Baada ya siku mbili, kesi
ilitangazwa tena, na mshitakiwa mkuu, alikuwa amepata unafuu japokuwa dakitari
alishauri kuwa mshitakiwa apate muda zaidi wa mapumziko, lakini kwa kauli ya mshitakiwa
mwenyewe alisema hataki kusubiri, anataka kuhakikisha kesi hiyo aliyoiita ya kubambikiwa imekwisha
‘Nataka haki itendeke,
nataka kumuona huyo anayejiita kuwa ni ndugu yangu…aonekane, na sio kujificha
kwenye minguo, anaogopa nini’akasema.
‘Sisi tunahisi hataki
kuonyesha jinsi gani alivyoungua….’akasema
‘Nyinyi mnasema tu, ule moto
ulivyokuwa asingeliweza utoka mtu mle…..’akasema na wakili wake akamtizama huyo
mzee, na kuuliza.
‘Ina maana wewe uliuona huo
moto ulivyokuwa?’ akauliza.
‘Sijauona, lakini wewe
mwenyewe kama uliwahi kuuona moto wa nyumba ulivyo, na ikizingatiwa nyumba ile
ilikuwa ya mti na kuezekwa kwa makuti, huo moto utakuwa wa namna gani….?’ Akawa
kama anauliza, na huyo wakili akatulia kwa muda, halafu akamuuliza mteja wake
‘Je kama kweli ni ndugu yako
utasema nini?’ akaulizwa
‘Nitajua hapo nikithibitisha
hilo, ..kwanza ni kuhakikisha kuwa kweli ni ndugu yangu…’akasema
‘Je utajuaje kuwa ni ndugu
yako?’akaulizwa
‘Kama ni ndugu yangu
nitamgundua kwa vile sote wawili tulikuwa na alama ya kuzaliwa zinazofanana ipo
chini ya mkono wa kushoto, ….kama hii hapa’akasema akimuonyeshea huyo wakili
wake alama nyeusi, iliyotuna, kama uvimbe, na wakili wake, akaitizama kwa muda,
na baadaye akauliza.
‘Je wewe na ndugu yako
mlikuwa vipi?akaulizwa
‘Mimi na ndugu yangu
tulikuwa tunapendana sana, unajua
utotoni tena dada na kaka walivyo, …sikutarajia itatokea tuje kutenganishwa kihivyo, lakini hayo ni ya
zamani, na sisi kama watoto hatukuwa tunajua undani wa wazazi wetu kuwa hivyo,
na mimi mwenyewe sikupenda kuyafutailia zaidi, lakini mimi nina mashaka kuwa
huenda huyo asiwe huyo ndugu yangu, kama kweli yeye ni ndugu basi yaliyotokea
ni bahati mbaya na mimi sikuwa na dhamira mbaya juu yake..’akasema.
‘Kwanini uwe na shaka kuw
huyo sio ndugu yako?’ akauliza
‘Kwasababu hajawahi kuishi
hapa, na kama aliwahi kuishi hapa kwanini asije kujitambulisha,…?’ akauliza
‘Je kama angelikuja
kujitambulisha ungelimtambua?’ akaulizwa
‘Sijui…maana ni siku nyingi,
hebu fikiria tulitengenishwa tukiwa na miaka minne, tuli[pisha kwa mwaka mmoja
tu, …..sura zinabadilika, sura ya utoto sio sawa na ya sasa, sina uhakika sana
na hilo….’akasema
‘Na ulikuwa na maana gani ya
kusema hukuwa na dhamira mbaya juu yake na wakati wewe unashukuwa kuwa ndiye
uliyeamrisha wale vijana wachome nyumba moto huku ukijua yeye yupo ndani….’akaambiwa.
‘Ni nani aliniona nikifanya
hivyo…hebu tumia akili bwana, hilo hata mie ambaye sio hakimu, naweza kulipinga
kwa hoja hiyo…usimezwe na hoja zao, ukiwasiliza hawo, utashindwa kunitetea,,
tatizo nimegundua kitu…..’akatulia.
‘Umegundua nini?’ akauliza
wakili wake akiangalia saa yake.
‘Nyie mnawasikiliza hawa
wahuni…maana ni bora niwaite hivyo, wahuni, wao wamekaa na kubuni mambo yao,
kwa vile wanaogopa kuumbuka, ….’akasema
‘Kuumbuka kwa vipi?’
akauliza wakili wake, akiwa anaonekana kukerwa na kitu fulani, lakini hakutaka
kumkatisha mteja wake, akageuka kushoto na kulia, halafu akamgeukia mteja wake,
ambaye alikuwa katulia, akimwangalai jinsi anavyogeuza kichwa kushoto na kulia.
‘Sikiliza wakili wangu hawa
watu, wamemkosa aliyefanya hivyo, sasa ni lazima wafanye hivyo, na njia rahisi
wakaona waninyoshee kidole mimi, kwa kunisingizia, eti kwa vile ni kiongozi wa
kijiji….wewe hulioni hivyo, kuwa ukiwa kiongozi unakuwa jalala la matatizo yote
ya watu,…wewe huoni hilo kuwa kama ni wakushukiwa basi angelikuwa ni huyo
kiongozi wa kundi hilo la hawo vijana….huyo marehemu Jemedari, ndiye mshukiwa
na angelikuwepo hai, angelithibitisha hayo,…..’akatulia akitikisa kichwa kicha
kama kuthibitisha kuwa hayo aliyoongea ni ya kweli.
‘Sikiliza wakili wangu, cha
muhimu, tena sana ukumbuke siku lilipotokea hilo tukio sikuwepo kabisa,
nimekuaj kuhadithia ilivyokuwa, na walisema moto ulikuwa mkali sana, hakuna
kiumbe angeliweza kupona, kama alikuwepo humo ndani,…..mimi siku hiyo sikuwepo,
muulizeni hata mke wangu atathibitisha hilo…’akasema huku akiangalia pembeni.
‘Hiyo ni dhana ya kila mmoja
wetu kwa sasa, ….kuwa wewe unahusika moja kwa moja na matukio hayo na ushahidi
wa wenzetu una nguvu sana,…..cha muhimu ili kuwaweza kupinga ushahidi wao ni
wewe kunitafuta ushahidi wa kuthibitisha kuwa kweli hukuwepo siku hiyo, mkeo
hana nguvu sana za kisheria maana ni mkeo, inawezekana ulimpanga aseme hivyo, ….na
pia hata kama hukumpanga, unaweza ukaaga kuwa unaondoka, lakini hukwenda huko
ulipokusidia,….kwa kifupi hapo, nina maana kuwa mke wako peke yake hawezi
kulithibitisha hilo, mpaka apatikane mtu mwingine ….je tunaweza kumpata huyo
mtu mwingine?’ akaulizwa
‘Kwanini asipatikane, kuna
njia nyingi tu, lakini kwa sasa kwa vile muda haupo, tunaweza kutumia pesa…tumia
pesa, pesa sio tatizo, wewe weka yote kwenye madai yako, utalipwa na zaidi….’akasema
na wakili wake, akatikisa kichwa.
‘Mzee, mimi ninachotaka ni
ukweli….’akasema huyo wakili huku akiangalia saa yake, na huyo mzee naye akawa
anamuangalia huyo wakili kwa mshangao.
‘Ina maana wewe huoni kuwa
pesa inaweza kufanya lolote…?’ akauliza.
‘Mzee, kwanini kila jambo
unakimbilia kutaja pesa, …sio kila jambo linahitajia pesa, nataka uniambie
ukweli ulivyokuwa, ni nani atakayethibitisha kuwa kweli siku hiyo hukuwepo
wakati hayo yanafanyika,….sio kutafuta mtu wa kumtengeneza, hapana nahitaji mtu
ambaye ama kweli ulikuwa naye kwenye hiyo safari au alikuona wakati ukiondoka,
na yeye awe na vithibitisho, je huyo mtu yupo au hayupo?’ akaulizwa
‘Wewe ni wakili wangu sio,
na mimi ndiye ninayekulipa, kwahiyo huhitajiki, kuwa hakimu wangu, …kwa hivi
sasa siwezi kumpata huyo mtu, maana wengi wamenigeuka,kwa hali kama hii
utamwamini nani, na mimi nipo rumande, kama ningelikuwa nje, ningeliwapata
wengi … huoni kuwa wengi kwasasa hawataki kusema ukweli, lakini nina uhakika
ukiwapa kitu kidogo, watakubali kusem ukweli…hilo ndio wazo langu sikuwa na
maana ya kumtengeneza mtu….eeh, wewe wakili bwana, ina maana huniamni tena’akasema
na wakili wake, akatulia akiwaza jambo
‘Mzee, hebu niambie ukweli
ulivyokuwa, nahisi unanificha jambo,na hali ilivyo kwasasa, hutakiwi kunificha
jambo, sitaki nishitukiziwe na mambo, kama vile sijui,….kwahiyo una mawili,
kuniambai ukweli ili niweze kujua jinsi ya kusaidia au ukae kimiya, mimi
nitaiendesha jinsi nijuavyo mimi, lakini ….ujue kuwa itakula kwako?’ akamuuliza
huku akimwangalia huyo mzee.
‘Hivi kweli huniamini wakili
wangu, nimekutoa huko mbali, nikijua wewe ni mkali, jembe, la nguvu,….kama
huniamini mimi basi sema nitafute wakili mwingine, nimeshakuona kuwa wewe hunifai,
nimeona jinsi gani unavyowaachia hawo watu wanaongea tu, mpaka watu wanaamini
kuwa kweli mimi ni mtu mbaya sana, hata pale ambapo ulihitajika kuweka pingamzi
hufanyi hivyo, unakuwa kama mtu aliyepagawa, kwanini huyo mwanadada anakuzidi
kiakili, yule ni mwanamke tu,…' akasema na kutulia kidogo, halafu akawa kama kakumbuka jambo, akasema
'Au wewe umeshampenda sana huyo dada nini....huyo ni mchumba wa mtu,....'akasema na huyo wakili akawa anatabasamu tu, na alipoona wakili wake hasemi kitu akaendelea kuongea kwa kusema
'Sasa amua moja, ufanye kazi
yangu, ili ulipwe, au ujitoe nitafute mwingine, na nakuapia hutpati hata senti
yangu moja, ukijitoa, na nitahakikisha kuwa uwakili wao hauna maana tena…’akasema
akimkunjia uso huyo wakili, na huyo wakili akawa anatabasamu tu.
‘Usione kuwa nafanya utani,
wewe…huwezi kumuachia huyo mwanadada kutamba, na kujiona kama yeye anaweza
kutugaragaza , wanaume wazima tunashindwa na huyo mwanamke, kwakweli umenidisapoiti sana…. 'akawa anatikisa kichwa kuashiria kusikitika.
'Na isingelikuwa kupata hiyo mishituko, nahisi sasa hivi kesi ingelikuwa imekwisha na mimi
nachezea kitanzi, na mimi sitakubali hilo…..’akatulia huku akishika mkono upande wake wa
kushoto, kuashiria maumivu.
Wakili wake akamwangalia huyo mzee kwa makini, na
alipoona kuwa huyo mzee anaongea sana, na inaonyesha hatanii, kweli hali yake inaonyesha anapata maumivu makali
akamuuliza.
‘Upo sawa kweli mzee, kama
unaumwa useme, nikaiahirishe hii kesi…maana ikitokea tena hakimu anaweza
akachukua maamuzi mengine, …..bado tuna safari ndefu, kama hujisikii vyema weka
bayana, hiyo ni haki yako kisheria kama unaumwa, hulazimishwi kufika
mahakamani, ninaweza kuongea hata jama haupo….,?’ akaumuuliza huku akimwangalia
huyu mzee kwa mashaka.
‘Nipo sawa, ni maumivu
ambayo huja na kuacha, yanauma upande huu wa kushoto, toka kidole cha gumba mguuni
hadi kichwani..na vidole vinakuwa kama vimeumwa na nge….ni tatizo gani hili…naona
linakuja kwa aksi kweli kweli…?’ akauliza na huyo wakili wake akasema
‘Huenda umepatwa na tatizo
la Angina na dawa yake ni kuhakikisha
unakwepa yale yatakayo kupeleka kuwaza sana, ….na kesi yenyewe hii inahitajika
uwaze, hukutakiwa uwaze, ulitakiwa uniambie ukweli, ili mimi mawazo yako
niyabebe mimi, …..mimi ndiye wakili wako, na nihitajai kujue ukweli, lakini
nahisi kuwa unanificha mambo muhimu, na ukiyaficha ukabakia nayo moyoni,
yatazidi kukuumiza, ni bora ukaniambai ili nijue jinsi gani ya kuyaweka sawa
kisheria…’akasema
‘Kwahiyo unataka nikuambia
ukweli ulivyokuwa…na utaweza kuyaweka mambo sawa sio ndio hivyo, mimi
nakuaminia, na ni kweli, kama ninakulipa pesa nyingi, kwanini nisikuambie kila
kitu, na pesa sio tatizo kwetu, ukifanikiwa kuyaweka haya mambo sawa, nitakupa
pesa na eneo la shamba…hilo nakuahidi….hizo tulizokulipa ni cha
mtoto…unanielewa lakini?’ akasema kwa kuuuliza.
‘Hiyo ndiyo kazi yangu
uliyoniitia nije kuifanya, cha muhimu kwa sasa ni wewe uniambie ukweli ili
nijue jinsi gani ya kuyaweka haya mambo sawa, swala la pesa na eneo hilo la
shamba sio muhimu kwa sasa…..naomba unielewe hivyo mzee…’akasema huyo wakili
wakawa wanaangaliana na huyo mzee, akainama chini na kusema
‘Nitakuambia na usikilize
kwa makini, na ole wako ukinisaliti,….’akasema an yule wakili akachukua simu
yake na kuanza kurekodi maneno ya
huyo mzee
*************
‘Kooorti………’sauti ya kuashiria kuwa hakimu anaingia
ilisikika, nakila mmoja akawa makini kusikiliza ni nini kinachotakiwa kuanza, kwani
watu walishaanza kunongo’ona pale walipoona hakimu akichelewa kuingia, na hata
kufikia kusema huenda kesi hiyo itaahirishwa tena,
‘Mnaona huyo mzee alivyo, ana nguvu za ajabu, anaweza
akafanya kesi hii iharishwe hadi ije ifutwe…’akasema mtu mmoja.
‘Acha hizo imani wewe, imani kama hizo hazina maendelea kabisa,....hiyo kesi ipo, vinginevyo, tungelijua kuwa haipo,
hawawezi kuwaweka watu hapa , halafu waje kusema kesi haipo…’akasem a mtu
mwingine.
‘Kesi ilitakiwa ianze asubuhi na mapema, saa mbili na nusu,
sasa ni saa nne, hebu jiulizeni kuna nini kinaendelea huko…..’akasema mtu
mwingine.
‘Tuvuteni subira, mimi nina imani kuna jambo muhimu
linatendeka, wasingelikaa kimiya bila kusema lolote…’akasema msemaji mwingine.
‘Haya ndio matatizo ya nchi yetu, hatujali muda, hatujali
hisia za watu wengine, kwanini mmoja wao asiseme lolote, kuwa kuna tatizo gani,
ili na sisi tuwe na amani…’akalalamika
mtu mwingine.
‘Mimi nina imani kuw hilo linalofanyika ni muhimu sana, ndio
maana hata wao wamekaa kimiya…..’kabla hajamaliza, ndio sauti hiyo ya
`kooortiii’, ikasikika.
Muheshimiwa hakim aliingia na taratibu za kimahakama
zikafanyika, na hakimu alipotulia ikatajwa kesi hiyo, na hakimu akaanza
kuongea;
‘Kuna mswala ya kisheria tulikuwa tukiyaweka sawa kuhusu
kesi hii,…kama mnavyoona kesi hii imekuwa ya aina yake,..kwahiyo ilinibidi mimi
nikutane na jopo la mahakimu wenzangu kuangalia baadhi ya mambo yaliyojitokeza,
…kwahiyo msione kuwa nimechelewa kwa mambo mengine, hapana nilichelewa kwa
mambo ya hii kesi….na sikuweza kutoka na kumwamba mtu aaje kuelezea ni nini
kinaendelea, nikijua kuwa hicho kikao hakitachukua muda, lakini…tukajikuta
tumetumia muda zaidi ya tulivyotajia…’akasema muheshimiwa hakimu
‘Sasa tuanze kesi yetu, na wakili mwanadada endelea na
mashahidi wako,….’akasema hakimu, na wakili mwanadada akasogea mbele, na
kusema;
‘Najua wengi wanahitaji tuendelee na shahidi wetu muhimu,
ambaye alikuwa hajamalizia maelezo yake, lakini kwasababu zilizo nje ya uwezo
wetu, shahidi huyo kapatwa na dharura, kama mjuavyo yule ni hakimu wa mahakama
ya mwazo , na alikuja hapa kwasababu h
ii kesi, yetu, tunamtarajia kuwepo baadaye kwenye siku itakapotajwa …’akasema
wakili mwanadada,
‘Hata hivyo hakijaharibika kitu, maana tuna mashidi wengi,
na wote ni muhimu sana katika kesi yetu hii, na wanajua kila kitu kilichotokea
kwenye kijiji hicho, kwahiyo kwasasa nitamuomba muongozaji wetu wa mashahidi
amlete shahidi maalumu kwa leo….’akasema na kabla hajamaliza wakili mtetezi
akaweka pingamizi.
‘Ndugu muheshimiwa hakimu, hii ni mara nyingine tunalalamika
kuhusu tabia hii ya wenzetu, jinsi wenzetu wanavyofanya, …kila mara wanakuja na
shihidi mpya, kabla haujamalizana na shahidi aliyetangulia, tukumbuke kuwa
ilikuwa nafasi yetu sisi kama walalamikaji kumhoji huyo shahidi, …’akasema
‘Lakini umesiki kuwa shahidi huyo hayupo, na nilipokea
taarifa hiyo, mkumbuke kuwa yule ni hakimu, wa mahakama ya mwanzo, ana ofisi
yake huko alipohamishiwa, na alitarajia kuwa siku ile angelimaliza kila kitu,
lakini kukatokea hilo lilotokea, hawezi kusubiria, wakati ofisi yake
inamsubiria….’akasema hakimu
‘Sawa muheshimiwa hakimu, kwa huyo shahidi tunakubali
….hatuna pingamizi naye, tutakutana naye akija…,Je shahidi aliyetangulia kabla
ya huyo, yeye ana sabau gani za kimsingi, ambazo zinamfanya asiweze kuwepo leo….tunamuhitajia
afike amalizie sehemy yake, ili na sisi tuweze kumhoji,…na pia afika akiwa
hajajifunika, ili tumuone vyema. Tutahakikishaje kuwa ndiye huyo mama
mkunga…’akasema
‘Ina maana huiamini hii mahakama?’ akauliza hakimu
‘Sijasema siiamini mahakama hii, muheshimiwa hakimu, lakini
ni haki yetu kudai kile tunachoona kinatufaa sisi kama watetezi…’akasema wakili
huyo
‘Kwahiyo nyia mnataka nini hasa?’ akauliza hakimu
‘Tulikuwa tunataka asimamishwe shahidi huyo , yule
aliyetambulikana kama mama mkunga, ili kwanza tuthibitishe wenyewe kuwa ndio
yeye, na pili tuweze kumhoji’akasema na hakimu akamgeukia wakili mwanadada, na
wakili mwanadada akasema;
‘Kwanini wenzetu mna wasiwasi, huyu shahidi yupo, lakini
bado ana matatizo ya kiafya, hatuwezi kumsimamisha hapa kwa leo, kwa masaa
mengi, ndio maana tunampa muda, ili aweze kuwa na afya njema na muda ukifika
atakuwepo, na mtamuhoji vyovyote mpendavyo, na mtamuona kwa mapana…’akasema
wakili mwanadada.
‘Kwahiyo bado anaumwa, kama bado anaumwa, mbona sijasikia
muheshimiwa hakimua kisema kuwa kapokea taar?’ akauliza wakili mtetezi.
‘Bado yupo kwenye uangalizi wa dakitari, na yeye ndiye
atakayemruhusu …lakini kwa leo dakitari kasema kuna vipimo, ambavyo
alichukuliwa na majibu yake ni leo, baada ya hapo ndipo anaanza amtibabu
stahiki,…na sikuhitajai kumwambia hakimu, kwa vile nilijua kuwa tunaendelea na
shahidi mwingine, kutokuwepo kwake, leo,hakuzuii kesi yetu kuendelea…..’akasema
wakili mwanadada.
‘Haya tusipoteze muda, waendesha mashitaka, tunahitajai
shahidi wenu wa leo, na hatutavumilia malumbano yasiyo ya kisheria kwenye
mahakama hii..’akasema hakimu na mara mlango wa kuingilia mashahidi
ukafunguliwa…
Shidi aliyetokea, aliwafanya watu wote wainuke kwenye viti
vyao, hata hakimu aliyekuwa kashikilia
rungu lake akitaka kuligonga kuashiria watu watulie, akajikuta akiwa
kalishikilia hewani, na hata yeye alibakia mdomo wazi…
NB: Tengua kitandawili hiki ni nani shahidi huyu?
WAZO LA LEO: Tuweni
makini sana tunapofanya makabidhiano au malipo iwe kwa pesa au kwa vitu. Ni
vyema matendo hayo yawahusishe mashahidi, na maandishi ya kisheria, kuhesabiana
nk. Kuna tabia ya watu wanapenda kukopeshana pesa bila mashahidi au maandishi, au
kupeana pesa bila maandishi au mashahidi,au kuhesabu kile walichopewa au
kulipwa, wakisema kuwa wanaaminiana, hiyo sio sahihi, kwani ubinadamu una
mapunguzfu yake, kuna kusahau, na hujui hatima yako itakuwa lini, fanyeni kwa
audilifu kwa kuhakiki, na kuandikishana mbele ya mashahidi.
Ni mimi:
emu-three
3 comments :
Mmh, patamu hapo❗
jemedari
jemedari anafuata!
Post a Comment