alikuwa wakili mtetezi, yeye alionekana mnyonge isivyo kawaida yake, na pembeni yake, alikuwepo mteja wake, mshitakiwa mkuu, kiongozi wa kijiji, ambaye alikuwa akimwangalia huyo shahidi, huku katoa macho utafikiri ameona jambo la kutisha.

‘Hebu tuambie kwanini wanakuita hivyo, `mtaalamu’?’

‘Kwasababu ya kazi zetu,…’akasema huyu mjamaa akichezesha chezesha kile kirungu, au mkia wa mnyama huku na huku kupitisha mbele ya uso wake.

‘Hebu tuambie kazi zenu ni zipi?’

‘Mimi ni mganga wa kienyeji, na pamoja na uganga huo, bado kuna mambo ya ziada ambayo yanatufanya tuwe zaidi ya mganga wa kienyeji, na ndipo hapo watu hutuita wataalamu…’akasema huku akijipepea na hicho kifimbo chake ambacho akikigeuza upande mwingine ni mkia wa mnyama, na akikigeuza upande mwingine ni kirungu kilichopambwa kwa shanga za hariri

‘Hebu tufafanulie mambo gani hayo ya ziada ambayo yanakwenda zaidi ya uganga wa kienyeji’

‘Uganga wa kienyeji ni kutibia tu, unajua dawa za ugonjwa fulani, unawapa watu wanapona…lakini kuna mambo kama ya kuangalizia, wengine huyaita `ramli’ kuna mambo ya kusafisha nyota wengine huyaita 
`unajimu’ kuna mambo ya mizimu…hayo yote ninayo mimi, ndio maana naitwa `mtaalamu’…’akasema akionyesha matambo .

‘Sawa mtaalamu, hebu sasa turejee kwenye kesi yetu hii, kama unavyoona watu wanakushangaa, maana ulipotea kabisa, na ikasadikiwa kuwa umeshakufa.…je ulikuwa wapi na imekuwaje leo kutokea hapa, …?’ akaulizwa.

‘Kama nilivyokuambia kuwa pamoja na uganga, lakini pia nahusika na mambo ya mizimu, na mizimu ni nini, mizimu ni mababu waliotangulia, ambao walikuwa na kazi kama hii. Kazi kama hizi ni kurithi, na niliporisishwa, nilipewa masharti mengi, ambayo nilihitajika kuyafuata, lakini kutokana na mambo haya ya kidunia, nikajikuta nimeyavunja moja baada ya jingine…’akasema.

‘Ili tusiende mbali na kesi yetu hebu tuambie ni masharti gani uliyavunja, ambayo, yalikusababisha hadi utokomee huko ulipokwenda….’akaulizwa.

‘Ili nieleweke vyema, naona uniachie nijielezee kidogo,….’akasema na wakili mwanadada akaangalia saa yake, na kumwangalia muheshimiwa hakimu, na baadaye akawaangalia kambi ya utetezi, kama wanapingamizi lolote, lakini cha ajabu, alishangaa kumuona wakili wa utetezi, kakaa na kutulia, na alionekana kama vile hayupo hapo kabisa, alikuwa kainama huku kashika kichwa.

‘Mimi nilipochukua nafasi hiyo ya utaalamu kwenye kijiji chetu, sikujua kuwa nitakutana na mitihani mingi, kwasababu nilipata nafsi hiyo nikiwa bado kijana, na mambo ya ujana unayafahamu yalivyo,damu inachemka, akili ina tamaa ya kupata, kufurahi, kujirusha na vitu kama hivyo,…hilo sio la siri tamaa za hapa na pale ndio mtizamo wa ujana. Kwa hali hiyo, japo nilikanywa nikakubali, lakini ilifikia wakati mwingine, nikawa sijali sana yale masharti niliyopewa, na hili lilifanya mara kwa mara niwe ninapotea kimaajabu, …’akasema

‘Nilikuwa nikiitwa na mizumu,…na ujue ukiitwa kuna mawili, umeharibu au unatakiwa kupewa majukumu fulani,  na mara tatu nilizowahi kuitwa, nilikuwa nimeharibu na karibu niangamizwe kabisa, kwani nilikuwa nimezidi kiburi, na hili lilitokana na kundi nililokuwa nalo,….nilionywa niachane nalo…lakini haikuwa rahisi hivyo…’akatulia kidogo.

‘Kundi hili lilianzishwa ndani ya kijiji chetu, na lilijumuisha watu mashuhuri wa kijiji, likiongozwa na mzee wetu wakijiji…na ukiangalia watu mashuhuri ni nani, ni ukoo wetu tu, walionacho wanaongezewa….au nasema uwongo ndugu yangu?’akasema na kumnyoshea kile kirungu cha manyoya mshitakiwa mkuu…na mshitakiwa mkuu,alikuwa vile vile akimkodolea macho, kama vile kashikwa na bumbuwazi.

‘Na haya ninayoongea kama ni uwongo, aseme…najua ananishangaa, kuwa msaliti, huwezi ukawa msalitu kwenye kundi ukasalimika, sasa mimi haina tofauti , …nikikaa kimiya nitaangamia, kubaya zaidi, ni bora niseme, kwani hawo walionituma wana ujuzi wa kunisaidia,…angalau,…

‘Mzee wetu, kiongozi wa kijiji, yeye alichaguliwa kwa kura zote kuwa atakuwa ndiye kiongozi wa maaliwatani wa kijiji, tunaweza kusema wanafamilia, japokuwa kuna watu fulani, waliingizwa, lakini ni kwa vile walionekana kuwepo kwao ni masilahi ya kundi,…na uongozi ndani ya kundi inahitajika uwe kweli umeimarika,  na kutokana na wadhifa huo, ilibidi tumtii kwa kila atakalolisema, lakini hilo atakalolisema ni lazima liwe limekubaliwa na kundi zima…’akatulia.

‘Kundi hilo lilikuwa la siri sana, na ilibidi kutengenezwa yamini. Yamini ni nini, yamini ni kiapo kinachoambatishwa na imani, na kafara, na ukikiuka yamini hiyo, huwezi kusalimika, , ukienda kinyuma na msharti, wenzako hawana hiari, ni kukuua, tu,… adhabu yake ni damu yako, au ya mtoto wako unayempenda sana…na haina masihara…’akatulia.

‘Moja ya kazi za kundi hilo, ni kuhakikisha kuwa kijiji chote kinakuwa mikononi mwetu, na mali hasa viwanja, mashamba na miradi mikubwa tunakuwa tunaimiliki sisi wenyewe, hata kama kuna mtu ambaye ndiye mwenye kumiliki huo mradi, duka au shamba, au mifugo, sisi kwa kutumia utaalamuu wetu, yeye anakuwa kama picha tu…’akatulia.

‘Utaona kama ni maongezi tu, lakini ndivyo ilivyokuwa, …kama unabisha waulize matajiri au wamiliki wa maduka, na miradi hapo kijijini, watakuambia,…kuwa wao walikuwa wakihangaika na kuchuma, lakini kila wakipatacho sio sawa na mahesabu yao….sasa jiulize hayo mahesabu mengine yalikuwa yakienda wapi, jiulizeni, sisi ambao tulikuwa hatufanyi kazi, mbona ndio tuliokuwa matajiri wa kiaina…kwanini ukoo, na kundi letu sote ni matajiri….’akatabasamu.

‘Kuna kitu wengine hukiita `chuma ulete…’ maana wengine wanahangaika kuchuma, na wengine wanasubiria tu, ulete ulichochuma, na ndivyo tulivyokuwa tukifanya,…’akatulia huku akitabasamu lakini usoni kulikuwa na huzuni.

‘Hili mizimu ilikuwa haitaki hayo, lakini mimi kwa kiburi nikiwa na kundi hili, tulilifanya hayo bil kujali masharti ya mizumu,,…na wale walioleta kiburi, walikipata cha moto…na mmoja wa hao, alikuwa mama mkunga…..’akasema na watu wakaguna.

‘Mama mkunga , tulimtaka awe kwenye kundi letu, lakini alikataa kabisa, ..na tulimtaka awe hivyo kwa vile yeye alikuwa akizalisha watoto wachanga, na sisi moja ya vitu tulivyovihitajia ili kuwezesha mambo yetu, ni damu za watoto wachanga, na viungo vyao maana vile havina madoa,…viuongo vya watu, hasa wale wenye utofauti fulani, kama hawo wenye ngozi nyeupee’akatulia huku akiangalia huku na kule kama anaona vitu ambavyo wengine hawavioni.

‘Huyu mama mkunga, alitukaidi, na tulimuhitajia sana kwenye kundi kwa vile alikuwa na karama ya kuona watu wasioonekana, ….simnajua kuwa wachawi wanaweza kupita mahali hata msiwaone, lakini huyu mama alikuwa akiwaona, na kwa karama hiyo alihitajika sana kwenye kundi letu, ili asije akatuumbua….’akatulia.

‘Hapo ndipo tulipoanzia kumsakama, na haikutakiwa auwawe…maana kama tungelimuua, kwa mikono yetu, tungeliangamia sote, ilitakiwa afanyiwe jambo, aonekane mbaya, achukiwe,…na hapo tukagundua kuwa ukitaka kumuua mbwa,kwanza anza kwa kumuita majina mbaya,….na ndipo tukamuanzishia fitina kuwa yeye ni mchawi, yeye ndiye anayeua watoto, kumbe ni sis tunafanya hivyo, na ….kwa vile yeye ndiye aliyesimamia ukunga, huo anaonekana ndiyo yeye muuaji, mchawi…

‘Pia hatukutakiwa kumuua, sisi wenyewe, kwa vile yeye ni damu ya kundi letu…’hapo akatulia.

‘Nasikia ameshajitambulisha na mumeshajua kuwa yeye ni ndugu wa mzee wetu, kiongozi wa kundi, na kiongozi wa kijiji, mimi nilikuwa msaidizi wake, na kulikuwa na katibu ambaye mtakuja kumjua baadaye….’akatulia.

‘Nayasema haya kama amri kutoka kwa mizimu, vinginevyo kutokana na yamini tuliyokula, nisingeliweza kuongea chochote, hapa, …kama unasaliti kundi, utajiwa na vitu usivyoviona na kujikuta ukichanwa chanwa na damu yako hunyonywa na mashetani, …nakumbuka vifo kama hivyo vimeshatokea maeneo ya huko kwetu, zilikutwa maiti zimechanwachanwa,….na mwili ukawa umekakamaa kwa kukosa damu……hakuna aliyejua sababu ya vifo vyao, ukabakia uvumi tu, ….’akatulia.

‘Hawo walikuwa wasaliti wa kundi….’akatulia na kumwangalia mzee, mshitakiwa mkuu, na akatikisha kichwa kama anakubali jambo, halafu akageuka na kungalia mbele…

‘Mama huyu ni ndugu wa damu wa mzee wetu , na aliondolewa hapa kijijini, na mizumu,..japokuwa watu walikuwa hawalijui hilo,…mizimu ilijua kuwa akiendelea kuwepo hapo, angeliuwawa mapema kabla hajaweza kuifanya kazi aliyotakiwa kuifanya…’akatulia.

‘Mizimu ya mababu zetu sisi katika ukoo wetu,haitaki uchafu, haitaki umwagaji wa damu,…na inahitaji vipaji vya asili, kama hivyo vya ukunga wa jadi, uwashi, ujenzi,…nk, vile vitu mtu anazaliwa navyo bila kujifunza kokote, na mama huyu alikuwa na kipaji cha ukunga wa jadi, ni zaidi ya wakunga mnaoona huko mahospitalini, wenyewe walimvulia kofia, ni mama mwenye kipaji cha hali ya juu….nendeni mkawaulize…’akatulia.

Mama huyu alipendwa sana na baba yake tangu alipozaliwa, lakini kukawa na msuguano wa ndani, hadi baba yake akaamua kuoa mke wapili, na hapo hali ikawa mbaya zaidi...na mke wa pili alipoona kuwa mume wake anampenda sana huyo binti, akazua mambo, ….akawa anamchukia sana huyo mtoto, na hata ilipofika mume hawezi kuvumilia tena, akaamua kumuacha mke wake wa kwanza.

Kutokana na hali ilivyokuwa, …wao walihisi ni maamuzi yao, ikabidi mama huyo aondoke na mtoto huyo wa kike, kwa vile yeye alikuwa bado mdogo, na alipoondoka hawakujua kalekea wapi, miaka ikapita, na baba mtu alijaribu kumtafuta huyo mama ili ampate binti yake, lakini hawakuweza kumpata…’akatulia.

Kumbe Mama wa huyo mama mkunga alipoondoka hapo alikwenda akaolewa na mume mwingine na wakahama na  kwenda kuishi mbali,…na ghafla mama wa mama mkunga akashikiwa na ugonjwa, wa hafla na haikuchukua muda akafariki dunia, na kumuacha mama mkunga akiwa bado mdogo…..’akatulia.

‘Mama mkunga alikuja kulelewa na mama mwingine, kwa baba wa kufikia,…hakupata shida, wazazi wake wapya hawo,walikuwa watu wazuri, na hakuona tofauti, na siku zilivyozidi kwenda wazazi hawo wapya walishanga sana kuona binti huyo akiwa na karama mbali mbali, ikiwemo ya kujua dawa gani itamsaidia mama mja mzito, au mama aliyejifungua, na akawa na matatizo ya kukosa maziwa, kuangakuka kifafa, degedege na magonjwa ya kila aina…’akatikisa mkia-kirungu chake kama vile anajipepea.

‘Huku nyuma, alibakia mzee wetu huyo, na aliyelelewa na mama yake huyo mdogo, ambaye hakuwa na kinyongo naye, na akawa kama vile mtoto wa mama huyo, na hata ilionekana kama vile ni mtoto wa mama huyo…’akatulia.

Ikafikia muda wazee wa familia hii, yaani baba na mama, wakawa wanaumwa sana, na ilionekana hawataishi muda mrefu, na ndipo baba wa mzee wetu wa kijiji, akamuita mwanae huyo, akiwa bado kijana, mimi sikuwepo, nilikuja kuitwa baadaye, na kutambulishwa kuwa kumbe huyo ni baba yangu pia,…wengi hawalijui hilo, ila mimi ni mtoto halali wa baba huyo, ina maana kiongozi wa kijiji na mimi ni mtu na kaka yake mimi nilizaliwa na mama huyo mdogo….’aliposema hivyo watu wakatoa mshangao wa `haaaaa’

‘Yote hayo yalifanyika yawe hivyo, kutokana na mizimu, haikutaka familia hiyo ijuilikana nani ni nani, na kwahiyo hata mimi nilichukuliwa nikiwa mdogo na kwenda kuishi mbali kabisa na niliporudi nilikuwa mtu mzima, ….watu wengi hawalijui hilo, wanaolijua hilo ni watu wa kundi letu tulilolianzisha, na walitakiwa hayo yawe siri, hawakutakiwa kuongea lolote kuhusu familia yetu ilivyokuwa.

‘Baba yetu huyo, alifanya kila mbinu mpaka nikafika mara moja, na siku hiyo akatupa urithi, wa mashamba na maeneo….maeneo mengi hapa yalikuwa ya kwetu, yamefanywa kuuzwa uzwa, na kugawanywa baada ya wazazi wetu kufariki, na aliyekuwa akifanya hivyo ni mzee wetu wa kijiji, ni ndugu yangu, sikuwa na kinyongo na yeye…’akasema na kucheka.

‘Baba alitugawia maeneo, kila mmoja na ukanda wake na eneo moja hakuligawa, akasema ni eneo la mtoto wake, ambaye hajui yupo wapi, na kama akitokea tuhakikishe tunapa sehemu yake,na tulimpomuuliza ni nani, akasema kaka yangu huyo, yaani mzee wetu wa kijiji anamfahamu, …na nikakumbuka kuwa enzi za utoto wetu kulikuwepo na mtoto mdogo wa kike, ambaye aliondoka na mama yake……’akatulia.

‘Sasa mnaona ilivyo, kuwa kundi hili limeundwa na wanafamilia, ambao walitawanyika na baadaye wakarejea, na tuliporejea maeneo yetu mengi yalikuwa yameuzwa au kugawiwa watu wengine, na hapo tukaanza kuyadai, na kaka yangu akasema ilivyo kwa sasa ni lazima tutumie mbinu nyingine, kwani tukutumia nguvu, hatutayapata..

‘Ndio chanzo cha kuanzishwa hilo kundi, ….na ukichunguza kwa undani, wote waliopo kwenye hilo kundi, ni wanandugu, kwa upande wa mama yangu, ambaye ni mama mdogo wa mzee wa kijiji…na kwa upande wake, wa mama yake alikuwepo yeye mwenyewe na watoto wake…ana watoto wengi mzee wetu huyo, na wengine hatuwajui.’hapa akatulia watu walipocheka kidgogo.

‘Ili kundi liwe la kisasa ziaidi tuligundua kuwa ni lazima tuwe na wataalamu, wasomi, tuwe na watetezi wa kisheria, tuwe na watu wakutukingia kifua kama likitokea tatizo, kwahiyo kwa vile familia yetu ni kubwa na ina vijana, ambao wamesoma,tukawajumuisha baada ya kuwaelimisha na kuiva…ni kweli familia yetu ina wasomi, ina watu wana nyadhifa mbalimbali…ila sio wote walioaminika,….’akatulia.

‘Kwenye usalama, wapo watu wetu, na hapa karibu tu tuna kijana wetu, ambaye ni mkuu wa kituo cha usalama …ambaye alikuja kuwa katibu wa kundi kutokana na akili na uwezo wa kuongea na kushawishi,….na huyu amekuwa nguzo muhimu kwenye kundi, maana kutokana na yeye, wakubwa wengi, wamekuwa wakituamini…utasema nini,utaenda wapo ukose mtu wetu, ….hata yule kijana aliyehusika na kugushi stakabadhi ya malipo ya mwanamama ni kijana ndani ya mmoja wa wanafamilia wetu,…’akasema an watu wakacheka.

‘Msicheke, mimi nisingeliweza kuja kuisaliti familia yangu hapa, kama isingelikuwa hii adhabu niliyo nayo, hamjui ni taabu gani ninayopambana nayo, nina adhambu kutoka kwa mizimu, na nimerejeshwa hapa kwa muda tu, na kila siku tangu nilipochukuliwa kimiujiza, nilikuwa nikipata adhabu, nikivua shati langu, mtaona michirizi ya mijelezi, niliyokuwa nikichwapwa, na kuchomwa moto,….’akasema na akavua kijoho chake na kata mikono,na mahirizi yake aliyoyavaa na manyoya, shanga, na kubakiwa wazi mgongoni, sehemu yote ya mgongoni kulikuwa na michirizi ambayo alisema ni ya fimbo,na kuonyesha mwili wake, uliokuwa kama umchorwa chorwa na michirizi..’

‘Haya sio mapambo, sikuwa nayo kabla, muulizeni ndugu yangu pale kama mwili wangu ulikuwa hivi…hii ni adhabu niliyoipata kutoka kwa mizimu, na kila siku nilikuwa nikiteswa, maana licha ya vipigo hivi, nilikuwa nabanikwa juu ya moto, kwa ajili ya kulipizwa kwa kumchoma mama mkunga moto, na mimi nilitakiwa nionje utamu wa moto ulivyo….’akatulia.

‘Kesi hii ilipoanza, nikaambiwa kwa ajili ya mapumziko, nihitajika kuja hapa kuelezea kila kitu, vingiunevyo nitaendelea kuteseka kwenye adhabu hiyo..na nashukuru kuwa siku mbili hizi nilizokuwa huku nimekuwa nje ya kifungo cha mateso, na ….moja ya masharti ni kuwa niseme kila kitu , bila kujali kuwa huyo ni ndugu yangu au nani, na nikisema uwongo, narejeshwa haraka huko kwenye mateso yangu…’akatulia.

‘Kwahiyo nawaomba msamaha sana ndugu zangu, kuwa haya ninayoyafanya nayafanya kutokana na mateso ninayoyapata…na hali niliyofikia ni bora kila mtu aubebe mzigo wake mwenyewe…’hapo akatulia kwa muda, na wakili mwanadada akahisi kuwa huyo jamaa kapotewa na maneno, na akamsogelea na kumshika.

Wakili mwanadada alimwangalia huyo mtu machoni, alimuona akiwa kabadilika, na sura ilikuw ikiashiria maumivu makali, na macho yake yalikuwa yametawaliwa na waupe, na kuwa mtu mwenye sura ya kutisha, hata wakili mwanadada akasogea nyuma kama anaogopa na hakimu akawa anawaangalia kwa mshangao.

‘Vipi mbona kimiya?’ akauliza hakimu

‘Oooh, samahani kidogo, nilikuwa nakumbushwa jambo…mizumu ilinitembelea ghafla, wamesema kuna mambo nimeyaruka au nayakwepa kuyasema ni  muhimu…sana’akasema huyo mtaalamu akionyesha dalili kuwa anapata shida ya maumivu.

‘Ni kuhusu, ndugu yangu huyo, mzee wa kijiji, kuwa ndiye aliyesimamia operesheni ya kumchoma moto mwanamama, siku hiyo aliaga kuwa anaondoka, lakini hakuondoka, alikuwa kwenye nyumba zake ndogo, maana ndugu yangu huyu ana nyumba ndogo nyingi za siri…kama mnabisha ninaweza kumleta mwanamke aliyekuwa kwake siku hiyo…’akasema na kumwangalia ndugu yake, ambaye alikuwa katulia vile vile kama kagandishwa.

‘Siku hiyo ya tukio, alikuwa kajificha akiwaangiza hawo vijana jinsi gani ya kufanya, na alipohakikisha kuwa nyumba hiyo imeteketea kabisa, akaondoa kuelekea huko aliposema alikuwa amekwenda kabla ya tukio hilo…’akatulia

‘Ndugu yangu huyo ndiye aliyewanywesha sumu wale vijana, ambao walihusika kwenye uchomaji moto, maana wao walimuona, na ilionekana dhahiri hawo vijana wanaweza kuja kusema, na haikutakiwa kujulikana…kwahiyo akawapa dawa ya kienyeji, ambayo inauwa na hata ukipmwa hospitalini, haionyesho kuwa ni sumu. Mtu anakuwa kama kapagawa…halafu ile sumu inakwenda kuharibu ubongo na kwenye mapigo ya moja…mtu huyo anakufa kwa kifo cha kuteseka kweli, ….’akatulia

‘Kama nasema uwongo, nampa nafsi ndugu yangu apinge…’akasema na kutulia na mzee wa kijiji, alikuwa katulia vile vile….na hakimu akamgeukia kumwangalia huyo mshitakiwa mkuu, lakini mshitakiwa mkuu, alikuwa kama kaganda, alikuwa akimwangalia huyo shahidi bila kugeuka, au kupepesa macho na hakimu akaingiwa na mashaka, na akibidi aulize;

‘Kuna tatizo lolote kwa mzee mshitakiwa?’ akauliza na wakili mtetezi, akageuka kumwangalia mteja wake, na kumgusa kwa mkono, na hapo mshitakiwa mkuu, akawa kama anaamuka kwenye usingizi mzito na kusema;

‘Hakuna tatizo muheshimiwa, yote ni sahihi kabisa…’akasema na watu wakacheke, na wengine kuguna, na hata kuzomea wakisema ;

‘Muuwaji…’ na hakimu akagonga kirungu chake kwa nguvu, kuashiria watu watulie.

‘Hawezi kukataa, maana hiyo ndiyo salama yake, aamue moja,akateseke na adhambu ya mizumu kama ninayoteseka mimi au atumikie kifungi, mtakachomuadhibu nyie….’akasema huyo shahidi na kutulia.

‘Sumu hiyo hiyo iliyowaua hawo vijana ndio hiyo hiyo ilimuua jemedari…’akasema na hapo watu wakashindwa kuvumilia, na kuanza kusema;

‘Anyongwe huyo, muuaji huyo…’na hakimu akagonga kirungu chake na kusema kwa hasira

‘Ninaweza nikawatoa wote humu ndani tukaendesha kesi hii bila ya nyie kuwepo,….hii ni mara ya mwisho, kama hamtaweza kuvumilia, ni bora msiingie humu ndani….’akasema na watu wakatulia kimiya.

‘Ina maana Jemedari aliuwawa kwa sumu?.....’akauliza mwanadada kwa mhsngao, na kuendelea kuuliza akiwa kwenye mshngao `Ni nani aliyempa hiyo sumu…?’ akaulizwa.

‘Sistahili kulisema hilo mimi, ..yupo wa kuja kulisema hilo, na kama mtamruhusu aingie sasa hivi, atakiri hayo yote,…mimi ninaweza kukaa pembeni, aje athibitishe mwenyewe, na aelezee ni nani aliyemtuma, na kama mtanihitajia tena, nipo tayari kusimama na kuelezea,..’akasema

‘Ndugu muheshimiwa hakimu,..nawaruhusu watetezi kumhoji shahidi wetu huyu, na kama hawana maswali basi, tutamuita shahidi mwingine kuja kuthibitisha kifo cha jemedari, kabla ya kumleta shadii ambaye wenzetu wana hamu sana ya kumuona na kumhoji, …’akasema na hakimu akawageukia watetezi, na wakili mtetezi akasimama, na kumkabili huyo shahidi,….

NB: Je wakili mtetezi atauliza nini, je kitasadia kitu gani, baada ya maelezo hayo, na kuna shahidi anakuja kuthibitisha sumu aliyopewa Jemedari ni nani huyo?


WAZO LA LEO:Ukweli na uaminifu una siri kubwa sana, ukiwa na sifa hizi kiukweli kabisa, maisha yako yatakuwa na raha, hutapata shida, na kila mtu atakuwa ni rafiki yako , maana wahenga husema ukweli ukidhihiri uwongo hujitenga mbali kabisa na wewe. 
Ni mimi: emu-three

No comments :