‘Ndugu muheshimiwa
hakimu,..nawaruhusu watetezi kumhoji shahidi wetu huyu(mtaalamu), na kama hawana maswali
basi, tutamuita shahidi mwingine kuja kuthibitisha kifo cha jemedari, kabla ya
kumleta shadidi ambaye wenzetu wana hamu sana ya kumuona na kumhoji, …’akasema
na hakimu akawageukia watetezi, na wakili mtetezi akasimama, na kumkabili huyo
shahidi,….
Tuendeleze sehemu iliyopita kidogo….kwani sehemu hii ina mambo muhimu ambayo utakuja kuyaona baadaye.
‘Wewe unajiita mtaalamu au unaitwa mtaalamu?’ Wakili mtetezi
akauliza swali huku akimwangalia huyo shahidi, na huyo shahidi, akainua macho
yake kumtizama, macho ambayo yalikuwa kama ya mtu aliyeosa usingizi,
akamwangalia wakili huyo kwa huku akipepesa macho.
‘Wao ndio wananiita mimi mtalaamu, siwezi kujiita mwenyewe
mtalaamu…wewe vipi bwana’akasema kwa sauti ya ukakamavu.
‘Wanakuiita hivyo kwasababu una-utalalmu wa zaida kama
ulivyodai, au sio, ya kuwa unaweza kumtizamia mtu, kwa kupiga ramli au sio?’
akauliza
‘Kama ulivyosikia maelezo yangu ya awali, ndivyo hivyo
hivyo…kwani wewe unasemaje?’akasema na akawa kama anauliza kuonyesha kuwa
anajiamini
‘Unapopiga ramli, unamwambia mtu yale ambayo yatatokea, au
yaliyotokea hadi kufikwa na tatizo lililomleta kwako, na kutoa tiba yake au
ushauri, au jinsi gani ifanyike, au sio?’ akauliza
‘Ndio hivyo hivyo….kumbe unajua bwana, unapoteza muda
kuniuliza, au sio au sio…haisaidii, ….’akasema huku akitikisa kichwa kama
kukubali
‘Kwahiyo yote yanayokuja kutokea baadaye kwa mteja wako, ni
kutokana na ramli yako?’ akauliza
‘Unajua bwana mdogo, nikuambie kitu, ongea unachotaka
kuongea kwanini unazunguka kwa maswali yasiyo na tija, eti….kwanini hasemi
anachokitaka..’akasema shahidi huyo kwa ukali huku akimwangalia wakili
mwanadada, ambaye alikuwa akiwaangalia wanavyojibizana.
‘Mimi ndiye ninayekuuliza maswali na ukiulizwa maswali
unahitajika kuyajibu, ndio taratibu za hapa, hapa sio kwenye ofisi yako ya
kupiga ramli, unasikia…?’akasema huyu wakili mtetezi huku akitabasamu.
‘Nimekuelewa, ila nataka uulize swali kwa kujiamini, sio kwa
kuzunguka zunguka, maana najua ni kitu gani unataka kuniuliza, na mimi siogopi,
….kwasababu sio mimi, , nayafanya haya kutokana na mizumu, hamjui mateso gani
ninayoyapata…nisingeliweza kumsaliti ndugu yangu kamwe, hata yeye atakuwa analifahamu
hilo, kamwe, nisingeliweza kufanya haya ninayoyafanya hapa…’akawa anaongea kwa
haraharaka kama vile anaogopa kukatishwa.
‘Swali langu ni kuwa wateja wako ukishawaambai kuwa mtu fulani
ni mchawi, una uhakika gani kuwa huyo mtu ni mchawi kweli?’ akaulizwa.
‘Unapoenda kwa dakitari kwenye mahospitali yetu, ukaambiwa
una malaria una uhakika gani kuwa kweli una malaria,?’ akauliza
‘Usiniulize swali jibu swali…’yule wakili akacheka kidogo,
huku akitikisa kichwa kama kusikitika.
‘Hilo ndio jibu langu, kwani ulikuwa unataka nikujibu vipi…’akasema
huyo shahidi kama vile anauliza
‘Hilo ni jibu au ni swali ?’ akaambiwa na wakili ambaye
alionyesha uso wa kushangaa.
‘Kwangu mimi ni jibu maana ukijibu swali langu utakuwa umeshajibu
swali lako uliloniuliza…’akasema huyu shahidi akiwa kamkazia macho huyo wakili,
na huyo wakili akamtizama na akageuka kuangalai watu huku akiuliza swali
jingine.
‘Kuna matukuio mengi sasa hivi yanatokea, kuna maujai ya watu
wenye matatizo ya ngozi wanaoitwa Alibino, wanauwawa kutokana na nyie mnaojiita
wataalamu, na hata huyu….mama mkunga aliuwawa kutokana na … ramli zako za
uwongo…..’kabla hajamaliza wakili mwanadada akaweka pingamizi kuwa wakili
anaongea mambo yasiyohusika, anapnadikiza mambo ambayo shahidi hayajayasema.
‘Sawa …nitauliza kwa namna nyingine…’akasema wakili mtetezi
baada ya hakimu kukubali pingamizi hilo.
‘Mteja nikiwa na maana mgonjwa au mtu mwenye matatizo yake anapokuja
kwako, ukamwangalizia, au kama muitavyo, kumpigia ramli, na kumwambia mtu
fulani ni mchawi wako,..na ukampa dawa, ambayo inakwenda kumdhuru huyu
uliyemuita ni mchawi , huoni kuwa wewe ndiyo chanzo cha hayo…?’ akauliza na
wakili mwanadada akaweka pingamizi, lakini ajabu hakimu akataka swali hilo
lijibiwe.
‘Mimi sitaki kwenda mbali na kesi yetu hii, maana mimi sio
mwanasheria lakini nina uzoefu na mambo haya, ….., nitakijibu kwa mujibu wa kesi
yetu, maana hapa nilipo kama nilivyokuambia, nipo kwenye uangalizi wa hawa
mizimu,mizimu ipo nami hapa inaniangalia kila ninalolifanya….sitakiwi
kuongopa….mnasikia sana’akataka kuongea lakini wakili mtetezi, akasema inatosha
hana swali jingine.
Wakili mwanadada akasema; ‘ Ndugu muheshimiwa hakimu, kwa
vile wakili mtetezi kauliza hilo swali hebu naona ni vyema shahidi akalijibu,
nilikuwa nataka shahidi huyu atuambie je ni kweli kuwa yeye alipiga ramli kuwa
mama mkunga ni mchawi, na je ni kweli kuwa yeye ndiye aliyeamrisha kuwa mama
huyo auwawe kwa moto kutokana na ramli
yake hiyo?’ akaulizwa wakili mwanadada.
Wakili mtetezi kusikia hivyo akaweka pingamizi kuwa yeye
alisharizika na maelezo yake, hahitajii hilo swali kujibiwa tena, lakini hakimu
akasema alisharuhusu hilo swali lijibiwe, na hapo shahidi akageuka kumwangalia
kiongozi wa kijiji, na kusema;
‘Samahani sana ndugu yangu, nasema haya kwa vile sina jinsi,,
na ingelikuwa ni uwezo wangu nisingelisema haya nitakayoyasema sasa hivi, na inabidi
niyaongee haya kwa vile nihisi itakuwa ndio mara yangu ya mwisho kuonana mimi
na wewe au kuniona tena katika ulimwengu huu….’akasema akionyesha huzuni, na
huku akikunja uso kuashiria machungu, na sekunde cache zikapita bila ya yeye
kusema kitu, halafu akasema;
‘Haya , haya waungana niachieni, nitasema yote…tafadahali
niachieni,…..’akasema huku akijinyosha nyosha kama vile mtu anayehisi mauimvu
mwilini.Hakimu alikuwa kaduwaa akimwangalia huyo mtu, huku akionyesha uso wa
kushangaa, lakini hakusema kitu, akageuka kumwangalia wakili mwanadada, ambaye
naye alikuwa kaduwaa vile vile, akimwangalia shahidi wake huyo.
Shahidi huyu akafuta jasho, halafu akaanza kuongea, huku
akimwangalia mshitakiwa mkuu, na mshitakwia mkuu, alionekana kuwa mbali
kimawazo, na hakuacha kumwangalia shahidi huyo, kama vile hataki jambo limpita,
au alikuwa haamini hayo anayosema ndugu yake….
‘Kutokana na hali
ilivyokuwa, kuwa mali aliyoacha baba yetu, yaani mali ya aridhi kama alivyoigawa
mafungu, kuwa shemu hii ni ya huyu na sehemu hii ni ya yule, na akatuambia tusiiguse
sehemu ya pembeni, kwani ni mali ya m toto wake mwingine wa kike, yaani mama
mkunga….’akatulia.
‘Kwa kipindi hicho sikuwa ninatambua kuwa ni huyo ni mama
mkunga, nilikuja kufahamishwa baadaye na ndugu yangu huyo, kiongozi wa kijiji,
lakini ndugu yangu huyo, pamoja na wanandugu wengine, hawakuwa tayari kufanya
hivyo….’akatulia na kubetua mdom.
‘Unajua tena baba hakuwepo tena duniani, sisi ndio tulikuwa
na mamlaka ya kufanya lolote, tukasahahu usia, ndivyo ndivyo tulivyo binadamu,
au sio….., wengi wetu, tukaona hayo yalikuwa ya mzee, akiwemo ndugu yangu huyo,wakasema
huyo ni mwanamke tu, hana stahili ya kurithi kitu , kwanza ana mume wake,kwahiyo
hana mamlaka na mali hiyo tena…huko alipoolewa, atapata hicho anachokitaka,
kwahiyo hastahili, kupewa chochote….’akatulia.
‘Wapo waliosema kuwa ni haki yake, lakini hawakuwa na nguvu
sana kwasababu ni wachache…maamuzi yakapitishwa kuwa mama huyo asipate kitu,…na
kweli eneo hilo likawekwa chini ya mamlaka ya familia, na ilivyopangwa, ni kuwa
kama sipo kuuzwa, basi tugawane….ikapitishwa’akatulia kidogo.
‘Haaah, baadaye mama mkunga akatokea na kuanza kudai haki
yake, kwani alishaambiwa kuwa kuna haki yake, na …..sisi kama wanafamilia,
tukaziba masikio, na kujifanay kushangaa, lakini kama nilivyokuambai kati yetu
kuna walioona kuwa ni haki yake, hawo, wakawa wanampa ndogondogo, …hapo sasa
tutakaona ni tatizo, kwahiyo ikabidi itafute njia ya kuhakikisha mama huyo ,
hawezi kufanya lolote, na na hapo….mhhh, ile njia ya ukitaka kumuua mbwa kwanza
umuite majina mabaya ikaanza kutumika, …’akasema na kutulia huku akitabasamu.
‘Kwahiyo mimi kama mtaalamu nikatakiwa kusema nimepiga
ramli, na imeonekana mchawi wa watoto wachanga wanaokufa mara kwa mara hapo
kijijini ameshafahamika….kuwa ni yeye, kuwa mama huyo ndiyee chazo cha yote
hayo, anajifanya mkunga, huku anafanya mambo yake….’ Akakunja uso kuashiria
huzuni.
‘Nikatakiwa kusema mama huyo ndiye mchawi ndiye anayewauwa watoto
hawo kwa ajili ya mambo yake ya kichawi,….na ufahamu kuwa mimi ninaaminika
kweli nitakachokisema huwa kinaaminika…kwani mambo yangu sio mchezo, na ni
kweli nikikuangalizia nikasema kuna kitu…chunga sana, kweli kuan kitu, lakini
kwa mama huyo nilitakiwa niongope…hapo niseme ukweli…’akacheka kidogo.
‘Basi, …., na ilikuwaje, maana nisingelisema tu, kilichofanyika
ni kuwa alikuja mke wa Jemedari akiwa na matatizo yake kuhusiana na matatizo ya
uzazi, huwa kila akijifungua, mtoto anafariki, basi tukaona ni hapo hapo,
nikatakiwa kumwambia mchawi wake ni huyo mama….’ Akabetua mdomo kama
anatabsamu.
‘Huyo mama kama walivyokuwa akina mama wengine, au watu
wengi wanaoamini sana mambo hayo, wakakubali, …kwanini asikubali, wakati mimi
naaminika kwa kazi hiyo, ….basi yeye akaenda kumuelezea mume wake, na habari
zikaanza kutawanyika kwa haraka sana….unajua
uvumi wa uwongo husambaa kwa haraka sana, kama cheche za moto kwenye
jangwa… mama mkunga akaonekaa kuwa kweli ni mchawi….’akasema na hayo maneno ya
mwisho akayaongea kama ananong’ona.
‘Kwahiyo,kiukweli kutokana na huo utaalamu wako, mama mkunga
ni mchawi au sio mchawi?’ wakili mwanadada akauliza kwa haraka.
‘Kwakweli kama nilivyosema awali, hayo yalipangwa iwe hivyo,…na
nasikitika sana, kwani nilikiuka maadili ya akzi zangu, ……Inabidi nimuombe sana
mama huyo msamaha kwa hayo yaliyotokea, kiukweli mama huyo yupo mbali kabisa na
uchawi, …’aasema na kuangalia huku na kule kama vila anamtafuta huyo mama
mahali alipo.
‘Mama wa watu hajui uchawi kabisa, sio mchawi jamani,…mama
huyo ana kipaji cha kutibu watu na sio kuangamiza, ….ujue kuna tofauti ya mchawi
na mganga wa kienyeji, tusichangaye haya mambo, ila mtu yoyote anaweza akawa
mchawi, kama atakuwa anafanya mambo ya kuwaathiri wenzake….unalifahamu hilo,
hata wewe hata muheshimiwa pale anaweza akawa mchawi,…kwa kijicho, kwa husuda,
kwa wivu, akaona kwanini…..ile kwanini ni tabia za kichawi, sasa inategemea
uvumilivu, kuna atakayeona kijicho, akameza ndani kwa ndani, lakini kuna yule
atakayejenga fitina, ..na kuna yule atakayekwenda zaidi ya kutaka kuua….’akatulia
kidogo.
‘Unajua, mchawi anatengeneza mambo yake kuumiza watu wengine
….ukiangaia ni kwasababu ya husuda na chuki zake binafsi,…. lakini mganga….’akatulia
kidgogo.
‘Mganga ni kama hawo mnaowaita madakitari wa mahospitalini,…na
ndio huyo mama mkunga, yeye hutengeneza dawa tu kutokana na kipaji,…..mama huyo
hakuwa akitengeneza kutibia mtu aliyelogwa, kwasababu hayajui hayo mambo
kulogwa, yeye alikuwa akitengeneza dawa, kutokana na ugonjwa na uzoefu, au kipaji, alichokipata, hatumiii
mizimu au ramli kama sisi wataalamu,….ukifika kwake kama unaumwa tumbo,
atakuuliza tumbo linaumaje, yeye ukimfahamisha, anakupa dawa,anayoijua kuwa
inatibu tumbo la namna hiyo, maana kuna matumbo ya namna nyingi……ndivyo alivyo,
yeye sio mchawi kabisa, ….na zaidi ya hapo ana kipaji cha ukunga…’akatulia.
‘Je siku mama huyo alipochomewa nyumba yake moto ulikuwa
ukifahamu?’ akaulizwa.
‘Kiukweli kabisa, sikujua ni lini watafanya hivyo, ila
nilikuwa nafahamu kuwa kuna mpango kama huo, na shinikizo kubwa lilikuwa kutoka
kwa vijana, kuwa kama kweli mama huyo ni mchawi…kama nilivyoagizwa niseme,…,
basi dawa yake ni kumteketeza kwa moto….wao walipendekeza hivyo,lakini mizimu
hataki hivyo, ndio maana napewa adhabu….’akasema
‘Na wewe uliunga mkono wazo hilo….?’ akaulizwa.
‘Hapana, mimi nililipinga kwa nguvu zangu zote, maana
nilikuwa nafahamu kuwa mama huyo sio mchawi, na uzushi huo kwake, ulitungwa,
kutokana na matakwa ya familia, kuwa aonekane hivyo, na hata akidai madai yake,
jamii, isimuamini,..na tulijua kwa aibu kama hiyo asingeliweza kuishi tena hapo
kijijini, angelikimbia na sisi tufanye yetu kwa ulaini…lakini mama huyu
hakutishika na uzushi huo…akatukwaza….unafikiri hapo shetani keshajaa kichwani
mtafanyaje…mtu mmoja tu, atunyime raha….mhhhh.’akatulia.
‘Siku akichomewa moto, wewe ulikuwa wapi?’ akaulizwa.
‘Mimi niliitwa kijiji cha jirani, nilikuwa nafanya kazi
zangu…siunajua tena, leo nipo hapa kesho naitwa kwingine,…., na nilipata
taarifa hizo kuwa huyo mama keshachomewa nyumba yake moto, na inasadikiwa kuwa
kaungua kabisa, hata kiwiliwili chake hakikupatikana, hapo nikaingiwa na
wasiwasi,…haiwezekani mtu aungue kabisa, hata fuvu la kichwa
lisipatikane,…inawezekana kutegemeana na moto ulivyo, lakini sio kwa moto kama
huo, manyasi tu, na fito…na fito zenyewe basi fiti….hawakuwa na uwezo wa
kujuenga nyumba imara sana, kwahiyo moto huo, usingelimaliza kiwili wili chote….’akasema
‘Ni nani aliyekufahamisha hivyo, kuwa huyo mama kachomewa nyumba
yake moto, na kuteketea kabisa?
‘Wa kwanza kabisa ni ndugu yangu huyo mzee wa kijiji…..’akasema
huku akiona aibu kumwangalia ndugu yake huyo,akawa anamnyoshea kidole huku
akiwa katizama pembeni.
‘Je alikuwambia ni yeye kafanya hivyo ?’ akaulizwa
‘Alichoniambia ni kuwa ile kazi imefanyika, na nikaumuuliza
kazi gani, akasema yule mama wanayemuita kuwa ni mwanga ameshateketezwa kwa
moto, hayupo tena duniani , nikamuuliza una uhakika na hilo, je mwili wake ameuona…akasema
hakuwa na haja ya kuuona, ila amethibitisha kwani alishuhudia moto ulivyokuwa
na hakuona mtu aliyewahi kutoka nje…’akatulia na sauti ya kuguna ikasikika
kutoka kwa mshitakiwa mkuu, kama vile anapinga,lakini wakili wake akamtuliza.
‘Wewe ulifanya nini baada ya kusikia hivyo?’ akaulizwa.
‘Kwakweli niliumia sana…..sijawahi kujisikia vibaya kiasi
hicho, maana kupanga ni kitu kingine,
na kutekeleza yale mliyoyapanga ni kitu
kingine,..wakati tunapanga, ilikuwa ni kama maongezi tu, na sikuwa nayakini
kuwa jambo baya kama hilo litatekelezwa, …sasa kusikia kuwa limetekelezwa, na
mimi ndiye niliyetumiwa kama chambo, niliumia sana, na hapo hapo nikaanza kuandamwa
na ndoto mbaya, mizimu ikaanza kunisakama….kuwa nimekiuka masharti ya taaluma
yangu…’akasema.
‘Ulirejea nyumbani siku hiyo hiyo, baada ya kusikia hivyo?’
akaulizwa.
‘Niliposikia hivyo, nilimuaga mwenyeji wangu,…kuwa nimesikia
jambo la kuhuzunisha, na mimi ni mwanandugu, kwahiyo inabidi nirejee nyumbani
haraka iwezekanavyo,…nikarejea usiku ule ule…na nilifika eneo hilo na kukuta
bado moto unawake, nikazunguka, nikitumia hisia zangu za kitaalamu, lakini
hisia hizo zilikuwa zimeshaondolewa mwilini, nilikuwa mtupu kabisa….’akasema
‘Kilichobakia akilini mwangu ilikuwa ni uzoefu tu,…nikajua
kuwa mimi sio mtaalamu tena, ..sina changu tena, mizimu imeshanitoa kwenye
kundi lao, iliyobakia ni adhabu yao…nikalia sana,…nikajuta sana, na wakati
nazunguka eneo hilo, ndipo nikasikia mtu akigugumia kwa maumivu, hapo akili
ikaniashiria jambo, ….nikakumbuka hisia nilizokuwa nazo nilipopewa hiyo taarifa,
kuwa kama hawakuona mwili,au mabaki yoyote basi yamkini, mama huyo atakuwa
hajafa….’akatulia.
‘Nilifuatilia ile sauti imetoka wapi,..na karibu kabisa na eneo
hilo la nyumba, kuna mfereji wa maji, …mfereji huo walikuwa wakiutumia kunyweshea
bustani na kulishia mabata, kwa msimu kama huo, ulikuwa na maji mchafu tu,
katikati ya maji hayo, niliona kitu kimelala,…’akatulia.
‘Niliposogelea
nikagundua ni mtu, nikainama kumwangalia…mamamama….’akawa kama anaanglia
pembeni kama vile mtu kaona kitu cha kustaajibika, na kuogopa kukiangalia moja
moja kwa moja,…
‘Alikuwa ni mtu, kaungua,eneo lote la mgongoni, …..unajua
mtu akiungua anakuwaje, ….cha ajabu hapo hapo, nguvu za utalaamu zikanirejea, mizimu
ikanirejeshea nguvu hizo, ili niweze kumtibia huyo mama kama ilivyokuwa,….nikaanza
kuelekezwa jinsi gani ya kufanya,…nikambeba huyo mtu, hadi maporini….na kwa
muda huo sikuwa namtambau kuwa ni huyo mama…kwani nguo, zimeshangua, yupo na
mabaki mbai ya nguo…sikuwa na jinsi,…’akatulia
‘Huko nikaelekezwa aina fulani ya majani, ambayo
ukiyatangwa, yakawa laini, ukampaka mtu aliyeungua, hufanya kazi mara moja,
huyakausha yale majeraha kwa haraka, na baada ya masaa sita, yanaanza yale
majani yaliyogandana kwenye majeraha hubanduka na kuondoka na ngozi
iliyosinyaa, kinachobakia ni makovu tu….’akatulia.
‘Nilifanya hivyo, na adhabu niliyopewa nikuyatafuna, hayo
majani kwa mdogo wangu, hadi yatoshe mwili mzima, nilitafuna hadi kinywa kikawa
kinauma, lakini sikuweza kupumzika, hadi mwili wote, sehemu zilizoungua, zikawa
zimeweza kuenea ile dawa, na baada ya hapo nikaelekezwa dawa ya kumpa, ambayo
aliinywa , na nikaelekezwa nimjengee kibanda, na humo niwe ninamsaidia mpaka
apone….’akatulia kidogo.
‘Nilikaa na mgonjwa huyo kwa siku tatu, na alipozindukana,
…nikaambiwa niondoke haraka, ili asinione, na nikafanya hivyo, na hapo
nikachukuliwa na mizimu, sikujitambua nilijikuta ndani ya mapango ya watu wa
kale, huko nikaweka kwenye ulinzi na adhabu yangu ikaanza
kutekelezwa….’akatulia
‘Kwahiyo hukujua ni nini kilitokea huku nyuma baadaye?’
akaulizwa
‘Kwakweli hapo nilipokuwa nilikuwa nje ya dunia hii
mnayoifahamu nyie, na hata kama watu waneglifika hapo wasingeliweza kuniona….nilitoka
pale nilipoambiwa natakwia kuja kutoa ushahidi…’akatulia.
‘Kabla hujaondoka, tukuulize swali kuhusu sumu ambayo
ilitumiwa kuwaua hawo vijana waliohusika kumchomea huyo mama na pia sumu hiyo
ikatumika kumuua Jemedari , je ni wewe
uliyeitengeneza?’ akaulizwa.
‘Hapana,… ila niliwahi kumuelekeza ndugu yangu huyo jinsi ya
kutengeneza sumu ambayo inaweza ikamuua mtu, na hata ukitumia vipimo vya
hospitalini huwezi kugundua kuwa mtu huyo kauwawa kwa sumu, …sumu hiyo
ikashafika kwenye ubongo, mtu huyo anakuwa kama kapagawa, kwasababu huathiri,
mawasiliano ya ubongo, na kinachofuata hapo ni mtu huyo kuvuja damu sehemu zote
za mwili, na hachukui muda anafariki…’akasema.
Wakili mwanadada akasogea kwenye sehemu walipoweka vielelezo
vya ushahidi akatoa chupa mbili zenye vinywaji ndani akamuonyesha huyo shahidi.
‘Unaweza ukagundua vinywaji hivi ni kitu gani?’ akaulizwa na
huyo mtalaamu akachukua chupa mojawapo, na kuifungua akanusa, akatikisa kichwa
kuashiria sio yenyewe, halafu akachukua chupa nyingine akaitikisa, halafu akafungua
na kunusa, ….lipuliza kwa pua kuashiria muwasho ndani ya pua na kuanza kupiga
chafya, mfulululizo…na alipotulia akasema;
‘Ndio yenyewe, hii ni sumu, akiichanganywa kwenye kinywaji,
kijiko kimoja tu, inatosha…ukikinywa hicho kinywaji..inaanza kufanya kazi
taratibu,na kufanya kama nilivyoelezea awali…ni hatari kabisa, na mtengenezaji
hakuweza kutumia vipimo sawasawa, alizidisha ndio maana imenipa taabu lakini
mimi siwezi kuzurika maana nipo na mizimu inanilinda, ianasubiri muda wangu
ufike…nawashauri sumu hii muiharibu haraka isje ikafika kwa watu wabaya, ni
mbaya sana..’akasema na kuifunga, na wakili mwanadada,a akaichukua na kuiinua
juu, na kusema;
‘Muheshimiwa hakimu, nawakilisha kielelezo hiki kama
ushahidi wa sumu iliyowauwa vijana na ….Jemedari, na hapo aligeuka na kumwendea
msaidizi wake akamnongoneza jambo, halafu akageuka, kwenye kambi ya utetezi, na
kwa muda huo, mmoja katika kambi ya utetezi, alisimama, na kutoka nje, alikuwa
sio mwingine, bali ni mwanasheria wa familia, na wakili mwanadada hakujali
hilo, akaendelea kuonmgea, akasema;
‘Na sasa ni zamu ya shahidi wetu mwingine…..’ na aliyetoa
mguno wa nguvu, alikuwa ni kiongozi wa kijiji, na wakili wake akamtizama kwa
mshangao, na akataka kumuuliza jambo, lakini akasita, kwani shahidi huyo
alishafika mbele…
NB: Ni nani huyo tena, kwanini mshitakwia mkuu akatoa mguno,…je
ni mama mkunga tena, au kuna mtu mwingine..naona niishie hapa kwa leo.
WAZO LA LEO:Binadamu
ni kiumbe wa ajabu sana,…huwezi amini, kuwa pamoja na kujua kuwa mali, na
vilivyopo dunia ni vya kupita tu, kuwa ipo siku utaviacha, lakini kila mmoja
yupo mbioni kulimbikiza, na haitoshi , bado mtu anaona ni vyema kumdhulumu mwingine,
ili yeye apate zaidi, au kwanini yule kapata na sio mimi….hata kama anacho,
anapata kila siku, lakini kwanini zinakuwa nyingi….husuda, wivu, chuki, ubinafsi
vimetawala nafasi ya mwanadamu, ndio maana amani, na upendo vinatowekea
duniani. Tumuombe mungu atuepushe na tabia hizi mbaya.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment