Hakimu akiwa bado
kashikilia kirungu chake juu akageuka kuwaangalia wenzake, huku akiwa bado na
mshangao machoni , na wenzake wakiwa na wao wanaangalia kule alipotokea
shahidi, bila kujali kuwa muheshimiwa alikuwa akiwaangalia, kutaka kuongea
jambo, na kwa muda huo yule shahidi
alishafika sehemu ya mbele akisubiri amri nyingine.
Muheshimiwa hakimu,
akajiweka sawa, na kumwangalia wakili mwanadada, kabla hajasema kitu, na akiwa
na uso ule ule wa kushangaa akawageukiwa wenzake na kuwauliza
‘Haya ndio tuliyokuwa
tukiongea kwenye kikao chetu cha mahakimu,…unajua kila mahala kuna utaratibu
wake, hata kama una mambo yako….’akasema , halafu akageuka kumwangalia wakili
mwanadada, na kusema;
‘Mbona mnarudia makosa
yale yale, niliwaambia nini nilipowaita?’ akauliza.
‘Ndugu muheshimiwa
hakimu, ulituambia tuheshimu mahakama kwa kuvalia mavazi rasmi, kwani hapa pana
adabu yake, lakini tukumbuke kuwa kuna watu wana tamaduni zao, kama walivyo
wamasai, huwezi kuwalazimisha wavue mavazi yako na kuvaa suti, au nguo za
kawaida wakiingia hapa mahakamani, , ndio ni taratibu za kimahakama,
kutukujionyesha wewe ni nani, lakini na wao wana haki yao,ndivyo ilivyo kwa
shahidi huyu, kutokana na imani yake, ya kiitikadi,harushusiwi kuondokana na
mavazi yake hayo aliyoyavaa….’akasema wakili mwanadada.
Hakimu akainama na
kuandika kitu kwenye makabrasha yake, na alipoamliza akaangalia saa yake, na
kusema;
‘Tunaweza kuendelea…..
**********
Baada ya taratibu zote za kimahakama kukamilika kwa shahidi
huyo, wakili mwanadada alimsogelea yule shahidi, na kuanza kumuelekeza juu ya
ushahidi wake, akasema;
‘Ndugu shahidi, hebu tuelezee wewe ni nani na kazi zako hasa
ni zipi?’ akaulizwa . Na yule shahidi kwanza akainua kirungu chake
kilichotengenezwa kwa mkia wa mnyama, na kuzungushiwa shanga za hariri za rangi
mbali mbali, kwanza alianza kutaja jina lake halisi halafu akaendelea kwa
kusema;
‘Mimi najulikana kama `mtaalamu,’ na ndivyo wengi
wanavyonitambua hivyo…’akasema na kabla hajaendelea wakili mwanadada akageuka
upande ule wa wapinzani, ..
Upande ule, ulikuwa kimiya, na safari hii, aliyekuwa
kainama, na hata hakutaka kuongea kitu alikuwa wakili mtetezi, yeye alionekana
mnyonge isivyo kawaida yake, na pembeni yake, alikuwepo mteja wake, mshitakiwa
mkuu, kiongozi wa kijiji, ambaye alikuwa akimwangalia huyo shahidi, huku katoa
macho utafikiri ameona jambo la kutisha.
‘Hebu tuambie kwanini wanakuita hivyo, `mtaalamu’?’
‘Kwasababu ya kazi zetu,…’akasema huyu mjamaa akichezesha
chezesha kile kirungu, au mkia wa mnyama huku na huku kupitisha mbele ya uso
wake.
‘Hebu tuambie kazi zenu ni zipi?’
‘Mimi ni mganga wa kienyeji, na pamoja na uganga huo, bado
kuna mambo ya ziada ambayo yanatufanya tuwe zaidi ya mganga wa kienyeji, na
ndipo hapo watu hutuita wataalamu…’akasema huku akijipepea na hicho kifimbo
chake ambacho akikigeuza upande mwingine ni mkia wa mnyama, na akikigeuza
upande mwingine ni kirungu kilichopambwa kwa shanga za hariri
‘Hebu tufafanulie mambo gani hayo ya ziada ambayo yanakwenda
zaidi ya uganga wa kienyeji’
‘Uganga wa kienyeji ni kutibia tu, unajua dawa za ugonjwa
fulani, unawapa watu wanapona…lakini kuna mambo kama ya kuangalizia, wengine
huyaita `ramli’ kuna mambo ya
kusafisha nyota wengine huyaita
`unajimu’
kuna mambo ya mizimu…hayo yote ninayo mimi, ndio maana naitwa `mtaalamu’…’akasema akionyesha matambo .
‘Sawa mtaalamu, hebu sasa turejee kwenye kesi yetu hii, kama
unavyoona watu wanakushangaa, maana ulipotea kabisa, na ikasadikiwa kuwa
umeshakufa.…je ulikuwa wapi na imekuwaje leo kutokea hapa, …?’ akaulizwa.
‘Kama nilivyokuambia kuwa pamoja na uganga, lakini pia
nahusika na mambo ya mizimu, na mizimu ni nini, mizimu ni mababu waliotangulia,
ambao walikuwa na kazi kama hii. Kazi kama hizi ni kurithi, na niliporisishwa,
nilipewa masharti mengi, ambayo nilihitajika kuyafuata, lakini kutokana na
mambo haya ya kidunia, nikajikuta nimeyavunja moja baada ya jingine…’akasema.
‘Ili tusiende mbali na kesi yetu hebu tuambie ni masharti
gani uliyavunja, ambayo, yalikusababisha hadi utokomee huko ulipokwenda….’akaulizwa.
‘Ili nieleweke vyema, naona uniachie nijielezee kidogo,….’akasema
na wakili mwanadada akaangalia saa yake, na kumwangalia muheshimiwa hakimu, na
baadaye akawaangalia kambi ya utetezi, kama wanapingamizi lolote, lakini cha
ajabu, alishangaa kumuona wakili wa utetezi, kakaa na kutulia, na alionekana kama
vile hayupo hapo kabisa, alikuwa kainama huku kashika kichwa.
‘Mimi nilipochukua nafasi hiyo ya utaalamu kwenye kijiji
chetu, sikujua kuwa nitakutana na mitihani mingi, kwasababu nilipata nafsi hiyo
nikiwa bado kijana, na mambo ya ujana unayafahamu yalivyo,damu inachemka, akili
ina tamaa ya kupata, kufurahi, kujirusha na vitu kama hivyo,…hilo sio la siri
tamaa za hapa na pale ndio mtizamo wa ujana. Kwa hali hiyo, japo nilikanywa
nikakubali, lakini ilifikia wakati mwingine, nikawa sijali sana yale masharti
niliyopewa, na hili lilifanya mara kwa mara niwe ninapotea kimaajabu, …’akasema
‘Nilikuwa nikiitwa na mizumu,…na ujue ukiitwa kuna mawili,
umeharibu au unatakiwa kupewa majukumu fulani, na mara tatu nilizowahi kuitwa, nilikuwa
nimeharibu na karibu niangamizwe kabisa, kwani nilikuwa nimezidi kiburi, na
hili lilitokana na kundi nililokuwa nalo,….nilionywa niachane nalo…lakini
haikuwa rahisi hivyo…’akatulia kidogo.
‘Kundi hili lilianzishwa ndani ya kijiji chetu, na
lilijumuisha watu mashuhuri wa kijiji, likiongozwa na mzee wetu wakijiji…na
ukiangalia watu mashuhuri ni nani, ni ukoo wetu tu, walionacho wanaongezewa….au
nasema uwongo ndugu yangu?’akasema na kumnyoshea kile kirungu cha manyoya
mshitakiwa mkuu…na mshitakiwa mkuu,alikuwa vile vile akimkodolea macho, kama
vile kashikwa na bumbuwazi.
‘Na haya ninayoongea kama ni uwongo, aseme…najua
ananishangaa, kuwa msaliti, huwezi ukawa msalitu kwenye kundi ukasalimika, sasa
mimi haina tofauti , …nikikaa kimiya nitaangamia, kubaya zaidi, ni bora niseme,
kwani hawo walionituma wana ujuzi wa kunisaidia,…angalau,…
‘Mzee wetu, kiongozi wa kijiji, yeye alichaguliwa kwa kura
zote kuwa atakuwa ndiye kiongozi wa maaliwatani wa kijiji, tunaweza kusema
wanafamilia, japokuwa kuna watu fulani, waliingizwa, lakini ni kwa vile
walionekana kuwepo kwao ni masilahi ya kundi,…na uongozi ndani ya kundi
inahitajika uwe kweli umeimarika, na
kutokana na wadhifa huo, ilibidi tumtii kwa kila atakalolisema, lakini hilo
atakalolisema ni lazima liwe limekubaliwa na kundi zima…’akatulia.
‘Kundi hilo lilikuwa la siri sana, na ilibidi kutengenezwa
yamini. Yamini ni nini, yamini ni kiapo kinachoambatishwa na imani, na kafara, na
ukikiuka yamini hiyo, huwezi kusalimika, , ukienda kinyuma na msharti, wenzako
hawana hiari, ni kukuua, tu,… adhabu yake ni damu yako, au ya mtoto wako
unayempenda sana…na haina masihara…’akatulia.
‘Moja ya kazi za kundi hilo, ni kuhakikisha kuwa kijiji
chote kinakuwa mikononi mwetu, na mali hasa viwanja, mashamba na miradi mikubwa
tunakuwa tunaimiliki sisi wenyewe, hata kama kuna mtu ambaye ndiye mwenye kumiliki
huo mradi, duka au shamba, au mifugo, sisi kwa kutumia utaalamuu wetu, yeye
anakuwa kama picha tu…’akatulia.
‘Utaona kama ni maongezi tu, lakini ndivyo ilivyokuwa, …kama
unabisha waulize matajiri au wamiliki wa maduka, na miradi hapo kijijini,
watakuambia,…kuwa wao walikuwa wakihangaika na kuchuma, lakini kila wakipatacho
sio sawa na mahesabu yao….sasa jiulize hayo mahesabu mengine yalikuwa yakienda
wapi, jiulizeni, sisi ambao tulikuwa hatufanyi kazi, mbona ndio tuliokuwa
matajiri wa kiaina…kwanini ukoo, na kundi letu sote ni matajiri….’akatabasamu.
‘Kuna kitu wengine hukiita `chuma ulete…’ maana wengine wanahangaika kuchuma, na wengine
wanasubiria tu, ulete ulichochuma, na ndivyo tulivyokuwa tukifanya,…’akatulia
huku akitabasamu lakini usoni kulikuwa na huzuni.
‘Hili mizimu ilikuwa haitaki hayo, lakini mimi kwa kiburi
nikiwa na kundi hili, tulilifanya hayo bil kujali masharti ya mizumu,,…na wale
walioleta kiburi, walikipata cha moto…na mmoja wa hao, alikuwa mama mkunga…..’akasema
na watu wakaguna.
‘Mama mkunga , tulimtaka awe kwenye kundi letu, lakini
alikataa kabisa, ..na tulimtaka awe hivyo kwa vile yeye alikuwa akizalisha watoto
wachanga, na sisi moja ya vitu tulivyovihitajia ili kuwezesha mambo yetu, ni
damu za watoto wachanga, na viungo vyao maana vile havina madoa,…viuongo vya
watu, hasa wale wenye utofauti fulani, kama hawo wenye ngozi nyeupee’akatulia
huku akiangalia huku na kule kama anaona vitu ambavyo wengine hawavioni.
‘Huyu mama mkunga, alitukaidi, na tulimuhitajia sana kwenye
kundi kwa vile alikuwa na karama ya kuona watu wasioonekana, ….simnajua kuwa
wachawi wanaweza kupita mahali hata msiwaone, lakini huyu mama alikuwa
akiwaona, na kwa karama hiyo alihitajika sana kwenye kundi letu, ili asije
akatuumbua….’akatulia.
‘Hapo ndipo tulipoanzia kumsakama, na haikutakiwa auwawe…maana
kama tungelimuua, kwa mikono yetu, tungeliangamia sote, ilitakiwa afanyiwe
jambo, aonekane mbaya, achukiwe,…na hapo tukagundua kuwa ukitaka kumuua mbwa,kwanza
anza kwa kumuita majina mbaya,….na ndipo tukamuanzishia fitina kuwa yeye ni
mchawi, yeye ndiye anayeua watoto, kumbe ni sis tunafanya hivyo, na ….kwa vile
yeye ndiye aliyesimamia ukunga, huo anaonekana ndiyo yeye muuaji, mchawi…
‘Pia hatukutakiwa kumuua, sisi wenyewe, kwa vile yeye ni
damu ya kundi letu…’hapo akatulia.
‘Nasikia ameshajitambulisha na mumeshajua kuwa yeye ni ndugu
wa mzee wetu, kiongozi wa kundi, na kiongozi wa kijiji, mimi nilikuwa msaidizi
wake, na kulikuwa na katibu ambaye mtakuja kumjua baadaye….’akatulia.
‘Nayasema haya kama amri kutoka kwa mizimu, vinginevyo
kutokana na yamini tuliyokula, nisingeliweza kuongea chochote, hapa, …kama
unasaliti kundi, utajiwa na vitu usivyoviona na kujikuta ukichanwa chanwa na
damu yako hunyonywa na mashetani, …nakumbuka vifo kama hivyo vimeshatokea maeneo
ya huko kwetu, zilikutwa maiti zimechanwachanwa,….na mwili ukawa umekakamaa kwa
kukosa damu……hakuna aliyejua sababu ya vifo vyao, ukabakia uvumi tu, ….’akatulia.
‘Hawo walikuwa wasaliti wa kundi….’akatulia na kumwangalia
mzee, mshitakiwa mkuu, na akatikisha kichwa kama anakubali jambo, halafu
akageuka na kungalia mbele…
‘Mama huyu ni ndugu wa damu wa mzee wetu , na aliondolewa
hapa kijijini, na mizumu,..japokuwa watu walikuwa hawalijui hilo,…mizimu ilijua
kuwa akiendelea kuwepo hapo, angeliuwawa mapema kabla hajaweza kuifanya kazi
aliyotakiwa kuifanya…’akatulia.
‘Mizimu ya mababu zetu sisi katika ukoo wetu,haitaki uchafu,
haitaki umwagaji wa damu,…na inahitaji vipaji vya asili, kama hivyo vya ukunga
wa jadi, uwashi, ujenzi,…nk, vile vitu mtu anazaliwa navyo bila kujifunza
kokote, na mama huyu alikuwa na kipaji cha ukunga wa jadi, ni zaidi ya wakunga
mnaoona huko mahospitalini, wenyewe walimvulia kofia, ni mama mwenye kipaji cha
hali ya juu….nendeni mkawaulize…’akatulia.
Mama huyu alipendwa sana na baba yake tangu alipozaliwa,
lakini kukawa na msuguano wa ndani, hadi baba yake akaamua kuoa mke wapili, na
hapo hali ikawa mbaya zaidi...na mke wa pili alipoona kuwa mume wake anampenda
sana huyo binti, akazua mambo, ….akawa anamchukia sana huyo mtoto, na hata
ilipofika mume hawezi kuvumilia tena, akaamua kumuacha mke wake wa kwanza.
Kutokana na hali ilivyokuwa, …wao walihisi ni maamuzi yao,
ikabidi mama huyo aondoke na mtoto huyo wa kike, kwa vile yeye alikuwa bado
mdogo, na alipoondoka hawakujua kalekea wapi, miaka ikapita, na baba mtu
alijaribu kumtafuta huyo mama ili ampate binti yake, lakini hawakuweza kumpata…’akatulia.
Kumbe Mama wa huyo mama mkunga alipoondoka hapo alikwenda
akaolewa na mume mwingine na wakahama na kwenda kuishi mbali,…na ghafla mama wa mama
mkunga akashikiwa na ugonjwa, wa hafla na haikuchukua muda akafariki dunia, na
kumuacha mama mkunga akiwa bado mdogo…..’akatulia.
‘Mama mkunga alikuja kulelewa na mama mwingine, kwa baba wa
kufikia,…hakupata shida, wazazi wake wapya hawo,walikuwa watu wazuri, na hakuona
tofauti, na siku zilivyozidi kwenda wazazi hawo wapya walishanga sana kuona
binti huyo akiwa na karama mbali mbali, ikiwemo ya kujua dawa gani itamsaidia
mama mja mzito, au mama aliyejifungua, na akawa na matatizo ya kukosa maziwa,
kuangakuka kifafa, degedege na magonjwa ya kila aina…’akatikisa mkia-kirungu
chake kama vile anajipepea.
‘Huku nyuma, alibakia mzee wetu huyo, na aliyelelewa na mama
yake huyo mdogo, ambaye hakuwa na kinyongo naye, na akawa kama vile mtoto wa
mama huyo, na hata ilionekana kama vile ni mtoto wa mama huyo…’akatulia.
Ikafikia muda wazee wa familia hii, yaani baba na mama,
wakawa wanaumwa sana, na ilionekana hawataishi muda mrefu, na ndipo baba wa
mzee wetu wa kijiji, akamuita mwanae huyo, akiwa bado kijana, mimi sikuwepo,
nilikuja kuitwa baadaye, na kutambulishwa kuwa kumbe huyo ni baba yangu pia,…wengi
hawalijui hilo, ila mimi ni mtoto halali wa baba huyo, ina maana kiongozi wa
kijiji na mimi ni mtu na kaka yake mimi nilizaliwa na mama huyo mdogo….’aliposema
hivyo watu wakatoa mshangao wa `haaaaa’
‘Yote hayo yalifanyika yawe hivyo, kutokana na mizimu,
haikutaka familia hiyo ijuilikana nani ni nani, na kwahiyo hata mimi
nilichukuliwa nikiwa mdogo na kwenda kuishi mbali kabisa na niliporudi nilikuwa
mtu mzima, ….watu wengi hawalijui hilo, wanaolijua hilo ni watu wa kundi letu
tulilolianzisha, na walitakiwa hayo yawe siri, hawakutakiwa kuongea lolote
kuhusu familia yetu ilivyokuwa.
‘Baba yetu huyo, alifanya kila mbinu mpaka nikafika mara
moja, na siku hiyo akatupa urithi, wa mashamba na maeneo….maeneo mengi hapa
yalikuwa ya kwetu, yamefanywa kuuzwa uzwa, na kugawanywa baada ya wazazi wetu
kufariki, na aliyekuwa akifanya hivyo ni mzee wetu wa kijiji, ni ndugu yangu,
sikuwa na kinyongo na yeye…’akasema na kucheka.
‘Baba alitugawia maeneo, kila mmoja na ukanda wake na eneo
moja hakuligawa, akasema ni eneo la mtoto wake, ambaye hajui yupo wapi, na kama
akitokea tuhakikishe tunapa sehemu yake,na tulimpomuuliza ni nani, akasema kaka
yangu huyo, yaani mzee wetu wa kijiji anamfahamu, …na nikakumbuka kuwa enzi za
utoto wetu kulikuwepo na mtoto mdogo wa kike, ambaye aliondoka na mama yake……’akatulia.
‘Sasa mnaona ilivyo, kuwa kundi hili limeundwa na wanafamilia,
ambao walitawanyika na baadaye wakarejea, na tuliporejea maeneo yetu mengi yalikuwa
yameuzwa au kugawiwa watu wengine, na hapo tukaanza kuyadai, na kaka yangu
akasema ilivyo kwa sasa ni lazima tutumie mbinu nyingine, kwani tukutumia
nguvu, hatutayapata..
‘Ndio chanzo cha kuanzishwa hilo kundi, ….na ukichunguza kwa
undani, wote waliopo kwenye hilo kundi, ni wanandugu, kwa upande wa mama yangu,
ambaye ni mama mdogo wa mzee wa kijiji…na kwa upande wake, wa mama yake
alikuwepo yeye mwenyewe na watoto wake…ana watoto wengi mzee wetu huyo, na
wengine hatuwajui.’hapa akatulia watu walipocheka kidgogo.
‘Ili kundi liwe la kisasa ziaidi tuligundua kuwa ni lazima
tuwe na wataalamu, wasomi, tuwe na watetezi wa kisheria, tuwe na watu
wakutukingia kifua kama likitokea tatizo, kwahiyo kwa vile familia yetu ni
kubwa na ina vijana, ambao wamesoma,tukawajumuisha baada ya kuwaelimisha na
kuiva…ni kweli familia yetu ina wasomi, ina watu wana nyadhifa mbalimbali…ila
sio wote walioaminika,….’akatulia.
‘Kwenye usalama, wapo watu wetu, na hapa karibu tu tuna
kijana wetu, ambaye ni mkuu wa kituo cha usalama …ambaye alikuja kuwa katibu wa
kundi kutokana na akili na uwezo wa kuongea na kushawishi,….na huyu amekuwa
nguzo muhimu kwenye kundi, maana kutokana na yeye, wakubwa wengi, wamekuwa
wakituamini…utasema nini,utaenda wapo ukose mtu wetu, ….hata yule kijana
aliyehusika na kugushi stakabadhi ya malipo ya mwanamama ni kijana ndani ya
mmoja wa wanafamilia wetu,…’akasema an watu wakacheka.
‘Msicheke, mimi nisingeliweza kuja kuisaliti familia yangu
hapa, kama isingelikuwa hii adhabu niliyo nayo, hamjui ni taabu gani
ninayopambana nayo, nina adhambu kutoka kwa mizimu, na nimerejeshwa hapa kwa
muda tu, na kila siku tangu nilipochukuliwa kimiujiza, nilikuwa nikipata
adhabu, nikivua shati langu, mtaona michirizi ya mijelezi, niliyokuwa
nikichwapwa, na kuchomwa moto,….’akasema na akavua kijoho chake na kata mikono,na mahirizi yake aliyoyavaa na manyoya, shanga, na kubakiwa wazi mgongoni, sehemu yote ya mgongoni kulikuwa na michirizi ambayo alisema ni ya fimbo,na kuonyesha
mwili wake, uliokuwa kama umchorwa chorwa na michirizi..’
‘Haya sio mapambo, sikuwa nayo kabla, muulizeni ndugu yangu
pale kama mwili wangu ulikuwa hivi…hii ni adhabu niliyoipata kutoka kwa mizimu,
na kila siku nilikuwa nikiteswa, maana licha ya vipigo hivi, nilikuwa nabanikwa
juu ya moto, kwa ajili ya kulipizwa kwa kumchoma mama mkunga moto, na mimi
nilitakiwa nionje utamu wa moto ulivyo….’akatulia.
‘Kesi hii ilipoanza, nikaambiwa kwa ajili ya mapumziko,
nihitajika kuja hapa kuelezea kila kitu, vingiunevyo nitaendelea kuteseka
kwenye adhabu hiyo..na nashukuru kuwa siku mbili hizi nilizokuwa huku nimekuwa
nje ya kifungo cha mateso, na ….moja ya masharti ni kuwa niseme kila kitu ,
bila kujali kuwa huyo ni ndugu yangu au nani, na nikisema uwongo, narejeshwa
haraka huko kwenye mateso yangu…’akatulia.
‘Kwahiyo nawaomba msamaha sana ndugu zangu, kuwa haya
ninayoyafanya nayafanya kutokana na mateso ninayoyapata…na hali niliyofikia ni
bora kila mtu aubebe mzigo wake mwenyewe…’hapo akatulia kwa muda, na wakili
mwanadada akahisi kuwa huyo jamaa kapotewa na maneno, na akamsogelea na
kumshika.
Wakili mwanadada alimwangalia huyo mtu machoni, alimuona
akiwa kabadilika, na sura ilikuw ikiashiria maumivu makali, na macho yake
yalikuwa yametawaliwa na waupe, na kuwa mtu mwenye sura ya kutisha, hata wakili
mwanadada akasogea nyuma kama anaogopa na hakimu akawa anawaangalia kwa
mshangao.
‘Vipi mbona kimiya?’ akauliza hakimu
‘Oooh, samahani kidogo, nilikuwa nakumbushwa jambo…mizumu
ilinitembelea ghafla, wamesema kuna mambo nimeyaruka au nayakwepa kuyasema ni muhimu…sana’akasema huyo mtaalamu akionyesha
dalili kuwa anapata shida ya maumivu.
‘Ni kuhusu, ndugu yangu huyo, mzee wa kijiji, kuwa ndiye
aliyesimamia operesheni ya kumchoma moto mwanamama, siku hiyo aliaga kuwa
anaondoka, lakini hakuondoka, alikuwa kwenye nyumba zake ndogo, maana ndugu
yangu huyu ana nyumba ndogo nyingi za siri…kama mnabisha ninaweza kumleta
mwanamke aliyekuwa kwake siku hiyo…’akasema na kumwangalia ndugu yake, ambaye
alikuwa katulia vile vile kama kagandishwa.
‘Siku hiyo ya tukio, alikuwa kajificha akiwaangiza hawo
vijana jinsi gani ya kufanya, na alipohakikisha kuwa nyumba hiyo imeteketea
kabisa, akaondoa kuelekea huko aliposema alikuwa amekwenda kabla ya tukio hilo…’akatulia
‘Ndugu yangu huyo ndiye aliyewanywesha sumu wale vijana,
ambao walihusika kwenye uchomaji moto, maana wao walimuona, na ilionekana
dhahiri hawo vijana wanaweza kuja kusema, na haikutakiwa kujulikana…kwahiyo
akawapa dawa ya kienyeji, ambayo inauwa na hata ukipmwa hospitalini, haionyesho
kuwa ni sumu. Mtu anakuwa kama kapagawa…halafu ile sumu inakwenda kuharibu
ubongo na kwenye mapigo ya moja…mtu huyo anakufa kwa kifo cha kuteseka kweli, ….’akatulia
‘Kama nasema uwongo, nampa nafsi ndugu yangu apinge…’akasema
na kutulia na mzee wa kijiji, alikuwa katulia vile vile….na hakimu akamgeukia
kumwangalia huyo mshitakiwa mkuu, lakini mshitakiwa mkuu, alikuwa kama kaganda,
alikuwa akimwangalia huyo shahidi bila kugeuka, au kupepesa macho na hakimu
akaingiwa na mashaka, na akibidi aulize;
‘Kuna tatizo lolote kwa mzee mshitakiwa?’ akauliza na wakili
mtetezi, akageuka kumwangalia mteja wake, na kumgusa kwa mkono, na hapo mshitakiwa
mkuu, akawa kama anaamuka kwenye usingizi mzito na kusema;
‘Hakuna tatizo muheshimiwa, yote ni sahihi kabisa…’akasema
na watu wakacheke, na wengine kuguna, na hata kuzomea wakisema ;
‘Muuwaji…’ na hakimu akagonga kirungu chake kwa nguvu,
kuashiria watu watulie.
‘Hawezi kukataa, maana hiyo ndiyo salama yake, aamue
moja,akateseke na adhambu ya mizumu kama ninayoteseka mimi au atumikie kifungi,
mtakachomuadhibu nyie….’akasema huyo shahidi na kutulia.
‘Sumu hiyo hiyo iliyowaua hawo vijana ndio hiyo hiyo ilimuua
jemedari…’akasema na hapo watu wakashindwa kuvumilia, na kuanza kusema;
‘Anyongwe huyo, muuaji huyo…’na hakimu akagonga kirungu chake na
kusema kwa hasira
‘Ninaweza nikawatoa wote humu ndani tukaendesha kesi hii bila
ya nyie kuwepo,….hii ni mara ya mwisho, kama hamtaweza kuvumilia, ni bora
msiingie humu ndani….’akasema na watu wakatulia kimiya.
‘Ina maana Jemedari aliuwawa kwa sumu?.....’akauliza
mwanadada kwa mhsngao, na kuendelea kuuliza akiwa kwenye mshngao `Ni nani
aliyempa hiyo sumu…?’ akaulizwa.
‘Sistahili kulisema hilo mimi, ..yupo wa kuja kulisema hilo,
na kama mtamruhusu aingie sasa hivi, atakiri hayo yote,…mimi ninaweza kukaa
pembeni, aje athibitishe mwenyewe, na aelezee ni nani aliyemtuma, na kama
mtanihitajia tena, nipo tayari kusimama na kuelezea,..’akasema
‘Ndugu muheshimiwa hakimu,..nawaruhusu watetezi kumhoji
shahidi wetu huyu, na kama hawana maswali basi, tutamuita shahidi mwingine kuja
kuthibitisha kifo cha jemedari, kabla ya kumleta shadii ambaye wenzetu wana
hamu sana ya kumuona na kumhoji, …’akasema na hakimu akawageukia watetezi, na
wakili mtetezi akasimama, na kumkabili huyo shahidi,….
NB: Je wakili mtetezi atauliza nini, je kitasadia kitu gani,
baada ya maelezo hayo, na kuna shahidi anakuja kuthibitisha sumu aliyopewa
Jemedari ni nani huyo?
WAZO LA LEO:Ukweli
na uaminifu una siri kubwa sana, ukiwa na sifa hizi kiukweli kabisa, maisha
yako yatakuwa na raha, hutapata shida, na kila mtu atakuwa ni rafiki yako ,
maana wahenga husema ukweli ukidhihiri uwongo hujitenga mbali kabisa na wewe.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment