Kila mtu alikuwa na hamu ya kumuona huyo shahidi mpya alieingia, na wakati
anaingia ni wachache sana walikuwa na hamu ya kumuona, kwani walisikia kuwa
shahidi wa kwanza hatakuwepo, kwahiyo walijua ni shahidi mwingine ambaye sio
vutio kwao.
Alipoingia huyo shahidi mpya, na wale wachache waliomuna wakaguna
na kuanza kunong'ona, wengine na wao wakashindwa kuhimili, waliinuka kwenye viti
vyao, kuangalia upande ule anapotokea huyo shahidi, hata wakili upande wa utetezi alijikuta akiangalia upande ule kwa
mshangao na mshituko, na hata zile, tambo zote zilikwisha, akasogea na
kumnong’oneza mteja wake, ambaye alikuwa naye kaduwaa…..
Kisa chetu kwenye sehemu hii inaanzia hapo….
‘Unahisi huyu shahidi atasema kila kitu?’ akauliza
wakili huyo wa utetezi akimuuliza mteja wake ambaye hakuwa na amani na wakati
huo alikuwa akijifanya kukata kucha, kwa wembe aliokuwa kaomba ili aweze
kukacha kucha zake, zilizokuwa ni ndefu…,.
‘Mimi niliwaambia huyu mtu
hawezi kuuza kazi yake kwa tamaa ya pesa…’akasema huku akiwea ule wembe mbele
yake.
‘Lakini usijali, hii ndio
mitihani ya kazi zetu, mimi sitamtambua kwa wadhifa wake,kwangu mimi yoyote
atakayesimama kwenye kile kizimba cha ushahidi ni sawa sawa na wengine wote…tutapambaan
kisheria…’akasema huku akitikisa kichwa kwa kujiamini, …na mara sauti ya
hakimu, ikasema.
‘Najua unafahamu taratibu
zote za ushahidi, ….’akasema muheshimiwa hakimu, ambaye naye japokuwa alikuwa
akitabasamu, lakini mshangao haukufichika usoni kwake.
‘Nafahamu
muheshimiwa,…..’akasema huyo shahidi na kupita sehemu stahiki, akaapishwa,
halafu akapanda kizimbani.
Wakili mwanadada akageuka
kuwaangalia wenzake, ambao na wao walikuwa kwenye mshangao, hawakujua kabisa
kuwa atakuwepo shahidi kama huyu kwa upande wao, na hata yule ambaye siku zote
alikuwa akiendesha mashitaka alijikuta akimsogelea mwanadada, na kunyosha mkono
wa kutoa pongezi, kwa mwanadada huyo lakini pia akasema;
‘Una uhakika atasema yote
bila kuficha….?’ Akauliza
‘Wewe subiri,…’akasema
mwanadada na kugeuka upande wa kambi ya utetezi, ambapo wote bado walikuwa
wakikodoa macho kule mbele kumwangalia huyo shahidi, na mshitakiwa mkuu,
alikuwa kaamua kuinama chini, sijui alikuwa akiomba, au akilia au mawazo
yalimzidi na shinikizo la damu linampa shida.
‘Japokuwa ulishajitambulisha
kwenye kiapo, lakini sasa kila mmoja anataka kukusikia vyema, kwahiyo hebu
jitambulishe kwa uwazi zaidi, wewe ni nani na kazi yako ni ipi?’ akasema
mwanadada.
‘Mimi ni hakimu wa mahakama
ya mwanzo, lakini hapa sisimami kama hakimu, nasimama kama shahidi…’akasema
huyo muheshimiwa baada ya kutaja jina lake.
‘Ni ajabu kabisa, eeh,..
hakimu leo kawa shahidi, …..’akasema mwanadada akiwaangalia upande wa utetezi,
na wakati huo wakili mtetezi alikuwa akiandika andika na kujifanya hajali,
aliposikia hivyo, akainua kichwa na kujifanya kutabasamu.
‘Ndugu muheshimiwa,….eeh,
shahidi, maana humu ndani muheshimiwa ni mmoja, ….bwana hakimu pale mbele,
…’akasema mwanadada na hakimu akatabasamu, na watu wakacheka.
‘Ndugu shahidi, nafahamu kwa
uwazi unaifahamu kesi yetu hii, kwani kesi hii kwanza abisa ililetwa mbele yako
kwenye mahakama ya mwanzo, na kwa mujibu wa sheria, ikaamuliwa ipelekwe ngazi
za juu, je ni kwanini umeamua kuja kutoa ushahidi …?’ akauliza mwanadada.
Shahidi huyo alikohoa
kidogo, kusuuza koo, na baadaye akasema;
‘Ngoja niende moja kwa moja
kwenye hoja,..ni kweli kesi hii naifahamu huenda kuliko mtu yoyote, na
ilipoletwa mbele yangu kwa mara ya kwanza, nilifahamu kuwa itakuwa ngumu sana,
na hata pale nilipoamua kuwa iende hatua za juu bado nilikuwa sina amani, kwani
nilitenda kinyume na walivyotaka hawo watu, …., lakini japokuwa kesi hiyo
ilikwenda ngazi za juu, bado nilijua huenda , haki isingelitendeka….’akasema
‘Kwanini ulikuwa na wasiwasi
huo?’ akaulizwa.
‘Kwanza nianze kusema kuwa,
kuna baadhi ya wahusika, ambao ndio shina, hawapo kwenye kesi hii, je ni
kwanini, kwani nafahamu labda ni kutokana na wadhifa wao, lakini hata hivyo,
walistahili angalau kutajwa kama washitakiwa,…, je huoni hapo kuwa huenda
wanalindwa, na huko kulindwa, hakuwezi kuifanya haki isitendeke….’akasema na
wakili wa utetezi akaweka pingamizi kuwa hakimu huyo anataka kuleta kesi
isiyokuwepo kwenye kesi hiyo.
Hakimu akamwangalia hakimu
mwenzake,akatabasamu na kusema ;
‘Endelea muheshimiwa,….usiwe
na shaka haki itatendeka, nafahamu unafahamu hivyo…’hapo watu wakacheka.
‘Unaposema kuna wahusika
ambao ni kama shina ambao hujawaona hapa, una maana gani muheshimiwa….?’
Akaulizwa
‘Nina maana kuwa hawo watu
walikuwa mstari wa mbele, kuyakumbatia haya yote, na huenda kama wangelitimiza
wajibu wao, huenda tatizo hili lingelikwisha mapema,….na kwasabau ya hilo, hawa
watu wa chini, walijiona wana haki, na wasingelifaanywa lolote….’akasema
shahidi
‘Ndugu muheshimiwa ….oh,
samahani, ndugu shahidi,….’watu wakacheka.
‘Ndugu shahidi hebu tueleze
sasa, je wahusika hao unaosema ndio mashina, walifanya nini, ambacho kiliwahi
kuletwa kwako, na ukagundua kuwa ni wao…babadala ya hawa washitakiwa wengine?’
akauliza mwanadada, akijua kuwa kapeleka mbele zaidi, lakini alifanya hivyo,
akijua kuwa muheshimiwa huyu anajua ni nini kinatakiwa kufanyika kabla hajajibu
sehemu hiyo.
‘Kesi hii ilipoletwa mbele
yangu, na kuitangaza, kuwa itasikilizwa kwa tarehe iliyotajwa, nilishangaa
usiku nikijiwa na wageni,wageni hawo, walijitambulisha, kuwa ni wazee wa
kijiji,….akiwemo mkuu wa kijiji hicho?’ akasema muheshimiwa hakimu.
‘Una maana huyo mkuu wa
kijiji ndio huyo mshitakiwa mkuu?’ akaulizwa
‘Ndio yeye …yule pale,
…’akasema hakimu wa mahakama ya mwanzo
‘Walikuja kwako kwa ajili
gani?’ akaulizwa.
‘Kwanza hawakuliweka wazi
jambo walilonijia, lakini baada ya kuwahoji, zaidi, wakasema wazi wazi, kuwa
wanataka kesi hiyo ifutwe, na isisikilizwe tena…na nilipowaambia hilo
haliwezekani, wakasema niwe makini kwa hilo, kwani mimi bado ni mgeni, na eneo
hilo, lina taratibu ambazo nikizikiuka huenda , nikawa matatani…’akasema.
‘Ukawaambieje…?’ akaulizwa.
‘Nilijua ni vitisho ambavyo
nilizoea kuvipata nikazarau, na kusema, mimi ninajua ni nini ninachokifanya
hata hivyo, naomba wanipe muda wa kutuliza kichwa na kujua ni nini natakiwa
nikifanye,…’nikawaambia kwa busara
‘Je wao walikupa sababu
yoyote kuwa kwanini kesi hiyo isisikilizwe?’ akaulizwa.
‘Sababu walionitajia ni kuwa kesi hiyo ni kifahamilia
zaidi, imeingilia mambo ya mila na desturi na kama nitashinikiza na kukiuka
hizo taratibu, ….nitakuwa nimeingilia mambo yaliyokuwepo tangu enzi na enzi, na
kuleta mchanganyo…na yakuwa kama ni hayo mauaji yaliyotokea yalisababishwa na
vijana wavuta bangi tu….’akasema.
‘Nikawaambia kuwa polisi
walishafanya uchunguzi na wamegundua kuwa kuna mauaji ya kuwa hawakufa kama
ilivyotajwa awali, na kwahiyo ni haki kesi hiyo sikilizwe…’akasema
‘Ina maana kesi hiyo ilikuwa
ya mauji, …?’ akaulia mwanadada kama anashangaa.
‘Ndio ilikuwa ni mauaji…vijana
wale waliuwawa,..ushaidi upo, lakini uliibiwa, …., na ililetwa baada ya
uchunguzi, na kuletwa kwangu bado kulikuwa na utata, maana watu wa usalama
walikuwa kwenye makundi mawili, wengine wakipinga kuwa sio sahihi na wengine
wakisema ni sahihi…’akasema na kutulia.
‘Ukisema watu wa usalama una
maana gani?’ akaulizwa
‘Kesi inapoletwa kwenye
mahakama, hasa kesi ya muaji, ina maana polisi wameshafanya kazi yao, ya
uchunguzi, hawo ndio watu wa usalama ninaowaongelea….’akatulia kidogo.
‘Kwanza kesi hiyo ilikasitishwa
kuletwa mbele yangu, ikiaminika kuwai vijana hawo walikufa kwa kuvuta bangi,
lakini ukumbuke kuwa vijana hawo ndio waliokua walinzi wa kijiji, ...na moja ya
kazi yao ilikuwa kuwatafuta vijana wavuta bangi, leo unaambiwa kuwa wamekufa
kwa sababu ya bangi zao…haiingii akilini…sasa alipokuja huyo mkuu idara ya
upelelezi, nikamuomba afanye uchunguzi , na yeye akakubali, na ndipo, wakagundua
mengi, ambayo ndiyo yaliyonifanya nije hapa kuyafichua, baada ya vielelezo
vilivyokuwa vimeibiwa kupatikana….’akasema, na upande wa utetezi, ulitaka kutoa
hoja, lakini ukasita.
‘Haya
muheshimiwa uwanja ni wako unaweza kuendelea…’akasema mwanadada, akisogea
nyuma, kuonyesha kuwa hapo anamuachia shahidi aendelee mwenyewe.
‘Kwanza kabisa
niliamini waliyosema hawo wazee, unajue tena unapokuwa mgeni, na kutokana na
kazi yetu ilivyo, nisingeliwakatalia moja kwa moja, nikawaambia wanipe muda,
ili nione jinsi gani nitakavyofanya, maana wamekuja na ujumbe, na mimi siwezi
kuwaahidi moja kwa moja kuwa nitafanya wapendavyo wao….’akatulia.
‘Kilichonishitua
ni pale nilipokabidhiwa kitita cha pea na hati ya eneo la shamba, kuwa hivyo ni
mali yangu…’akasema
‘Samahani
kidogo muheshimiwa , nikurudishe nyuma, hawo vijana waliouwawa, uliweza
kugundua walikufa kufa vipi?’ akaulizwa
‘Kwa sumu,…nitakuja
kutoa ushahidi huo baadaye, na aina ya sumu waliyoitumia ambayo ni ya asili,
sio rahisi kupima kwa vipimo vya haraka ukagundua…..’akasema na kutulia kidogo
‘Na endelea
hapo uliposema ulipewa eneo , ni eneo lipo na lipo wapi….?’ akaulizwa.
‘Ni eneo kwenye
kijiji hicho chenye migogoro, na sehemu kubwa iliyotoka kwa mke wa marehemu, huyu
mwanamke, alinunua eneo, na hilo eneo hakutaka kuliweka katika madai yake,
kwani alikuja kuambiwa baaadaye kuwa katapeliwa, kuwa alikuwa kanunua eneo
langu, na alipoonyeshwa hati na kila kitu, akajiona hana chake…, hakutaka
kujihusisha nalo tena...sijui kwanini hakupambana na watu waliomuuzia,….labda
atakuja kuwakilisha madai yake kwenye kesi yake.’akasema hakimu huyo.
‘Kwakweli
nilipokuja kugundua baadaye kuwa eneo hilo ni mali halali ya mjane,..na yeye
mwenyewe katika madai yake hakuweza kuliweka, kama sehemu ya madai, iliniuma
sana…lakini sikuweza kuonyesha hisia zangu kwa wakati huo, niliona jambo bora
nikujifanya ni mmoja wao, na ipo siku nitayafuchua haya yote…na haki yake
itarejea mikono mwake’akasema huyo shahidi.
‘Je ulipokea
hizo pesa na hati ya nyumba waliyokupa?’ akauliza mwanadada.
‘Mwanzaoni nilikataa
kata kata,, …, na walipokuja mara ya pili nikavipokea, nikiwa kwani nilikuwa nimejiandaa,…’akasema
‘Ulikuwa
umejiandaa kwa vipi?’ akaulizwa.
‘Naomba
ushahidi wa kanda ya DvD, uwakilishwe mbele ya mahakama hii, kuonyesha tukio
zima lilivyokuwa, nahisi watakao-uona kwa haraka watafikiria kuwa mimi
nilikubali kupokea hiyo rushwa, lakini je ningekubali vipi, na hapo hapo
nijirekodi,…kama nilivyowaambia, nilifanya hivyo, nikiwa na maana ya kujifanya
nipo nao, ili baadaye niweze kuwanasa…’akasema
‘Endelea
muheshimiwa…tunakuelewa,’akasema mwanadada.
‘Ilibidi sasa
nijihusishe kwenye uchunguzi binafsi kufuatalia, ni kwanini haya yote, ni
kwanini ifikie hivyo, kwanza nikakutana na mkuu wa kituo cha polisi, nikaongea
naye,…’akacheka
‘Msione kwanini
nacheka, maana mkuu huyo alinisihi kuwa nichukue hizo pesa, na hiyo hati na
kama nahitaji zaidi niseme, na yeye atahakikisha kuwa napata zaidi….’akasema na
watu wakaguna na wengine kucheka.
‘Nikaona sasa
kazi ipo, kama mwenzangu ambaye niliona kuwa tutashirikiana naye, anasema
hivyo, je mimi nitafanya nini…elewa makosa kama hayo yakitoea, watu wazuri wa
kuyafuatilia ni watu wa usalama , na ukimpata kiongozi wa juu ni vyema zaidi
maana yeye atatoa amri kwa watu anaowaamini…sasa nimefika kwake, na kupewa hilo
jibu kama hilo ningefanyaje….’akatulia.
‘Hapo
nilichanganyikiwa, na ukumbuke kabla ya hapo nilishapata vitisho vingi, na hata
familia yangu ikatishiwa usalama wake, ndio maana familia yangu haipo hapa,
….hayo yalitokea nyuma kwenye kesi nyingine, maana ilifikia htua nachaguliwa
kesi za kusimamia, na nyingine naambiwa nizipotezee…’akasema na watu
wakacheka…’na yeye akatabasamu.
‘Nilipokuwa
mkaidi, …kama mnakumbuka vyema, binti yangu alipotea kijabu ajabu,…na ogopa mtu
akikugusia familia yako, na binti nilikuwa nampenda sana…nilikuja baadaye kuambiwa kuwa ili nimpate huyo binti
yangu, nihakikisha nafuata hayo wanayotaka wao…maaliwatani wa kijiji, …’akatulia.
‘Kiubinadamu,
unapogusiwa familia yako…hasa watoto wako, inashitua moyo, na hapo niliwaza
kwanini nisiwe upande wao kwa muda, ili niikoe familia yangu kwanza , kwahiyo
nikakubali, lakini hawakujua lengo langu ni-nini….’akatulia na wakili wa
utetezi, akasema;
‘Usitudanganye
muheshimiwa,…umewasaliti wenzako baada ya kuona mambo yanakuwa magumu…’akasema wakili
mtetezi chini kwa chini, na watu wakasikia na kucheka, na hakimu akamwangalia
huyo wakili, na huyo wakili akasema;
‘Samahani
muheshimiwa imenitoka tu….sikuwa na nia ya kusema….’akasema huku akiinama
kuomba msamaha, na atu wakacheka.
‘Tusifanye
mzaha,…hapa tupo kwenye kesi ngumu, ambayo inahitaji umakini….tusipotimiza
wajibu wetu, haki za watu zitapotea, na hata fitina zitatokea, nakuonya kwa
mara ya mwisho …sitaki mzaha, na ikitokea tena, nitaanza kutoa adhabu, kutokana
na vifungu vya sheria…’akasema hakimu.
‘Shahidi
endelea…’akasema hakimu huku akiandika jambo kwenye makabrsha yake.
‘Basi kweli
nilipoanza kufanya watakavyo wao, binti yangu akapatikana,…..sikuamini siku
hiyo, mke wangu alilia sana, na ungemuona huyo binti alivyokuwa machozi
yangekutoka, maana sisi tulishafikia hatua ya kuwa huyo binti keshafariki, na
tulipomuuliza ulikuwa wapi, yeye anasema hajui, hajui kabisa, …na alikuwa kama
kachanganyikiwa…akili haijui, imesimama, anakuwa kama zezeta fulani
hivi…kachafuka, ana minywele mirefu….’akasema
‘Siku alipofika,
kesho yake akaja mtu wanayemuita `mtaalamu’ yeye alisema kuwa ndiyo yeye
aliyesaidia binti yangu kupatikana…akadai kuwa bint yangu alichukuliwa msukule,
lakini hakufanywa kama wanavyochukuliwa watu wengine, alikuwa kahifadhiwa kwa
muda…., na kwahiyo kuna dawa atampa na binti yangu huyo atarejea kwenye hali
yake kama kawaida.
‘Mke wangu
aifiki ahdi kumpigia magoti, kuwa afanye hivyo, amrejeshe inti yangu kuwa
katika hali yake ya kawaida, na atamlipa pesa azitakazo, na huyo mtu akasema;
‘Mimi sitaki
pesa yenu, ….timizeni matakwa ya hawa watu, kuwa msitende kinyume na maagizo
yao, vinginevyo, binti yenu akipotea tena hamtamuona, maana atawekwa kwenye
kundi la hawo msukule wa kawaida…mimi natimiza wajibu wangu tu, sihitaji hata
senti moja kutoka kwenu…’akasema na kweli akampa dawa binti yangu na, kesho
yake akaamuka akiwa yule binti yetu tuliyemzoea, akiwa na afya yake kama ya kawaida, lakini hakuweza kukumbuka wapi
alikuwa anaishi kwa miezi hiyo mitatu
aliyopotea….’akasema.
‘Sisi mahakimu
hasa mahakimu wa mahakama ya mwanzo, tunafanya kazi hii kwenye mazingita
hatarishi, tunakutana na majaribu mengi, na usipokuwa makini, unaweza ukasahau
kazi yako na kufuata wayatakayo watu wenye ubinafsi , hasa wale wenye uwezo, au
wale wanajiita maaliwatani wa eneo husika…kwasababu mahakam hizo ndizo zilizopo
karibu na watu,…na nyingine ukifika zimechoka,…kama walivyo mahakimu wenyewe’akatulia
na watu wakacheka..
‘Tulishauriana
na mke wangu, kuwa ni bora wao waondoke, warudi huko kwetu, ili na mimi niweze
kufanya kazi yangu, na lolote likitokea nijue nipo peke yangu…ilifikia hatua
nilitaka kuacha kazi kabisa, japokuwa matukio kama haya sio mara yangu ya
kwanza kukutana nayo, ..lakini hili lilinishitua sana, kuona binti yangu
aanchukuliwa na anarejeshwa akiwa katika hiyo hali…..’akatikisa kichwa.
‘Basi nikawa
nauma huku naupilizia, nikitafuta wapi niende ili tuweze kusaidiana kukomesha
hii hali, na sehemu iliyotisha sana ni hicho kijiji,…na wengi wanakiita kijiji
cha wanga…’akasema na watu wakacheka.
‘Ni kweli, sio
kwamba natania, waulizeni watu, wanaokizunguak hicho kijiji,..na kila mara
kulikuwa kukitokea mauaji na kupotea kwa watu kiajabu ajabu, na yakitokea
mauaji, utakuta ni ya imani za kishirikiana…na ukiongea na polisi walifuatilie,
watakuahidi kuwa watafanya hivyo, lakini huwezi kupata hitimisho lake, na
wenyewe walifikia hatua ya kuogopa…mwisho wa siku kesi nyingi zilibakia kwenye
majalada, na nikaonekana kama mimi sitimizi wajibu wangu….’akatulia.
‘Bahati nzuri,
maombi yangu yakakubalika, kwani niliomba kutoka ngazi za juu, kuwa kuwe na
kitengo maalumu cha upelelezi, kichunguze hayo yanayotokea, …na nashukuru kuwa
kiongozi aliyeletwa hapo, alikuwa jasiri,…alijiamini, wanasema wenyewe aliga
kwao…’watu wakacheka.
‘Na japokuwa na
yeye alikuja kupata mitihani mingi, hadi…kufikia kuachana na mkewe….lakini
hakurudi nyuma, nashukuru sana kupata mtu kama huyo….lakini hawa watu, na wao hawakurudi
nyuma.
‘Kwa vipi
shahidi, ndio iliyokufanya uhamishwe…..na je vitisho vyao vilifanikiwa,
nakuharakisha shahidi wangu maana muda wako unakaribia kuisha..’akatulia.
‘Aendelee tu,
usimharakishe….’akasema hakimu, na wakili upande wa utetezi akashika kichwa
huku akiwa kainamia makabrasha yake, alikuwa kama vila hataki kuskia hayo
yanayoongewa.
‘Sasa kama
nilivyowakilisha huo ushahidi wa kanda za DvD, mtaona mengi yaliyokuwa
yakitendeka, ila swali kubwa ukizinaglia hizo kanda, za DvD, utaona kuna mtu
anatoa amri, lakini haonekani, je ni nani huyo, hapo ilikuwa kazi yangu ya
ziada kumtafuta,..na sio rahisi kama mnavyofikiria nyie, hakuwa kazi rahisi
kuja kumpata mtu huyo, na hata nilipompata, niligundua kuwa ni …..’akatulia na
kutabasamu, na watu wakacheka.…’akatulia na hakumalizia sehemu hiyo hata wakili
mwanadada hakupenda kumuuliza ni nani, kwani alijua hilo litakuja kujibiwa
baadaye.
‘Alipokuja huyu
mkuu wa kitengo cha upelelezi, nikakutana naye na nilimuelezea yote, na yeye
akasema nimpe muda, kwani ndio amefika, na ili kuweza kufanya kazi yake vyema,
ni vizuri, ukayasoma mazingira, na ndivyo alivyofanya, hakuwa na papara, …na
siku nyingine nilipokutana naye, akasema…’hapo akatulia.
‘Kuwa adui
mkubwa tunaishi naye….’akatulia na kutabasamu
‘Adui mkubwa ni
mtu asiyeshikika kirahisi, na tusipoangalia tutaumia, kwani mwenzetu kashikilia
mpini, kwahiyo tuwe makini kwa kila hatua,…nikamkubalia, na hakutaka kuniambia
ni nani, alisema ipo siku ataniambia, lakini mpaka apate uthibitishi ulio wazi,
..maana huyo mtu huwezi ukapeleka shutuma zako zisizo na mguu wala kichwa, hizi
shutuma zitakugeukia wewe mwenyewe…’akatulia.
‘Mimi
nikamwambia nina ushahidi, nimeshaukusanya, kwahiyo kama anautaka basi nitampa
ili tuufanyie kazi…’akasema bado hauhitaji huo ushahidi, yeye anataka
kukushanya ushahidi wake mwenyewe kwa namna anayoijua yeye…mwanzoni nikajua ni
wale wale…’akatulia na watu wakacheka
‘Na haikupita
muda, ushahidi wangu wote ukapotea….’akatulia.
‘Hebu wewe
fikiria ungelimshuku ni nani aliyeuiba huo ushahidi…sikuogopa nikamwendea huyu
mkuu wa upelelezi nikamwelezea hisia zangu, kuwa ni yeye peke yake ndiye anayejua
kuwa nina ushahidi kama huo, na sasa umepotea,…tukawa hatuelewani, kwani yeye
alikataa kata kata kuwa hakuchukua yeye…’akatulia.
‘Kwa hali kama
hiyo utakwenda wapi, utamwambia nani, na nimeshatishiwa kuwa huyo ambaye
hajulikani, ni mtu,anayejuana na wakubwa wote…’akatulia.
‘Siku moja
nikiwa nimetulia, nikiwa sasa naendesha hii kesi ya mwanamama, alifika mtu
mmoja, akiwa kava mawani meusi, akaniambia
‘Ndugu tunakupa
onyo la mwisho,…kesi hii ya mwanamama, ipotezee, au hakikisha huyo mwanamama
hashindi maana akishinda, hata eneo la shamba nililopewa, itabidi
lichukuliwe….na pia nisijidangenya kuwa kwa vile nipo peke yangu bila familia
…hakutafanyika kitu….akaniambia kuwa wenzangu hawo waliomtuma wana ushahidi kuwa nilipokea rushwa…kwahiyo
nisipofanya wapondavyo wao, watahakikisha nafukuzwa kazi na hiyo haitakuwa
mwisho, wataniandama mimi na familia ayngu hadi nitatamani kujiua…’akatulia.
‘Nikagundua
kuwa sasa kila kitu kimeharibika…na niligundua kuwa huenda ni kutokana na ule
ushahidi ulioibiwa, na kama nilivyowaambia, kuwa ukiuangalai huo ushahidi kwa
haraka utaona kama mimi nilikuwa napokea rushwa,….lakini ukitulia na kuangalai
kwa makini, utaona kuwa kuna shinikizoa ndani yake…ikawa hivyo, na nikawa njia
panda, nakujiuliza sasa nifanyeje…’
‘Hakikisha
unafanya kila tunalokuambia ufanye, kuna kesi hii ya mauaji, ambayo ililetwa na
watu wa usalama, unachotakiwa wewe ni kuipiga kalenda, na mengine tuachie sisi…’akasema
na mimi nikamwambia
‘Acha
nifikirie….’akatulia
‘Huyo mtu
akaniuliza kwani mimi nina shida gani, na kwanini nafanya kazi, …eti kazi
unafanya ili uate pesa, na hawo watu wapo tayari kunipa kila kitu, kama
nahitaji eneo jingine, au kama nahitaji nyumba, au kama nahitaji gari…nisema na
wao watanipa, lakini hakikisha kuwa kesi hii inafutika,…vinginevyo nitahama
hapa na nitapelekwa sehemu ambayo sipendi kwenda na huko utakuwa ndio mwanzo wa
kupoteza jira, na mwisho wake nitafukuzwa kazi na kubakia masikini …’akasema.
Hapo mimi
sikuvumilia uajsiri ukanijia, na siku hiyo nilikuwa nimeandaa kifaa cha
kurekodia kila kitakachotokea, kwahiyo niliongea kwa kujiamini, kuwa sasa
nimewapata, nina ushahidi mwingine…’akasema huyo shahidi
Nikamwambia huyo
mtu,….‘Mimi sifanyi kazi hii kwa ajili ya utajiri…kama ni utajiri wa namna hiyo
ningelishaupata siku nyingi, lakini najua kuwa utajiri wa namna hiyo ni wa muda
mfupi, …dhambi za namna hiyo hazina muamala, maana unakuwa rafiki wa shetani,
na mimi sio shetani….’nikasema na huyo jamaa kacheka sana, na kuondoka.
'Ulikuja kumgundua huyo mtu ni nani?' akaulizwa
'Ndio nilikuja kumgundua,
‘Haikupita muda
ndio nikapata huo uhamisho wa haraka haraka, na nilipata ujumbe kuwa huo ndio
mwanzo wa kuhakikisha maisha yangu yanapotea…haitachukua muda nitafukuzwa kazi..’akasema.
‘Ndio
umehamishwa na kazi umefukuzwa kama walivyodai wao…?’ akauliza mwanadada
kitabasamu.
‘Kuna barua
nimeletewa hivi karibuni, siwezi kuliongelea hili hapa kwasasa, …lakini hata
hivyo nipo tayari kufukuzwa kazi, nikijua ninachofanya ni haki, na nitasimamia
hiyo haki hadi hapo…na kadri ya uwezo
wangu, najua jinsi gani ilivyo ngumu , hasa familia yako inapoingiliwa, familia
isiyo na hatia,na wala haijui ni nini kinaendelea, najua jinsi gani maisha
yalivyo magumu, ukiacha kazi kwa hali tuliyo nayo, huna mbele wala nyuma,unaweza
ukaishia kubaya, nimeliona hili kwa watu wengi….kwani hutaamini huko
nilipohamishiwa kulikuwa na vitisho,juu ya vitisho, usiku mapaka yanahamia
kwangu……’akatulia na akawa kama anaangalia juu na watu wakacheka.
‘Msicheke,
…jamani kuna vioja huku duniani,….inataka moyo,..na kama huna imani thabiti,
huwezi kabisa kuifanya hii kazi yetu, lakini mimi imefika sehemu nimesema basi,
liwalo na liwe, kama niliamua kufanya
akzi hii, nahitajika kukubali matokea, ….na huwezi jua, ni bora ufe ukiwa
mpinaji kulikuwa kufa ukiwa msaliti, wan chi yako…nilikwenda nyumbani mara
moja, nikaaga,kiukweli,…’akasema na hapo watu wakacheka.
‘Sasa nimerudi
na nipo tayari kupambana na lolote lile….’akasema akijiamini …’Na kwa vile
ushahidi uliokuwa umepotea umepatikana, sioni kwanini nisije kutimiza azima
yangu…na kuna ushahidi mpya nilikusanya, na wapo watu wameshajitokea kusaidia
hili, wanajua, na walihusika, wataongea kila kitu,…nina imani haki itatendeka, …’akasema huku akitikisa kichwa
‘Sasa niingie
kwenye sehemu ya pili, naruhusiwa kuendelea muheshimiwa….?’ akauliza
‘Endelea
muheshimiwa….’akasema hakimu huku akiatabasamu na watu wakacheka.
‘Sasa basi
ngoja turejee kwenye ushahidi wa hii kesi, ili niweze kuelezea yote, na
nitamuhitajia mwenzangu upande wa usalama, mkuu wa upelelezi , aje anisaidie
kuthibitisha haya, maana bila yeye nitaonekana muongo…na pia nitauhijia
ushahidi huo wa kanda za DvD, uonyeshwe wazi ili muona ni nini kilikuwepo, …’akasema
na kumgeukiwa wakili mwanadada.
‘Usijali
muheshimiwa, …wewe ongea sehemu yako, na ikifikia muda huo wa ushahidi tutafanya
hivyo, kwa idhini ya muheshimiwa hakimu, na mashahidi wengine watakuja kwa wakati
muafaka, …tunakwenda kwa ratiba na …idhini ya muheshimiwa, usijali tupo pamoja’akasema
mwanadada.
‘Naanza kwa
kuelezea tukio la kuchomwa nyumba ya mama mkunga, ni tukio la kusikitisha sana
na tukio ambalo sijawahi kukutana nalo katika maisha yangu..na siku
nilipoletewa hiyo kesi, sikuamini…maana ni unyama wa hali ya yajuu…mtajionea
wenyewe muda ukifika wa kuona huo ushahidi.
‘Lakini cha
ajabu, nilikuja kugundua kuwa huyo muhanga, wa kuchomwa moto, sio mtu baki, kumbe
wana udugu kabisa na …kiongozi wa kijiji….huko nilipopelekwa nilikutana na
familia , sehemu ambapo huyo mama mkunga alilelewa, …kuna kisa cha aina yake
kilitokea kwenye huo ukoo…hapa sina muda wa kukismulia,….nilichoshangaa ni kuwa
huenda huyu mzee, wetu alifahamu hilo, au hakuwa analifahamu,…
‘Nilipofika
hapa jana, niliuliza kama huyo mzee anafahamu kuwa huyo mama mkunga ni ndugu
yake, nasikia alikuwa hajui kuwa huyo alikuwa dada yake, lakini kutokana na
mifarakano ya akina mama , ndugu yake huyo aliondoka na kwenda kulelewa huko
nilipopelekwa, na mungu akanikutanisha na walezi wa huyo mama…na bahati huyo
mama akaja kuolewa huku, sehemu yake alipozaliwa, bila kujulikana, bila hata ya
yeye kujua,…kwani yeye alirudi hapa akiwa mkubwa,…na hakuna aliyekuwa akijua
kuwa huyo mama na mzee wetu huyo wana udugu,
taarifa hiyo waliletewa hivi karibuni….’Alipofika hapo, akasikia mtu akipiga
yowe….’
Kila mtua
akageuka kule yowe lilipotokea, ilikuwa ni upande wa kambi ya utetezi na wakati
huo ilionekana, ni kama lile tatizo la mwanzo limetokea tena, lakini kwa sasa
ilikuwa ni zaidi ya hayo, kwani mshitakiwa mkuu alikuwa kalala sakafuni, na alioneka
mlinzi akijaribu kufanya kazi yake…..ya kuwasogeza watu wa kambi hiyo wakae mbali
na mshitakiwa mkuu, ili aone ni nini kimtokea…
‘Kuna nini….?’
Akauliza hakimu
‘Limetokea
tatizo kama lile la mwanzo, huyu mtu kashikwa na mshituko, na inaonyesha hali yake ni mbaya zaidi,….’akasema huyu
mlinzi na hakimu akaamrisha watu wa huduma ya kwanza wafike haraka, kuhakikisha
wanadhibiti hali ya mshitakiwa huyo....kama inawezekana kesi iendelee
Ilipita dakika
kumi, na mseamji wa wahudumu wa huduma ya kwanza akasema huyo mtu anahitajika
kuwahishwa hospitali haraka iwezekanavyo, kwani inawezekana ni shinikizo la
damu,ambalo limekuja ….na hali yake ni tete zaidi ya mwanzo.
****
‘Ilikuwaje…..?’
akauliza mmoja wa watu wa kambi ya utetezi ambaye hakuona jinsi ilivyokuwa,
akimuuliza mtu wa karibu wa mshitakiwa huyo.
‘Shahidi
alipokuwa akielezea habari za huyo mama mkunga, mzee wetu huyu, alionekana hana
amani, alikuwa mwingi wa mawazo, tofauti na siku nyingine, …alikuwa kama
hakuwepo mahakamani, na nilimweleza wakili wake, kama vipi tuombe kesi
iahirishwe, lakini mzee mwenyewe alisema lazima isikilizwe kwani anataka
kumuona huyo mama mkunga, …cha ajabu pale huyo shahidi alipooanza kuelezea
habari za huyo mama mkunga, ghafla akaanza kubadilika, na akawa anatingishwa,
..na kabla sijamuwahi, akadondoka sakafuni, na huku akisema;
‘Nisamehe ndugu
sikujua …sikuwa nakufahamu, sikujua, sikujua, oh nisamehe ndugu yangu, halafu
akapiga yowe…..ndio kauli yake niliyoiskia ya mwisho, kabla hajanyamaza na
kupoteza fahamu.
‘Ina maana
kweli ni ndugu yake?’ akaulizwa
‘Ni kweli,
lakini hawakuwa wakifahamiana, hadi alipokuja mzee mmoja ambapo mama huyo
alilelewa, na amabaye anafahamu historia ya wazazi wa hao, yeye ndiye aliyemlea
huyo mama, na ilikuwa hakupenda hilo lijulikane, lakini kutokana nah ii kesi,
akaona ni bora aeleze ukweli,
‘Je mshitakiwa
alikubaliana na hilo …?’ akaulizwa.
‘Alisema ni
kweli, anajua kuwa kuna ndugu yake, alichukuliwa akiwa mdogo, lakini
walifuatilia kwa muda mrefu, na kauli za mwisho, waliambiwa alifariki dunia,
kwahiyo hawakuwaweza kufuatilia tena,…ila kuna alama zao, na alitaka hiyo alama
ikithibiti, basi atajua ni ndugu yake….’akasema msemaji wa mzee huyo.
‘Kwahiyo hadi
hapo bado, ukweli hakuwa umetambulikana, ….?’ Akauliza.
‘Ulikuwa bado…maana
hakuna anayeruhusiwa kumuona huyo mama, na je ni kweli ni huyo mama, kama
mlivyoona, kafunikwa utafikiri ni kitu gani sijui….lakini leo tulijipanga
kushinikiza hadi huyo mama tumuone, ili tuthibitishe, ….’akasema.
‘Lakini mzee
huyu ni ngangari, sikujua kuwa leo anaweza kufika hapa, maana ule mshituko wa
mwanzo ulimchukua vibaya,….hadi jana, tulijua kuwa hataweza kufika mahakamani,
lakini asubuhi, anasema yupo tayari, na hata dakitari alithibitisha hilo..’akasema
mtu mwingine wa karibu wa huyo mzee.
‘Mhh, tuombe mzee
wetu aweze kusimama tena, maana mzigo wote katupiwa yeye, wakati inavyoonyesha
kuna watu wengine, wahusika, wapo nje,….hawajakamatwa,…wasiwasi wangu ni kuwa
dakitari alishauri, kama inawezekana kesi hii iahirishwe kwa wiki mbili hivi,
lakini mshitakiwa alikataa, akasema atajikongoja,, na dakitari alionya kuwa kama
hali hiyo ikitokea mara tatu, basi,
tunaweza kuongea mengine, ….’akasema huyo msemaji.
Sauti ikasikika
ikisema kesi imeahirishwa, hadi hapo itakapotangazwa tena, na amri ikatolewa
kukamatwa kwa washitakiwa wengine ambao hawakuwepo kwenye orodha ya
washitakiwa.
NB: Je ilikuwaje,….Je udugu
wa huyo mama mkunga na huyo mzee,ulikuwaje, kuna nini kimejificha hapa.je huyo
mshitakiwa ambaye hakamatiki ni nani,….kuna nini zaidi hapo….tuwepo kwenye
karibu na hitimisho cha kisa hiki.
WAZO LA LEO: Dua ya mwenye kudhulumuwa haina kizuizi, huenda moja
kwa moja kwa mwenyezimungu, tuogope dhuluma, kwa kutenda wema, ili dhuluma hiyo iweze kufutika, na kama umemtendea
mwenzako dhuluma, kwanza tubu na ikiwezekana nenda kamuombe msamaha, kabla
hujachelewa, kabla mlango wa toba haujafungwa, ….tusijidanganye kwa kufanya
ujanja ujanja, kwa vile tuna uwezo, …
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
Nasubiri kujya kinachoendelea kesi inaonekana ni ngumu kweli....inasisimua na kugopesha
First off I would like to say awesome blog! I had a quick question that I'd like to ask if you don't mind.
I was interested to find out how you center yourself and clear your thoughts
prior to writing. I've had trouble clearing my thoughts in getting my thoughts out there. I do enjoy writing however it just seems like the first 10 to 15 minutes are usually wasted simply just trying to figure out how to begin. Any recommendations or tips? Cheers!
Take a look at my web page: Laubsauger Test (smtp.Greatgiftcircle.com)
Post a Comment